JAMVI: Kuna hatari ya Raila ‘kujikwaa’ kisiasa kwa kumtetea Rais

Na WANDERI KAMAU

KUMEIBUKA hofu huenda kutajwa kwa Rais Uhuru Kenyatta kuwa miongoni mwa watu walioficha mabilioni ya fedha ng’ambo kukaathiri mpango wake kumuunga mkono kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kuwania urais 2022.

Rais Kenyatta alitajwa Jumatatu pamoja na jamaa zake kumiliki zaidi ya akaunti kumi na utajiri wa zaidi ya Sh3 bilioni katika akaunti fiche, kwenye ufichuzi unaoitwa ‘Pandora Papers.’

Wadadisi wanasema ingawa hilo halimaanishi Rais Kenyatta na familia yake walipora fedha hizo, kuna uwezekano ukatia doa juhudi za Rais kutangaza vita vikali dhidi ya ufisadi.

Vile vile, wameeleza hatua ya Bw Odinga kujitokeza wazi kumtetea Rais Kenyatta hadharani dhidi ya sakata hiyo itatia doa sifa yake kama mtetezi wa haki, uwajibikaji na ukweli.

Ijapokuwa viongozi na mashirika kadhaa ya kutetea umma yamejitokeza kumkashifu Rais, Bw Odinga alimtetea vikali Rais Kenyatta, akisema anapaswa kupewa nafasi kueleza ukweli kuhusu yale anayojua.

Kwenye mahojiano na vituo kadhaa vya redio Jumatano, Bw Odinga alisema “si makosa kwa Mkenya yeyote kuwa na akaunti fiche ughaibuni.”

“Sioni kosa, kwani kuna Wakenya wengi wenye akaunti hizo. Ningewaomba kujitokeza na kuzitangaza wazi. Imani yangu ni kuwa kama alivyoeleza Rais, ukweli kamili utajulikana,” akasema.

Sifa

Kutokana na kauli yake, wadadisi wa siasa wanaonya kwamba kuna uwezekano mkubwa Bw Odinga akaanza kupoteza sifa miongoni mwa baadhi ya wafuasi wake, kwani ataonekana kama mtetezi wa wafisadi.

“Tangu miaka ya tisini, Bw Odinga amejijengea sifa ya kisiasa kama mwanamageuzi, mtetezi wa haki na sauti ya mnyonge. Ni kutokana na uanaharakati wake ambapo alikamatwa na kufungwa gerezani na utawala wa marehemu Daniel Moi. Kuna hatari kubwa kwa kiongozi huyo kupoteza ushawishi wake kwani wengi wanamwona kama mtetezi wa watu wafisadi,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Wadadisi wanasema ni kinaya kwa Bw Odinga kunyamazia maovu yanayoendelea chini ya utawala wa Jubilee, ambapo sasa wajibu huo “ameuachia” Naibu Rais William Ruto na waandani wake.

“Katika muhula wa kwanza, Raila tuliyemwona wakati huo ni tofauti sana. Ni kupitia juhudi zake ambapo Wakenya walifahamu kuhusu sakata kama mikopo tata kama Eurobond. Je, ujasiri huo u wapi? Fichuzi kama hizo ndizo zilizomjengea sifa kama mtetezi wa wanyonge,” asema Bw Dismus Mokua, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kulingana na wadadisi, kuna hatari Bw Odinga “kujikwaa kisiasa” kwa kumtetea Rais Kenyatta, na badala yake kumpa nafasi Dkt Ruto kujijenga.

Hili linatokana na hatua ya baadhi ya washirika wa Dkt Ruto kujitokeza kumkashifu Rais Kenyatta na familia yake, wakimtaka kueleza na kutoa ufafanuzi kamili kuhusu fedha hizo.

“Kwa muda mrefu, Dkt Ruto amekuwa akihusishwa na sakata za ufisadi, hasa kutokana na michango mikubwa ya pesa ambayo amekuwa akitoa katika makanisa. Ni michango ambayo vigogo kama Bw Odinga wametilia shaka asili yake, wakiihusisha na uporaji wa fedha za umma. Amekuwa hata akiyarai makanisa kukataa fedha hizo, akidai zinatokana na ufiasadi. Anapojitokeza sasa kuanza kumtetea Rais Kenyatta, ataonekana kama kiongozi mnafiki, kwani ikiwa angekuwa anaeleza ukweli, wengi walimtarajia kumshinikiza Rais kuwajibika, kama ambavyo amekuwa akimhimiza Dkt Ruto,” asema Bw Wycliffe Muga, mdadisi wa siasa.

Ingawa Dkt Ruto hajazungumzia wazi ufichuzi huo tangu ulipoibuka, washirika wake wamemtaka Rais Kenyatta na jamaa zake kuwaeleza Wakenya kuhusu namna walivyopata fedha hizo.

Baadhi ya washirika hao ni wabunge Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Gladys Shollei (Uasin Gishu), Millicent Omanga (Seneta Maalum) kati ya wengine.

“Ni wakati Rais awaeleze Wakenya anachofahamu kuhusu fedha hizo. Je, zinatokana na uporaji wa mali ya umma? Mbona wakaziweka ng’anbo badal ya kuziwekeza nchini? Hayo ndiyo majibu ambayo Wakenya wanataka kutoka kwa Rais na jamaa zake,” akasema Bw Ichung’wa.

Wadadisi wanasema ikizingatiwa huu ni ufichuzi unaojulikana kimataifa, huenda ukaamwathiri sana kisiasa Bw Odinga, kwani huenda Wakenya wengi wakakosa kuamini kauli yake kuhusu juhudi atakazoweka kupambana na ufisadi.

Wanaonya ikiwa hataweka mikakati ifaayo kisiasa, huenda Dkt Ruto akaigeuza na kuanza kuwaponda wote wawili (Raila na Uhuru) kama wafisadi, hivyo “kujitakasa” dhidi ya lawama ambazo amekuwa akielekezwa na wawili hao kama kiongozi mfisadi.

“Wakenya wengi wanahangaika sana kutokana na gharama ya juu ya maisha. Wengi wanamtaka kiongozi ambaye atawahakikishia kwamba ataweka mikakati ya kutosha kuwakabili wafisadi. Hivyo, suala la ufisadi litakuwa miongoni mwa ajenda kuu zitakazozingatiwa kwenye kampeni za 2022,” asema Bw Muga.

Ingawa washirika wa Bw Odinga wanasisitiza hakumtetea Rais Kenyatta bali alieleza hisia zake, kambi ya Dkt Ruto inashikilia Bw Odinga amewasaliti Wakenya, hivyo “hii ni nafasi yake (Ruto) kuwakomboa Wakenya.”

JAMVI: Huyu atakayembwaga Ruto Mlimani ni nani?

Na BENSON MATHEKA

MABWANYENYE kutoka Mlima Kenya wanaodadisi wagombeaji urais wanakabiliwa na kibarua kigumu kumuidhinisha atakayeweza kumbwaga Naibu Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Dkt Ruto amepenya eneo la Mlima Kenya bila baraka za Rais Uhuru Kenyatta ambaye amekuwa akimlaumu kwa kumdharau na kumhujumu.

Mabwanyenye hao wenye ushawishi mkubwa wanasema kwamba wametumwa na Rais Kenyatta kuwahoji wagombeaji urais ili kumshauri anyeafaa kutetea na kulinda maslahi ya wakazi wa eneo la Mlima Kenya.

Wamekutana na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga waliyemmiminia sifa kwa kumsaidia Rais Kenyatta kwenye muhula wake wa pili uongozini wakisema kuna watu waliotaka kumhujumu.

Hii imechukuliwa na wengi kuwa waziri mkuu huyo wa zamani ndiye chaguo la matajiri hao kwa kuwa anaungwa na Rais Kenyatta.

Mnamo Alhamisi, walikutana na vinara wa muungano wa One Kenya Alliance Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi ( ANC), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gideon Moi (Kanu) kwa mazungumzo kuhusu ajenda zao kwa eneo la Mlima Kenya.

Duru zinasema baada ya mikutano hiyo miwili iliyofanyika katika hoteli ya Safari Park, Nairobi, kibarua cha matajiri hao ni kushawishi viongozi hao wa upinzani kuunga mmoja wao.

Bw Odinga hajatangaza azma yake ya kugombea urais japo amekuwa akiendeleza kampeni ya kujipigia debe chini ya kauli mbiu ya Azimio la Umoja na anaungwa mkono na Rais Kenyatta.

Katika OKA, Bw Mudavadi, Bw Musyoka na Bw Moi wametangaza kuwa watagombea urais na tayari wamekabidhiwa tiketi na vyama vyao huku washirika wao wakishikilia kuwa ni lazima majina yao yawe kwenye debe kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wadadisi wa siasa wanasema Dkt Ruto ambaye amepuuza mikutano ya matajiri hao na wapinzani wake, anafurahia kibarua kigumu ambacho kinawakabili mabwanyenye hao kutafuta mgombeaji mmoja wa kumenyana naye.

“Kwanza, itabidi wafanyabiashara hao washawishi vinara wa OKA kuunga mmoja wao ili waamue iwapo atakuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga. Japo wanasisitiza kwamba hawajaamua chaguo lao, ni wazi kama mchana kwamba chaguo la Rais Kenyatta wanayekiri aliwatuma ni Bw Odinga,” asema mchanganuzi wa siasa Betty Shayo.

Anasema jambo jingine linalowafanya wafanyabiashara hao kujikuna kichwa, ni kitakachofanyika wakiteua mgombea mwenza wa Bw Odinga mgombeaji urais mwingine kutoka eneo la Mlima Kenya.

“Kuna wasiwasi kwamba iwapo watateua mgombea mwenza wa Bw Odinga au wa mgombea urais wa muungano wa OKA kutoka eneo lao Mlima Kenya uasi utatokea na baadhi ya viongozi kuungana na Dkt Ruto,” asema Shayo.

Naibu Rais William Ruto (kulia) akiwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga katika hafla ya awali. Picha/ Maktaba

Hata kabla ya kuteua mgombeaji urais na mgombea mwenza, aeleza mchanganuzi wa siasa Peter Kamunya, matajiri hao wanakabiliwa na kibarua sawa na kilichomkabili Rais Kenyatta mwenyewe alipojaribu kupatanisha Bw Odinga na vinara wa OKA.

Katika mkutano wa Alhamisi, vinara wa OKA waliwaambia wafanyabiashara hao kwamba juhudi za kuwashinikiza kuunga Bw Odinga zitagonga mwamba.

Kulingana na aliyekuwa mbunge wa Lugari Cyrus Jirongo ambaye aliandamana na vinara hao katika mkutano huo, itakuwa kuharibu wakati kuwataka kuunga mgombeaji wasiyetaka.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Mount Kenya Foundation Bw Peter Munga na Naibu Wake Titus Ibui walisema kwamba watatoa uamuzi katika kongamano la tatu la Limuru litakalowaleta pamoja viongozi wa kisiasa, kibiashara, kijamii, kidini na vijana.

Baadhi ya wanasiasa na wadadisi wanasema kwamba vinara wa OKA wanafaa kuungana na Bw Odinga kumzuia Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Hofu ya wanamikakati wa Rais Kenyatta, wakiwemo wafanyabiashara hao ni kuwa iwapo upinzani utagawanyika itakuwa vigumu kumshinda Dkt Ruto.

Kinachowafanya wajikune kichwa ni kuwa hakuna viti vikubwa vya kugawia vinara wote baada ya kuzimwa kwa mchakato wa kubadilisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) ambao ulianzishwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Inasemekana kuwa japo wangetaka eneo lao kuwakilishwa katika serikali kuu, chini ya katiba ya sasa, kuteua mgombea urais kutoka Mlima Kenya kunaweza kusambaratisha mipango yao ya kumzuia Dkt Ruto.

Naibu Rais ameashiria kuwa atateua mgombea mwenza kutoka Mlima Kenya na ikizingatiwa ufuasi wake eneo hilo umeongezeka pakubwa, kutoungana kwa upinzani kunaweza kuvuruga mipango ya kumzuia kuingia Ikulu.

“Itabidi mabwanyenye hao kuunganisha vinara wa OKA na Bw Odinga, wafanye kampeni ya hali ya juu mashinani kubomoa umaarufu wa Dkt Ruto ili kujenga imani ya wakazi kwa Bw Odinga iwapo watamtawaza kuwa chaguo la mrithi wa Rais Kenyatta,” asema Shayo.

“Iwapo wataamua kuunga mgombeaji mwingine, jambo ambalo ni finyu sana kwa sasa, itabidi wamshawishi Bw Odinga na ngome zake kumuunga mkono,” aongeza.

JAMVI: Nyota ya kisiasa ya Karua inaingia doa?

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya kutangazwa kwa kiongozi wa Narck-Kenya, Bi Martha Karua, kama kaimu msemaji wa ukanda wa Mlima Kenya, imeibua maswali kuhusu ikiwa ametia doa sifa yake kama kiongozi wa kitaifa.

Bi Karua alitwikwa jukumu hilo kwenye kikao maalum cha viongozi wa ukanda huo, kilichofanyika mwanzoni mwa wiki hii, mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru.

Waliokuwepo kwenye kikao hicho ni Bi Karua, aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo na mbunge Moses Kuria (Gatundu Kusini).

Bw Kabogo ni kiongozi wa chama kipya cha Tujibebe Wakenya Party (TWP) huku Bw Kuria akiwa kiongozi wa Chama cha Kazi (CCK).

Viongozi hao walisema walifanya uamuzi huo baada ya kushauriana na viongozi wenzao kutoka sehemu mbalimbali katika ukanda huo.

Vile vile, walisema kuwa uamuzi wa kumtawaza Bi Karua kushikilia nafasi hiyo ulitokana na hali kuwa yeye haegemei mrengo wowote wa kisiasa.

Hata hivyo, wadadisi wa siasa wameeleza kuwa, ingawa huenda hatua hiyo inaonekana kumkweza Bi Karua kisiasa katika ukanda huo, kuna uwezekano ikampaka tope na kushusha nyota yake kitaifa kama mwanamageuzi anayeheshimika.

Kulingana na Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mchanganuzi wa siasa, kukwezwa kwa Bi Karua kama kaimu msemaji wa ukanda huo kutamwingiza kwenye “siasa chafu” za ushindani wa yule anayepaswa kuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta.

“Ni wazi kuwa kuna ushindani mkubwa ambao umejitokeza miongoni mwa wanasiasa wanaolenga kumrithi Rais Kenyatta. Ikizingatiwa Bi Karua amekuwa kwenye ligi ya kisiasa ya kitaifa, kuna uwezekano mkubwa akaanza kupigwa vita na wanasiasa wanapania kuchukua nafai hiyo,” akasema Prof Njoroge.

Bi Karua ni miongoni mwa viongozi wa eneo hilo ambao wamekuwa kwenye ulingo wa siasa kwa muda mrefu.

Alijitosa kwenye ulingo wa siasa katika miaka ya tisini, alipowania ubunge katika eneo la Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga na kuibuka mshindi.

Alihudumu kama waziri wa Maji na Haki na Masuala ya Katiba katika serikali ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki, hadi alipojiuzulu mnamo 2009.

Vile vile, alikuwa miongoni mwa viongozi walioshiriki katika Mazungumzo ya Serena baada ya ghasia za uchaguzi tata wa 2007, kumtetea Bw Kibaki.

Bi Karua alikuwa katika upande Bw Kibaki na chama cha PNU, akiwa pamoja na maseneta Moses Wetang’ula (Bungoma) na Prof Sam Ongeri (Kisii).

Kiongozi huyo pia aliwania urais mnamo 2013, ingawa hakuibuka mshindi.

Mnamo 2017, aliwania ugavana katika Kaunti ya Kirinyaga ingawa alishindwa na Gavana Anne Waiguru.

Wadadisi wanasema kuwa Bi Karua amejijengea sifa nzuri ya kiongozi anayeheshimika sana nchini na kimataifa, kwani kando na siasa, amekuwa akitumia taaluma yake ya uwakili kuwatetea wananchi.

“Hata ingawa Bi Karua analenga kurejea nyumbani kisiasa kama livyofanya mnamo 2017, nadhani kuna njia mbadala ambayo angetumia badala ya kukubali uteuzi wa kuwa msemaji wa Mlima Kenya. Kuna uwezekano mkubwa akajitosa kwenye vita na makabiliano ya kisiasa ambayo tumekuwa tukishuhudia baina ya mirengo mbalimbali katika ukanda huo,” asema Bw Ochieng’ Kanyadudi, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Baada ya uteuzi wake, Bi Karua alijitenga na madai ya kuwa mwanachama wa mrengo wowote wa kisiasa, akishikilia nia yake ni kuhakikisha eneo hilo limeungana ili kuwa na sauti moja kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“Mimi si mwanachana wa mrengo wowote. Ni mwanasiasa huru, anayelenga kuhakikisha watu wetu wamezungumza kwa sauti moja, kinyume na ilivyo sasa. Tunapaswa kuungana na kubuni njia tutakayofuata kwa wawaniaji wote wanaofika katika eneo letu kutuomba kuwaunga mkono,” akasema Bi Karua.

Mwanasiasa huyo amekuwa kiongozi wa Narc-Kenya kwa muda mrefu, akikitaja kuwa chama huru chenye misimamo yake kisiasa.

Kufikia sasa, viongozi waliotangaza ama kuonyesha nia ya kumrithi Rais Kenyatta ni aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri, magavana Mwangi wa Iria (Murang’a), Francis Kimemia (Nyandarua), Waiguru (Kirinyaga) kati ya wengine.

Hata hivyo, nia zao zimeandamwa na migawanyiko mikali, ambapo kwa sasa, kuna mirengo ya kisiasa ya ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga.’

Mrengo wa ‘Kieleweke’ umekuwa ukimtetea Rais Kenyatta huku ‘Tangatanga’ wakimtetea Naibu Rais William Ruto, kwenye nia yake kuwania urais 2022.

Bw Kanyadudi anasema kuwa kukubali nafasi hiyo, huenda Bi Karua analenga kuimarisha nafasi yake kuwania ugavana Kirinyaga, ikizingatiwa anakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa Mwakilishi wa Wanawake Wangui Ngirichi.

“Ilivyo sasa, Bi Karua ana kibarua kigumu kuwakabili Bi Ngirichi na Gavana Waiguru, ambao washatangaza azma ya kuwania ugavana. Kwa upande mmoja, nafasi hiyo itamsaidia kuinua nyota yake kisiasa, ila ajajipata tope ikiwa hatajiepusha na mizozo ya urithi ambayo huenda ikaibuka,” akasema mdadisi huyo.

JAMVI: Mtihani mgumu wamsubiri Ruto kuhusu miungano

Na CHARLES WASONGA

MSIMAMO wa Naibu Rais William Ruto kwamba chama cha United Democratic Alliance (UDA) hakitabuni muungano na vyama vidogo vinavyounga azma yake ya urais umeibua hisia mseto miongoni mwa wandani wake na wadadisi.

Baadhi ya wandani wa Dkt Ruto wanahisi kuwa UDA itazongwa na misukosuko endapo itabuni miungano na vyama vingine kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Lakini kuna tapo na wandani wake wanaohisi kuwa Dkt Ruto ataboresha nafasi yake ya kuingia Ikulu kwa kufanya muungano na vyama vingine vyenye “maono sawa na UDA.”

Kwa upande wake mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Dismus Mokua anashikilia kuwa Naibu Rais hana budi kukubali kuwa enzi ambapo Kenya ingeongozwa na chama kimoja ilipita baada ya KANU kuondolewa mamlakani 2002.

“Ikiwa kweli lengo la Dkt Ruto ni kuingia Ikulu, basi ni sharti akubali UDA ishirikiane na vyama vingine ambavyo havitadhamini wagombeaji urais lakini vimekubali kumuunga mkono. Itakuwa vigumu kwa chama chochote nchini kushinda urais kivyake,” anaeleza.

Lakini Dkt Ruto amesisitiza mara si moja kwamba vyama kama hivyo vinafaa kuvunjwa ili kuipa UDA nguvu sura ya kitaifa kilivyokuwa Jubilee kabla ya kuzongwa na changamoto 2018.

