• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Utamaduni Dei: Taswira mseto mahasla wakifungua biashara zao, sekta ya uchukuzi ikilia

Utamaduni Dei: Taswira mseto mahasla wakifungua biashara zao, sekta ya uchukuzi ikilia

NA SAMMY KIMATU

WAKENYA hawajajitokeza kwa wingi maeneo ya umma kuadhimisha Utamaduni Dei. 

Katika mitaa ya mabanda ya Mukuru, biashara za mahasla zimefunguliwa kama kawaida, wengi wao wakisema hawana muda wa kuenda Bomas ambako viongozi wamejumuika kuadhimisha siku hiyo muhimu kwa kalenda.

Mahasla wa mitaa ya Mukuru iliyoko katika maeneo bunge matatu ya Starehe, Makadara na Embakasi Kusini wamefungua biashara zao za vinyozi, vibanda vya mboga, buchari na saluni.

Baadhi yao wameambia Taifa Leo hawawezi kupumzika wakati mahitaji yakiongezeka kila uchao.

Kwa upande mwingine, wahudumu wa matatu wanaohudumu katika eneo la Industrial Area jijini Nairobi wamesema Jumanne hawakupata faida kama siku za kawaida kutokana na kampuni nyingi kufungwa siku ya Utamaduni.

Matatu zinazohudumu kutoka Muthurwa kuelekea Hillock na Muthurwa kuelekea Lunga Lunga hutegemea wafanyakazi wanaosafiri kuelekea eneo hilo la Industrial Area.

Ni matatu chache zilizohudumu Jumanne kutokana na upungufu wa abiria.

Katika vibanda vya juakali eneo la Kamukunji sawa na soko la Gikomba, wafanyakazi wameripoti kazini kama kawaida.

Katika barabara ya River Road jijini Nairobi, maduka yamefunguliwa kama kawaida lakini wafanyabiashara wamelalamika wakisema wateja walikuwa wachache siku hiyo ya mapumziko.

Biashara zikiwa zimefunguliwa katika barabara ya River Road jijini Nairobi. Wafanyabiashara wengi wamelalama kwamba wateja wamekuwa wachache Utamaduni Dei. PICHA | SAMMY KIMATU

Katika kituo cha matatu cha Tea Room, ambapo magari mengi huhudumu baina ya Nairobi na miji ya eneo la Mlima Kenya, wasafiri wameonekana wakiwa wachache ikilinganishwa na siku nyingine za kawaida kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa.

“Kwa kawaida, watu husafiri kwa wingi kuelekea kwa miji ya eneo la Mlima Kenya. Leo ni siku ya Utamaduni lakini wateja hawako. Pia uchumi sio mzuri kwa Wakenya baada ya mafuta kupanda,” dereva wa NNK Sacco ameambia Taifa Leo.

Utamaduni Dei: Wasafiri wamekuwa wachache katika kituo cha mabasi cha Tea Room jijini Nairobi. PICHA | SAMMY KIMATU
  • Tags

You can share this post!

Ndoa ya mitara inatambulika kisheria, Karen Nyamu ajitetea...

EACC yataka abiria wapige picha polisi fisadi wa trafiki

T L