Wakala akana kuiba Sh11 milioni za bima

Na RICHARD MUNGUTI

WAKALA wa kampuni ya kuuza bima alifikishwa kortini Jumanne kwa wizi wa Sh11.8milioni alizopokea kwa niaba ya kampuni ya Waiza Reinsurance Limited.

Wakili Peter Wena aliomba kesi hiyo iahirishwe hadi Machi 8,2021, Cecilia Bridgit Rague kuwezesha mshtakiwa asome mashtaka ambayo yamewasilishwa mengine mapya na mkurugenzi wa mashtaka (DPP) .

“Naomba mshtakiwa asisomewe mashtaka ndipo asome mashtaka mapya yaliyowasilishwa na DPP,” alirai Bw Wena.

Mahakama ilifahamishwa kuwa mshukiwa anatakiwa kujibu shtaka baada ya kuyaelewa.

Hakimu mkuu Bi Martha Mutuku alikubalia ombi la mshtakiwa na kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 8,2021.

Mshtakiwa anakabiliwa na shtaka la kuiba Sh11,850,027 mnamo Desemba 6 2019. Alishtakiwa aliiba pesa hizo kutoka benki ya NCBA tawi la Westlands Nairobi.

Wakala huyo na kampuni ya Underwriting Africa Insurance Brokers alipokea pesa hizo kwa niaba ya kampuni ya Waica Reinsurance Limited akidai atawapelekea.

Mshukiwa huyo yuko nje kwa dhamana.

“Mahakama imesikia kilio chako. Utarudi tena hapa mahakamani mnamo Machi 8 kujibu mashtaka mapya,” alisema Bi Mutuku.

Kila familia kulipa Sh6,000 katika mageuzi mapya NHIF

Na Otiato Guguyu

KILA familia italazimika kulipa ada ya lazima ya Sh500 kwa Mpango wa Bima ya Afya Nchini (NHIF) huku serikali ikiandaa bima ya afya kwa Wakenya wote.

Waziri wa Fedha Ukur Yatani alisema kila familia itatozwa Sh6,000 kila mwaka ili kujumuishwa katika Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) kwa huduma za wagonjwa waliolazwa na wasiolazwa ikiwemo huduma za uzazi, matibabu ya maradhi ya figo, saratani na upasuaji.

“Lengo la serikali ni kubuniwa kwa mpango wa lazima wa UHC utakaosimamiwa na NHIF na kudhibitiwa na Wizara ya Afya na kutumika kama mpango wa kitaifa kwa raia wote wa Kenya pasipo kujali hadhi ya mtu katika jamii,” alisema katika taarifa ya bajeti ya mwaka 2021/2022.

Mpango huo wa lazima wa kujiunga na NHIF kwa Wakenya wote umeboreshwa zaidi kinyume na ule uliopo sasa ambapo ni wafanyakazi katika sekta rasmi pekee wanaoshurutishwa kuwa wanachama.

Wakazi Kisauni wahimizwa wakate bima ya afya

Na WINNIE ATIENO

WAKAZI wa Kisauni wamehimizwa kuchukua Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF) iwagharimie matibabu wanapougua.

Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo alisema waendeshaji bodaboda na madereva wa matatu ni miongoni mwa watu ambao wako hatarini kutokana na kazi yao.

“Wako katika hatari ya kuhusika kwenye ajali maana mtu anaweza kuwa anatoka tu hivi mara gari limegongwa na ajali imetokea hivyo wanafaa kupelekwa hospitalini. Jiandikisheni kwa NHIF ili mtibiwe mkiwa wa wagonjwa na hata wake na watoto wenu watatibiwa,” alisema Bw Mbogo.

Alisema afisi yake itasaidia wahudumu wa sekta ya matatu na bodaboda ili wapate bima hiyo ya afya.

“Nitawalipia kwa mwaka mzima. NHIF ni muhimu sana. Wale hawana vibali wajihimize wawe na stakabadhi hizo muhimu,” alisisitiza.

Kadhalika alisema atawapeleka vijana 600 kujifunza udereva.

Bw Mbogo aliwataka vijana kujitosa katika biashara badala ya kungojea kuajiriwa.

“Pesa haziji kwa kuajiriwa kwa mwezi; biashara ndiyo inaleta maendeleo. Fanya biashara huku ukiwa umeajiriwa,” alishauri.

‘Wahudumu wa afya Mombasa hawana bima ya afya’

Na WINNIE ATIENO

WAHUDUMU wa afya katika Kaunti ya Mombasa wanafanya kazi bila bima ya afya wakiendelea kuhatarisha maisha yao wanapokabiliana na janga la corona.

Haya yalifichuka kwenye mahojiano kati ya kamati ya bunge la seneti kuhusu corona na vyama vya madaktari na wahudumu wa afya.

Madaktari walifichua namna mwenzao, Dkt Biabu Adam, alikuwa mgonjwa na kulazimika kugharimia matibabu alipolazwa hospitali moja ya mmiliki binafsi.

“Ugonjwa huo ulisababisha nijifungue kwa njia ya upasuaji ya dharura. Nilishangaa kwamba bima yangu ya afya ilikuwa haijalipwa ilhali sikuwa na uwezo wa kusimamia gharama hiyo kwa wakati huo, ” alisema Dkt Adam kwenye barua aliyomwandikia afisa wa afya Dkt Khadija Shikely mnamo Julai.

Baada ya upasuaji huo, daktari huyo ambaye anafanya kazi katika hospitali ya wilaya ya Tudor alipewa bili ya Sh190,000.

