Habari

Rais Kenyatta ampongeza Mutharika kwa kushinda urais Malawi

May 28th, 2019 1 min read

Na PSCU

NAIROBI, KENYA

RAIS Uhuru Kenyatta amempongeza mwenzake wa Malawi Prof Arthur Peter Mutharika kwa kufaulu kuhifadhi kiti chake baada ya uchaguzi mkuu.

“Kwa niaba ya watu na Serikali ya Jamhuri ya Kenya, nakupongeza kwa kuchaguliwa tena kwa kipindi cha pili kuwa Rais wa Jamhuri ya Malawi,” amesema Rais Kenyatta.

Kiongozi wa nchi amesema kuchaguliwa tena kwa Mutharika na mamilioni ya raia wa Malawi katika uchaguzi wa amani ni dhihirisho la imani ya watu walio naye na pia kuashiria kukomaa kwa demokrasia ya Barani Afrika.

Kenya na Malawi zinafurahia uhusiano mzuri na wa kihistoria wa tangu kabla ya uhuru, ukishirikishwa na ari ya ukuaji na maendeleo, na moyo thabiti wa mwamko wa Afrika unaotokana na kazi iliyofanywa na waanzilishi wa Jamhuri hizi mbili, hayati Mzee Jomo Kenyatta na hayati Hastings Kamuzu Banda.

Raia nchini Malawi walishiriki shughuli muhimu ya kumchagua Rais wao Mei 21.

Matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Malawi (MEC), Jane Ansah yalimweka mbele Mutharika aliyejizolea jumla ya asilimia 38.67 ya kura halali zilizohesabiwa, akimshinda mpinzani wake mkuu wa upinzani, Lazarus Chakwera aliyepata asilimia 35.71 za kura zote zilizohesabiwa.