• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
DRC kuandaa uchaguzi mkuu mzozo ukichacha

DRC kuandaa uchaguzi mkuu mzozo ukichacha

NA MASHIRIKA

KINSHASA, DRC

JAMHURI ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) itafanya uchaguzi ujao wa urais Desemba 20, 2023.

Tangazo hilo la tume ya uchaguzi lilijiri huku wanamgambo wakiendeleza mashambulio yao mashariki mwa taifa hilo, ambapo wamewafurusha maelfu ya watu kutoka makwao.

Katika taifa hilo, uchaguzi wa urais huwa unafanyika wakati sawa na chaguzi za ubunge, mkoa na mitaa.Rais mteule atachukua uongozi Januari 2024 baada ya uchaguzi huo.

Rais Felix Tshisekedi alichukua uongozi Januari 2019 kutoka kwa Joseph Kabila, aliyekuwa amehudumu kwa jumla ya miaka 18.

Huo ndiyo ulikuwa mchakato wa kwanza kiongozi kumkabidhi mamlaka kiongozi mwingine kwa amani, bila mivutano wala umwagikaji damu.

MUHULA WA PILI

Rais Tshisekedi ametangaza nia yake kuwania urais kwa muhula wa pili, licha ya hofu ya ghasia kuibuka kuhusu matokeo ya uchaguzi huo.

Watu wengine wanaopigiwa upatu kuwania urais ni Martin Fayulu, aliyeibuka wa pili kwenye uchaguzi uliofanyika 2018.

Viongozi wengine wanaotarajiwa kuwania nafasi hiyo ijapokuwa hawajatangaza rasmi ni waziri mkuu wa zamani, Adolphe Muzito na gavana wa zamani wa Katanga, Moise Katumbi.

Waziri Mkuu mwingine za zamani, Augustin Matata Ponyo, amesema atawania.

Mwaka 2021, Ponyo alishtakiwa kuwa alipora fedha za umma, ijapokuwa mahakama ya kikatiba ilisema haina mamlaka kumhukumu.

Hata hivyo, mahakama hiyo imebadilisha msimamo wake, ikisema itajaribu kumfungulia mashtaka.

Chaguzi za urais za 2006 na 2011, ambazo Kabila aliibuka mshindi, zilikumbwa na umwagikaji damu, huku mamia ya watu wakifariki kutokana na maandamano yaliyozuka.

DRC ilikuwa koloni la Ubelgiji na imekumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi.

Kundi la wanamgambo la M23 lilianza mashambulio mwishoni mwa 2021, likidai serikali ilikuwa imefeli kuzingatia ahadi ya kuwaingiza wanamgambo katika jeshi, kati ya malalamishi mengine.

Rais Mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta amekuwa akiendesha juhudi za kuipatanisha serikali na wanamgambo hao.

Baada ya miezi minne ya utulivu, mapigano yalizuka tena Oktoba 20, wanamgambo wakielekea mjini Goma.

Mapigano hayo yameathiri uhusiano kati ya DRC na Rwanda, taifa hilo likiilaumu Rwanda kwa kuwaunga mkono wapiganaji wa M23.

Ni kauli ambayo imeungwa mkono na maafisa wa Umoja wa Mataifa (UN) na Amerika.

Hata hivyo, Rwanda imekuwa ikikanusha madai hayo.

You can share this post!

Coe afurahia juhudi za Kenya kuimarisha vita dhidi ya pufya

Hasira polisi aliyehusishwa na ubakaji akitoweka

T L