• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
SHINA LA UHAI: Nilizaliwa na HIV; kila siku napambana kuhamasisha jamii kujilinda

SHINA LA UHAI: Nilizaliwa na HIV; kila siku napambana kuhamasisha jamii kujilinda

NA PETER CHANGTOEK

ALIZALIWA akiwa na virusi vya Ukimwi na amekuwa akiishi na virusi hivyo kwa takribani miongo mitatu.

Cleopatra Wanjiku Machira alizaliwa 1993, na hakujua kuwa alizaliwa na virusi hivyo, hadi 2007.

Anasema kuwa, kila mara, alikuwa akiuguaugua, pasi na kujua chanzo cha kuugua kwake kila mara.

Hata hivyo, alipokuwa na umri wa miaka kumi na mitatu, alipokuwa akitibiwa ugonjwa wa kifua, ndipo daktari alipoamua kumpima, na ikabainika bayana kuwa alikuwa na virusi vya Ukimwi.

Anasema kwamba, alipigwa na butwaa, alipofichuliwa siri ambayo hakuwa amejua kwa muda huo wote.

“Kusema ukweli, kumpoteza mamangu nikiwa na umri wa miaka minane, na kuambiwa nina virusi vya ukimwi, ikadhihirika kuwa dunia si ya kuaminika. Nilihisi kana kwamba dunia imefika mwisho,” asimulia.

Wanjiku, mwenye umri wa miaka 29, akaanza kuzitumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo, na amekuwa akizitumia kwa muda wa miaka 16.

Hata hivyo, hajafa moyo. Amekuwa katika mstari wa mbele kuwahamasisha waja kuhusu ugonjwa huo, na ameanzisha shirika linalojulikana kama The Voice of a Black Child – Sauti ya Mtoto Mweusi.

Amekuwa akilitumia shirika hilo kuwahamasisha watu kujua hali zao, kupimwa, kuacha unyanyapaa, kuacha kusambaza virusi, miongoni mwa masuala mengine.

Yeye pia ni mwanafasheni na anamiliki duka la kuuza mavazi ya Kiafrika, linalojulikana kama Pabaa Collections, lililoko jijini Nairobi.

Huuza bidhaa za Ankara na za shanga, kama vile herini, bangili, mikufu na vikuku.

“Nimekuwa na familia ambayo imekuwa ikinishika mkono kila wakati. Imekuwa ni safari yenye ujasiri, maamuzi na ukakamavu,” asema.

Wanjiku anaongeza kwamba, shirika lake limesajiliwa na halishughuliki tu na uhamasishaji kuhusu athari za Ukimwi, bali pia, hushughulika na afya ya uzazi na haki, pamoja na uhamasishaji kuhusu upangaji wa uzazi.

Aidha, huimarisha vita dhidi ya unyanyapaa na ubaguzi katika jamii.

“Nilianzisha shirika hili baada ya kutangaza kwa umma hali yangu, na mwaka mmoja umepita tangu tuanze kubadilisha maisha ya wale tunaowanufaisha,” aongeza Wanjiku.

Alianzisha mwaka 2021, alipokuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Wamekuwa wakitembelea makao ya watu na sehemu nyingine. Wametoa uhamasishaji mara tatu katika makao ya watoto walio na virusi vya Ukimwi, katika gereza la Nyeri na katika Dayosisi ya Sacred, Murang’a.

“Tumepata fursa ya kushirikiana na kampuni za Indomie Kenya, Tropical Heat, Zingo Africa, Cakes & Muffin House, Street Artskool,” afichua, akiongeza kwamba, wamekuwa wakiwapa bidhaa za vyakula wale wanaowatembelea.

Wanjiku anasema kwamba, changamoto kuu ni kupata fedha za kutosha za kuendesha shughuli zao. Hata hivyo, anasema washirika wake wana ushirikiano mwema.

Anawashauri wale ambao hawajaathirika kuendelea kujikinga na kwa wale walioathirika, anawashauri kuwa maisha yanafaa kuendelea hata baada ya kuambukizwa.

“Maisha hayatasimama kwa sababu tuna dawa zinazohakikisha kuwa unaishi maisha yako kikamilifu,” ashauri Wanjiku.

Ombi lake ni kukua kwa shirika lake ili liwasaidie wengi.

“Utafiti unaonyesha kwamba, vijana 15 huathirika na virusi vya Ukimwi kila siku; kumaanisha kuwa, kuna kazi kubwa ambayo tunafaa kufanya ili kuzuia maambukizi mapya,” afichua.

Anadokeza kwamba, wamezuru kaunti tano nchini, na wanalenga kupeleka huduma zizo hizo katika kaunti nyinginezo, ili kuwaokoa vijana kutokana na janga la Ukimwi.

Hata hivyo, anasema kuwa hawajajitosheleza kifedha.

“Lakini tunaamini kuwa, malengo yetu na matendo yetu yatatimia; kuwasaidia wasiojiweza katika jamii na kuboresha maisha, hususan wale walioathirika sana na virusi vya Ukimwi, hasa vijana wasiomudu kupata chakula, mazingira yanayofaa na kupata dawa. Yeyote aliye na nia ya kushirikiana nasi anakaribishwa,” asema.

You can share this post!

Nyama ya sehemu ya ubavu iliyookwa katika ovena

BENSON MATHEKA: Tuchukulie kwa wema pendekezo la kuundwa...

T L