• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
DAWA ZA KULEVYA: Mnigeria abubujikwa na machozi kortini akitaka simu

DAWA ZA KULEVYA: Mnigeria abubujikwa na machozi kortini akitaka simu

Na BENSON MATHEKA

Mwanamke raia wa Nigeria anayekabiliwa na mashtaka ya kulangua dawa za kulevya alizodaiwa kuficha ndani ya chupa za maziwa, Alhamisi alilia mahakamani akitaka polisi waagizwe kumpa simu yake ili awasiliane na familia yake nchini Italia.

Princess Okoye aliambia mahakama ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi kwamba aliacha mtoto mchanga nchini Italia na hajui hali yake kwa sababu simu yake ilitwaliwa na polisi alipokamatwa Machi 3 mwaka huu kwa madai ya kulangua dawa za kulevya.

“Ninaomba mahakama iagize polisi wanipe simu niweze kuwasiliana na familia yangu inieleze mtoto wangu anavyoendelea hata kama nitazungumza mbele yao( polisi),”; alisema mshtakiwa huyo.

Hata hivyo, upande wa mashtaka uliambia Hakimu Mkuu Lucas Onyina kwamba simu hiyo iliwasilishwa kwa wataalamu ikaguliwe.

“Polisi wamenifahamisha kwamba simu hiyo inakaguliwa na wataalamu. Mchunguzi wa kesi anaahidi kumkabidhi mshtakiwa simu hiyo akiipata ili aweze kuwasiliana na familia yake alivyoomba,” kiongozi wa mashtaka alisema.

Okoye anakabiliwa na mashtaka mawili ya kulangua dawa za kulevya aina ya heroini za thamani ya Sh3.7 milioni.

Polisi wanasema alikamatwa muda mfupi kabla ya kupanda ndege kuelekea Italia akiwa ameficha dawa hizo kwenye chupa za maziwa na kumeza vidonge 16 za dawa hiyo.

Kesi itasikilizwa Mei 10 na 14 mwaka huu.

You can share this post!

Magufuli awaongoza Watanzania kumwomboleza Reginald Mengi

Matangazo ya uchezaji kamari ni marufuku – Serikali

adminleo