RAILA: Sina ubaya na Ruto
Na WANDERI KAMAU
KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga, amesema hana ubaya wowote na Naibu Rais William Ruto, licha ya tofauti ambazo zimekuwa zikionekana kuwepo kati ya viongozi hao wawili.
Badala yake, Bw Odinga amesisitiza kwamba Dkt Ruto ndiye amekuwa akimwingilia kila mara kwa kumtukana.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio Jumanne asubuhi, Bw Odinga amesisitiza kuwa yeye amekuwa akijihusisha na uendeshaji wa mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI) na hakuna wakati hata mmoja ambapo amemjibu Dkt Ruto, licha ya matamshi yake.
“Tangu handisheki mnamo 2018 nimekuwa nikijihusisha na masuala ya BBI. Badala yake, Dkt Ruto ndiye amekuwa akiniita ‘mganga’ na ‘mtu wa vitendawili.’ Mimi sijawahi kumjibu hata kidogo,” akasema Bw Odinga.
Kauli yake inajiri huku uhasama kati ya viongozi hao wawili ukionekama kuendelea kupanuka, hasa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuiagiza Seneti kuwaondoa uongozini baadhi ya viongozi ambao ni waandani wa Dkt Ruto.
Viongozi hao ni aliyekuwa Kiongozi wa Wengi, Kipchumba Murkomen, aliyekuwa Kiranja wa Wengi, Bi Susan Kihika na aliyekuwa Naibu Spika, Prof Kindiki Kithure.
Dkt Ruto amekuwa akidai kuwa lengo kuu la Bw Odinga “kuivamia” Jubilee ni kumfurusha kutoka chama hicho.
Mwaka 2019 Dkt Ruto alisema kwamba hangemruhusu Bw Odinga kumwondoa Jubilee, kama alivyofanya wakati alikuwa katika ODM.
“Jubilee si ODM. Ikiwa lengo lenu (Odinga na washirika wake) ni kunifurusha kutoka Jubilee, msahau. Hamniondoi ng’o, kwani Jubilee siondoki!” akasema Dkt Ruto akiwa katika ziarani Pwani.
Lakini Jumanne Bw Odinga amesisitiza kuwa Dkt Ruto anafaa kujilaumu kwa masaibu ya kisiasa anayopitia katika Jubilee kwa sasa.
Wakati huo huo, Bw Odinga ameirai serikali kufungua upya shughuli za kiuchumi japo kwa masharti ili kuwaruhusu Wakenya kurejelea kazi zao kama kawaida.
Ameeleza kuwa lazima serikali ichukue hatua kali kuhakikisha kuwa Wakenya wanaendelea kuzingatia kanuni ilizoweka kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
Mnamo Jumamosi, Rais Kenyatta alitoa kauli ya uwezekano wa kufungua upya shughuli hizo, ingawa hakueleza ni lini.