Mwezi mmoja baadaye anang’ang’ana kulipa pesa hizo huku wenzake wakiendelea na mchango.

“Alidhania bima yake ya afya itasimamia gharama hiyo lakini tukagundua kaunti ilisitisha malipo. Inasikitisha kuwa madaktari na wahudumu wengine wa afya wanakabiliana na janga hili na hawana bima ya afya,” alisema naibu katibu wa chama cha madaktari nchini tawi la Pwani Dkt Niko Gichana.

Hii ni taswira ambayo inawakumba zaidi ya madaktari 100 na wahudumu wa afya ambao wanalalamika kuwa hawana bima ya afya.

Hata hivyo, serikali ya Kaunti ya Mombasa ilijitetea huku ikiilaumu hazina ya bima ya afya chini NHIF kwa kukataa kuwapa wafanyakazi hao huduma hiyo.

Afisa wa afya ya umma Kaunti ya Mombasa Bi Pauline Oginga akihutubia wahudumu wa afya kwenye uzinduzi wa mafunzo ya namna ya kudhibiti maambukizi ya corona miongoni mwao. Picha/ Winnie Atieno

Walisema NHIF inawalazimu kulipa Sh142 milioni kabla wapewe bima hiyo.

Zaidi ya wahumudu wa afya 42 waliambukizwa virusi hivyo kaunti ya Mombasa.

Gavana Hassan Joho alisema serikali yake ilitafuta njia mbadala kwa kuwapa wafanyakazi hao matibabu ya bure katika hospitali kuu ya Pwani.

“Tumejaribu kukabiliana na swala hili lakini kuna changamoto,” Joho aliiambia kamati hiyo.

Bima ya afya bado ghali kwa Wakenya, lakini suluhu zipo

Na SAMMY WAWERU

Kulingana na Wizara ya Afya takriban asilimia 13 ya Wakenya hawana uwezo kupata huduma za afya kwa sababu ya ukosefu wa fedha, huku asilimia 6 wakiwa katika hatari inayotokana na gharama ya ghafla ya matibabu wanapougua.

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Mpango wa Afya kwa Wote (UHC), asilimia 62 ya Wakenya hawana bima ya afya, bima ya NHIF ikiwakilisha asilimia 35 pekee ya Wakenya wote.

Aidha, inakadiriwa kuwa Wakenya wapatao milioni 1.5, sawa na asilimia 3 wanatumia bima ya kibinafsi kugharamia matibabu.

Huku Rais Uhuru Kenyatta akijikakamua kuimarisha huduma za afya nchini, kupitia mojawapo ya ajenda nne kuu, Afya Bora kwa Wote, upataji wa huduma bora za matibabu na kwa gharama nafuu kwa wananchi wengi ni bayana ungali kikwazo.

Waathiriwa ni wenye mapato ya chini na wafanyabiashara wadogo na wa kiwango cha kadri – SMEs, katika sekta ya Juakali.

Ili kuangazia changamoto hizo, 4G Capital Group Limited (4G Capital) ambalo ni shirika la kifedha kwa ushirikiano na kampuni ya bima ya Insurtech Innovator Turaco, imebuni mpango wa utoaji bima ya afya kwa bei nafuu. Mpango huo unalenga wafanyabiashara wa mapato ya chini na ya kadri.

4G Capital imekuwa nchini Kenya tangu 2013, ambapo imekuwa ikitoa mikopo kwa SMEs Ukanda wa Afrika Mashariki, pamoja na ushauri namna ya matumizi ya fedha na pia mafunzo jinsi ya kuimarisha biashara.

Hapa nchini, shirika hilo lina wateja 104, 000, Uganda 46, 000, na linasema kuzinduliwa kwa mpango wa bima ya afya ya bei nafuu kutasaidia kuwalinda kutokana na changamoto za kifedha zinazoibuka wanapogonjeka au kupata majeraha.

Wengi wa wateja, wanahudumu katika sekta ya Juakali na wanapougua biashara zao huwa katika hatari ya kufilisika. Kila baada ya miaka mitano hapa nchini, asilimia 42 ya wenye mapato madogo hupitia nyakati ngumu kifedha hasa wanapolazwa hospitalini kupata matibabu.

4G Capital kwa ushirikiano na Turaco, mpango wa bima iliyozindua utasaidia kupunguza gharama ya pesa inayoibuka hasa mteja anapolazwa au kufariki. Aidha, ada ya malipo ya chini katika kipindi cha miezi 12, sawa na mwaka mmoja ni Sh1, 000.

Kulingana na 4G Capital, bima hiyo italinda mteja aliyelazwa zaidi ya siku tatu hospitalini au kugharamia mazishi.

Isitoshe, kufidiwa, mteja anaweza kuwasiliana na shirika hilo kwa njia ya simu au mtandao wa WhatsApp, na kupokea fidia baada ya saa 72.

Huku janga la Covid – 19 likiendelea kuwa kikwazo kwa taifa na ulimwengu, sekta mbalimbali nchini, ikiwemo ya SMEs, zimeathirika kwa kiasi kikuu. Turaco pia inatoa huduma za bima kwa waathiriwa wa janga la corona, ambalo limekuwa kero la kimataifa. “Tunafurahia kushirikiana na Turaco kutoa huduma za bima ya afya kwa wateja wetu, hasa wakati huu wanapitia nyakati ngumu zinazotokana na athari za Covid – 19.

