• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 2:10 PM
Kane abeba Spurs hadi hatua ya makundi ya Europa Conference League

Kane abeba Spurs hadi hatua ya makundi ya Europa Conference League

Na MASHIRIKA

KOCHA Nuno Espirito Santo amesema Harry Kane amedhihirisha ukubwa wa kiwango cha kujitolea kwake kuwajibikia klabu yake ya Tottenham Hotspur baada ya kupachika wavuni mabao mawili na kusaidia waajiri wake kupepeta Pacos de Ferreira 3-0 katika marudiano ya Europa Conference League.

Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kwa Kane kushiriki tangu atangaze kwamba amezika mpango wa kuondoka Spurs na hivyo kuzima tetesi zote zilizokuwa zikimhusisha na uwezekano wa kutua Manchester City.

“Mengi yaliyosemwa kuhusu mustakabali wa Kane kitaaluma sasa yamekwisha. Ni wakati wa kusonga mbele kama kikosi kimoja. Kane amedhihirisha hivyo,” akasema Nuno.

Spurs walijibwaga ugani kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya Pacos mnamo Alhamisi usiku wakiwa na ulazima wa kubatilisha kichapo cha 1-0 walichopokezwa katika mchuano wa mkondo wa kwanza.

Kane alifungulia Spurs ukurasa wa mabao katika dakika ya tisa baada ya kushirikiana vilivyo na Bryan Gil. Alipachika wavuni goli la pili katika dakika ya 34 kabla ya Pacheco Antunes wa Pacos kujifunga kutokana na kombora la Giovani lo Celso.

Hiyo ilikuwa mechi ya kwanza kwa Kane kuanza akiwa katika kikosi cha kwanza cha Spurs tangu Mei 23, 2021. Nyota huyo ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza, aliondolewa uwanjani katika dakika ya 72 kama sehemu ya mikakati ya kumpa fursa ya kujiandaa vilivyo kwa gozi lijalo la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Watford.

Kane sasa anajivunia kufungia Spurs jumla ya mabao 223 kutokana na mashindano mbalimbali.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Okutoyi apigwa breki nusu-fainali ya tenisi ya kimataifa ya...

DOMO KAYA: Wanaume twakwama wapi?