Akihutubu wiki jana nyumbani kwake, Sugoi, kaunti ya Uasin Gishu alipokea ujumbe wanasiasa kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya, Naibu Rais alitaja vyama hivyo kama “vya kikabila ambavyo haviwezi kuunganisha taifa hili.”

“Nia yetu ni kustawisha UDA ili kiwa chama kikubwa cha kitaifa ndiposa kiweze kuendeleza ajenda yake ya kuinua maisha ya mahasla kupitia mfumo wa kukuza uchumi kuanzia chini. Kwa hivyo, nataka ieleweke kwamba UDA haitashiriki muungano na hivyo vya vidogo vya kikabila,” Dkt Ruto akasema.

Naibu Rais alikuwa akirejelea chama cha The Service Party (TSP) kinachoongozwa na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, Chama cha Kazi (CCK) chake Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria na Chama cha Mashinani (CCM) kinachoongozwa na aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Rutto.

Kuvunja vyama

Licha ya Mbw Kiunjuri, Kuria na Rutto kutangaza wazi kwamba wanaunga mkono azma ya Dkt Ruto ya kuingia Ikulu 2022, wameshikilia kuwa katu hawatavunja vyama vyao ili kuungana na UDA.

“Sisi kama wanachama wa TSP tumekubali kuunga mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu kwa sababu tunakubaliana na sera na mpango wa Hustler Nation ambao unalenga kuwaimarisha Wakenya wa tabaka la chini kiuchumi. Lakini tutafanya hivyo ndani ya chama chetu; hatutakivuja ili kuungana na UDA,” Bw Kiunjuri akasema wiki jana kwenye mahojiano katika runinga ya KTN.

Aidha, wanasiasa huyo ambaye zamani alihudumu kama Mbunge wa Laikipia Mashariki, alipasua mbarika na kufichua kuwa sababu kuu ya yeye kukataa kujiunga na UDA kama mwanachama wa kawaida ni kwamba haamini kuwa mchujo wa chama hicho utaendeshwa kwa njia huru na haki.

“Sote tunajua yale yaliyoendelea katika makao makuu ya Jubilee kule Pangani ambapo watu fulani walinyimwa tiketi licha ya kwamba walishinda katika mchujo. Hatutaki kuingia kwenye kichinjio kama hicho na ndiposa tumekataa kuvunja chama chetu na kujiunga na UDA, “ akaeleza huku akiongeza kuwa TSP kitadhamini wagombeaji kwa nyadhifa zote tano isipokuwa wadhifa wa urais.

Kwa upande wake Bw Kuria anashikilia kuwa chama chake cha CCK hakitavunjwa kwa sababu lengo lake ni kutetea masilahi ya wakazi wa Mlima Kenya kwa ujumla.

“Ikiwa lengo la kuundwa kwa chama chetu lilikuwa ni kupigania ugavi sawa na rasilimali za kitaifa na nyadhifa serikalini kwa manufaa ya Mlima Kenya, mbona tuambiwe tukivunje? Ningependa kufafanua kuwa chama chetu kinamuunga mkono Dkt Ruto katika kinyang’anyiro cha urais lakini hakitavunjwa,” Mbunge huyo wa Gatundu Kusini akaambia ‘Taifa Jumapili‘ kwenye mahojiano kwa njia ya simu.

Uchaguzi ujao

Sawa na Bw Kiunjuri, Bw Kuria anasema kuwa CCK kitadhamini wagombeaji wa viti vya udiwani, ubunge, useneta na ugavana katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.

Hata hivyo, mbunge huyo alisema hatawania kiti chochote katika uchaguzi huo ila atasalia kuwa kiongozi wa kitaifa wa chama hicho.

“Mimi sitawania kiti chochote lakini tutatumia idadi ya madiwani, wabunge, maseneta na magavana ambao watashinda kwa tiketi ya CCK kupigania ugavi sawa wa rasimali za kitaifa kwa watu wetu wa Mlima Kenya. Hilo tutafanya na mgombeaji wa urais yeyote ambaye ataibuka mshindi, sio Dkt Ruto pekee,” Bw Kuria anafafanua huku akikariri msimamo wake kwa eneo hilo sharti litengewe asilimia 40 za nyadhifa serikalini.

Bw Rutto, naye anashikilia kuwa CCM ni chama kongwe zaidi kuliko UDA na hivyo haiwezi kuvunjwa.

“Mnamo 2020, nilitangaza wazi katika uwanja wa Bomet Green Stadium kwamba nimeamua kuzika tofauti za kisiasa na Naibu Rais William Ruto na kuunga mkono azma yake ya kuingia Ikulu 2022. Kadhalika nilichukua hatua hiyo kwa ajili ya umoja wa jamii yetu ya Kalenjin. Sasa mbona watu wengine wanataka nivunje chama cha CCM ilhali katiba inaruhusu demokrasia ya vyama vingi?” akauliza mwanasiasa huyo ambaye pia alihudumu kama mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) kati ya 2013 na 2015.

Lakini Seneta wa Meru Mithika Linturi na wabunge Rigathi Gachagua (Mathira) na Benjamin Washiali (Mumias Mashariki) wanaunga kauli ya Dkt Ruto kwamba UDA haifai kubuni muungano na vyama vingine.

“Wanasiasa hawa kutoka Mlima Kenya wanawakanganya raia kwa kubuni vyama vidogo ili kuendeleza masilahi yao lakini sio ya wananchi. Nia yao ni kumwekea masharti Naibu Rais uchaguzi mkuu unapowadia kwa manufaa yao ya kibinafsi. Hatufai kubuni muungano na watu kama hawa,” anaeleza.

Anaongeza: “Kiunjuri alikuwa na chama chake cha Grand National Unity (GNU); aliuzia Uhuru na akateuliwa waziri. Munya (Peter) alikuwa na PNU; akaipiga mnada na akapata cheo cha waziri wa Kilimo. Hayo ndiyo masilahi ya kibinafsi ninayoerejelea.”

Kwa upande wake Bw Gachagua anadai Mbw Kuria na Kiunjuri wanaongozwa vyama visivyo na ufuasi wowote katika eneo la Mlima Kenya.

“Kando na Kuria, je unafahamu mwanachama mwingine wa CCK katika eneo la Kati mwaka Kenya au popote nchini?” Hatutaki kuyumbishwa na vyama vya mikoba ilhali azma yetu kuu ni kunadi UDA,” akaeleza.

Lakini kulingana na Bw Mokua, vyama hivyo vidogo huenda vikageuka kuwa kimbilio la wanasiasa ambao watatendewa hiana katika mchujo wa UDA.

“Tayari minong’ono imeanza kuibuka kuwa Dkt Ruto amekwisha kuidhinisha wanasiasa fulani kwa nyadhifa fulani katika ngome za UDA za Mlima Kenya na Rift Valley. Hii ni ishara tosha kwamba baadhi ya wagombeaji wa UDA watakaohisi kutotendewa haki watahamia vyama hivi. Kwa hivyo, ni muhimu kwa Dkt Ruto kuvikumbatia la sivyo vitaamua kuunga mkono wapinzani wake haswa Raila Odinga,” anaeleza.

JAMVI: Waiguru njiapanda katika kivumbi cha 2022

Na WANDERI KAMAU

GAVANA Anne Waiguru wa Kirinyaga yupo kwenye njiapanda kuhusu mwelekeo wa kisiasa atakaofuata, uchaguzi mkuu wa 2022 unapokaribia.

Bi Waiguru amejipata akitapatapa kisiasa, asijue atakakoenda, kwani sasa anaonekana kuchanganyikiwa kabisa kuhusu mrengo atakaounga mkono ili kuokoa merikebu yake kwenye ulingo wa siasa.

Kwa sasa, guu moja la gavana huyo lipo katika Chama cha Jubilee (JP), anakodai anapigwa kisiasa, lingine kwa mrengo wa Naibu Rais William Ruto na la tatu katika chama cha ANC, chake Musalia Musalia Mudavadi.

Wadadisi wanasema huenda huu ukawa wakati mgumu sana kwa Bi Waiguru kufanya maamuzi muhimu yatakayoamua mustakabali wake kisiasa, la sivyo kuna hatari merikebu yake ikazama na kusahaulika kabisa.

Masaibu ya Bi Waiguru yalianza majuma machache yaliyopita, alipodai kuwa kuna “watu maarufu” katika Jubilee wanaompiga vita, ili kuvuruga ushawishi wake kisiasa katika Kaunti ya Kirinyaga na ukanda wa Mlima Kenya kwa jumla.

Bila kuwataja moja kwa moja, Bi Waiguru alidai walikuwa wakitumia ushawishi wao serikalini kumhangaisha kupitia Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

“Ni watu maarufu wanaolenga kufanya lolote wawezavyo kuhakikisha wamenivuruga kabisa kisiasa,” akasema.

Ingawa Bi Waiguru hajakuwa akiwataja watu hao, wadadisi wanaeleza uhasama wa gavana unatokana na ushindani wa kisiasa ambao umekuwepo kwa muda mrefu kati yake na Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho.

“Ni wazi Dkt Kibicho ni miongoni mwa watu wanaopigiwa upatu kuwania ugavana katika kaunti hiyo 2022. Hivyo, si ajabu kwa uhasama huo kuwepo. Matamshi ya Bi Waiguru yanatokana na joto la kisiasa linalotokana na ushawishi wa Dkt Kibicho serikalini,” asema Bw Julius Mukuha, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Wadadisi wanasema kuwa huenda Bi Waiguru akawa na kibarua kigumu kuhifadhi kiti chake, ikizingatiwa kuwa baadhi ya watu ambao wametangaza nia ya kuwania nafasi hiyo wanaonekana kuwa na ushawishi mkubwa kumliko.

Baadhi yao ni Mwakilishi wa Wanawake Wangui Ngirici, kiongozi wa Narc-Kenya, gavana wa zamani Joseph Ndathi kati ya wengine.

Wadadisi wanasema hali inayoashiria huenda Bi Waiguru ameingiwa na tumbojoto ni kauli aliyotoa majuzi, kwamba huenda akakosa kuhifadhi nafasi yake ikiwa angewania tena nafasi hiyo kwa tiketi ya Jubilee.

Aelekee wapi?

Kulingana na wadadisi wa siasa, Bi Waiguru ana kibarua kigumu sana, kwani ikiwa ataamua kujiunga na chama cha UDA, chake Dkt Ruto, huenda akakosa kupewa tiketi kwani tayari chama hicho kinaonekana kumpendelea Bi Ngirici kuwania ugavana kwa tiketi yake.

Alipofanya ziara katika ukanda wa Mlima Kenya wiki mbili zilizopita, Dkt Ruto aliwarai wenyeji wa Kirinyaga kumchagua Bi Ngirichi kama gavana wao kwa “kusimama nao katika kila hali.”

“Hali ilivyo, ni wazi kuwa Bi Ngirici ashapewa tiketi ya UDA. Hivyo, itakuwa vigumu sana kwa Bi Waiguru kupewa tiketi hiyo, hata ikiwa watashiriki kwenye shughuli ya mchujo,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Wadadisi wanasema hali hiyo pia inamyima nafasi Bi Waiguru kuteuliwa kama mgombea-mwenza wa Dkt Ruto kwenye uchaguzi wa 2022.

“Itakuwa vigumu sana kwa Bi Waiguru kukabidhiwa nafasi kubwa kama hiyo, ilhali kuna viongozi ambao wamekuwa wakiipigania kwa kumuunga mkono Dkt Ruto licha ya mahangaiko ya kisiasa ambayo wamekuwa wakipitia. Itakuwa vigumu sana kwake,” asema Bw Mutai.

Kauli hiyo inalingana na matamshi ya mbunge Rigathi Gachagua (Mathira), aliyesema majuzi kuwa “hawatawakubalia wageni kuchukua nafasi za ‘wenyeji’ katika UDA.”

Je, Bi Waiguru ana nafasi katika ANC?

Wadadisi wanasema ikiwa patazuka uwezekano wowote wa Bw Mudavadi kuungana na Bi Waiguru, basi Bw Mudavadi atakuwa ametia doa sifa yake kama mwanasiasa muungwana na mwadilifu.

Dalili za Bi Waiguru kujiunga na kambi ya Bw Mudavadi ziliibuka Alhamisi, wakati alipoandamana na baadhi ya washirika wa kiongozi huyo katika afisi za EACC, jijini Nairobi.

Bi Waiguru alikuwa amefika katika afisi hizo kujibu tuhuma za ufisadi zinazomkabili.

Kwenye kikao na wanahabari, mbunge Ayub Savula (Lugari), alisema kuwa watasimama kidete na Bi Waiguru kwa tuhuma hizo, huku wakiendelea kumrai kujiunga na kambi yao.

“Unapomtaka msichana, unamzungumzia polepole ili kumshawishi kujiunga nawe. Tutaendelea kuzungumza na Bi Waiguru hadi atakapokubali wito wetu,” akasema Bw Savula, ambaye ndiye Naibu Kiongozi wa ANC.

Jumanne, Bw Mudavadi pia alieleza uwezekano wa kumteua mgombea-mwenza kutoka Mlima Kenya.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kuwa Bi Waiguru anaandamwa na kivuli cha sakata za ufisadi, hivyo litakuwa “kosa la kimkakati” kwa Bw Mudavadi kushirikiana naye.

“Bi Waiguru bado anaandamwa na zimwi la sakata la ufisadi katika Shirika la Kitaifa la Vijana (NYS). Sasa, ana tuhuma zingine ambazo zimechipuka upya. Huenda taswira yake isikubalike, hasa kwa viongozi wanaosisitiza watakabiliana na ufisadi,” asema Dkt Godfrey Sang’, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kijumla, ingawa wadadisi wanasema bado Bi Waiguru ana nafasi kujiunda upya kisiasa, kibarua alicho nacho ni kujisafisha na kuondoa zigo la tuhuma za ufisadi linalomwandama.

JAMVI: Oparanya upanga wa kuifyeka mizizi ya OKA Magharibi

Na CHARLES WASONGA

MASWALI mengi yameibuliwa kuhusu sababu ya kushirikishwa kwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya katika mikutano ambayo Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akifanya na viongozi wa upinzani katika Ikulu za Nairobi na Mombasa.

Kwanza, wadadisi wamehoji nafasi ya gavana huyo katika mikutano hiyo ikizingatiwa kuwa yeye si kiongozi wa chama walivyo washiriki wengine kama vile Raila Odinga (ODM), Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Gideon Moi (KANU).

Pili, japo ikulu imeshikilia kuwa Rais Kenyatta, huitisha mikutano hiyo kujadili athari za janga la Covid-19, mikakati ya kufufua uchumi na masuala yanayohusiana na amani, umoja na uwiano wa kitaifa, duru zasema ajenda kuu huwa ni siasa za urithi wa urais.

Inasemekana kuwa katika mkutano wa Agosti 18, uliofanywa katika Ikulu ya Mombasa, Bw Musyoka alihoji uwepo wa Bw Oparanya katika kikao hicho “ilhali amewakilishwa kikamilifu na Raila.”

“Ni kweli kwamba Kalonzo juzi aliuliza ni kwa nini Oparanya amekuwa akihudhuria mikutano hiyo ilhali chama chake kinawakilishwa na kiongozi wake, Raila Odinga. Lakini majibu aliyopata ni kwamba Gavana Oparanya ni sehemu ya uwakilishi wa ODM katika mikutano hiyo inayoitishwa na Rais,” mmoja wa wandani wa Bw Odinga, ambaye aliomba tulibane jina lake, anasema.

Kwa upande wake, Bw Oparanya juzi alitetea uwepo wake katika mikutano ya Ikulu akisema yeye hupata mwaliko wa moja kwa moja kutoka kwa Rais Kenyatta.

“Kulingana na itifaki, watu wote ambao huenda Ikulu, hufanya hivyo kwa mwaliko wa rais mwenyewe kupitia afisi ya msimamizi wa asasi hiyo. Wale wote wenye maswali yoyote kuhusu wageni wa rais wanapaswa kuyawasilisha kwa asasi husika,” akanukuliwa akisema.

Kwa upande wake mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi ambaye ni Mkurugenzi wa Masuala ya Kisiasa katika ODM, Bw Oparanya hualikwa katika mikutano kati ya Rais Kenyatta na viongozi wa upinzani kwa “sababu ni mmoja wa washirika wa rais katika juhudi zake za kuleta umoja nchini.”

“Ifahamike kwamba Oparanya ni naibu kiongozi wa chama chetu cha ODM. Bw Oparanya amehudumu kwa mihula miwili kama mwenyekiti wa Baraza la Magavana Nchini (COG) sawa na wadhifa wake kama Gavana wa Kakamega. Hii ni kando na kwamba ni yeye pamoja na Waziri Eugene Wamalwa walioteuliwa kushirikisha ajenda ya maendeleo katika eneo la Magharibi ya Kenya,” asema mbunge huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC).

Mchanganuzi

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Herman Manyora anakubaliana na Bw Wandayi kuhusu hadhi ya Bw Oparanya, katika eneo la Magharibi na kitaifa.

Lakini kwa mujibu wa msomi huyo ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi, uwepo wa Bw Oparanya katika mikutano hiyo ya Ikulu unalenga “kuyeyusha ushawishi wa Bw Wetang’ula na Mudavadi ndani na nje ya vikao hivyo.”

“Raila huandamana na Oparanya katika mikutano hiyo kwa idhini ya Rais, kuwapa Mudavadi na Wetang’ula ujumbe kwamba endapo watakataa kuunga mkono kiongozi huyo wa ODM katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2022 basi atakwezwa kujaza mapengo yao,” Bw Manyora anasema.

Inasemekana kuwa lengo kuu la Rais Kenyatta ni kuwashawishi vinara wa muungano wa OKA wamuunge mkono Bw Odinga kwa imani kuwa yeye ndiye anaweza kumwangusha Naibu Rais William Ruto debeni.

Lakini Mbw Musyoka na Mudavadi bado wanahisi kuwa kila mmoja wao ndiye anatosha kupambana na Dkt Ruto katika uchaguzi huo.

Naye Bw Wetang’ula ameonyesha ishara kwamba yu tayari kuunga mkono azma ya Bw Mudavadi huku Seneta Gideon Moi akionekana kuwa tayari kuweka kando ndoto yake ya urais na kufuata ushauri wa Rais Kenyatta.

“Binafsi nimewahi kuwashauri ndugu zangu Mudavadi na Wetang’ula kwamba endapo watadiriki kusimama kivyao, bila shaka watafeli. Sasa ni wazi kwamba Rais Kenyatta amejitolea kuunganisha viongozi wote wa upinzani kwa lengo la kumzuia Dkt Ruto kumrithi,” Bw Manyora anaeleza.

Juzi, Rais Kenyatta alionyesha ishara ya wazi wazi kwamba hatamuunga mkono naibu wake katika kinyang’anyiro cha urais 2022, alipomsuta kwa kile alichodai ni mwenendo wake wa kuikosoa serikali.

Katika mahojiano na wahariri wa vyombo vya habari vya humu nchini katika Ikulu ya Nairobi, kiongozi wa taifa alimtaka Dkt Ruto ajiuzulu badala ya kuendelea “kukosoa serikali ambaye yeye bado ni mshirika”.

Bw Javas Bigambo pia anaafikiana na kauli ya Bw Manyora kwamba, Bw Odinga anamkuza Bw Oparanya kwa nia ya kuwadhibiti Mbw Mudavadi na Wetang’ula katika eneo la Magharibi.

“Hii ni kwa sababu wawili hao wameonyesha wazi kwamba hawako tayari kumuunga mkono tena baada ya kuwasaliti katika uliokuwa muungano wa NASA. Sasa Raila ameamua kumtumia gavana Oparanya kama nguzo yake mbadala katika eneo la Magharibi. Hii ndiyo maana Rais humshirikisha katika msururu wa mikutano ya Ikulu,” akasema.

Mapema mwaka huu 2021 Bw Oparanya ambaye ni Naibu Kiongozi wa ODM, alitangaza kuwa atajitosa katika kinyang’anyiro cha urais 2022, lakini hivi sasa anaonekana kuunga mkono azma ya Bw Odinga kutwaa wadhifa huo.

Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho pia alikuwa ametangaza kuwa atawania tiketi ya ODM ili kufanikisha ndoto yake ya kuingia Ikulu.