“Wafanyabiashara wa kiwango cha chini na cha kadri, ambao ni nguzo ya uchumi wa Kenya ndio wameathirika kwa kiasi kikuu. Kupitia ushirikiano wetu, tutaweza kuimarisha upataji wa huduma zao za matibabu,” Wayne Hennessy-Barrett, Mwanzilishi na Afisa Mkuu Mtendaji wa 4G Capital akaambia ‘Taifa Leo’ katika mahojiano ya kipekee.

Sekta ya SME inachangia asilimia 50 ya ushuru wa Kenya, huku ikiwakilisha asilimia 75 ya nguvukazi nchini.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Turaco, Ted Pantone alisema huduma za bima ya afya kwa bei nafuu kupitia ushirikiano huo, pia zinalenga kuondoa hofu inayogubika Wakenya wakati huu mgumu wa Covid – 19.

“Ingawa mambo mengi maishani hayatabiriki, upataji wa huduma bora na nafuu za afya hufai kuwa kikwazo kwa wananchi. Ni fahari yetu kushirikiana na 4G Capital kuona kuwa huduma za afya zinaimarika,” Ted akaeleza, akihimiza Wakenya kukumbatia mpango huo uliozinduliwa.

Ikizingatiwa kuwa wateja wengi wa 4G Capital ni wafanyabiashara wa mapato ya chini na ya kadri, wanaohudumu katika mazingira ya soko yanayoshuhudia misongamano ya watu, shirika hilo limeungana na wadau husika kutoa misaada ya sabuni, vitakasa mikono na vifaa vya kunawa mikono ili kuzuia kusambaa kwa Homa ya Corona.

“Lengo letu si kuimarisha uwezo wa wateja kifedha pekee, ila tunawajali. Wasimamizi, wawekezaji na wafanyakazi wetu, tumejitolea kulinda wateja wote,” anasema Wayne Hennessy-Barrett, Afisa Mkuu Mtendaji 4G Capital.

Tangu kuwepo kwa shirika hilo Afrika Mashariki, limetoa zaidi ya mikopo 900, 000 yenye thamani zaidi ya Dola 100 milioni, sawa na Sh10, 635, 000 thamani ya pesa za Kenya.

4G Capital ina jumla ya matawi 100 Kenya na Uganda, yaliyobuni nafasi za ajira kwa zaidi ya watu 500.

Madaktari washinikiza kupewa bima ya afya

JUMA NAMLOLA na WINNIE ATIENO

MADAKTARI katika hospitali za umma Kaunti ya Mombasa, sasa wanataka serikali iwape bima ya afya huku visa vya maambukizi nchini vikifika 22,053.

Ingawa Mombasa ilikuwa na kisa kimoja pekee kati ya watu 690 walioambukizwa kote nchini jana, madaktari wanaotibu wagonjwa wa corona walisema wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa, ilhali hawana bima ya afya.

“Ni kinaya kwamba madaktari katika kaunti hii hawana bima ya afya, hata baada ya kujitolea kusaidia nchi kukabiliana na janga hili la corona,” alisema Dkt Abidan Mwachi, mwakilishi wa Pwani katika chama cha KMPDU.

Alisema kukosekana kwa bima ya afya ni hatari ambayo wahudumu wa afya wanakodolea macho, hasa wakati huu ambapo tayari wahudumu 45 wameambukizwa virusi hivyo wakiwa kazini.

Dkt Mwachi alimsihi Gavana Hassan Joho na Hazina ya Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) kutatua jambo hilo, ili wahudumu wa afya waweze kupata huduma hiyo muhimu

.“Mgogoro ulioko kati ya NHIF na serikali ya Kaunti ya Mombasa unafaa kutatuliwa haraka iwezekanavyo ili wahudumu wa afya waweze kuwekwa kwenye bima hiyo ya afya,” alisema Dkt Mwachi.

Pia chama hicho cha KMPDU kilitoa wito kwa serikali za kaunti kuhakikisha wahudumu wa afya wanapewa barakoa maalum za N95 ili kujikinga dhidi ya virusi hivyo.

“Barakoa za N95 ndizo zinazofaa kutumiwa na wahudumu wa afya katika janga hili. Pia tunaonya Wakenya dhidi ya unyanyapaa miongoni mwa watu wanaouguza virusi vya corona,” alisisitiza Dkt Mwachi.

Kaunti ya Mombasa bado ni ya pili kwa maambukizi ikiwa na watu 2,067 baada ya mtu mmoja kuambukizwa jana.

Nairobi jana iliongoza kwa visa 535 na kufanya idadi ya watu wote walioambukizwa katika kaunti hiyo kuwa 13,416, ambayo ni zaidi ya nusu ya maambukizi yote nchini.

Idadi ya wagonjwa walioruhusiwa kuondoka hospitalini na karantini pia iliongezeka kwa watu 58 huku watu watano wakiaga dunia.

Binti apiga hatua katika biashara ya bima licha ya changamoto

PAULINE ONGAJI

Sio wengi wanaweza kumudu huduma za bima hapa nchini. Na hii ni mojawapo ya sababu zilizomsukuma Bi Wanjiru Githiomi, 45, kuanzisha kampuni ya BimaNet, jukwaa linaloshirikiana na kampuni za bima ili kutoa huduma hii kwa bei nafuu.

Ni huduma ambayo hasa inalenga watu binafsi na biashara ndogo ambapo wamekuwa wakishirikiana na zaidi ya wasambazaji 60 wa huduma za bima wanaotangaza bidhaa hii hasa kwa biashara ndogo.

