Wakili Karim Khan kujiondoa kwenye kesi ya Ruto ICC

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Bi Fatou Bansouda, ametangaza kuwa wakili Karim Khan atakayechukua nafasi yake Juni atahitajika kutoshiriki katika kesi ambazo aliwahi kuwakilisha washtakiwa akiwa wakili.

Bw Khan alipata umaarufu humu nchini alipoongoza kikundi cha mawakili ambao walimwakilisha Naibu Rais, Dkt William Ruto aliyeandamwa na mashtaka kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Ijapokuwa kesi ya Dkt Ruto ilisitishwa sawa na ile ya Rais Uhuru Kenyatta na mwanahabari Joshua Sang, majaji waliruhusu upande wa mashtaka kuzifufua endapo ushahidi mpya utapatikana baadaye.

Bw Khan alipigiwa kura kwa wingi mnamo Februari 12 na mataifa yaliyo wanachama wa ICC, ili kumrithi Bi Bensouda hatamu yake itakapoisha Juni 16.Alimshinda Bw Fergal Geynor aliyekuwa wakili wa waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007. Serikali ilikuwa imepinga uteuzi wa Bw Geynor.

“Ninataka kuondoa hofu yoyote iliyopo kuhusu uwezekano wa Bw Khan kuwa na mapendeleo atakapohudumu kama kiongozi mpya wa mashtaka ICC. Katika mawasiliano yetu, alinihakikishia kuwa hatasimamia kesi yoyote ambayo aliwahi kuwakilisha washtakiwa au washukiwa,” Bi Bensouda akasema katika taarifa Ijumaa.

Kwa sasa mahakama hiyo inaendeleza kesi dhidi ya wakili Paul Gicheru anayedaiwa kushawishi mashahidi kujiondoa katika kesi iliyomwandama Dkt Ruto.

Bi Bensouda alieleza kuwa waandishi wa sheria zinazotumiwa ICC walitabiri uwezekano wa wakili wa washtakiwa kuajiriwa baadaye kuhudumu katika afisi ya kiongozi wa mashtaka ndiposa wakabuni sheria inayopiga marufuku kiongozi wa mashtaka na naibu wake kushiriki katika kesi yoyote ambayo itaibua hofu ya mapendeleo kutoka kwao.

“Bw Khan atatimiza hitaji hilo la kisheria kila wakati atakapohitajika kufanya hivyo,” akasema.Kesi ya Dkt Ruto ilisitishwa Aprili 2016 baada ya upande wa mashtaka kuambia mahakama kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha.

Bi Bensouda alidai hili lilisababishwa na jinsi mashahidi wengi walivyoshawishiwa kujiondoa huku wengine wakitoweka kwa njia zisizoeleweka.

Upande wa mashtaka pia ulidai kuwa serikali ya Kenya ilikataa kusaidia katika ukusanyaji wa ushahidi zaidi uliohitajika.Hata hivyo, madai hayo yalipuuziliwa mbali na Dkt Ruto pamoja na mawakili wa serikali ambao walisisitiza kuwa upande wa mashtaka haukuwahi kuwa na ushahidi tangu kesi hizo zilipoanza chini ya aliyekuwa kiongozi wa mashtaka Louis Moreno Ocampo.

Kwingineko, kesi ya ulanguzi wa dawa za kulevya dhidi ya raia wa Tanzania aliyekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi itatajwa leo katika Mahakama ya Mombasa.

Maimuna Jumanne Amir aliyekamatwa Machi 14 na kukaa korokoroni kwa siku nne, alifunguliwa mashtaka ya kukamatwa akiwa anasafirisha gramu 5,389 za heroini.

Mshukiwa alikanusha shtaka hilo alipofikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Bw Vincent Adet.Polisi wanadai kuwa mtuhumiwa huyo alisafiri kutoka Afrika Kusini, kupitia Addis Ababa, Ethiopia kabla ya kutua nchini.

Alikamatwa siku chache baada ya watu wanne kukamatwa eneo la Mji wa Kale, Mombasa wakisafirisha kilo mbili za dawa ya heroini yenye thamani ya Sh6 milioni.

Maelezo zaidi na Brian Ocharo

Bensouda afurahia kuruhusiwa kukagua vifaa vilivyomilikiwa na wakili Gicheru

Na VALENTINE OBARA

AFISI ya Kiongozi wa Mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) inayoongozwa na Bi Fatou Bensouda, imepata ushindi wake mkubwa wa kwanza dhidi ya wakili Paul Gicheru aliyejisalimisha mwaka uliopita.

Bw Gicheru angali amezuiliwa ICC kwa madai ya kushawishi mashahidi wajiondoe katika kesi iliyomwandama Naibu Rais, Dkt William Ruto na mwanahabari Joshua Sang kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Mahakama imeamua kwamba afisi ya Bi Bensouda ikabidhiwe vifaa vitano ambavyo havijatajwa, vinavyomilikiwa na wakili huyo ambavyo alikuwa amewasili navyo jijini The Hague (Uholanzi) alipojisalimisha.

Imebainika polisi wa Uholanzi walimpekua Bw Gicheru alipofika nchini humo na wakampata na vitu mbalimbali, vikiwemo vitano ambavyo waliamua kuviweka kando.

Walipomwasilisha kwa ICC, maafisa katika kitengo cha usajili wa mahakama waliamua kuhifadhi vitu hivyo vitano, na kuwasilisha ombi kwa Jaji Reine Alapini-Gansou anayesikiliza kesi hiyo atoe mwelekeo kuhusu wanachofaa kuvifanyia.

Bi Bensouda aliwaomba majaji, aruhusiwe kuvikagua ili atumie chochote atakachopata kuimarisha ushahidi wake, lakini wakili Michael Karnavas, anayemwakilisha Bw Gicheru, akapinga ombi hilo akisema litaingilia mambo ya siri ya mteja wake.

Mnamo Jumatatu jioni, Jaji Gansou alitoa uamuzi kwamba aliridhishwa na ombi la Bi Bensouda na hivyo akatupilia mbali ombi la Bw Gicheru kutaka arudishiwe mali yake bila kuchunguzwa.

Kulingana na jaji huyo, makosa ambayo Bw Gicheru anashtakiwa nayo ni mazito na yanahusu mtandao mkubwa wa kihalifu uliotumiwa tangu Aprili 2013 kushawishi mashahidi kujiondoa katika kesi za uhalifu dhidi ya haki za binadamu.

“Kiongozi wa mashtaka ana jukumu kuchunguza vifaa hivi kwa msingi wa kanuni za kisheria za mahakama, na ikiwezekana, mlalamishi anaweza kutaja masuala yoyote yatakayoibuka baadaye kuhusu suala hili wakati kesi itakapokuwa ikiendelea,” akasema Jaji katika uamuzi wake.

Jaji huyo alieleza kuwa, uamuzi huo ulizingatia agizo lililokuwa limetolewa awali la kukamatwa kwa Bw Gicheru pamoja na mshukiwa mwingine, Philip Kipkoech Bett kwa madai ya kuhujumu utendaji wa haki kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi.

Alisema, katika agizo la kukamatwa kwao lilihitaji wapekuliwe pamoja na sehemu ambapo wangekamatwa ikiwemo nyumba au afisi zao, na chochote ambacho kingeaminika kinaweza kutegemewa kama ushahidi kiwasilishwe mahakamani.

Bw Gicheru alijisalimisha kwa ICC mnamo Novemba 2, akafikishwa mbele ya mahakama Novemba 6 ambapo alikana kuhusika katika madai yaliyotolewa dhidi yake.

Ijapokuwa aliomba kuachiliwa huru, kesi yake ikiendelea na upande wa mashtaka haukupinga ombi hilo, Serikali ya Kenya ilikataa kujihusisha na kesi yake na hivyo basi kufanya aendelee kukaa kizuizini The Hague.

Hali hii ni kutokana na kuwa, serikali inahitajika kuahidi kuwa itasaidia mahakama hiyo kuendeleza kesi hiyo, ikiwemo kwa kurahisisha safari zake kati ya Kenya na Uholanzi.

Kupitia kwa Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki, Serikali ilisema Bw Gicheru hakufuata sheria za nchi alipojisalimisha na hivyo basi Kenya itakuwa inakiuka sheria ikijihusisha na kesi hiyo.

