Habari Mseto

Serikali saidia, king’ora chalia Gatong’ora Ruiru, mafuriko na majitaka yakikera wakazi

April 23rd, 2024 2 min read

NA LABAAN SHABAAN

AGHALABU jamii hutarajia mvua kuwa baraka kwao ila hali si hivyo kwa wakazi wa mtaa wa Gatong’ora eneobunge la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Mvua iliyoponda jiji la Nairobi na viunga vyake wikendi imesababisha taswira inayoweka hali ya miundomsingi ya majitaka, mijengo na barabara kwenye mizani.

Wakazi wa Gatong’ora wanalazimika kuweka mawe kwenye vidimbwi vya maji barabarani ili kuweza kutembea.

Huku wengine waking’ang’ana kutembea, upande mwingine magari yanakwama majini.

Ni picha ya masaibu yenye aibu kwa wakazi na jumuiya ya uongozi inayofaa kuweka miundombinu thabiti kukinga wananchi dhidi ya majanga.

Maji ya mvua yazingira makazi na jengo la ibada na kuwawia wakazi vigumu kupita. PICHA | LABAAN SHABAAN

“Yaani serikali ya Kaunti ya Kiambu hupita hapa karibu kila siku lakini hawaoni haja ya kuimarisha mfumo wa majitaka!” alisikitika mkazi mmoja aliyetuomba tubane utambulisho wake.

Baadhi ya mabomba ya majitaka yalikuwa yamejaa pomoni huku maji yakimwagika barabarani kuumba vidimbwi.

Mengine yalitiririka na hata kuzuia watu kuingia katika makazi na makanisa yaliyoundwa kwa mabati bila msingi imara.

“Angalia sasa; mtu akitaka kuingia nyumbani anapita wapi?” Rose Migwi ambaye hufanya biashara ya kuuza mboga alisikitika.

“Tunaomba serikali isuluhishe suala la maji kufurika nyumbani na barabarani kikamilifu. Kila mara wanakuja kuunda mabomba ya majitaka lakini bado hali ni ile ile,” aliongeza.

Baadhi ya barabara pia ziko katika hali mbovu hata nyakati za kiangazi. Na mvua inaponyesha, taswira huwa mbaya zaidi kwa wakazi.

Wanabiashara wanaochuuza mboga, vyakula katika vibanda na wengine wanaochoma mahindi pia wanalalama.

Taifa Leo imebaini kuwa kuvuja kwa mabomba ya majitaka kumewafanya wachuuzi kuhamahama wakitafuta sehemu nyingine ya kufanyia biashara: tukio ambalo linawapotezea wateja.

Wakazi wasukuma lori lililokwama baada ya maji ya mvua kuharibu barabara. PICHA | LABAAN SHABAAN

“Wateja hawawezi kuja katika biashara yako kama wanasikia harufu hii mbaya,” aliteta Migwi.

Matatizo haya yamefanya baadhi ya wanabiashara kuacha biashara ya vibanda na kutafuta shughuli nyingine ya kujikimu.

Katika pitapita zetu, tuliona kibanda kilichoharibika na kuachwa kwa sababu ya matatizo ya maji kufurika na majitaka kuenea.

Vile vile, bustani ya miti ambayo pengine ingefaa kuwa sehemu nzuri ya kujivinjari na kutulia imejaa maji.

Karibu na hapa, bomba la majitaka limevuja na kutiririsha maji katika eneo pana.

Kilio cha wakazi hawa kinaelekezwa kwa ofisi ya mbunge wa Ruiru na Serikali ya Kaunti ya Kiambu.

Wakazi wanataka barabara na mfumo wa maji ukarabatiwe kuwakinga dhidi ya majanga yanayowatwanga sasa na kila mara