Habari za Kitaifa

Ruto ajitetea kwa kubomoa upinzani

Na GITONGA MARETE July 26th, 2024 2 min read

RAIS William Ruto ametetea hatua yake ya kujumuisha viongozi wa upinzani katika serikali yake akisema kuwa ananuiwa kuhakikisha kuwa Wakenya wote wanashiriki katika ujenzi wa taifa.

Rais alisema ili kutatua changamoto zinazokabili taifa kutokana na maandamano ya Gen Z na wanaharakati, alifanya uamuzi mgumu wa kujumuisha upinzani katika utawala wake.

Maandamano hayo yalimfanya rais kuondoa Mswada wa Fedha wa 2024 ambao ulikuwa umependekeza Wakenya kutozwa ushuru mkubwa na kufuta baraza lake lote la mawaziri.

Siku ya Jumatano, Rais aliwateua wanasiasa wa upinzani katika baraza lake la mawaziri ambao watapigwa msasa na bunge.

Wanajumuisha mwenyekiti wa ODM John Mbadi (Hazina na Mipango ya Kitaifa) Wycliffe Oparanya (Biashara na Vyama vya Ushirika), Hassan Joho (Madini na Uchumi wa Baharini) na Opiyo Wandayi (Kawi na Petroli).

Dkt Ruto alikariri kuwa hatua yake itaunganisha taifa kwa manufaa ya Wakenya wote na kuipeleka nchi katika viwango vya juu vya maendeleo.

“Nimeamua tuunde serikali ambayo itatuunganisha sote ili kila Mkenya sasa ashiriki katika ujenzi wa taifa. Kuanzia sasa na kuendelea, sote tutatafuta njia za kuongeza mapato pamoja na kulipa madeni yetu. Hakuna atakayeachwa nyuma,” alisema.

Rais alizungumza Alhamisi katika mji wa Marimanti katika Kaunti ya Tharaka Nithi ambapo alizindua miradi ikijumuisha mradi wa maji wa Sh180 milioni katika eneo bunge la Kibung’a. Pia alizindua jengo la ofisi la kamishna wa kaunti na kituo cha Huduma.

Aliandamana na naibu wake Rigathi Gachagua, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki ambaye ameteuliwa kuhudumu katika wadhifa huo na Gavana wa Tharaka Nithi Muthomi Njuki.

Wengine walikuwa Naibu Spika wa Seneti Kathuri Murungi, Mwenda Gataya (Seneta Tharaka Nithi) mwakilishi wa wanawake wa Meru Elizabeth Kailemia na mwenzake wa Tharaka Nithi Susan Muindu, wabunge Gitonga Murugara (Tharaka), Mpuru Aburi (Tigania Mashariki) Patrick Munene (Igambang’ombe) na Kareke Mbiuki (Maara).

Dkt Ruto alimmiminia Prof Kindiki sifa na kumtaja kuwa mmoja wa mawaziri waliofanya kazi kwa bidii katika utawala wake, akisema hiyo ndiyo sababu aliyomteua kuhudumu katika baraza lake jipya la mawaziri.

“Prof Kindiki aliangamiza ujangili katika kaunti na alifanya kazi nzuri. Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii baadhi ya shule huko Baringo zilifunguliwa tena baada ya zaidi ya miaka 15. Pia alikabiliana na magaidi na kuhakikisha kuwa nchi yetu iko salama. Mtu akifanya kazi nzuri ni lazima apongezwe,” rais alisema.

Dkt Ruto aliahidi kuwa serikali yake itahakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa nchini na kuahidi ujenzi wa nyumba 500 katika makao makuu ya kaunti ya Tharaka Nithi mjini Kathwana.