• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 6:55 PM
Presha kwa Raila

Presha kwa Raila

NA LEONARD ONYANGO

UCHAGUZI

Siku moja baada ya kinara wa Narc-K, Martha Karua kumeza chambo cha mwaniaji urais kwa tikiti ya Azimio la Umoja katika uchaguzi mkuu wa Agosti, Raila Odinga, sasa yumo katika njiapanda amteue nani kuwa naibu wake. Tayari, mkoba wake umejaa majina ya waliopendekezwa na washauri wake kushikilia wadhifa huo wenye umuhimu mkubwa serikalini. Karua anaungana kwenye foleni na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Waziri wa Kilimo Peter Munya, aliyekuwa Mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth, Gavana wa Kitui Charity Ngilu na mwenzake wa Nakuru, Lee Kinyanjui ambao inaaminika wanamezea mate unaibu wa urais. Je, Raila na Uhuru watamteua nani?

KINARA wa ODM Raila Odinga amejipata katika njiapanda kuhusu uteuzi wa mwaniaji mwenza huku akiwa amesalia na chini ya siku 60 kufanya uamuzi.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itapokea majina ya wawaniaji urais pamoja na wagombea wenza wao kati ya Mei 29 na Juni 6.

Kuingia kwa kiongozi wa NARC Kenya Martha Karua ndani ya muungano wa Azimio la Umoja, kumefanya Bw Odinga kuwa na kibarua kigumu zaidi cha kuteua mwaniaji mwenza.

Bw Odinga pia anakabiliwa na shinikizo za kuteua kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, Waziri wa Kilimo Peter Munya au mbunge wa zamani wa Gatanga Peter Kenneth kuwa mwaniaji mwenza wake. Wengine wanaomezea mate wadhifa huo wenye ushawishi mkubwa serikalini ni Gavana wa Kitui, Charity Ngilu na mwenzake wa Nakuru, Lee Kinyanjui.

Jana Alhamisi, viongozi wa Jubilee kutoka Kaunti ya Kirinyaga walimtaka Bw Odinga kumteua Bi Karua kuwa mgombea mwenza wake.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa Jubilee tawi la Kirinyaga Bw Mureithi Kanga’ara, viongozi hao walimtaja Bi Karua kama kiongozi jasiri, mwenye busara na mwadilifu asiyependa kujihusisha na ufisadi.

“Sawa na Bw Odinga, Bi Martha ni kiongozi mzalendo. Viongozi hao wawili walipigania nchi hii kupata demokrasia ya vyama vingi na wanaweza kufanya kazi pamoja kuhakikisha Kenya imepata mafanikio ya kiuchumi,” alisema Bw Kanga’ara.

Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a, Sabina Chege ambaye amekuwa akizunguka kote nchini akipigia debe Azimio la Umoja, pia amemtaka Bw Odinga kuteua Bi Karua kuwa mwaniaji mwenza wake.

“Bi Karua ana sifa zote za kuwa naibu wa rais, hivyo ni vyema Bw Odinga amteue kuwa mwaniaji mwenza wake,” akasema Bi Chege.

Wadadisi wa kisiasa wanasema Bw Odinga huenda akajipatia kura nyingi za wanawake iwapo atateua mwanamke kuwa mwaniaji mwenza wake.

Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni, hata hivyo, amesema Rais Uhuru Kenyatta ndiye amejitwika jukumu la kutafuta mwaniaji mwenza wa Bw Odinga.

Chama cha National Party of Unity (PNU), kwa upande mwingine, kinataka Bw Munya, kuteuliwa kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga.

Rais Uhuru Kenyatta alipokutana na viongozi wa eneo la Mlima Kenya katika Ikulu ndogo ya Sagana, Nyeri, mwezi uliopita, alimiminia sifa tele Bw Munya – hatua ambayo imefanya chama cha PNU kuamini anamwandaa kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga.

SIASA ZA KITAIFA

Wakati wa Mkutano Mkuu wa Wajumbe (NDC) wa PNU katika ukumbi wa Bomas, mnamo Februari, Bw Odinga aliahidi ‘kumpeleka’ Bw Munya katika siasa za kitaifa huku akisema ameridhishwa na uchapakazi wake katika wizara ya Kilimo.

“Nataka tuungane na nimchukue nimpeleke katika ngazi ya kitaifa tufanye kazi pamoja kubadilisha maisha ya Wakenya,” alisema Bw Odinga.

Uteuzi wa Bw Munya kuwa mwaniaji mwenza kutasaidia Bw Odinga kutia kapuni sehemu kubwa ya kura 780,000 za Kaunti ya Meru. Muungano wa Azimio la Umoja unalenga asilimia 40 ya kura za eneo la Mlima Kenya, kumwezesha Bw Odinga kuibuka mshindi, kulingana na Mbunge Maalumu, Maina Kamanda.

“Bw Odinga akipata asilimia 40 ya kura katika eneo la Mlima Kenya atashinda urais kwa kishindo,” Bw Kamanda akaambia Taifa Leo.

Viongozi wa Wiper, wakiongozwa na Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior, wametishia kugura muungano wa Azimio la Umoja iwapo kiongozi wao Bw Musyoka hatateuliwa kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga.

“Sisi wanachama wa Wiper tumepigana sana ili Kalonzo awe mgombeaji urais kwa sababu 2017 tulikuwa tumekubaliana na Raila kwamba ataunga Kalonzo 2022.

“Lakini kwa sababu Kalonzo anapenda Kenya, akakubali Raila awe mgombea urais. Sisi tumesema na tunauliza apatiwe nafasi awe naibu wa rais wa Raila Odinga,” akasema Bw Kilonzo Junior alipokuwa akizungumza katika eneo la Wote, Kaunti ya Makueni wikendi iliyopita.

Bw Musyoka amesisitiza yuko tayari kuachana na kinyang’anyiro cha mwaniaji mwenza iwapo atatengewa asilimia 30 ya nyadhifa katika serikali ya Bw Odinga.

Hatua ya Bw Musyoka kujiunga na Azimio la Umoja huenda ikamwezesha Bw Odinga kuzoa asilimia kubwa ya kura milioni 2.3 za eneo la Ukambani. Magavana wote watatu wa kaunti za Ukambani; Bi Charity Ngilu (Kitui), Prof Kivutha Kibwana (Makueni) na Dkt Alfred Mutua (Machakos) wanaunga mkono Bw Odinga.

Mbunge wa zamani wa Gatanga, Peter Kenneth amekuwa akipigiwa upatu kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga. Tafiti za kura za maoni zimekuwa zikionyesha kuwa Bw Kenneth ndiye anapendelewa na Wakenya kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga.

Bw Kenneth amekuwa akiandamana na Bw Odinga katika mikutano mbalimbali ya kisiasa na alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliosafiri pamoja na kiongozi huyo wa ODM nchini Uingereza wiki iliyopita.

Mapema Machi, Bw Odinga alikanusha ripoti kwamba, tayari ameteua Bw Kenneth kuwa mwaniaji mwenza wake.

“Mheshimiwa Peter Kenneth hajaniomba kuwa mwaniaji mwenza wake. Hatujaanza mazungumzo kuhusu nani atakuwa mwaniaji mwenza. Tunaendelea na juhudi za kuimarisha muungano wa Azimio la Umoja,” akasema Bw Odinga.

You can share this post!

Ureno wacharaza Uturuki na kuweka hai matumaini ya kuingia...

GWIJI WA WIKI: Bethwel Wanjala

T L