“Naweza sema kwamba huduma hii inawapa watu binafsi, na wamilikia wa biashara ndogo, kupokea huduma hii,” aeleza.

Kulingana naye, BimaNet pia imeshirikiana na mashirika kadhaa ya bima na kulingana na mapato yao, wanachangia katika hazina ya kusaidia kuelimisha wanafunzi kutoka familia maskini.

“Pia, tuko katika harakati za kushirikiana na majukwaa mengine kama vile makanisa, taasisi za kimasomo, vyama, sacco miongoni mwa mengine iliyo na wanachama wanaokaribiana na vikundi tunavyolenga,” asema.

Mpangilio wao wa kipekee wa kibiashara unawawezesha kupunguza gharama ya kutoa huduma hii na hivyo kupitisha kipunguzio hiki kwa wateja na washirika wao. “Aidha, mawakala wa bima na mabroka wetu wanapata vipunguzio vya juu kumaanisha kwamba kila mtu ananufaika,” aongeza.

Kulingana naye, changamoto kuu imekuwa kupata wauzaji. “Aidha, Wakenya kwa ujumla hawatambui umuhimu wa bima ya maisha kwa sababu wengi wetu hutegemea harambee ili kuchanga pesa, kila tunapokumbwa na majanga,” aeleza.

Pia, mkurupuko wa maradhi ya COVID-19 umesababisha hasara kubwa katika biashara hii. “Lakini badala ya kufa moyo na kuishiwa nguvu, tumeamua kutumia wakati huu kuunda mikakati ya kutumia fursa hii kujiimarisha. Pindi baada ya mawimbi haya kupita, tunaamini kwamba bima ya afya itakuwa mojawapo ya bidhaa zitakazohitajika sana na wengi,” aeleza.

Pia anazungumzia changamoto ya kusawazisha muda wa kukaa nyumbani kwake jijini Cape Town, na pia kuendesha biashara nchini Kenya.

Bi Githiomi ambaye ni mkazi wa Afrika Kusini, alizaliwa na kusomea humu nchini kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Cape Town, nchini Afrika Kusini ambapo alisomea masuala ya sheria.

Baadaye alihudumu katika Nyanja ya sheria kwa mwaka mmoja unusu kabla ya kujitosa katika taaluma ya mauzo na udhamini na kuanzisha kampuni yake kwa jina Leverage Inc. Hata hivyo, aliuza biashara hii miaka mitatu iliyopita, alipohitaji mtaji wa kuanzisha biashara yake mpya nchini Kenya.

Anasema kwamba kamwe hajutii kuacha kazi iliyokuwa na mapato na kujitosa katika ujasiriamali. “Uamuzi huo ulinisaidia kujivunia kipato kizuri, huku ikiniachi muda wa kuwa mama na mke,” aeleza.

Wanafunzi wote kunufaika na bima ya afya

Na FAITH NYAMAI

WANAFUNZI wote milioni 10 nchini watapokea bima ya serikali ya afya mwaka huu bila kujali iwapo maelezo yao yamejumuishwa katika Mfumo wa Kitaifa wa Kuhifadhi Habari kuhusu Elimu (NEMIS) au la.

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha jana alisema walimu wakuu wa shule sasa wanahitajika kuwahesabu wanafunzi wao katika shule za msingi na za upili na kuwasilisha data hiyo kwa Wizara ya Elimu ili kuwezesha usambazaji wa fedha katika taasisi hizo.

“Masuala ya habari za wanafunzi kutoweka katika Nemis kwa sababu hawana cheti cha kuzaliwa hayapaswi kuwa kizingiti dhidi ya haki ya wanafunzi ya kupata elimu,” alisema Bw Magoha.

Waziri huyo alisema serikali itasambaza fedha shuleni ili kuwezesha uendeshwaji shwari wa taasisi hizo katika muhula wa kwanza.

Aidha, alisema watahiniwa wote wa darasa la nane na kidato cha kwanza pia watasajiliwa kwa mitihani yao ya kitaifa mwaka huu pasipo kujali ikiwa wana vyeti vya kuzaliwa au la.

Serikali imekuwa ikisambaza fedha shuleni kuwafadhili wanafunzi ambao habari zao zimejumuishwa katika Nemis.

Wanafunzi wa sekondari pia hawawezi kupata Bima ya Afya Nchini katika mpango wa elimu ikiwa habari zao hazijajumuishwa katika Nemis.

Mfumo huo huwatambulisha wanafunzi kwa kutumia data iliyojumuishwa na kutuma habari hizo kwa NHIF kwa matibabu.

“Changamoto chache ambazo shule zimekumbana nazo wakati wa kujumuisha maelezo ya wanafunzi kwa kutumia Nemis zinasuluhishwa na Wizara,” alisema.

Waziri huyo alikuwa akizungumza jana katika uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili kuhusu Elimu.

Ufadhili huo umenufaisha wanafunzi 9,000 maskini kutoka maeneo 110 na miji 15 yenye vitongoji duni.

Mpango huo unafadhiliwa na Mradi wa Kuboresha Viwango vya Ubora katika Elimu ya Sekondari (SEQIP) na Wizara ya Elimu, kwa usaidizi kutoka kwa Benki ya Dunia na unatekelezwa kupitia Wakfu wa Equity Group

Ufadhili huo wa Sh3 bilioni ambao sasa upo katika mwaka wake wa pili umedhamiriwa kuhakikisha kwamba watahiniwa wote wa KCPE 2019 ambao ni maskini na wasiojiweza wanasaidiwa kujiunga na shule walizochagua.

