• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:55 AM
Mudavadi achemkia Uhuru kwa madai Ruto alitaka kumng’oa mamlakani

Mudavadi achemkia Uhuru kwa madai Ruto alitaka kumng’oa mamlakani

NA DERICK LUVEGA

KINARA wa ANC Musalia Mudavadi hapo jana alimshambulia vikali Rais Uhuru Kenyatta kuhusu madai kuwa Naibu Rais Dkt William Ruto alipanga njama ya kumwondoa mamlakani mwanzoni mwa muhula wake wa pili.

Rais Kenyatta alifichua kuwa alikosana na Naibu wake baada ya kugundua kuwa alikuwa akitumia njia za kichinichini kumtimua mamlakani ikiwemo kumfikia Kinara wa ODM Raila Odinga ili kupata uungwaji mkono wake.

Kiongozi wa nchi alisema hayo katika mkutano na wazee wa jamii ya Agikuyu katika Ikulu ya Nairobi. Aliutumia mkutano huo kuwashawishi wamuunge mkono Bw Odinga kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Hata hivyo, Bw Mudavadi alimkemea Rais Kenyatta, akishangaa kwa nini hakumchukulia Dkt Ruto hatua wakati huo au kuweka suala hilo hadharani. Bw Mudavadi pamoja na Kinara wa Ford Kenya Moses Wetang’ula wapo kwenye muungano wa Kenya Kwanza na

Dkt Ruto. “Inashangaza kuwa Naibu Rais ana mamlaka kiasi kuwa anaweza kupanga njama ya kumwondoa bosi wake ofisini. Hilo lingetimia aje ilhali bado anashikilia wadhifa huo hadi leo? Rais Kenyatta anajaribu tu kuhadaa umma,” akasema Bw Mudavadi wakati wa mkutano wa kisiasa katika kijiji cha Muhudu, eneobunge la Hamisi, Kaunti ya Vihiga.

“Ruto bado ni naibu wako. Kwa nini hukumwondoa mamlakani wakati huo? Kwa nini alitaka kukuondoa mamlakani?” Naibu waziri huyo mkuu wa zamani alisema kuwa Rais Kenyatta anazua masuala ambayo hayana ukweli wowote na anasaka huruma za Wakenya hasa ngome yake ya kisiasa ili kumuuza Bw Odinga.

Mkutano wa Rais Kenyatta na wazee hao zaidi ya 3,000 ulionekana kama mbinu ya kuwashawishi wamvumishe Bw Odinga katika eneo la Kati. Bw Odinga analenga Urais kwa mara ya tano ila mara hii kupitia vuguvu la Azimio la Umoja.

Kulingana na habari katika gazeti moja hapa nchini jana, Rais Kenyatta aliwasimulia wazee hao

jinsi alivyohadaiwa kuwa ashughulike masuala ya serikali huku Dkt Ruto akisimamia chama tawala cha Jubilee.

Alidai ni kutokana na hilo ambapo baadhi ya wandani wake walienguliwa kwenye uteuzi wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017.

Kwenye misururu ya kampeni katika ngome yake ya kisiasa, Bw Mudavadi alisema nia ya Rais Kenyatta ni kuelekeza jamii ya Mulembe katika upinzani, akidai kuwa Bw Odinga hawezi kumpiku Dkt Ruto kwenye uchaguzi mkuu.

“Hawezi kumshawishi mbunge wake na seneta waunge Azimio. Kama vuguvugu hilo ni zuri kwa nini asianze na jamii yake? Hawezi kwa sababu watu kutoka Mlima Kenya wanafahamu Kenya Kwanza ndiyo itaunga mkono serikali,” akaongeza.

Alikuwa ameandamana na wabunge Alfred Agoi (Sabatia), Omboko Milemba (Emuhaya), Charles Gimose (Hamisi), Benjamin Washiali (Mumias East) na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Vihiga Beatrice Adagala.

  • Tags

You can share this post!

Wagonjwa wa figo Lamu taabani, wahamishiwa Mombasa

Hoteli zapata pigo kufuatia gharama ya juu ya bidhaa

T L