Chokoraa 15 washtakiwa kwa kutovalia barakoa

Na TITUS OMINDE

VIJANA 15 wa kurandaranda mjini Eldoret, walikiri mashtaka ya kukosa kuvalia barakoa. Vijana hao walipatikana katika maeneo tofauti ya umma mjini Eldoret.

Hata hivyo, korti iliwaachilia huru baada ya kuwaonya dhidi ya kukosa kuvalia barakoa.Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Eldoret, Bw Barnabas Kiptoo, alielezwa kuwa washukiwa walikamatwa wakati wa msako wa wato wanaokiuka kanuni za kudhibiti msambao wa corona.

“Hata kama mahakama hii imewasamehe kwa onyo kwamba ikiwa utarudia kosa lile lile utakamatwa, kuvaa barakoa ni kwa afya yako na watu walio karibu nawe, si adhabu,” hakimu aliwaeleza.

Kamishna aagiza wauzaji wa barakoa feki wanaswe

Na TOM MATOKE

MAAFISA wa Usalama katika Kaunti ya Nandi wameagizwa kukamata wafanyabiashara wanaouza barakoa feki.

Kamishna wa Kaunti ya Nandi Herman Shambi, alisema kuwa barakoa nyingi zinazouzwa kwa kati ya Sh5 na Sh10 katika miji mbalimbali ya Kaunti hiyo ni feki na zinachangia kusambaa kwa virusi vya corona.

Alisema kuwa maelfu ya wafanyabiashara wamefurika katika miji mbalimbali ya kaunti hiyo kuuza barakoa hizo zisizo na uwezo wa kuzuia virusi.

“Ndani ya miezi mitatu iliyopita, Kaunti ya Nandi imepoteza watu 54 kutokana na virusi vya corona. Nandi inapakana jimbo moja na kaunti za Nyanza na Magharibi ambazo zina maambukizi ya juu ya virusi vya corona,” akasema Bw Shambi.

Kamishna huyo pia alisema kuwa maafisa wa usalama watakamata watu watakaopatikana wakila chakula matangani na sherehe za harusi.

Aliagiza kuwa miili ya watu wanaofariki izikwe ndani ya saa 72 na machifu watekeleze marufuku ya waombolezaji kula matangani.

Bw Shambi pia aliagiza machifu kuhakikisha kuwa idadi ya waombolezaji wakati wa mazishi haipiti watu 50.

Bw Shambi aliyeandamana na Naibu Gavana wa Nandi Dkt Yulita Mitei na waziri wa afya Ruth Koech, alikuwa akizungumza alipoongoza kamati ya kukabiliana na corona mjini Kapsabet.

Aliagiza wahudumu wa matatu kuhakikisha kuwa abiria wote wanavalia barakoa.Naye Bw Koech alifichua hospitali za kaunti hiyo hazina gesi ya oksijeni ya kutosha.

 

Mwanamke afa kwa ‘hofu ya kukamatwa na polisi’ Kilifi

Na MAUREEN ONGALA

MWANAMKE katika kijiji cha Kwa Mwango, Kaunti ya Kilifi amefariki kwa kile wakazi wametaja kuwa mshtuko uliotokana na msako wa polisi dhidi ya watu ambao hawakuwa wamevaa barakoa mnamo Jumatatu.

Wakazi walisema alikimbizwa katika hospitali ya kibinafsi alipozirai baada ya kushtuka, wakati habari zilipoenea kwamba maafisa wa polisi walikuwa wanakamata watu ambao hawakuwa wamevaa barakoa.

“Alikuwa ameniambia niandamane naye kuchukua pesa alizokuwa akidai wateja wake eneo la Kiwandani. Tulipokuwa tunarudi nyumbani tulikutana na kijana aliyetwambia tuvae barakoa kwa sababu polisi walikuwa wanaelekea upande wetu,” akasema rafiki yake, Bi Nelvina Nzai.

Kulingana na Bi Nzai, kijana huyo alikuwa anawatoroka polisi hao kwa vile hakuwa na barakoa.

“Kitsao alikuwa anang’ang’ana kutoa barakoa yake mkobani lakini hakuwa anaiona. Wakati mmoja alitaka kutoroka lakini nikamwambia atulie na aitafute tu polepole,” akasimulia Bi Nzai.

“Hata alipofanikiwa kuipata alikuwa bado anashindwa kuivaa na akaanza kulalamika kuwa moyo wake ulikuwa unapiga kwa kasi kuliko ilivyo kawaida. Alinishikilia kwa nguvu akisema moyo wake unadunda kwa kasi kisha akaanza kukohoa damu,” akasema.

Alipandishwa pikipiki na kukimbizwa hospitalini na walipokuwa njiani, waliona gari la polisi mbele yao eneo la Kavunjeni likiwa limejaa watu waliokamatwa.

Jamaa yake, Bw Stephen Wanje, alisema marehemu alikuwa anaugua ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu.

Familia hiyo ililaumu polisi kwa ukatili ambao hufanya raia kuwaogopa hata kama hawana makosa au wakiwa na makosa madogo.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kilifi Kaskazini, Jonathan Koech, alishauri familia hiyo iwasilishe ripoti rasmi kwa polisi ili uchunguzi ufanywe.

“Ni muhimu upasuaji wa mwili ufanywe kwanza ili kujua chanzo cha kifo. Sisi kama polisi tunataka kufanya kazi yetu kwa kuheshimu haki za binadamu, na kama kuna yeyote aliye na malalamishi kuhusu dhuluma, inafaa apige ripoti,” akasema Bw Koech.

Pia aliwataka raia wafuate sheria kila wakati ikiwemo zinazolenga kuzuia ueneaji wa virusi vya corona.

Bi Tecla Katana, ambaye alimlea marehemu, alisema binti yake alikuwa mwenye bidii licha ya kuugua.

“Alikuwa na bidii ya kujitafutia riziki ili kugharimia matibabu yake. Alifariki akijitafutia riziki. Ningali nimeshtuka,” akaomboleza.

Marehemu alikuwa ni mshonaji nguo na muuzaji leso.

Alisema alianza kumlea marehemu pamoja na dadake baada ya wazazi wao kufa alipokuwa na umri wa miaka minne na dadake miaka 10.

Kitendawili cha barakoa

NA PAULINE ONGAJI

WIKI moja baada ya shule kufunguliwa – baada ya wanafunzi kukaa nyumbani kwa muda wa miezi kumi kufuatia janga la virusi vya corona – wazazi wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kusimulia visa kuhusu watoto wao na barakoa shuleni.

Baadhi ya wazazi wamekuwa wakielezea jinsi watoto wao, haswa wanaosoma chekechea na Gredi 1, wamekuwa wakirejea nyumbani jioni na barakoa za rangi tofauti na walizoenda nazo asubuhi.

“Mtoto wangu alitoka na barakoa ya rangi ya bluu asubuhi lakini alirudi jioni na nyeupe. Sijui kilichofanyika shuleni. Ni maombi tu,” akaandika Mercy Aoko katika mtandao wa Twitter.Naye John Wanyoike alisema kuwa bintiye anayesoma chekechea alirejea nyumbani bila barakoa licha ya kwenda nayo shuleni asubuhi.

“Mwanangu anayesoma ‘Play Group’ (darasa la kuwaandaa watoto kujiunga na chekechea) alirejea na barakoa mbili jioni na nilipojaribu kumhoji aliniambia kuwa alipewa moja na rafiki yake. Lakini barakoa aliyodai kupewa ilikuwa tayari imevaliwa!” akaelezea Evans Makori kupitia Facebook.

Visa hivyo ni ithibati kuwa kuna changamoto kubwa ya kuhakikisha kuwa watoto wanavalia barakoa shuleni ili kupunguza maambukizi ya virusi vya corona shuleni.

Evelyne Musyoka anayefundisha watoto wa ‘Play Group’ katika shule ya Wonderland, mtaani Kahawa West jijini Nairobi, anakiri kuwa amekuwa na kibarua kigumu kuhakikisha kuwa watoto wanavalia barakoa wakati wote wanapokuwa shuleni.

Anasema kwamba huwa anatumia wakati mwingi kuwakumbusha kuvalia barakoa, kutokaribiana na kunawa mikono mara kwa mara.“Ni kibarua kigumu kuhakikisha kuwa wanavalia barakoa kila wakati. Vilevile, kuna changamoto kubwa kuwazuia kukaribiana wanapokuwa shuleni ili kuwakinga na maambukizi ya corona,” anasema.

Kabla ya kufunguliwa kwa shule wiki iliyopita, waziri wa Elimu Prof George Magoha alisema kuwa hakuna mtoto anayefaa kwenda shuleni bila barakoa.

“Hakuna mwanafunzi ambaye atafukuzwa kutokana na ukosefu wa karo, lakini hakuna mwanafunzi ataruhusiwa kusoma bila kuwa na barakoa. Wazazi wanunulie watoto wao barakoa. Kuanzia sasa barakoa itakuwa sehemu ya sare ya shule,” akasema Prof MagohaNi agizo hilo la Prof Magoha ambalo limesababisha baadhi ya shule kuwarejesha nyumbani wanafunzi wanaofika bila barakoa.

Wizara ya Elimu haijatoa mwongozo kuhusu umri wa watoto ambao hawafai kuvalia barakoa.

Suala la Umri

Umri ambao watoto hawafai kuvalia barakoa limesalia suala la mjadala kote duniani.Mnamo Juni, mwaka jana, Prof Magoha alitoa mwongozo ambapo alisema kuwa watoto wa chini ya umri wa miaka sita hawakufaa kuvalia barakoa endapo shule zingefunguliwa Agosti 1, 2020.

Lakini siku chache kabla ya shule kufunguliwa Januari 4, mwaka huu, waziri huyo wa Elimu aligeuka na kuagiza kuwa ni sharti kila mtoto; kuanzia chekechea hadi Kidato cha Nne, avalie barakoa.

Kaimu mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kuzuia Maradhi Dkt Pacifica Onyancha, mnamo Juni mwaka uliopita, alifafanua kuwa watoto wa chini ya umri wa miaka miwili ndio pekee hawafai kuvalishwa barakoa.

Dkt Onyancha alisema kuwa watoto wa umri wa kati ya miaka 2-5 hawafai kuvalia barakoa wanapokuwa katika ndani ya gari la kibinafsi au peke yao nyumbani.

Mwongozo uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mnamo Agosti mwaka jana, unasema kuwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano hawafai kuvalia barakoa.

“Hili linatokana na ukweli kwamba ni vigumu kuwalazimisha watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kuvalia barakoa kila wakati. Vilevile, kuna uwezekano wa barakoa kutatiza ukuaji wa watoto,” linasema shirika la WHO.Shirika hilo la Umoja wa Mataifa (UN), hata hivyo, lilikiri kuwa uamuzi wa kuwataka watoto wa chini ya umri wa miaka mitano wasivalie barakoa ulitolewa bila kuwa na ushahidi wowote unaotokana na utafiti wa kisayansi.

“Wataalamu wetu waliafikia uamuzi huo baada ya kukubaliana kuwa miili ya watoto hukua kwa kasi wanapokuwa chini ya umri wa miaka mitano. Wakivalia barakoa kwa muda mrefu huenda ukuaji huo ukatatizika,” linasema shirika la WHO.

Badala yake shirika la WHO linapendekeza kuwa njia mbadala kama vile kunawa mikono na kuwatenganisha zinafaa kutumika kuhakikisha kuwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano hawaambukizani corona, haswa wanapokuwa darasani.

“Endapo baadhi ya nchi zitaamua kuwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano wavalie barakoa, basi kunafaa kuwa na uangalizi wa karibu kuhakikisha kuwa hawadhuriki. Lakini mbinu mbadala zinaweza kutumika kudhibiti maambukizi miongoni mwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano badala ya kuwavalisha barakoa,” unaelezea mwongozo wa WHO.

Aidha WHO linapendekeza kuwa watoto wa zaidi ya miaka 12 wanastahili kuvalia barakoa kila wakati sawa na watu wazima.Kituo cha Kudhibiti Maradhi (CDC) kinapendekeza kuwa ni watoto wa umri wa chini ya miaka miwili tu ndio hawafai kuvalishwa barakoa.

CDC pia inapendekeza kuwa watoto walio na ugonjwa wa pumu (asthma) na matatizo mengineyo ya kiafya yanayosababisha ugumu wa kupumua pia hawafai kuvalishwa barakoa.“Watoto walio na ulemavu au wasio na uwezo wa kujitoa barakoa puani bila kusaidiwa pia hawafai kuvalishwa,” unasema mwongozo wa CDC.

Nchini Uingereza, si lazima watoto wa chini ya umri wa miaka 11 kuvalia barakoa shuleni. Nchini humo wanafunzi wa shule za sekondari ndio wanatakiwa kuvalia barakoa mara kwa mara.