Tuelezwe Sh636m za bima kwa afya ya wakongwe zilivyotumika – Wabunge

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wameitaka Wizara ya Afya na Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF) kutoa maelezo kamili kuhusu namna Sh636 milioni zilitumika kufadhili matibabu ya wakongwe chini ya mpango wa Inua Jamii katika mwaka wa kifedha wa 2018/2019.

Hii ni baada ya kufichuka kwamba wengi wa wakongwe hao hawajakuwa wakipata huduma za afya katika hospitali za serikali licha ya wao kuwa na kadi za NHIF.

Waziri Msaidizi wa Afya Rashid Amana Jumanne aliwaambia wabunge wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Afya kwamba kati ya Sh2.2 bilioni zilizoetengewa mpango huo wa bima ya afya katika mwaka huo wa kifedha, ni Sh636 milioni ambazo Wizara ya Afya iliwasilisha kwa NHIF.

“Katika mwaka wa kifedha wa 2018/2019 wizara haikuwasilisha fedha zote za kufadhili huduma za afya kwa wakongwe kwa NHIF kwa sababu Hazina ya Kitaifa haikutuma fedha za kutosha. Kati ya Sh2.2 bilioni ambazo wizara iliomba ni Sh636,262,500 pekee ziliwasilishwa kwa NHIF,”akasema.

Dkt Amana alikuwa ajibu swali la Mbunge wa Nakuru Mjini Magharibi David Gikaria ambaye alitaka serikali ieleze ni kwa nini serikali ilifeli kuwasilisha fedha za huduma za matibabu kwa wakongozwe kwa NHIF baada ya wao kupewa kadi za bima hiyo.

Bw Gikaria alilalamika kwa wakongwe wengi katika eneo bunge lake hunyimwa huduma afya katika hospital za serikali licha ya wao kuwa na kadi hizo.

“Hata jana (Jumatatu) jumla wazee 17 walifika afisini mwangu wakilalamika kuwa hospitali zimekataa kuwatiba licha ya wao kuwa na kadi za NHIF. Mbona serikali ilito ahadi ambayo hawawezi kutimizia wazee?” akauliza.

Naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Swarup Mishra alipomtaka Dkt Amana kutoa maelezo kuhusu idadi kamili ya wakongwe waliofaidi na sehemu wanakotoka.

“Jibu lako halijaturidhisha kwa sababu haujatueleza ni idadi ya wazee walioonufaika na sehemu wanakotoka ili tujue ikiwa baadhi yao wanatoka eneo bunge lake Mheshimwa Gikaria au la,” akasema Dkt Mishra.

Akijibu Dkt Amana alisema hakuwa na maelezo hayo wakati huo na akaahidi kuyawasilisha kwa kamati hiyo baada ya siku 14 kwa sababu hakuandamana na maafisa wa NHIF.

“Kwa sababu zikuandamana na maafisa wa NHIF naomba kamati hii inipe muda wa siku 14 niweze kurejea hapa na maelezo kamili juhusu namna Sh636 milioni zilitumika na idadi ya wazee waliohudumiwa,” akasema.

BIMA: Wamiliki wa 14 Riverside kuvuna fidia ya Sh400m

Na BERNARDINE MUTANU

WAMILIKI wa jengo la 14 Riverside mtaani Westlands, Nairobi wanatarajia kulipwa Sh400 milioni kama bima kutokana na hasara waliyopata wakati wa shambulizi la kigaidi la Januari 15, lililosababisha vifo vya watu 21.

Fidia hiyo inahusiana na uharibifu wa mali na kupoteza kwa mapato katika jumba lote la 14 Riverside, ikiwemo hoteli ya DusitD2 Hotel.

Wamiliki wa jumba hilo walikuwa wamechukua bima dhidi ya ugaidi na kampuni ya GA Insurance.

“Huwa tunatoa bima ya kupoteza faida vile vile, hasara inayoweza kuwa kubwa zaidi ya kuharibiwa kwa vifaa na majumba,” alisema afisa mkuu mkurugenzi wa GA Insurance Vijay Srivastava katika mahojiano.

“Hasara inayosababishwa na uharibifu wa mali inaweza kuwa sio kubwa sana, lakini baada ya hoteli kufungwa kwa miezi sita, tisa au zaidi, hatujui kabisa, hilo litaongeza kiwango cha hasara kwa sababu tulikuwa tumetoa bima ya kupoteza fidia,” aliongeza.

14 Riverside huwa na biashara tofauti zikiwemo ni pamoja na biashara rejareja, vyombo vya habari na biashara zingine ikiwemo hoteli ya DusitD2.

Hoteli hiyo ilitarajiwa kufunguliwa mapema Juni, lakini tarehe ya kufunguliwa imesongeshwa hadi Agosti, kulingana na habari zilizoko katika tovuti yake.

Hata hivyo, hoteli hiyo bado inapokea maombi kutoka kwa wateja kuwahifadhia vyumba au kumbi.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab lilikiri kuhusika katika shambulizi hilo, ambalo pia liliacha baadhi ya wateja wakiwa na majeraha.

Itikadi zazuia wengi kuchukua bima ya mazishi wakiwa hai

Na MWANDISHI WETU

LICHA ya kauli kuwa kuzaliwa ni bahati kufa ni lazima, jamii nyingi barani Afrika bado hazitaki kujadili wazi uwezekano wa mtu kufa kutokana na itikadi na mila ambazo zimepitwa na wakati.

