Hoteli iliyovamiwa na magaidi yauzwa

Na BRIAN OCHARO

MMILIKI wa Hoteli ya Paradise Beach ambayo ilishambuliwa kwa bomu na magaidi wanaohusishwa na Al Qaeda mwaka wa 2002, ameamua kuiuza kutokana na hasara.

Stakabadhi zilizoonwa na Taifa Leo zinaonyesha kuwa hoteli hiyo iliyokuwa ya kifahari inauzwa kwa Sh800 milioni baada ya kupoteza biashara kwa miaka 21 kutokana na uvamizi huo.Hoteli hiyo imejengwa katika ardhi ya ekari 20 eneo la Kikambala, Kaunti ya Kilifi, mita 100 kutoka Bahari ya Hindi.

Hoteli hiyo yenye vitanda 340 ilianza kupata hasara baada ya shambulio la kigaidi lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 13.Katika mahojiano ya awali na Taifa Leo, msamimzi wa hoteli hiyo, Bw Yehuda Sulami alisema hoteli hiyo ilianza kupoteza biashara baada ya kuvamiwa na magaidi.

Bw Sulami ambaye pia ni mwenyekiti wa kampuni ya Simba Group Kenya alisema bomu hilo lilivuruga biashara katika hoteli hiyo ambayo ilitegemea watalii kutoka Israeli, Ujerumani, Ufaransa, Italia na nchi nyingine za Ulaya.’Jitihada za kufufua hoteli hii hazijazaa matunda. Hatuna budi ila tumelazimika kuiuza,’ alisema.

Kwa miaka mingi, usimamizi wa hoteli hiyo umejaribu kufufua biashara hiyo kwa kushawishi watalii wa ndani lakini juhudi hizo hazijafaulu.Kulingana na Bw Sulami, Wazungu waliacha kumiminika katika hoteli hiyo kwa kuhofia kulengwa na magaidi.

Shambulio hilo la kigaidi lilisababisha ndege za kukodisha kutoka Uropa, ambazo zilikuwa zikileta hadi wageni 270 kwa kila ndege, kupunguza kabla ya kusimamisha huduma huku hoteli hiyo ikibaki ikihangaika kutafuta watalii wa ndani.Katika jaribio la kurudisha umaridadi wake, zaidi ya Sh300m zimetumika kuikarabati hoteli hiyo lakini kwa sababu ya ukosefu wa wateja, imebaki mahame.

Hoteli hii ni moja ya hoteli katika eneo la Pwani ambazo zimeteseka kwa sababu ya vitisho vya ugaidi.Wakati hoteli nyingine zimenusurika vitisho na zinajitahidi kubaki katika biashara, hoteli hii inayomilikiwa na raia huyo wa Israeli imeamua kujiondoa kwenye soko la utalii la Kenya.

Shambulio hilo la kigaidi la Al Qaeda la Novemba 28, 2002 lilitokea wakati mshambuliaji wa kujitoa mhanga alipolipua hoteli hiyo na kuwaua Wakenya na wageni wakiwemo raia wa Israeli.

Java yawaomba wafanyakazi wajiuzulu kwa hiari

NA WANGU KANURI

Mkahawa wa Java wenye afisi zake kuu jijini Nairobi umewapa wafanyikazi wake notisi ya kujiuzulu  kwa hiari kabla ya wiki mbili kutamatika. Fomu za kujiuzulu zitakuwepo tayari kwa wafanyikazi hapo Novemba 27, 2020.

Kupitia ilani ambayo iliandikiwa wafanyikazi hao, hoteli hiyo ilisema kuwa hata baada ya vikwazo walivyoweka kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19, mauzo yao yamedidimia ikilinganishwa na mwaka jana.

Imesema kuwa kwa wale ambao watajiuzulu kwa hiari yao watapewa marupurupu yao. Mpango huo utakuwa kwa kila tawi la mkahawa huo haswa kwa wafanyikazi ambao wamefanya kazi kwa miaka minne, wafanyikazi ambao hulipwa kutokana na mauzo na wafanyikazi ambao wamefanya kazi kwa miaka mitatu pamoja na wapishi, wanaboda boda, wahudumu na mabawabu ambao wamefanya kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu.

Vile vile wafanyikazi hao watapokea mshahara wa siku 15 kwa kila mwaka waliofanya kazi na nyongeza ya mshahara wa mwezi mmoja na nusu ili kufidia siku ambazo hawaendi kazini.

Mkahawa huo wa Java ambao una mikahawa 80 katika nchi zilizoko Afrika Mashariki, umetatizika sana tangu corona ilipobisha. Mnamo Aprili, mkahawa huo uliwakata wafanyikazi mshahara kwa asilimia 40 ili kushughulikia matakwa yaliyowekwa na serikali kwa mahoteli.

