Wimbi katika jahazi la UhuRuto latikisa nchi
Na BENSON MATHEKA
UHASAMA wa kisiasa kati ya mirengo miwili katika chama cha Jubilee inaendelea kuwagawanya Wakenya na kulemaza huduma huku siasa za urithi zikishika kasi miaka miwili kabla ya uchaguzi wa 2022.
Viongozi wa chama hicho wameonyesha mfano mbaya kwa kutofautiana hadharani wakati ambao wanapaswa kuwa wakihudumia Wakenya.
Tofauti kati ya wafuasi wa Rais Uhuru Kenyatta na wale wa Naibu Wake William Ruto zilichacha jana huku Katibu Mkuu wa chama hicho Raphael Tuju akifichua mipango ya kumpokonya Dkt Ruto wadhifa wa naibu kiongozi.
“Imekuwa vigumu kuvumilia Naibu Rais akitumia chama ikiwemo kutumia makao makuu ya chama kutoa matamshi ya kuendeleza siasa za mgawanyiko anazoita siasa za hasla kinyume na msimamo wa chama na wito wa Rais wa kuunganisha Wakenya,” alisema Bw Tuju.
Alisema kwamba kamati simamizi ya chama imempiga marufuku Dkt Ruto na washirika wake wa kisiasa kukanyaga makao makuu ya Jubilee.
Wabunge wa chama hicho na maseneta wamegawanyika katika mirengo miwili ya Kieleweke na Tangatanga ambayo badala ya kutekeleza majukumu yao bungeni na kupiga jeki serikali, wamekuwa wakilumbana kila siku.
Uhasama huu umezorotesha huduma na kutoa nafasi ya ufisadi kuendelea katika idara tofauti za serikali.
Ingawa kwa kawaida chama tawala kinafaa kuonyesha nidhamu ya hali ya juu, viongozi wa Jubilee wanaendelea kuanika hadharani chuki kati yao.
Jana, Bw Tuju alimlaumu Dkt Ruto kwa kugeuza makao makuu ya chama tawala kuwa ofisi ya kampeni zake za urais anazofanya kwa kumkaidi Rais Kenyatta.
Mnamo Alhamisi, Dkt Ruto na wabunge 32 washirika wake wa kisiasa walikutana kwa zaidi ya saa sita katika ofisi hizo bila kufahamisha maafisa wa chama.
Maafisa wa chama hicho walitaja hatua hiyo kama jaribio la mapinduzi lakini wabunge waliohudhuria mkutano huo wakasema kama wanachama wana haki ya kutumia ofisi hizo na kuuliza maswali kuhusu usimamizi wa chama. Bw Tuju alimlaumu Dkt Ruto kwa kujiondoa chamani na serikalini, akidai amekuwa akimdharau Rais, kukwepa hafla za serikali na kutishia maafisa wa serikali.
“Tunataka ieleweke wazi kwamba, tunahudumia Rais mmoja kwa wakati mmoja. Naibu Rais, ambaye amejitangaza mgombea urais kwenye uchaguzi wa 2022, hataruhusiwa kutumia makao makuu ya chama kama kituo cha kuendeleza kampeni yake na vitisho,” Bw Tuju alisema baada ya mkutano wa baraza simamizi la chama cha Jubilee.
Alisema kwamba baada ya kushauriana, baraza hilo lilipendekeza kwa Baraza Kuu la Kitaifa la chama hicho kwamba Dkt Ruto apokonywe wadhifa wa naibu kiongozi wa chama. Hatua hiyo inaweza kuwagawanya Wakenya zaidi wakati huu joto la siasa linapoendelea kupanda.
Alimlaumu Dkt Ruto kwa kuvuruga chama hicho na kusema makao makuu hayatatumiwa kutoa matamshi ya kugawanya wanachama.
Kulingana na Bw Tuju, Dkt Ruto alitelekeza wadhifa wake wa naibu kiongozi wa chama na anafaa kuupokonywa rasmi.
Wakizungumza wakiwa Nakuru, washirika wa Dkt Ruto walipuuza marufuku ya kutokanyaga makao makuu ya Jubilee na kusema kwamba wataendelea kukutana katika ofisi hizo.