BBI: Raila apuuza mapendekezo ya viongozi wa kidini
LEONARD ONYANGO Na BENSON MATHEKA
KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amepuuzilia mbali mapendekezo ya viongozi wa makanisa wanaotaka mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) urekebishwe kabla ya kuwasilishwa kwa kura ya maamuzi.
Bw Odinga jana alisema viongozi wa makanisa walitoa mapendekezo yao mbele ya jopokazi la BBI, na kwa hivyo, hawafai kuwasilisha maoni mengine.
Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini, viongozi wa Baraza la Miungano ya Makanisa (KCCAM) na Muungano wa Makanisa ya Kievanjelisti Kenya (EAK) wametoa orodha ya mambo wanayotaka yabadilishwe katika mswada wa BBI.Maaskofu hao walitaka kuwe na mdahalo wa kitaifa kuhusu masuala tata kabla ya kura ya maamuzi.
Walisema kuna haja ya mazungumzo kuhusu kuundwa na Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC), kuanzishwa kwa baraza la polisi, kuongozwa kwa idadi ya wabunge na uhuru wa mahakama miongoni mwa masuala mengine tata.
Nao viongozi wa EAK na KCCAM, Askofu Mark Kariuki, Askofu Kepha Omae na Askofu Stephen Mutua, walisema kuwa pendekezo la BBI kuwa waziri wa Usalama awe akiongoza Baraza la Kitaifa la Idara ya Polisi, halifai.Kulingana nao, hatua hiyo itatoa mwanya kwa rais kutatiza uhuru wa Idara ya Polisi.
Viongozi hao pia walipinga kufutiliwa mbali kwa wadhifa wa wawakilishi wa wanawake.“Pendekezo la BBI kwamba wanawake wanaochaguliwa katika Kaunti wahudumu katika Seneti halifai kwa sababu watapoteza usemi katika kufanya maamuzi muhimu ya taifa katika Bunge la Kitaifa,” wakasema viongozi hao.
Aidha, wanataka Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kuandaa kongamano la kitaifa ili kuwezesha Wakenya kutatua mambo yenye utata yaliyomo ndani ya ripoti ya BBI.
Walisema kuwa wameandaa orodha ya mapendekezo yao ambayo watayawasilisha kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga.Jana, Bw Odinga aliwaambia kwamba mapendekezo ya ripoti hiyo hayatabadilishwa kamwe.
“Viongozi wa kidini walikuwa na muda wa miaka miwili kuwasilisha mapendekezo yao. Hakuna mapendekezo mapya yatakayoongezwa kwenye ripoti ya BBI. Hayo ni maoni yao, sisi tutaendelea na mapendekezo ya wengi yaliyomo kwenye ripoti,” akasema Bw Odinga alipokuwa akizungumza jana katika afisi yake katika Jumba la Capitol Hill.
Lakini licha ya kusema hayo, anaendelea kukutana na makundi yanayotaka masuala kadhaa yazingatiwe.Kati ya leo na Jumatatu, atakutana na wawakilishi wa magavana. Jumanne, Bw Odinga atakutana na wawakilishi wa wanawake na viongozi wa jukwaa la madiwani.
Hata hivyo, hakufichua ikiwa Rais Kenyatta atahudhuria vikao hivyo.Bw Odinga pia hakudokeza ikiwa watakubali kuongeza mapendekezo mapya ya magavana na madiwani kwenye mswada wa BBI baada ya kukutana.
Waziri Mkuu wa zamani alisema kuwa shughuli ya kukusanya saini zitakazowasilishwa kwa IEBC kuunga mswada utakaowasilishwa kwa kura ya maamuzi itazinduliwa mwishoni mwa wiki ijayo.
“Baada ya kukusanya angalau saini milioni moja zinazohitajika, tutapeleka mswada wa BBI kwa IEBC na kisha upelekwe kwa mabunge ya kaunti,” akasema.Kura ya maamuzi kubadili Katiba itafanyika Aprili, mwaka ujao, kwa mujibu wa Bw Odinga.
Mbali na viongozi wa kidini, magavana wanataka watengewe fedha za kiinua mgongo baada ya kustaafu. Magavana pia wanapendekeza waruhusiwe kuteua manaibu wao baada ya kuchaguliwa tofauti na sasa ambapo wanachaguliwa pamoja.
Mswada wa BBI unapendekeza kuwa gavana na naibu wake wawe watu wa jinsia tofauti.
Nao madiwani wanataka wateuliwe mawaziri wa kaunti, waongezewe pesa za hazina ya wadi iliyopendekezwa kutoka asilimia tano hadi asilimia 30 miongoni mwa matakwa mengine.