Kuwepo kwa kafyu nchini kumetatiza saa ambazo hoteli hufungwa kwa kawaida na hilo likapunguza faida.

Wamiliki wa mikahawa walia kuponzwa na corona

Na SAMMY WAWERU

Huku Rais Uhuru Kenyatta akitarajiwa kuhutubia taifa mnamo Alhamisi katika majengo ya bunge, wamiliki wa hoteli wanamsihi kuangazia masaibu yanayozingira sekta hiyo.

Wanalalamikia biashara yao kuendelea kuhangaishwa na makali ya ugonjwa wa Covid-19, wakitakiwa kuhakikisha wametii sheria na mikakati iliyowekwa kuzuia msambao.

Chini ya muda wa majuma kadhaa yaliyopita, visa vya maambukizi ya Homa ya corona vimeonekana kuongezeka mara dufu na kwa kasi, hasa tangu Rais Kenyatta atangaze kulegeza kanuni.

Kufuatia mkurupuko wa awamu ya pili ya corona, Wizara ya Afya ikisisitiza haja ya kuzingatia sheria na mikakati iliyopendekezwa, wamiliki wa mikahawa na hoteli wanasema idadi ya wateja imepungua kwa kiwango kikubwa.

Kutokana na idadi ya juu ya wagonjwa wanaoandikishwa kila siku, wamiliki wa hoteli eneo la Zimmerman tuliozungumza nao wanasema kiwango cha wateja kimeanza kushuk,a hali inayochangia kuathirika kwa biashara zao.

“Kwa muda wa wiki mbili mfululizo, kiwango cha wateja kimekuwa kikishuka. Kwa sasa idadi ya tunaohudumia ni chini ya nusu ya tuliokuwa tukipokea Rais alipotangaza kulegeza sheria kuzuia kuenea kwa corona,” akalalamika mmiliki wa Corner Cafe.

Kwenye hotuba yake kwa taifa juma lililopita, Rais alitathmini saa za kufungwa kwa mikahawa, hoteli na vituo vya kuchuuza vyakula, na pia mabaa akitaka maeneo hayo kufungwa saa tatu jioni.

“Tunamuomba baada ya kutangaza kukaza kamba sheria alizolegeza angalau atengee sekta ya hoteli mgao wa fedha kuikwamua kwa sababu wengi wetu tunaelekea kufunga mikahawa,” akasihi mmiliki wa Planet Classic Hotel.

Wamiliki na wahudumu tuliozungumza nao wanasema ongezeko la visa vinavyoandikishwa kila siku, limesababisha wateja kupunguza ari ya kutafuta huduma za mikahawa.

Ombi la wamiliki hao kwa Rais Kenyatta linajiri wakati ambapo serikali inafanya msako mkali katika hoteli, mikahawa, mabaa na maeneo ya burudani yanayokiuka sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kudhibiti msambao wa corona.

Corona ilitufungua macho, sasa tunavuna maelfu kwa biashara yetu

NA RICHARD MAOSI

Mlipuko wa janga la corona umekuja na changamoto si haba, huku idadi kubwa ya watu wanaokaa mijini,wakipoteza ajira, wengi wao wakiwa ni wafanyibiashara.

Sekta ya utalii ilisalia kuzorota, baada ya serikali kuifunga nchi kwa miezi minne. Wanafunzi wa vyuo na taasisi za kiufundi nao waliamua kurudi mashambani ama kuajiriwa kama vibarua mitaani , na kupokea malipo duni.

Lakini kwa Mary Wambui na Eunice Muthoni, pacha wa toka nitoke ambao ni wakazi wa eneo la Uthiru, Kaunti ya Nairobi, pamoja na dada yao mkubwa Ruth Wanjira, walitumia mwanya huo kufikiria jinsi ya kujikimu maishani na kujianzishia kazi ya kuuza chakula mtaani humo.

Eunice anasema walianza kazi yenyewe mnamo Machi 2020, baada ya taasisi wanayosomea kufungwa, ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kurudi nyumbani wakati wa virusi vya covid-19.

Haikuchukua muda na walipochoka kukaa nyumbani, walijadiliana kisha wakafanya utafiti wa kina wakilenga kutambua kazi ambayo ingewasaidia kujipatia kipato.

“Awali tukiwa shuleni tulikuwa na wazo la kujianzishia biashara, lakini hatukua tumeamua ni aina gani ya kazi ambayo ingefanya vyema katika eneo hili,” akasema.

Eunice na Mary wamesomea taaluma ya kuandaa vyakula katika taasisi ya PC (Paramount Chief) Kinyanjui, Nairobi.

Anasema walianzisha mradi huu kwa mtaji wa 50,000, hela ambazo zilikuwa ni akiba yao, pamoja na mchango kutoka kwa jamaa zake.