Hata hivyo, baadaye wawili hawa wameonekana kukunja mkia baada ya Bw Odinga kuimarisha nia yake kuwania urais kwa mara ya tano.

JAMVI: Ruto kukabiliwa na mtihani mkali 2022 bila ya miungano

Na WANDERI KAMAU

“NI kinaya kuwa Bw Mwangi Kiunjuri na Bw Moses Kuria ndio wanaoongoza harakati za kushinikiza muungano wa kisiasa katika Mlima Kenya ilhali walikuwa katika mstari wa mbele kumpigia debe Dkt Ruto kuhusu azma yake ya urais 2022. Hili ni dhihirisho la uwepo wa vita baridi vya kisiasa miongoni mwa washirika wa Ruto,” asema Bw Mwangi Waithaka, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Wadadisi pia wanaeleza kuwa, ingawa Dkt Ruto analenga kukita siasa zake katika jukwaa la ‘kuondoa ukabila’, huenda hilo likawa gumu, ukizingatia kwamba siasa za Kenya zimejikita katika ukabila.

“Ingawa kuna kizazi tofauti ambacho kimeanza kukita mitazamo ya kisiasa tofauti na ukabila, ni vigumu kwa kiongozi yeyote kuendeleza mikakati ya kujipigia debe bila kuzingatia uhalisia wa kikabila,” asema Bw Samuel Njung’e, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Bw Njung’e anasema kuwa hata ikiwa mbinu hiyo ilifaulu mnamo 2017, wakati vyama 14 viliungana ili kubuni Chama cha Jubilee (JP), mazingira ya kisiasa ni tofauti sana wakati huu.

“Kati ya 2013 na 2017, Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto walionekana kufanikiwa kuiunganisha nchi. Hakukuwa na migawanyiko na taharuki ya kisiasa kama ilivyo sasa. Uthabiti huo ndio uliwasaidia kuifanya Jubilee kuibuka maarufu na kushinda viti hata katika ngome za uliokuwa muungano wa NASA,” akasema.

Wadadisi wanaeleza kuwa tatizo jingine linalomwandama Dkt Ruto ni ‘laana’ ya kung’ang’aniwa kwa tiketi ya UDA miongoni mwa wagombeaji watakaowania nyadhifa mbalimbali za kisiasa.

Wanasema tatizo hilo ndilo liliandama Jubilee, kiasi kwamba ilikilazimu chama kuandaa duru ya pili ya uchaguzi wa mchujo.

“Ukosefu wa chama kingine utajenga taswira iliyoshuhudiwa 2017, ambapo wawaniaji wengi waliachwa nje baada ya kushindwa kupata tiketi ya Jubilee kuwania nyadhifa hizo. Hali hiyo ni miongoni mwa viini vikuu vya mvutano unaoshuhudiwa kwa sasa katika chama cha UDA,” asema Bw Oscar Plato ambaye ni mdadisi wa siasa.

JAMVI: Misimamo mikali OKA inaweza kuwafaidi au kuwabomoa 2022

Na BENSON MATHEKA

MSIMAMO mkali wa baadhi ya vinara wanaosuka muungano wa One Kenya Alliance (OKA) wa kukataa kumuunga kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, huenda ukawa baraka kwao au ukawasukuma kwenye baridi kali zaidi ya kisiasa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Muungano huo ambao unaendelea kusukwa, unaleta pamoja kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper, Moses Wetang’ula wa Ford Kenya na Gideon Moi wa chama cha Kanu.

Bw Mudavadi, Bw Musyoka na Bw Wetang’ula wamesimama kidete kwamba hawatamuunga Bw Odinga huku ikisemekana kuwa Bw Moi hana tatizo kumuunga waziri mkuu huyo wa zamani.

Watatu hao ambao walikuwa vinara wenza wa Bw Odinga katika uliokuwa muungano wa NASA wanasema kwamba wanaweza tu kushirikiana naye akijiunga na OKA bila masharti.

Licha ya kushauriwa na Rais Uhuru Kenyatta kumuunga Bw Odinga ili waweze kumshinda Naibu Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao, Bw Mudavadi na Bw Musyoka wamekaa ngumu kila mmoja akisisitiza kuwa jina lake litakuwa kwenye debe.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, sio siri kwamba Bw Odinga ndiye mwanasiasa maarufu zaidi kote nchini kuweza kutoa jasho Dkt Ruto na kwa kukataa kuungana naye, huenda wakapoteza nafasi ya kuwa kwenye serikali ijayo.

“Iwapo Bw Odinga atafanikiwa kuunda muungano thabiti kukabiliana na Dkt Ruto na mmoja wao apate zaidi ya asilimia 50 ya kura, vinara wa OKA watalazimika kuumia kwenye baridi ya kisiasa,” asema.

“Lakini ikiwa hakutakuwa na mshindi wa moja kwa moja wa kura ya urais kwenye uchaguzi mkuu ujao na wanawaweza kulazimisha hilo kufanyika, watakuwa katika nafasi nzuri ya kuungana na mrengo wa Bw Odinga au Dkt Ruto kwenye raundi ya pili ya uchaguzi na kuwa kwenye serikali ijayo,” asema mdadisi wa siasa Tom Maosa.

Anasema kwamba misimamo mikali pia inadhihirika ndani ya OKA na inaweza kufanya muungano huo kusambaratika hata kabla ya kuzinduliwa.

“Kuna vinara wawili ambao wanashikilia kuwa hawawezi kuunga Bw Odinga huku kila mmoja akisisitiza hawezi kumuachia mwenzake kupeperusha bendera. Hii inaweza kuchangia kuwasukuma katika baridi ya kisiasa wakikosa muafaka,” asema Maosa.

Mnamo Ijumaa, Bw Mudavadi alisema mwanasiasa yeyote anayetarajia atamuunga mkono anaota.

“Nitakuwa kwenye debe. Niko na mipango ya kuongoza Kenya kupata ustawi mkubwa wa kiuchumi,” alisema Bw Mudavadi.

Kauli yake ilijiri siku tatu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuhimiza vinara wa OKA, kumuunga Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kulingana na mdadisi wa siasa Geff Kamwanah, vinara hao wanakabiliwa na hatari ya kujipata njia panda, iwapo Bw Odinga atafaulu kuunda muungano mpya na kuwafungia nje na kisha Rais Uhuru Kenyatta awaache kwenye mataa.

“Hali inaweza kuwa mbaya kwao iwapo Dkt Ruto atasisitiza kuwa amejipanga na hahitaji ushirika wa vigogo ambao amekuwa akidai walifanya akafukuzwa serikalini. Hii ikifanyika, watakuwa mayatima kwenye siasa za Kenya,” asema Bw Kamwanah.

“Kwa kuwa siasa za Kenya zinabadilika haraka, kuna hatari yao kujichimbia kaburi kisiasa wakikosa kwenye serikali ijayo,” aongeza mchanganuzi huyu.

Baadhi ya wadadisi wanasema misimamo ya vinara wa OKA inaweza kufanya kila mmoja wao akipigana kuokoa maisha yake ya kisiasa kivyake.

“Iwapo Bw Mudavadi atatofautiana na Bw Musyoka kuhusu anayefaa kuwa mgombea urais wa muungano wao, wanaweza kugawanyika na kulegeza msimamo mmoja aelekee kwa Dkt Ruto na mwingine kwa Bw Odinga. Hii inaweza kubadilisha mkondo wa siasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022,” asema Bw Richard Kakai, wakili na mdadisi wa siasa.

Kulingana na Bw Kakai, makosa ambayo wawili hao wanaweza kufanya ni kutengana na kila mmoja kugombea kivyake.

“Kutengana kwao, ambao kunaweza kuepukwa kwa kulegeza misimamo, kutawaingiza katika baridi ya kisiasa. Umoja wao, ukikitwa kwenye msingi wa msimamo mmoja, unaweza kuwafanya kuamua atakayeunda serikali ijayo kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga lakini sio mmoja wao,” asema Kakai.

Vinara wa OKA wanatarajiwa kukutana wikendi kujadili pendekezo la Rais Kenyatta kwamba wamuunge Bw Odinga chini ya mkataba mpya.

Inasemekana kuwa Rais Kenyatta yuko tayari kuwa mdhamini wa mkataba wa kuunda muungano mpya utakaomshinda Dkt Ruto.

Hata hivyo, washirika wa vinara hao wanasisitiza kuwa ni lazima viongozi wa vyama vyao wawe kwenye debe.Kulingana na seneta wa Kitui Enock Wambua, Wiper kilimkabidhi Bw Musyoka tiketi ya kugombea urais pekee.

“Kama chama, mgombea urais wetu ni Bw Kalonzo Musyoka na huo ndio msimamo wake na wa chama,” asema.

Naye mwenzake wa Kakamega Cleophas Malala anasisitiza kwamba vinara wengine wanafaa kumuunga Bw Mudavadi.

“Ninataka kusema wazi kuwa utakuwa kwenye debe. Kuna uvumi kwamba utaunga mtu mwingine kugombea urais. Chama kilikupa tiketi na huo ndio msimamo wetu,” Bw Malala alimwambia Bw Mudavadi.

Kulingana na Bw Kakai, misimamo ya Bw Musyoka na Bw Mudavadi inaweza kuwafanya watorokwe na vinara wenzao katika OKA na kuwatumbukiza katika baridi ya kisiasa.

Vigogo wanavyoviziana kuwania ubabe 2022

Na BENSON MATHEKA

Vigogo wa kisiasa wanaomezea mate urais wanaendelea kuviziana kila moja akisubiri kuona hatua ambayo mwenzake atachukua katika juhudi za kubuni miungano ya kisiasa kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Hakuna anayetaka kuanika wazi mipango yake kwa sasa japo mazungumzo ya kusuka miungano yanaendelea chini kwa chini hata kati ya wanaochukuliwa kuwa mahasimu wa kisiasa.

Hata Naibu Rais William Ruto ambaye amekuwa akitangaza wazi kwamba amejipanga kukabiliana na wapinzani anasemekana kuwa kwenye mazungumzo na baadhi ya wanasiasa wakuu wakiwemo vinara wa muungano unaoendelea kusukwa wa One Kenya Alliance.

Duru zinasema kwamba Dkt Ruto amekutana mara kadhaa na vinara wawili wa OKA katika juhudi za kuwashawishi wamuunge mkono.

Muungano wa OKA unaleta pamoja Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper, Musalia Mudavadi wa Amani National Congress, Moses Wetangula wa Ford Kenya na Gideon Moi wa Kanu.

Ingawa wanne hao wanasisitiza kuwa wako pamoja na wanaendelea kujipanga kabla ya kuzindua rasmi muungano huo, inasemekana kuwa kuna tofauti zinazoweza kuwafanya watengane.

Tayari chama cha Kanu kimeashiria kuwa huenda kikajiondoa kwa kuwa kina mkataba wa muungano na chama cha Jubilee ambacho kinawania kuungana na ODM cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.

Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula wamesema kuwa hawawezi kumuunga Bw Odinga ambaye alikuwa mshirika wao katika uliokuwa muungano wa NASA kugombea urais.

Ingawa kufikia sasa Bw Odinga hajatangaza azima yake ya kugombea uais kwa mara ya tano kwenye uchaguzi mkuu ujao, hatua ambazo yeye na chama chake kimechukua zinaonyesha jina lake litakuwa kwenye debe.

Wadadisi wa siasa wanasema hii ndiyo sababu ODM kiliondoka NASA ili mkataba uliomfunga Bw Odinga usiwe kizingiti kwake kugombea na kusuka muungano mpya.

ODM na Jubilee zimetangaza kuwa zitaungana kwenye uchaguzi mkuu ujao, muungano ambao huenda ukahusisha vyama vingine vikubwa na vidogo.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, mviziano unaoendelea ni kwa sababu hakuna mwanasiasa anayetaka kujitokeza kujifunga katika muungano ambao utamtumbukiza kwenye baridi ya kisiasa.

“Baadhi ya vigogo wa kisiasa wanaomezea mate urais wamekuwa kwenye baridi ya kisiasa kwa miaka mingi na hawataki kufanya makosa kwa kujifunga kwenye miungano. Pia, kuna presha kutoka kwa wanaoshawishi hali ya siasa nchini kwamba wanafaa kufuata mkondo fulani,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Larry Ouko.

Inasemekana kuwa ingawa vinara wa OKA waliokuwa kwenye NASA wamesema hawatamuunga Bw Odinga, baadhi yao wamekuwa wakizungumza naye kwa lengo la kushirikiana kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Bw Odinga amekuwa akisisitiza kuwa ingawa chama chake kinasuka muungano na Jubilee anapanga chombo kikubwa kitakachomshinda Dkt Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Vinara wa OKA nao wamekuwa wakisema kwamba wanapanua muungano wanaosuka kushirikisha vigogo wengine akiwemo Bw Odinga kama kinara mwenza na sio mgombea urais.

Kuna minong’ono kwamba lengo la vinara wa OKA ni kuunda chombo vya kuongeza thamani kwenye meza ya mazungumzo ya kubuni muungano mkubwa kabla au baada ya uchaguzi.

Inasemekana tayari Bw Odinga na Dkt Ruto wameanza kuvizia vinara wa muunagano huo kila mmoja akitaka kuwavuta upande wake.

Tayari, Bw Odinga amekutana na Bw Moi na kuna kila dalili kwamba watashirikiana kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Duru za kuaminika zinasema kwamba Bw Odinga na Bw Musyoka wamekuwa wakizungumza bila kuhusisha washirika wao ambao inaaminika wana misimamo mikali.

Kulingana na mdadisi wa siasa Gabrel Kauma, kinachoendelea kwa sasa ni kupimana tu lakini miungano halisi itajitokeza mwaka ujao.

“Kitu kingine ambacho kitafanya vigogo wa kisiasa kutoka kwenye viota vyao ni uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kuhusu Mswada wa kura ya maamuzi kuhusu BBI. Mswada huo una minofu kwa wanasiasa kwa kuwa unatoa nafasi za kugawana,” asema Kauma.

Mahakama ya Rufaa inatarajiwa kutoa uamuzi wake Agosti 20 na Bw Kauma anasema huu utakuwa ufunguo wa miungano ya kisiasa.

Bw Kauma anasema kwamba mviziano huu umejitokeza pia katika maeneo baada ya viongozi kukosa kuwapa mwelekeo uchaguzi mkuu ukikaribia.

“Kwa mfano, eneo la Mlima Kenya liko katika ulimbo wa kisiasa kwa kuwa Rais Kenyatta hajatangaza anayetaka kuwa mrithi wake. Kwa wakati huu ni dalili kwamba huenda hatatimiza ahadi yake ya kumunga Dkt Ruto ambaye ameunda chombo kujiandaa kugombea urais. Kuna dalili pia anaweza kumuunga Bw Odinga ambaye ni mshirika wake kwenye handisheki,” asema.

Mdadisi huyu anasema kwa kutopatia ngome yake mwelekeo wa siasa za urithi wake kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, Rais Kenyatta amewaacha washirika wake njia panda.

JAMVI: Namna Raila anapanga kuyumbisha akina OKA

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga ameweka mikakati tosha ya kuyumbisha muungano wa One Kenya Alliance (OKA) unaoshirikisha waliokuwa washirika wake katika muungano wa National Super Alliance (NASA) ili kuhakikisha hawataungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta walivyotarajia.

Mikakati yake inaonekana kuzaa matunda huku kukiwa na kila ishara kwamba huenda muungano huo ukatibuka.

Wadadisi wa siasa za humu nchini wanasema kwamba moja ya mikakati yake ni kuwagawanya vinara waliomtenga kusuka muungano huo ili kuunyima sura ya kitaifa.

Muungano huo ulileta pamoja vyama vya Wiper cha Stephen Kalonzo Musyoka, Amani National Congress (ANC) cha Musalia Mudavadi, Ford Kenya cha Moses Wetangula na Gideon Moi wa Kanu.

Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Bw Wetangula ambao walikuwa washirika wa Bw Odinga katika NASA wamekuwa wakisisitiza kuwa hawatamuunga mkono waziri mkuu huyo wa zamani kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Akihisi kuwa kutengwa na watatu hao kungemnyima baadhi ya kura alizopata kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 na akielewa kwamba wanaweza kushawishika kujiunga na mpinzani wake mkuu, Dkt William Ruto, Bw Odinga aliamua kuyumbisha OKA hata kabla muungano huo kuzinduliwa rasmi.

Kulingana na wadadisi, Bw Odinga alianza kwa kuhakikisha Rais Kenyatta hataunga muungano huo kwa kutumia wandani wake kudai kwamba kulikuwa na watu serikalini waliokuwa wakipanga siasa za urithi bila kumshirikisha.

Madai haya yalitolewa na kiranja wa wachache katika seneti Junet Mohamed aliyedai kwamba baadhi ya maafisa wakuu serikalini walikuwa wameteka mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI) kwa lengo la kumtenga Bw Odinga.

Madai hayo yalijiri wakati wa chaguzi ndogo za Matungu, Kabuchai na Machakos ambapo Musyoka, Mudavadi, Moi na Wetangula waliungana dhidi ya ODM na kutangaza kwamba watakuwa pamoja kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“Kwa ODM kudai kwamba watu wenye ushawishi walikuwa wamepanga siasa za urithi wakimtenga kiongozi wao na kwamba walikuwa wameteka mchakato wa BBI ilikuwa njama ya kuvuruga muungano wa OKA. Kumbuka wakati huo, Rais Kenyatta alimtembelea Odinga aliyekuwa akiungua na wakajitokeza pamoja kukagua miradi ya maendeleo,” asema mdadasi wa siasa Geff Kamwanah.

Hii ilifuatiwa na misururu ya mikutano kati ya Bw Odinga na Bw Moi, hatua iliyozua madai ya usaliti katika OKA.

“Moi alitajwa kuwa fuko wa Bw Odinga katika OKA jambo ambalo huenda lina ukweli kufuatia tangazo lake kwamba Kanu haitavunja muungano wake na Jubilee kujiunga na OKA. Kumbuka pia ODM kinasuka muungano na Jubilee. Kuna mkono wa Odinga kwa Kanu kukataa kujiunga na OKA,” asema mdadisi wa siasa Peter Wafula.

Duru zinasema kuwa baada ya juhudi za kushawishi Mudavadi, Musyoka na Wetangula kumuunga Bw Odinga kugonga mwamba, Rais Kenyatta alimshauri Bw Moi kujitenga na OKA na kuungana na Bw Odinga ishara kwamba ameamua kumuunga waziri mkuu huyo wa zamani.

Inasemekana kuwa Bw Odinga amekumbatia wapinzani wa vinara wa OKA katika ngome zao katika juhudi za kuwakata miguu kama njia moja ya kutibua muungano huo.

“Kujiondoa kwa ODM katika muungano wa NASA ni miongoni mwa mikakati ya Bw Odinga ya kuwaonyesha washirika wake kwamba anaweza kupata marafiki wapya wa kisiasa. Kwa mfano, amekumbatia Gavana wa Machakos Alfred Mutua ambaye ni hasimu wa kisiasa wa Bw Musyoka eneo la Ukambani. Hana wasiwasi eneo la Magharibi wanakotoka Mudavadi na Wetangula ambako amekuwa akipata kura kwa wingi na anataka kumkweza Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya,” asema Wafula.

Chama cha Maendeleo Chap Chap cha Dkt Mutua kilimuunga Rais Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 sawa na Kanu ingawa hakina mkataba wa ushirikiana na chama tawala cha Jubilee.

Kulingana na Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, chama hicho kimeamua kutafuta washirika wapya kinapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

“Tunataka kutafuta marafiki wapya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022. Hatuwezi kujifunga na marafiki wachache wanaotupatia masharti,” alisema Bw Sifuna.

Duru zinasema kwamba licha ya kujiondoa NASA, Bw Odinga amekuwa akizungumza na waliokuwa vinara wenza katika muungano huo binafsi hatua ambayo wadadisi wanasema ni ya kuwagawanya zaidi.

“Kwanza alihakikisha hawatapata baraka za Rais Kenyatta, pili akapanda mbegu ya usaliti na tatu akafanya wagawanyike ili kuhakikisha hawataungana na Dkt Ruto wote pamoja,” asema Wafula.

