Wataalamu wailaumu ICC kwa kusitisha kesi za UhuRuto
NA VALENTINE OBARA
MAHAKAMA ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imekosolewa kwa kufanya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, Dkt William Ruto, kuendelea kuwa na wasiwasi hata baada ya kesi zao kusitishwa.
Wawili hao walikuwa wameshtakiwa ICC kwa madai ya kuhusika katika ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, lakini kesi zao zikasitishwa kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.
Katika ripoti iliyotolewa na kikundi cha wataalamu kilichoajiriwa na Baraza la Mataifa Wanachama wa ICC, almaarufu kama ASP, kuchunguza utendakazi wa mahakama hiyo, ilibainika kulikuwa na madoa kadhaa jinsi kesi za Rais Kenyatta na Dkt Ruto ziliendeshwa.
Wataalamu hao wa kisheria kutoka nchi mbalimbali waliikosoa ICC kwa kutosema wazi kama viongozi hao wawili pamoja na mwanahabari Joshua arap Sang, sasa wako huru au waendelee kujiandaa kwa kesi baadaye.
Wakati kesi zao zilisitishwa majaji walisema upande wa mashtaka, unaoongozwa na Bi Fatou Bensouda, uko huru kuwasilisha kesi upya baadaye endapo ushahidi zaidi utapatikana.
Tangu wakati huo wapelelezi wa ICC huendeleza upelelezi wao, hasa kuhusu kesi ya Dkt Ruto, humu nchini kisiri kila mwaka.
Wataalamu hao walioanza kazi yao Desemba 2019 sasa wanasema mwenendo huu si wa haki kwani kisheria, mshtakiwa anafaa kufahamishwa iwapo ana hatia au la kesi inapotamatika.
“Maamuzi haya hayaendi sambamba na hali ya kawaida ambapo uamuzi unastahili kuwa kwamba, mshtakiwa hana kesi ya kujibu au kesi itamatishwe,” inasema ripoti hiyo iliyotolewa Jumatano jioni.
Kando na suala hilo, ICC ilikosolewa kwa kutotilia maanani malalamishi ya washtakiwa kwamba upande wa mashtaka ulihujumu mashahidi ambao washtakiwa waliwategemea katika kujitetea.
Katika kesi ya Rais na naibu wake, wataalamu walikosoa afisi ya Bi Bensouda kwa kukataa kuchunguza madai kwamba washirika wake walibuni ushahidi ambao ulitegemewa kuwashtaki wawili hao.
Mawakili wa washtakiwa walikuwa wameibua malalamishi tele kwamba upande wa mashtaka ulishirikiana na mashirika ya kijamii nchini Kenya kubuni ushahidi wa uongo na kuwafunza mashahidi jinsi ya kudanganya mahakamani.
“Mahakama ilikataa kuteua mpelelezi huru kuchunguza madai hayo. Wakati wa kesi ya Kenyatta, kulikuwa na madai mazito kuhusu kuhujumiwa kwa watetezi wake na washirika wa upande wa mashtaka. Japo madai haya yaliripotiwa na mawakili wa walalamishi kwa afisi ya kiongozi wa mashtaka, hakuna hatua yoyote ilichukuliwa,” ripoti iliendelea kueleza.
Wataalamu hao walipendekeza kuwa kuendelea mbele, ICC ibuni mfumo mwafaka wa kuhakikisha malalamishi yote kuhusu hujuma za haki yanachunguzwa kikamilifu na adhabu kutolewa haraka.
Aidha, waliongeza, wakati malalamishi kama hayo yanatolewa kuhusu upande wa mashtaka, ni vyema Msajili wa Mahakama aagizwe kuajiri mpelelezi huru kisha ripoti ya uchunguzi iwasilishe ili uamuzi ufanywe.
Akipokea ripoti hiyo, Rais wa ASP Bw O-Gon Kwon alisema ripoti itafanyiwa tathmini kisha hatua zichukuliwe.
Uundaji wa kamati hiyo ya wataalamu ulitokana na malalamishi mengi ya nchi mbalimbali, hasa za Afrika kuhusu utendakazi wa ICC.Baadhi ya viongozi wa Afrika hulalamika kwamba mahakama hiyo inatumiwa kuhujumu uhuru wa utawala wao.