Akiba hii iliwasaidia kununua sufuria, mashine ya kupika vinanzi (chips), mashine ya kupasha joto chakula na vyombo vya kupikia na kupakulia. Aidha hela zingine zilienda kulipa kodi na kulipia umeme.

Eunice akimhudumia mteja katika mkahawa wao eneo la Uthiru, Nairobi. PICHA/ RICHARD MAOSI

Kutokana na soko la uhakika, walianza kuwauzia chakula wafanyibiashara, mafundi , waendeshaji boda na wahandisi wanaotengeneza magari katika eneo la Uthiru.

Ruth tayari alikuwa na uzoefu na tajriba katika sekta ya uuzaji chakula, na hilo lilikuwa chocheo kwa kunawiri kwa biashara hiyo licha ya ushindani kutoka kwa wawekezaji wengine.

“Nilielewa kuvutia wateja wapya kunahitaji chakula kilichoandaliwa kwa ustadi wa juu, kuwahudumia wateja kwa moyo wa kujitolea, kuimarisha usafi katika hoteli na kuhakikisha bei inalingana na mifuko yao,” Ruth aliambia Taifa Leo Dijitali.

Eunice anasema aghalabu wao huagiza chakula kutoka kaunti jirani za Nyahururu, Kiambu na Muranga, ambapo wao huandaa pilau, vibanzi,wali, viazi, chapati, chai, mahamri na lishe za kienyeji.

Kwa siku moja wanaweza kutengeneza Sh5000, ila wakati mwingine mapato hupungua hadi Sh3000 kulingana na idadi ya wateja wanaozuru mkahawa wao.

“Tukiondoa pesa za matumizi kwa siku tunaweza kutenga Sh2000 kama akiba, hesabu ambayo sio chini ya Sh6000 kwa mwezi,”alisema.

Wakazi wa mtaa huu hufurika katika mkahawa huu kwa staftahi na maankuli. PICHA/ RICHARD MAOSI

Kutokana na juhudi zao mabinti hawa wanasema, ni faida ambayo itawasaidia kupanua biashara yao siku za mbeleni na kuwaboreshea wateja huduma.

Hii ndio sababu Eunice anawaomba vijana kuiga mfano wake bila kuchagua ajira, kwa sababi kazi ni kazi muradi inaweza kukidhi mahitaji ya kila siku.

Anasema baadhi ya vijana hususan akina dada wanapenda kutumia njia ya mkato, kutafuta pesa badala ya kutumia hekima na bidii.

“Wengi wa vijana katika mtaa huu wamezoea vya bwerere, hawataki kutoa jasho. Wengi pia wamezamia katika uraibu wa dawa za kulevya na ulevi chakari. Vijana wanafaa kutumia fursa ndogo waliyo nayo kujijenga. Ni aibu kumwitisha mzazi wako hela kila mara, na alikusomesha,” anasema Mary.

Aidha anaomba serikali kuwekeza katika nguvu kazi ya vijana na kutoa mazingira mwafaka ya kufanyia biashara , mbali na kutoa mtaji wa kujianzishia biashara

Changamoto

Licha ya kutengeneza hela nzuri, Mary anasema hakuna kizuri kisichokuwa na doa maana mwezi mmoja tu baada ya kuanza biashara wezi walivunja mkahawa wao na kuiba vyombo vya zaidi ya Sh15,000.

Kutoka kushoto: Ruth Wanjira, Eunice Muthoni na Mary Wambui ambao wamewekeza kwa mkahawa kwa jina Quick Stop Cafe mtaani Uthiru, Nairobi. PICHA/ RICHARD MAOSI

Ingawa walivunjika moyo mama yao aliwatia moyo na kuwahimiza waendelee na biashara.”Hiyo ni kawaida ya biashara kwani ni lazima mtu kupata faida na wakati mwingine hasara,”alisema.

“Ni pigo ambalo lilituongezea hekima, ndiposa tukaaimarisha ulinzi kwa kuweka langoni kufuli inayofaa na kuweka camera za CCTV, kufuatilia mienendo ya watu wanaoingia na kutoka.”

Mary aliongezea kuwa chakula kinapobaki, wao hulazimika kukiuza kwa bei nafuu ama kuwapatia majirani.Hii ilikuwa ikitendeka siku za awali kabla hawajajifundisha namna ya kupima chakula.

Pia wakati mwingine wanakumbana na ushindani mkali kutoka kwa watu wanaochuuza chakula cha bei rahisi, wasiozingatia kanuni za Wizara ya Afya.