JAMVI: Joho atuliza boli uwanja wa siasa ukialika Nassir, Shahbal

VALENTINE OBARA na ANTHONY KITIMO

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho, anazidi kujiweka nyuma nyuma kuhusu ubabe wa kisiasa Pwani wakati ambapo vuta nikuvute yaendelea kushuhudiwa kati ya Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir na mfanyabiashara Suleiman Shahbal.

Mabw Nassir na Shahbal wanamezea mate tikiti ya Chama cha ODM kuwania ugavana wa Mombasa mwaka ujao wakati kipindi cha Bw Joho kitakapotamatika.

Kufikia sasa, Bw Joho hajatangaza mwanasiasa ambaye angependelea achukue nafasi yake na hali hii imewafanya wawili hao kujizatiti kujaribu kuthibitisha wametosha kukalia kiti hicho.

Wawili hao wamekuwa wakifuatana na viongozi wakuu wa ODM hasa Bw Odinga na Bw Joho hadharani na faraghani, hata wanapoendeleza mikutano na wananchi mashinani.

Tofauti na jinsi ilivyokuwa katika miaka iliyopita ambapo Bw Joho ndiye alikuwa akisimamia hafla kubwa za kisiasa au kuwakilisha Mombasa na hata Pwani katika hafla nyingine za kisiasa nje ya eneo hilo, gavana huyo ameonekana kuwaachia Mabw Nassir na Shahbal nafasi kabla wakutane katika debe la kupigania tikiti ya ODM kuwania ugavana mwaka ujao.

Hivi majuzi, baadhi ya wandani wa Bw Joho ambao ni madiwani Mombasa waliambia Taifa Jumapili kuwa Bw Joho ameamua kusudi kutoingilia mashindano ya wawili hao kwani msimamo wake unaweza kumharibia sifa alizopata kufikia sasa kisiasa.

Wiki iliyopita, Bw Shahbal alisafiri kwa ndege moja na Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt Oburu Oginga ambaye ni ndugu mkubwa wa Bw Odinga kwa hafla Kaunti ya Murang’a.

Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho akiwa na mfanyabiashara maarufu Suleiman Shahbal (kulia). Picha/ Maktaba

Duru ziliambia Taifa Jumapili kwamba walisafiri pamoja kwa hafla hiyo ya wanamuziki ambayo mgeni wa heshima alikuwa Bw Odinga, aliyeandamana na wanasiasa mbalimbali wakiwemo wabunge, maseneta, na magavana kutoka maeneo tofauti ya nchi.

“Shahbal pekee ndiye alikuwa kiongozi kutoka Pwani ambaye aliandamana na ‘Baba’ kwa hafla ya Murang’a. Alisafiri na Oburu Oginga kwa helikopta moja,” mdakuzi wetu akasema.

Bw Oginga huwa ni mmoja wa washauri wakuu wa kinara wa ODM na hivyo basi safari yake na Bw Shahbal ingeonekana kama mojawapo ya mikakati ya mfanyabiashara huyo kutafuta uungwaji mkono kwa Bw Odinga kupitia kwa ndugu yake.

Hii ni licha ya jinsi Bw Odinga husisitiza kuwa, chama chake kitaandaa kura ya mchujo kwa njia huru na ya haki ili yeyote anayetaka tikiti ya kuwania ugavana Mombasa apimane nguvu na wenzake debeni.

Katika mahojiano na Taifa Jumapili, Bw Shahbal alisema alihudhuria hafla hiyo kwa mwaliko wa kinara wa ODM.

“Nilipokea mwaliko kutoka kwa Bw Odinga ili niende Murang’a. Mkutano huo ulikuwa ni wa kupanga mikakati na tuliona hitaji la kuwa hapo. Nilikuwa nawakilisha eneo letu kwa msingi wa mwaliko niliopokea,” akasema Bw Shahbal.

Jukumu hilo la kuwakilisha Mombasa au Pwani kwa jumla katika hafla zinazohusiana na ODM zamani lilikuwa la Bw Joho, ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama.

Wakati Bw Odinga alipofanya ziara kaunti za Pwani hivi majuzi, ni Bw Nassir ambaye alikuwa katika mstari wa mbele kuandamana naye katika maeneo tofauti walikofanya mikutano ya hadhara.

Bw Joho alijitokeza wakati Bw Odinga alipohudhuria hafla ya kusherehekea Idd-Ul-Adha mjini Mombasa.

Hafla hiyo ambayo miaka iliyopita ilikuwa ikiandaliwa na gavana, mwaka huu iliandaliwa na Bw Nassir na hii ikawa ishara nyingine ya jinsi Bw Joho anavyozidi kujiondolea majukumu ya kusimamia siasa za Pwani.

Lakini Bw Nassir alisema anapoonekana akikutana na Bw Odinga au Bw Joho, haifai kuchukuliwa kwamba anataka wamtangaze kuwa ndiye ametosha kukalia kiti cha gavana.

“Uhusiano wangu wa karibu na Bw Odinga na Bw Joho haufai kuchukuliwa kumaanisha kuwa nataka waniunge mkono. Ninapotembea nao huwa ni kwa manufaa ya umoja wa chama. Wapigakura pekee ndio wanaweza kunichagua,” akasema Bw Nassir.

Katika hotuba zake, Bw Joho ambaye tayari alituma ombi kwa ODM kuwania tikiti ya kushindania urais, husisitiza kwamba lengo lake ni kujitosa katika siasa za kitaifa kwa hivyo amewaachia wengine nafasi ya kuongoza siasa za eneo hilo.

“Hivi karibuni nitaelekea kwa siasa za kitaifa nitawaachia hawa kina Abdulswamad washindane huku chini,” alisema Bw Joho katika mojawapo ya hafla alizohudhuria majuzi.

Bw Nassir amekuwa akitumia mafanikio yake ya ubunge Mvita kama kigezo kikuu cha kutafuta uungwaji mkono kwa siasa za ugavana.

Kufikia sasa, azimio lake limeungwa mkono na wabunge wengi wa Mombasa.

Kwa upande mwingine, azimio la Bw Shahbal limeungwa mkono na wandani wa karibu wa Bw Joho wakiwemo washauri wa kisiasa na madiwani.

Ni hali hii ambayo iliibua gumzo kuhusu uwezekano wa kuwa Bw Joho anamuunga mkono Bw Shahbal kisiri, ingawa gavana huyo husema ameacha uwanja uwe wazi.

Mfanyabiashara huyo aliwania ugavana mwaka wa 2013 na 2017 kupitia Chama cha Wiper na Jubilee mtawalia lakini hakufanikiwa kushinda.

Alihama Jubilee hivi majuzi lakini wiki iliyopita ilifichuka hajakamilisha mpango wa kuhamia ODM jinsi alivyokusudia.

Kando na wawili hao tikiti ya ODM kuwania ugavana yamezewa mate pia na Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi.

Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko ambaye awali alitaka kuwania ugavana kupitia ODM, baadaye alibadili nia na sasa anaunga mkono azimio la Bw Nassir.

Viongozi wengine ambao wanatarajiwa kuwania ugavana wa Mombasa mwaka ujao ni aliyekuwa seneta, Bw Hassan Omar na Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo.

Wawili hao ni wandani wa Naibu Rais William Ruto ambaye amepanga kuwania urais kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

JAMVI: Vizingiti vya Raila kugeuzwa kuwa mradi wa Uhuru

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta ya kushirikisha kiongozi wa ODM Raila Odinga katika ziara zake za kuzindua na kukagua miradi inayofadhiliwa na serikali kuu maeneo mbalimbali nchini imesawiriwa kama hatua ya kupiga jeki azma ya mwanasiasa huyo mkongwe ya kumrithi.

Lakini wadadisi wanatilia shaka kufaulu kwa mkakati huu kutokana na pingamizi kutoka viongozi wa maeneo husika kando na kuendeleza dhana kwamba Odinga ni “mradi wa serikali”.

Kwa mfano, hivi majuzi, kiongozi wa taifa aliandamana na Bw Odinga katika ziara yake, ya siku moja, katika eneo la Ukambani, hatua ambayo iliwakera zaidi viongozi kutoka eneo hilo.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alisema hakuwa na habari kwamba Waziri huyu Mkuu wa zamani angeandamana na Rais Kenyatta katika ziara hiyo.

Kwa upande wao maseneta; Mutula Kilonzo Junior (Makueni) na mwenzake Kitui Enock Wambua walimwonya Bw Odinga dhidi ya kutaka “kuvuna asichopanda.”

Vile vile, baadhi ya wanasiasa kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya wamepiga wazo la kumshirikisha Bw Odinga katika ziara ya Rais Kenyatta katika eneo hilo. Katika ziara hiyo ya siku tatu, Rais Kenyatta ameratibiwa kuzindua na kukagua miradi kadha ya maendeleo katika Kaunti za Kakamega, Trans Nzoia, Vihiga, Bungoma na Busia.

“Raila hafai kuandamana na Rais Kenyatta kwa sababu kiongozi wa taifa atakuwa akishughulikia masuala yanayowahusu watu wa eneo letu pekee. Akae kando kwa sababu mwezi jana, vigogo wetu kama Musalia Mudavadi na Moses Wetangula hawakumfuata Rais katika ziara yake ya Luo Nyanza,” akasema mbunge mmoja ambaye aliomba tulibane jina lake.

Lakini Seneta wa Kakamega Cleophas Malala alimlaumu Gavana wa eneo hilo Wycliffe Oparanya (Kakamega) kwa kuwatenga maseneta na wabunge katika maandalizi ya ziara hiyo “huku wakishirikisha wageni katika masuala yetu ya nyumbani,”

“Ziara ya Rais eneo la magharibi haifai kutumiwa kuendeleza masilahi ya kibinafsi ya mwanasiasa fulani kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Badala yake hii ni fursa yetu kama viongozi kuelezea rais matatizo yetu kama jamii,” akasema Bw Malala.

Akiongea alipozuru Kaunti ya Murang’a Jumanne, Odinga alithibitisha kuwa atazuru eneo hilo mara kadhaa akiandamana na Rais Kenyatta “kupalilia umoja kwa kitaifa kwa moyo wa handisheki tukielekea uchaguzi mkuu ujao.”

“Tumefika hapa na mnaona wazi kwamba Kenya yote imewakilishwa hapa. Mwamko mpya umeanza hapa nyumbani kwa S. K Macharia, mwanzo mpya wa kuunganisha Wakenya wote,” Odinga akasema.

“Kutoka hapa tutaelekea Magharibi mwa Kenya, kisha Nyanza ikifuatwa na Pwani na sehemu zote za nchini huku Uhuru akisimama upande mmoja nami nikisimamia upande mwingine,” akaongeza alipohudhuria hafla moja ya wanamuziki nyumbani kwa mmiliki wa shirika la habari la Royal Media Service, maeneo ya Ndakaini, eneobunge la Gatanga.

Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Dismus Mokua. itakuwa vigumu kwa Bw Odinga kukubalika katika ngome za wapinzani wake ambao vile vile wametangaza nia ya kuwania urais. Hii ni endapo Rais atafeli kushawishi waliokuwa washirika wa Odinga katika NASA, Mabw Musyoka, Mudavadi na Wetangula kumuunga Raila mkono tena.

“Hii ni kwa sababu tayari tumeona kuwa muungano wa NASA umesambaratika baada ya vyama vya ANC na Wiper kutangaza kujiondoa. Isitoshe, mnamo Alhamisi ODM pia ilifuata mkondo huo na kutangaza kujiondoa. Kwa upande mwingine chama cha Jubilee kimesalia vigae baada ya Naibu Rais William Ruto na wandani wake kuhamia chama kipya cha UDA ambacho kinaibua msisimko mkubwa katika ulingo wa siasa,” anasema Bw Mokua.

“Vile vile, kuna hatari ya hatua ya Rais Kenyatta kuandamana na Raila katika ziara zake za kikazi nchini kumfanya kiongozi huyo wa ODM kuonekana kama mradi wa serikali katika kinyang’anyiro cha urais 2022. Hali hii itamwathiri pakubwa kisiasa ikizingatiwa kuwa Raila ni mwanasiasa mwenye historia ya kujisimamia kivyake,” anaongeza.

Naibu Rais Dkt Ruto amekuwa akidai kuwa mambo yalianza kwenda mrama katika serikali ya Jubilee baada ya Bw Odinga “kuingia serikalini” kupitia handisheki mnamo Machi 9, 2018.

“Kwa hivyo, Raila na wenzake katika NASA waliojiunga na serikali na sisi wengine tukawekwa kando wanafaa kubebeshwa makosa yote ambayo yametokea katika serikali ikiwemo wizi wa pesa za kuwanunulia dawa wagonjwa wa corona,” akasema mwezi jana baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa moja mtaa wa Umoja, Nairobi.

Lakini Mkurugenzi wa Masuala ya Kisiasa katika ODM Opiyo Wandayi amepuuzilia mbali madai kuwa ziara za pamoja kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga zinalenga kumfaidi kisiasa waziri huyo mkuu wa zamani kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

“Raila amesema kila mara kwamba hatategemea uungwaji mkono kutoka kwa Rais Kenyatta endapo ataamua kuwania urais. Lakini ninavyoelewa ni kwamba msururu wa ziara ya pamoja ya vigogo hao wawili unalenga kuleta umoja nchini chini ya mwavuli wa Handisheki baada ya migawanyiko iliyosababishwa na vuguvugu la hasla,” anasema mbunge huyo wa Ugunja.

Kauli hii inakinzana na yake Mbunge wa Lugari Ayub Savula ambaye anashikilia kuwa Rais Kenyatta anapania kutumia ziara hizo kama jukwaa la kupigia debe azma ya Odinga ya kuingia Ikulu 2022.

“Ningependa kumwonya Raila kwamba njama hii itafeli kabisa. Kwanza asahau kabisa kura za eneo la Mlima Kenya kufuatia kushindwa kwa Jubilee katika chaguzi ndogo kadha, mmoja wa hivi punde ukiwa uchaguzi mdogo wa Kiambaa. Mojawapo ya sababu ya kushindwa kwa Jubilee ilikuwa ni dhana kwamba kimeungana na ODM kwa ajili ya kufanikisha ndoto ya Raila za kuingia Ikulu 2022,” anaeleza.

JAMVI: Hofu waliohamia Tangatanga ni ‘majasusi’

Na WANDERI KAMAU

LICHA ya baadhi ya wanasiasa kutangaza kuhamia katika mrengo wa ‘Tangatanga’ kutoka ‘Kieleweke’ na mirengo mingine ya kisiasa nchini, imeibuka kuwa baadhi yao wanaonekana kama “majasusi” wa kisiasa.

Ni hali ambayo imezua wasiwasi katika kundi hilo ambalo huwa linamuunga mkono Naibu Rais William Ruto, baadhi ya washirika wakuu wakisema wanapaswa kutahadhari kuhusu wanasiasa wanaotangaza kujiunga nao ama kurejea kwenye mrengo huo.

Katika siku za hivi karibuni, baadhi ya wanasiasa ambao wametangaza hadharani kurejea katika kundi hilo ni wabunge David Gikaria (Nakuru Mashariki) na Catherine Waruguru (Laikipia).

Wawili hao walikuwa wanachama wa kundi hilo kabla ya kugura na kujiunga na ‘Kieleweke.’

Wale ambao wametangaza kugura ‘Kieleweke’ na kujiunga na ‘Tangatanga’ katika siku za hivi karibuni ni wabunge Gathoni wa Muchomba (Kiambu), Kago wa Lydia (Githunguri) na Samuel Gacobe (Subukia).

Naibu Rais William Ruto akijibu salamu za wananchi alipowasili katika Shule ya Msingi ya Mary Immaculate iliyoko Laikipia akiwa na Catherine Waruguru (kulia) na Spika wa Seneti Ken Lusaka miongoni mwa viongozi wengine Juni 9, 2018. Picha/ Joseph Kanyi

Hata hivyo, hatua ya kurejea kwa wabunge Waruguru na Gikaria ndiyo imezua hofu katika mrengo huo, baadhi ya wabunge wakieleza tashwishi yao kuwa huenda wakawa “mawakala wa wapinzani wao.”

Kwenye mahojiano na Jamvi la Siasa, mshirika mmoja wa ‘Tangatanga’, alisema ni kinaya kuwa wabunge hao wanarejea katika kambi hiyo baada ya kutumia muda wao kumkosoa vikali Dkt Ruto na mipango yao kwa jumla.

“Hawa si watu wa kuaminika hata kidogo. Walikuwa nasi mwanzoni japo wakavuka katika mrengo pinzani. Wamekuwa wakitazama tukihangaishwa na serikali bila yao kututetea kwa namna yoyote ile. Wengine hata waligeuka na kuanza kumtusi Dkt Ruto. Ni vipi tena tunaweza kuwaamini?” akashangaa mbunge huyo ambaye hakutaka kutajwa.

Wasiwasi mkuu ulio katika ‘Tangatanga’ kuwa huenda wabunge wanaojiunga nao kwa kisingizio cha “kugura” ‘Kieleweke’ wakafichua mipango na mikakati ya kisiasa na Dkt Ruto, siri ambazo serikali itazitumia baadaye kuwahangaisha.

Baada ya kuhama kutoka ‘Tangatanga’ na kujiunga na Kieleweke, Bi Waruguru alimtaja Dkt Ruto kama “mwanasiasa mwongo na mnafiki, ambaye hapaswi kuaminiwa na yeyote.”

Bi Waruguru alitangaza kujitoa ‘Tangatanga’ Agosti mwaka uliopita, siku chache baada ya kukutana na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, aliyemtaja kuwa “mwanga wa kisiasa utakaowaongoza Wakenya kuelekea Kanani.”

“Niliondoka katika Tangatanga baada ya kugundua kuwa Dkt Ruto anapigania maslahi yake binafsi wala si ya ukanda wa Mlima Kenya. Niligundua pia kuwa wanasiasa wengi ambao wanamfuata ni kama wanashurutishwa kufanya hivyo, wala si maamuzi yao huru,” akasema Bi Waruguru.

Tangu wakati huo, mbunge huyo amekuwa akimsifu Rais Kenyatta, akimtaja kuwa mwanasiasa shupavu, atakayeleta mabadiliko kamili ya kisiasa na kiuchumi kabla ya kustaafu kwake.

Kama “zawadi” ya kumwasi Dkt Ruto, Bi Waruguru aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo.

Kutokana na mwelekeo huo, mbunge Rigathi Gachagu (Mathira) anasema ikiwa kutaibuka nafasi katika mrengo wa Tangatanga, basi wale “waliovumilia kuhangaishwa na serikali ndio wanaopaswa kuzingatiwa kwanza.”

“Taswira iliyopo ni kama zoezi la kujenga nyumba. Kuna baadhi ya wajenzi waliotutoroka tulipokuwa tukiweka msingi wa nyumba yetu, ijapokuwa sasa wanataka kurejea wakati tuko karibu kuikamilisha. Hatutawafukuza wakirejea. Hata hivyo, lazima nafasi zitakazoibuka zikabidhiwe wale ambao wamevumilia mateso ambayo tumekuwa tukielekezwa na serikali,” akasema mbunge huyo.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga akiwa na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Laikipia Catherine Waruguru (kushoto) Juni 09, 2020 katika Capitol Hill, Nairobi. Picha/ Maktaba

Licha ya hayo, wadadisi wa siasa wanasema kuwa sababu kuu ya mwelekeo huo ni ubabe uliopo miongoni mwa washirika wa Dkt Ruto kuhusu kiongozi anayefaa kuwa mgombea-mwenza wake.

Wanasema washirika wake wakuu wanahofia huenda wanasiasa wanaotangaza kujiunga na kundi hilo wakawa tisho kwao.

“Siasa zilizopo zinasukumwa na ubabe uliopo kuhusu kiongozi anayepaswa kuwa mgombea-mwenza wa Dkt Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Wanahisi wamehimili mawimbi ambayo mrengo huo umekuwa ukipitia, hivyo wanapaswa ‘kuzawadiwa’ kwa kutohama,” asema Bw Wycliffe Muga ambaye ni mdadisi wa masuala ya siasa.