Barakoa pia si lazima kwa wanafunzi wa umri wa miaka 11 nchini Ufaransa. Wanafunzi wanaruhusiwa kutangamana wanapokuwa shuleni ila sharti wawe wachache. Madawati na vifaa vingine ambavyo huguswa mara kwa mara na wanafunzi vinanyunyiziwa dawa ya kuua virusi angalau mara moja kwa siku.

Oksijeni

Wataalamu wa afya wamepuuzilia mbali madai ya kupotosha ambayo yamekuwa yakisambazwa katika mitandao ya kijamii kuwa watoto au vijana wanapovalia barakoa, ubongo hushindwa kukua vyema kutokana na uhaba wa oksijeni.

Utafiti uliofanywa na wanasayansi wa nchini Amerika mnamo Julai mwaka jana ulibaini kuwa hakuna ushahidi wa kuthibitisha kuwa barakoa inasababisha ubongo kukosa oksijeni ya kutosha.

Kulingana na CDC, barakoa ni salama kwa watoto na watu wazima.“Kuvalia barakoa ndio njia salama ya kupunguza maambukizi ya virusi vya corona,” kinasema kituo cha CDC.

WHO linashauri kuwa watoto wa chini ya umri wa miaka 12 wasio na matatizo ya kiafya wavalie barakoa zilizotengenezwa kwa kipande cha nguo (fabric).Barakoa zilizojulikana kama ‘surgical’ zinafaa kuvaliwa tu na watoto walio na matatizo ya kiafya kama vile kisukari.

Mwongozo wa WHO pia unahitaji watoto wasivalie barakoa wanapocheza uwanjani ili zisiwazuie kupumua vyema.“Wakati wa michezo, wanafunzi hawafai kukaribiana na walimu wahakikishe kuwa watoto wananawa mikono mara kwa mara,” unasema mwongozo wa WHO.

Tafiti ambazo zimefanywa nchini Amerika, Sweden na Norway zimebaini kuwa kuna kiwango cha chini cha maambukizi miongoni mwa wanafunzi wa chekechea.Ili kuepuka visa vya kubadilishana barakoa shuleni, mtaalamu wa masuala ya saikolojia ya watoto Dkt Dorcas Magai, anasema kuwa wazazi au walimu wanafaa kuhakikisha kuwa wanawapa watoto barakoa za rangi wanazopenda

.“Mnapoenda kununua barakoa, basi mwachie mtoto achague rangi ya barakoa anayohitaji. Hii ni kwa sababu ukimnunulia rangi asiyoipenda akifika shuleni anabadilishana na mwenzake,“Mtoto anaposhirikishwa katika kuchagua barakoa ataipenda na ataivalia bila kumezea mate za wenzake,” anasema Dkt Magai.

Anasema kuwa mzazi au mwalimu anastahili kuchukua hatua mtoto anapolalamika kwamba hahisi vyema anapovalia aina fulani ya barakoa.

“Mtoto akilalamika kwamba anafinywa na barakoa au hahisi vyema mzazi au mwalimu anastahili kuchukua hatua aibadilishe sio kumlazimisha kuivaa. Ukimlazimisha kuivaa ataitoa akifika darasani na haitakuwa imesaidia,” anaelezea.

Mtaalamu huyo anasema kuwa wazazi wanafaa kumvalisha mtoto barakoa ambayo inamtoshea vyema. Barakoa inayompwaya inaweza kumletea usumbufu wa kuirejesha mara kwa mara.

“Aidha, wazazi au walimu wanafaa kujadili suala la kuvalia barakoa na watoto ili wafahamu umuhimu wake. Watoto wakielewa kwa nini wanavalia haitakuwa rahisi kwao kuitoa,” anasema.

Walimu

Tofauti na mwongozo wa wizara ya Afya kuwa walimu sharti wavalie barakoa wakati wote wanapokuwa darasani, shirika la WHO linasema kuwa walimu wanafaa kuvalia tu wanapokuwa karibu na wanafunzi.

Mwongozo wa WHO unasema kuwa mwalimu anapokuwa umbali wa zaidi ya mita 2 kutoka kwa watoto anaweza kufundisha watoto bila kuvalia barakoa.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Illinois ulibaini kuwa walimu wanapovalia barakoa zilizotengenezwa kwa vitambaa kama vile vitenge, wanafunzi wanakuwa na ugumu wa kusikia anachozungumza.

Watafiti waligundua kuwa barakoa za vitambaa zinapunguza sauti hivyo kusababisha wanafunzi kushindwa kusikia anachosema.Watafiti walipendekeza kuwa walimu wawe wakitumia barakoa zinazojulikana kama N95 au ‘surgical’ ambazo zimebainika kuwa hazizuii sauti.

Kenya sasa yapokea barakoa zinazouzwa moja kwa Sh17,000

Na BRIAN AMBANI

WAHUDUMU wa afya watakuwa wa miongoni mwa watu wa kwanza humu nchini kutumia barakoa zilizotengenezwa kwa teknolojia ya kisasa, ambazo zinagharimu maelfu ya fedha kila moja.

Hapa nchini, wananchi wengi wamezoea kutumia barakoa ambazo zinagharimu kati ya Sh10 hadi Sh100 pekee.

Hata hivyo, barakoa za kielektroniki ambazo zilitangazwa Jumanne nchini na kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya LG zina uwezo wa kusafisha hewa wakati wa kupumua ili kukinga mtumiaji dhidi ya kuvuta hewa chafu, ikiwemo hewa iliyo na viini vya virusi vya corona.

Kampuni ya LG ilitoa msaada wa barakoa 300 aina ya PuriCare zitakazosambazwa kwa madaktari nchini kupitia kwa Muungano wahudumu wa Kimatibabu (KMA).

Kampuni hiyo ilitangaza kwamba zote ni za thamani ya Sh5 milioni kwa pamoja, ambayo inamaanisha kila barakoa ni takriban Sh17,000.

Hata hivyo, upekuzi wa Taifa Leo katika maduka ya mitandaoni ilibainisha kuna mataifa ambapo barakoa aina hiyo huuzwa hadi Sh30,000 kila moja.

Kampuni hiyo sasa inapanga kuanza kuuza barakoa hizo kote nchini mwaka 2021.

Mkurugenzi Mkuu wa LG Afrika Mashariki, Bw Sa Nyoung Kim alisema barakoa hizo zimeletwa wakati ambapo vita dhidi ya virusi vya corona vinashika kasi na watu wanahitaji magwanda ya kujilinda dhidi ya virusi hivyo.

“Barakoa za PuriCare zilitengenezwa ili kukidhi hitaji la vifaa ambavyo vinaweza kuwakinga watu dhidi ya virusi vya corona kote duniani. Barakoa hii inahakikisha kwamba anayeitumia anapumua vyema na kukingwa vizuri,” akasema.

Barakoa hizo ni za kipekee kwa kusafisha hewa inayoingia kwenye pua na ina betri ambayo hufanya kazi kwa muda wa saa nane kabla ya kuzima.

Kuna sehemu maalumu ya kuondoa hewa chafu mwilini mtu anapopumua, bila kuingiza uchafu kupitia sehemu hiyo.

Pia muundo wa barakoa hizo humpa anayezitumia nafasi ya kupumua bila tatizo lolote kwani kuna kidubwasha kinachohisi nguvu za mtu kupumua.

Kidubwasha hicho kitaongeza au kupunguza hewa inayoingia kwa msingi wa nguvu ambayo mtu anapumua nayo.

Kwa mfano, mtu anapoivaa akifanya mazoezi kama vile kukimbia, kiwango cha hewa inayoingia kitaongezeka kuliko kiwango cha mtu aliyekaa kwa utulivu.

Betri ya barakoa hizo huchukua muda wa saa mbili pekee kuchajiwa huku barakoa ikiwa na sehemu ya ndani ambayo inaweza kubadilishwa baada ya anayeivaa kuitumia kwa muda fulani.

Kutumika tena

Barakoa hizo pia zinaweza kusafishwa kisha kutumika tena.

Tayari zaidi ya wahudumu 1,500 wameambukizwa virusi vya corona wakiwa kazini.

Mara nyingi baadhi yao wamelazimika kuwahudumia wagonjwa wa Covid-19 bila kuvaa magwanda ya PPE ilhali wamekuwa mstari wa mbele kupambana na virusi hivyo.

Kulingana na KMA, karibu wahudumu 20 wamefariki baada ya kuugua virusi vya corona mwezi huu pekee huku ugonjwa huo ukiendelea kuenea nchini.

“Kukosekana kwa vifaa vya kujikinga kwa wahudumu wa afya kumekuwa changamoto kubwa kwa utoaji wa huduma hasa kwa madaktari na wahudumu kote nchini. Ingawa KMA inatambua uwezo wa watengenezaji bidhaa kote nchini wa kutengeneza barakoa, tunashukuru kampuni ya LG kwa kutoa barakoa hizi kwa wahudumu wetu wa afya wanaojali maslahi ya wagonjwa,” akasema Rais wa KMA, Dkt Were Onyino.

Kampeni yaja magavana kusisitizia raia umuhimu wa barakoa

Na CHARLES WASONGA

BARAZA la Magavana (CoG) linapanga kuzindua kampeni ya kuwahimiza wananchi kuvalia barakoa nyakati zote kabla ya kuhudumiwa katika afisi za serikali zote 47 za kaunti.

Kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya baraza hilo, Jumba la Delta, Westlands, Nairobi, mwenyekiti wa baraza hilo Wycliffe Oparanya amesema Ijumaa kampeni hiyo inalenga kupiga jeki msimamo wa Serikali Kuu kwamba wajibu wa mtu binafsi ni njia bora ya kudhibiti kuenea kwa Covid-19.

Kauli mbiu ya kampeni hiyo ni “Bila Maski, Hakuna Huduma.”

Hata hivyo Bw Oparanya hakusema ni lini kampeni hiyo inayojulikana kwa kimombo kama “No Mask, No Service”, itaanza kote nchini.

“Kampeni hii itaendeshwa kwa kutumia njia salama na bora za kupitisha ujumbe, zikiwemo redio zinazopeperusha matangazo kwa lugha za kienyeji na mbinu nyinginezo za mawasiliano katika ngazi ya kaunti,” akawaambia wanahabari.

Vile vile, Bw Oparanya alisema serikali za kaunti zinafanya kazi kwa ushirikiano na makamishna wa kaunti, chini ya mwavuli wa Kamati za Kukabiliana na Janga la Covid-19 (CERC).

Hatua za pamoja

Ushirikiano huo, akasema, unalenga kuhakikisha kufanikisha uzinduzi wa hatua za pamoja za kuhakikisha kuwa masharti ya kudhibiti msambao wa corona zinatekelezwa.

Na kama hatua ya kuzuia maambukizi miongoni mwa wahudumu wa afya, Oparanya alisema baraza lake litajizatiti kuhakikisha kuwa wahudumu hao wanapata vifaa kinga (PPEs) vilivyoidhinishwa na Shirika la Kuthibitisha Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBs).

“Ili kufanikisha hili, kaunti zinashirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya kuhakikisha zinanunua PPEs zenye ubora wa hali ya juu kutoka kwa Mamlaka ya Usambazaji Dawa na Vifaa vya Kimatibabu Nchini (KEMSA),” akasema Bw Oparanya ambaye ni Gavana wa Kakamega.

Wahudumu wa afya wametisha kugoma ikiwa serikali kuu na zile za kaunti hazitahakikisha kuwa wanapewa PPEs zenye ubora wa juu ili kujikinga, miongoni mwa sababu nyinginezo.

Hii ni kufuatia vifo vya madaktari na wahudumu wengine wa afya baada ya kuambukizwa virusi vya corona.

Kenya imeandikisha idadi ya juu ya maambukizi tangu mwezi jana ambapo kufukia Ijumaa, Novemba 20, 2020, idadi jumla ya maambukizi ilikuwa imetimu 75, 190 huku idadi ya waliofariki ikifikia 1, 349. Hii ni baada ya watu 19 zaidi kuthibitishwa kufariki kutokana na corona Ijumaa.

Mnamo Alhamisi, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilizindua kampeni kwa jina “Mask Up, Not Down” inayolenga kuwahimiza watu kuvalia barakao ipasavyo ili kujikinga na maambukizi.

Kampeni hiyo inalenga kuwafikia zaidi ya vijana 40 milioni kote Afrika kupitia mitandao ya kijamii miongoni mwa njia nyinginezo za mawasiliano.

Ngilu kusambaza barakoa bila malipo kwa wanafunzi 72,000

Na KITAVI MUTUA

WANAFUNZI 72,000 katika Kaunti ya Kitui watanufaika na barakoa za bure kutoka kwa serikali ya kaunti.

Gavana Charity Ngilu jana alitangaza kuwa, wanafunzi wa Gredi 4, Darasa la Nane na Kidato cha Nne kutoka shule zote 1,400 za msingi na sekondari watapewa barakoa.