Baadhi ya jamii nchini bado zinaamini kutaja ama kuwazia kifo ni hatua ya kishirikina au kujitakia mkosi, na ndio maana watu wengi wanaachia jamaa zao mzigo mkubwa wa kuwazika badala ya kujipanga mapema.

Miaka ya hivi karibuni, kampuni za bima humu nchini zimezidi kuongeza bima ya kuwafadhili watu pesa za gharama za mazishi wakati wanapokufa.

Hata hivyo, hatua yao hii imekumbana na kibarua kigumu cha kuwaeliwisha Wakenya umuhimu wa kuchukua bima hii, bila kukinzana na itikadi za jamii nyingi zisizokaribisha mjadala kuhusu uwezekano wa kifo.

Kampuni hizo zinajaribu kuwapigia hesabu Wakenya kuwa pale mtu anapokufa, badala ya kusumbua familia na majirani kwa michango ya pesa ili kufanikisha mazishi, mtu anaweza kuhifadhi pesa kidogokidogo nao kisha pale atakapofariki kampuni itoe pesa za kugharamia mazishi yake.

Hadi sasa, kampuni 22 kati ya 26 za bima zimeongeza bima ya kufadhili gharama za mazishi na matukio ya baada ya kifo kwa jumla, kama mbinu nyingine ya kupanua soko. Bima hizi zinahusisha mtu kugharamiwa malipo ya mochari, kununuliwa jeneza, maua, mipango ya mazishi na chakula.

Japo bima zimepewa majina tofauti kulingana na kampuni na mengine yakiwa ya kuvutia, ujumbe ni mmoja tu, kuwa siku moja utakufa na hivyo unahitaji kuanza kuweka akiba itakayokufaa wakati huo. Kampuni hizo zinaahidi kulipa pesa hizo kati ya saa 48 za kupigwa kwa ripoti kuhusu kifo cha mteja wao.

“Tunafahamu kuwa bidhaa hii ya bima ya kifo bado ina mwendo mrefu hapa Kenya. Lakini angalau imekubalika na ‘Chamas’ kwa ajili ya wanachama wao na hiyo ni ishara njema,” Bw Tom Gitogo, Afisa Mkuu Mtendaji wa CIC Insurance.

Wakenya washauriwa kuchukua bima ya mazishi

Na BERNARDINE MUTANU

WAKENYA wameombwa kuchukua bima ya mazishi ili kuwafaa zaidi wanapopatwa na msiba.

Shirikisho la Watoaji Bima nchini (AKI) Alhamisi lilitoa ushauri huo kutokana na changamoto za kifedha kubwa ambazo ushuhudiwa wakati wa msiba.

“Kwa kutoa Sh100 kwa mwezi, hili ni suluhu ambalo litahakikisha familia haziachwi taabani kifedha zinapompoteza mpendwa,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa AKI, Tom Gichuhi.

Kwa sasa, ni asilimia tatu ya Wakenya ambao wamechukua bima ya mazishi kulingana na utafiti uliofanywa na Ipsos Synovate.

Utafiti huo ulifanywa miongoni mwa makundi 10 Nairobi, Kisii, Kisumu, Nyeri na Bungoma. Ulionyesha kuwa gharama ya mazishi imeendelea kuongezeka.

Walioshiriki walilalamika kuwa mazishi yamefanywa suala la kibiashara ambapo hafla huandaliwa kwa kati ya Sh50, 000 na Sh300, 000.

Familia ambazo huzika wapendwa wao katika kipindi cha siku moja hutumia takriban Sh10, 000.

Wakati marehemu ameaga dunia akiwa hospitalini, familia hutumia kati ya Sh400, 000 na Sh2.5 milioni na kutatiza familia zilizoachwa kifedha.

Amuua mpwa wake ili ajitajirishe na mamilioni ya bima

NA PETER MBURU

MWANAMUME anayetuhumiwa kumuua mpwa yake ili kudai Sh9 milioni kutoka kwa kampuni za bima hatimaye amefikishwa kortini na kufunguliwa mashtaka ya mauaji.

Mshukiwa, Evans Masaku Kasyoki alifikishwa katika mahakama za Kangundo Jumatano, ambako amri ilitolewa apelekwe katika hospitali ya Mathare jijini Nairobi kwanza kupimwa ikiwa yuko timamu.

Mshukiwa atazuiliwa katika jela ya Machakos GK hadi Septemba 17 wakati kesi yake itatajwa, baada ya kunyimwa bondi.

Kushikwa kwake kulijia mwaka mmoja baada ya kisa chake kuchukua bima mbili za maisha kwa mpwa wake ambaye hakuwa na chochote, kupanga mauaji yake na kisha maiti ya marehemu kutupwa eneo la Kangundo kumulikwa.

Baada ya mauaji hayo, mshukiwa anadaiwa kuharakisha kuzidai kampuni za bima malipo.

Mshukiwa, ambaye alikuwa mfanyakazi katika kampuni ya bima alikuwa amemchukulia bima ya Sh10 milioni na Sh1 milioni mpwa wake wa miaka 27 kutoka kwa kampuni mbili tofauti.

Hata hivyo, mauaji ya marehemu yalitokea mwezi mmoja tu baada ya mshukiwa kuanza kulipia bima.

Mnamo Jumapili, runinga ya Citizen ilieleza namna utepetevu miongoni mwa maafisa wa polisi ulisababisha mshukiwa kuachiliwa huru hata baada ya kukamatwa, huku wazazi wa marehemu wakiishi kwa kilio.

