Habari za Kitaifa

Mashtaka ya walioandamana yaondolewe, ukatili wa polisi uchunguzwe- Ruto


RAIS William Ruto ametangaza kuwa serikali itaondoa mashtaka dhidi ya watu wasio na hatia waliokamatwa wakati wa maandamano dhidi ya serikali.

Kiongozi wa nchi pia aliahidi kuhakikisha ukatili wa polisi wakati wa maandamano utachunguzwa na hatua za  haraka kuchukuliwa.

Akihutubia wanahabari katika Ikulu, Rais Ruto alisema washukiwa waliokamatwa wakati wa maandamano hata hivyo watafikishwa mahakamani.

“Ni kwa masikitiko makubwa ninalazimika kusema kwamba Wakenya wengi walipoteza maisha yao na wengine kujeruhiwa. Hivi sivyo demokrasia yetu inapaswa kuendelea,” akasema Rais Ruto.

“Watu wengi wamekamatwa na kushtakiwa kwa makosa mbalimbali. Mashtaka yataondolewa kwa watu wasio na hatia waliokamatwa wakati wa maandamano. Lakini washukiwa watafikishwa mahakamani na kuadhibiwa,” aliongeza.

Rais aliongeza kuwa serikali pia itatoa msaada unaohitajika kwa familia zilizopoteza wapendwa wao wakati wa maandamano hayo.

“Serikali itatoa usaidizi unaohitajika kwa familia zilizopoteza wapendwa wao. Maisha ya watu wasio na hatia yameharibiwa katika muda wa mwezi mmoja uliopita. Serikali itawasaidia watu hawa kupata afueni,” akasema Dkt Ruto.

Rais alikumbusha polisi nchini kutumia mamlaka yao kwa kufuata Katiba kikamilifu.

“Ukatili wowote wa polisi lazima uchunguzwe kwa haraka. Kama raia, tunapaswa kusawazisha  haki zetu ili tusiharibu  taifa letu lenye amani,” alisema rais.