HAMNITISHI: Joho awajibu wakosoaji wake
MOHAMED AHMED na VALENTINE OBARA
GAVANA wa Mombasa, Hassan Joho amepuuzilia mbali viongozi ambao wamekuwa wakimkosoa kwa hatua anazochukua kuepusha ueneaji virusi vya corona katika kaunti yake.
Licha ya Bw Joho kusifiwa na wengi kitaifa, ikiwemo Rais Uhuru Kenyatta kwa juhudi zake, kumekuwepo wanasiasa wa Mombasa ambao hudai anajifanyia mambo bila kujali athari kwa wakazi, wala kuwahusisha viongozi wenzake.
Wakosoaji wake hudai kuwa Bw Joho anataka kuonekana yeye ndiye anayebuka kidedea katika kupambana na janga hili ambalo limeathiri dunia nzima, na anatumia fursa hiyo kumwandaa mwanasiasa na mfanyabiashara Hussein Shahbal kumrithi ifikapo mwaka wa 2022.
Mmoja wa viongozi aliyejitokeza wazi kumpinga gavana huyo ni Mbunge wa Nyali Mohammed Ali ambaye hudai Bw Joho anafanya maamuzi mengi anayofaa kuwaachia maafisa wa masuala ya afya.
Mnamo Alhamisi, gavana huyo alisema hatababaishwa na mahasimu wake kwani amejitolea kuokoa maisha ya wananchi.
“Tuna jukumu la kuokoa maisha ya watu wetu. Hatutachanganywa na vitimbi. Tutajishughulisha katika kusaidia maisha ya watu wa Mombasa. Hilo ndilo jukumu letu,” akasema.
Alitoa wito kwa viongozi wote na wanaharakati mjini humo kushirikiana wakati huu wa janga la corona.
Wachanganuzi wa siasa eneo la Pwani wanahoji kuwa, Bw Joho anapata maadui wakati huu kwa vile anavyoonekana akichapa kazi kivyake.
Prof Hassan Mwakimako, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za Pwani, anasema kuna dhana inayoenea kwamba Joho hataki kushirikiana na wenzake.
“Ni wazi kuwa Bw Joho ametekeleza juhudi ambazo zinaonekana kila mahali, lakini kwa sababu ameonekana kuwa hataki kusikiza mtu na kila anachosema yeye ndio kitafanyika ndio maana anaanza kupata upinzani,” akasema Prof Mwakimako.
Alisema misimamo ya Bw Joho wakati wote wa janga hili imemfanya aonekane kama kwamba ni yeye alichochea serikali kuu kufunga Old Town ghafla.
“Shida ni vile amezoea kuonekana mbele, ndiyo maana hata kazi ambayo anegekuwa ametuma waziri wake wa afya tunamwona anafanya mwenyewe. Lakini hiyo ni kwa sababu ya namna alivyojizoesha katika siasa zake,” akaongeza Prof Mwakimako.