• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Utapeli ofisi kuu

Utapeli ofisi kuu

Na VALENTINE OBARA

KASHFA ya utapeli inayogusa afisi ya Naibu Rais William Ruto, inaendeleza mtindo wa watu mashuhuri na ofisi kuu nchini kutumiwa kuwalaghai watu mamilioni ya pesa.

Dkt Ruto amejipata katika kona mbaya baada ya kuibuka aliyekuwa waziri wa michezo Rashid Echesa alitumia ofisi na jina lake kutapeli wafanyabiashara wa ng’ambo mamilioni ya pesa.

Echesa alikuwa ameahidi kuwa angewasaidia wageni hao kupewa kandarasi ya kuuzia jeshi la Kenya silaha za thamani ya Sh39.5 bilioni.

Majina ya Rais Uhuru Kenyatta, Kiongozi wa ODM Raila Odinga na Waziri wa Usalama Fred Matiang’i pia yamewahi kutumiwa na walaghai kutapeli watu nchini na ng’ambo mamilioni ya pesa.

Polisi wanasema matapeli wanaotumia majina ya watu mashuhuri katika ulaghai huwa na stakabadhi zenye hati halisi za serikali, na hutumia picha walizopigwa kwenye hafla na viongozi hao kushawishi wanaolengwa kuingia kwenye mitego yao.

“Huwa wanaendesha magari ya kifahari, huvaa suti za bei ya juu, huzuru hoteli za hadhi ya juu na huishi mitaa ya kifahari. Wana pesa nyingi na wana uhusiano wa karibu na watu wenye ushawishi mkubwa serikalini,” zikasema duru za polisi.

Matapeli hao pia wameripotiwa kuwa kuna wakati wanapokutana na waathiriwa katika ofisi za serikali ili kudhihirishia kuwa dili wanazoahidiwa ni halali.

Mbinu hizi zinazua maswali kuhusu matapeli hao wanavyopata hati halisi za serikali, paspoti za kidiplomasia na hata kuweza kuingia ofisi za wakuu wapendavyo.

ZABUNI YA LAPTOPU

Polisi wanasema walaghai hao wanashirikiana na maafisa wafisadi katika ofisi za wakuu katika sakata hizo.

Hapo jana Echesa pamoja na Kevin Oyoo Mboya, Clifford Okoth Onyango na Daniel Otieno Omondi walifunguliwa mashtaka 12 kuhusu sakata hiyo.

Walalamishi ambao ni kutoka Poland waliambia polisi kuwa Echesa aliwatumia barua Oktoba mwaka jana akisema angewasaidia kupata zabuni hiyo, kisha akaitisha Sh11.5 milioni kama ada yake ya mwanzo.

Kisha aliwaalika nchini ambapo alikutana nao akiandamana na mtu aliyekuwa amevaa magwanda ya kijeshi na akajitambulisha kama Jenerali Omondi.

Wageni hao kisha walimwalika Echesa na watu wengine watatu kwenda Poland kuonyeshwa vifaa hivyo vya kijeshi, ambapo waziri huyo wa zamani alisafiri kwa paspoti ya kidiplomasia.

Wageni hao walisema ni wakati wa ziara hiyo ambapo Echesa alipewa pesa zaidi baada ya kuthibitisha vifaa hivyo vilifikia viwango vilivyohitajika na jeshi la Kenya.

Alhamisi iliyopita Echesa aliwapeleka wageni hao katika ofisi ya Dkt Ruto, ambako “mkataba” wa zabuni hiyo ungetolewa, na baada ya kuweka sahihi wangelipa Sh3.9 bilioni zaidi kwa mabroka wa Kenya kwa kufanikisha zabuni hiyo.

Wageni hao walisema walikuwa wamehakikishiwa kuwa zabuni hiyo ingewekwa sahihi mbele ya Dkt Ruto ofisini mwake.

Hapo jana polisi walifanya ukaguzi katika ofisi ya Naibu Rais, ambaye amekiri kuwa Echesa na watu wengine walifika ofisini mwake wiki iliyopita lakini amekanusha kukutana nao.