Sababu ya hoteli za Norfolk kufunga biashara Kenya

NA ADONIJAH OCHIENG

Kampuni ya hoteli za Fairmont Norfork Nairobi imetangaza kufungwa kwake kwa ghafla na kuwafuta wafanyakazi wote kutokana na kuzorota kwa biashara kuliosababishwa na mikakati hasi iliyowekwa kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Kulingana na barua aliyotoa meneja wa hoteli hizo Mehdi Morad ya Mei 27, kutokuwa na uhakika kuhusu mkondo utakaochukuliwa na sekta ya hoteli katika janga hili la corona kumelazimisha kukatisha mikataba yao na wafanyakazi.

Wafanyakazi watapokea barua zao za kutamatisha huduma zao kufikia Juni 5. Hoteli nyingi za kifarahi zinazotegemea utalii na makongamano kupata faida zinapitia wakati mgumu wakati huu wa janga la corona.

Mwezi Machi  hoteli za Nairobi kama vile Ole Sereni, Tribe Hotels na Dusit D2 zilisimamisha shughuli zake serekali ilipoweka mikakati ya kutotangamana na kusimamisha usafiri ili kuzuia kusambaa kwa corona.

Amri ya kutotoka au kuingia nchini imeathiri sana sekta ya utalii iliyoletea nchi Sh163.56 milioni mwaka uliopita.

COVID-19: Serikali kulipia upimaji wa wahudumu wa hoteli

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imewaondolea waamiliki ya mikahawa na hoteli mzigo kwa kutangaza italipia gharama ya wafanyakazi wao kupimwa virusi vya corona kabla ya wao kuruhusiwa kurejea kazini.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Afya Dkt Patrick Amoth ameongeza kuwa serikali pia ndiyo inagharimia mpango unaoendelea sasa wa kuwapima madereva wa matrela katika mipaka ya Kenya na mataifa jirani, kubaini ikiwa wanavirusi vya corona.

“Ningependa kuwahakikishia wamiliki ya wa mikahawa na hoteli kwamba serikali italipia gharama ya kupimwa kwa wafanyakazi wao. Hii ni kwa sababu serikali ndio imetangaza kufunguliwa kwa biashara hizo, japo kwa kufuata mwongozo mpya uliotangazwa na Wizara ya Afya wa ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona,” Dkt Amoth akasema kwenye mahojiano na runinga ya Citizen Jumatatu usiku.

Afisa huyo alishauri watu wanaotaka kupimwa virusi vya corona kutembelea vituo vya Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu Nchini (KEMRI), Nairobi na Kisumu, National Influenza Centre, Nairobi, Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH), Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) Eldoret na Hospitali ya Rufaa ya Pwani na ile ya Nyeri.

“Vile vile, huduma za kupima washukiwa wa Covid-19 vinapatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Wajir ambayo itahudumia eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya,” Dkt Amoth akaongeza.

Saa chache baada ya serikali kutangaza kuwa itaruhusu kufunguliwa kwa mikahawa na hoteli mradi wamiliki wazingatie masharti kadha ikiwemo kupimwa kwa wafanyakazi wao, baadhi ya wamiliki wa biashara hiyo mjini Nakuru walilalamikia gharama ya juu ya huduma hiyo.

Mnamo Jumatatu Nairobi Hospitali ilitangaza kuwa itaanza kutoa huduma za kupima virusi vya corona lakini kwa gharama ya Sh10,000.

Wakati huo huo, Dkt Amoth ameelezea matumaini kuwa kero la msongamano ya matrela kutokana na kucheleweshwa kwa shughuli za kuwapima wahudumu, litapungua wiki hii baada ya serikali kupokea vifaa 40,000 vya kuendesha shughuli hiyo.

CORONA: Mshubiri kwa hoteli za kifahari

MARGARET MAINA NA RICHARD MAOSI

Tangu Waziri wa Afya Mutahi Kagwe atangaze kisa cha kwanza cha Covid -19 nchini, kulizuka tumbojoto miongoni mwa wamiliki wa mikahawa na maduka ya kuuza bidhaa kwa bei ya kijumla.

Wauzaji wengi hatimaye walliamua kujaza akiba ya vyakula, maji na vyombo vya usalama kwa ajili ya ongezeko la mahitaji ya vifaa hivi kwa wanunuzi.

Hali ni kama hiyo katika mkahawa wa kifahari wa ALPS, eneo la Milimani Nakuru, ambapo Taifa Leo ilibaini ni marufuku kuchukua hela mkononi.

Wakati wa mahojiano haya sehemu ya kuegesha magari ilikuwa tupu, vyumba vya malazi havikuwa vimepata wageni katika mkahawa huo ambao una vyumba 35, na sehemu ya kuogelea pembeni.

Meneja mkuu John Kiruthi anasema mkahawa wa Alps unadumisha usafi wa hali ya juu, wafanyikazi wakishauriwa kusafisha kila mahali, ili kutoa hakikisho kwa wageni na wenyeji.

“Tumekadiria hasara kubwa ikizingatiwa tunamiliki matawi mawili ya wafanyikazi 180, wanaoshughulika Nakuru na KCB Leadership Centre Nairobi,”akasema.

Wakati wa mazungumzo haya Kiruthi anasema alikuwa amefutilia mbali safari ya watalii kutoka Ujerumani, ambao wangetoa milioni tano kugfharamia malazi na vyakula.Isitoshe idadi ya watalii wanaoingia Nakuru imepungua.

“Tumeweka mikakati kuhakikisha wafanyikazi wetu wanaendesha shughuli katika mazingira safi kwa kuwahimiza wavalie vifaa vya kuziba mapua na kupima viwango vya joto mwilini kila mara,”akasema.

Kiruthi anawashauri wamiliki wa mikahawa mingine kuwa tayari kukabiliana na mkurupuko wa Corona, ambao kufikia sasa ni visa nne vimeripotiwa na serikali.

“Vyakula vyetu huandaliwa vyema na kuhifadhiwa ndani ya majokofu, ili wanunuzi wasipate matatizo ya kiafya yanayoweza kutokana na chakula kibovu,”aliongezea.

Wauzaji wa chakula cha kuzungusha, baa na sehemu za burudani wakionekana kupata pigo zaidi, wengi wao wameona ni afadhali wabakie majumbani pao badala ya kutangamana kwenye kumbi za starehe.

Bi Josephine Obote wa Aramatose Restaurant amekuwa akifanya kazi ya kuzungusha chakula, ndani ya benki na ofisi lakini sasa anaona italazimika afunge kazi kwa sababu sehemu za kazi zimebakia kuwa mahame.

“Nimeajiri vijana watano na pia ninalipia umeme na kodi ya nyumba, aidha ninagharamika kununua vyombo vya kudumisha usafi kama sabuni ya Dettol na huenda hivi karibuni nitafunganya virago, hususan tangu serikali itoe agizo la wafanyikazi kuchapa kazi kutoka nyumbani,”akasema.

Hatua chache kutoka hapo, tunakumbana na Leonard Kamau anayefanya kazi katikati ya mji wa Nakuru. Leonard anamiliki mikahawa mitatu katika barabara ya Kenyatta, anasema amekadiria hasara kuanzia siku tatu zilizopita.

“Tunapoteza wateja kila siku, ikizingatiwa kuwa mimi huagiza vyombo vyangu kutoka China ili kuendesha shughuli ya kutengeneza juisi ya matunda na meko za kisasa kupikia chakula,kwa idadi kubwa ya wateja”akasema.

Aliongezea kuwa tangu weita waanze kuvalia glavu na vifaa vya kujifunika usoni, baadhi ya wateja walianza kujawa na wasiwasi wakatoweka na kukwamisha shughuli.

Wachuuzi wanaomiliki mikahawa midogo midogo wanalazimika kumwaga chakula kila siku, huku baadhi ya wateja wakiamua kula chakula kutoka makwao.

Wateja kadhaa waliokubali kuzungumza na Taifa Leo wanasema wanaogopa kushika sahani, vikombe au kutangamana na walaji wengine wakihofia kuambukizwa virusi vya Corona.

Wengine waliopata pigo ni wauzaji matunda na samaki. Kulingana nao wanasema wateja wamekataa kutembelea vibanda vyao kufuatia tishia la Covid -19.

Kwingineko George Kihara meneja katika klabu maarufu ya SEBS, Nakuru anasema, ameshangaa kuona jinsi mambo yamebadilika kwa haraka, wateja wamepungua kuhudhuria matamasha katika mkahawa wao.

“Tumeweka mikakati yote kuhakikisha wanunuzi wetu ni salama lakini bado hali ya biashara ni mbaya,na huenda ikachukua muda kabla ya hali ya kawaida kurejea,” aliongezea.

Hoteli ya Hemingways yajumuishwa kwenye mpango wa hoteli za hadhi

Na WANDERI KAMAU

HOTELI ya Hemingways jijini Nairobi, imejiunga na mpango maalum wa Hoteli za Hadhi ya Juu nchini Amerika, maarufu kama ‘AmEx Fine Hotels and Resorts Program‘.

Hoteli hiyo ndiyo ya pekee nchini Kenya kujiunga na mpango huo.

Mpango unashirikisha zaidi ya hoteli 1,000 kote duniani.

Chini ya mpango huo, wanachama huwa wanapata manufaa mengi, baadhi yakiwa pointi na zawadi maalum.

Mkurugenzi Mkuu wa Shughuli katika hoteli hiyo Bw Ross Evans, alisema kwamba hatua hiyo ni dhihirisho la ubora wa huduma ambazo huwa wanatoa.