Jubilee Insurance kuwapa bima Wakenya wa pato la chini

Na BERNARDINE MUTANI

Kampuni ya bima ya Jubilee Jumatano ilizindua mpango wa bima kwa watu wa mapato ya chini zaidi nchini.

Kampuni hiyo inashirikiana na kampuni ya Bluewave Microfinance kutekeleza mradi huo.

Huduma hiyo, Imarisha Jamii itapatikana kwa njia ya simu na itafadhili bima ya maisha, ajali ya kibinafsi, ulemavu, na bima ya afya ili kusaidia wananchi wa mapato ya chini kuepuka baadhi ya changamoto maishani.

Watakaochukua huduma hiyo watalipa hata Sh20 kwa wiki na wataweza kunufaika kwa kupata pesa za kufadhili matibabu, mazishi na ulemavu hadi Sh100,000.

Pia wataweza kupokea Sh10,000 pesa za kusimamia matibabu wanapolazwa hospitalini siku tatu au zaidi.

Mkurugenzi Mkuu wa Jubilee Holdings Juliua Kipng’etich alisema huduma hiyo itafanya rahisi kulipa ada ya bima(premium) na upokeaji wa malipo kwa sababu inatumia simu.

Huduma hiyo inatarajiwa kugeuza sekta ya bima nchini kwa sababu inalenga mahitaji ya wateja, alisema Bw Kipng’etich.

Hospitali 5,000 kuwahudumia wanafunzi kupitia NHIF

Na CHARLES WASONGA
SERIKALI imetoa orodha ya hospitali ambazo zitawahudumia wanafunzi wa shule za upili chini ya mpango wa bima ya kitaifa ya matibabu (NHIF).
Zaidi ya shule 8,700 zimepewa orodha ya hospitali 5,314 ambazo kwazo walimu wakuu wanapaswa kuchagua kadhaa na kuwasilisha orodha zao kwa makao makuu ya NHIF. Hospitali hizo zinapatikana kote nchini.
“Mwaombwa kutambua hospitali ambayo zitawahudumia wanafunzi wenu kutoka kwa orodha iliyoandamanishwa na taarifa hii. Hizi ndizo hospitali zilizoidhinishwa… na sharti ziwe karibu na shule husika,” akasema Katibu wa Wizara ya Elimu Belio Kipsang’ katika taarifa kwa walimu wakuu wa shule zote za upili za umma iliyotumwa Aprili 26.
Dkt Kipsang’ aliagiza kila mwalimu mkuu kuwasilisha orodha yake kwa matawi ya NHIF kupitia Wakurugenzi wa Elimu katika kaunti.
Hospitali hizo zitawatambua wanafunzi kwa kutumia data ya wanafunzi zilizohifadhiwa katika Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Maelezo kuhusu Elimu (NEMIS) huku zikisubiri NHIF kutayatisha kadi maalum za huduma.
Ili kunufaika kwa huduma ya matibabu chini ya bima hiyo mwanafunzi atahitajika kutoa kazi ya uanachama wa NHIF au barua ya kumtambulisha.
“Wanafunzi watawasilisha barua, za kuwatambua zilizoandikwa na walimu wakuu, kwa hospitali hizo.
Barua hiyo sharti iwe na maelezo yafuatayo: Jina la mwanafunzi, Umri/ Jinsia, Jina la Shule, Nambari ya Usajili na sahihi ya shule. Wanafunzi wataanza kufaidi kwa hudumu hiyo mara moja,” kulingana na mwongozo huo.
Dkt Kipsang’ aliwaambia wanahabari kwamba Wizara yake iko tayari kupokea maoni na mapendekezo yoyote ambayo yanaweza kuimarisha mpango huo.
“Tumejitolea kuona kwamba kila mwanafunzi anafaidi. Na wapata huduma za matibabu chini ya mpango huo hata wakiwa likizoni,” akasema Dkt Kipsang’.
Azma kuu ya wizara hiyo ni kuimarisha viwango vya elimu na kuwapunguzia wazazi gharama ya matibabu.

Mawakili wapinga NHIF kuitisha Wakenya cheti cha ndoa

Na RICHARD MUNGUTI

CHAMA cha wanasheria nchini LSK Jumatatu kiliwasilisha kesi katika mahakama kuu kupinga agizo la bima ya kitaifa ya huduma za afya (NHIF) la kutaka thibitisho la ndoa.

LSK inasema kwamba agizo la NHIF kwamba lazima wawili wathibitishe wamefunga pingu za maisha na wanaishi kama mke na mume kabla ya kunufaika na huduma zake linakaidi na kukandamiza haki za wanachama wake.

Chama hicho kinaomba korti iharamishe agizo hilo kwamba ni ushahidi tu wa afidaviti zilizotayarishwa na mahakimu utakaokubalika kwamba “wawili wameonana na wanaishi kama mke na mume.”

Chama hiki cha kutetea mawakili nchini kimeishtaki NHIF pamoja na mkurugenzi wake mkuu kikidai agizo hilo limepotoka na ukiukaji wa hali ya juu wa haki za wanachama wake wanaolipa ada zao kwa bima hiyo.

“Naomba hii mahakama ifutilie mbali agizo hilo la NHIF la kutaka cheti cha ndoa kuthibitisha mke au mume wamefunga ndoa ndipo wafaidi kwa huduma za bima za NHIF,” anasema kinara wa LSK katika kesi iliyowasilishwa katika mahakama kuu ya Milimani.

LSK inaomba mahakama ifutilie mbali kabisa agizo la NHIF kwamba “haitaki ushahidi wa afidaviti uliopigwa muhuri na wakili kuwa ushahidi wa kutosha kuthibitisha wawili wameoana.”

