Siasa

JAMVI: Ushirika mpya wa Muthama na Kibwana mwiba kwa Kalonzo

July 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na BENSON MATHEKA

USHIRIKA mpya wa kisiasa kati ya aliyekuwa Seneta wa Machakos bwanyenye Johnson Muthama na Gavana wa Makueni, Prof Kivutha Kibwana, ni pigo kwa juhudi za kiongozi wa Wiper, Bw Stephen Kalonzo Musyoka za kuunganisha ngome ya Ukambani nyuma yake.

Wadadisi wanasema kuungana kwa wawili hao ambao walikuwa mahasimu wa kisiasa zimemkosesha usingizi Bw Musyoka ambaye ananuia kutumia umaarufu wake eneo hilo kugombea urais.

Bw Muthama alikihama chama cha Wiper na kutangaza kuwa atazindua chama chake kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022, naye Prof Kibwana akatangaza kuwa atagombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo.

Wawili hao walitangaza mipango yao siku chache baada ya kufichua kuwa wamekuwa wakikutana kujadili siasa na maendeleo katika eneo la Ukambani.

Kulingana na wadadisi wa siasa za eneo hilo, kuungana kwa wawili hao kulichochewa na hatua ya Musyoka kuongoza chama chake cha Wiper kushirikiana na Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta bila kuwashirikisha viongozi wa eneo hilo.

“Ubinafsi wa Bw Musyoka umefanya atemwe na viongozi waliosimama naye kwa miaka mingi. Walikasirika alipoamua kivyake kuwa mtu wa mkono wa Rais Kenyatta bila kujali maslahi ya jamii yake. Kwao, aliacha wadhifa wake kama kiongozi wa jamii ili kutimiza maslahi yake ya kibinafsi. Walichotaka ni kuwepo kwa mazungumzo ya kina na mkataba wa kuhakikisha jamii ingefaidika na ushirikiano huo lakini Bw Musyoka aliwapuuza na kuwaambia kwamba hataki kuulizwa maswali,” alisema mdadasi wa siasa Jacob Kiilu.

Baada ya Bw Musyoka kutangaza kuwa atakuwa mtu wa mkono wa Rais Kenyatta, Prof Kibwana alikuwa wa kwanza kumkemea na kumlaumu kwa kutelekeza jamii.

Kulingana na gavana huyo ambaye alikuwa mwenyekiti wa Wiper wakati huo, hatua ya Bw Musyoka ilionyesha kuwa alikuwa ametupilia mbali azma yake ya kuwa Rais.

Alijiuzulu kama mwenyekiti wa Wiper na kuungana na magavana wa kaunti za Machakos, Dkt Alfred Mutua na Bi Charity Ngilu wa Kitui kumshambulia Bw Musyoka wakimlaumu kwa ubinafsi na kutojali jamii.

Juhudi za Bw Muthama za kuleta viongozi wote wa Ukambani pamoja ziliambulia patupu na sasa anamlaumu Bw Musyoka kwa kupuuza ushauri wake.

“Nilifadhili Wiper, chama ambacho nilikuwa mmoja wa waanzilishi wake kwa sababu nilidhani kingetetea maslahi ya jamii. Maoni ya viongozi yalipuuzwa kikawa chama cha mtu mmoja na familia yake hadi akatangaza kuwa atakuwa mtu wa mkono wa Uhuru. Kiongozi wa jamii akiwa mtu wa mkono wa mtu mwingine, jamii itafaidika na nini?” Bw Muthama amekuwa akiuliza.

Alisema kwamba alihama chama cha Wiper alipokataa kutetea kiti cha useneta wa Kaunti ya Machakos kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 kwa sababu ya uteuzi uliovurugwa.

Bw Kiilu anasema tangazo la Bw Muthama kwamba atakuwa na chama chake 2022 na ukuruba wake mpya na Prof Kibwana vitamkosesha usingizi Bw Musyoka.

“Kwanza, watamnyima Musyoka umaarufu ambao amefurahia walipokuwa wakimuunga mkono. Ikizingatiwa Muthama ni mtu wa mifuko mizito na mwanasiasa mweledi, si ajabu akawavutia wanasiasa wa Wiper upande wake kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Kugawanyika kwa wanasiasa wa Ukambani kutamnyima Bw Musyoka ushawishi wake katika siasa za kitaifa,” alisema Bw Kiilu.

Mbunge mmoja wa chama cha Wiper ambaye aliomba tusitaje jina lake alisema kutofautiana na Bw Muthama ni pigo kwa Musyoka.

“Ninaweza kukuhakikishia kwamba iwapo upepo wa siasa za Ukambani hautabadilika, ushawishi wa Bw Musyoka eneo hilo utafifia wakati Muthama atakapozindua chama. Wengi wetu tunasubiri wakati ufaao tutangaze msimamo,” alisema mbunge huyo.

Duru zinasema kwamba Gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu anaunga azma ya Prof Kibwana ya kugombea urais.

Gavana huyo amekuwa akimlaumu Bw Musyoka kwa kuchochea madiwani wa chama chake cha Wiper ili wamuondoe ofisini.

Walipokutana wiki mbili zilizopita, Muthama na Kibwana walisema walijadili mswada wa kumtimua Bi Ngilu ofisini.

Ingawa wandani wa Bw Musyoka wanasema Bw Muthama alikasirika kiongozi wa Wiper alipokataa kumuunga Naibu Rais William Ruto, wadadisi wanasema tofauti zao zilianza 2017 kufuatia uteuzi wa wagombeaji wa chama hicho.

Mwaka 2019 Bw Muthama alitangaza kuwa alikuwa akiongoza mazungumzo kwa lengo la Musyoka kushirikiana na Dkt Ruto, madai ambayo Makamu Rais huyo wa zamani alikanusha na kusisitiza kuwa anamuunga Rais Kenyatta.

Juzi alisisitiza kuwa hatajali iwapo Rais Kenyatta atakuwa waziri mkuu Katiba ikifanyiwa mageuzi kupitia Mchakato wa Maridhiano (BBI) ambao Bw Muthama hajauchangamkia.

Wadadisi wanasema kwamba vita vya ubabe wa kisiasa eneo la Ukambani vitachukua mkondo mpya kufuatia ushirikiano wa Kibwana na Muthama. Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua ambaye pia ametangaza kwamba atagombea urais, ni hasimu wa kisiasa wa Bw Muthama na amekuwa akishirikiana kwa karibu na Kibwana kumpiga vita Bw Musyoka.