Imeibuka kuwa moja ya makubaliano yaliyopo kati ya Dkt Ruto na viongozi wa Mlima Kenya ni kuwa lazima awatengee nafasi hiyo.

Baadhi ya viongozi wanaopigiwa upatu kupewa nafasi hiyo ni Bw Gachagua, mbunge Moses Kuria (Gatundu Kusini), aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri kati ya wengine.

Hata hivyo, Bi Wamuchomba anasema uamuzi wao ulichochewa na mwelekeo wa kisiasa ulio katika ukanda huo.

“Maamuzi yetu hayapaswi kumtishia yeyote. Yamechochewa na mwelekeo ambao wananchi wetu wamechukua,” akasema Bi Wamucomba.

Wachanganuzi wanasema kuwa kibarua kikubwa alicho nacho Dkt Ruto ni kuhakikisha kuwa taharuki miongoni mwa viongozi hao haigeuki kuwa hali itakayozua migawanyiko ya kisiasa.

“Ikiwa analenga kuibuka mshindi kwenye uchaguzi ujao, lazima Dkt Ruto afanye kila awezalo kuhakikisha washirika wake wamedumisha umoja,” asema Dkt Godfrey Sang’, ambaye ni mdadisi wa siasa.

JAMVI: Raila kuvizia ziara za Rais Ukambani kwaibua hofu

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga, ya kuandamana na Rais Uhuru Kenyatta alipozuru kaunti za Machakos na Makueni imewapa mchecheto washirika wa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka wanaohisi kwamba iliwaharibia fursa ya kushauriana na rais masuala ya kisiasa ya eneo lao.

Bw Musyoka alikiri mbele ya Rais Kenyatta kwamba hakutarajia kumuona Bw Odinga kwenye ziara hiyo huku wadadisi wakisema kiongozi wa nchi alitaka kutoa ujumbe kwa viongozi wa kisiasa wa Ukambani kwamba anampendelea waziri mkuu huyo wa zamani kuwa mrithi wake.

Bw Odinga na Bw Musyoka wamekuwa wakitofautiana kuhusu mkataba wa muungano wa NASA wa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017. Kiongozi wa Wiper anasema kwamba Bw Odinga alimsaliti kwa kukataa kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kwa upande wake, Bw Odinga anadai kwamba hitaji hilo katika mkataba wa NASA lilipitwa na wakati kwa kuwa hawakuunda serikali.

Bw Musyoka anaunga mkono handisheki kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta lakini ameapa kuwa hatamuunga mkono kiongozi huyo wa ODM kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa mara ya tatu.

Vyama vyao vinashirikiana na Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta na ODM imeanza kusuka muungano na chama hicho tawala huku Wiper kikishirikiana na Kanu, Amani National Congress (ANC) na Ford Kenya kubuni muungano wa One Kenya Alliance (OKA).

Kulingana na washirika wa Bw Musyoka, kujitokeza kwa Bw Odinga kwenye ziara ya Rais Ukambani kulimharibia kiongozi wao aliyetaka kutumia ziara hiyo kupigia debe azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi wa 2022 kwa kuonekana kuungwa mkono na rais.

Seneta wa Kitui Enock Wambua ambaye ni mwandani wa Bw Musyoka alisema kwamba Bw Odinga aliwadharau kwa kuzuru eneo hilo bila kualikwa.

“Tulishangaa kumuona Bw Odinga katika mkutano (katika eneo kunakojengwa bwawa la Thwake) ilhali tulitaka kuzungumza kivyetu na rais kuhusu masuala ya kijamii na kiuchumi ya eneo letu,” Bw Wambua alisema na kuongeza kuwa kujitokeza kwa Bw Odinga kuliwaharibia mipango yao.

Mchanganuzi wa siasa, Geff Kamwanah anasema kauli za wanasiasa wa Wiper ni sehemu ya siasa za kumrithi Rais Kenyatta kati ya Bw Odinga na Bw Musyoka.

“Wawili hao wanawania baraka za Rais Kenyatta na kwa hivyo, kujitokeza kwa Bw Odinga eneo la Ukambani kwa mwaliko wa rais, hakukufurahisha Bw Musyoka na washirika wake,” asema Bw Kamwanah.

Mchanganuzi huyu anasema kwamba hasira za washirika wa Bw Musyoka kwa Bw Odinga zinatokana na ujumbe ambao Rais Kenyatta alitaka kuwasilisha kwa kumwalika mshirika wake wa handisheki kwenye ziara yake Ukambani.

Kumekuwa na minong’ono kwamba Rais Kenyatta anawashawishi vinara wa OKA, akiwemo Bw Musyoka na vinara wenza katika NASA, kuungana chini ya Bw Odinga ili waweze kumshinda Naibu Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Ingawa Bw Odinga anasema kwamba hajatangaza azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, ameashirika nia yake ya kuendelea kushirikiana na Bw Musyoka.

Mbunge wa Mwingi North Musembi Nzengu, anasema kwamba Bw Odinga anafaa kuzungumza moja kwa moja na Bw Musyoka iwapo anataka kuungwa mkono na wakazi wa eneo la Ukambani.

Bw Kamwanah anasema kinachowauma wandani wa Bw Musyoka ni kuwa Rais Kenyatta hakualika vigogo wengine wa upinzani kwenye ziara yake eneo la Nyanza alikoanzisha miradi mikubwa ya maendeleo.

“Uwepo wa Bw Odinga ulivuruga mipango ya Bw Musyoka na hii ndiyo imefanya washirika wake kueleza kiongozi wao alivyohisi. Lakini ninasisitiza kuwa nia ya rais ilikuwa ya kuwasilisha ujumbe kwa viongozi wa Ukambani kwamba anamtambua Bw Odinga zaidi ya anavyomtambua Bw Musyoka,” asema na kuongeza: “Wanafaa kumlaumu rais kwa kumwalika Bw Odinga kwa kuwa hiyo ilikuwa ziara ya rais.”

Kulingana na Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua ambaye ni hasimu wa kisiasa wa Bw Musyoka eneo la Ukambani na ambaye pia ametangaza azima ya kugombea urais, Bw Odinga ni kiongozi wa kitaifa na wanaomlaumu kwa kujitokeza kwenye ziara ya rais eneo la Ukambani wanajidunisha.

“Bw Odinga ana haki ya kutembelea eneo lolote bila ruhusa kwa sababu ni kiongozi wa kitaifa,” asema.

Duru zinasema ingawa Rais Kenyatta anataka vigogo wa kisiasa wanaomuunga kuunda muungano mkubwa wa vyama vya kisiasa kumkabili Dkt Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, washirika wa Bw Musyoka wamekuwa wakimshinikiza asikubali kwa urahisi kuungana na Bw Odinga.

“Kuna kitu ambacho Bw Musyoka anaficha washirika wake kwa sababu amekuwa akizungumza na Bw Odinga bila kuwahusisha. Hii ndiyo sababu alikuwa mwepesi wa kusema mbele ya rais kwamba hajaketi na Bw Odinga kuzungumzia uchaguzi wa 2022,” asema mbunge mmoja wa Wiper ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Alisema kwamba Rais Kenyatta anatumia mbinu aliyotumia kwenye mazungumzo yaliyozaa handisheki yake na Bw Odinga kuwaleta pamoja vigogo wa kisiasa hasa vinara wenza wa NASA ambao wameshinikizwa na washirika wao kuchukua misimamo mikali kuhusu 2022.

Rais Kenyatta na Bw Odinga hawakuhusisha washirika wao wa kisiasa waliokuwa na misimamo mikali kwenye mazungumzo yaliyozaa handisheki yao ya Machi 2018.

JAMVI: Ruto hatarini kupoteza chambo chake kisiasa

VALENTINE OBARA na PATRICK LANG’AT

NAIBU Rais William Ruto yuko hatarini kupoteza ushawishi ambao amepata miongoni mwa wananchi wa tabaka la chini kufikia sasa.

Hii ni baada ya wapinzani wake wa kisiasa kuvamia chambo alichokuwa akitumia kunasa imani za wananchi hao kisiasa.

Kwa muda mrefu sasa, Dkt Ruto anayepanga kuwania urais mwaka ujao amekuwa akitumia falsafa ya kuinua kiuchumi wananchi wa matabaka ya chini anayewatambua kama ‘hustlers’, kama mbinu ya kujenga uchumi wa nchi endapo ataunda serikali ijayo.

Falsafa hii ilikosolewa na wapinzani wake wa kisiasa kama mbinu ya kusababisha mgawanyiko unaoweza kuleta vita kati ya matajiri na maskini nchini.

Lakini kwa wiki chache zilizopita, vigogo wengine wa kisiasa nchini wameonekana wakianza kushabikia falsafa hiyo hiyo ya kutilia maanani kuinua uchumi wa raia mashinani kama njia ya kuboresha uchumi wa kitaifa.

Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi katika hotuba zao wameanza kusisitiza kuhusu umuhimu wa serikali kuwekeza zaidi katika mbinu ambazo zitainua walalahoi kiriziki.

Ijapokuwa hatua hii huenda ikafanya raia ambao walikuwa wameanza kumtazama Naibu Rais kama mkombozi wao waone kuna viongozi wengine wenye uwezo wa kuwatendea yale ambayo Dkt Ruto alikuwa akiwaahidi, naibu rais na wandani wake wamejipiga kifua kwamba hiyo ni ishara tosha wapinzani wake wameingia baridi.

Kulingana na Seneta wa Murang’a, Bw Irungu Kang’ata, ambaye ni mmoja wa wandani wakuu wa Dkt Ruto, wapinzani wa naibu rais wamegundua kwamba ujumbe wake ulikuwa unapokewa vyema na raia wa kawaida.

“Ujumbe huo sasa umewapa wanasiasa wengine ajenda ya kuzungumzia. Hii ni hatua nzuri kwa vile inafanya siasa iwe ya kujadili masuala muhimu badala ya mambo ya kibinafsi na ukabila ambazo ni hatari kwa utulivu wa nchi. Inaridhisha kuwa Ruto ndiye alianzisha mazungumzo aina hii,” akaeleza.

Bw Odinga ambaye kwa siku kadhaa sasa amekuwa akionyesha dalili za kujiandaa kuwania urais 2022, alisema hitaji la kuinua wananchi wa ngazi za chini kiuchumi ili kukuza uchumi wa kitaifa ni mbinu inayowezekana kutekelezwa.

Katika taarifa alizotoa wiki iliyopita, Bw Odinga alieleza kuwa ukuaji wa uchumi wa nchi hustahili kufaidi kila mmoja bila ubaguzi, badala ya kunufaisha watu wa tabaka la juu pekee.

Kulingana naye, mpango huu unaweza kutekelezwa kwa kulenga wakazi wa maeneo ya mashambani na wafanyabishara wadogo mijini.

“Biashara ndogo ndogo ndizo uti wa mgongo kwa ukuaji wa uchumi. Huwezi kutegemea uwekezaji unaotoka nchi za kigeni pekee. Si jukumu la wawekezaji wa kigeni kuja nchini kukuza uchumi. Lengo lao ni kupata faida na kuzirudisha katika nchi zao. Lakini mwekezaji wa humu nchini atarudisha faida hizo kujenga uchumi wa nchi hii,” alisema Bw Odinga.

Kwa upande wake, Bw Mudavadi ambaye ameanzisha kaulimbiu ya ‘Uchumi Bora’ anapopanga kuwania urais mwaka ujao hushikilia kuwa uchumi wa nchi umezorota na unahitaji mikakati kabambe kufufuliwa ili kunusuru hali ya kiriziki kwa wananchi.

Sawa na Bw Odinga, kiongozi huyo wa ANC alisema katika taarifa kwamba hakutakuwa na mafanikio makubwa ikiwa serikali itaendelea kujishughulisha na utekelezaji wa miradi mikubwa wakati ambapo raia wa ngazi za chini wangali wanateseka kujitafutia riziki yao ya kila siku.

“Ni vizuri kujenga barabara na reli za kisasa, na pia viwanda vikubwa vya kuzalisha umeme. Lakini, je, hayo yote yatakuwa kwa manufaa gani wakati ambapo wananchi hawana uwezo wa kugharamia huzuma zinazotokana na miradi hiyo kwa sababu tumepuuza kuinua uwezo wao kupitia kwa miradi kama vile kilimo, afya na usambazaji maji safi?” akauliza Bw Mudavadi.

MASHINANI

Akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo eneo la Ukambani, Bw Musyoka alisisitiza kwamba amekuwa katika mstari wa mbele kutetea maendeleo ya mashinani kwa muda mrefu.

Hata hivyo, alisema misimamo yake haifanani ya ile ya Dkt Ruto, akieleza kuwa naibu rais ana falsafa ya kuwapa wananchi vya bwerere wala si kupeleka maendeleo ambayo yatawainua kiuchumi kwa muda mrefu.

“Kiongozi kama mimi sio kwenda kupeleka vitu na wilibaro. Sio kupeana vitu vya bwerere bali maendeleo ya kikweli kuanzia chini. Ni kupotosha watu unapowapa wilibaro kisha unadai hiyo ni njia ya kukuza uchumi kutoka chini. Aina hiyo ya kisiasa ni ya kuwapa wananchi vya bwerere na tulitoka huko,” akasema.

Licha ya kuwa misimamo hii inaweza kumvurugia Dkt Ruto hesabu zake za kunasa wapigakura wa mashinani kupitia kwa falsafa aliyoanzisha, naibu rais na wandani wake husema kilicho muhimu ni kwamba sasa viongozi wanajadiliana kuhusu mbinu wanazonuia kuinua uchumi badala ya kushambuliana kwa misingi ya ubinafsi ambayo haitakuwa na manufaa kwa umma.

Hata hivyo, baadhi ya wandani wa wapinzani hao wa Dkt Ruto walidai kuwa falsafa inayoenezwa na vigogo hao watatu ni tofauti na ile ya naibu rais.

Kulingana nao, falsafa ya naibu rais ilinuia kuwapa raia vitu vya bwerere ili wampigie kura uchaguzini na hilo halingewasaidia wananchi katika miaka ya usoni.

Kwa upande mwingine, wanadai kuwa falsafa ya vinara wao inagusia kwa mapana na marefu jinsi watakavyowekeza katika uchumi wa mashinani ili raia wa ngazi za chini wawe na pesa mifukoni mwao.

“Wao wamezoea kupiga domo bila mpango kwa njia ambayo maoni yao hupotea punde tu wanapoambiwa wajieleze kwa kina. Huu ni wakati ambapo watu wanafaa kukoma kupiga domo na waanze kueleza kwa kina jinsi watakavyoinua uchumi na kuwezesha wananchi kuwa na pesa mifukoni. Wakenya wachanganue kwa undani mapendekezo yote yanayowasilishwa kwao,” akasema Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna.

Kwa upande wake, Katibu Mwandalizi wa Wiper, Bw Robert Mbui alisema katika mahojiano ya runinga: “Kinachofaa kupingwa ni jinsi wanasiasa wanavyosambazia wananchi pesa. Vijana wanafaa kujua taifa linawategemea wao, kuwa wanaweza kuanzisha biashara bali si kusubiri serikali iwasaidie. Tunataka wajue serikali ipo kuwasaidia. Ukiambia watu kuwa utawapa pesa kujiendeleza watakuwa wavivu wakisubiri hizo pesa.”

Hata hivyo, mtaalamu wa masuala ya kiuchumi, Bw Mohamed Wehliye aliwarai wananchi wajihadhari na mapendekezo yote yanayotolewa na wanasiasa kwani viongozi hawaelezi mipango yao kwa uwazi inavyofaa.

Kando na mbinu ya kufufua uchumi kuanzia chini, mbinu nyingine zinazoweza kuzingatiwa ni kuanzia ngazi za juu kwenda chini au kuanzia katikati.

“Mbinu yoyote ile inayopendekezwa kuinua uchumi itahitaji rasilimali. Wanasiasa wanaotaka kuwania urais hawafai tu kutuambia kuhusu mwelekeo watakaochukua bali pia jinsi watakavyotatua tatizo la madeni ambayo watarithi ili wapate fedha wanazohitaji kufadhili mipango yao,” akasema, kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter.

JAMVI: Kalonzo alivyowazidimaarifa magavana wa Ukambani

Na BENSON MATHEKA

Juhudi za magavana wa kaunti tatu za Ukambani kuzima kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka asiwike kwenye ziara ya Rais Uhuru Kenyatta eneo lao ziligonga mwamba makamu rais huyo wa zamani alipomshawishi kiongozi wa nchi kubadilisha nia yake ya kufuta ziara hiyo.

Ikulu ilitangaza Jumatatu wiki hii kwamba Rais alikuwa ameahirisha ziara hiyo kwa sababu ya hofu ya kukiuka kanuni za kuzuia corona lakini ikasemekana ni tofauti za magavana hao na Bw Musyoka zilizofanya rais kuchukua hatua hiyo.

Magavana Alfred Mutua wa Machakos, Charity Ngilu wa Kitui na Kivutha Kibwana walikuwa wamedai kwamba Bw Musyoka alitaka kutumia miradi ambayo Rais alitembelea kupigia debe azima yake ya urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 na wakaonya kuwa hawangemruhusu kufanya hivyo.

“Hatutarajii wanasiasa wasio na la kufanya kutumia ziara hiyo kuonekana wakitembea pamoja na rais,” Dkt Mutua alisema.

Inasemekana viongozi walitofautiana kuhusu miradi ambayo ilipaswa kufunguliwa na Rais, hatua ambayo ilichangia ikulu kuahirisha ziara hiyo japo ilisema ni kwa sababu ya hofu ya corona.

Duru zinasema kwamba magavana hao hawakutaka Rais Kenyatta kumuidhinisha Bw Musyoka kama msemaji wa jamii ya Wakamba.

Wamekuwa wakimlaumu Bw Musyoka kwa kutumia madiwani wa chama chake walio wengi katika mabunge ya kaunti zao kuhujumu ajenda za serikali zao.

Imeibuka kuwa baada ya Ikulu kutangaza kuwa ziara ya Rais katika kaunti za Ukambani ilikuwa imeahirishwa, Bw Musyoka alimpigia simu Rais Kenyatta na kumshawishi abadilishe nia.

Kulingana na mwandani mmoja wa kiongozi huyo wa Wiper, Rais Kenyatta alikubali na ndipo akaita mkutano wa viongozi wa Ukambani Jumanne jioni ambapo alikubali kuzuru eneo hilo kwa kuzingatia kanuni za kuzuia msambao wa corona.

“Bw Musyoka alihisi kwamba kuahirishwa kwa ziara ya Rais eneo la Ukambani mara ya tatu kungetoa taswira mbaya kwa uongozi wa eneo hilo na hasa kwake kama msemaji wa jamii na ndio sababu aliwasiliana na rais. Anafahamu kwamba magavana hao wana azima zao na wanafikiri anatumia miradi waliyoanzishwa kujipigia debe lakini sivyo,” asema mwandani huyo aliyeomba tusitaje jina lake.

Kwenye mkutano wa Jumanne jioni, Rais Kenyatta alikubali kuzuru miradi ya serikali ya kitaifa katika eneo hilo Ijumaa lakini kwa kuzingatia kanuni za corona.

Hii, kulingana na wadadisi wa siasa, ilihakikisha kwamba hatahutubia mikutano ya kisiasa jambo ambalo ni pigo kwa magavana waliotaka kumpiga kumbo Bw Musyoka.

“Kwa kufanya hivi, rais aliepuka hali ambapo viongozi wa eneo hilo wangeendeleza siasa zao za mgawanyiko mbele yake,” alisema.

Ingawa awali ziara hiyo ilipangiwa kuchukua siku mbili, ilipunguzwa kuwa ya siku moja. Rais Kenyatta alizuru jiji la kitekinolojia la Konza na bwawa la Thwake katika kaunti za Machakos na Makueni.

Ingawa ziara hiyo ilishirikisha viongozi wa kaunti hizo, Bw Musyoka alitekeleza wajibu muhimu hatua ambayo wadadisi wa siasa wanasema ilikuwa ujumbe kwamba rais anamtambua kama kigogo wa siasa eneo hilo.