Bi Ngilu alisema barakoa hizo zilizotengenezwa na kiwanda cha nguo cha Kitui (Kicotec), zitaanza kusambazwa kesho.

“Serikali ya kaunti imetenga barakoa 200,000 na kila mwanafunzi atapewa mbili,” akasema Bi Ngilu.

Alizungumza hayo katika kiwanda cha Kicotec baada ya kufanya kikao na washikadau wa elimu kujadili jinsi ya kusambaza barakoa hizo. Mkutano huo ulihudhuriwa na maafisa wa wizara ya elimu, viongozi wa vyama vya walimu na wawakilishi kutoka chama cha wakuu wa shule.

Katibu wa Chama cha Walimu wa Shule za Upili na vyuo (Kuppet) tawi la Kitui Benjamin Mutia alisema hatua hiyo ya Gavana Ngilu ni afueni kwa wazazi.

 

Wakazi Nyali wagomea barakoa wakidai viongozi ni wafisadi

Na DIANA MUTHEU

BAADHI ya wakazi katika eneo bunge la Nyali kaunti ya Mombasa wamesusia kuvalia barakoa wakidai kuwa viongozi wa kisiasa nchini wanatumia janga la corona kujitajirisha.

Wakizungumza katika hafla moja katika eneo la Bombolulu, ambapo wahudumu wa afya ya umma walikuwa wakihamasisha wakazi kuhusu janga la corona, wakazi hao waliwataka viongozi kukomesha ufisadi unaoendelea nchini.

Wengi wao walisema huwa wanavalia barakoa wanapowaona maafisa wa polisi tu ili wasikamatwe.

“Tunavalia barakoa kuifurahisha serikali tu. Ufisadi ambao umekithiri wakati huu unasikitisha. Mwananchi wa kawaida anaendelea kuumia, ilhali kuna watu wanaendelea kujichumia pesa bila kujali,” alisema Bw Wycliffe Mogire ambaye anamiliki kibanda cha mboga.

Mhudumu wa bodaboda aliyejitambulisha kama Leonard aliwataka viongozi kusambaza barakoa kwa watu wote.

“Wakati wa uchaguzi, wanasiasa hawa huleta kofia, shati na hata pesa za bure. Kwa nini wasifanye hivyo msimu huu wa janga la corona ilhali tunasikia katika vyombo vya habari kuwa vifaa hivyo vililetwa nchini kama msaada?aliuliza Bw Leonard.

Afisa wa afya ya umma, Bw James Zuri alisema kuwa ni muhimu watu kuchukua jukumu la kujikinga na maradhi ya Covid-19.

Alisema kuwa baadhi ya wakazi wa Mombasa wanapuuza hatua zilizowekwa na Wizara ya Afya, wakihatarisha maisha yao na watu karibu nao.

Bw Zuri pia aliwaonya wakazi dhidi ya kusambaza habari za uongo kuhusu janga hilo.

“Kwa muda huu kuna changamoto mingi lakini ni vyema tujikinge. Wengine wanasema kuwa janga la corona limekwisha. Corona bado ipo, na ni wajibu wetu kuelimisha jamii wafuate maagizo yanayotolewa na wizara ya afya,” akasema.

Mshirikishi kutoka shirika la The United Front ambalo linashirikiana na kaunti hiyo kuhamasisha watu kuhusu janga hilo, Dkt Suleiman Mwamburi alisema kuwa watatafuta mbinu za kupata barakoa, ili wanapowahamasisha wakazi, pia waweze kusambaza kifaa hicho ambacho ni muhimu wakati huu.

Wasiwasi barakoa zilizotumika zikiendelea kutupwa ovyo

Na SAMMY WAWERU

Serikali imeeleza wasiwasi wake kuhusu utupaji kiholela maski zilizotumika ikisema utepetevu huo unatia watu katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona iwapo waliozivalia walikuwa wameugua.

Waziri Msaidizi katika Wizara ya Afya Dkt Rashid Aman amesema kiwango ambacho maski zinaonekana kutupwa katika maeneo ya umma kama vile masoko, vituo vya matatu, kandokando mwa barabara na njia na pia katika vituo vya garimoshi vinazua hofu.

“Tunapaswa kujitahadhari tunavyotupa maski ili kuepuka uchafu wa mazingira na kuhatarisha maisha yetu wenyewe,” Waziri akaonya.

Pia, alihimiza wahudumu wa afya kuwa kielelezo kwa umma katika suala la maski na vifaa vya kuzuia kuambukizwa (PPE) corona baada ya kuvitumia.

Dkt Aman alisema utafiti wa wataalamu wa afya umeonyesha chembechembe za virusi vya corona (Covid-19) vinasalia kwenye maski kwa walioambukizwa.

Alisema utupaji wa maski kiholela unawaweka katika hatari watoto, na ambao ni vigumu kuwadhibiti wanapocheza.

Aidha, Waziri alionya kuwa maski zilizotumika na kutapakaa zinapofurushwa na upepo ni hatari kwa watu.

“Tuwajibike tunapotoa maski na kutupa zilizotumika mahali zinakofaa, na kwa mujibu wa maelekezo ya Idara ya Afya. Kimsingi, utupaji wa taka kiholela ni hatari na ni kuchafua mazingira. Taifa hili lina takriban watu milioni 50, hebu jiulize sote tukitupa maski kiholela hali itakuwaje?” Waziri akahoji, akidokeza kwamba Wizara ya Afya inashirikiana kwa karibu na serikali za kaunti kuibuka na mikakati maalum ya utupaji maski.

Alisema usafi wa mazingira wakati huu taifa linaendelea kuhangaishwa na janga la Covid-19 unapaswa kuwa wa hadhi ya juu.

Waziri pia alisema Wizara ya Afya kwa ushirikiano na serikali za kaunti zinaendelea kuimarisha mikakati kupulizia maeneo ya umma kama vile masoko na vituo vya matatu dawa zenye kemikali kuua viini virusi vya corona.

Waziri alisisitiza haja ya watu kuendelea kuvalia maski hasa wakiwa katika maeneo ya umma, akisema uchunguzi umeonyesha mkakati huo unaosaidia kuzuia kusambaa kwa corona unakiukwa na wengi.

“Uvaliaji maski na umbali kati ya mtu na mwenzake umeidhinishwa kusaidia kuzuia msambao wa virusi vya corona,” alieleza. Pia, watu wanahimizwa kunawa mikono kila wakati kwa sabuni au kwa jeli.

Wanaotupa maski kiholela waonywa

Na SAMMY WAWERU

Maski zilizotumika na kutupwa kiholela na kutapakaa kwenye majaa ya taka huenda zikaweka watu katika hatari ya kuambukizwa Covid-19.

Hofu hiyo imeibuka kufuatia barakoa zinazoonekana kutapakaa kwenye dampo na njia za mitaa, isijulikane hali ya watumizi wake.

Dampo la Dandora, Nairobi, limetajwa kama lililoathirika pakubwa.

Ikikiri kufahamu kuwepo kwa utepetevu huo miongoni mwa wananchi, Wizara ya Afya imesema Kenya ina changamoto nyingi za utupaji wa taka.

“Hapa hapa katika Bustani ya Uhuru Park, utaona maski zilizotupwa kiholela zimetapakaa. Kuna shida kubwa nchini namna ya kutupa taka,” akasema Waziri Msaidizi katika Wizara Dkt Mercy Mwangangi Alhamisi katika kikao na wanahabari katika makao Makuu ya Afya, Nairobi, wakati akitoa taarifa ya maambukizi ya Covid-19 nchini.

Aidha, Waziri alisema ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha mazingira ni safi badala ya kuachia jukumu hilo asasi husika kama vile Mamlaka ya Kitaifa Kuhifadhi Mazingira (Nema).

“Tuwajibike na kuhakikisha mazingira yetu ni safi,” Dkt Mwangangi akahimiza, wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kufuatia malalamishi ya maski kutapakaa katika majaa na njia za mitaa.

Suala la utupaji maski kiholela limeibuka wakati ambapo visa vya maambukizi ya Covid-19 vinaendelea kuongezeka kwa kasi.

Mnamo Alhamisi, Kenya iliandikisha idadi kubwa zaidi ya maambukizi ya corona katika kipindi cha saa 24 zilizopita, baada ya watu 796 kupatikana kuwa na virusi kutoka kwa sampuli 6,754 zilizofanyiwa vipimo, huku wagonjwa watatu wakithibitishwa kufariki.

Barakoa na sanitaiza feki zafurika sokoni

JAMES MURIMI Na BENSON MATHEKA

Huku idadi ya wahudumu wa afya wanaoambukizwa virusi vya corona ikiongezeka, imebainika kuwa serikali imekuwa ikiuziwa vifaa feki vya kujikinga (PPEs).

Shirika la serikali la kupambana na bidhaa feki (ACA) limesema limeanza oparesheni ya kuwasaka wafanyabiashara wanaoagiza, kutengeneza na kuuza vifaa hivyo feki.

ACA ilisema hayo wakati Wizara ya Afya ikitangaza visa vipya 796 vya maambukizi jana , hiyo ikiwa idadi kubwa zaidi kuripotiwa kwa siku moja nchini.

Wizara ya Afya ilisema kuna jumula ya visa 15,601 nchini vya maambukizi ya corona.Kulingana na shirika la ACA, baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiuza sanitaiza na barakoa ambazo ni za ubora wa chini.

Hali hii imetajwa kama mojawapo za sababu zinazolemaza vita dhidi ya virusi vya corona kote nchini huku idadi ya maambukizi ikizidi kupanda.A

fisa Mkuu Mtendaji wa ACA, Elema Halake, jana alisema kikosi cha kupambana na wafanyabiashara wakora kinaendelea kuzunguka kote nchini na kitashirikiana na serikali za kaunti kuwanasa wenye kampuni zinazotengeneza sanitaiza na barakoa feki.

“Hili ni janga la kitaifa na usalama wa kila raia ni muhimu sana. Ili kuhakikisha tunajilinda dhidi ya virusi, lazima tutumie barakoa na sanitaiza zenye ubora wa hali ya juu. Tayari msako wetu umenasa bidhaa katika baadhi ya maeneo nchini,”akasema Bw Halake.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, amekuwa akisema serikali ina uwezo wa kutengeneza vifaa vya kujikinga na virusi vya corona vya ubora wa juu.

Chama cha Madaktari na Wataalamu wa Meno (KMPDU) kimeteta kuwa baadhi ya vifaa vinavyotolewa na serikali ni duni na vinaweka watu katika hatari ya kuambukizwa corona.

Jana, ACA liliandaa kikao na serikali ya Kaunti ya Laikipia pamoja na washikadau wengine kujadili namna ya kufanikisha vita dhidi ya bidhaa haramu.

Mkutano huo ulifanyika mjini Nanyuki.

‘Tutakuwa macho kwenye mipaka yetu, viwanja vya ndege na bandarini ili kuhakikisha sanitaiza na barakoa zisizotimiza viwango vya ubora unaohitajika haziingizwi nchini. Lazima bidhaa zote zinazoingizwa nchini ziwe na cheti cha ubora unaohitajika,’ akaongeza.

Wanaoteremsha maski kwa kidevu washtakiwe, asema gavana

Na SAMMY WAWERU
Ni jambo la kushangaza kuona mtu akiwa na maski na kuining’iniza chini ya kidevu badala ya kuivalia ipasavyo. 
Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga amesema wanaofanya hivyo wanapaswa kukamatwa na kuchukuliwa hatua kisheria, kwa kile anahoji ni kujitia katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona na pia kuambukiza wengine.
Akitumia mfano wa Kaunti ya Nyeri, gavana alisema utepetevu huo unaonyesha wazi wananchi hawajali hatari inayowakodolea macho.
“Katika kaunti ya Nyeri, idadi kubwa ya wakazi ina maski ila wanaining’iniza kwenye kidevu hata wakiwa maeneo ya umma,” Bw Kahiga akasema.
“Nikielekea Embu majuzi, nilishangaa kuona baadhi ya watu Kirinyaga hawavalii maski. Matukio hayo ni taswira ya maeneo mengine nchini,” Gavana akasema.
Alisema licha ya Wizara ya Afya kuhimiza Wakenya haja ya kutilia maanani sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kudhibiti kuenea kwa Covid-19, huenda jitihada hizo zikaambulia patupu endapo wananchi hawatatii.
Huku zuio la kusafiri likiwa limeondolewa, Gavana Kahiga alisema mienendo ya wananchi inachangia kuenea kwa corona kutokana na utepetevu wao.
“Itafika mahali kaunti ya Nyeri tutaamuru maafisa wa polisi kukamata na kushtaki wanaoning’niza maski kwenye kidevu, kwa kuwa wanalemaza vita dhidi ya Covid-19,” alionya.
Tangu zuio la kuingia kaunti ya Nairobi, Mombasa na Mandera kuondolewa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Julai 6, 2020, visa vya maambukizi ya corona vimeongezeka mara dufu.
Rais Kenyatta akisubiriwa kufanya kikao na magavana mnamo Ijumaa, juma hili, inahofiwa huenda serikali ikarejesha amri ya kutoingia na kutotoka nje ya kaunti zilizokuwa zimefungwa awali, kutokana na ongezeko la maambukizi.
Kufikia sasa, Kenya imeandikisha zaidi ya visa 14,000 vya maambukizi ya corona, tangu kisa cha kwanza kiripotiwe nchini mnamo Machi 13, 2020.

