Habari

Sukari yenye sumu yanaswa maeneo kadhaa nchini

June 19th, 2018 2 min read

Na WAANDISHI WETU

MSAKO dhidi ya sukari ya magendo umechacha nchini huku serikali ikionya kuwa sukari yenye sumu tayari inauzwa madukani.

Mkurugenzi wa Afya ya Umma, Dkt Kepha Ombacho, Jumatatu aliyataka maduka ya jumla kupima sukari waliyo nayo ili kuthibitisha ikiwa inakidhi viwango vya ubora.

Dkt Ombacho alionya kuwa sukari itakayopatikana haijatimiza viwango vya ubora itaondolewa madukani na kupigwa marufuku.

“Tumebaini kuwa sukari hatari kwa afya tayari inauzwa madukani. Hivyo mnatakiwa kupima na kuthibitisha ubora wa sukari hiyo kabla ya kuuzia wateja,” akasema Dkt Omacho kupitia kwa barua yake iliyoandikwa June 18, 2018 kwa wasambazaji na wamiliki wa maduka ya jumla.

Msako umeshika kasi baada ya kubainika kuwa Wakenya wamekuwa wakitumia sukari iliyochanganywa na madini ya shaba na mekyuri ambayo ni hatari kwa afya na yanaweza kusababisha maradhi ya kansa yanapoingia mwilini.

Katika Kaunti ya Meru, Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) jana ilinasa magunia 3,000 ya sukari inayoshukiwa ni ya magendo.

Kamishna wa Kaunti ya Meru Wilfred Nyagwanga alisema sukari hiyo ambayo iliingizwa nchini kutoka Brazil, ilipatikana ikipakiwa kwenye mifuko ya kuonyesha kuwa ilitoka Zambia.

Watu 13 ambao walifumaniwa wakipakia sukari hiyo katika mifuko mipya walikamatwa pamoja na mmiliki wa duka hilo.

Mjini Kitale, polisi walifanikiwa kunasa sukari zaidi ya magunia 550 ambayo ilikuwa imefichwa na mfanyibiashara mmoja inayoshukiwa ni ya kutoka nchi jirani.

Kamanda wa Polisi Kaunti ya Trans-Nzoia, Bw Samson Ole Kina alisema polisi walimnasa mmiliki wa duka hilo na amezuiliwa.

Mjini Nyahururu, sukari zaidi ilinaswa kwenye msako uliotekelezwa kwa pamoja na maafisa wa usalama, KRA na wa utawala.

Hayo yanajiri huku Jaji Lucy Gitari akimwachilia huru Bw Patrick Njiru na mkewe Bi Leah Njeri Njiru kwa dhamana ya Sh200,000 kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi waliyowasilisha katika mahakama kuu ya Kerugoya kupitia kwa wakili Njiru Ndegwa.

Bw Kuria ni nduguye mwakilishi wa akina mama kaunti ya Kirinyaga Bi Wangui Ngirici.

Jaji Gitari aliratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuamuru walalamishi wafike kortini katika muda wa siku saba.

Katika kesi hiyo, Bw Kuria amewashtaki Mwanasheria mkuu (AG) Paul Kihara Kariuki, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji na Mkurugenzi wa Jinai (DCI).

Wiki iliyopita mkewe Njiru, Bi Leah Njeri pamoja na washukiwa wengine wawili Simon Gichovi Maria na Douglas Kuria Njiru walifikishwa katika mahakama ya Nairobi wakidaiwa walikutwa wamehifadhi magunia 1,000 ya sukari iliyodhaniwa haifai kwa matumizi ya binadamu.

Hakimu mkazi Bi Christine Njagi aliwaachilia baada ya kukabidhiwa agizo la mahakama kuu ikiamuru polisi wasiwatie nguvuni washukiwa hao.