• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Huzuni 1 akiuawa na nyumba 10 kuteketezwa moto kwenye shambulio la Al-Shabaab Lamu

Huzuni 1 akiuawa na nyumba 10 kuteketezwa moto kwenye shambulio la Al-Shabaab Lamu

NA KALUME KAZUNGU

MTU mmoja ameuawa na nyumba 10 kuteketezwa moto baada ya washukiwa wa kundi linaloaminikiwa kuwa Al-Shabaab kuvamia vijiji vya Marafa na Poromoko, katika Kaunti ya Lamu, Jumamosi usiku, Novemba 25, 2023.

Walioshuhudia walisema kundi la magaidi wapatao 30 waliojihami kwa silaha hatari, ikiwemo bunduki na visu, walivamia vijiji hivyo majira ya saa tatu usiku, ambapo waliingia kila boma, huku wakichoma nyumba, kuchinja kuku na mbuzi na kuiba vyakula; unga, mahindi na vinginevyo.

Maafisa wa usalama waliozungumza na Taifa Leo Dijitali, japo waliomba kubana majina yao, walithibitisha mauaji ya mkazi huyo, na uharibifu wa mali uliotekelezwa na magaidi hao kabla ya kutokomea msitu wa Boni.

Aliyeuawa alitambuliwa kama John Thuo mwenye umri wa miaka 72 ambaye alikatwa shingo.

“Ni kweli. Magaidi wamevamia Poromoko na Marafa usiku wa Jumamosi. Katika eneo la Poromoko, walichoma nyumba sita na Marafa wakaua mzee wa miaka 72 na kuteketeza nyumba nne. Maafisa wetu tayari wamefika maeneo husika kudhibiti usalama na kusaka magaidi waliotorokea mafichoni Msituni Boni. Mwili wa mwendazake umehifadhiwa kwenye makafani ya hospitali ya Mpeketoni,” akasema mmoja wa maafisa wa ngazi za juu wa usalama Lamu.

Kufuatia tukio hilo, taharuki imetanda Poromoko, Marafa na viunga vyake, wakazi wakiililia serikali kudhibiti usalama maeneo hayo.

Ikumbukwe kuwa mauaji na uchomaji nyumba uliotekelezwa Jumamosi usiku unajiri wakati ambapo zaidi ya familia 100 bado zinaendelea kuishi kwenye kambi ya wakimbizi katika Shule ya Msingi ya Juhudi, Lamu Magharibi.

Mauaji ya Jumamosi pia yanajiri miezi mitatu baada ya mwanamume mmoja kuuawa kwa kuchinjwa eneo la Widho-Mashambani, Lamu Magharibi.

Nyumba saba pia zilichomwa wakati wa shambulio hilo la Septemba 20, 2023.

Kaunti ya Lamu mwaka huu (2023) imekumbwa na mashambulizi na mauaji ya Al-Shabaab ambayo yameacha watu zaidi ya 30, wakiwemo walinda usalama na raia kuuawa, huku nyumba zaidi ya 20 na kanisa zikiteketezwa.

Vijiji vilivyoathithiriwa zaidi na mashambulio hayo ni Juhudi, Salama, Widho, Mlima Faru, Pandanguo, Nyongoro na Lango la Simba Kaunti Ndogo ya Lamu Magharibi.

Lamu Mashariki, maeneo yaliyoshuhudia uvamizi na mauaji ni Bodhei, Baure, Milimani, Sankuri na sehemu nyingine za Msitu wa Boni.

  • Tags

You can share this post!

Kaunti kuvuna Ripoti ya Kamati ya Mazungumzo ikipendekeza...

Ruto asema serikali itaanza kukopa mama mboga na wahudumu...

T L