• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
NCPB mabingwa wa handiboli

NCPB mabingwa wa handiboli

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wanaume ya Halmashauri ya Nafaka na Mazao nchini (NCPB) imeibuka mabingwa wa Ligi Kuu ya Handiboli msimu wa 2018/2019 baada ya kuikung’uta Black Mamba mabao 23-18 uwanjani Kaloleni, Nairobi. Madume hao ambao hutiwa makali na kocha, Dunstan Eshikumo walibeba ubingwa wa taji hilo na kumaliza ukame wa miaka minne.

Black Mamba ya kocha Martin Abunde ilitangulia kuongoza kwa mabao 5-3 kabla ya NCPB kubadili mambo na kuwa magoli 5-5, 9-9, 13-11, 17-13 kisha kumaliza kazi kwa kufikisha alama 23-18. NCPB ilitawazwa wafalme wa msimu huu wiki mbili baada ya malkia wa Nairobi Water kutangazwa kuhifadhi ubingwa wa ngarambe kwa mara ya sita mfululizo tena bila kushindwa mchezo wowote.

”Wachezaji wangu waliteleza na kufanya makosa machache yaliyochangia kukosa ujanja mbele ya mahasimu wetu na kudondosha alama zote muhimu,” kocha wa Black Mamba alisema na kuongeza kwamba hawakuwa na budi mbali kuacha yaishe.

Akipongeza wachezaji wake kocha wa NCPB alisema “Tumejaa furaha tele maana msimu huu tumefanya vizuri baada ya kukosa taji hilo tulipoteza kwenye mchezo wa mwisho msimu uliyopita.” Kadhalika alidokeza kuwa tangu mwanzo wa kampeni za msimu huu wachezaji wake wamekuwa na hamu sana kuvuruga rekodi ya Black Mamba ambayo imelibeba mara nne.

Nao Kelvin Obunga na Maxwell Munene walitikisa nyavu mara saba na sita mtawalia na kubeba Strathmore University kunasa ufanisi wa magoli 30-13 dhidi ya Ulinzi (KDF). Nicholas Ireri aliibuka mchezaji bora alipotingia Ulinzi mabao sita.

You can share this post!

TAHARIRI: Ukimwi bado hauna tiba japo kuna tumaini

Vita kati ya Ruto na Raila vyazidi kupamba moto

adminleo