Makala

TAHARIRI: Mtaala mpya unahitaji umakinifu

October 3rd, 2018 2 min read

Na MHARIRI

KENYA inapojiandaa kuzindua mtaala mpya wa elimu, itakuwa muhimu mambo kadhaa muhimu yazingatiwe kwa makini.

Mfumo wa 2-6-3-3-3 unaochukuliwa kama madhubuti zaidi maadamu mbali na kuwapa wanafunzi maarifa, unawaandaa kwa maisha ya siku za usoni na jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali (Competency Based Curriculum) ni mfumo mzuri unaowiana na mabadiliko ya kiwakati.

Maarifa ya darasani bila ujuzi wa kutatua changamoto za kila siku kwa hakika hayana manufaa mengi.

Hii ndiyo maana tunapounga mkono utekelezaji wa mtaala huo mpya unaoanza rasmi mwakani hasa baada ya kuidhinishwa na wataalamu wa kigeni Jumatano, ni muhimu kuhakikisha kuwa utekelezaji huo unafanyika kwa njia nzuri bila kuathiri maendeleo ya wanafunzi.

Ni dhahiri kuwa, japo mtaala huu unakaribia kuanza, nyenzo za masomo kama vile vitabu vya kiada na vya ziada hazijawa tayari. Ni muhimu serikali ihakikishe kuwa nyenzo hizo zinakuwa tayari kabla ya mfumo huo kuanza hapo Januari kama ilivyopangwa.

Vilevile, walimu wengi wamelalama kuwa hawajapewa mafunzo ya kutosha ya kufaulisha utekelezaji wa mfumo huo mpya wa elimu.

Maadamu dhamira kuu ya mtaala huu ni kuhakikisha kuwa mwanafunzi anaandaliwa kukabili maisha ya kisasa jinsi yalivyo, ni busara serikali kuhakikisha kuwa kila mwalimu amepata mafunzo ya kutosha kuhusu mtaala wenye huo. Kama sivyo, tusitarajie mabadiliko makubwa katika wanda la elimu, bali mambo kuwa yaleyale ya zamani ambayo tunajaribu kuyakwepa.

Haya yanapotekelezwa pia itakuwa muhimu serikali kufahamu kuwa hivi karibuni masomo yatakuwa yakifanyika kupitia mitandao, hivyo basi, ipo haja ya kuendeleza mradi wa vipakatalishi shuleni. Hii inamaanisha kuwa sharti miundomsingi iliyopo kwa sasa ikarabatiwe na hata mingine kujengwa upya.

Miundomsingi kama vile madarasa ya masomo itafaa kupanuliwa kwa sababu kwa mujibu wa mtaala huo, 2-6 itamaanisha miaka miwili ya shule ya chekechea na mingine sita ya shule ya msingi.

Ikichukuliwa kuwa shule ya upili ya kiwango cha chini itachukua miaka mitatu ya kwanza, pana uwezekano mkubwa kuwa badala ya kujenga majengo mapya, madarasa ya sasa ya darasa la saba na nane yatatumika. Hii inamaanisha kuwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho katika kiwango hicho watahitaji angaa darasa moja zaidi.