Mnamo 2018 ilifichuka kulikuwa na kikundi cha watu waliomhadaa mfanyabiashara Stephen Ngei kwa kujifanya wanawakilisha afisi ya Dkt Ruto kununua laptopu.

Washukiwa kadhaa walikamatwa na wakafikishwa mahakamani kwa kashfa hiyo ya ununuzi wa vipakatalishi 2,800 vilivyogharimu Sh180 milioni.

Polisi walisema mmoja wa washukiwa, Joy Wangari Kamau alikuwa akiandamana na watu aliodai kuwa maafisa wa ujasusi alipokuwa akikutana na Bw Ngei.

Vile vile mwanamke huyo alidaiwa kuwa aliwahi kumtapeli Bw Charles Ng’ang’a jumla ya Sh136 milioni akijifanya yeye ni afisa katika Ikulu ya Rais Kenyatta na angemwezesha kupata zabuni ya kuuzia serikali vifaa vya kijeshi.

Mwaka jana, majina ya Rais Kenyatta, Bw Odinga na Bw Matiang’i yalitajwa kwenye kashfa ambapo matapeli waliwalaghai watu kutoka nje ya nchi mamilioni ya pesa wakidai wangewauzia dhahabu.

Kwenye kashfa hiyo, raia wa Milki za Kiarabu (UAE) ambaye ana uhusiano na familia ya kifalme, Ali Zandi alinaswa kwenye mtego wa matapeli waliojifanya ni washirika wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Zandi alitapeliwa Sh250 milioni na watu waliojifanya wangemuuzia dhahabu.

Washukiwa takriban 15 wakiwemo raia wa kigeni walikamatwa kuhusiana na kashfa hiyo ambayo ilisemekana walitumia pia jina la Dkt Matiang’i kufanikisha shughuli zao.

KUIGA SAUTI YA UHURU

Kisa kingine mwaka huo kilihusu mwanamume aliyeiga sauti ya Rais Kenyatta kumtapeli mfanyabiashara mashuhuri Naushad Merali Sh10 milioni. Watu saba walikamatwa na kushtakiwa kwa sakata hiyo.

“Mlalamishi alipigiwa simu kutoka kwa nambari zilizodaiwa kuwa za Rais Kenyatta. Mlalamishi aligundua alikuwa anawasiliana na matapeli baada ya kupoteza Sh10 milioni kwao,” mahakama ikaambiwa.

Kulingana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Kidijitali katika Ikulu, Bw Dennis Itumbi, visa aina hii hutokea sana katika afisi kuu za serikali.

“Sijui kama wale wote wanaotajwa wana hatia. Lakini ninachofahamu ni kwamba mambo haya hutokea katika afisi za serikali bila ufahamu wa rais, naibu wake wala mawaziri,” akasema Bw Itumbi.

Kando na afisi hizo kubwa, Idara ya Uhamiaji na afisi za ardhi kote nchini hutajwa kuwa miongoni mwa zile zilizojaa matapeli ambao huwatia wananchi mtegoni wakidai wana uwezo wa kuwasaidia kupata huduma kwa haraka.

Imebainika kuwa, watu hao ambao si wafanyakazi wa serikali wakati mwingine hushirikiana na maafisa wanaofanya kazi katika idara hizo kuwapunja wananchi.

Wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, mojawapo ya sakata kubwa zaidi zilizoibuka ilihusu uagizaji wa mahindi kwa Bodi ya Kitaifa ya Mazao na Nafaka (NCPB) mnamo 2009.

Katika uchunguzi uliofanywa, wahusika waligunduliwa kuwa maafisa katika afisi ya Bw Odinga ambao walitumia nafasi zao kujinufaisha kibinafsi.

Aina hizo za utapeli zinaongeza changamoto kuhusu uadilifu katika nchi ambayo tayari inakumbwa na janga la ufisadi katika wizara mbalimbali na serikali za kaunti.

You can share this post!

Matumaini ya Arsenal UEFA yangali finyu

Mudavadi alitaka jopo la BBI kuhakikishia Wakenya ripoti...

adminleo