AFYA: Barakoa chafu zinavyosambaza corona vijijini

Na LEONARD ONYANGO

VIDEO ya mwanaume aliyeonekana akisafisha barakoa zilizotumika iliwatia hofu Wakenya ilipochipuza katika mitandao ya kijamii miezi mitatu iliyopita.

Katika video hiyo, mwanaume huyo alionekana akisafisha rundo la barakoa zilizotumika kwenye maji machafu yanayoaminika kuchotwa ndani ya Mto Nairobi ambao umegeuka ‘jaa’ la kila aina ya takataka.

Kwa mujibu wa ripoti, mwanaume huyo aliokota barakoa zilizotumika karibu na hospitali ya Mbagathi jijini Nairobi, ambapo wagonjwa wa virusi vya corona wanatibiwa, na kwenda kuzisafisha kabla ya kuziuza tena jijini Nairobi.

Wakenya, haswa katika vitongoji duni jijini Nairobi, sasa wanahofia kuwa huenda baadhi ya barakoa zinazouzwa mitaani zikawafanya kuambukizwa virusi vya corona badala ya kuwakinga.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo katika mitaa ya Mathare, Kibera na Mukuru kwa Njenga jijini Nairobi, ulibaini kuwa takataka ya barakoa zilizotumika zimetapakaa kila mahali.

Barakoa zilizotumika zinatupwa ovyo hivyo kuwaweka wakazi katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona.

Katika, mtaa wa Kibera, barakoa zilizotumika zimetupwa kando ya barabara na ndani ya Mto Nairobi uliosheheni takataka

Lakini Bw Jack Omondi ambaye ni mkazi wa Kibera anasema kuwa wengi wanalazimika kutupa barakoa kiholela kutokana na ukosefu wa vyoo na majaa ya takataka.

Kibera na Mathare ni miongoni mwa maeneo jijini Nairobi yaliyo na idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona.

Wataalamu wa afya na wanaharakati wanahofia kuwa uchafu wa barakoa na glovu zilizotumika unaweza kuchangia katika kusambaa kwa virusi vya corona.

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (UN Environment) tayari limeonya kuwa janga la virusi vya corona litasababisha kuongezeka kwa maelfu ya tani za takataka ambazo ni hatari kwa afya na mazingira.

Shirika hilo linasema kuwa takataka hatari zinajumuisha zinajumuisha barakoa, glovu na vifaa vya matibabu vilivyotumiwa katika kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Ripoti kuhusu Hali ya Uchumi nchini ya 2020 iliyotolewa na Shirika la Takwimu (KNBS) miezi miwili iliyopita inaonyesha kuwa serikali za kaunti tayari zimelemewa na kiasi kikibwa cha takataka zinazozalishwa katika miji mbalimbali nchini.

Jijini Nairobi, kwa mfano, kiasi cha takataka kiliongezeka mwaka jana kutoka tani milioni 2.7 mnamo 2018 hadi tani milioni 2.9.

Serikali ya Kaunti ya Nairobi ilifanikiwa kuzoa asilimia 55.3 ya takataka hizo na kuacha asilimia 45.7 ya uchafu umetapakaa mitaani.

Kati ya tani 320,000 za takataka zilizozalishwa jijini Mombasa mwaka jana ni tani 147,000 tu zilizokusanywa na serikali ya kaunti.

Serikali ya Kaunti ya Kisumu ilifanikiwa kuzoa tani 63,000 tu kati ya tani 210,000 za uchafu uliozalishwa jijini humo.

Kuna hofu kuwa takataka za barakoa zilizotumika huenda zikasababisha ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona nchini huku mitaa ya mabanda ikitarajiwa kuathirika zaidi.

Ripoti ya sensa ya 2019, inaonyesha kuwa mitaa ya mabanda inaongoza kwa kutupa takataka kiholela bila kuzingatia kanuni za usafi.

Asilimia 42.6 ya wakazi wa mtaa wa Kibra, ambao unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona jijini Nairobi, hutupa takataka barabarani, mitaroni au vyanzo vya maji, kulingana na ripoti ya sensa ya 2019.

Asilimia 20.1 na asilimia 15.1 ya wakazi wa mtaa wa Mathare na Starehe mtawalia hutupa takataka zao za nyumbani kiholela katika vyanzo vya maji, mitaro ya kupitisha maji taka na barabarani.

Ripoti ya Sensa inaonyesha kuwa asilimia 7.8 ya familia milioni 1.5 zilizoko jijini Nairobi hutupa takataka za nyumbani ovyo ovyo barabarani na mitaroni. Familia hizo ndizo huchangia kwa kiasi kikubwa katika uchafuzi wa Mto Nairobi.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa takribani familia 20,000 jijini Mombasa zinatupa takataka za nyumbani kiholela.

Nchini Kenya, kulingana na ripoti ya sense ya 2019, kuna jumla ya kaya milioni 12 lakini ni asilimia 6.3 tu ambazo takataka zao huzolewa na serikali za kaunti.

Katibu mkuu wa shirika la kutetea mazingira la United Green Movement, Hamisa Zaja, anasema kuwa utupaji ovyo wa barakoa na mavazi mengineyo ya kukinga virusi vya corona kunaweza kusababisha maradhi hayo kusambaa zaidi, haswa katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu.

Bi Zaja anasema idadi kubwa ya Wakenya hawana ufahamu kuhusu njia salama za kutupa barakoa, glovu au mavazi mengineyo ya kuwakinga dhidi ya kuambukizwa virusi vya corona.

“Wakati huu wa janga la virusi vya corona, idadi kubwa ya Wakenya wanatumia barakoa na glovu kujikinga dhidi ya maambukizi. Lakini baada ya kuzitumia hawajui mahali pa kupeleka takataka hizo,” anasema.

Bi Zaja anaitaka serikali kuimarisha juhudi za kuwaelimisha Wakenya kuhusu njia mwafaka za kutupa uchafu unaotokana na vifaa au mavazi ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

James Wambugu ambaye ni muuzaji wa barakoa mtaani Mukuru kwa Njenga anasema kwamba amekuwa akijaribu kuwaelimisha wateja wake kuhusu njia mwafaka za kutupa barakoa zilizotumika lakini wengi wao wanapuuzilia mbali ushauri wake.

“Serikali inafaa kuhamasisha umma kuhusu jinsi ya kukusanya uchafu wa barakoa ili usije ukaambukiza zaidi virusi vya corona,” anasema.

Tafiti ambazo zimefanywa zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya Wakenya wanaamini kuwa kuvalia barakoa ni njia mojawapo ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Utafiti uliofanywa na KNBS mwezi uliopita ulionyesha kuwa asilimia 79 ya Wakenya wanaamini kuwa wakivalia barakoa wanazuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Utafiti uliofanywa na shirika la TIFA katika mitaa duni jijini Mombasa na Nairobi pia ulionyesha kuwa asilimia 3 ya Wakenya wanaamini kuwa kuvalia glovu kunawakinga dhidi ya virusi vya corona.

Mwongozo

Katibu wa Wizara ya Mazingira na Misitu Chris Kiptoo anasema kuwa wananchi wanafaa kufuata mwongozo wa Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira (Nema) kuhusu njia mwafaka za kutupa barakoa au vifaa vya kujikinga na virusi vya corona.

Dkt Kiptoo anasema kuwa utupaji kiholela barakoa au vifaa vinginevyo vya kimatibabu ni hatari kwa mazingira na afya ya binadamu.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe mnamo Aprili alikiri kuwa kuna changamoto ya utupaji takataka kuhusu utupaji wa vifaa ya kujikinga na virusi vya corona kama vile barakoa na glovu.

Bw Kagwe, hata hivyo, alisema kuwa serikali imeandaa mwongozo kuhusu njia salama za kutupa takataka hizo bila kuhatarisha mazingira na afya ya watu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Nema Mamo Mamo anasema kuwa uchafu wa barakoa na glovu ni miongoni mwa takataka zilizowekwa kwenye kundi la ‘uchafu hatari wa hospitalini’.

“Asilimia 85 ya takataka zinazotokana na vifaa vya kimatibabu huwa hazina madhara. Lakini asilimia 15 ni hatari kwa afya kwani zinaweza kuwa na virusi, bakteria, sumu na hata zinaweza kulipuka,”anasema Bw Mamo.

“Baadhi ya vifaa vya kujikinga na virusi vya corona kama vile barakoa na glovu hutumika mara moja na kisha kutupwa. Hali hiyo imesababisha ongezeko la takataka nchini. Iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa basi huenda kukawa na maambukizi zaidi ya virusi vya corona na uchafuzi wa mazingira,” anaongezea.

Anasema kuwa barakoa, glovu na vifaa vinginevyo vya kujikinga na virusi vya corona vinajumuishwa katika kundi la takataka za hospitalini hivyo unafaa kutupwa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya 1999.

Kulingana na mwongozo wa Nema; barakoa, glovu, chupa za sabuni na dawa ya kuua viini (sanitaiza) hazifai kuchanganywa na takataka nyingine nyumbani.

“Virusi vya corona vinaishi kwa siku nyingi juu ya vitu kama vile barakoa au glovu hivyo unapotupa takataka ndani ya nyumba au njiani, sokoni, nje ya dirisha la matatu, nakadhalika, unahatarisha maisha yaw engine,” anasema Bw Mamo.

Mkurugenzi wa Nema, hata hivyo, anakiri kuwa idadi kubwa ya Wakenya hawana mazoea ya kutenganisha takataka na wamekuwa wakitupa kiholela.

“Kuchanganya barakoa na takataka nyinginezo za nyumbani kunatia hatarini watu ambao huokota chupa na vitu vingine katika majaa,” anasema.

Mwongozo wa Nema unahitaji wamiliki wa nyumba za kupanga kuweka jaa, linalofunguliwa kwa miguu kuwezesha wapangaji kutupa hapo takataka hatari kama kama vile barakoa zilizotumia.

Matatu na afisi pia zinafaa kuwa na majaa hayo spesheli ya kutupa takataka zinazoweza kusababisha maambukizi ya maradhi, kwa mujibu wa mwongozo wa Nema.

Katika maeneo ya vijijini, mwongozo wa Nema unahitaji serikali za kaunti kusambaza majaa ya kukusanya takataka zinazoweza kusababish maambukizi katika afisi za machifu, sokoni au eneo lolote linaloweza kufikiwa na watu wengi.

Bw Mamo anasema kuwa nyumbani, haswa katika maeneo ya vijijini, takataka zilizo na barakoa zinafaa kunyunyuziwa kemikali ya Sodium hypochlorite na kisha kutumbukizwa kwenye shimo la choo.

Ripoti ya Sensa inaonyesha kuwa asilimia 3.6 ya familia, ambazo ni sawa na familia 434,000, kote nchini hutupa takataka ndani ya shimo la choo.

Marufuku

Serikali mnamo Aprili ilipiga marufuku watu kuabiri magari ya umma, kwenda madukani, sokoni au kuabiri bodaboda bila kuvalia barakoa.

Mtu anayepatikana na hatia ya kuvunja sheria hiyo anatozwa faini ya Sh20,000 au kifungo cha miezi sita gerezani.

Barakoa zimejizolea umaarufu kutoka na ukweli kwamba zimesaidia kupunguza maambukizi ya virusi vya corona kote duniani.

Shirika la WHO linasema kuwa watu wanapozungumza, kukohoa, kuchemua au kucheka wanatoa mate ambayo yanaweza kuwa na virusi vya corona ambavyo husalia hewani kwa muda mrefu.

Shirika la WHO linapendekeza kuwa watu wasio na barakoa watumie katarasi shashi au kitambaa wanachoweza kutupa mara baada ya kukohoa au kuchemua.

Watu ambao hawajavalia barakoa wanapoenda katika eneo lililo na virusi vya corona hewani wanaambukizwa bila hata baada ya waathiriwa kuondoka.

Hiyo ndiyo maana serikali sasa inataka kila mtu anayeenda nje ya nyumba yake kuvalia maski ili kujikinga.

Tafiti zilizofanywa zinaonyesha kuwa ni vigumu kuambukizwa virusi vya corona iwapo utatangamana na mwathiriwa ikiwa wote mmevalia barakoa.