“Kukubaliwa kwetu kujiunga na Mpango wa Hoteli za Hadhi ya Juu nchini Amerika ni ishara kwamba huduma zetu ni za kipekee na za hadhi ya juu,” akasema Bw Evans.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa wateja ambao wana kadi maalum za hoteli zilizo kwenye mpango huo, watafaidika pakubwa kwa kupewa huduma za kipekee popote walipo duniani.

Manufaa mengine wanayopata ni muda wa kutosha wa kuingia na kutoka, vyumba vya hadhi ya juu na Sh10,000 za kugharimia vyakula na vinywaji.

“Tunafurahia sana kuwa hoteli ya pekee nchini kukubaliwa kwenye mpango huu. Hilo pia litaimarisha nafasi ya Kenya kama kivutio cha watalii duniani,” akasema.

Ili hoteli husika kukubaliwa kwenye mpango huo, huwa inatuma ombi maalum, ambalo baadaye hukaguliwa kwa kina.

Ukaguzi huwa unaikagua hoteli hiyo ikiwa imetimiza viwango vinavyohitajika, kabla ya kukubaliwa.

Kando na Nairobi, hoteli hiyo ina matawi mengine katika maeneo ya Mara na Watamu.

Wachina waliochapa Mkenya mijeledi kuadhibiwa vikali na serikali

Na LEONARD ONYANGO

POLISI wamekamata raia wanne wa China kuhusiana na video iliyochipuka mtandaoni ikionyesha Mchina akichapa viboko Mkenya katika hoteli ya Chez Wou iliyoko mtaa wa Kileleshwa, Nairobi.

Maafisa kutoka Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) walisema kuwa Wachina hao walimakatwa baada ya kufanya uchunguzi kuhusiana na video hiyo ambayo imezua imewakera Wakenya.

Maafisa wa DCI walivamia hoteli hiyo jana na kuwanasa Deng Hailan, raia wa China ambaye anafanyakazi hotelini hapo, wapishi Chang Yueping, na Ou Qiang, na Yu Ling ambaye ni keshia.

Kulingana na DCI, Deng hana kibali cha kufanya kazi humu nchini.Chang Yueping na Ou Qiang wana viza zilizopitwa na wakati. Chang ana kibali cha kufanya kazi humu nchini lakini mwenzake hana, kwa mujibu wa DCI.

Yu Ling ambaye ni keshia ana viza ya wageni lakini hana kibali cha kufanya kazi humu nchini.“Kufuatia ripoti kuhusu mwanaume raia wa China aliyeonekana akimchapa mfanyakazi wa kiume, maafisa wa polisi kutoka Kituo cha Kilimani Jumapili walivamia hoteli ya Chez Wou mtaani Kileleshwa,” ikasema idara ya DCI.

Wakenya wanane wanaotekeleza majukumu mbalimbali hotelini hapo walipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kilimani kuhojiwa.

Katika video hiyo, mwanaume wa Kichina anayeaminika kuwa Deng, anaonekana akiagiza Mkenya, anayedaiwa kuwa mhudumu hotelini hapo, kulala kifudifudi.

Mchina huyo amesimama kando huku akishikilia kiboko. Mwathiriwa analala chini na Mchina anamtandika viboko huku wenzake wakimtazama kutoka mbali.Mchina anasikika akimuuliza mwathiriwa sehemu ya mwili anayotaka kuchapwa.

Mkenya huyo alichapwa ubavuni na anaonekana akiwa mwenye maumivu. Mwathiriwa baadaye aliripoti dhuluma hizo katika Kituo cha Polisi cha Mlimani hivyo maafisa wa polisi wakaanzisha uchunguzi.Washukiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.

Mwaka jana, raia watatu wa China walikamatwa baada ya kupatikana wakiuza nyama ya mbwana wanyama wa porini kama vile kobe.

Washukiwa pia walikuwa na pembe za ndovu.Mnamo 2018, serikali ilimrejesha Mchina kwao baada ya kuwaita Wakenya nyani.

Mchina huyo Liu Jiaqi alitoa kauli hiyo ya ubaguzi wa rangi baada ya kuzozana na mmoja wa wafanyakazi katika kampuni moja iliyoko katika eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Hoteli Kisumu zavuna matunda ya muafaka kwenye ziara ya Rais

Na ELIZABETH OJINA-250

MIKAHAWA ya kifahari jijini Kisumu imevuna pakubwa kutokana na ziara ya Rais Uhuru Kenyatta kuzindua mpango wa Afya kwa Wote hapo Alhamisi.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Rais Kenyatta kuzuru kaunti hiyo baada ya kuingia kwa muafaka baina yake na kiongozi wa upinzani Bw Raila Odinga, ambao wamiliki wa hoteli walikiri umewaletea mapeni.

Kulingana na mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Hoteli wa Magharibi mwa Kenya  Bw Robinson Anyal, hoteli kama Acacia, Imperial na Sovereign zilijaa wateja.