“Kwa maoni yangu, magavana hao hawakuweza kuzima Bw Musyoka walivyonuia hasa Gavana Mutua na Gavana Kibwana ambao wananuia kugombea urais. Angalau Gavana Ngilu amekuwa akihimiza Musyoka kuungana na vinara wenzake wa NASA katika siasa za kitaifa,” asema mdadisi wa siasa za Ukambani Bw Nicholas Kitetu.

Mnamo Jumatano, Bw Musyoka aliungana na baadhi ya viongozi wanaomuunga mkono kuzuru miradi ya serikali ya kitaifa ambayo Rais alitembelea Ijumaa na kupuuza madai kwamba anaitumia kujipigia debe.

“Wanachoogopa ( wapinzani) ni umaarufu wa Wiper na azima yangu ya urais. Wanajua haturudi nyuma,” alisema Bw Musyoka na kuongeza kuwa ziara yake ilikuwa ya kukagua miradi hiyo kabla ya rais kuitembelea.

Kulingana na Bw Kitetu, japo Rais aliepuka kuvunja kanuni za kuzuia corona kwa kutohutubia mikutano ya kisiasa, magavana wanaompiga vita Bw Musyoka wamepata pigo.

“Hakuna kati yao anaweza kudhihirishia rais kwamba ameshinda Bw Musyoka kwa umaarufu. Hilo ni bayana. Ikiwa ni kweli Bw Musyoka alimpigia simu rais kumshawishi abadilishe nia na kuzuru eneo hilo bila kuhutubia mikutano ya kisiasa, aliwashinda magavana hao waliodhani angetumia mikutano hiyo kujipigia debe kwa umma,” asema.

JAMVI: Madhara yanukia IEBC ikibanwa na muda wa maandalizi ya uchaguzi

Na CHARLES WASONGA

TANGAZO la Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwamba haitaweza kuweka mipaka mipya ya maeneo wakilishi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu ujao, limeibua wasiwasi kuhusu kiwango cha utayari wa tume kwa uchaguzi mkuu ujao.

Licha ya mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati kuwahakikishia maseneta kwamba ina uwezo wa kuendesha uchaguzi huo Agosti 9, 2022, inalalamikia uhaba wa fedha za kufadhili shughuli muhimu za maandalizi ya zoezi

.Kwa mfano, huku ikisalia miezi 13 pekee kabla ya Wakenya kuelekea debeni kuwachagua viongozi wapya, IEBC haijaanza shughuli ya usajili wa wapiga kura kwa wingi (mass voter registration.).

Aidha, haijanunua vifaa hitajika kwa uchaguzi huo kama mitambo ya kieletroniki (KIEMs kits) wala kuanza taratibu za utoaji zabuni ya uchapishaji wa karatasi za kupigia kura.

Kando na hayo, jopo la kuteua makamishna wapya wanne halijakamilisha shughuli hiyo huku nafasi ya Afisi Mkuu Mtendaji ikiwa ingali wazi tangu Ezra Chiloba alipopigwa kalamu mnamo Agosti 2019.

Hii ndio maana licha ya Bw Chebukati kuwahakikishia maseneta kwamba tume hiyo ina uwezo wa kuendesha uchaguzi wadadisi wanasema ina muda mfupi kuandaa zoezi hilo.

Kulingana nao, hali hii kwa kiwango fulani kimechangia na hatua ya serikali na wabunge kuelekeza juhudi zao katika masuala ya marekebisho ya katiba badala ya uchaguzi mkuu.

“Licha ya kwamba wanasiasa na serikali walifahamu fika kwamba tarehe ya uchaguzi mkuu ujao ni Agosti 9, 2022, kwa miaka mitatu iliyopita wanasiasa na maafisa wa serikali wamejikita zaidi katika mchakato wa BBI wala sio maandalizi ya uchaguzi. Kila mara, IEBC imekuwa ikilalamikia uhaba wa fedha za kuendesha shughuli zake lakini hakuna anayeshughulikia suala hilo,” asema Bw Felix Otieno, wakili na mtaalamu katika masuala ya uchaguzi.

Aidha, mtaalamu huyo anamlaumu Rais Uhuru Kenyatta kwa hali inayoikumba IEBC akisema kiongozi wa taifa alijivuta kutangaza wazi nafasi nne za makamishna waliojiuzulu mnamo 2018.

Wao ni aliyekuwa naibu mwenyekiti Connie Nkatha, Dkt Paul Kurgat na Margaret Mwachanya Wanjala pamoja na Dkt Roselyn Akombe aliyejiondoa kabla ya marudio ya uchaguzi wa urais mnamo Oktoba 26, 2017.

“Kujivuta huku kwa Rais Kenyatta kutangaza nafasi hizi kuwa wazi ndiko kulichangia IEBC kuendesha shughuli zake kwa karibu miaka mitatu ikiwa na makamishna watatu pekee. Wao ni mwenyekiti Bw Chebukati, Boya Molu na Profesa Abdi Guliye. Nadhani hii ndio maana tangu 2017 tume hii haijaendesha shughuli zozote za usajili wa wapiga kura ilivyofanya kabla ya uchaguzi wa 2017,” anasema Bw Otieno.

Kulingana na ripoti ya mwanasheria Johns Kriegler aliyechunguza kiini cha ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007, muundo wa tume ya uchaguzi unapaswa kuwa mkamilifu miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu.

“Hii ndio itawezesha makamishna kupata uzoezi tosha wa kuendesha uchaguzi kwa njia ambayo itavutia imani ya washiriki wote. Bila kufanya hivyo, udhaifu fulani unaweza kutokea na hivyo kuibua hali ya sintoifahamu kuhusu uamunifu wa shughuli nzima ya uchaguzi,” ikasema ripoti hiyo iliyotolewa iliyokabidhiwa Rais mstaafu Mwai Kibaki mnamo Mei 15, 2008.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa kuhusu Sera na Utatuzi Mizozo (ICPC) Ndung’u Wainaina anasema baadhi ya wanasiasa wameanza kuzungumzia uwezekano wa kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu ujao kutokana na dhana kuwa IEBC haiko tayari kwa zoezi hilo.

“Huu ni unafiki mkubwa. Ni wanasiasa wawa hawa, ambao wamekuwa wakiendeleza siasa za BBI ambayo tayari imefyoza karibu Sh20 bilioni pesa za mlipa ushuru huku IEBC ikinywa fedha za maandalizi ya uchaguzi. Uchaguzi mkuu haowezi kuahirishwa isipokuwa ikiwa Kenya itavamiwa na taifa jirani,” anaeleza.

Kulingana na kipengele cha 102 (5) cha Katiba kipindi cha kuhudumu kwa bunge kinaweza tu kuongezwa ikiwa Kenya itakuwa ikishiriki vita na taifa jirani.

“Muhula bunge unaweza tu kuongezwa kwa miezi sita au muda usiozidi miezi 12 kupitia hoja itakayoungwa na angalau thuluthi mbili ya idadi jumla ya wabunge,” kipengele hicho kinasema.

Kikatiba, muhula wa bunge hufikia kikomo, wakati wa uchaguzi mkuu mwingine.Kutokana na hali hii, Bw Wainaina anaunga mkono pendekezo la Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki kwamba mchakato wa marekebisho ya Katiba kupitia Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) usitishwe ili juhudi zote zielekezwe katia maandalizi ya uchaguni mkuu ujao.

“Jopo la uteuzi wa makamishna wapya linaloongozwa na Bw Elizabeth Muli likamilisha shughuli hiyo haraka ili makamishna wanne wapya wateuliwe. Wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC pia ujazwe na tume itengewe fedha zaidi za kufadhili maandalizi ya uchaguzi mkuu ili kuepusha ghasia zilizoshuhudiwa katika chaguzi za hapo nyuma,” anaeleza.

Itakumbukwa kwamba dosari katika sajili ya wapiga kura na utendakazi wa vifaa vya kielektroniki vilivyotumiwa katika uchaguzi mkuu wa 2017, ndio baadhi ya sababu zilizochangia kufutuliwa mbali kwa matokeo ya uchaguzi wa urais.

Hii ni kwa sababu, zabuni ya ununuzi wa vifaa hivyo ilitolewa kwa pupa, na pasina sheria kufuatwa, kwa sababu IEBC ilibanwa na wakati.Hii ni kwa sababu, mwenyekiti wa Bw Chebukati na wenzake sita, waliteuliwa Desemba 30, 2016 miezi minane kabla ya siku ya uchaguzi (8/8 2017).

Makamishna hao hawakuwa na muda tosha wa kujifahamisha na utendakazi wa asasi hiyo muhimu.Katika bajeti iliyosomwa bunge mwezi huu, Waziri wa Fedha Ukur Yatani aliitengea IEBC Sh15 bilioni za kufadhili maandalizi ya uchaguzi, fedha ambazo Bw Chebukati anasema ni finyu mnamo.

2022: Kuna dalili Uhuru atasema ‘Raila Tosha’

Na BENSON MATHEKA

DALILI za wazi kuwa Rais Uhuru Kenyatta huenda akamtangaza kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga kuwa mrithi wake, zilijitokeza baada ya kiongozi wa nchi kuahidi kwamba wataendelea kushirikina kwa manufaa ya Wakenya siku zijazo.

Akizungumza akiwa Kisumu alipoongoza sherehe za 58 za Madaraka Dei, Rais Kenyatta alisema kwamba ataendelea kushirikiana na Bw Odinga ili kuhakikishia Kenya ustawi.

“Ninataka kusema hapa leo kwamba hata iweje siku zijazo, nitaendelea kushirikiana naye na viongozi wote wa Kenya na Wakenya ili kufanya Kenya, Afrika Mashariki na Afrika kuwa bora, iliyoungana zaidi na yenye ustawi,” alisema Rais.

Ingawa wawili hao wamekuwa wakitetea ushirikiano wao kufuatia handisheki yao ya Machi 9 2018, wamekuwa wakisema haihusu uchaguzi mkuu wa 2022, tamko la Jumanne linaashiria kuwa kuna uwezekano Rais Kenyatta atamtangaza Bw Odinga kuwa chaguo la mrithi wake.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba kauli yoyote ya kiongozi wa nchi wakati wa sherehe ya kitaifa kama Madaraka haiwezi kupuuzwa.

“Kumekuwa na kila dalili kwamba ushirika wao wa kisiasa unahusu uchaguzi mkuu wa 2022 japo wamekuwa wakikanusha. Kwa kusema ataendelea kushirikiana naye ni kumaanisha kwamba handisheki yao inahusu zaidi ya kubadilisha katiba,” alisema mchanganuzi wa siasa Peter Katana.

Anasema kauli ya rais ililenga kuhakikishia ngome yake ya Nyanza kwamba hatamsaliti baadhi ya viongozi wa ODM wanavyohofia.

Mapema mwaka huu, baadhi ya viongozi wa ODM walidai kwamba washirika wa rais walikuwa wakipanga siasa za urithi kwa kumtenga Bw Odinga.

Hii ilifuatia madai kwamba Rais Kenyatta alikuwa akiunga muungano wa One Kenya Alliance unaoshirikisha mwenyekiti wa chama cha Kanu Gideon Moi, kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula wa Ford Kenya.

Hofu ya viongozi wa ODM, ilimfanya Rais Kenyatta kuchukua hatua ya kuhakikishia Bw Odinga kuwa handisheki ingali imara na hana nia ya kumsaliti.

Duru zinasema Rais Kenyatta ameanza mikakati ya kupatanisha vinara wa One Kenya Alliance na Bw Odinga kwa lengo la kuepusha migawanyiko ambayo Naibu Rais William Ruto anaweza kutumia kushinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“Kuna mikakati ya kupatanisha vyama vinavyounga BBI na kilele chake kitakuwa kumtangaza Odinga kuwa nahodha wa timu moja kubwa itakayomkabili Dkt Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Kwa maoni yangu, hivi ndivyo rais aliashiria alipoahakikishia wafuasi wa Bw Odinga eneo la Nyanza kwamba atamuacha,” alisema mbunge mmoja wa Jubilee ambaye aliomba tusitaje jina asionekana kumwaga mtama bila idhini.

Hata hivyo mwenyekiti wa chama cha ODM, John Mbadi alitaja kauli ya rais kuwa sababu kuu ya handisheki.

“Nafikiri kile ambacho rais alisisitiza ni kwamba handisheki yao ilihusu siku zijazo za nchi na sio kwa maslahi ya kibinafsi,” alisema Bw Mbadi.

Akizungumza na kituo kimoja cha redio cha lugha ya Dholuo mnamo Jumatatu, Bw Odinga aliambia wakazi wa ngome yake ya Nyanza kwamba uchaguzi mkuu wa 2022, utakuwa uwindaji mkubwa na kwamba eneo lao halitakosa minofu. Wachanganuzi wa siasa wanasema hii pamoja na kauli ya rais kwamba atatembea naye siku zijazo ni sawa na kuwaandaa wafuasi wa Bw Odinga kwa tangazo la “Raila tosha” kabla ya 2022.

“Hii ilikuwa kuwaandaa wafuasi wa Bw Odinga kwa tangazo kubwa. Kuna uwezekano litakuwa ni baba anatosha. Muhimu kukumbuka ni kuwa Rais Kenyatta amewahi kusema kwamba rais anaweza kutoka nje ya jamii mbili zilizowahi kutoka rais,” alisema mchanganuzi wa siasa Jacob Kituyi.

Kwenye hotuba yake ya Madaraka Dei, Rais Kenyatta alimshehenezea sifa Bw Odinga kwa hatua waliyochukua kutuliza nchi baada ya joto la kisiasa lililopanda baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Hata hivyo baadhi ya wanasiasa wanahisi kwamba kauli hiyo ilikuwa ya kisiasa kufurahisha wafuasi wa Bw Odinga katika Nyanza tu.

“Mwelekeo kwa siasa za urithi utabainika baada ya Agosti mwaka huu kwa kutegemea hatima ya mswada wa kura ya maamuzi,” asema mdadisi wa siasa, Geff Kamwanah.

JAMVI: Ruto kupokelewa kishujaa Kisumu kunaashiria nini?

Na CHARLES WASONGA

HISIA mseto imeibuka kuhusu mapokezi mazuri ambayo Naibu Rais William Ruto alipokea mjini Kisumu Jumanne wakati wa sherehe za Siku Kuu ya Madaraka Dei mjini Kisumu.

Wandani wake, haswa wamechangamkia hatua ya wakazi wa eneo la Kondele kumshabikia Dkt Ruto kwa mbwembwe na hoi hoi alipokuwa akiondoka uga mpya wa michezo wa Jomo Kenyatta baada ya kukamilika kwa sherehe hizo zilizoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta Jumanne.

Baadhi yao walisema mapokezi hayo yaliashiria kuwa wakazi wa kitongoji hicho na Nyanza kwa ujumla sasa wamezinduka na kuamua kukumbatia sera za vuguvugu la hasla za kutetea masilahi ya wanyonge.

Lakini wafuasi wa ODM wamepuuzilia mbali dhana hiyo wakisema wakazi wa Kondele, na Kisumu kwa ujumla sasa “wamekomaa na wamebadilisha mienendo yao baada ya kuingiwa na injili ya maridhiano iliyoasisiwa na handisheki kati ya Rais Kenyatta na Raila Odinga.”

Kinyume na matajio ya wengi, wakazi hao, haswa vijana, walisimamisha msafara wa Naibu Rais wakimtaka awahutubie licha ya kwamba wao ni wafuasi sugu Bw Odinga ambaye ni kiongozi wa ODM.

Lakini Dkt Ruto, ambaye ni hasimu mkubwa wa kisiasa wa Waziri huyo mkuu wa zamani, alijibu kwa kuwapungia mikono kwa sababu gari lenye mitambo ya sauti lilikuwa mita kadhaa nyuma.

Mtaa wa Kondele, haswa karibu na daraja la juu kwa juu (Flyover), umekuwa kitovu cha machafuko ya kisiasa tangu 2007 ambako wafuasi wa ODM walikabiliana na polisi wakipinga kile walichodai ni Bw Odinga kuibiwa kura za urais.

Kwenye mahojiano na Jamvi, mshiriki mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) eneo la Nyanza, Eliud Owallo, alisema kuwa mapokezi ambayo Dkt Ruto alipata Kisumu yanaashiria kuwa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu ujao zitaongozwa na sera wala sio siasa za vyama au watu binafsi.

“Yale ambayo Wakenya walishuhudia Kisumu na haswa eneo la Kondele juzi, yanaonyesha watu wa Nyanza wamezinduka. Wameona mwanga na ifikapo uchaguzi mkuu ujao, bila shaka watafanya maamuzi yao sio kwa misingi ya maagizo kutoka chama fulani au mwanasiasa fulani, bali sera ambazo zitabadilisha maisha yao,” akasema.

“Hivi karibuni Dkt Ruto atarejea Nyanza kwa ziara ya kukutana na wananchi moja kwa moja na kusikiza matakwa ya mahasla mashinani,” akaongeza Bw Owalo ambaye mnamo 2013 alihudumu kama mkurugenzi mkuu wa sekritariati iliyoshirikisha kampeni za urais za Bw Odinga.

Kwa upande wao wabunge Nelson Koech (Belgut) na Oscar Sudi (Kapseret) walisema kuwa mapokezi ambayo Dkt Ruto alipata Kisumu ni kielelezo cha kiwango ambacho “injili” ya hasla imepenyeza katika ngome hiyo ya kisiasa ya Bw Odinga.

“Sasa wakazi wa Kondole na Kisumu kwa ujumla sio mali ya mtu binafsi. Wameonyesha kuwa hawataki kuachwa nyuma katika wimbi hili la mageuzi. Bila shaka wanataka kuvuna matunda ya sera za kiuchumi zinazoratibiwa na vuguvugu la hasla. Wamechoshwa na ahadi tasa za ODM ambazo hazijawakwamua kutoka lindi la umasikini miaka nenda miaka rudi,” Bw Sudi akaambia Taifa Jumapili.

Kwa upande wake Bw Koech aliweka ujumbe shukrani, kwa lugha ya dholuo, kwenye kaunti yake ya twitter uliosema hivi: “Erokamano Kisumo. Wabiro duogo kendo Kondele” (Asanteni watu wa Kisumu. Tutarejea tena Kondele).

Wandani wengine wa Naibu Rais waliochangamkia mapokezi yake Kisumu ni aliyekuwa Seneta wa Kakamega Bonny Khalwale na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

Lakini Mwenyekiti wa ODM John Mbadi alipuuzilia kauli za wakereketwa wa UDA wakazi wa Kisumu wamekumbatia chama hicho akizitaja kama “ndoto za mchana”.

“Jumanne haikuwa siku ya siasa. Ilikuwa ni siku ya kipekee kwa wakazi wa Kisumu na hata Kondele kwani kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hili, wao ndio walikuwa wenyeji wa sherehe muhimu ya kitaifa kama Madaraka Dei. Bila shaka ilikuwa ni siku ya fuhara na nafasi yao ya kukaribisha viongozi wote kwa msisimko, akiwemo Naibu Rais William Ruto,”

“Wale wanaodai msisimko ulioshuhudiwa miongoni mwa wakazi wa Kondele unaonyesha kuwa wamebadili msimamo wao wa kisiasa wanaota mchana. Kisumu na Nyanza, ingali ngome ya ODM na itasalia kuwa hivyo,” akaeleza Bw Mbadi ambaye ni kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa.

Lakini mchanganuzi wa siasa za Luo Nyanza Tom Mboya anakinzana kimawazo na mbunge huyo wa Suba Kusini.

Kulingana na mhadhiri huyu wa Chuo Kikuu cha Maseno, yale yaliyoshuhudiwa Kisumu Jumanne yanaashiria kuwa siasa za eneo hilo na Nyanza kwa ujumla yamechukua mkondo mpya.

Kwamba wakazi na viongozi wa kisiasa wameng’amua kuwa hawatapoteza chochote kwa kukumbatia vyama au mirengo tofauti ya kisiasa kando na wake Bw Odinga na chama chake cha ODM.

“Naamini kuwa mapokezi mazuri aliyopewa Naibu Rais kule Kondele, yalipitisha ujumbe fulani wa kisiasa. Aidha, ilikuwa ni onyo kwa Raila Odinga na chama chake cha ODM kwamba endapo hawatapigania mahitaji ya kimsingi ya wakazi hao basi waweza kuunga mkono mirengo pinzani 2022,” anaeleza Dkt Mboya.