LSK inasema uamuzi huo wa NHIF umepotoka kabisa na kwamba utamlimbikizia mahakimu kazi ikitiliwa maanani kwamba “kuna mrundiko wa kesi katika baadhi ya mahakama.”

NHIF imesema tu itakubalia cheti cha kufunga ndoa kilichotolewa na maafisa wanaotambulika kisheria kama vile Wasajili wa masuala ya ndoa kutoka afisi ya mwanasheria mkuu, kadhi, mapadri, makasisi au afidaviti zilizotayarishwa na mahakimu kwamba wawili ni mke na mume.

“Ikiwa agizo hili litatekelezwa mawakili watanyimwa kazi,” LSK chasema.

Chama hiki kinasema kwamba afidaviti zinazotayarishwa na mawakili ndizo zinazotumika kama ushahidi kwa wanawake wanaoishi katika sehemu za mashambani kuthibitisha wameolewa.

LSK chasema ikiwa mawakili watanyimwa kazi hii bila shaka mamilioni ya wanawake wanaotegemea afidaviti zao kujaza Fomu za NHIF kutibiwa wataumia na “haki zao zitakandamizwa.”

Korti imeombwa itangaze kwamba uamuzi huo wa NHIF umepotoka na ni ukandamizaji wa hali ya juu wa haki za waliofunga ndoa na hawana vyeti rasmi.

Kwa sasa NHIF inataka wanaopeleka maombi watibiwe ama kurudishiwa pesa awe akitoa ushahidi amefunga ndoa kwa kutoa cheti cha kufunga ndoa rasmi ama afidaviti iliyotayarishwa na hakimu wa mahakama.

Huenda NHIF ikaanza kufadhili huduma zote

Na LUCY KILALO

SERIKALI inafanyia majaribio mpango wa kuhakikisha bima ya kitaifa ya matibabu (NHIF) inashughulikia huduma zote za matibabu.

Waziri wa Afya Sicily Kariuki alisema tayari, mpango huo unafanyiwa majaribio katika Kaunti nne – Nyeri, Machakos, Kisumu na Isiolo.

“Madhumuni ni kuhakikisha kwamba, tunaziba mapengo na kufanya utafiti kuonyesha sehemu zinazohitaji kuboreshwa kwa NHIF,” aliongeza.

Alisema katika muda wa wiki tatu zijazo, serikali italezea ikiwa muda wa kusubiri kusajiliwa kwa NHIF utapunguzwa na kuwezesha Wakenya kupata bima hiyo mara moja.

Wanaojisajili kwa bima hiyo huhitajika kusubiri kwa siku 60 kabla ya kuanza kuitumia. Bi Kariuki alikuwa akijibu maswali kutoka kwa wabunge.

Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Tharaka Nithi, Beatrice Nkatha alikuwa amesema muda huo wa kusubiri siku 60 ni mrefu mno na baadhi wanahitaji kupata huduma hiyo.

“Inawezekana kupunguza muda kutoka siku 60 hadi 30. Lakini suala hilo nimelielekeza kwa bodi ya NHIF kuangalia uwezekano wake,” waziri aliambia kamati, huku afisa mkuu wa NHIF, Bw Geoffrey Mwangi akisema jibu kamili litapatikana katika muda wa majuma matatu.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bi Sabina Chege, alitaka kujua ikiwa bima hiyo inaweza kuimarishwa na kuwa ndiyo pekee inayotoa huduma hiyo nchini.

Hata hivyo, waziri alieleza kuwa wameangalia nchi nyingine kama Thailand na Afrika Kusini, lakini wanalenga kujifunza na kuona jinsi ya kuboresha bima hiyo kulingana na hali ya humu nchini na sio kuiga nyingine moja kwa moja.

 

Usisafiri mbali

Pia akijibu swali la mbunge wa Nakuru Mjini Mashariki, Bw David Gikaria kutaka kuwepo kwa vituo kadha vya usajili wa NHIF kwa wazee wa zaidi ya miaka 60, Bi Kariuki alisema hakuna Mkenya anastahili kusafiri mbali kusajiliwa.

“NHIF ina matawi 62 nchini, matawi 37 madogo pamoja na kupatikana kwa kila kituo cha Huduma. Vile vile, tupo kwa hospitali kadha na hakuna Mkenya anastahili kusafiri mbali kutafuta huduma hiyo,” alisema.

Baadhi ya wanakamati walitaka kujua jinsi Wakenya wanaweza kuhamasishwa zaidi kuhusu bima hiyo, hatua ambayo huenda ikapunguza hafla za uchangishaji pesa wanazolazimika kuhudhuria kila wakati.

Wakati huo huo, mbunge wa Tongaren, Dkt David Eseli aliitahadharisha NHIF kutofuata maagizo ya kisiasa bila kuthibitisha ufaafu wake.

“Mkiamua kufuata maagizo ya kisiasa huenda mkafeli. Lazima muwe na ushahidi kamili kuhusu matokeo yake,” alisema.

Naibu Rais William Ruto alitangaza majuzi kuwa Sh4 bilioni zimetengwa kutoa bima hiyo kwa wanafunzi milioni tatu wa sekondari.

Serikali inatarajiwa kutenga Sh1,999 kwa kila mwanafunzi. Hata hivyo, baadhi ya maswali ibuka ni kuwa wanafunzi hao hudhaminiwa na wazazi wao wanapojisajili kwa bima hiyo.