“Hoteli kuu tatu zimejaa. Acacia ina vitanda 91, Imperial 80 na Sovereign 40. Paliposalia na nafasi labda ni Grand Royal Swiss Hotel,” akaambia Taifa Leo.

Aliongeza, “Kando na malazi katika Hoteli ya Acacia, biashara ya vyakula imenoga. Tunatarajia mikahawa mingine hapa jijini kushuhudia kuongezeka kwa mapato.”

Alisema ziara ya Rais itafungua nafasi za biashara kwa mikahawa kama Kakwacha, Tilapia Resort na mikahawa mingine inayouza samaki eneo la ufuo wa Lwang’.

“Biashara ya teksi pia itaendelea kuvutia wateja katika siku mbili zijazo kufuatia ziara ya Rais,” akasema.

Alikariri kuwa ziara hiyo inapiga jeki biashara ya hoteli, huku nyingi zikitamatisha  biashara ya kukodisha maeneo ya hotuba.

“Ziara ya Rais ni hakikisho kuu kwamba jiji la Kisumu li salama. Biashara ya kumbi za hotuba inaendelea kutamatika. Hoteli nyingi zinategemea watalii wa humu nchini,” akasema.

Meneja wa Hoteli ya Acacia Duncan Mwangi alisema hoteli hiyo ilipata wateja wengi zaidi wiki hii kutokana na ziara hiyo.

“Ziara ya Rais imeleta imani kuu na kuyeyusha hisia na fikra potovu ambazo watu wamekuwa nazo kuhusu Kisumu. Tunatarajia kuwa itaimarisha utalii wetu. Kwa hakika, muafaka wa Bw Kenyatta na Bw Raila umezaa matunda,” akasema.

Mbunge na mumewe watimuliwa gesti kwa kukosa cheti cha ndoa

Na ANITA CHEPKOECH

MBUNGE Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Laikipia, Bi Catherine Waruguru na mumewe, mnamo Jumamosi walifukuzwa katika hoteli moja mjini Kericho kwa kukosa kuonyesha cheti chao cha ndoa.

Mumewe Bw Kiprotich Kiget alikuwa amekodisha chumba cha malazi mwendo wa saa kumi jioni katika gesti ya Sunshine kabla ya kuelekea kwao mashambani..

Lakini waliporudi hotelini mwendo wa saa tatu unusu za usiku, wasimamizi waliwakataza kuingia chumbani hadi watoa cheti cha kuonyesha wao ni mume na mke.

Hata juhudi za wabunge watatu wa eneo hilo kupigia simu wasimamizi hao wakiwahakikishia wawili hao ni wanandoa hazikuwafanya kubadili msimamo. Iliwabidi kutafuta hoteli nyingine.

Lakini wasimamizi wa hoteli hiyo walijitetea wakisema walikuwa na haki ya kukataa kuwapa wawili hao chumba cha kulala na ni sheria kwa hoteli hiyo kutoruhusu mwanamume na mwanamke ambao hawajaoana kulala chumba kimoja.

 

Serikali yajiondoa kwa biashara ya hoteli

Na BERNARDINE MUTANU

Serikali imeanza mikakati ya kuuza hisa zake katika hoteli kubwa za kifahari nchini.

Hoteli hizo ni InterContinental, Hilton na Mountain Lodge. Tume ya kubinafsisha inatafuta wataalamu kufanyia hoteli hizo uchunguzi na hoteli zingine ndogo kwa lengo la kuziuzia wawekezaji wa kibinafsi.

Tume hiyo hata hivyo haikuelezea pesa inazotarajia kupata kutoka kwa mauzo ya hoteli hizo.

Wachunguzi hao wanatarajiwa kubainisha hali ya kifedha ya hoteli hizo na kutayarisha kandarasi ikiwemo ni pamoja na mikataba ya kuhawalisha hisa hizo.

Mauzo ya hoteli hizo yalitangazwa mara ya kwanza 2011 kama sehemu ya kuimarisha mapato ya serikali.

Serikali ina hisa 40.57 katika Mahoteli ya Intercontinental yanayomiliki Hoteli ya Hilton.

Inalenga kutoa asilimia 33.83 ya hisa zake kwa Kenya Hotel Properties Limited ambayo inasimamia InterContinental na asilimi 39.11 inazomiliki katika Hoteli ya Mountain Lodge, chini ya usimamizi wa TPS Serena.

Hoteli motoni kwa kuzuia mwanamke kunyonyesha

Na BENSON MATHEKA

WANAWAKE jijini Nairobi, wanatarajiwa kuandamana kesho kufuatia ripoti kwamba mama mmoja alifurushwa kutoka hotelini kwa sababu ya kumnyonyesha mtoto.

