• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
JAMVI: Abagusii hatimaye wapata kigogo awaongoze kisiasa

JAMVI: Abagusii hatimaye wapata kigogo awaongoze kisiasa

Na VALENTINE OBARA

BAADA ya kukaa miaka mingi bila kigogo mahiri wa kuwaongoza kisiasa, jamii ya Wakisii sasa imeweka matumaini yao kwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i.

Suala linaloibuka ni kama, Dkt Matiang’i, ambaye kufikia sasa hajatangaza wazi malengo yake ya kisiasa, atafanikiwa kuziba mgawanyiko ambao umekuwa ukikumba jamii hiyo kila wakati wa uchaguzi mkuu.

Kwa mujibu wa wadadisi wa kisiasa, ni mgawanyiko huo ambao hufanya jamii ya Wakisii kuwa miongoni mwa janibu zinazovutia wagombeaji urais ambao hulenga kujijazia kura kapuni mwao baada ya kuzoa tele katika ngome zao za kisiasa zinazopiga kura za urais kwa umoja.

Katika miaka iliyotangulia, vigogo wa kisiasa waliotoa mwelekeo wa kisiasa katika jamii hiyo ni mawaziri wa zamani Zachary Onyonka aliyefariki mwaka wa 1996, Simeon Nyachae aliyestaafu siasa mwaka wa 2007 na Seneta wa Kisii Prof Sam Ongeri.

Lakini hata wakati huo jamii hiyo ilikuwa haipigi kura za urais kwa umoja.

“Itakuwa changamoto kubwa kwa Matiang’i kushawishi jamii yake ichague mgombeaji wa urais kwa umoja ifikapo 2022. Jamii hiyo hufahamu ni vigumu kwao kuwa na mgombeaji urais au hata mgombea mwenza kwa hivyo wanasiasa eneo hilo hutaka kuelekeza wapigakura upande ambao wanaamini utashinda urais,” asema mchanganuzi wa kisiasa, Bw Holo Oiro.

Kulingana na Bw Oiro, si rahisi kushawishi wapigakura wote kwamba mgombeaji fulani ndiye anayetarajiwa zaidi kushinda urais, hasa katika jamii ambapo kila ukoo na wanasiasa wana malengo yanayotofautiana.

Alizidi kusema kuwa jamii ya Wakisii imekuwa na bahati katika kila utawala kwani huwa hawaachwi nje ya serikali bali hupata nyadhifa kubwa kubwa serikalini bila kujali jinsi wanavyopiga kura za urais. Hivyo basi, ni vigumu kushawishi wapigakura kuwa watakosa rojo za utawala wakipiga kura kwa njia fulani.

Kwa sasa Naibu Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga ndio wanaotarajiwa kushindana kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ifikapo mwaka wa 2022. Katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2017, Rais Kenyatta alipata kura 174, 978 (asilimia 43.22) naye Bw Odinga akapata kura 224,317 (asilimia 55.40) katika Kaunti ya Kisii.

Katika Kaunti ya Nyamira ambayo pia ni eneo la jamii ya Wakisii, Rais Kenyatta alipata kura 101,113 (asilimia 52) naye Bw Odinga akapata kura 90,315 (asilimia 46) katika uchaguzi huo.

“Inavyoonekana ushindani wa mwaka wa 2022 ni kati ya Ruto na Raila. Upande wowote ule ambao Matiang’i ataegemea, bado kura za Wakisii zitagawanyika,” ahoji Bw Oiro. Dkt Ruto tayari ana viongozi wa kisiasa katika jamii hiyo wanaompigia debe huku akizindua miradi mingi eneo hilo, na vilevile Bw Odinga ana kikosi chake.

Baadhi ya wanasiasa wa Kisii ambao wamejitokeza wazi kumtangaza Dkt Matiang’i kama kiongozi wao halisi wa kijamii wameonyesha ishara kwamba hawataunga mkono azimio la Dkt Ruto, lakini wengine wanasema wako tayari kushauriana na mgombeaji yeyote.

“Tunataka wakati jamii nyingine zinapoanza kujipanga kuhusu uongozi wa Kenya, sisi nasi lazima tuwe kwenye hiyo meza. Hakuna mtu tunayesema asije hapa, kila mtu yuko huru kuja vile anataka lakini tunataka ukija lazima ujue yule utamwongelesha kwani hata kwenu wewe ndiwe tunayekuongelesha,” Mbunge wa Kitutu Chache Kusini, Bw Richard Onyonka alisema wikendi iliyopita.

Itakumbukwa kuwa uhusiano wa Dkt Matiang’i na Naibu Rais hasa katika siku za hivi majuzi haujawa mwema kwa muda mrefu na hivyo basi jinsi hali ilivyo kwa sasa hawatarajiwi kushirikiana kisiasa. Wandani wa Dkt Ruto hutishia kuwasilisha hoja bungeni kumng’oa mamlakani wakidai anatumia mamlaka yake kumhanganisha Naibu Rais, naye Bw Odinga ameibuka katika siku za hivi majuzi kuwa mtetezi mkubwa wa Dkt Matiang’i.

Miongoni mwa wanasiasa ambao wameonyesha nia ya kutaka jamii ya Wakisii isimfuate Dkt Ruto ni Mbunge wa Nakuru Magharibi, Bw Samuel Arama.

Bw Arama alisema ingawa wanaamini Dkt Matiang’i ametosha kuwania urais, wamejitolea kumuunga mkono mgombeaji urais atakayetoka katika kabila ambalo halijawahi kuongoza nchi hii.

“Kile tunachosema ni kuwa yule tutakayempa kura katika jamii ya Wakisii lazima aje afike karibu nasi. Hatuwezi kusema eti sasa urais unazunguka kwa makabila mawili pekee. Sisi tunataka wakati huu tupatie urais wa 2022 yule mtu anayeweza kutuongoza vizuri na atoke kabila lingine,” akasema.

Alikuwa akizungumza kwenye harambee iliyohudhuriwa na Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua katika Shule ya Msingi ya Tindereti iliyo eneobunge la Borabu, Kaunti ya Nyamira wiki iliyopita.

You can share this post!

Uhuru aendelea kutua katika ngome kuu za Raila

Bwire shujaa akiongoza Sharks kurarua Everton mbele ya...

adminleo