Wazee wavalie barakoa aina ya N95, WHO yashauri

CHARLES WASONGA na SAMMY WAWERU

SHIRIKA la Afya Ulimwenguni (WHO) limependekeza kuwa wazee wenye umri wa miaka 60 kwenda juu na watu wenye magonjwa sugu wawe wakivalia barakoa aina ya N95 nyakati zote maeneo ya umma.

Hii, shirika hilo linasema, ni kutoka na hali kwamba watu hawa wana kinga ya chini miilini mwao kutokana na uzee au kutokana na magonjwa hayo.

Kwenye kikao na wanahabari Jumatatu, Waziri Msaidizi wa Afya Dkt Rashid Aman alisema kuwa wale wanaowatunza wagonjwa wa Covid-19 chini ya mpango wa kuwatunza nyumbani pia wanahitaji kuvalia maski aina ya N95 wanapowahudumia watu hao.

“Maski aina ya N95 ina kinga zaidi kwa sababu ya namna ilivyotenzwa. Hii ndio maana hutumiwa katika hali ambapo kinga inahitajika; kama wakati ambapo wahudumu wa afya wanawatunza wagonjwa hospitalini. Wagonjwa wanaohudumiwa pia wanapaswa kutumia maski hizi,” akasema Dkt Aman.

Aliongeza kuwa raia wa kawaida wanapaswa kuendelea kuvalia maski zilizotengenezwa kwa njia ya kawaida nyakati zote ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Hata hivyo, Dkt Aman alisisitiza kuwa wazee wenye umri wa miaka 60 kwenda juu wanapaswa kujaribu wawezavyo kukaa nyumbani.

Mnamo Ijumaa WHO iliyataka mataifa ya ulimwengu kuhimiwa raia kuvalia maski katika maeneo ambako kuna uwezekano mkubwa wa virusi vya corona kusambaa.

“Na wahudumu wa afya na wale wanaowatunza wagonjwa wanapaswa kuvalia maski ya kimatibabu nyakati zote wakiwa kazini,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus kwenye kikao na wanahabari jijini Geneva, Uswisi.

“Pili, katika maeneo ambako virusi vya corona vinasambaa katika jamii, tunawashauri watu wenye umri wa miaka 60 kwenda juu au wenye magonjwa sugu, kuvalia maski katika mazingira ambapo hawawezi kutengana na wenzao kwa urahisi,” Tedros akasema.

“Na tatu WHO inahimiza serikali mataifa yahimize umma kuvalia maski nyakati zote katika maeneo ambako ni vigumu kwa watu kutotengana kama vile ndani ya magari ya uchukuzi wa umma, madukani miongoni mwa maeneo mengine,” akaongeza.

Wagonjwa wasioonyesha dalili

Haya yanajiri huku Wizara ya Afya nchini Kenya ikikiri kuwa vituo vya afya vimejaa wagonjwa.

Ongezeko hilo pia limechangia wahudumu wa afya kuzidiwa na kazi.

“Vituo vya afya vimelemewa, vifaa na wahudumu wa afya ni haba ikilinganishwa na idadi kuu ya wagonjwa,” Dkt Aman akasema.

Awali, Wizara ya Afya ilikuwa imedokeza kwamba kutokana na vituo vya afya kuashiria kujaa wagonjwa, itaruhusu baadhi yao kuondoka ili kuchungiwa nyumbani.

Huku pendekezo hilo likizua mdahalo, jinsi wagonjwa wa virusi hatari vya corona watachungiwa nyumbani ikizingatiwa kuwa wengi wao wanapatia changamoto za unyanyapaa, Dkt Aman amesema wanaolengwa ni waliopimwa na kuthibitishwa kuugua ila hawaonyeshi dalili zozote.

Dalili za homa ya corona ni kiwango cha joto cha mwathiriwa mwilini kupanda kuliko cha kawaida, maumivu ya kichwa, kikohozi kizito, matatizo ya kupumua, miongoni mwa zingine, Dkt Aman akieleza kwamba wanaonyesha dalili hizo watalazwa hospitalini.

“Wasioonyesha dalili ndio tunalenga wachungiwe nyumbani,” waziri akasema, akieleza kwamba mikakati maalum itawekwa kufanikisha shughuli hiyo.

Mnamo Jumamosi katika hotuba yake kwa taifa, Rais Uhuru Kenyatta alisema wiki hii atakutana na magavana wote 47 ili kujadili mikakati itakayowekwa na kila kaunti kudhibiti msambao wa Covid-19.

Aidha, Rais alisema kila kaunti inapaswa kuwa na uwezo wa kulaza zaidi ya wagonjwa 300 ili uchumi ufunguliwe kikamilifu.

SHINA LA UHAI: Corona si hatari tu kwa afya bali pia mazingira

Na LEONARD ONYANGO

VIDEO ya mwanaume aliyeonekana akisafisha barakoa/maski zilizotumika iliwatia hofu Wakenya ilipochipuza katika mitandao ya kijamii miezi miwili iliyopita.

Katika video hiyo, mwanaume huyo alionekana akifua rundo la barakoa zilizotumika kwenye maji machafu yanayoaminika kuchotwa ndani ya Mto Nairobi.

Kwa mujibu wa ripoti, mwanaume huyo aliokota barakoa zilizotumika karibu na hospitali ya Mbagathi, jijini Nairobi ambapo wagonjwa wa virusi vya corona wanatibiwa, na kwenda kuzisafisha kabla ya kuziuza tena.

“Niliona mtu akisafisha barakoa alizookota katika eneo la Gikomba na kisha kuziuza tena,” akasema mtumiaji wa mitandao ya kijamii, Lilian Wambui.

Wakenya sasa wanahofia kuwa huenda baadhi ya barakoa zinazouzwa mitaani zikawafanya kuambukizwa virusi vya corona badala ya kuwakinga.

Uchunguzi uliofanywa na Jarida la Afya Jamii katika mitaa mbalimbali ya Nairobi ulibaini kuwa takataka ya barakoa zilizotumika imetapakaa kila mahali.

Wataalamu wa afya na wanaharakati wanasema kuwa uchafu huo wa barakoa na glovu zilizotumika huenda ukasababisha virusi vya corona kusambaa zaidi.

Shirika la la Umoja wa Kimataifa kuhusu Mazingira (UNEP) limeonya kuwa janga la corona litasababisha kuongezeka kwa maelfu ya tani za takataka ambayo ni hatari kwa afya na mazingira.

Shirika hilo linasema kuwa takataka hizo zinajumuisha barakoa, glovu na vifaa vya matibabu vilivyotumiwa katika kuzuia maambukizi ya virusi hivi.

Ripoti kuhusu Hali ya Uchumi nchini ya 2020 iliyotolewa na Shirika la Takwimu (KNBS) miezi miwili iliyopita inaonyesha kuwa serikali za kaunti tayari zimelemewa na kiasi kikubwa cha takataka zinazozalishwa katika miji mbalimbali nchini.

Jijini Nairobi, kwa mfano, kiasi cha takataka kiliongezeka mwaka 2019 kutoka tani milioni 2.7 mnamo 2018 hadi tani milioni 2.9.

Serikali ya Kaunti ya Nairobi ilifanikiwa kuzoa asilimia 55.3 ya takataka hizo na kuacha asilimia 45.7 ya uchafu umetapakaa mitaani.

Kati ya tani 320,000 za takataka zilizozalishwa jijini Mombasa mwaka jana, ni tani 147,000 tu zilizokusanywa na serikali ya kaunti.

Serikali ya Kaunti ya Kisumu ilifanikiwa kuzoa tani 63,000 tu kati ya tani 210,000 za uchafu uliozalishwa jijini humo.

Wataalamu wanasema kuwa janga hili litasababisha serikali za kaunti kulemewa zaidi hivyo kuwatia wakazi katika hatari ya kupatwa na Covid-19 kutoka kwa barakoa, glovu na vifaa vinginevyo vilivyotumika.

Kuna hofu kuwa uchafu wa barakoa na glovu zilizotumika huenda ukasababisha ongezeko la maambukizi huku mitaa ya mabanda ikitarajiwa kuathirika zaidi.

Ripoti ya sensa ya 2019, inaonyesha kuwa mitaa ya mabanda inaongoza kwa kutupa takataka kiholela bila kuzingatia kanuni za usafi.

Asilimia 42.6 ya wakazi wa mtaa wa Kibra, ambao unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya maambukizi ya corona jijini Nairobi, hutupa takataka barabarani, mitaroni au vyanzo vya maji.

Asilimia 20.1 na asilimia 15.1 ya wakazi wa mtaa wa Mathare na Starehe mtawalia, hutupa takataka zao za nyumbani kiholela katika vyanzo vya maji, mitaro ya kupitisha maji taka na barabarani.

Mathare ni miongoni mwa mitaa iliyo na idadi kubwa ya waathiriwa wa corona jijini Nairobi.

Aidha ripoti hiyo inaonyesha kuwa asilimia 7.8 ya familia milioni 1.5 zilizoko jijini Nairobi, hutupa takataka za nyumbani ovyoovyo barabarani na mitaroni. Familia hizo ndizo huchangia kwa kiasi kikubwa katika uchafuzi wa Mto Nairobi.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa takribani familia 20,000 jijini Mombasa zinatupa takataka za nyumbani kiholela.

Nchini Kenya, kuna jumla ya kaya milioni 12 lakini ni asilimia 6.3 tu ambazo takataka zao huzolewa na serikali za kaunti.

Katibu mkuu wa shirika la kutetea mazingira la United Green Movement, Hamisa Zaja, anasema kuwa utupaji ovyo wa barakoa na mavazi mengineyo ya kukinga virusi vya corona kunaweza kusababisha maradhi hayo kusambaa zaidi, haswa katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu.

Bi Zaja anasema idadi kubwa ya Wakenya hawana ufahamu kuhusu njia salama za kutupa barakoa, glovu au mavazi mengineyo ya kuwakinga dhidi ya kuambukizwa corona.

“Wakati huu wa janga la virusi vya corona, idadi kubwa ya Wakenya wanatumia barakoa na glovu kujikinga dhidi ya maambukizi. Lakini baada ya kuzitumia hawajui mahali pa kupeleka takataka hizo,” anasema.

Bi Zaja anaitaka serikali kuimarisha juhudi za kuwaelimisha Wakenya kuhusu njia mwafaka za kutupa uchafu unaotokana na vifaa au mavazi ya kuzuia maambukizi.

James Wambugu ambaye ni muuzaji wa barakoa jijini Nairobi, anasema kwamba amekuwa akijaribu kuwaelimisha wateja wake kuhusu njia mwafaka za kutupa zilizotumika lakini wengi wao wanapuuzilia mbali ushauri wake.

“Serikali inafaa kuhamasisha umma kuhusu jinsi ya kukusanya uchafu wa barakoa ili usije ukasambaza zaidi corona,” anasema.

Tafiti ambazo zimefanywa zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya Wakenya wanaamini kuwa kuvalia barakoa ni njia mojawapo ya kuzuia maambukizi.

Utafiti uliofanywa na KNBS mwezi uliopita ulionyesha kuwa asilimia 79 ya Wakenya wanaamini kuwa wakivalia barakoa wanazuia kusambaa kwa virusi hivi.

Utafiti uliofanywa na shirika la TIFA jijini Mombasa na Nairobi pia ulionyesha kuwa asilimia 3 ya Wakenya wanaamini kuwa kuvalia glovu kunawakinga dhidi ya corona.

Mwongozo wa Nema kuhusu utupaji taka

Katibu wa Wizara ya Mazingira na Misitu Chris Kiptoo anasema kuwa wananchi wanafaa kufuata mwongozo wa Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira (Nema) kuhusu njia mwafaka za kutupa barakoa au vifaa vya kujikinga na virusi vya corona.

Dkt Kiptoo anasema kuwa utupaji kiholela barakoa au vifaa vinginevyo vya kimatibabu ni hatari kwa mazingira na afya ya binadamu.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, mnamo Aprili alikiri kuwa kuna changamoto ya utupaji takataka ya vifaa ya kujikinga na virusi vya corona kama vile barakoa na glavu.

Bw Kagwe, hata hivyo, alisema kuwa serikali imeandaa mwongozo kuhusu njia salama za kutupa takataka hizo bila kuhatarisha mazingira na afya ya watu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Nema Mamo Boru Mamo, anasema kuwa barakoa na glovu ni miongoni mwa vitu vilivyowekwa kwenye kundi la takataka hatari zinazoweza kusababisha maradhi.

“Asilimia 85 ya takataka zinazotokana na vifaa vya kimatibabu huwa hazina madhara. Lakini asilimia 15 ni hatari kwa afya kwani zinaweza kuwa na virusi, bakteria, sumu na hata zinaweza kulipuka,” anasema Bw Mamo.