Anabashiri kuwa wakazi wa Nyanza huenda wakaendeleza mtindo waliouanza 2013 wa kuwachagua wabunge na hata magavana wasiodhaminiwa na ODM. Kwa mfano, katika uchaguzi mkuu wa 2017, ODM ilipoteza viti vya ubunge vya Kisumu Mjini Mashariki, Kisumu Mjini Magharibi na Uriri vinavyoshikiliwa na Olago Aluoch (Ford Kenya), Shakeel Shabiri (Kujitegemea) na Peter Masara (Kujitegemea), mtawalia.

JAMVI: Mwamko mpya Pwani 2022

Na WAANDISHI WETU

UKANDA wa Pwani huenda ukapata magavana wa kwanza wa kike katika uchaguzi mkuu ujao, iwapo wanasiasa walioonyesha maazimio kufikia sasa hawatalegeza kamba.

Kaunti tatu za Pwani tayari zimevutia wanasiasa wa kike walio na ari ya kuondoa dhana kuwa wadhifa huo unastahili kuwa wa wanaume pekee.

Wanasiasa hao ni mbunge wa Malindi Aisha Jumwa anayemezea mate ugavana wa Kaunti ya Kilifi, Naibu Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani anayetaka kupanda ngazi uongozini katika kaunti hiyo kisha yupo mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko anayemezea mate ugavana wa Mombasa naye mtaalamu wa haki za kijamii, Bi Umra Omar anaangazia wadhifa huo katika Kauntui ya Lamu.

Wanne hawa wameonyesha nia ya kutaka kuwarithi magavana Amason Kingi, Salim Mvurya, Hassan Joho na Fahim Twaha mtawalia.

Kaunti nyingine za Pwani ni Taita Taveta na Tana River ambapo kufikia sasa hakuna mwanamke aliyejitokeza wazi akiazimia kuwania ugavana 2022.

Mnamo wikendi, Bi Jumwa aliendelea kusisitiza kuhusu azimio lake la kutaka kuwa mrithi wa Bw Kingi.

Mbunge huyo aliye mtetezi sugu wa Naibu Rais William Ruto, alisema hayo alipohudhuria mazishi eneo la Rabai.

Baadaye kupitia kwa mtandao wa Twitter, alitangaza kwamba ‘Kilifi itaongozwa na mwanamke 2022’.

Azimio lake limepokea uungwaji mkono kutoka kwa wanawake wa kaunti hiyo ambao tayari wameanza kumpigia debe.

Aliyekuwa Seneta Maalum wa Jubilee, Bi Emma Mbura alisema umefika wakati kwa wakazi wa Kilifi kuwa na kiongozi mwanamke ambaye ataendeleza ajenda ya kupiga vita umaskini.

“Sisi wanawake ndio tunaelewa shida tunazozipitia shuleni, hospitalini na shida ya maji ambapo inawalazimu kina mama kutembea mwendo mrefu ili kupata huduma hizo,” akasema.

Aliongeza kuwa wanaume katika Kaunti ya Kilifi wamekuwa wakieneza chuki na siasa za kuwagawanya wanawake ili kutoa twasira kuwa wanawake ni adui wao wenyewe.

“Mara hii akina mama tutazunguka na kukesha hadi tuhakikishe kuwa kiti cha ugavana tunampa mwenzetu. Tunataka kuona uongozi wa mwanamke utatusaidia vipi,” akasema Bi Mbura.

Katika Kaunti ya Kwale, hali isiyo ya kawaida imeibuka ambapo gavana wa sasa amejitokeza wazi kumpigia debe naibu wake amrithi. Kwa kawaida humu nchini, uhusiano kati ya magavana na manaibu wao katika kaunti nyingi huwa si mzuri.

Lakini Gavana Mvurya amekuwa akimpigia debe Bi Achani, akiamini kwamba ndiye kiongozi bora aliye na uwezo wa kuendeleza mbele miradi ya maendeleo iliyokuwa imeanzishwa na utawala wake.

Katika hafla ya majuzi zaidi, gavana huyo alimsifu naibu wake kama anayestahili kumrithi. Alitoa mfano wa Tanzania ambapo Rais Samia Suluhu alipokezwa mamlaka kikatiba baada ya kifo cha aliyekuwa Rais John Pombe Magufuli.

Akizungumza katika mazishi ya Askofu Morris Mwarandu mwezi uliopita, gavana huyo alisema ni Bi Achani pekee atakayeweza kuendeleza mafanikio ambayo kaunti hiyo imeshuhudia tangu 2013.

“Ni vile hapa ni mazishini sitaongea zaidi. Lakini Askofu aliniambia ‘muda wako unaisha hivyo ututayarishie siku za usoni’. Naibu gavana ametayarishwa. Mnaona Tanzania hakujawa na msukosuko. Katika taasisi ni lazima watu watayarishwe,” akasema.

Kwa upande wake, Bi Mboko ambaye ni mwandani wa Gavana Joho, amekimezea mate kiti hicho kwa muda sasa ingawa kufikia sasa hajajitokeza kimasomaso.

Azimio lake lilikuwa tayari limepokea uungwaji mkono kutoka kwa wanawake ndani na nje ya kaunti hiyo hasa kupitia kwa vuguvugu la wanawake wanaounga mkono handisheki, la Embrace.

Katika Kaunti ya Lamu, Bi Umra Omar aliambia Taifa Jumapili katika mahojiano ya awali kwamba hataruhusu tamaduni zinazodhalilisha wanawake eneo hilo kuzima azimio lake la kutaka kuwa gavana.

Bi Omar ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kijamii, ndiye mwanzilishi wa shirika la Safari Doctors ambalo limepokea tuzo tele kimataifa kwa kujitolea kufikisha huduma za matibabu kwa umma kupitia njia ya barabarani, angani na baharini.

“Mimi ni mwanamke wa Kibajuni lakini hilo halitanizuia kupigania kile ninachoamini ni haki. Naamini kiongozi mwema hafai kuogopa visiki vilivyo mbele yake. Kwa hivyo nahimiza wanawake hapa wasiruhusu ubaguzi dhidi ya wanawake”, akasema.

Mwanaharakati wa Lamu, Bi Raya Famau, alisifu uamuzi wa Bi Omar kuwania ugavana katika kaunti hiyo.

Bi Famau alisema hatua hiyo ni bora kwa wanawake wa Lamu ambao kwa miaka mingi wamekandamizwa na mila na desturi za kibaguzi ambazo hupendelea wanaume.

“Ubaguzi dhidi ya wanawake unatokana na ubinafsi. Tunaweza kuinuka dhidi ya kila aina ya ubaguzi tunaorushiwa na kuongoza si kaunti hii pekee bali nchi nzima. Hakuna tatizo lolote katika kuwa na gavana wa kike, mbunge, seneta au hata kiongozi wa taifa,” akasema Bi Famau.

Tangu ugatuzi ulipoanza kutekelezwa mwaka wa 2013, Kenya imekuwa na magavana watatu pekee wa kike ambao ni Anne Waiguru (Kirinyaga), Charity Ngilu (Kitui) na Joyce Laboso (Bomet). Bi Laboso alifariki katika mwaka wa 2019 baada ya kuugua saratani.

Ripoti za Charles Lwanga, Maureen Ongala, Valentine Obara na Kalume Kazungu

JAMVI: Wandani wauma Raila kichwa huku 2022 ikibisha hodi

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga anakabiliwa na kizungumkuti kikubwa kuamua wagombeaji atakaowaunga mkono katika viti mbalimbali 2022 hususan katika ngome yake ya Nyanza.

Hii ni baada ya kubainika kwamba wandani wake wa karibu katika eneo hilo wanamezea mate viti vya ugavana katika kaunti nne za Homa Bay, Migori, Siaya na Kisumu kwa tiketi ya chama hicho cha chungwa.

Kwa mfano, katika kaunti ya Homa Bay, kiti cha ugavana kimevutia mwenyekiti wa ODM John Mbadi (Mbunge wa Suba Kusini), Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Gladys Wanga (mwenyekiti wa ODM Homa Bay) na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero.

Katika kaunti ya Migori wandani wa Bw Odinga wanaomezea mate kiti cha ugavana ni Seneta wa kaunti hiyo Ochilo Ayacko na mbunge wa Suna Mashariki ambaye pia ni mkurugenzi wa uchaguzi katika chama cha ODM, Junet Mohamed.

Huku Profesa Anyang’ Nyong’o akipania kutetea kiti chake Kisumu, anakoseshwa usingizi na seneta wa kaunti hiyo Fred Outa ambaye pia ni mshirika wa karibu wa Bw Odinga.

Katika kaunti ya Siaya anakotoka Waziri huyo Mkuu wa zamani, amejipata katika njia panda aunge nani kati ya Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Seneti Seneta James Orengo na mkurugenzi wa masuala ya siasa katika ODM, Mbunge wa Ugunja James Opiyo Wandayi.

Ni kutokana na hali ambapo wadadisi sasa wanaonya kwamba hali hii huenda ikavuruga uthabiti wa ODM katika ngome hiyo hasa ikizingatiwa kuwa tayari inakabiliwa na ushindani kutoka kwa chama cha People Democratic Party (PDP), chake Gavana wa Migori Okoth Obado.

Mbali na PDP, chama kipya cha United Democratic Alliance (UDA) chake Naibu Rais William Ruto pia kimeanza kupenya Luo Nyanza kupitia juhudi za mwanasiasa Eliud Owalo. Hii ni kando na vyama vinginevyo ikiwemo Ford Kenya ambacho kilitwaa ubunge wa Kisumu Mjini Magharibi 2017 kupitia Bw Olago Aluoch.

“Kwa misingi hii, wagombeaji ambao watahisi kuwa hawatapata haki wakati wa mchujo wa ODM bila shaka watagura na kusaka tiketi za vyama vingine au waamue kuwania kama wagombea huru,” anasema Dkt Tom Mboya.

Kwa mujibu wa mchanganuzi huyu wa masuala ya siasa za Nyanza, Bw Odinga anakabiliwa na kibarua kikuu kuhakikishia wagombeaji kuwa haki itatendeka wakati wa mchujo wa chama hicho.

Ugavana

“Hata hivyo, kibarua kikubwa kitakuwa katika kiti cha ugavana hasa ikizingatiwa kwamba tayari wandani wake wameanza kavutana inavyodhihirika katika kaunti ya Siaya baina ya Orengo na Wandayi huku ugavana wa Homa Bay uking’ang’aniwa na Mbadi, Wanga, Kidero miongoni mwa wengine,” anaeleza Dkt Mboya ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Maseno.

Itakumbukwa kwamba katika chaguzi kuu za miaka ya 2013 na 2017, baadhi ya wanasiasa waligura ODM na kujiunga na vyama vingine baada ya kutendewa hiana katika kura za mchujo. Wengine waliamua kuwania nyadhifa mbalimbali kama wagombeaji huru.

Kwa mfano, mnamo 2013 Obado aligura ODM na kuwania ugavana kwa tiketi ya PDP baada ya kunyimwa tiketi ilhali alimwangusha Profesa Edward Oyugi katika mchujo wa ODM. Baadaye Bw Obado alimbwaga Profesa Oyugi katika uchaguzi mkuu na kuwa gavana wa kwanza wa Migori.

Wanasiasa wengine kama vile Bw Olago, Onyango K’Oyoo na James Opiyo walifaulu kushinda viti vya ubunge vya Kisumu Mjini Magharibi, Muhoroni na Awendo, mtawalia kwa tiketi za vyama vya Ford Kenya na PDP baada ya kupokonywa ushindi katika mchujo wa ODM.

Wilson Agenya ambaye ni mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Nairobi anasema itakuwa muhimu zaidi kwa Bw Odinga kuhakikisha kuwa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) haiingiliwi itakapokuwa ikiendesha kura za mchujo haswa za viti vya ugavana.

“Wananchi wapewe nafasi ya kuteua wagombeaji bora watakaoisaidia ODM kuvuna ushindi katika uchaguzi mkuu wa 2022. Wagombeaji nao wasitumie ukaribu wao na Odinga kuwahadaa wapiga kura ili wawateue,” akasema Profesa Agenya.

Hata hivyo, msomi huyo anabashiri kuwa kivumbi kitashuhudiwa katika mchujo wa ugavana ambapo wagombeaji wanatarajiwa kutumia mbinu zote, ikiwemo kutumia fedha kupata tiketi ya ODM.

Kwa mfano, katika kaunti ya Homa Bay inaaminika kuwa Dkt Kidero atatumia utajiri wake kuboresha nafasi yake ya kupata tiketi ya ugavana huku Bi Wanga akitarajiwa kutumia cheo chake cha mwenyekiti wa ODM katika kaunti hiyo na uungwaji kutoka kwa wanawake kufanikisha ndoto zake.

Vile vile, kuna minong’ono kwamba Bw Mbadi atategemea wadhifa wake kama Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM kupata tiketi ya chama hicho kuwania ugavana wa Homa Bay.

“Hii ndio maana, Bw Odinga akiwa kiongozi wa ODM ana kazi kubwa kuhakikisha kuwa bodi ya NEB inaendesha majukumu yake kwa njia huru na haki bila kuingiliwa kwa njia yoyote. Watakaoshindwa wakubali matokeo na kuunga mkono washindi ili kudumisha umoja ndani ya chama hicho,” akasema msomi huyo.

JAMVI: Mirindimo mipya ya Tangatanga baada ya BBI kuzikwa

Na WANDERI KAMAU

MRENGO wa ‘Tangatanga’ umepata msisimko mpya wa kisiasa katika ukanda wa Mlima Kenya na Bonde la Ufa, kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu kufutilia mbali mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Mara tu baada ya uamuzi huo, Naibu Rais William Ruto alitoa ujumbe “kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuipenda Kenya.”Dkt Ruto alisema huu ni wakati nchi iheshimu maamuzi yanayotolewa na taasisi huru.

Sherehe hizo zilitanda katika maeneo ya Kati, hasa Kaunti za Muranga, Nyeri na Nyandarua, viongozi wa mrengo huo wakiwaongoza wafuasi wao “kusherehekea” ushindi.Wabunge wanaoegemea mrengo huo walisema hatimaye mahakama imedhihirisha kuwa wao ndio “watetezi halisi” wa wananchi.

“Huu ni uamuzi unaooyesha wazi sisi ndio watetezi halisi wa wananchi. BBI ni njama na mpango wa watu wachache kujitengeneze nyadhifa za uongozi. Kama ambavyo tumekuwa tukishikilia, huu ni wakati kwa viongozi na serikali kuangazia masuala ya maendeleo na kufufua uchumi wa nchi. Mageuzi ya kikatiba ni jambo tunaloweza kushughulikia baadaye,” akasema mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu) ambaye ni miongoni mwa washirika wakuu wa karibu wa Dkt Ruto.

Kauli kama hizo zilitolewa na wabunge Rigathi Gachagua (Mathira), Faith Gitau (Nyandarua), Milicent Omanga (Seneta Maalum) kati ya wengine ambao walikuwa miongonu mwa wale waliopiga kura ya ‘La.’

Katika kaunti za Baringo, Uasin Gishu na maeneo mengine ambayo ni ngome za kisiasa za Dkt Ruto, wananchi pia walijumuika pamoja kushabikia uamuzi huo.

Bunge la Kaunti ya Baringo lilikuwa miongoni mwa yale yalipiga kura kupinga mswada huo.Licha ya msisimko huo, wadadisi wa siasa wanasema kuwa ingawa huenda hilo likaonekana kama “ushindi” kwa wakati huu, bado ni mapema kwa mrengo huo kuanza kusherehekea.

Wanasema ingali mapema kudhani mchakato huo umevurugika kabisa, kwani bado kuna nafasi kwa wale wanaouendesha kuakata rufaa katika Mahakama ya Rufaa.

“Huu ni mchakato wa kisiasa na kisheria kwa wakati mmoja. Kwa wale wanaounga mkono BBI, wana nafasi kukata rufaa mahakamani. Kisiasa, huu ni mradi wa Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga. Ingawa kwa wakati huu wanaonekana kupata pigo kisiasa, wao ni wanasiasa, hivyo huenda wakabuni njia mbadala kutimiza malengo yao,” Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Mnamo Ijumaa, mwenyekiti-mwenza wa Sekretariati inayoendesha mchakato huo, Bw Junet Mohamed, alisema wanaandaa kundi la mawakili ambao watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo wiki ijayo.

Bw Mohamed, ambaye pia ni mbunge wa Suna Mashariki, alitaja uamuzi huo kama “mapinduzi ya kisheria” yanayoendeshwa na majaji wanaolenga “kulipiza kisasi” dhidi ya Rais Kenyatta.

“Uamuzi huu ni ushirikiano fiche uliopo kati ya baadhi ya maafisa wa Idara ya Mahakama na wanaharakati ili kuilemaza serikali na utendakazi wake. Ni njama zinazoendeshwa kwa ushirikiano na wanasiasa wanaoipinga serikali na juhudi za kuiunganisha nchi ambazo zinazoendelezwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga,” akasema Bw Mohamed.

Hata hivyo, wadadisi wanaeleza kuwa licha ya baadhi ya viongozi wanaounga mchakato huo kupuuza maamuzi ya mahakama, ni hatua ambayo inaonekana kumjenga kisiasa Dkt Ruto na viongozi ambao walijitokeza wazi kuipinga BBI.

Baadhi yao ni kiongozi wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua na Gavana Kivutha Kibwana wa Makueni.Mdadisi wa siasa Godfrey Sang’ anasema taswira ambayo imewekwa na uamuzi huo nyoyoni mwa Wakenya wengi ni kuwa Dkt Ruto ni “mtetezi wa wananchi” hata ingawa huenda hilo lisiwe kweli.

Anaeleza kuwa ingawa Dkt Ruto hakuwa amejitokeza moja kwa moja kuupinga mpango huo, kauli zake kuwa kuna masuala muhimu yanayopaswa kushughulikiwa kwanza ndiyo yanaonekana kuwateka wengi.

“Ujenzi wa dhana ni muhimu sana katika siasa. Hilo ndilo huwavutia ama kutowavutia wananchi. Ilivyo sasa, Dkt Ruto na washirika wake wanaonekana kuwa washindi kutokana na uamuzi huo, ikizingatiwa wengi wao wameadhibiwa kutokana na misimamo yao kisiasa,” akasema Dkt Sang.

Baadhi ya washirika wake waliopoteza nyadhifa zao ni Seneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) kama Kiongozi wa Wengi Kwenye Seneti, Seneta Susan Kihika (Nakuru) kama Kiranja wa Wengi kwenye Seneti, Seneta Irungu Kang’ata (Murang’a) kama Kiranja wa Wengi kati ya wengine.

“Ni wazi wanasiasa hao wataonekana kama ‘mashujaa’ miongoni mwa wafuasi wao kwani wataanza kujipigia debe kwa misingi ya masaibu ya kisiasa ambayo wamekuwa wakipitia. Ni mbinu ambayo Dkt Ruto amekuwa akitumia pia, hasa kwa kutengwa serikalini na Rais Kenyatta. Bila shaka, huu ni wakati mwafaka kwao kujijenga kisiasa,” asema Dkt Sang.

Hata hivyo, wadadisi wanasema bado ni mapema, kwani hatima kamili ya uamuzi huo bado haifahamiki.“Ingawa hii ni nafasi yao kujijenga, itabidi wangoje hadi mwelekeo kamili wa mchakato huo ufahamike,” akasema.

JAMVI: ‘Baba’ anajua kwamba UhuRuto wanamkata miguu kule Nyanza?

Na LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta na Naibu wa Rais William wameanza mchakato wa kutaka kumlemaza kisiasa kiongozi wa ODM Raila Odinga katika eneo la Nyanza.

Huku Rais Kenyatta akilenga kumpokonya Bw Odinga udhibiti wa maeneo ya Kisii na sehemu ya Kaunti ya Migori, Naibu wa Rais Ruto analenga kunyakua vigogo wa ODM na wasomi kutoka maeneo ya Luo Nyanza.

Rais Kenyatta, kupitia kwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i, analenga kudhihirisha ubabe wake kupitia uchaguzi mdogo wa Bonchari ambapo vyama vya ODM na Jubilee vimesimamisha wawaniaji.