Kundi la Pregnant and Nursing Mums Kenya, limesisitiza kuwa litaongoza maandamano hayo licha ya wasimamizi wa hoteli ya Olives iliyoko barabara ya Accra, katikati ya jiji kusema haijapokea malalamishi yoyote kuhusu kisa hicho.

Kulingana na Bi Wanjeri Nderi, anayeshirikisha maandamano hayo, visa vya wanawake kudhulumiwa kwa sababu ya kunyonyesha vimeongezeka nchini.

“Hii sio mara ya kwanza wanawake wanaonyonyesha kunyanyaswa wakiwa maeneo ya umma. Wamefukuzwa au kukatazwa kunyonyesha wakiwa katika benki na mashirika mengine,” Bi Wanjeri aliambia tovuti ya NairobiNews.

Alisema wanawake wataandamana kutoka Freedom Corner hadi hoteli ya Olives kuonyesha ghadhabu zao.

Mwanamke aliyetambuliwa kama Betty Kim, 26, alidai kwenye Facebook kwamba alifukuzwa na wahudumu wa hoteli hiyo mnamo Mei 7 kwa kumnyonyesha mtoto wake. Wanawake walikasirishwa na tukio hilo wakilitaja kama dhuluma na dharau kwa wanawake.

Hata hivyo, hoteli hiyo iliwataka wanawake na wateja wake kuwa watulivu ikisema inaendelea kufanya uchunguzi ili kutatua suala hilo.

Kwenye taarifa, hoteli hiyo ilisema kuwa ilifahamu tukio hilo kupitia mitandao ya kijamii na kumtaka mama aliyetoa madai hayo kujitokeza kuwasilisha malalamiko rasmi.

Ilisema kwamba ina haki zake kama biashara ikiwa ni pamoja na kupatiwa nafasi ya kuchukua hatua za kinidhamu kwa wafanyakazi waliohusika iwapo mwanamke huyo atawasilisha malalamiko yake rasmi.

Mwanamke huyo alidai kwamba wahudumu wa hoteli hiyo walimkabili alipoanza kumnyonyesha mtoto japo alikuwa akisubiri chakula alichoagiza.

“Nilikuwa nikisubiri chakula wakati mhudumu mwanamke aliponikabili kwa dharau na kuniambia niache kumnyonyesha mtoto au nijifunike,” mwanamke huyo alisema.

Alisema alishangaa kwa sababu haikuwa mara yake ya kwanza kufanya hivyo na ulikuwa wakati wa mvua.

Mhudumu mwingine alimwendea na kumwambia kwamba alikuwa akifanya kitendo kisichofaa na alipomuuliza alikofaa kwenda kumnyonyeshea mtoto, alimwelekeza chooni. “ Alipofanya hivyo, nilihisi kudharauliwa na nikaacha kumnyonyesha mtoto,” alieleza.

Kulingana na bango lililosambazwa kwenye mitandao, maandamano yataanza Freedom Corner kupitia barabara ya Parliament hadi Olive Restaurant.

 

Gor Mahia kortini kwa kukataa kuilipa hoteli

Na JOSEPH OPENDA

KLABU ya Gor Mahia huenda ikaadhibiwa na mahakama kwa kukataa kulipa deni, baada ya kupokea huduma za hoteli moja mjini Nakuru.

Mahakama ya Nakuru imewataka maafisa wanne wa klabu hiyo kufika mbele ya korti ili kueleza sababu za kutotii amri ya mahakama iliyowataka kulipa kampuni ya Donnies Bar and Hotel Sh524,730 ambazo ni sehemu ya deni baada ya kupata huduma zake.

Maafisa hao wakiongozwa na mwenyekiti Ambrose Rachier, John Pesa, Ronald Ngala na Jolawi Obongo na Kennedy Otieno, walishtakiwa kwa niaba ya klabu hiyo baada ya kususia kukamilisha deni hilo.

Hoteli ya Donnies kupitia kwa wakili wake, Bw Gordon Ogolla, iliishutumu Gor Mahia kwa kukataa kuheshimu mkataba waliokubaliana kuhusu kulipia huduma zake.

Kulingana na karatasi zilizoko kortini, hoteli ya Donnies ilikubaliana na klabu hiyo kupokea malipo kwa awamu Sh737,080 kwa huduma watakazopata mnamo Januari 15, 2015.

Aidha korti iliambiwa kwamba klabu hiyo ililipa Sh300,000 pekee kisha ikakataa kukamilisha deni lililokuwa limebaki.

Mnamo Juni 2017, korti iliamuru maafisa hao kukamilisha deni hilo.

Wenye hoteli hiyo walirudi kortini kutaka klabu hiyo iadhibiwe kwa kukosa kutii amri ya mahakama.

“Unahitajika kufika mbele ya korti hii mnamo Aprili 17 kueleza korti sababu zinazoweza kufanya msiadhibiwe,” ilisoma sehemu ya amri hiyo.