Makala

Raila ataumwa na kichwa kujaza nafasi ya Wandayi Ugunja

Na CECIL ODONGO August 12th, 2024 2 min read

KINARA wa chama cha ODM Raila Odinga atakuwa akikabiliwa na mtihani mwingine mgumu wa kisiasa katika ngome yake ya Luo Nyanza baada ya aliyekuwa Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi kuteuliwa waziri katika serikali ya Kenya Kwanza.

Eneobunge la Ugunja litakuwa kati ya maeneo 11 ambayo yataandaa uchaguzi mdogo iwapo mchakato kuwateua Makamishina wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) utakamilishwa kwa wakati.

Bw Wandayi sasa ni Waziri wa Kawi baada ya uteuzi wake kuidhinishwa na bunge.

IEBC kwa sasa haina makamishina wa kutosha baada ya muhula wa kudumu kwa aliyekuwa Mwenyekiti Wafula Chebukati na makamishina wawili Boya Mulu na Abdi Guliye kukamilika mnamo 2023.

Kwa sasa IEBC inasimamiwa na sekretarieti ambayo haiwezi kutekeleza baadhi ya majukumu kisheria.

Hivi majuzi, mchakato wa kubuni jopo la kuwateua makamishina wa IEBC ulipigwa breki  kutokana na mzozo ambao upo katika Jopo la Kutatua Mizozo ya Kisiasa (PPDT).

Mzozo huo upo kwa sababu vyama vya Wiper na NLP vinazozania mwakilishi katika jopo hilo ambalo linastahili kutoka mrengo wa Muungano wa Azimio.

Kando na Ugunja kuna maeneobunge ya Banisa na Magarini ambayo yanastahili kuwa na uchaguzi mdogo. Mbunge wa Banisa Hassaa na Kullow aliaga dunia katika ajali ya barabarani mnamo Machi 29, 2023.

Hata hivyo, Mbunge wa Magarini Harrison Kombe naye hana lake baada ya Mahakama ya Juu kudumisha uamuzi wa kufutilia ushindi wake mnamo Mei 31, mwaka huu.

Kando na maeneobunge hayo matatu kuna chaguzi ndogo zinazostahili kufanyika katika wadi saba ambazo wawakilishi wao waliaga dunia.

Japo nafasi ya Bw Mbadi ni wazi, itamwendea Kiongozi wa Vijana wa ODM John Ketora kutoka jamii ya Maasai, mrithi wa Bw Wandayi lazima apatikane kupitia uchaguzi mdogo, mtihani mkubwa ambao unasubiri ODM.

Bw Ketora atakuwa akichukua nafasi ya Bw Mbadi kwa sababu alikuwa wa tatu kwenye orodha ya majina ambayo ODM iliwasilisha kwa IEBC ya watu waliostahili kuteuliwa wa wabunge baada ya uchaguzi wa 2022.

Seneta Catherine Mumma aliongoza orodha hiyo kama mwakilishi wa wanawake naye Bw Mbadi akawa mwakilishi wa upande wa wachache katika bunge la kitaifa.

Eneobunge la Ugunja lilitolewa kutoka kwa ile ya Ugenya wakati wa kutekelezwa kwa ripoti ya Tume ya Andrew Ligale ambayo ilikuwa ikiamua mipaka ya maeneo mbalimbali mnamo 2012.

Bw Wandayi alikuwa akihudumu kama mbunge wa eneo hilo kwa mihula mitatu.

Hata hivyo, umaarufu wa MDG katika eneobunge jirani la Ugenya huenda utakipa chama cha ODM kibarua kigumu cha kuhifadhi kiti hicho.

Mbunge wa sasa wa Ugenya David Ochieng’ alichaguliwa kuhudumu muhula wake wa tatu kupitia MDG huku akiwabwaga wawaniaji wa ODM kwenye uchaguzi mdogo wa 2019 na pia mnamo 2022.

Bw Ochieng ambaye alihudumu kama mbunge wa Ugenya kati ya 2013-2017 kabla ya kumbwaga Bw Otieno Karan wa ODM kwenye uchaguzi mdogo wa 2019 amekuwa akivumisha sana MDG Nyanza na Magharibi mwa nchi.

Katika uchaguzi wa 2022, Bw Ochieng’ alihimili mawimbi ya ODM na kumshinda Dkt Dan Odhiambo baada ya kupata kura 25520 dhidi ya 22,928 zake Bw Odhiambo.

“Iwapo MDG itakuwa na mwaniaji bora na ODM ijikwae kwa kumteua mwanasiasa ambaye si maarufu basi itapoteza kiti hicho. Chaguzi ndogo siku hizi hazizingatii sana miegemeo ya kisiasa na itakuwa vigumu kwa ODM kurejelea MDG kama adui baada ya Rais Ruto na Raila kuelewana,” akasema Mchanganuzi wa Kisiasa Martin Andati