Habari za Kitaifa

Serikali kuajiri wahudumu zaidi wa afya kufaulisha UHC

May 12th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI imeahidi kuajiri wahudumu zaidi wa afya katika sekta ya afya ili kupiga jeki mpango wake wa kuafikia azma ya Afya kwa Wote (UHC).

Rais William Ruto ambaye akikutana na viongozi wa Chama cha Madaktari Nchini (KMPDU) Jumamosi katika Ikulu ya Nairobi, alikariri kuwa serikali ya Kenya Kwanza imejitolea kuhakikisha kuwa sekta ya afya ina idadi tosha ya wahudumu ili kuimarisha utoaji huduma kwa Wakenya.

“Serikali imejitolea kushughulikia tatizo la uhaba wa wahudumu ambao unachelewesha uafikiaji wa Mpango wa Afya kwa Wote. Kwa kushauriana kila mara na wadau, haswa vyama vya kutetea masilahi ya wafanyakazi, tunalenga kuendeleza utulivu katika sekta ya afya na kupata suluhu kwa changamoto zinazotukabili,” akasema Dkt Ruto.

Hata hivyo, Rais hakusema ni lini wahudumu hao wa afya wataajiriwa wala kiasi cha fedha zilizotengwa kufadhili uajiri wa wahudumu hao.

Mkutano huo wa Ikulu, kati ya viongozi wa KMPDU na Rais Ruto, unajiri siku chache baada ya madaktari kufutilia mbali mgomo ambao ulikuwa umedumu kwa siku 56.

KMPDU ilikubali kuwa wanachama wake watarejelea kazi baada ya kutia saini makubaliano ya kurejea kazini na Serikali Kuu na serikali za kaunti mnamo Mei 8, 2024.

“Mgomo umefutiliwa mbali na madaktari wanapaswa kurejelea kazini haraka iwezekanavyo,” Katibu Mkuu wa KMPDU Davji Atellah akasisitiza.

Masuala makuu yaliyochangia mgomo huo ni malipo ya madaktari wanafunzi, mazingira mabaya ya utendakazi, uhaba wa madaktari wa kutosha katika hospitali za umma na makubaliano kuhusu nyongeza ya mishahara (CBA) yaliyotiwa saini mwaka 2017.

Hata hivyo, wakati wa kutiwa saini kwa makubaliano ya kurejea kazini, Dkt Atella alisema kuwa suala kuhusu malipo ya madaktari wanagenzi halikusuluhishwa kwa sababu liko kortini.

Katibu huyo mkuu alisema KMPDU ilikubaliana na serikali kuwa siku 60 zitengwe za kushughulikia suala hilo kwa msingi kuwa lingali mahakamani.