Chadema washindwa kumshtaki Magufuli ICC

Na THE CITIZEN

MAAFISA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameshindwa kushtaki serikali ya Rais John Pombe Magufuli katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kibinadamu (ICC) baada ya kesi yao kukosa kuungwa mkono na Kiongozi wa Mashtaka Fatou Bensouda.

Aliyekuwa mwaniaji wa urais kupitia Chadema, Tundu Lissu wikendi alisema, mawakili wa chama hicho hawaruhusiwi kuwasilisha kesi yao katika mahakama hiyo ya kimataifa iliyoko jijini Hague, Uswizi, bila kupitia afisi ya Bensouda.

Lissu aliyekuwa akizungumza katika mjadala wa mtandaoni, alisema Mkataba wa Roma unaruhusu tu kiongozi wa mashtaka wa ICC kuwasilisha kesi katika mahakama hiyo.

Chadema kilikuwa kimekusanya ushahidi ambao kilidai ulionyesha jinsi serikali ilikiuka haki za kibinadamu na kuwadhulumu viongozi wa upinzani kabla na baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 28, mwaka jana.

 

Wakili aliyejisalimisha ICC asalia pweke Kenya ikijitenga

Na VALENTINE OBARA

WAKILI Paul Gicheru aliyejisalimisha kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ameikosoa serikali ya Kenya kwa kukataa kumsaidia kuendeleza kesi yake.

Wiki iliyopita, serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki ilikataa wito wa ICC iliyotaka hakikisho kwamba Bw Gicheru atasaidiwa kusafiri kutoka Kenya hadi Uholanzi wakati wowote atakapohitajika mahakamani.

Bw Kariuki alikuwa amesema, Bw Gicheru hakufuata sheria kwani alihitajika kuifahamisha Mahakama Kuu humu nchini kuhusu nia yake kujisalimisha ICC na hivyo basi serikali ikiingilia itakuwa inakiuka sheria.

Msimamo huo wa serikali sasa unamweka hatarini Bw Gicheru kuendelea kukaa kizuizini The Hague, Uholanzi hadi kesi yake itakapokamilika.

Hii ni kutokana na kuwa, serikali ya Uholanzi pia haijatoa hakikisho kama itampa kibali cha kuishi katika taifa hilo kwa muda kesi ikiendelea.

Wakili wa mshtakiwa, Bw Michael Karnavas, aliambia mahakama kuwa msimamo wa serikali ya Kenya ni kinyume na matakwa ya sheria zinazosimamia ICC ikizingatiwa kuwa Kenya ni mwanachama wa mahakama hiyo.

Vile vile, alisema Uholanzi haikufuata agizo la mahakama kwani taifa hilo halikusema wazi kama litakubali Bw Gicheru aishi nchini humo wakati wa kesi yake.

“Tunaomba Jaji aagize Kenya na Uholanzi kufafanua misimamo yao kwa msingi wa sheria za ICC,” akasema Bw Karnavas.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Reine Alapini-Gansou.

Bw Gicheru anakumbwa na madai ya kushawishi mashahidi kujiondoa katika kesi iliyomwandama Naibu Rais William Ruto kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Kesi ya Bw Ruto aliyekuwa ameshtakiwa pamoja na mwanahabari Joshua arap Sang ilisitishwa wakati Kiongozi wa Mashtaka, Bi Fatou Bensouda aliposema hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuiendeleza.

Bi Bensouda alilalamika kuwa, hali hiyo ilisababishwa na jinsi mashahidi aliowategemea walivyoshawishiwa kujiondoa.

Ilidaiwa mashahidi wakuu walihongwa, kupewa ahadi za ajira huku wengine wakitoweka wasijulikane waliko.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipewa uhuru wa kufufua kesi hizo baadaye endapo ushahidi mpya utapatikana.

Wakenya waliokuwa wameshtakiwa ICC kwa madai ya kuhusika kwa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 akiwemo Rais Uhuru Kenyatta, waliruhusiwa na mahakama kuja nchini wakati kesi zao zilipokuwa zikiendelea.

Wakati mwingine kesi hizo zilifanywa kwa njia ya video.

Katika kesi zinazohusu mataifa mengine, washtakiwa waliruhusiwa kuishi Uholanzi wakati kesi zao zikiendelea.

“Jaji hakuuliza Uholanzi tu kama itamsaidia Bw Gicheru kusafiri kati ya Kenya na Uholanzi, bali pia kama inaweza kumruhusu kuishi kwa muda Uholanzi wakati kesi ikiendelea,” akasema Bw Karnavas.

Hata hivyo, ICC inaweza kuomba ushirikiano wa mataifa mengine kumsitiri mshtakiwa endapo haitawezekana Kenya au Uholanzi.

Ruto aingiwa na baridi kesi yake ya ICC ikifufuliwa

Na BENSON MATHEKA

?HATUA ya Naibu Rais William Ruto ya kusitisha mikutano yake ya kisiasa, imeibua hofu kwamba, ameingiza baridi kufuatia matukio ya hivi majuzi ikiwa ni pamoja na hofu ya kufufuliwa kwa kesi iliyomkabili katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC).?

Mnamo Jumanne wiki jana, Dkt Ruto alitangaza kuwa amefuta mikutano ya kampeni yake ya kusaidia walala hoi kufuatia ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona nchini.

“Kuongezeka kwa maambukizi ya corona kuna hatari ya kuzuka kwa mkumbo wa pili wa msambao wa virusi hivyo. Kwa sababu hii, nimeamua kusitisha hafla zangu za umma hadi nitakapotangaza,” Dkt Ruto alisema.

Tangazo hilo lilijiri siku moja baada ya ICC kutangaza kuwa wakili Paul Gicheru aliyekuwa akisakwa kwa miaka mitano kwa madai ya kuhonga mashahidi wa kesi ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 dhidi ya Ruto kujisalimisha.

Ingawa Dkt Ruto alisema aliahirisha mikutano yake aliyopanga Makueni, Machakos na Kitui kufuatia ongezeko la maambukizi ya corona, maswali yameibuka kuhusu sadfa ya hatua hiyo na kujisalimisha kwa Bw Gicheru huko ICC.

Kuna wasiwasi kwamba, kujisalimisha kwa wakili huyo ICC ambako hakukutarajiwa, kunaweza kuvuruga azima ya Dkt Ruto ya kugombea urais 2022.

Corona na ICC zimemtoa pumzi Ruto – Wadadisi

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya Naibu Rais William Ruto ya kusitisha mikutano yake ya kisiasa, imeibua hofu kwamba ameingiza baridi kufuatia matukio ya hivi majuzi ikiwa ni pamoja na hofu ya kufufuliwa kwa kesi iliyomkabili katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC).

Mnamo Jumanne wiki jana, Dkt Ruto alitangaza kuwa amefuta mikutano ya kampeni yake ya kusaidia walala hoi kufuatia ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona nchini.

“Kuongezeka kwa maambukizi ya corona kuna hatari ya kuzuka kwa mkumbo wa pili wa msambao wa virusi hivyo. Kwa sababu hii, nimeamua kusitisha hafla zangu za umma hadi nitakapotangaza,” Dkt Ruto alisema.

Tangazo hilo lilijiri siku moja baada ya ICC kutangaza kuwa wakili Paul Gicheru aliyekuwa akisakwa kwa miaka mitano kwa madai ya kuhonga mashahidi wa kesi ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 dhidi ya Ruto kujisalimisha.

Ingawa Dkt Ruto alisema kwamba aliahirisha mikutano yake aliyopanga Makueni, Machakos na Kitui kufuatia ongezeko la maambukizi ya corona, maswali yameibuka kuhusu sadfa ya hatua hiyo na kujisalimisha kwa Bw Gicheru huko ICC.

Kuna wasiwasi kwamba kujisalimisha kwa wakili huyo ICC ambako hakukutarajiwa, kunaweza kuvuruga azima ya Dkt Ruto ya kugombea urais 2022.Mnamo Jumatano, ICC ilitangaza kuwa kesi ya Bw Gicheru itaanza mara moja hatua ambayo wadadisi wanasema huenda imemfanya Dkt Ruto kutokwa na pumzi.

“Hii ndiyo sababu ya kusitisha mikutano ya kisiasa. Anataka kujipanga upya,” Ike Kenneth Ojuok alisema kwenye Twitter kujibu taarifa ya Dkt Ruto.

Wakili huyo alifikishwa mahakamani Ijumaa kutambuliwa ambapo alisema hakushurutishwa na yeyote kujisalimisha.Ikizingatiwa kwamba amekuwa akikaidi marufuku ya wizara ya afya kuhusu mikutano ya hadhara, wachanganuzi wanasema kwamba huenda amegundua kwamba atalaumiwa kwa maambukizi ya corona yanayoongezeka kwa viwango vikubwa katika kaunti.

Baadhi ya Wakenya wanasema kwamba ikizingatiwa ugonjwa huo umeanza kusambaa na kuua watu wengi mashuhuri, huenda Dkt Ruto anahisi kwamba anaweka afya yake hatarini kwa kuandaa mikutano hiyo.

Watu wamekuwa wakisongamana katika mikutano anayoandaa wakiwa hawajavalia barakoa, ikiwa ni kukiuka kanuni za wizara ya afya za kuzuia msambao wa corona.

Mwezi jana, kamati ya kitaifa ya ushauri wa usalama (NSAC) ilipopiga marufuku mikutano yake kaunti za Nyamira, Kakamega na Muranga, Dkt Ruto na wandani wake walilalamika vikali.Kamati hiyo ilitaja ukiukaji wa kanuni za kuzuia corona kama sababu ya kuharamisha mikutano ya kisiasa nchini.

Kulingana kanuni za baraza hilo, mikutano ya kisiasa inafaa kuidhinishwa na wakuu wa vituo vya polisi inakoandaliwa.Baada ya Dkt Ruto na wandani wake kuteta kwamba ndio walilengwa na kanuni hizo, waliruhusiwa kuendelea na mikutano.

“Inashangaza anaweza kusitisha mikutano ambayo alilaumu maafisa wa serikali kwa kutumia polisi kuisimamisha kana kwamba hakukuwa na corona nchini wakati alipolalamika. Kuna sababu kuu kuliko ongezeko la corona na ninahisi inatokana na hofu fulani,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

Duru zinasema kuwa Dkt Ruto amechanganyikiwa baada ya juhudi zake za kutaka mdahalo kuhusu mapendekezo ya ripoti ya maridhiano kuzimwa.

Mchanganuzi wa masuala ya siasa Herman Manyora anasema kwamba Dkt Ruto ameingiwa na baridi baada ya kugundua kuwa mbinu zake za kupinga BBI hazifaulu.

Kwa kusitisha mikutano ambayo amekuwa akitetea hata mbele ya rais, wachanganuzi wanasema kwamba huenda Dkt Ruto ametambua ni hatari kushindana na rais aliye mamlakani.

Watatiza nchi kwa siasa za ubabe

Na WANDERI KAMAU

MZOZO wa kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto umegeuka kero kwa maendeleo, umoja na usalama wa nchi.

Wachanganuzi wanaeleza kwa Rais na Naibu Rais kukosa kushirikiana, utendakazi serikalini unatatizika, na wanaoumia ni wananchi, huku wafuasi wao wakizuia ghasia na kurushiana matusi na chuki mitandaoni.

Kwa mujibu wa Javas Bigambo, ambaye ni mdadisi wa siasa, ushindani wa kisiasa unaoshuhudiwa kwa sasa unatokana na tamaa ya viongozi husika na ubinafsi.

Anasema mwelekeo huo unajenga hali ambapo ni vigumu hali ya kuaminiana kuwepo katika siasa nchini, ambapo matokeo yake yamekuwa ni wananchi kukosa kuhudumiwa ipasavyo na uadui baina ya raia.

Mnamo Jumapili watu wawili waliuawa katika Kaunti ya Murang’a kwenye ghasia kati ya wafuasi wa Rais Kenyatta na wale wa Dkt Ruto.

“Tamaa na maslahi ya kibinafsi ndiyo misukumo halisi inayowafanya viongozi kuungana kisiasa. Hawajali uwepo wa malengo au mikakati ya muda mrefu itakayowafaidi wananchi bali wao wenyewe kibinafsi. Ukosefu wa malengo yaliyokitwa kwenye ustawi wa kisiasa daima utatufanya kukwama kama nchi ikiwa hili halitarekebishwa,” akasema.

“Hali ya mikataba kubuniwa na kuvunjika ni jambo la kawaida kwenye siasa kwani lengo kuu la wahusika huwa ni kuona ikiwa watatimiza maslahi yao,” asema mtaalamu wa siasa Prof Macharia Munene.

Wafuasi wa Dkt Ruto na Rais Kenyatta wamekuwa wakilaumiana kila upande ukidai kusalitiwa na mwingine.

Upande wa Naibu Rais unasisitiza kuwa Rais Kenyatta amemsaliti naibu wake kwa kwa kutozingatia ahadi ya kumuunga mkono kuwania urais wa 2022, licha yake kuahidi wakati wa kampeni.

Mrengo wa Rais Kenyatta nao unasema Dkt Ruto ndiye wa kulaumiwa kwa kuanza kampeni za mapema kinyume na ushauri wa Rais.

Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe, ambaye ni mwandani wa karibu wa Rais Kenyatta anasema Dkt Ruto ndiye aliyeanza kuyumbisha jahazi la Jubilee alipoanza kampeni za mapema za 2022.

“Hatua ya Dkt Ruto kuanza kampeni mapema ni kumchokoza Rais moja kwa moja. Ni vipi mume anaweza kukaa na mke ambaye hamheshimu?” akasema Bw Murathe.

Lakini Bw Murkomen anamkosoa Rais Kenyatta akisema ndiye chanzo kikuu cha mtafaruku uliopo kati yake na Dkt Ruto na pia ndani ya Jubilee.

“Jubilee imegeuka kuwa nyumba inayoongozwa na mtu mmoja ambaye usemi wake ndio amri. Hivyo ndivyo chama kinapaswa kuongozwa?” anashangaa Bw Murkomen, ambaye ni mwandani wa karibu wa Dkt Ruto.

Kwa mujibu wa Prof Peter Kagwanja, ambaye ni mdadisi wa siasa, si mshangao mzozo wa sasa kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto, kwani msingi wa muungano wao ulijengwa kwenye mashtaka yaliyowakabili kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mnamo 2012.

“Muungano wa UhuRuto uliwahusisha waathiriwa wawili wa mchakato wa ICC, wala si marafiki wa kweli. Ilitegemewa ungesambaratika mara tu baada ya mashtaka yao kukamilika,” aeleza Prof Kagwanja.

Aliongeza kuwa katika kubuni Jubilee, wawili hao walikosa kutatua changamoto za kisiasa zilizochangia ghasia za kikabila za 2007/2008.

Anaonya kuwa mtindo wa miungano kuvunjika kila mara ni ishara kuwa huenda Kenya ikachukua muda mrefu kupatauthabiti wa kisiasa.

Bw Bigambo anasema tabia hii ya usaliti katika siasa ina madhara zaidi kwa wananchi hata kuliko wanasiasa wahusika: “Ikiwa wanasiasa wanaweza kusalitiana baina yao, je, ni kiasi kipi wanaweza kuwasaliti wananchi waliowachagua?”

Wataalamu wailaumu ICC kwa kusitisha kesi za UhuRuto

NA VALENTINE OBARA

MAHAKAMA ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imekosolewa kwa kufanya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, Dkt William Ruto, kuendelea kuwa na wasiwasi hata baada ya kesi zao kusitishwa.

Wawili hao walikuwa wameshtakiwa ICC kwa madai ya kuhusika katika ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, lakini kesi zao zikasitishwa kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

Katika ripoti iliyotolewa na kikundi cha wataalamu kilichoajiriwa na Baraza la Mataifa Wanachama wa ICC, almaarufu kama ASP, kuchunguza utendakazi wa mahakama hiyo, ilibainika kulikuwa na madoa kadhaa jinsi kesi za Rais Kenyatta na Dkt Ruto ziliendeshwa.

Wataalamu hao wa kisheria kutoka nchi mbalimbali waliikosoa ICC kwa kutosema wazi kama viongozi hao wawili pamoja na mwanahabari Joshua arap Sang, sasa wako huru au waendelee kujiandaa kwa kesi baadaye.

Wakati kesi zao zilisitishwa majaji walisema upande wa mashtaka, unaoongozwa na Bi Fatou Bensouda, uko huru kuwasilisha kesi upya baadaye endapo ushahidi zaidi utapatikana.

Tangu wakati huo wapelelezi wa ICC huendeleza upelelezi wao, hasa kuhusu kesi ya Dkt Ruto, humu nchini kisiri kila mwaka.

Wataalamu hao walioanza kazi yao Desemba 2019 sasa wanasema mwenendo huu si wa haki kwani kisheria, mshtakiwa anafaa kufahamishwa iwapo ana hatia au la kesi inapotamatika.

“Maamuzi haya hayaendi sambamba na hali ya kawaida ambapo uamuzi unastahili kuwa kwamba, mshtakiwa hana kesi ya kujibu au kesi itamatishwe,” inasema ripoti hiyo iliyotolewa Jumatano jioni.

Kando na suala hilo, ICC ilikosolewa kwa kutotilia maanani malalamishi ya washtakiwa kwamba upande wa mashtaka ulihujumu mashahidi ambao washtakiwa waliwategemea katika kujitetea.

Katika kesi ya Rais na naibu wake, wataalamu walikosoa afisi ya Bi Bensouda kwa kukataa kuchunguza madai kwamba washirika wake walibuni ushahidi ambao ulitegemewa kuwashtaki wawili hao.

Mawakili wa washtakiwa walikuwa wameibua malalamishi tele kwamba upande wa mashtaka ulishirikiana na mashirika ya kijamii nchini Kenya kubuni ushahidi wa uongo na kuwafunza mashahidi jinsi ya kudanganya mahakamani.

“Mahakama ilikataa kuteua mpelelezi huru kuchunguza madai hayo. Wakati wa kesi ya Kenyatta, kulikuwa na madai mazito kuhusu kuhujumiwa kwa watetezi wake na washirika wa upande wa mashtaka. Japo madai haya yaliripotiwa na mawakili wa walalamishi kwa afisi ya kiongozi wa mashtaka, hakuna hatua yoyote ilichukuliwa,” ripoti iliendelea kueleza.

Wataalamu hao walipendekeza kuwa kuendelea mbele, ICC ibuni mfumo mwafaka wa kuhakikisha malalamishi yote kuhusu hujuma za haki yanachunguzwa kikamilifu na adhabu kutolewa haraka.

Aidha, waliongeza, wakati malalamishi kama hayo yanatolewa kuhusu upande wa mashtaka, ni vyema Msajili wa Mahakama aagizwe kuajiri mpelelezi huru kisha ripoti ya uchunguzi iwasilishe ili uamuzi ufanywe.

Akipokea ripoti hiyo, Rais wa ASP Bw O-Gon Kwon alisema ripoti itafanyiwa tathmini kisha hatua zichukuliwe.

Uundaji wa kamati hiyo ya wataalamu ulitokana na malalamishi mengi ya nchi mbalimbali, hasa za Afrika kuhusu utendakazi wa ICC.Baadhi ya viongozi wa Afrika hulalamika kwamba mahakama hiyo inatumiwa kuhujumu uhuru wa utawala wao.

ICC yazua baridi mpya kwa UhuRuto

Na VALENTINE OBARA

WASIWASI kuhusu kufufuliwa kwa kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), umeibuka upya.

Hii ni baada ya kufichuka kuwa aliyekuwa wakili wa waathiriwa wa ghasia hizo, Fergal Gaynor ana nafasi bora zaidi kuchukua mahali pa Bi Fatou Bensouda, ambaye anatarajiwa kukamilisha hatamu yake Juni 2021.

Tayari Kenya imepinga orodha ya walioteuliwa kuwania wadhifa huo ikisema mtu mmoja anapendelewa.

Katika barua iliyofichuliwa Jumatano, Balozi wa Kenya nchini Uholanzi ambako ni makao makuu ya ICC, Bw Lawrence Lenayapa, aliambia mahakama hiyo kwamba Kenya inapinga majina ya walioteuliwa kumrithi Bi Bensouda.

Ijapokuwa Bw Lenayapa hakutaja mteuliwa ambaye Kenya inaamini anapendelewa kuwa mkuu mpya wa mashtaka, wataalamu wa sheria za kimataifa wanasema ni wazi Kenya ina wasiwasi endapo Bw Gaynor atamrithi Bi Bensouda.

Kwa msingi wa kuwakilisha waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini, Bw Gaynor ana ufahamu mkubwa kuhusu kesi zote za Kenya.

Ijapokuwa kesi za Rais Kenyatta na Dkt Ruto zilisitishwa kwa madai kwamba hapakuwa na ushahidi wa kutosha , majaji wa ICC walitoa fursa kwa Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka (OTP) kuzifufua tena endapo wapelelezi wataridhishwa kwamba wamepata ushahidi mpya ulio na uzito.

Wasiwasi wa Kenya ni kuwa iwapo Bw Gaynor atapewa kazi hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kufufua kesi dhidi ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto, ikizingatiwa alikuwa wakili wa waathiriwa wa ghasia za 2007/08.

Bw Mark Kersten, ambaye ni mtaalamu wa sheria za kimataifa, alisema wasiwasi wa Kenya hauhusu utaalamu wa watu walioteuliwa kujaza nafasi ya Bi Bensouda mbali kesi kufufuliwa.

“Kesi zile za awali hazifai kutumiwa kama kigezo cha kuamua ufaafu wa wakuu wa mashtaka wanaoteuliwa. Naamini malalamishi ya Kenya yametokana na kuwa Morris na Gaynor walihusika katika kesi za Kenya. Wale walioshtakiwa bado wako mamlakani na wana wasiwasi kuhusu uwezekano wa ICC kufufua kesi za Kenya,” akasema.

Ripoti za kila mwaka kutoka kwa afisi ya Bi Bensouda huonyesha kwamba, licha ya kesi kusitishwa, wapelelezi wa ICC bado huzuru Kenya mara kwa mara kuendeleza ukusanyaji wa ushahidi mpya kuhusu kesi za ghasia zilizoua watu zaidi ya 1,300 na kuacha maelfu wengine bila makao hadi leo hii.

Mnamo Januari 2020 Dkt Ruto alisema anafahamu kuhusu mipango ya kufufua kesi hizo, tena akadai ni kati ya njama za kuzima maazimio yake ya kumrithi Rais Kenyatta ifikapo mwaka wa 2022.

Hata hivyo, ICC ilipuuza madai yake ikasema uamuzi wa korti mnamo 2016 ulikuwa wazi kwamba kesi zinaweza kufufuliwa ushahidi ukipatikana, na shughuli za mahakama hazifai kuingiziwa siasa.

Kando na Bw Gaynor, wengine walioteuliwa ni Bi Susan Okalany kutoka Uganda, Bw Richard Roy ambaye ni raia wa Canada na Bw Morris Anyah wa Nigeria, ambaye pia aliwakilisha waathiriwa wa ghasia za Kenya katika ICC kwa muda mfupi.

Mtaalamu wa sheria za kimataifa, Bw Astrid Coracini, alieleza kuwa ni desturi katika mashirika ya kimataifa kwamba nyadhifa kubwa hushikiliwa kwa mzunguko kutoka kwa ukanda mmoja hadi mwingine, hali inayomweka Bw Gaynor katika nafasi bora zaidi kupata kazi hiyo.

Hivyo basi, kutokana na kuwa Bi Bensouda ni Mwafrika aliye raia wa Gambia, itakuwa vigumu kushawishi mataifa kumchagua mwafrika kwa mara nyingine kumrithi.

Kwa upande mwingine, Naibu Mkuu wa Mashtaka aliye mamlakani kwa sasa ni raia wa Canada, Bw James Stewart, kwa hivyo haitawezekana kumchagua Bw Roy kujaza nafasi ya mkuu wa mashtaka.

ICC yapuuzilia mbali madai ya Ruto

Na WALTER MENYA

MAHAKAMA ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC), imekana madai ya Naibu Rais William Ruto kwamba kuna njama ya kufufua kesi dhidi yake katika chombo hicho.

Kwenye mahojiano yaliyochapishwa katika gazeti la ‘Daily Nation’ Ijumaa, Naibu Rais alidai kuwa wale ambao walipanga njama ya kuwazuia kuingia mamlakani mnamo 2013 sasa wanapanga kumzuia kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“Mwaka jana nilipokuwa nikizungumza na mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) Philip Kameru, niligundua kuwa kuna watu ambao wanataka kufungua upya kesi za ICC,” alisema Dkt Ruto.

Lakini Jumamosi, Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka katika mahakama ya ICC ilikana madai hayo.

“Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka haiwezi kutoa kauli yoyote,” ikasema taarifa ya aya tatu kwa maswala ambayo ‘Taifa Jumapili’ iliona.

Katika taarifa hiyo, afisi ya kiongozi wa mashtaka ilisema kuwa licha ya kwamba mashtaka dhidi yao kuondolewa, bado milango i wazi na mashtaka yanaweza kufunguliwa ikiwa ushahidi mpya utapatikana.

Lakini afisi hiyo haikuweza kufichua ikiwa kuna ushahidi wowote ambao unaweza kupelekwa kuchunguzwa upya au kufufuliwa kwa kesi dhidi ya Dkt Ruto.

“Kama mnavyofahamu mnamo Aprili 5, 2016, mahakama iliondoa mashtaka dhidi ya William Samoei Ruto na Joshua Arap Sang’ lakini ikasema wazi kuwa itafufua kesi endapo kutapatikana ushahidi mpya,” taarifa hiyo ikasema.

Ikaongeza: “Kulingana na Kipengee cha 15 cha Sheria za Roma zilizobuniwa mahakama ya ICC, mtu yeyote au kundi la watu kutoka popote duniani anaweza kutuma habari kuhusu makosa kwa kiongozi wa mashtaka. Na afisi hiyo ina wajibu wa kuweka siri habari zozote itakazopokea. Afisi hii huchambua inavyohitajika kulingana na Sheria za Roma bila mapendeleo.”

Kwenye ripoti yake katika shirika la Umoja wa Mataifa mwaka wa 2018, ICC ilisema kwamba uchunguzi kuhusu kesi za Kenya ungali unaendelea licha ya kutamatishwa kwa kesi hizo.

Hakuna mwandani wa Dkt Ruto aliyekuwa na habari kuhusu madai hayo. Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen alisema hakuwa na habari kuhusu uchunguzi dhidi ya Naibu Rais.

OBARA: ICC ikome kutonesha vidonda vya wahanga wa fujo 2007

Na VALENTINE OBARA

MAJIBIZANO kuhusu kesi za ghasia zilizotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007 ni kama kukejeli waathiriwa wa ghasia hizo.

Kila mwaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) hutoa ripoti ya shughuli zake ambapo mojawapo ya masuala yanayogusiwa ni kuhusu kesi hizo, ambazo zote zilisitishwa kwa sababu mbalimbali.

Ripoti hizo kutoka kwa kitengo cha kuendesha mashtaka ambacho kinasimamiwa na Bi Fatou Bensouda huwa hazituelezi chochote kipya ila kurudia mambo yale yale tunayofahamu.

Hayo ni kama vile kwamba, kesi zilifeli kwa ssbabu ya mashahidi kuhongwa, kutishiwa au kuuawa, na vile vile ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa serikali ya Kenya kukusanya ushahidi muhimu uliohitajika.

Wiki iliyopita, kitengo hicho kilitoa ripoti ya kina ijapokuwa si kamili ya uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa sheria za haki za kibinadamu kimataifa kuhusu kilichosababisha kesi hizo kusitishwa.

Kando na mambo ya kawaida tuliyoyazoea, kulionekana pia hali ya kulaumiana kati ya wasimamizi wa sasa wa idara ya kuendesha mashtaka, na wale waliotangulia wakiongozwa na Bw Louis Moreno-Ocampo.

Hii haikuwa mara ya kwanza Bw Ocampo kulaumiwa kwa usimamizi mbaya wakati wa ukusanyaji ushahidi ambao ungetegemewa katika kesi za washukiwa wakuu waliojumuisha Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, Dkt William Ruto.

Vijisababu hivi vinavyotolewa na ICC pamoja na lawama hazisaidii kivyovyote kumletea haki Mkenya mlala hoi ambaye alipoteza mali yake, akajeruhiwa kwa kiasi cha kuwa mlemavu daima, na yule ambaye alipoteza wapendwa wake kwa ukatili uliofanywa na majambazi na polisi waliotegemewa kulinda raia.

Matukio ya kutisha tuliyoshuhudia mwishoni mwa mwaka wa 2007 hadi mwanzoni mwa 2008 si jambo la kufanyia mzaha.

Inachukiza mno ikiwa kila mara tutakuwa tukiona matukio hayo yakitumiwa tu kama msingi wa kufanya utafiti au wa watu kujitafutia ubabe katika nyanja tofauti ilhali bado kuna maelfu ya waathiriwa ambao hawajatendewa haki hadi sasa.

Waathiriwa wengi walipewa matumaini ya kupokea haki katika ICC kwani inavyoonekana, serikali haijajitolea kikamilifu hadi sasa kuchukua hatua dhidi ya wahusika wa ghasia hizo wala kulipa ridhaa ya kutosha kwa waliopata hasara.

Inafahamika kwamba kesi zilizopelekwa ICC zingali wazi kufunguliwa upya ikiwa ushahidi mpya unaoweza kutegemewa utapatikana katika siku za usoni.

Kile ambacho waathiriwa pamoja na watetezi wa haki walio na utu wanataka kujua ni kama wanafaa kuendelea kuwa na matumaini ya kupata haki, au wakubali hatima yao ya kuishi kwa athari zilizowakumba milele.

Itakuwa busara kama kitengo cha kuendesha mashtaka katika mahakama hiyo ya kimataifa itakoma kuwapa waathiriwa matumaini bila nia ya kutenda lolote jipya kwani ripoti hizi zinazotolewa mara kwa mara zinaibua kumbukumbu tusizipenda.

Kitabu chenye mada zinazohusu ICC na changamoto ya uhalifu barani Afrika chazinduliwa

Na LAWRENCE ONGARO

KITABU kipya chenye mada zinazohusu Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC) na ambacho vilevile kinamulika changamoto ya uhalifu barani Afrika kimezinduliwa.

Hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho imehudhuriwa na mwakilishi wa balozi wa Uholanzi nchini Bi Kirsten Hommes, Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) Prof Paul Wainaina, wahadhiri wakuu wa chuo hicho na wadau wengine muhimu waliochangia kukamilika kwa kitabu hicho.

Kitabu hicho kilichopewa anwani ‘International Criminal Justice In Africa Since The Rome Statute’ kimezinduliwa Ijumaa katika chuo hicho cha KU ambapo kimepigiwa chapuo na watu wengi.

Kinaangazia na kujadili kwa kina mada na maswala nyeti.

Wasomi kadha walitoa mchango wao kuhusu umuhimu wa kudumisha amani na kutenda haki kwa wananchi ili kuepukana na machafuko yanayoshuhudiwa kila mara barani Afrika.

Bi Hommes amesema cha muhimu kwa viongozi katika nchi za bara Afrika ni kutendea watu haki popote walipo na kuhakikisha kuna usawa.

Amekisifia kitabu hicho kipya kwa kusema kimeangazia maswala mengi kuhusu jinsi haki inavyostahili kutendewa kila mmoja bila kubagua.

Ametoa wito kwa watu kukisoma kitabu hicho ili kuelewa jinsi kesi zinavyoendeshwa kule The Hague, Uholanzi ambako ndiko yaliko makao makuu ya ICC na jinsi viongozi wanavyostahili kuepuka kusafirishwa hadi huko kwa tuhuma za mauaji ya halaiki katika nchi zao.

Naibu Chansela wa KU Prof Wainaina amekosoa viongozi wa mataifa ya bara Afrika ambao hukiuka sheria iliyowekwa kimataifa huku wakijifanya kutaka hiyo sheria itekelezwe kwa mwananchi wa chini.

“Ni vyema sheria zilizowekwa zifuatwe kikamilifu na kila mmoja ili haki iweze kutekelezwa ipasavyo. Tungetaka sisi wote tuwe sawa chini ya sheria,” amesema Prof Wainaina.

Amesema kuna nchi pia za nje ambazo hazitaki kufuata sheria za kimataifa na kanuni za ICC huku zikitaka mzigo wa makosa uwasilishwe au ubebwe na mataifa ya bara Afrika.

Pongezi

Amewapongeza wote waliochangia kwa njia moja ama nyingine kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hicho hasa wahariri na waandishi.

“Kazi mliofanya ni muhimu na itaweza kuelimisha watu wengi kuhusu jinsi ya kufuata sheria na kutendea watu haki bila kutumia fujo katika kutatua changamoto zilizopo,” amesema Prof Wainaina.

Hata hivyo, amesema kitabu hicho kinastahili kufanyiwa uchunguzi wa kila mara ili kuja na mawazo mengine mapya kuhusiana na mahakama hiyo ya ICC.

Pia amependekeza kuwe na hafla za kila mara kujadiliana mengi kuhusu maswala ya ICC ili kuja na mawazo tofauti.

Dkt Faith Kabata ambaye pia alitoa maoni yake amesema ni vyema viongozi wa Afrika wawe wakiheshimu sheria ya kimataifa ili kutendea wananchi haki.

“Sheria inastahili kufuatwa na kila mmoja. Hakuna haja ya watu wa kiwango cha chini kunyanyaswa huku wakubwa wakiepuka hiyo sheria,” amesema Dkt Kabata.

MWANAMKE MWELEDI: Bidii imemweka upeoni

Na KENYA YEARBOOK

NI mmojawapo wa majaji wenye tajriba pevu zaidi nchini Kenya.

Joyce Aluoch, ni jaji wa kwanza kutoka Kenya kuhudumu katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), wadhifa aliopata miezi mitatu pekee baada ya kupandishwa madaraka na kuwa jaji wa mahakama ya rufaa.

Sio hayo tu! Machi 2015, alikuwa jaji wa kwanza Mwafrika kuteuliwa kama Naibu wa Rais wa mahakama ya ICC ambapo alihitajika kuhudumu katika kipindi cha miaka mitatu.

Jaji Aluoch, ana shahada ya Sheria kutoka Chuo kikuu cha Nairobi na stashahada katika masuala ya sheria kutoka chuo cha Kenya School of Law.

Ajabu ni kwamba, hakuwahi kudhania kwamba wakati mmoja angekuwa wakili.

Baada ya kufanya vyema katika masomo ya shule ya upili alijua kwamba alitaka kuwa mhudumu wa kijamii, wakati huo akifanya kazi katika idara ya uhamiaji.

Babake alikuwa na mawazo tofauti. Siku moja aliandamana naye kazini, na kujipata katika chuo cha mafunzo cha sheria cha Kenya School of Law, ambapo walikutana na mkuu wa chuo hicho.

Ziara hiyo ilithibitisha safari yake katika Uanasheria ambapo baadaye alihitimu kama wakili kutoka chuo kikuu cha Nairobi na kujiunga na idara ya sheria kama Hakimu wa Wilaya pindi baada ya kukamilisha masomo yake.

Alipoanza safari yake katika sheria, alikuwa na ari ya kuendelea kujiimarisha na kupanda ngazi, hasa ikizingatiwa kwamba wakati huo, idadi ya wanawake katika idara hii ilikuwa ndogo.

Kwa hivyo alijizatiti kuhakikisha kwamba idadi ya wanawake inaongezeka kwa kuendesha mipango ya unasihi kuandaa mawakili wa kike kuwazia kuwa mahakimu na majaji.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kwani shughuli ya kusaidia wanawake wanaohudumu katika idara ya sheria kupanda madaraka ilijikokota mno.

“Sio kwamba wanawake hawakuwa wanatia bidii. Tulikuwa tunajitahidi sawa na wanaume, bali na kuwa akina mama na wake. Sikuelewa kwa nini jitihada zetu zilichukua muda mrefu kutambuliwa,” asema.

Licha ya changamoto hizi, Jaji Aluoch aliendelea kupanda madaraka. Alikuwa mwanamke wa pili kuteuliwa kama Jaji wa Mahakama Kuu baada ya mwenzake, Effie Owuor.

Anakumbuka jinsi kama wanawake wawili pekee katika idara ya mahakama, hawakuwa wanapokea marupurupu ya nyumba eti kwa sababu walikuwa wameolewa.

Siku moja wawili hawa walimtembelea Rais katika Ikulu jijini Nairobi na kuangazia matatizo ya wanawake katika utumishi wa umma.

Huenda usawa ambao wanawake katika utumishi wa umma wanashuhudia kwa sasa ni kutokana na matunda ya ujasiri wa majaji hawa.

Changamoto ni zipi?

Ni safari ambayo imekuwa na pandashuka zake.

Aliolewa na kumpata mwanawe wa kwanza akiwa angali mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Nairobi. Anakumbuka jinsi alivyotatizika kusawazisha majukumu ya mama, mwanafunzi na baadaye jaji.

“Nakumbuka wanangu walipokuwa bado wananyonya, ilinibidi kuwa nyumbani wakati wa asubuhi na kuandaa vikao vya mahakama adhuhuri. Hii kidogo ilinirudisha nyuma,” aeleza.

Lakini pia anasisitiza kuwa mama na afisa wa mahakama kulimpa msukumo wa kujizatiti katika taaluma yake.
Baada ya kuteuliwa kama hakimu wa wilaya, Jaji Aluoch alipanda hadi viwango vya Jaji wa Mahakama kuu, nafasi aliyoishikilia kwa miaka 20.

Alikuwa mwenyekiti wa kwanza katika Kamati ya wataalamu Waafrika kuhusu haki na maslahi ya watoto, na naibu mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watoto kati ya 2003 na 2009.

Hii ni kando na kuhudumu katika jopo dhidi ya uhalifu wa dhuluma za kimapenzi, suala lililopelekea kuundwa kwa Sheria ya Dhuluma ya Kimapenzi Mwaka wa 2006.

Jaji Aluoch anataja uteuzi wake kama Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kama ufanisi wake mkubwa.

“Nilishinda kwa kura 100 kutoka mataifa 108. Wakati huo nilikuwa nafanya shahada yangu ya uzamifu na nilikuwa nashughulikia masuala ya Mahakama ya Rufaa, kumaanisha kwamba sikuwa na muda wa kufanya kampeni. Ni Mungu aliyenisaidia,” asema.

Jaji Aluoch alipata shahada yake ya uzamifu katika masuala ya kimataifa kutoka kwa Chuo Kikuu cha Tufts nchini Amerika. Mwaka wa 2015, chuo hicho kilimpa tuzo ya heshima kama mwanafunzi wa zamani na kama utambuzi wa huduma yake kuu katika jamii.

Ufanisi huu haujamzuia kuzidi kuhudumia jamii ambapo alipohamia jijini Hague, alijiunga na chama cha Rotary Club na kuhudumu kama mwenyekiti wa huduma za kijamii.

Mbali na hayo, anazidi kunasihi wasichana kama mbinu ya kujitolea kuhudumia jamii nchini Kenya na Uholanzi.

Wandani wa Ruto wakashifu mahasimu kutoa ushahidi mpya kuhusu ICC

GRACE GITAU Na VALENTINE OBARA

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto, wamedai mahasimu wake ndio wanapeana ushahidi mpya kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Hivi majuzi, iliibuka mahakama hiyo ingali inakusanya ushahidi kuhusu ghasia hizo ambapo Bw Ruto na Rais Uhuru Kenyatta walikuwa miongoni mwa washukiwa wakuu.

Hii ni licha ya kuwa kesi zao zilisitishwa baada ya kupatikana hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha walihusika kuchochea au kufadhili ghasia hizo.

Huku ikihofiwa kwamba ufufuzi wa kesi hizo unaweza kumharibia Bw Ruto nafasi kushinda urais 2022, wandani wake jana walidai ripoti hizo kutoka kwa ICC nchini Uholanzi ni njama ya mahasimu wake.

“Ulipelekwa Uholanzi pamoja na Rais, ukashinda. Bado utaibuka mshindi na hatimaye utakuwa rais wetu,” akasema Mbunge wa Tetu, Bw James Gichuhi.

Alizungumza alipoandamana na Bw Ruto na viongozi wengine kwa ibada katika Kaunti ya Nyeri Jumapili.

Wasomi nchini kutathmini kama ICC ni muhimu kwa Kenya

NA LAWRENCE ONGARO

WASOMI wa kisheria nchini wanapanga kuchapisha kitabu kitakachochanganua kwa undani kuhusu kama Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ni muhimu kwa Kenya.

Kwenye kongamano la siku mbili lililofanyika katika Chuo cha Kenyatta kujadili kuhusu utenda kazi wa Mahakama ya kimataifa ya ICC, wasomi mbalimbali walitoa maoni yao kuhusu mahakama hiyo ambayo imekuwa ikikashifiwa vikali na viongozi wa Afrika

Miaka 20 imepita tangu kutiwa saini mkataba wa Roma ulioasisi Mahakama ya ICC na kongamano hilo lilikuwa kati ya shughuli nyinginezo zinazoendelezwa kimataifa kwa maadhimisho ya kuanzishwa kwake.

Msomi wa kisheria Profesa Makau Mutua alisema mahakama hiyo inastahili kuwepo lakini isiwe ikibagua kwa kuwashtaki Waafrika pekee.

Aliongeza kuwa mahakama hiyo inastahili kupata mamlaka zaidi ili kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

“Waathiriwa wengi huachwa wakisononeka kwa sababu washukiwa wengi hawapewi adhabu inayostahili,” alisema Profesa Mutua.

Ilidaiwa kuwa lawama chungu nzima zinazolimbikiziwa ICC zimeponza juhudi zake za kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Wakili Mkuu wa Serikali, Bw Kenneth Ogetto aliyemwakilisha mwanasheria mkuu Bw Kihara Kariuki, alisema ni muhimu kutathmini kwa kina umuhimu wa mahakama hiyo.

Humu nchini, majukumu ya mahakama hiyo yalizua ubishi mkubwa baada ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kulazimika kuwa kizimbani wakifuatilia kesi za ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Bw Ogetoalitoa mfano wa John Bolton, ambaye ndiye mkuu wa kiusalama nchini Marekani ambaye ambaye hivi majuzi alikosoa mahakama ya ICC kuhusu utenda kazi wake inapoendeleza uchunguzi kuhusu matukio ya ghasia Afghanistan ambako wanajeshi wa Amerika walihusika pakubwa.

Kwa kauli moja wasomi waliohudhuria walikubaliana kuchapisha kitabu kitakacho angazia maswala muhimu ya ICC.

ICC yamtupa Bemba jela mwaka mmoja

MASHIRIKA na PETER MBURU

HAGUE, UHOLANZI

MAHAKAMA ya Kimataifa kuhusu Kesi za Jinai Jumatatu ilimfunga kwa mwaka mmoja gerezani aliyekuwa naibu wa Rais Congo Jean-Pierre Bemba kwa kuwahonga mashahidi katika kesi ya awali, ambayo ilimfanya akatazwe kuwania Urais.

Majaji hao walimfunga Bemba kwa kipindi hicho, hata baada yao kulalamika mbeleni kuwa kipindi hicho kilikuwa kidogo sana, huku upande wa mashtaka ukiwa ulikuwa umeitaka korti kumfunga kwa kipindi cha juu zaidi kisheria cha miaka mitano.

 Mwanasiasa huyo wa miaka 55 ambaye alikuwa amekuwa kiongozi wa waasi Congo mbeleni alikuwa ameachiliwa na mahakama ya ICC mbeleni kwa mashtaka ya kivita na dhuluma za jinai dhidi ya binadamu alipokata rufaa miezi mitatu iliyopita.

“Korti inamhukumu Bw Bemba kwa jumla ya miezi 12 jela. Baada ya kupunguza muda kutokana na muda aliokaa ndani mbeleni, korti inachukulia muda huo kama aliotumikia kifungo,”akasema Jaji Bertram Schmitt.

Aidha, Bemba alipigwa faini ya Euro 300,000.

Kifungo chake hicho kilitokana na mashtaka kuwa alipokuwa akifanya kesi ya vita na dhuluma dhidi ya binadamu aliwahonga mashahidi na kuwaeleza mashahidi 14 cha kusema kortini.

Alifungwa kifungo sawia Machi baada ya kupatikana na hatia hiyo, akiwa pamoja na 14 wenzake, lakini majaji wa mahakama ya rufaa ICC wakarejesha kesi jikoni kwa madai kuwa kifungo hicho cha mwaka na faini ya Euro 300,000 kilikuwa kidogo mno.

Lakini Jumatatu, Jaji Schmitt alisema kuwa kifungo cha muda mrefu sana kinachoruhusiwa kisheria hakifai katika kesi hiyo.

Kifungo hicho sasa kimekuwa pigo kwa Bemba ambaye amekuwa na malengo ya kuongoza taifa hilo lililokumbwa na ghasia kwa miaka mingi.

ICC yafikisha miaka 20 huku ikikosolewa

Na VALENTINE OBARA

MAHAKAMA ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) Jumatatu itaanza maadhimisho ya miaka 20 tangu ilipobuniwa Julai 17, 1998 huku makali yake ya kutenda haki kuhusu dhuluma za kivita kimataifa yakizidi kutiliwa shaka.

Viongozi wa Afrika bado wanalalamika kuhusu ICC ambayo wanadai hutumiwa kuingilia uhuru wa bara hili ikizingatiwa kuwa karibu kesi zote zilizo mbele yake ni za mataifa ya Afrika.

Mkataba wa Roma, ambao ndio msingi wa sheria za ICC, uliundwa katika mwaka wa 1998 na kuidhinishwa na mataifa 123 kufikia sasa, mengi yakiwa ni ya Afrika.

“Kuundwa kwa Mkataba wa Roma katika mwaka wa 1998 ilikuwa ni tukio la kihistoria na hatua kubwa katika juhudi za kutenda haki ulimwenguni. ICC inaazimia kupata ushirikiano kimataifa kulinda kila mtu kutokana na aina za uhalifu zilizotajwa kwenye Mkataba wa Roma,” mahakama hiyo ilisema kwenye taarifa.

Aina za uhalifu ambazo hupelekwa katika mahakama hiyo ni kuhusu uhalifu wa kivita ikiwemo mauaji ya halaiki, utumizi wa watoto katika vita na ubakaji wakati wa vita.

Muungano wa Afrika (AU) ulipinga zaidi mahakama hiyo wakati wa kesi zilizowakumba Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kuhusiana na ghasia za baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007.

Ingawa kesi hizo zilizojumuisha Wakenya wengine wanne zilianza 2010 kabla wawili hao waingie mamlakani mwaka wa 2013, AU ilighadhabishwa na jinsi walivyohitajika kuwa kizimbani licha ya kuwa viongozi wa taifa lililo huru.

Kesi zote zilisitishwa baada ya upande wa mashtaka unaoongozwa na Bi Fatou Bensouda kusema hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuhukumu washukiwa.

“Nimekuwa nikisema mahakama itakuwa ya kushtaki Waafrika pekee, na sidhani kama nimekosolewa. Kuna watu wengi ulimwenguni ambao wanafaa kushtakiwa na mahakama hiyo,” Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambaye pia ni Mwenyekiti wa AU alisema hivi majuzi.

Kwa sasa, viongozi barani wanamtetea Rais wa Sudan Omar al-Bashir ambaye kuna agizo la kukamatwa kwake lililotolewa na ICC.

Rais huyo huzuru mataifa mbalimbali ya Afrika ambapo viongozi wa Au wamekubaliana kutotekeleza agizo la kumkamata na kumfikisha ICC.

Majaji wapya wateuliwa ICC kusikiza kesi za Uhuru na Ruto zikifufuliwa

Na VALENTINE OBARA

MAHAKAMA ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) imechagua majaji wapya kusimamia kesi za Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake, Bw William Ruto kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, iwapo Kiongozi wa Mashtaka wa korti hiyo ataamua kuzifufua.

Ingawa kesi hizo zilisitishwa kufuatia ukosefu wa ushahidi wa kutosha, Kiongozi wa Mashtaka, Bi Fatou Bensouda, aliambiwa yuko huru kuzifufua endapo atafanikiwa kukusanya ushahidi mpya.

Mwishoni mwa 2017, ilifichuka wapelelezi wa ICC walikuwa nchini Kenya kuchunguza masuala yanayohusiana na kesi ya Bw Ruto ambaye alishtakiwa pamoja na mtangazaji wa zamani wa redio, Bw Joshua Sang.

Ufichuzi huo ulitolewa kupitia kwa ripoti ya kila mwaka kuhusu shughuli za afisi ya upande wa mashtaka.

Mahakama hiyo Jumamosi ilifanya mabadiliko ya majaji baada ya majaji sita wapya kuchaguliwa wiki mbili zilizopita huku wengine waliokuwepo wakipewa majukumu mapya na baadhi yao kukamilisha muda wao wa kuhudumu.

Jaji Chile Eboe-Osuji ambaye wiki iliyopita alichaguliwa kuwa rais wa ICC, sasa atakuwa akihudumu kwenye kitengo cha rufaa cha mahakama hiyo. Awali, alikuwa Jaji Msimamizi wa kesi ya Mabw Ruto na Sang.

