Habari za Kaunti

Shughuli muhimu zakwama Chuo Kikuu cha Rongo

Na VICTOR RABALLA September 2nd, 2024 1 min read

KUTOKAMILISHWA kwa miradi muhimu ya maendeleo kunaendelea kukwamisha shughuli za masomo na hudumA nyinginezo katika Chuo Kikuu cha Rongo, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameonya.

Bi Nancy Gathungu alisema mradi wa ujenzi wa jengo la maktaba lililotarajiwa kugharimu Sh1.3 bilioni halijakamilika tangu kuanzishwa kwake Januari 15, 2021.

“Shughuli ya uthibitishwaji iliyoendeshwa Desembe 2023, ilibaini kuwa mradi huo haujakamilika. Sasa muda wa kukamilishwa kwake umeongezwa hadi Februari 2025,” akasema katika ripoti yake ya hivi punde.

Hata hivyo, Taifa Dijitali imebaini kuwa shughuli za ujenzi wa jengo hilo hazijarelewa ilhali tarehe ya makataa ya Februari 2025 inakaribia.

Kulingana na ripoti ya ukaguzi wa mwaka uliokamilika Juni 30, 2023, Chuo Kikuu cha Rongo kilimpa mwanakandarasi fulani wa eneo hilo zabuni ya ujenzi kwa gharama ya Sh1, 358, 342, 492 huku tarehe ya kazi kuanza ikiwa Januari 4, 2019.
Matokea ya ukaguzi wa rekodi yanaonyesha kuwa awali mwanakandarasi huyo aliomba muda wa mwaka mmoja mnamo Machi 12, 2021.

Lakini tangu wakati huo, hajakamilisha mradi huo wenye umuhimu mkubwa kwa Chuo hicho cha Rongo kilichopewa cheti cha kutambuliwa rasmi mnamo 2016. Vilevile, mradi wa ujenzi wa kidimbwi cha kufugia samaki katika chuo hicho haujakamilika.

Ukaguzi uliofanywa na maafisa wa afisi ya Bi Gathungu katika mradi huo Desemba 2023 ulibaini utekelezaji wake umecheleweshwa pakubwa kwani ulitekelezwa kwa kiwango cha asilimia 45 pekee kufikia Juni 30, 2023.

Maafisa hao walipofika katika eneo la mradi, shughuli za ujenzi hazikuwa zikiendelea ishara ya kukwama kwake.

Zabuni ya Sh4.5 milioni ya ujenzi wa kidimbwi hicho pia ilipewa mwanakandarasi mmoja wa eneo hilo kulingana na ripoti ya ukaguzi ya Bi Gathungu.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga