Habari za Kaunti

Serikali yafunga viwanda vitatu vya gesi Murang’a

February 7th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

KAMATI ya usalama ya Murang’a Kusini ikiongozwa na Naibu Kamishna Gitonga Murungi ambaye pia ndiye mwenyekiti, imefunga kampuni tatu za kupakia gesi ya kupikia.

Hii ni baada ya operesheni ya kupiga msasa kampuni hizo pamoja na vituo vyao vya mauzo.

Kampuni hizo ni Nugge, Virji, na Tanga ambazo amri imetolewa zisitishe huduma mara moja.

Licha ya kwamba msako huo unajiri baada ya mlipuko wa gesi katika eneo la Embakasi jijini Nairobi ambao ulisababisha vifo vya watu sita na kujeruhi wengine 300, Bw Murungi alishikilia kwamba lengo ni kupambana na bidhaa ghushi pamoja na wale wanaokwepa kulipa ushuru.

Fukuto la moshi kutokana na mlipuko wa gesi Embakasi, Nairobi, Kenya, mnamo Februari 1, 2024. PICHA | REUTERS

“Ilani sasa imetolewa kwamba kampuni hizo zisitishe biashara katika eneo hili mara moja na zitakubaliwa kurejea iwapo zitaafikia viwango vya kisheria kama vilivyowekwa,” akasema Bw Murungi.

Kamishna huyo aliongeza kwamba kampuni ya Virji haina hata chembe cha utiifu kwa sheria za kuhudumu na cha kukera zaidi, huvumisha huduma zake ndani ya makazi ya wapangaji.

“Kampuni hii hata haina leseni yoyote ya kutoka kwa Mamlaka ya Kudhibiti biashara ya Kawi na Petroli (Epra) ama ile ya kudhibiti masuala ya mazingira (Nema). Kwa ufupi, ni kampuni haramu kwa kiwango cha asilimia 100,” akasema.

Kampuni ya Tanga nayo inadaiwa kukosa leseni za uhifadhi, upakiaji na usafirishaji wa gesi hiyo ya mapishi pamoja na kuwa na uchukuzi haramu wa wafanyakazi wake.

Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini Gitonga Murungi akihutubia wakazi. PICHA | MWANGI MUIRURI

Aidha, barua yao ya usajili ilipatikana kuwa ya kiwanda kingine katika eneo tofauti.

Kilichojiri katika kampuni ya Nugge ni kwamba wasimamizi wake walipata fununu ya operesheni hiyo ya msasa na wasimamizi wake wakaingia mitini.

“Hata hivyo, ni bayana kwamba kiwanda hicho kiko katika makazi ya umma na majengo hayana mikakati ya kiusalama na kwa hayo tu, kinaamrishwa kufunga huduma,” akasema Bw Murungi.

Vituo vya mauzo vilivyopigwa msasa ni Nugge, Tanga, na Rubis katika mji wa Kenol. 

Alisema misako hiyo itadumu hadi masharti na sheria kutimizwa na wote walio katika biashara za kawi eneo hilo.