• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
SHINA LA UHAI: Abainisha mchango wa wanaume katika upangaji uzazi

SHINA LA UHAI: Abainisha mchango wa wanaume katika upangaji uzazi

NA WANGU KANURI

BAADA ya kumpata kitinda mimba wake, mnamo 2014, Tony Hutia aliamua kukatwa mrija wa uzazi (vasectomy).

Baba huyo wa watoto wanne, alikubali kuhasiwa ili kumuondolea mke wake kero zinazotokana na mbinu za upangaji uzazi kwa wanawake.

Anasema kuwa mara ya kwanza kumweleza mke wake kuwa alinuia kuhasiwa, alijawa na matumaini licha ya dukuduku za kama angekubali au la.

Siku chache kabla ya kufanyiwa upasuaji, Bw Hutia alimfahamisha mke wake tena lakini bado alimshuku mpaka aliporudi nyumbani na ripoti kutoka kwa daktari.

Hali kadhalika, Bw Hutia aliogopa sana kama angeweza kusisimka kingono kama awali.

“Isitoshe nilihofia mbegu za kiume kupita licha ya kuhasiwa,” anasema.

Huku upasuaji huo ukimchukua dakika 30, Bw Hutia anaeleza kuwa alikuwa amepata afueni chini ya wiki moja.

“Nilishauriwa kutoshiriki ngono na kutofanya kazi ngumu katika kipindi hicho,” anaeleza.

Hata hivyo, Bw Hutia anasema kuzungumzia kuhasiwa kwake kumewafanya wengi kumshangaa huku wengine wakishuku uwezo wake wa kusisimka kingono.

“Wanaume wengi wameshikilia itikadi potovu kuhusu kukatwa mrija wa uzazi huku asilimia kubwa wakishikilia kuwa upangaji uzazi ni jukumu la mwanamke.”

Dkt Muigai Mararo, mtaalamu wa masuala ya mfumo wa kupitisha mkojo katika hospitali ya RFH Healthcare, anaeleza kuwa kuhasiwa ni namna ya upangaji uzazi ambayo mwanamume hukatwa mrija unaopeleka mbegu za kiume.

Unapokatwa mrija huo hufungwa ili kuzuia mbegu za kiume kufika kwenye uke wa mwanamke wanaposhiriki katika tendo la ndoa.

Njia hii ya upangaji uzazi na japo inaweza kugeuzwa, Dkt Mararo anashauri kuwa uhakika wa kugeuza ni mdogo.

“Baada ya mwanamume kuhasiwa anaweza akawa na maumivu na akafura kidogo kwenye korodani zake na akatokwa na damu lakini wengi wao hupona baada ya siku kadhaa,” anasema Dkt Mararo.

Hata hivyo, mwanamume aliyehasiwa anaweza akamtia mwanamke mimba iwapo kuna mbegu za kiume kwenye mirija yake.

Dkt Mararo anasema kuwa kwa kipindi cha wiki nane baada ya mwanamume kukatwa mrija wake wa uzazi, anaweza mtia mwanamke mimba.

“Baada ya wiki nane, mwanamume aliyehasiwa anapaswa kuchunguzwa kuangalia iwapo mbegu zipo au la,” anasema.

Ukataji mrija wa uzazi hukadiria asilimia 99 ya kutomringa mwanamke mimba.Licha ya kutokuwa na wakati maalum wa kushiriki katika tendo la ndoa baada ya kuhasiwa, Dkt Mararo anashauri kuwa mwanamume anapaswa kukumbuka kuwa kabla ya wiki nane, anaweza mtia mpenziwe mimba.

“Ninapigia debe kuhasiwa kwa wanaume kwani wao pia wanaweza kupanga familia zao.”

Hata hivyo, Dkt Mararo anasema kuwa ipo haja ya kuwaelimisha watu kuhusu ukataji mrija wa uzazi kwa wanaume ili kuondoa itikadi potovu na hata kuwa maarifa yasiyo kweli.

Bw Hutia ambaye amekuwa mstari wa mbele kubadilisha mtazamo wa upangaji uzazi kwa wanaume, anasema kuwa ushirikiano uliopo baina ya wanandoa wakati wa kumpata mtoto unapaswa kusheheni wanapopanga uzazi.

“Upangaji uzazi kwa wanaume hauna madhara mengi ikiwa mtu hana magonjwa mengine ikilinganishwa na wanawake,” anasema.

Maarifa

Ukosefu wa maarifa kuhusu kuhasiwa pia kumechangia katika idadi ndogo ya wanaume waliokatwa mrija.

Bw Hutia anaeleza kuwa alipozungumzia suala hilo na daktari wa uzazi wa mke wake, alishauriwa kutofanyiwa upasuaji huo.

Hata hivyo, wanaume wengine pia hukataa kuhasiwa kwa kutaka watoto wengine huku Bw Hutia akisema kuwa wakati Mungu aliwapa watu uhuru wa kujaza dunia hakukueleza wewe peke yako.

Kulingana na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Maradhi barani Afrika (CDC), mmoja kati ya wanawake 100 hupata mimba mwaka wa kwanza baada ya mpenzi wao kuhasiwa.

Hata hivyo, mwanamume aliyekatwa mrija wa uzazi hawezi epuka magonjwa yanayoenezwa kupitia ngono kama vile kisonono, kaswende, ukimwi huku CDC ikishauri matumizi ya mipira ya kondomu wakati wa kushiriki katika tendo la ndoa.

“Njia hii ya upangaji uzazi haiathiri tendo la ndoa huku mwanamume huyo akiweza kusisimka kama kawaida lakini majimaji yake hayatakuwa na mbegu za kiume,” inasema ripoti ya CDC.

Baada ya upasuaji, majimaji ya mwanamume aliyehasiwa yanaweza kuwa na damu.Hakikisha kuwa unakadiria usafi na kujipangusa vizuri unapotoka kuoga.

“Vaa chupi iliyokushika wakati wa mchana na usiku siku za kwanza baada ya kufanyiwa upasuaji ili kupunguza maumivu kwenye korodani. Vile vile, badilisha chupi hiyo kila siku.”

Madaktari wengi hushauri wanaume walio na zaidi ya miaka 30 na waliotosheka na idadi ya watoto walio nao kufanyiwa upasuaji huu japo kwa hiari ya mtu.

Mwanamume aliyehasiwa anaweza endelea na shughuli za kujitafutia riziki baada ya siku moja au mbili lakini asiinue vitu nzito kabla wiki moja kuisha.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yajikokota kukamilisha ujenzi wa daraja la mbao...

TIBA NA TABIBU: Wakenya wapokea chanjo kudhibiti...

T L