Siasa

Majonzi Nyagarama akizikwa na sifa tele

December 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DIANA MUTHEU

GAVANA wa Kaunti ya Nyamira, Bw John Nyagarama, alizikwa jana huku viongozi mbalimbali nchini wakimsifia kwa juhudi alizofanya kuendeleza Kaunti hiyo na jamii kwa jumla.

Viongozi hao ambao waliungana na waombolezaji pamoja na familia ya marehemu katika safari ya mwisho ya gavana huyo, walimtaja kuwa mtu aliyekuwa na bidii na ambaye alijitahidi katika majukumu yake, hatua ambayo ilimpatia fursa ya kuzidi kupaa katika nyanja ya uongozi.

Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i akisoma ujumbe wa rambirambi kutoka kwa Rais Uhuru Kenyattta, alimtaja Gavana Nyagarama kama kiongozi aliyekuwa na bidii iliyomfungulia milango mbalimbali ya uongozi.

“Alipenda kutafuta suluhu ya matatizo yanayomkumba mwananchi kila siku, na alipenda amani. Uwezo wake wa kipekee wa kuelewa changamoto anazozipitia mwananchi wa kawaida na maadili yake mema kazini ndiyo yalimwezesha kupanda cheo na kuhudumu katika ofisi mbalimbali za umma na kibinafsi,” akasema Rais Kenyatta katika ujumbe huo.

Rais Kenyatta alimsifia marehemu kwa kuimarisha sekta ya elimu kwa kuhakikisha kila mtoto anapata elimu, na pia kufufua sekta ya majani chai katika kaunti yake.

Aliyekuwa waziri mkuu, Bw Raila Odinga alimtaja marehemu kama simba shujaa, mpole, mungwana, aliyependa maendeleo na kudumisha amani.

Akisimulia kuhusu baadhi ya mikutano yake ya mwisho na marehemu, Bw Odinga aliwahakikishia wakazi wa Nyamira kuwa serikali itahakikisha matakwa aliyokuwa anatazamia kukamilisha yataangaziwa na kushughulikiwa.Bw Odinga alisema kuwa Bw Nyagarama alipenda amani, na kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), Wakenya wanaweza kuungana tena.

“Ningependa kuona Wakenya wakiwa na umoja. Hilo ndilo azimio kuu la handisheki,” akasema huku akiwaomba Wakenya wote kuunga mkono BBI.Waziri wa Ugatuzi, Bw Eugene Wamalwa akizungumza katika hafla hiyo alitoa rambirambi zake na kuwaahidi wakazi wa Nyamira kuwa serikali kuu itaendelea kufanya kazi nao.

Pia aliomba viongozi wa Kaunti hiyo kuhakikisha kuwa Naibu Gavana, Bw Amos Nyaribo anachukua nafasi iliyoachwa na Bw Nyagarama bila matatizo yeyote.

“Natumai Bw Nyaribo atashikilia usukani kukamilisha kazi aliyoianzisha Bw Nyagarama,” akasema Bw Wamalwa.Jaji Mkuu, David Maraga naye alimsifia marehemu kwa uongozi wake na pia kumtaja kama mpenda amani.

“Kwa kweli tumempoteza kiongozi mzuri na mpenda amani,” akasema Bw Maraga.Gavana Nyagarama alifariki Ijumaa iliyopita akiwa na umri wa miaka 74 katika Nairobi Hospital ambako alikuwa akipokea matibabu kwa muda.