Habari

Ruto ashambulia ODM kupendekeza Raila arithi Uhuru

June 15th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA, BENSON MATHEKA na JOSEPH WANGUI

VIONGOZI wa ODM wamechochea malumbano mapya na Naibu Rais William Ruto kwa kumtaka Rais Uhuru Kenyatta kuteua mrithi wake kwa uangalifu ili asiwe mtu fisadi wa kupora mali ya Wakenya.

Wakizungumza katika mazishi ya mama ya Gavana wa Kisumu Peter Anyang’ Nyong’o mnamo Ijumaa viongozi hao walisema ili kudumisha juhudi alizoanzisha za kupambana na ufisadi, Rais Kenyatta anafaa kuhakikisha kuwa atakayechukua hatamu za urais 2022 ni mtu mwadilifu.

“Nakuomba Mheshimiwa Rais uwe mwangalifu na kutafakari kwa kina kuhusu urithi ambao ataacha kwa kuhakikisha kuwa mrithi wako anaendeleza juhudi zako za kupambana na ufisadi wala si mtu atakayerudisha nyuma juhudi hizo. Shiriki nami kwenye maombi ili usituachie mtu ambaye ni mwizi,” alisema mwenyekiti wa ODM John Mbadi.

Hata hivyo, akiwa Nyeri, Bw Ruto aliwashutumu viongozi wa ODM kwa kumshinikiza Rais kumteua kiongozi wao Raila Odinga kuwa mrithi wake.

Akiongea Jumamosi katika Shule ya Upili ya St Bonventure Kaheti katika eneobunge la Mukurwe-ini, Dkt Ruto pia alipuuzilia mbali azma ya Bw Odinga kuwania urais katika uchaguzi ujao akisema ndoto hiyo haitatimia.

“Nataka kuwakosoa wale wengine mlioona wakisumbua Rais jana (Ijumaa) kule Kisumu. Jubilee ndiyo itaendelea na rekodi yake ya maendeleo wakati huo. Huyo wanayempendekeza kwa Rais hana rekodi ya maendeleo na hivyo atafeli kama miaka ya awali,” akasema.

Zaidi ya wabunge 10 ambao waliandamana na Dkt Ruto pia waliwaambia wenzao wa ODM wakome kumshinikiza Rais Kenyatta kutaja mrithi wake wakisema kwamba chama cha Jubilee tayari kina mipango kuhusu suala hilo.

“Rais Kenyatta ni kiongozi wa chama chetu cha Jubilee. Kwa hivyo, watu wa ODM hawafai kumshinikiza kumtaja mrithi wake kwingineko ilhali ni wazi kwamba mtu huyo si mwingine bali naibu wake, William Samoei Ruto,” akasema Mbunge wa Mukurweini Anthony Kiai.

Mnamo Ijumaa, Seneta wa Siaya James Orengo na mwenyekiti wa ODM John Mbadi waliwaongoza wenzao kumshinikiza Rais Kenyatta kutomteua Dkt Ruto kuwa mrithi wake wakidai amekuwa akihujumu vita dhidi ya ufisadi.

Waliunga mkono muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga wakisema umeleta amani na utulivu katika eneo hilo na wakaahidi kuwaunga mkono.

‘Inafurahisha kwamba wewe Rais sasa unaweza kushiriki jukwaa mmoja na Bw Odinga. Kabla ya hapo haikuwa rahisi kwangu kuishi nyumbani kwa amani. Sasa ninaweza kulala kwa utulivu,” akasema Seneta wa Siaya James Orengo.

Alisema ODM ina imani kuwa viongozi hao wawili wataongoza taifa hili katika enzi mpya ikiwemo kura ya maamuzi. Dkt Ruto amekuwa akipinga kura ya maamuzi na jinsi vita dhidi ya ufisadi vinaendeshwa.

Aidha, viongozi wa ODM wamekuwa wakiendeleza shinikizo za kutaka kufanywe mabadiliko ya Katiba ili kubadili mfumo wa uongozi naye Bw Ruto akisema wanalenga kutengea watu fulani nyadhifa za uongozi.

“Hii ndiyo maana tunaunga mkono kamati ya maridhiano (BBI) inayoendeleza mipango ya kuhakikisha kuwa amani na utulivu unadumu nchini,” akasema Bw Orengo.

Alisema ingawa Rais Kenyatta amewashauri wanasiasa kusitisha siasa za uchaguzi wa 2022 na kuzingatia mpango wa kujenga nchi pekee, viongozi wa Jubilee hawaonekani kutii ushauri huo.