• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 10:50 AM
KYSD Soccer Stars, Kinyago mtazikoma hakuna kuzaa

KYSD Soccer Stars, Kinyago mtazikoma hakuna kuzaa

Na JOHN KIMWERE

KWA mara ya pili Kinyago United ya wasiozidi umri wa miaka 11, imeshindwa kutwaa ubingwa wa Ligi ambayo huandaliwa na kituo cha Kinyago Youth and Sports Development (KYSD).

Kocha wake, Anthony Maina anasema ”Ninaamini lazima tubebe taji hilo muhula mpya. Sina shaka kushauri wapinzani wetu kuwa shughuli hazitakuwa mteremko mbele ya chipukizi wangu,” alisema na kutoa wito kwa wapinzani wao kukubali wakishindwa.

KYSD TOP EIGHT

Kwenye ngarambe ya msimu wa 2021/2022, Soccer Stars imeibuka washindi huku Kinyago United kumaliza ya pili katika ligi hiyo imetawazwa mabingwa wa kipute cha KYSD Top 8. Katika mpango mzima Kinyago United imetwaa ubingwa wa kipute hicho mara nne ndani ya mihula miwili.

Soccer Stars imetawazwa mabingwa wa ligi hiyo baada ya kuibuka kidedea kwa alama 18, mbili mbele ya Kinyago United. Katika kile kinaodhihirisha kampeni kali zilijumuisha wapinzani hao Black Angels iliyomaliza ya tatu ilisajili alama 33 sawa na Sharp Boys tofauti ikiwa idadi ya mabao.

KUKOSA HUDUMA

”Hakika tuliteleza kiasi tungebeba mataji mawili msimu huo,” alisema nahodha wa Kinyago, Brian Kimeu na kuongeza kuwa msimu mpya wamepania kutifua vumbi la kufa mtu.

Anadokeza kuwa kukosa huduma za wachezaji watatu muhimu kulipelekea kwa asilimia fulani kudondosha mechi mbili na kutoka nguvu sawa mara tatu. Kwenye mechi ilikopoteza alama mbili kila moja ilitoka sare tasa na Black Angels kisha kutoka bao 1-1 mara mbili mbele ya Sharp Boys na Makongeni Young Stars.

Timu hiyo ilizikosa huduma za wachezaji Fidelis Muinde, Farouk Ramadhan na Shawn Lubanga waliokuwa wameshikika na shughuli zingine. Kocha Anthony Maina anasema ”Kusema kweli Soccer Stars na Blue Bentos kila moja ilitupatia kibarua kigumu kwenye mechi za msimu huo.”

STARS: Timu ya Soccer Stars bingwa wa Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 11 msimu wa 2021/2022. ..Picha/JOHN KIMWERE

Licha ya Kinyago United kutwaa taji la Top 8, kocha wake anakiri kuwa haikuwa kazi rahisi. Katika fainali, Kinyago iliibuka wakali ilipozaba Sharp Boys kwa bao 1-0 lililofunikwa kimiani na Justus Omondi.

Kwenye nusu fainali, Kinyago iliangusha Fighting Destiny kwa mabao 2-1 kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1. Nao chipukizi wa Sharp Boys ya kocha, Boniface Kyalo walizaba Blue Bentos kwa magoli 2-1 kupitia Daniel Kamau na Dennis Mwangi. Naye Tevin Lugusa alifungia Blue Bentos bao la kufutia machozi.

TUZO

Kwenye tuzo za kibinafsi, Samuel Mtemba (Kinyago) alituzwa mnyakaji bora baada ya kuokoa mikwaju ya penalti katika robo fainali pia nusu fainali na kuibeba timu yake kutwaa taji hilo.

Felix Ochieng (Fighting Destiny) allibuka mchezaji anayeibukia aliposaidia kikosi chake kwa kukifungia mabao 13 kati ya 15 kiliofunga muhula huu naye Gabriel Timmo (Fighting Stars Academy) alitawazwa mfungaji bora kwa kucheka na wavu mara 25.

Kituo cha KYSD kinajivunia kulea baadhi ya wachana nyavu wanaoshiriki mechi za Ligi Kuu ya Soka la Kenya (KWPL). Kati ya orodha hiyo inajumuisha: David ‘Calaba’ Owino na Teddy Osok, Brian Bwire (Tusker FC), Eugene Wethuli (Mathare United), Keith Imbali na Brian Opiyo wote (Kariobangi Sharks), Stephen Ochola (Sofapaka) kati ya wengine.

”Kama mwanzilishi wa KYSD nina imani tosha kuwa endapo tutafaulu kupata wadhamini tuna uwezo wa kukuza wachezaji wanaokuja na kuibuka kati ya wachezaji mahiri nchini, akasema huku akiongeza kuwa eneo hilo limefurika wachezaji wengi wanaokuja ila huwa vigumu kutambuliwa maana wametokeo mitaa ya viwango vya chini.

KINYAG:Timu ya Kinyago United mabingwa wa KYSD Top 8…Picha/JOHN KIMWERE

You can share this post!

Kocha Lennon ayoyomea Cyprus kudhibiti mikoba ya Omonia...

Afisa bandia wa polisi asukumwa jela miezi sita

T L