Habari

Ruto asema baraka zikija 'watu waelewe'

May 30th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

NAIBU RAIS William Ruto ametoa ufafanuzi Alhamisi kuhusu michango na sadaka anazotoa kanisani, akisema hufanya hivyo kama njia mojawapo ya kumshukuru Mungu kwa umbali aliomtoa.

“Baadhi yetu unapotuona kanisani tukiinua mikono tukiomba na kutoa michango ni kwa sababu ya umbali ambao Mungu ametutoa. Mungu ametutoa mbali,” amesema Ruto.

Naibu Rais amesema hayo katika hafla ya maombi ya kitaifa yaliyofanyika katika mkahawa wa kifahari wa Safari Park ulioko jijini Nairobi.

Ruto akisimulia historia yake hasa akiwa mdogo, amesema alizaliwa katika familia maskini na hatua ambazo amepiga kimaisha ana kila sababu za kumshukuru Mungu.

“Ninakumbuka miaka ya sabini nilitembea bila viatu, ndio huyu mimi sasa katika meza moja na vijana wa kina baba waanzilishi wa taifa hili,” akasema.

Akionekana kusuta wakosoaji wake, Dkt Ruto amesema wanapaswa kuelewa baraka ambazo Mungu amewajalia.

“Tafadhali ninaomba muelewe, kwa sababu wakati mwingine hutuhukumu isivyofaa,” akasisitiza.

Kauli ya Ruto imejiri siku moja baada ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma DPP Noordin Haji kufanya mkutano na viongozi na makasisi wa dini mbalimbali nchini.

Bw Haji aliwasihi kukataa michango inayotiliwa shaka akidai inachochea kukithiri kwa ufisadi.

Alisema baadhi ya viongozi wanapora mali ya umma, na kutumia fedha hizo kufanya kampeni ya 2022 na zingine kwa manufaa yao binafsi.

“Pesa hizo pia zinapelekwa katika maeneo takatifu ili kupata uungwaji mkono na waumini,” alisema Bw Haji katika mkutano na viongozi hao wa dini uliofanyika Jumatano katika Serena Hotel jijini Nairobi.

Ushirikiano

Viongozi hao wa dini waliahidi kushirikiana na serikali katika vita dhidi ya ufisadi.

Katika hotuba ya Rais Kenyatta katika maombi ya kitaifa ya mwaka huu, na ambayo haikuzidi dakika kumi, amewasihi viongozi kutekeleza kwa matendo maneno wanayosema.

“Mimi leo sina mengi, nina mambo mawili pekee. La kwanza; ninamsihi mzungumze kiasi tu na kutia katika matendo mnayosema. Viongozi Kenya wana hulka ya kuzungumza bila kutekeleza kimatendo wanayosema,” akasema kiongozi wa taifa.

Suala la pili la Rais Kenyatta lilikuwa kuhusu amani Sudan Kusini, ikizingatiwa kuwa Rais wa nchi hiyo Salva Kiir amekuwa mmoja wa viongozi mashuhuri walioalikwa.

“Ndugu yangu Salva Kiir, wananchi wa Sudan Kusini wanahitaji amani. Walipopigania uhuru walipigania kupata amani,” akasema Rais.

Kwa muda, Sudan Kusini imekuwa ikipitia wakati mgumu hasa kutokana na mvutano wa serikali tawala na miungano ya upinzani.

Hafla hiyo ya maombi imehudhuriwa na zaidi ya viongozi na wageni mashuhuri 3,000 kutoka humu nchini na mataifa ya kigeni.

Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na Wiper Party Kalonzo Musyoka ni baadhi ya waliohudhuria.