“Baadhi ya vifaa vya kujikinga na virusi vya corona kama vile barakoa na glovu hutumika mara moja na kisha kutupwa. Hali hiyo imesababisha ongezeko la takataka nchini. Iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa, basi huenda kukawa na maambukizi zaidi ya virusi vya corona na uchafuzi wa mazingira,”anaongezea.

Anasema kuwa barakoa, glovu na vifaa vinginevyo vya kujikinga na corona vinajumuishwa katika kundi la takataka za hospitalini hivyo vinafaa kutupwa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya 1999.

Kulingana na mwongozo wa Nema; barakoa, glovu, chupa za sabuni na dawa ya kuua viini (sanitaiza) hazifai kuchanganywa na takataka nyingine nyumbani.

“Virusi vya corona vinaishi kwa siku nyingi juu ya vitu kama vile barakoa au glovu hivyo unapotupa takataka ndani ya nyumba au njiani, sokoni, nje ya dirisha la matatu, na kadhalika, unahatarisha maisha ya wengine,” anasema Bw Mamo.

Hata hivyo, anakiri kuwa idadi kubwa ya Wakenya hawana mazoea ya kutenganisha takataka na wamekuwa wakitupa kiholela.

“Kuchanganya barakoa na takataka nyinginezo za nyumbani kunatia hatarini watu ambao huokota chupa na vitu vingine katika majaa,” anasema.

Mwongozo wa Nema unahitaji wamiliki wa nyumba za kupanga kuweka jaa, linalofunguliwa kwa miguu kuwezesha wapangaji kutupa hapo takataka hatari kama kama vile barakoa zilizotumia.

Matatu na afisi pia zinafaa kuwa na majaa hayo spesheli ya kutupa takataka zinazoweza kusababisha maambukizi ya maradhi.

Katika maeneo ya vijijini, Nema inahitaji serikali za kaunti kusambaza majaa ya kukusanya takataka zinazoweza kusababisha maambukizi katika afisi za machifu, sokoni au eneo lolote linaloweza kufikiwa na watu wengi.

Bw Mamo anasema kuwa nyumbani, haswa katika maeneo ya vijijini, takataka zilizo na barakoa zinafaa kunyunyuziwa kemikali ya Sodium hypochlorite na kisha kutumbukizwa kwenye shimo la choo.

Ripoti ya Sensa 2019 inaonyesha kuwa asilimia 3.6 ya familia, ambazo ni sawa na familia 434,000, kote nchini hutupa takataka ndani ya shimo la choo.

Marufuku ya serikali

Serikali mnamo Aprili ilipiga marufuku watu kuabiri magari ya umma, kwenda madukani, sokoni au kuabiri bodaboda bila kuvalia barakoa.

Mtu anayepatikana na hatia ya kuvunja sheria hiyo anatozwa faini ya Sh20,000 au kifungo cha miezi sita gerezani.

Barakoa zimejizolea umaarufu kutokana na ukweli kwamba zimesaidia kupunguza maambukizi ya virusi vya corona kote duniani.

Shirika la WHO linasema kuwa watu wanapozungumza, kukohoa, kuchemua au kucheka wanatoa mate ambayo yanaweza kuwa na virusi vya corona ambavyo husalia hewani kwa muda mrefu.

Shirika la WHO linapendekeza kuwa watu wasio na barakoa watumie katarasi shashi au kitambaa wanachoweza kutupa mara baada ya kukohoa au kuchemua.

Watu ambao hawajavalia barakoa wanapoenda katika eneo lililo na virusi vya corona hewani, wanaambukizwa hata baada ya waathiriwa kuondoka.

Hiyo ndiyo maana serikali sasa inataka kila mtu anayeenda nje ya nyumba yake kuvalia ili kujikinga.

Tafiti zilizofanywa zinaonyesha kuwa ni vigumu kuambukizwa corona iwapo utatangamana na mwathiriwa ikiwa nyote mmevalia barakoa.

Walimu wakuu wawapa wanafunzi barakoa

NA WAWERU WAIRIMU

Walimu wakuu wa shule za upili katika Kaunti ya Isiolo wameanza kuwasambazia barakoa wanafunzi nyumbani kufuatia hatari inayowakodolea macho watoto hao ya kupatwa na ugonjwa wa corona kwa sababu wao hucheza kwa makundi nyumbani.

Walimu hao tayari wamewapa watoto zaidi ya 300 katika wadi ya Ngaremara barakoa na kuwaelimisha familia kuhusiana na jinsi ya kujikinga dhidi ya virusi vya corona.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wakuu wa Shule za Upili tawi la Isiolo Abdi Diba alisema kwamba ni jambo la kusitikisha kuona watu wazima wakikijinga kutokana na corona huku wakiwaachilia watoto wao bila barakoa hali inayowaweka kwenye hatari ya kuambukizwa corona.

“Tunataka kuhakikisha kwamba wanafunzi wote walio nyumbani wamekingwa kutokana na virusi hivyo,” alisema Bw Diba. Walimu walilalamika kwamba familia nyingi hazina redio na hilo linalemaza masomo ya wanafunzi.

“Tuliwakuta wnafunzi 20 wakiwa wamekutana kwa familia moja kusikiliza redio, tunatafuta njia ya kuwasaidia wakati huu wako nyumbani,” alisema mkuu wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Isiolo.

Bw Diba aliwaomba wazazi kuhakikisha wamewatunza watoto wao vizuri wakati huu wa corona na kuhakikisha hawataingizwa kwenye utumiaji wa dawa za kulevya.

Wasio na uwezo kusikia kutumia maski spesheli kusoma midomo ya wazungumzaji

Na MISHI GONGO

WALEMAVU wasio na uwezo wa kusikia katika Kaunti ya Mombasa wamepokea maski spesheli kutoka kwa Muungano wa Watu Wanaoishi na Ulemavu Pwani.

Maski hizo zimeundwa kwa vitambaa maalum, lakini vyenye sehemu za kuonyesha midomo ya wazungumzaji kinyume na maski zingine zinazotumika kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Aidha, wamepewa chakula kitakachowafaa pakubwa wakati huu ambapo wakazi wanapitia wakati mgumu kutokana na athari hasi za kiuchumi kufuatia janga la Covid-19.

Bi Hamisa Zaja (kulia) na wanachama wengine wakitoa chakula kiwafae walioathirika vibaya sana kiuchumi na janga la Covid-19 Kaunti ya Mombasa Mei 21, 2020. Picha/ Mishi Gongo

Akizungumza Alhamisi katika hafla iliyofanyika Tudor, muuguzi katika hospitali kuu ya eneo la Pwani Bi Fatma Ngoto ambaye pia anashughulikia lugha ya ishara katika hospitali hiyo, aliwafuwandisha jinsi ya kutumia maski hizo na kudumisha usafi.

“Maski hizi zitawawezesha kuzungumza kati na baina yenu kwa urahisi,” akasema.

Muuguzi huyo alisema kukosa uhamasisho na mafunzo ya kutosha ni changamoto kuu katika vita dhidi ya virusi vya corona.

Afisa mkuu katika muungano huo Bi Hamisa Zaja aliilaumu serikali kwa kuwaacha nyuma katika vita dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.

“Serikali inapaswa kujumuisha watu wanaoishi na ulemavu katika vita hivi. Katika ugavi wa chakula na maski, watu wanaoishi na ulemavu wanafaa kuwekwa katika mstari wa mbele,” akasema.

Bi Hamisa Zaja (kulia) na Bi Fatma Ngoto (kati nyuma) wakipeana maski spesheli kwa wakazi wa Kaunti ya Mombasa. Picha/ Mishi Gongo

Aidha Bi Zaja aliiomba serikali kuleta maski maalum.

Alisema maski zilizoko sokoni kwa sasa haziwafai watu wanaoishi na ulemavu; hasa wasio na uwezo wa kusikia.

“Ni vigumu kutumia lugha ya ishara bila kuona midomo na maski zilizoko sokoni kwa sasa zinaficha midomo hivyo kuwanyima wasio na uwezo wa kusikia fursa ya kuzungumza,” akasema.

Wanafunzi wa vyuo vya ufundi Garissa waanzisha mradi wa utengenezaji barakoa

Na FARHIYA HUSSEIN

WANAFUNZI katika vyuo vya ufundi Kaunti ya Garissa wameanzisha mpango wa utengenezaji barakoa kusaidia katika mapambano dhidi ya janga la Covid 19.

Wanafunzi hao kufikia sasa wametengeneza barakoa zaidi ya 50,000 katika kipindi cha wiki mbili.

Afisa Mkuu wa elimu katika kaunti hiyo, Bw Mohammed Gure amethibitisha.

“Utenegenezaji wa barakoa hizi unafanyika katika chuo cha ufundi cha Garissa. Lengo kuu ni kusambaza barakoa katika maeneo yanayokubwa na uhaba kwenye kaunti hii,” Bw Gure akasema.

Amesisitiza kwamba wakipata mashine za kutengezea vifaa hivyo na msaada unaofaa wanaweza kutengeneza barakoa zaidi ya 100,000 kwa mwezi mmoja.

“Shughuli hiyo inaendelezwa na kikosi kutoka vyuo vya mafunzo ya kiufundi vya Bura, Mkono na Garissa. Tayari tumefanikiwa kutengeneza na kusambaza barakoa 50,000. Hii itasaidia sana katika kupambana na ugonjwa wa Covid-19,” afisa mkuu huyo alisema.

Watakaofaidi zaidi ni waathiriwa wa mafuriko katika kambi za IDP, hospitali, magereza na sehemu nyinginezo za kijamii ambazo zinakisiwa kuwa dhaifu.

“Tumekuwa katika kituo hicho na tumevutiwa sana. Tunashukuru juhudi kutoka kwa timu hiyo. Tunawaunga mkono na tutawapa msaada kutoka upande wetu,” Bw Gure akaahidi.

Timu hiyo iliongozwa na wakuu wa vyuo hivyo vya elimu ya kiufundi akiwemo Bw Ahmed Hassan wa chuo cha mafunzo ya kiufundi, Bi Amina Hassan kutoka Chuo cha Biashara, Ufundi na Kazi za Mikono na Bw Osman Abdi Ali wa Chuo cha Ufundi cha Bura.

Bw Gure pamoja na Mkurugenzi wa mafunzo ya ufundi Bw Hassan Yarrow na Mkurugenzi Msaidizi Mohamed Noor wamehakikishiwa kuwa vifaa vilivyotumika vilikuwa vya ufanisi na vya kisasa kulingana na mahitaji ya Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (Kebs).

“Waathiriwa wa mafuriko ambao wanaishi katika kituo cha mafunzo ya ufundi tayari wamepokea barakoa hizo za bure zanazotengenzwa katika kituo hicho,” alisema Gure.

Wakati huo huo, timu ya wataalamu wa mabomba na ile ya ujenzi kutoka kwa vyuo hivyo vya ufundi wamevumbua kifaa cha kunawa mikono (hand sanitizer dispenser).

Polisi wampiga risasi babake seneta wa Lamu kwa kutovaa barakoa

JUMA NAMLOLA na KALUME KAZUNGU

POLISI katika Kaunti ya Laikipia wanalaumiwa kwa kumpiga risasi babake Seneta wa Kaunti ya Lamu, Anwar Loititip kwa madai hakuwa amevaa barakoa.

Kwenye kisa hicho cha Jumapili, maafisa wa polisi wa Doldol walimpiga risasi mguuni mzee David Kiwaka, walipokuwa wakijaribu kumkamata kwa nguvu, kwa madai alihatarisha maisha yake kwa kutojikinga na corona.

Bw Loitiptip alikashifu polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi, katika harakati za kuhakikisha masharti ya Wizara ya Afya yanazingatiwa.

“Babangu David Kiwaka amepigwa risasi mguuni na kujeruhiwa vibaya na polisi wa kituo cha Doldol. Walikuwa wakijaribu kumkamata kwa nguvu kwa madai kwamba hakuwa amevaa barakoa. Tumempeleka babangu hospitalini Nanyuki anakoendelea kutibiwa,” akasema.

Seneta huyo anataka uchunguzi wa haraka ili afisa wa polisi aliyehusika na unyama huo akamatwe na kushtakiwa.

Tukio hili lilijiri siku moja baada ya mfanyabiashara mjini Nyeri kulazimishwa atoe hongo, alipofumaniwa na polisi akila bila kuvaa barakoa.

Wiki jana, nyanya mwenye umri wa miaka 93 katika kaunti ya Nyamira alilazimika kuuza kuku wake na kupata pesa za kuwahonga polisi. Ajuza huyo alipatikana na maafisa hao akiwa hana barakoa.

Juhudi hizo za polisi ziliendelea huku jana watu wengine 25 wakiripotiwa kuambukizwa virusi vya corona.

Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Rashid Aman alisema wanaume 23 na wanawake wawili katika kaunti nane walitambuliwa kutoka kwa watu 1,139 waliopimwa.

“Visa hivi 25 vinafikisha idadi ya maambukizi kuwa 912. Kwa jumla tumepima watu 44,851 kufikia sasa,” akasema.

Dkt Aman alitangaza kuwa kaunti tatu – Garissa, Taita Taveta na Meru – ziliripoti kwa mara ya kwanza, jumla visa vitano.

Garissa na Taita Taveta zilikuwa na visa viwili kila moja huku Meru ikiwa na kimoja.

Kajiado ilikuwa na visa sita, Mombasa (5), Nairobi (3), Kiambu (3) na Kwale (3).

Serikali pia ilitangaza kuwa madereva 53 wa matrela kutoka nchi jirani ya Tanzania walipimwa na kupatikana na virusi hivyo wakiwa mpakani. Ingawa serikali ilifunga mpaka wake wana Tanzania na Somalia, wadereva wa kusafirisha mizigo bado wanaruhusiwa kuvuka, kwa sharti wawe wamepimwa na kuwa hawajaambukizwa.

Vyuo vya kiufundi Kiambu kuendelea kushona barakoa

Na LAWRENCE ONGARO

VYUO vya kiufundi katika Kaunti ya Kiambu vitaendelea kushona barakoa kwa wingi ili kutosheleza mahitaji ya wananchi.

Mnamo Jumatatu, Gavana wa Kiambu Dkr James Nyoro alizuru chuo cha Kamirithu mjini Limuru na kujionea jinsi barakoa zinavyoshonwa.

Alisema vyuo vichache vilivyoko katika kaunti hiyo vitalazimika kushona barakoa 50,000 kila wiki ili ziweze kusambazwa kwa wananchi katika kaunti hiyo.

“Ni muhimu tujitegemee kwa kushona barakoa na kusambaza kwa wananchi kwa lengo la kukabiliana na homa ya corona,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema hatua hiyo pia itasaidia kwa njia moja au nyingine kuajiri vijana wengi.

Gavana wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro alipozuru chuo cha kiufundi cha Kamirithu mjini Limuru Mei 11, 2020. Picha/ Lawrence Ongaro

Aliahidi kaunti hiyo itahakikisha kila mwananchi anapata barakoa kwa lengo la kujikinga na dhidi ya corona.

Alisema atawasiliana na benki kadha ili kutoka mikopo kwa wafanyabiashara wa chini kwa lengo la kuwainua kiuchumi.

Alisema ni vyema kuwainua vijana ili kupunguza shida ya ajira inayoshuhudiwa nchini kote.

Alisema kaunti ya Kiambu imeweka mikakati ili kukabiliana na coronavirus.

Tayari dawa imepulizwa katika maeneo muhimu kama maokoni, katika vituo vya magari, vituo vya polisi na makazi ya watu.

“Tunataka kuona ya kwamba tunakabiliana na janga hili ili watu waweze kurejelea shughuli zao za kawaida,” alisema Dkt Nyoro.

Baada barakoa hizo kushonwa watu watakaonufaika pakubwa ni raia kwa jumla, waendeshaji bodaboda, waendeshaji tuktuk, na wahudumu katika sekta ya matatu.

“Tunataka kuhakikisha kuwa tunapambana na janga hili tukiwa pamoja. Kila mmoja ni lazima ajihusishe kwa mtihani huo,” alisema.

Wakati wa ziara hiyo ya Limuru, gavana huyo aliandamana na naibu wake Bi Joyce Ngugi, Waziri wa Elimu katika kaunti Bi Mary Kamau, Askofu David Kariuki Ngari, kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti ya Kiambu Bw Gedion Gachara, na diwani wa Limuru ya Kati Bw Joseph Kahenya.

Alisema ataendelea kuzuru maeneo mengine ili kujionea mwenyewe kile kinachoendelea huko.

Wasiovalia barakoa wamulikwa na maafisa baadhi ya maeneo Nairobi

Na SAMMY WAWERU

MAAFISA wa polisi katika baadhi ya mitaa Nairobi walionekana ‘kuwamulika’ wakazi walioonekana bila barakoa.

Kisa cha kwanza cha maambukizi ya Covid-19 kiliporitiwa nchini Machi 2020, serikali ilitoa taratibu na maagizo jinsi ya kudhibiti maradhi hayo yasienee.

Uvaliaji barakoa hasa katika maeneo ya umma, ni mojawapo ya taratibu zilizoorodheshwa kuzuia maambukizi ya Covid-19, ugonjwa unaosababishwa na virusi hatari vya corona.

Mnamo Jumamosi, operesheni hiyo ya maafisa ilikuwa katika mtaa wa Kasarani, Roysambu na Zimmerman.

Maafisa wa polisi walionekana katika maeneo hayo mchana ambapo waliopatikana bila barakoa wakijipata pabaya.

“Tutachukulia hatua wasiojali hatari ya Covid-19 kwa kutovalia maski,” afisa mmoja akaambia umma eneo la Zimmerman.

Aidha, waliingia kwenye saluni, maduka, vinyozi na mikahawa kuona ikiwa utaratibu wa serikali ulikuwa unazingatiwa.

Walikuwa na gari lao kuwarahisishia usafiri wakiwa kazini.

Operesheni hiyo ililenga hasa kusambaratisha mikusanyiko ya watu.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi walilamika wakisema wanaitishwa hongo katika shughuli hiyo kwa wanaopatikana bila barakoa.

“Ni pesa tu wanakusanya na kuhangaisha raia,” akalalamika mkazi.

Wizara ya Afya imeripoti visa kadhaa vya maambukizi ya corona katika mtaa wa Kasarani, maafisa wa polisi wakitakiwa kuhakikisha wenyeji wanafuata taratibu na sheria zilizotolewa kuzuia usambaaji zaidi.

Kizimbani kwa kuiba maski za Sh950,000

Na Richard Munguti

Wafanyabiashara wawili walishtakiwa Ijumaa kwa kumlaghai mfanyabiashara maski zipatao 252 zenye thamani ya Sh957,600.

Mabwana Charles Nyamai Nzivani (kulia pichani) na Benson Mutuku Nzioki walikanusha mashtaka mawili ya kula njama ya kumtapeli Erick Mwiti Gitiye barakoa hizo.

Washtakiwa pia walikabiliwa na shtaka la pili la kupokea bidhaa wakidai walikuwa na uwezo wa kuzinunua.

Walikana walipokea maski hizo za hali ya juu mnamo Aprili 22 2020 jijini Nairobi. Waliomba waachiliwe kwa dhamana.

Hakimu mkazi Daniel Ndungi aliwaachilia kwa dhamana ya Sh300,000 kila mmoja.

Washtakiwa hao waliomba wapinguziwe dhamana hiyo wakisema “ni ya juu na kamwe hawawezi kuipata dhamana hiyo.”

Washtakiwa hao waliomba wapunguziwe dhamama wakidai “mapato yao ni kidogo.”

Akitoa uamuzi Bw Ndungi alisema “dhamana hiyo inalingana na makosa dhidi yao.”

Aliongeza kusema baroko hizo zilikuwa zapelekwa kupewa wataalam wa matibabu wanaopambana kuangamiza gonjwa la Corona.

“Yadaiwa mlimfuja mlalamishi maski ambazo zatumika kuzuia kuenezwa kwa gonjwa la Corona ambalo limekuwa janga,” Bw Ndungi alisema.

Alikataa kuwapunguzia dhamana hiyo na kusema “inalingana na makosa dhidi yao.”

Wizara ya Afya yafundisha Wakenya jinsi ya kuvalia barakoa

Na GEOFFREY ANENE

WIZARA ya Afya imeonekana kugundua Wakenya wengi hawajui kuvalia barakoa baada ya kuanza kuwahamasisha jinsi ya kuzivalia ili kuzuia maambukizi wakati huu wa janga la virusi hatari vya corona.

Kupitia mtandao wake wa kijamii hapo Alhamisi, wizara hiyo imeonyesha makosa mengi, ambayo Wakenya wanafanya na kufanya vita dhidi ya virusi hivyo kuwa kazi bure.

Kosa la kwanza ni kuwa Wakenya wamekuwa wakifanya ni kuvalia barakoa kufunika kinywa pekee. Pili, kuvalia barakoa kwenye kipaji. Tatu, mtu kuvalia barakoa kwenye kidevu. Kuvalia barakoa kwa kufunga kamba zake zikipitana pia ni kosa.

Kuvalia barakoa vizuri, wizara hiyo inasema, kutasaidia kukomesha uenezaji ya ugonjwa wa covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Hapo Jumatano, Shirika la Amref Health Africa pia lilisema kuvalia barakoa chafu, kuacha kamba zikining’inia ama kunining’iniza barakoa kwa kutumia kamba moja pamoja na kuachilia nywele kando ya uso ni makosa.

Mwandishi huyu pia ameshuhudia Wakenya wengi wakibeba barakoa mkononi badala ya kuzivalia.

Njia nzuri ya kuvalia barakoa ni kuhakikisha inafunika kinywa na pua. Hakikisha nywele zinalala mgongoni. Funga kamba za barakoa nyuma ya kichwa na shingo bila ya kuzipitanisha. Unapotaka kuvua barakoa, itoe kutokea nyuma ya kichwa.

Kufikia Aprili 23, Kenya ilikuwa imeripoti visa 320 baada ya watu 17 kupatikana na virusi hivyo katika saa 24 zilizopita. Virusi hivyo vimeua watu 14 nchini Kenya na 185, 461 duniani.

Polo aona moto kuchezea maski

NA MARU WANGARI

LIMURU MJINI

JAMAA mjini hapa alijipata mashakani kwa kufanyia utani masharti ya kujikinga na corona.

Yote yalianza kalameni huyo alipojipaka rangi nyeupe usoni kuwatania maafisa wa usalama kuwa alikuwa amevalia maski.

Polo huyo ajichora rangi hiyo kuanzia kwenye pua lake, midomoni mashavuni na hadi kwenye masikio yake kwa namna iliyofanya aonekana alikuwa amevalia maski.

Wakazi hawakuamini macho yao walipogundua polo huyo alikuwa amejichora ionekane amevalia maski huku akiendelea na shughuli zake kama kawaida na kutangamana na watu sokoni.

Baadhi walikashifu kitendo cha jamaa huyo huku wakisema alikuwa akihatarisha sio tu maisha yake, bali pia maisha ya wakazi kwa kufanyia utani maagizo yaliyotolewa na serikali kuhusu kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

Hata hivyo, jombi huyo alijipata mashakani alipokutana na maafisa wa polisi waliokuwa wakipiga doria mjini humo.

Baada ya polo huyo kufahamu kwamba utukutu wake ulikuwa umegunduliwa na maafisa hao, alichana mbuga kuwakwepa polisi ambao walimfuata unyo unyo na kumkamata.Kulingana na mdokezi wetu, kalameni huyo, alijitetea kwa polisi akisema aliamua kufanya hivyo kwa kukosa hela za kununua maski.

‘Maski zinauzwa Sh50 na sina uwezo wa kununua kwa sababu sijakuwa nikifanya kazi sasa kwa karibu mwezi mmoja tangu tuliposimamishwa. Nilitafuta mbinu za kusaka chakula na wakati huo huo kuepuka kukamatwa kwa kutokuwa na maski ndipo wazo hilo liliponijia,’ alijitetea akiwaomba polisi kumwachilia.

Juhudi zake za kujitetea ziliambulia patupu huku polisi wakimburura na kumweka katika gari lao akisubiri adhabu kisheria.

Na Mary Wangari

Je, ni kweli barakoa za kushonewa mtaani zinazuia maambukizi ya corona?

Na GEOFFREY ANENE

HUKU biashara ya kushona na kuuza barakoa zilizotengenezwa kwa kutumia vitambaa ikinoga kote nchini Kenya, mjadala umezuka kuhusu uwezo wa barakoa za aina hiyo kuzuia maambukizi ya virusi hatari vya corona.

Aina tatu za barakoa zimekuwa zikizungumziwa sana kwenye mitandao ya kijamii, huku ile ya N95 ikiaminika kuwa bora kabisa kwa sababu inaweza kuzuia maambukizi ya virusi hivyo kwa asilimia 95.

Inafuatiwa na barakoa za kufanyia upasuaji, ambazo pia zina uwezo wa asilimia 95 wa kuzuia virusi kupenyeza, lakini haziwezi kuzuia bakteria, vumbi na poleni kwa asilimia 100 kama N95.

Madai ni kuwa barakoa za kushona kwa kutumia nguo hazina uwezo wa kuzuia maambukizi.

Mwandishi huyu alitafuta ukweli wa habari hizo kutoka kwa madaktari watatu wanaohudumu hapa jijini Nairobi na kuthibitisha kuwa kuvalia barakoa za vitambaa ni afadhali kuliko kuwa bure.

