Sitafyata ulimi, Gachagua aapa
KIONGOZI wa Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, Desemba 10, 2025 aliwajibu wakosoaji wanaomlaumu kwa kuzungumza kupita kiasi na kufichua siri za kisiasa zinazofaa kubaki kwenye milango ya mazungumzo, hasa kabla ya makubaliano yoyote kutiwa saini.
Naibu rais huyo wa zamani alisema hana mpango wa kunyamaza na ataendelea kujieleza bila kizuizi chochote, akisisitiza kuwa anaongozwa na ukweli, uwazi na uadilifu.
“Nimesikia watu wakisema nisiweke wazi mikakati ama siri zangu, hakuna siri. Mimi ni kitabu wazi,” aliambia KTN.
Aliongeza: “Ninazungumza kwa niaba ya watu wanaoniunga mkono, na wana haki ya kujua ninachowapangia.”
Bw Gachagua alisema hatashiriki katika siasa za kuchezeana karata ama kufanya maamuzi ya siri.
“Mimi si mtu wa kukubaliana kwa faragha. Nitakuja mbele ya wafuasi wangu kuwaeleza bayana aina ya makubaliano ninayowaingiza,” alisema.
Alisema kuwa hulka ya kufanya mambo kwa siri ndiyo inaathiri serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto, “kwa kuwa hatukuwahi kuwaambia wananchi tulichokubaliana naye.”
Katika mahojiano hayo, Bw Gachagua alizungumzia pia utata ulioibuka baada ya kudai kwamba ana makubaliano na kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, kuhusu kugawana viti Nairobi, kauli iliyozua upinzani mkali ndani ya muungano wa upinzani.
“Namaanisha nilichosema, na si kwa DCP pekee. Ni baina ya Wiper na DCP — mimi na Kalonzo,” alisema.
Alisisitiza kuwa hotuba yake ya Novemba 30, 2025 katika Kanisa la PCEA Embakasi ilipotoshwa kudai kwamba alitaka viti vya Nairobi vihifadhiwe kwa jamii ya Wakikuyu.
“Sikusema hivyo. Nilisema tu kwamba namtambua Bw Musyoka kwa nafasi yake muhimu katika siasa za Nairobi, na amekuwa akisaidia ODM kushinda viti huko,” akasema.
Katika hotuba hiyo, alisema:“Tuna makubaliano na Kalonzo Musyoka na chama cha Wiper kwamba DCP itachukua ugavana, useneta, mwakilishi wa wanawake, na kwa pamoja tuchukue maeneo bunge 16 kati ya 17, na wadi 75 kati ya 85.”
Katika mahojiano alisisitiza “Si uwongo, maana hata Bw Musyoka ameeleza wazi kwamba tumekubaliana kushirikiana ili kuimarisha ushindi.”
Bw Gachagua alisema ana kila haki ya kutafuta nafasi muhimu za kisiasa kwa chama chake ndani ya muungano wa upinzani na kwamba kama kushirikiana na Wiper kunahitajika, basi atafanya hivyo.
“Watu wanadhani mimi ni nani? Nisishughulikie maslahi ya chama changu? Nisiwe na mikakati ya kushinda Nairobi? Ningekuwa mjinga. Nimeongea na Kalonzo, na nitaendelea kufanya hivyo,” alisema.
Kwa upande wake, Bw Musyoka amekuwa akibadilisha misimamo, akikanusha kwanza kuwepo kwa mkataba wowote, kisha baadaye akamsifu Gachagua kwa “ukweli na ujasiri.”
Hata hivyo, alisisitiza kuwa Nairobi haiwezi kugawanywa kwa misingi ya vyama.
“Nairobi haiwezi kuwekewa mipaka ya vyama. Hili ni jiji la kimataifa, linahitaji demokrasia ya wazi,” alisema.
Bw Gachagua alidai kuwa Rais Ruto na washauri wake “wana wasiwasi” kuhusu umaarufu wake unaoongezeka na kukua kwa ushawishi wa DCP kuelekea 2027.
“Ndio maana wanapiga kelele kwamba mimi ni mkabila na kwamba DCP ni chama cha kujitenga. Hawatafanikiwa,” alisema.
Alisema yeye na Bw Musyoka wamekubaliana kuepuka “kuumizana kisiasa” Nairobi katika Uchaguzi Mkuu wa 2027 “ili kumnyima Rais Ruto mianya ya kushinda viti.”
Alirudia madai kwamba baadhi ya vyama vya upinzani vinasaidia UDA kwa siri, akirejelea alama ya UDA ya wilibaro
Alitaja mfano wa uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini ambapo mgombeaji wa upinzani Newton Kariuki alishindwa na Leonard Wa Muthende wa UDA.
Alisema chama cha Moses Kuria, Chama Cha Kazi (CCK), kiligawanya kura za upinzani.