Siasa

Jubilee yatangaza itaunga Kalonzo 2027 ikikemea Ruto na Raila kwa ‘kugawanya Mlima’

Na PAUL MUTUA October 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA cha Jubilee kimetangaza kuwa kitamuunga mkono Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kama mwaniaji wa urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni Jumapili alisema wana uhakika kuwa Bw Musyoka atasimama na kumlemea Rais William Ruto debeni kwa urahisi.

Alisema kuwa hatua ya Rais Ruto kutumia uimla kumwondoa Rigathi Gachagua kama naibu rais ni ishara tosha kuwa hathamini uungwaji mkono alioupata kutoka Mlima Kenya mnamo 2022.

Bw Kioni alisema kuwa Jubilee ambayo ni chama tanzu ndani ya Muungano wa Azimio, imeafikia uamuzi huo wala hawatafuti mwaniaji mwengine wa urais 2027.

“Kama Jubilee hatumtafuti mwaniaji mwengine wa urais kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa sababu tuna Kalonzo. Ombi letu kwa Wakenya ni kuwa wawe nyuma ya Kalonzo ili tuondoe utawala huu dhalimu wa Ruto,” akasema Bw Kioni.

Alikuwa akiongea kwenye Kanisa AIC mjini Mwingi, Kitui wakati wa ibada ambayo pia ilihudhuriwa na makamu huyo wa rais wa zamani. Alisema kwa sasa Rais na Kinara wa Upinzani Raila Odinga wameungana kuhakikisha kuwa Bw Gachagua anaondolewa mamlakani.

Pia alizua kumbukumbu za ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 ambapo alidai Ruto na Raila waliungana kumhangaisha Rais Mwai Kibaki kisha kuingia mamlakani kwa mlango wa nyuma.

Alimrejelea Bw Musyoka kama kiongozi mwenye hekima ambaye wakati huo alitumia ushawishi wake kumwokoa Rais Kibaki baada ya kuteuliwa makamu wa Rais.

“Kwa sasa njama ya Raila na Ruto ni kugawanya Mlima Kenya ili ifikapo uchaguzi wa 2022, eneo hilo lisiwe na umoja wa kisiasa. Hata hivyo, tunawaambia kuwa tunafuatilia kwa makini na tunazielewa karata zao,” akasema Bw Kioni.

Aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinard Waititu alisema kuwa mwelekeo ambao Mlima Kenya sasa unastahili kuchukua ni kuungana na Bw Musyoka ambaye anatoka ukanda wa Mashariki ya Chini.

Aliposimama kuhutubu, Bw Musyoka alishukuru Jubilee kwa uungwaji mkono huo akiahidi kuwa lazima atakuwa mrengo moja wa kisiasa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta mnamo 2027.

Aliongeza kuwa mara hii, eneo la Ukambani litaelekeza kura zake mahali ambapo ndugu zao Mlima Kenya watakuwa wala hawatamuunga mkono Rais Ruto au Raila.

Alijinadi kama mwanasiasa ambaye hana doa la ufisadi na mtu ambaye amesaidia kurejesha amani katika mataifa mbalimbali ndiposa anatosha kuongoza nchi.

“Kila Mkenya lazima azinduke na kukataa utawala wa Rais Ruto ambao unawakandamiza Wakenya. Sote tunastahili kukataa udikteta huu,” akasema Bw Musyoka.

Seneta wa Kitui Enoch Wambua alisema kuwa 2027 ni wa Kalonzo na Wiper itaingia kwenye mikataba mingine ya kisiasa na vyama vingine kabla ya uchaguzi huo wa 2027.

Viongozi wengine ambao walipigia Kalonzo debe ni Mbunge Mwakilishi wa Kitui Irene Kasalu na mwenzake wa Mwingi ya Kati Gideon Mulyungi.