“Barakoa za kushonwa kwa kutumia vitambaa zinapitisha vitone. Hata hivyo, kuwa na barakoa hii ni bora kuliko kukosa kuvalia barakoa. Ndio hazizuii vitone, lakini ni porojo kuwa asilimia yake ya kuzuia maambukizi ni sifuri. Hakuna mtu amefanya utafiti kuthibitisha kuwa uwezo wake ni asilimia sifuri. Hata hivyo, zinasaidia katika kufumba polisi macho ili ukiivalia usikamatwe na kushtakiwa ama kupigwa faini,” alisema daktari Magada, ambaye anajihusisha na matibabu ya mgonjwa ya kuambukizana.

Dkt Tom Mboya anasema virusi vya corona vinasambazwa kupitia vitone kwenye hewa. “Vinaenezwa mtu anapokohoa ama kupiga chafya na pia mtu anayepata vitone hivyo kuvuta pumzi hiyo ama kugusa macho yake ama kinywa. Kwa jumla, barakoa inazuia mtu aliyeivalia kuangukiwa na vitone hivyo, lakini pia inazuia mtu ambaye ni mgonjwa kueneza virusi hivyo,” anasema Mboya na kukubaliana na Magada kuwa kuvalia barakoa yoyote ni bora kuliko kukosa kuvalia barakoa.

“Barakoa za aina ya N95 na upasuaji ndizo nzuri kabisa, lakini zinafaa kutengewa wahudumu wa afya pekee kwa sababu ziko chache kote ulimwenguni na pia wako katika hatari zaidi ya kuambukizwa wanapohudumia wagonjwa. Barakoa za kutumia vitambaa hazina uwezo mkubwa wa kuzuia maambukizi ya virusi, lakini ni nzuri katika kuzuia vitone kuanguka ovyo na kwa hivyo zinazuia nafasi ya kuambukiza watu karibu nasi,” anasema.

Kuhusu barakoa za kutengenezwa kwa kutumia vitambaa, daktari Fredrick Okong’o anasema lazima ziwe zimeshonwa kwa kutumia vitambaa vitatu. Amesifu barakoa za kushonwa akisema, “ni rahisi kuoshwa.”

Aidha, Magada ameonya Wakenya dhidi ya kuvua na kuvaa barakoa kila mara bila ya kusafisha mikono yao. “Tunafanya kazi bure tukivaa barakoa halafu kila mara mtu anaivua na kuivaa bila ya kusafisha mikono. Inafaa ukivua barakoa, safisha mikono yako kwanza kabla ya kuivaa tena,” alisema.

Naye Mboya ameshauri, “Mataifa ambayo yamefaulu kupunguza visa vya maambukizi yamefuata maagizo inavyotakikana. Naomba sisi sote tufuate maagizo ya kunawa mikono kwa kutumia sabuni na maji, kusafisha mikono kwa kutumia ‘sanitaiza’ na kuvalia barakoa tunapokuwa kwenye umma. Kumbuka kukaa mbali na watu wengine kila wakati.”

Okong’o pia ametaka Wakenya wote wavalie barakoa “kwa sababu huwezi kujua nani ana virusi vya corona na nani hana.” “Hakikisha barakoa yako ni safi kabla ya kuivalia kila asubuhi. Iweke kwenye kemikali ya kuua viini vya maradhi usiku mzima,” anashauri.

‘Ninashona barakoa moja kwa dakika 15’

Na GEOFFREY ANENE

Barakoa zimeokoa biashara ya fundi cherehani Jacob Onyango ambayo ilikuwa inazama kutokana na uhaba wa wateja kwa sababu ya janga la virusi hatari vya corona.

Onyango ana duka la kushona nguo mtaani Kariobangi South Civil Servants katika kaunti ya Nairobi. Kwa miaka 15, amekuwa akishona suti. Hata hivyo, alilazimika kujifunza kutengeneza barakoa baada ya janga lilo hilo kumfungulia mlango mwingine.

“Biashara yetu hapa huwa ni kushonea wateja suti. Tulikuwa tunauza angaa suti tatu kila wiki kabla ya janga la virusi vya corona. Hata hivyo, hatujaona mteja hata mmoja amekuja hapa kwa kipindi cha mwezi mmoja na wiki moja hivi kupima suti. Tulikuwa tunauza kila suti Sh4,500,” alieleza Onyango, ambaye ni mmiliki wa duka hilo na ameajiri watu wengine wawili.

“Badala ya kukaa tu tukijisikitia kwa sababu biashara ilikuwa imeenda chini sana, tuliamua kushona barakoa. Barakoa sasa inafanya mwisho wa siku tuende nyumbani na chakula. Tulianza kushona barakoa Aprili 1. Kila mmoja wetu anashona barakoa 20 kila siku. Kutoka barakoa 60 tunazoshona, robo tatu huwa zinanunuliwa kila siku. Tunauza barakoa moja Sh50,” anasema Onyango.

Bernard Wanjare, ambaye ni mmoja wa watu wanaofanya kazi na Onyango, anasema hawakuwa na ujuzi wa kushona barakoa. “Tulitumia mtandao wa YouTube kupata mafunzo ya kushona barakoa. Ujuzi huo tulipata kutoka kwa Mjerumani mmoja, ambaye alikuwa anapeana mafunzo hayo. Ilinichukua binafsi dakika 10 kupata maarifa hayo kwa sababu kazi yetu ni ya fundi wa nguo,” alisema Wanjera, huku akionyesha mwandishi huyu jinsi wanavyotengeneza barakoa.

Anasema walifikia uamuzi wa kuuza barakoa Sh50 kwa sababu ya mali ghafi wanayotumia na pia uwezo wa wananchi kununua.

Onyango anasema kuwa bei ya barakoa katika duka lake ni moja tu iwe mtu mzima ama mtoto kwa sababu mbinu ya kuzitengeneza na nyenzo ni zile zile.

“Tunashona barakoa moja kwa kati ya dakika 15 na 25 kwa kutegemea kama tunaweka mipira ya kunyumbulika ama kamba ya kushonwa. Barakoa za kamba zinachukua muda mwingi,” anasema Onyango na kufichua kuwa kuna wateja wanaopenda barakoa zilizoongezwa nyumbufu kwa sababu ni rahisi kuvaa. “Wengine hawapendi barakoa za nyumbufu kwa sababu wanasema zinawaumiza masikio,” Onyango alieleza Taifa Leo katika mahojiano.

Kuhusu rangi ya barakoa ambazo Wakenya wananua sana, Onyango anasema, “Watu wanapenda sana rangi nyeupe na buluu, ingawa kila mtu huwa na rangi anayopenda zaidi kuliko zingine.”

Hata hivyo, anasema watu wengi wanaona aibu kuvalia barakoa. Pia, kuna wale walio na dhana kuwa wakivalia buluu wataonekana kama wahudumu wa afya kwa hivyo wanachagua barakoa za rangi hiyo. “Kama si faini kali (Sh20,000) ama kufungwa jela miezi sita, sidhani kama watu wengi wangevalia barakoa. Wengi wanazivalia kwa sababu wamelazimishwa,” anasema.

Onyango alikamilisha mahojiano haya kwa kushauri Wakenya, “Kila mtu ajilinde. Osha mikono inavyotakikana. Dumisha usafi. Tufuate maagizo na tutakuwa salama. Tujilinde.”

Mkenya anayeishi Dubai asema bila kuvalia barakoa na glavu hakuna kuuziwa chochote

Na GEOFFREY ANENE

Wakenya wanapenda kuzuru na kufanya biashara mjini Dubai katika Milki za Kiarabu. Zaidi ya Wakenya 50, 000 wanaishi nchini humo, hasa Dubai.

Wakati huu, mambo ni magumu katika nchi hiyo anavyosimulia Mkenya Lilian Adongo kuwa watu wanafutwa kazi kutokana na janga la virusi vya corona.

“Kabla ya mkurupuko wa virusi vya corona, mambo hapa Dubai yalikuwa sawa. Watu walitembea bila hofu, na hata kujaa kwenye ufukwe.

Hata hivyo, sasa hivi mambo yamebadilika. Kufikia saa mbili usiku, hakuna mtu anafaa kuwa nje ya nyumba. Ninavyozungumza nawe sasa hivi ni saa tatu usiku; Dubai ni kimya kama maji mtungini.

Hakuna mtu anakubaliwa kununua bidhaa ‘supermarket’ bila kuvalia barakoa na glavu. Bila vitu hivi vyakuzuia maambukizi ya virusi vya corona, huwezi kuuziwa chochote.

Makanisa yote, misikiti, taasisi za elimu na maeneo ya burudani kama vile ya kuona sinema, yalifungwa.

Nimekuwa Dubai kwa miaka mitano sasa. Nilipowasili hapa, nilifanyia kampuni moja kazi, lakini nikajiuzulu kwa sababu mshahara ulikuwa mdogo. Sasa najishughulisha na biashara ambayo nilianzisha baada ya kujiuzulu. Biashara yenyewe ni ya kuuza bidhaa mtandaoni.

Changamoto mpya imejitokeza katika biashara yangu wakati huu wa janga la virus ivy corona. Wateja wameongezeka, lakini hakuna njia ya kuwafikishia bidhaa ni balaa. Nalazimika kutumia mabasi ya bure kusafirisha bidhaa zilizonunuliwa ama niitishe teksi kwa niaba yao halafu wanalipa ada ya teksi wakipokea bidhaa zao.

Jamaa zangu wako Kenya, lakini naishi pekee yangu hapa Dubai. Ningependa kusihi Wakenya wajiweke salama wasije wakaambukizwa virusi hatari vya corona. Pia, nawashauri wasijaribu kuomba kazi wakati huu. Wasijaribu kutafuta kazi yoyote kupitia kwa maajenti kwa sababu wataliwa pesa bure. Vilevile, wasijaribu kuja na visa ya kutalii kwa sababu hakuna kazi. Watu wengi wamepoteza kazi kwa njia ya kufutwa bila ya kulipwa mishahara yao. Sasa hivi ni kubaya kabisa.”

Milki za Kiarabu imethibitisha watu 2, 659 katika nchi hiyo wameambukizwa virusi vya corona, ambavyo vinasababisha ugonjwa wa Covid-19. Watu 12 wamefariki nchini Milki za Kiarabu kutokana na ugonjwa huo. Virusi hivyo, ambavyo vilianzia mjini Wuhan nchini Uchina, vimeenea katika mataifa 209.

Joho awapa polisi maski kusambazia umma

DIANA MUTHEU na MOHAMED AHMED

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho ametoa msaada wa barakoa kwa maafisa wa polisi ili wazipeane kwa wananchi wasiokuwa nazo, badala ya kuwakamata.

Haya yalijiri baada ya gavana huyo kupokea chakula cha msaada mnamo Jumatano kutoka kwa Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai.

Akizungumza katika ofisi yake, Gavana Joho alimwomba Bw Mutyambai kuwaelekeza maafisa wa polisi wawape barakoa wananchi watakaopatikana wakitembea au kusafiri bila kujikinga, badala ya kuwanyaka.

“Tumepata bandali nne ya unga kutoka kwa Idara ya Polisi ambazo tumepewa na Inspekta Jenerali. Kwa upande wetu, tunakupa barakoa uwape maafisa wako na zingine zaidi zipewe wananchi katika vizuizi vya polisi,” akasema Bw Joho.

Bw Joho alimwomba Bw Mutyambai kuwaelekeza maafisa wake kuchukua barakoa hizo katika ofisi zake.

“Tumekubaliana na Inspekta Jenerali kuwa watu watakaopita katika vizuizi watapewa barakoa hizo. Hata hivyo, ni onyo kwa watu wote kuwa lazima wavae maski hizo baada ya kuzipata au la sivyo, sheria itachukua mkondo wake,” akasema.

Ombi la gavana huyo linakuja siku moja baada ya Bw Mutyambai kutangaza kuwa wananchi watakaopatikana bila barakoa hizo watakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Hii ni baada ya Wizara ya Afya kutangaza kuwa mtu yeyote atakayepatikana bila barakoa atatozwa faini ya Sh20,000 au kifungo cha hadi miezi sita.

Bw Mutyambai alikubali ombi la gavana huyo akisema, “Namshukuru Gavana Joho kwa kutupa barakoa za kutosha kwa maafisa wa polisi. Tumekubaliana maafisa hao watatotoa zingine kwa wananchi.”

Alisema kuwa agizo la kila mtu kuvalia kifaa hicho ni moja ya hatua ya kuzuia ueneaji wa virusi vya corona.

“Tunaelewa kuwa si kila mmoja anaweza kupata pesa za kununua barakoa lakini polisi watatoa msaada wao. Pia ni vizuri tufuate maagizo kwa kuzivalia,” akasema.