Kesi hiyo sasa itaendeshwa na Majaji Robert Fremr, Reine Alapini-Gansou na Kimberly Prost, ambao pia wataendesha kesi dhidi ya Rais Kenyatta.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, mahakama hiyo jana ilisema mabadiliko hayo ambayo yameathiri kesi karibu zote zilizo mbele yake yamechukuliwa ili kuboresha utoaji huduma.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa afisi ya rais wa ICC ilizingatia uwezo na weledi wa majaji katika sheria za uhalifu wa kimataifa wakati mabadiliko hayo yalipofanywa.

“Majaji watahudumu kwa miaka mitatu, na baadaye hadi wakati kesi zitakapokamilika,” ikasema taarifa hiyo.

Kufuatia hatua hii, vyumba vya mahakama vya Tano (A) na Tano (B) ambavyo vilikuwa vikutumika kusikiliza kesi ya Bw Ruto na Rais Kenyatta mtawalia vilivunjiliwa mbali.

Kesi zote za Wakenya sita waliodaiwa kuhusika pakubaa zaidi na ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 zilisitishwa baada ya kukosekana ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuhusika kwao.

Bi Bensouda alilalamika kuwa uamuzi wake kusitisha kesi za Rais Kenyatta, Bw Ruto na Bw Sanga ulitokana na kuwa mashahidi walishawishiwa kujiondoa ambapo baadhi walitishiwa maisha yao, wengine wakauawa na wengine wakatoweka katika hali ya kutatanisha.

Alidai pia serikali ya Kenya ilikataa kumsaidia kukusanya ushahidi aliohitaji ilhali serikali ina jukumu hilo kwani taifa hili ni mwanachama wa ICC kupitia uratibishaji wa Mkataba wa Roma ambao ndio msingi wa sheria za mahakama hiyo iliyo The Hague, Uholanzi.

Hata hivyo, madai haya yalikanushwa na serikali ambayo iliwakilishwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Prof Githu Muigai.

Majaji waliosikiliza kesi ya Ruto ICC wapandishwa vyeo

Na VALENTINE OBARA

MAJAJI wawili waliosikiliza kesi dhidi ya Naibu Rais William Ruto, katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) wamepandishwa vyeo.

Katika uchaguzi wa viongozi wa mahakama hiyo uliofanywa Jumapili, Jaji Chile Eboe-Osuji alichaguliwa kuwa Rais wa ICC huku Jaji Robert Fremr, akichaguliwa kuwa Naibu Rais wa Kwanza.

Jaji Osuji ambaye ni raia wa Nigeria alipata umaarufu Kenya alipokuwa jaji kiongozi wa kesi kuhusu vita vya baada ya uchaguzi wa 2007 iliyomkabili Bw Ruto na mtangazaji wa redio wa zamani, Bw Joshua Sang. Alijiondoa kwenye kesi ya Rais Uhuru Kenyatta katika mwaka wa 2014.

Kwenye hotuba yake baada ya kuchaguliwa kuchukua mahala pa Jaji Silvia Fernández de Gurmendi, aliahidi kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wote wa mahakama hiyo ili kuwezesha utendaji wa haki kwa njia bora zaidi.

“Ninatazamia kushirikiana na Baraza la Mataifa Wanachama, mashirika ya kijamii na jamii ya kimataifa kwa jumla, kuchukua hatua pamoja ili kuimarisha mfumo wa Mkataba wa Roma,” akasema.

Mkataba wa Roma ndio msingi wa kisheria unaoongoza shughuli za mahakama hiyo.

Katika uchaguzi huo wa Jumapili, Jaji Joyce Aluoch ambaye ni Mkenya, alikamilisha hatamu yake ya kushikilia wadhifa wa Naibu Rais wa Kwanza wa ICC tangu mwaka wa 2015.

Jaji Marc Perrin de Brichambaut ambaye ni raia wa Ufaransa alichaguliwa kuwa Naibu Rais wa Pili wa mahakama hiyo, kuchukua mahali pa Jaji Kuniko Ozaki.

Kulingana na ICC, Afisi ya Rais wa ICC ina jukumu la usimamizi wa mahakama nzima isipokuwa Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka ambayo ni kitengo huru.

Miongoni mwa majukumu yake ni kusimamia idara ya msajili wa mahakama na kutanya utathmini wa maamuzi kadhaa ya idara hiyo, mali na utekelezaji wa maelewano yanayoekwa kati ya mahakama na mataifa na mashirika ya kimataifa.

Kesi zote za Wakenya sita kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 zilisitishwa baada ya upande wa mashtaka kusema hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha washukiwa walihusika.

Hata hivyo, kuna agizo la kukamatwa kwa Wakenya watatu, Walter Barasa, Paul Gicheru na Philip Kipkoech Bett, ambao inadaiwa walifanya njama za kushawishi mashahidi wajiondoe kwenye kesi iliyomkabili Bw Ruto.

Wiki iliyopita, Bw Barasa, aliripotiwa kusema yuko tayari kwenda The Hague baada ya kupinga kukamatwa kwake mahakamani nchini tangu ICC ilipoagiza akamatwe mwaka wa 2013.

Wataalamu wa ICC kukutana Nairobi kuhusu utafutaji haki

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw António Guterres. Picha/ AFP

Na VALENTINE OBARA

WATAALAMU wa masuala ya sheria za uhalifu wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali watakutana Nairobi kujadili mbinu bora za utendaji wa haki.

Kongamano hilo litafanyika wakati ambapo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) inaadhimisha miaka 20 tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Roma ambao ndio msingi wa sheria zake, na pia wakati ambapo utawala wa Jubilee unazidi kushutumiwa kwa kuhujumu uhuru wa mahakama nchini.

Mkutano huo ulioandaliwa na shirika lisilo la serikali la Wayamo Foundation na lile la Africa Group for Justice and Accountability utafanyika kuanzia Februari 27 hadi Machi 2 katika Chuo Kikuu cha Strathmore.

Watakaohudhuria ni wadau wa masuala ya haki kutoka kwa serikali, mashirika yasiyo ya serikali, wasomi, wafanyakazi na wanachama wa mashirika ya kijamii.

Miongoni mwa masuala yaliyopangiwa kujadiliwa ni kuhusu uwajibikaji katika utendaji wa haki kimataifa, barani na kitaifa.

Masuala mengine ni kuhusu uhalifu wa kimataifa, maoni kutoka kwa mahakama na kutoka kwa makundi ya watu walio hatarini zaidi kudhulumiwa kihalifu kama vile watoto na waathiriwa wa dhuluma za kimapenzi.

Ijumaa iliyopita, maadhimisho ya miaka 20 tangu kubuniwa kwa ICC yalifanywa katika makao makuu ya mahakama hiyo yaliyo The Hague, Uholanzi.

Maadhimisho hayo yalikuwa yaliandaliwa na shirika lisilo la serikali la Coalition for the International Criminal Court.

Waliohutubia maadhimisho hayo walizungumzia mafanikio yaliyopatikana kufikia sasa katika juhudi za kusaka haki kwa waathiriwa wa uhalifu wa kimataifa na changamoto zilizopo, huku wito ukitolewa kuimarisha mfumo wa utendakazi katika mahakama hiyo.

 

Umuhimu wa haki

Katika hotuba yake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw António Guterres, alisema kwamba maadhimisho hayo yametoa nafasi kwa wadau wote kutafakari kuhusu umuhimu wa haki katika kudumisha amani, usalama na kutetea haki za kimataifa.

“Hakuwezi kukawa na matumaini ya kuzuia uhalifu na kudumisha amani katika siku za usoni iwapo wahusika wa uhalifu wa aina hizo hawatashtakiwa na kuadhibiwa,” akasema.

Wengine waliohutubu ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa UN, Bw Kofi Annan, Rais wa ICC, Jaji Silvia Fernández de Gurmendi, Kiongozi wa Mashtaka katika mahakama hiyo, Bi Fatou Bensouda na Balozi wa Mashauri ya Kigeni katika Muungano wa Ulaya, Bi Federica Mogherini miongoni mwa wengine.

“Sote tunafahamu kuwa tunaelekea katika kipindi chenye misukosuko zaidi ulimwenguni. Ushirikiano wa mataifa ambao ulisaidia kufanikisha kubuniwa kwa mahakama hii uko hatarini,” akasema Jaji Gurmendi.

Mahakama hiyo ilikashifiwa vikali na viongozi wa Afrika wakati wa kesi kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.