• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Ofa ya Arsenal kusajili Declan Rice kwa Sh18.7 bilioni yakubaliwa na West Ham

Ofa ya Arsenal kusajili Declan Rice kwa Sh18.7 bilioni yakubaliwa na West Ham

Na MASHIRIKA

OFA ya Arsenal ya kumsajili kiungo matata wa Uingereza, Declan Rice, kwa kima cha Sh18.7 bilioni kutoka West Ham United imekubaliwa.

Kwa sasa mazungumzo kati ya West Ham na Arsenal yanaendelea kuhusu jinsi ada hiyo kwa ajili ya sogora huyo mwenye umri wa miaka 24 italipwa.

Ofa mpya ya Arsenal kwa Rice ni ya tatu baada ya majaribio mawili ya awali kukataliwa huku West Ham wakisisitiza kuwa thamani ya sogora huyo aliyekuwa pia akihemewa na Manchester City ilikuwa zaidi ya Sh17.8 bilioni.

Man-City walijiondoa kwenye vita vya kupigania saini ya Rice baada ya ofa yao ya Sh16 bilioni kukataliwa na West Ham.

Rice amekuwa nahodha wa West Ham na alijiunga rasmi na akademia ya kikosi hicho baada ya kuagana na Chelsea mnamo 2014.

Mapema Juni 2024, aliongoza West Ham kupepeta Fiorentina 2-1 na kujizolea taji la Europa Conference League ambalo lilikuwa la kwanza kwa historia ya kikosi hicho tangu 1980.

Mkataba wa Rice kambini mwa West Ham ulikuwa ukatike rasmi mnamo Juni 2024.

Kwa mujibu wa maafikiano yao na West Ham, Arsenal watalipa ada ya kwanza ya Sh17.8 bilioni kabla ya kulipa awamu ya pili ya Sh900 milioni polepole. Ada ya awali ya Sh17.8 bilioni inawiana na kiasi cha fedha kilichowekwa mezani na Man-City kwa ajili ya kiungo Jack Grealish kutoka Aston Villa.

Mapema mwezi huu wa Juni 2023, kiungo matata raia wa Uingereza, Jude Bellingham alisajiliwa na Real Madrid ya Uhispania kwa Sh15.8 bilioni ingawa ada hiyo inatarajiwa kufikia Sh20.5 bilioni.

Enzo Fernandez wa Argentina ndiye sogora ghali zaidi katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kusajiliwa na Chelsea kwa Sh19 bilioni kutoka Benfica ya Ureno mnamo Januari 2023.

Mwenyekiti wa West Ham, David Sullivan, amesema ana uhakika wa asilimia 99 kuwa Rice atabanduka kambini mwao muhula huu licha ya nahodha huyo kuwaongoza kujizolea taji la  Europa Conference League mwezi huu na hivyo kufuzu kwa Europa League msimu ujao.

Rice amevalia jezi za West Ham mara 245 na kuwafungia mabao 15 tangu msimu wa 2016-17. Amewajibishwa mara 43 kimataifa na alinogesha michuano yote mitano iliyosakatwa na Uingereza katika Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

Rice atakuwa sogora wa pili kusajiliwa na Arsenal muhula huu baada ya kujinasia maarifa ya Mjerumani Kai Havertz kutoka Chelsea kwa Sh11.6 bilioni.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

  • Tags

You can share this post!

Hatua ya Ruto kuruhusu washauri watatu kwenye Baraza la...

Mourinho apigwa marufuku ya siku 10 na kutozwa faini ya...

T L