Habari za Kitaifa

Raila asiachie ‘mtu wa nje’ ODM akiwahi kiti cha AUC

Na CECIL ODONGO August 27th, 2024 2 min read

KINARA wa upinzani Raila Odinga akifanikiwa kutwaa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) asidhubutu kuiachia kiongozi kutoka nje ya jamii yake usukani wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM).

Hatua hiyo itakuwa mwanzo wa mwisho wa chama hicho maarufu cha upinzani nchini.

Kwa kuwa Bw Odinga, 79, ameonekana kuwa kifua mbele katika kiny’ang’anyiro cha AUC, mivutano imeanza kuchipuza kuhusu uongozi wa ODM na kuashiria kwamba kutazuka kambi mbalimbali kung’ang’ania nani anastahili kuelekeza chama hicho cha chungwa.

Akiwa AUC, kinara huyo hatakuwa na muda wa kushiriki siasa za nyumbani kwa sababu ya safari na majukumu yatakayoandamana na kazi yake ya uenyekiti.

Hata hivyo, Waziri Mkuu huyo wa zamani asiachie uongozi wa ODM mwanasiasa anayetoka nje ya eneo la Luo Nyanza.

Akijaribu kumpa usukani mtu wa nje basi chama hicho kitasambaratika na kuchukua mwelekeo ambao hautaridhisha wafuasi wake kuelekea uchaguzi wa 2027.

Tangu 2005, Bw Odinga amewekeza nguvukazi, muda, mali na mawazo kukuza ODM kiasi cha kuwa chama tisti cha kitaifa chenye ufuasi mkubwa Nyanza, Magharibi, Pwani, Kaskazini Mashariki na miongoni mwa jamii za wafugaji.

Hata hivyo, baadhi ya wale wanaovutana ndani ya ODM wakitaka kumrithi kigogo huyo ni wanasiasa walafi na wakipewa nafasi ya kutwaa usukani basi ODM itafifia.

Kwa sasa Naibu Rais Rigathi Gachagua yuko mkao wa atiati ndani ya chama tawala cha United Democratic Allliance (UDA).

Baadhi ya wandani wake wamemwambia wazi kwamba hali yake imesababishwa na ukanda wake wa Mlima Kenya kutokuwa na chama mahususi cha kisiasa.

Ndiyo maana Bw Gachagua alibaki tu kulalamikia kutemwa kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Cleophas Malala bila uwezo wala ushawishi wowote wa kumuokoa, kwa sababu UDA si yake.

Bw Raila akiachia uongozi wa ODM mtu ambaye si wa jamii yake, basi Waluo wawe tayari kuhangaishwa ndani ya chama ‘chao’ ambacho wamekikweza miaka hiyo yote kikawa imara.

Wakati ODM-Kenya iliundwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2007, Kalonzo Musyoka alifanikiwa kupiga kumbo mrengo wa Bw Odinga kwa sababu Daniel Maanzo (kutoka jamii ya Kamba yake Bw Musyoka) ndiye alikuwa na cheti rasmi cha usajili wa chama.

Ilibidi Bw Odinga na wenzake waongee na Bw Mugambi Imanyara kwa unyenyekevu ili awape stakabadhi zilizotumika katika kusajili ODM, kwa sababu ndiye alikuwa amesajili chama hicho.

Baada ya hilo, Bw Odinga alihakikisha anaweka wandani kutoka eneo lake la Luo Nyanza kama viongozi katika nyadhifa mbalimbali kuimarisha na kudhibiti chama.

Aidha, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ana usemi katika utawala wa sasa kuliko Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, kutokana na mchango wa chama chake cha Ford Kenya kumzolea ushindi Rais William Ruto mnamo 2022.

Mchango huo ndio umemfanya kukaa ngumu licha ya kushurutishwa avunje Ford Kenya ili wawe chini ya mwavuli mmoja wa UDA kuelekea 2027.

Hii ni tofauti na Bw Mudavadi ambaye ANC yake haikuleta chochote cha maana kwa Rais Ruto, na tayari ameshakivunja na kuingia UDA.

Siasa za Kenya ni za kikabila ndiposa hata kiongozi atakayerithi usukani wa ODM kutoka kwa Bw Odinga anastahili kutoka Luo Nyanza ili chama kisitekwe na ‘mtu wa nje’.