Habari za Kitaifa

Raila aomba Kalonzo, wanahabari msamaha kwa kushambuliwa na wahuni

Na JUSTUS OCHIENG July 18th, 2024 2 min read

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga ameomba radhi kwa wanahabari na viongozi waliofukuzwa Jumatano na vijana katika hafla ya muungano huo jijini Nairobi.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alikuwa miongoni mwa viongozi waliofukuzwa na vijana waliozua ghasia walipokuwa wakisoma maazimio ya muungano huo baada ya mkutano wa Kundi la Wabunge (PG).

Katika taarifa ya msemaji wa Bw Odinga, Dennis Onyango, kiongozi huyo wa ODM alitaja kisa hicho  kilichotokea katika afisi za  Jaramogi Oginga Odinga Foundation (JOOF) kuwa cha kusikitisha.

“Jana (Jumatano), kuelekea mwisho wa majadiliano marefu na yaliyofaulu kuhusu maendeleo ya nchi na msimamo wa vyama vya Upinzani, vijana, baadhi wanaojulikana, na wengine wasiojulikana, walivamia ukumbi na kuwatimua washiriki. Tunaelewa kuwa wakati wa kisa hicho, wanahabari kadhaa waliokuwa wamealikwa kuangazia mkutano wa ODM-Azimio la Umoja One Kenya walipigwa,” ilisema taarifa ya Bw Onyango.

Alisema ukumbi wa mkutano huo, umekuwa ukiandaa mikutano muhimu bila ya matukio ya fujo.

“Mheshimiwa Raila Odinga anajutia matukio ya jana na anachukua fursa hii mapema kuwaomba radhi wanahabari na viongozi waliojipata katika tukio hilo la kusikitisha,” aliandika.

“Bw Odinga, anawahakikishia wanahabari na viongozi wenzake kwamba muungano huo utachunguza tukio hilo na kuziba mianya iliyosababisha dosari za usalama kwa nia ya kuhakikisha kwamba wanahabari na viongozi wanasalia salama na huru katika shughuli zote za Azimio ikiwa ni pamoja na waliokuwa katika ukumbi huo,” Bw Onyango alisema,”

Wanahabari waliokuwa wakiangazia tukio hilo, kupitia kwa mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari wa Kisiasa nchini (PJAK) Rawlings Otieno, wametaka kuombwa msamaha baada ya baadhi ya waandishi kujeruhiwa wakati wa ghasia hizo.

“Kitendo cha unyanyasaji kinachoelekezwa kwa wanahabari si tu kibaya, bali ni kudhalilisha uhuru wa vyombo vya habari, ambao ndio msingi wa demokrasia ya Kenya,” Bw Otieno alisema.

Alitaka hatua zichukuliwe dhidi ya wahuni waliowashambulia waandishi wa habari.

Mkutano huo ulitibuka baada ya vijana kuvamia wanahabari baada ya Bw Musyoka, ambaye ni kinara mwenza wa Azimio kuanza kusoma maazimio hayo viongozi wa muungano huo kuhusu mazungumzo ya kitaifa na serikali ya umoja wa kitaifa iliyoitishwa na Rais William Ruto.