Chama cha Jubilee kimesimamisha mbunge wa zamani wa Bonchari Zebedeo Opore huku aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kawi nchini (EPRA) Mhandisi Pavel Oimeke akipeperusha bendera ya ODM kwenye uchaguzi huo mdogo utakaofanyika Jumanne.

Hii ni mara ya kwanza kwa ODM na Jubilee kushindana kwenye chaguzi ndogo tangu Rais Kenyatta na Bw Odinga kuafikiana kushirikiana, almaarufu handisheki, mnamo 2018.Chama cha ODM kimekuwa kikishutumu Jubilee kwa kutumia maafisa wa polisi kuhangaisha viongozi wake wanaoendesha kampeni za Bw Oimeke.

Alhamisi, polisi walivamia nyumbani kwa Gavana wa Kisii James Ongwae – anayeongoza kampeni za ODM katika eneobunge la Bonchari – na kufukuza Seneta wa Kisii Profesa Sam Ongeri, Mwakilishi wa Kike Kisii Bi Janet Onge’era na mwenzake kutoka Migori Bi Pamela Odhiambo waliomtembelea.

Polisi walidai kuwa viongozi hao walikuwa wakifanya mkutano kinyume na marufuku ya kufanya mikutano ya kisiasa iliyotolewa na siasa kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.Chama cha ODM pia kinadai kuwa serikali imekuwa ikitumia machifu na wazee wa Nyumba Kumi kupigia debe Bw Opore.

“Chama cha ODM ni lazima kishinde uchaguzi mdogo wa Bonchari ili kudhihirisha kwamba Bw Odinga angali anadhibiti kisiasa eneo la Kisii. Iwapo chama cha Jubilee kitashinda, ujumbe utakuwa kwamba ODM imepoteza umaarufu,” anasema Bw Mark Bichachi, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

KUHANGAISHA ODM

Wadadisi wa masuala ya kisiasa pia wanasema kuwa hatua ya polisi kuhangaisha viongozi wa ODM katika eneobunge la Bonchari ni ishara kwamba uhusiano baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga tayari umesambaratika.

Baadhi ya viongozi wa Jubilee waliambia Jamvi kuwa Rais Kenyatta pia analenga Kaunti ya Migori iliyo na maeneobunge manane.Wakazi wa maeneobunge ya Kuria Magharibi na Kuria Mashariki zimekuwa zikipiga kura upande wa serikali.

Rais Kenyatta pia analenga kuvutia upande wake Gavana Okoth Obado aliye na idadi kubwa ya wafuasi katika Kaunti ya Migori.Kwa upande mwingine, ujumbe wa Naibu Rais Ruto ukiongozwa na Eliud Owalo, ulikutana na viongozi mbalimbali wa ODM pamoja na wasomi kutoka Nyanza.

Viongozi hao walikutana katika Hoteli ya Hermosa jijini Nairobi.Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho ni aliyekuwa gavana wa Kisumu Jack Ranguma na waziri wa zamani Dalmas Otieno.

Wengine waliokuwa katika mkutano huo ni mbunge wa zamani wa Rangwe Martin Ogindo, aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya simiti ya East Africa Portland na kampuni ya sukari ya Muhoroni Sugar Co Ltd, John Nyambok, mkuu wa biashara ndogondogo wa Benki ya KCB Christopher Migunde na mtaalamu wa masuala ya elimu Profesa David Otieno Okelo.

Mkutano huo uliandaliwa na Bw Owalo ambaye sasa ni mwandani wa Dkt Ruto baada ya kuachana na Bw Odinga.Dkt Ruto, hivi karibuni, alisema kuwa amekubaliana kufanya kazi na magavana zaidi ya 20 pamoja na mawaziri ambao hawajajitokeza hadharani kutokana na hofu ya kupoteza viti vyao.

Lakini mbunge wa Suba Kusini John Mbadi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM, amepuuzilia mbali viongozi wa Nyanza waliokutana na ujumbe wa Dkt Ruto.

Bw Mbadi aliambia Taifa Jumapili kuwa viongozi hao waliokutana na ujumbe wa Dkt Ruto hana ushawishi wowote wa kisiasa katika eneo la Nyanza.Mbunge Maalumu wa ODM Rose Nyamunga pia amepuuzilia mbali viongozi hao akisema kuwa ‘wanatafuta pesa za kampeni kutoka kwa Naibu wa Rais’.

“Raila ndiye kiongozi wa pekee aliye na mamlaka ya kufanya mazungumzo na viongozi kutoka maeneo mengine ya nchi. Waliokutana na ujumbe wa Ruto wanapoteza wakati na wanasumbuliwa na njaa,” akadai Bi Nyamunga.

JAMVI: Mwaura alivyojikwaa na kujiponza kisiasa

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya Chama cha Jubilee (JP) kumtimua aliyekuwa Seneta Maalum, Bw Isaac Mwaura, kutoka chama hicho imezima nyota ya mojawapo ya wanasiasa waliotazamwa kwa matumaini makubwa.

Bw Mwaura alipoteza nafasi yake rasmi Jumanne, baada Spika wa Seneti, Kenneth Lusaka kutangaza nafasi yake kuwa wazi.Hali iliendelea kumzidia maji Bw Mwaura baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumtangaza aliyekuwa Seneta wa Samburu, Bw Sammy Leshore, kuchukua nafasi yake.

Hata hivyo, masaibu hayo yalimwandama licha yake kupata agizo la mahakama kuizuia Jubilee kujaza nafasi yake.Kutokana na mwelekeo huo, wadadisi wanasema hatua hiyo ni pigo kubwa kwa Bw Mwaura, kwani alionekana kama mwanasiasa ambaye angeleta mwanga mpya, hasa kwa walemavu.

“Kama mwanasiasa aliyekuwa akiendelea kujijenga kisiasa, hilo ni pigo kubwa kwake. Angetumia nafasi hiyo kujijenga badala ya kuanza kufarakana na wakubwa wake katika Jubilee,” asema Bw Martin Andati, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Kenyatta mnamo 2006, Bw Mwaura alijiunga na chama cha ODM kama mwanachama wa kawaida, lakini akapanda ngazi hadi kuwa Katibu Mkuu wa Walemavu.Kwenye uchaguzi mkuu wa 2007, Bw Mwaura alishiriki pakubwa kumpigia debe Bw Odinga.

Kutokana na hilo, aliteuliwa kuwa mshauri mkuu kuhusu masuala ya makundi yaliyotengwa katika jamii katika Afisi ya Waziri Mkuu kati ya 2010 na 2012.Mnamo 2013, aliteuliwa kama mbunge maalum na ODM.Mwaka 2016, aligura ODM na kujiunga na Jubilee.

Alijaribu kuwania ubunge katika eneo la Ruiru, kaunti ya Kiambu, lakini akashindwa kwenye shughuli za mchujo.Hata hivyo, “aliokolewa kisiasa” na Rais Uhuru Kenyatta baada ya kuteuliwa kama Seneta Malum mnamo 2017, kuwakilisha watu wenye ulemavu. Kutokana na kutimuliwa kwake, wadadisi wanamlaumu kwa “kujikwaa mwenyewe kisiasa.”

Wakosoaji wake wanamtaja kuwa mwanasiasa anayetapatapa na asiyekuwa na msimamo wa kisiasa hata kidogo.“Baada ya kuteuliwa na Jubilee, Bw Mwaura alikuwa na nafasi nzuri kujiboresha kisiasa ili kuhakikisha hangekumbwa na vikwazo alivyokumbana navyo 2017,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Wanasema ukakamavu wake ulionekana mnamo 2014, wakati aliwaongoza wanachama wa ODM kulalamikia kuondolewa kwa majina yao katika sajili ya upigaji kura katika hali tatanishi.

Ni kwenye kizaazaa hicho ambapo alikuwa miongoni mwa waliowakabili watu waliovuzua ghasia kwenye uchaguzi huo maarufu kama “Men in Black.”

Licha ya ukakamavu huo, masaibu ya kiongozi huyo yanadaiwa kuanza Desemba mwaka uliopita, baada ya kutangaza kujiunga na chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto.

Bw Mwaura alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa kusherehekea ushindi wa mbunge Feisal Bader (Mswambweni) katika Kaunti ya Kwale.Kwenye mkutano huo, alisema imefika wakati kwa “vijana kuchukua uongozi wa nchi, ambao umeendelea kushikiliwa na familia chache.”

“Kuanzia leo mimi ni mwanachama wa ‘Hustler Nation (Muungano wa Watu Maskini). Tumechoshwa na uongozi wa familia chache tangu tulipojipatia uhuru. Wakati umefika tuikomboe Kenya,” akasema.

Alizilaumu za Mzee Jomo Kenyatta na marehemu Daniel Moi, akisema zimeitawala Kenya kwa zaidi ya miaka 50.Matamshi yake yalionekana kumkera Rais Kenyatta, aliyesema kuwa ikiwa kuna yeyote katika chama hicho aliyechoshwa na uongozi wake, basi aondoke.Rais pia alijitetea vikali, akisema wananchi ndio walimchagua.

“Kama umechoshwa na uongozi wa watu wa familia chache basi waendee wananchi uchaguliwe pia kwani hata nafasi ulio nayo ni kitokana na kura yangu,” akasema Rais, kwenye kauli iliyoonekana kumlenga Bw Mwaura.

Ni kuanzia hapo ambapo wadadisi wanasema “kitumbua chake kilianza kuingia mchanga.”“Huwezi kumtukana kiongozi aliyekupa kazi na utarajie kuendelea kuwa kazini. Ilikuwa wazi lazima angetimuliwa chamani. Huo ni ukaidi wa wazi,” asema Bw Muga.

Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, Bw David Murathe, anamtaja Bw Mwaura kama “mwanasiasa mwenye tamaa” anayetegemea “kuvuna tu kutoka kwa vyama vya kisiasa.”

“Alisaidiwa na ODM kwa kuteuliwa kama mbunge maalum. Jubilee ilimteua kama Seneta Maalum. Aligura Jubilee na kujiunga na UDA akilenga kupata uteuzi baada ya uchaguzi mkuu ujao,” akasema Bw Murathe.

Kando na Bw Mwaura, maseneta wengine wanaotarajiwa kukabiliwa na chama kwa madai ya kukiuka kanuni za chama ni Bi Millicent Omanga, Victor Prengei, Mary Seneta, Falhada Dekow na Naomi Waqo.

Kama Bw Mwaura, watano hao wanalaumiwa kwa kukiuka kanuni za chama, hasa kwa kujiunga na mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao umekuwa ukimpigia debe Dkt Ruto kuwania urais 2022.

Watetezi wa Bw Mwaura wanamtaja kuwa mwanasiasa mwenye shujaa na mwenye msimamo huru, anayeadhibiwa kutokana na imani zake za kisiasa.

Maseneta James Orengo (Siaya) na Irungu Kang’ata (Murang’a) wanamtaja kuwa mwanasiasa mchanga, aliye na mustakabali mzuri kwenye siasa za Kenya.

Wawili hao wanasema vyama vya kisiasa vinapaswa kuwa huru katika maamuzi yake, wala havipaswi kudhibitiwa na viongozi wake vinapofanya maamuzi muhimu.

JAMVI: Mbio za Ngilu kutuliza zogo, uasi katika ODM

HATUA ya Gavana Charity Ngilu wa Kitui ya kukutanisha Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga na washirika wake James Orengo, Otiende Amollo na Wycliffe Oparanya walipotofautiana kuhusu mswada wa BBI kabla ya kuharamishwa na mahakama zilituliza joto katika uongozi wa chama hicho cha chungwa.

Baada ya kuona hatari iliyokodolea macho washirika wake wa kisiasa wa miaka mingi, Bi Ngilu aliwasiliana na pande zote na wakapanga kukutana kwa Bw Odinga ambapo alihimiza umuhimu wa kudumisha umoja katika chama hicho kikubwa cha upinzani.

Kabla ya mkutano huo, Bw Orengo na Bw Otiende walikuwa wametofautiana na msimamo wa viongozi wa ODM bungeni kuhusu pendekezo la kubuniwa kwa maeneo bunge mapya 70.

Msimamo wao ulichukuliwa kama uasi ikizingatiwa kwamba Bw Odinga alikuwa akiunga pendekezo hilo na kuagiza wabunge wote wa ODM kuunga mswada huo.

Hali ilizidi kuwa mbaya pale Bw Otiende aliposusia mkutano ambao Bw Odinga aliitisha nyumbani kwake na ikabidi apokonywe wadhifa wake wa Naibu mwenyekiti wa Kamati ya bunge kuhusu sheria (JLAC).

Hii ilikuwa siku moja baada ya kukutana na Bw Oparanya nyumbani kwake Kakamega. Ikizingatiwa kuwa baadhi ya wandani wa Bw Odinga walishuku uhusiano wa Gavana huyo na Naibu Rais William Ruto, mkutano wa watatu hao ulizua taharuki ndani ya ODM kwamba walikuwa na njama dhidi ya ODM na Bw Odinga.

Duru zinasema kuwa Bi Ngilu aliwaambia wanasiasa hao kwamba walikuwa wakitoa picha mbaya kwa kuanika wazi tofauti za chama chao hasa baada ya kumvua Bw Otiende wadhifa wake katika JLAC. Kulingana na wandani wa gavana huyo, ni viongozi hao watatu wa ODM waliomuomba Bi Ngilu kuzungumza na Bw Odinga.

“Mama ameshirikiana kisiasa na wanasiasa hao na kwa vile hawangeweza kumkabili baba kufuatia madai kwamba walikuwa wameasi msimamo.wake walimuomba awe mpatanishi,” alisema msaidizi wa Bi Ngilu ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Bi Ngilu hakukanusha wala kukubali kuwa alikutanisha viongozi hao kwa Bw Odinga.?“Tulizungumzia masuala kadhaa kutoka BBI, siasa na hali ya sasa ya janga la corona nchini. Tulikubaliana kwamba kuna haja ya dharura ya kuendelea kuungana kwa kuwa kuna adui mkubwa mbele yetu,” Bi Ngilu alisema baada ya mkutano huo.

Gavana huyo ambaye ni kiongozi wa chama cha Narc alisema kwamba muhimu kwake ni kuona nchi ikiwa imeungana.?“Sisi sote tunataka kilicho bora kwa Wakenya,” alisema bila kufafanua zaidi.

Duru zinasema kwamba japo joto ilipanda kwenye mkutano huo, Bi Ngilu aliweza kuwapatanisha na Bw Odinga.?Viongozi hao walimhakikishia Bw Odinga kwamba wangali waaminifu kwa chama cha ODM na sio waasi inavyochukuliwa walipokosoa BBI.

Mnamo Alhamisi, mahakama kuu ilitaja kubuniwa kwa maeneobunge 70 ambayo viongozi hao walikosoa katika BBI kuwa haramu. Pia ilisema mchakato wote wa BBI ulikuwa haramu.

Inasemekana kwamba Bw Orengo na Bw Otiende walishikilia kuwa kauli zao kuhusu mchakato huo zilitokana na tajiriba yao ya uanasheria na sio kudharau viongozi wa vyama.

Japo inasemekana Bi Ngilu aliwaacha wakijadili masuala ya ndani ya ODM uhusiano wake na viongozi hao na msimamo wake wa kisiasa umefanya wamuamini. Yeye na Bi Ngilu wamewahi kuwa wanachama wa chama cha Social Democratic Party SDP miaka ya tisini. Bw Orengo, Oparanya na Bi Ngilu walihudumu katika baraza la mawaziri katika serikali ya muungano wa Narc mwaka wa 2003 kwa hisani ya Bw Odinga?.

“Wako na historia ndefu ya uhusiano wa kisiasa na kumtumia Bi Ngilu kuwapatanisha au kuwaombea radhi kwa Bw Odinga ni kutambua uwezo wake. Kwa kuwa anatoka nje ya ngome zao za Nyanza na Magharibi na ikizingatiwa msimamo wake wa kisiasa kulisaidia kurekebisha hali katika chama hicho cha upinzani,” alisema mchanganuzi wa siasa David Wanyama.

Baada ya mkutano huo, ODM kilisema kimemrejesha Otiende katika JLAC ingawa nafasi yake ilikuwa imetwaliwa na mbunge wa Ruaraka TJ Kajwang. Bw Oparanya alikiri kwamba mkutano huo ulikuwa wa kuzima hofu kwamba wameasi ODM.

“Mkutano wetu unafaa kuondoa uvumi kwamba kuna uasi katika ODM kwa kuwa haya ni madai ya mahasimu wetu wa kisiasa. Nashukuru dada yetu Mheshimiwa Ngilu kwa usaidizi wake,” alisema.

JAMVI: Yaelekea huu ndio mwanzo mpya EAC

Na WANDERI KAMAU

MSISIMKO mpya wa urafiki kati ya Kenya na Tanzania umeibua maswali kuhusu ikiwa mataifa hayo yamefungua ukurasa mwingine kwenye mahusiano yake ambayo yalikuwa yamedorora.

Hilo pia limezua maswali ikiwa hatimaye nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeanza safari mpya kwenye mahusiano na mwingiliano wao.

Hilo linafuatia ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania nchini Jumanne na Jumatano wiki hii, ambapo uwepo wake ulizua msisimko wa aina yake nchini.

Kwenye ziara hiyo, Rais Suluhu na mwenyeji wake, Uhuru Kenyatta, walitia saini mkataba wa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mombasa hadi Dar es Salaam, utakaogharimu Sh63 bilioni.

Viongozi hao vile vile waliziagiza wizara za Mashauri ya Kigeni na zile za Biashara na Viwanda katika mataifa hayo kuanza mchakato wa kutatua vikwazo vya kibiashara ambavyo vimekuwepo katika maeneo ya mipakani.

Upeo wa ziara ya Rais Suluhu ulikuwa ni kulihutubia Bunge la Kitaifa na Seneti, ambapo alisisitiza kuhusu haja ya nchi hizo kusahau “yaliyopita na kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika masuala muhimu kama biashara.”

Kwa mujibu wa wadadisi wa siasa, ingawa lengo kuu la Bi Suluhu lilikuwa kuondoa uhasama uliokuwepo kati ya nchi hizo wakati wa utawala wa mtangulizi wake, Dkt John Magufuli, huenda hilo likaashiria mwanzo mpya kwa jumuiya hiyo.

Wachanganuzi wa mahusiano ya kimataifa wanaitaja Tanzania kuwa kikwazo kikuu kwa ukuaji wa jumuiya hiyo tangu miaka ya sitini, kutokana na mitazamo yake hasi, hasa kuhusu Kenya.

Hivyo, wanataja mwelekeo huo kuwa muhimu kwa mustakabali wa jumuiya hiyo.

“Tanzania ndio imekuwa kikwazo kikuu kwa juhudi, mipango na mikakati yote ya kuunganisha wanachama wa EAC kutokana na misimamo yake ya kisiasa. Ikiwa hilo litabadilika, basi huenda mipango ambayo imekuwepo, kama vile kubuniwa kwa sarafu moja miongoni mwa wanachama ikafaulu,” asema Dkt Godfrey Sang’, ambaye ni mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa.

EAC iliasisiwa mnamo 1967 kati ya Kenya, Uganda na Tanzania, ikilenga kuzisaidia nchi hizo kuunganisha na kuwianisha masuala muhimu kama vile afya, biashara na miundomsingi.

Viongozi waliokuwepo wakati wa kuanzishwa kwake ni hayati Mzee Jomo Kenyatta (Kenya), Julius Nyerere (Tanzania) na Milton Obote (Uganda).

Sambaratika 1977

Licha ya kuwa na malengo makubwa, muungano ulisambaratika mnamo 1977, kutokana na ushindani miongoni mwa wanachama kudhibiti baadhi ya sekta muhimu.

Hilo pia linatajwa kuchangiwa na hatua ya Kenya kuomba nyadhifa nyingi katika taasisi kuu za kufanya maamuzi kuhusu mwelekeo wa jumuiya hiyo, hali ya kutoelewana miongoni mwa wanachama na tofauti kwenye mifumo ya utawala katika nchi hizo, hasa Kenya na Tanzania.

Hata hivyo, jumuiya hiyo ilifufuliwa upya mwaka 2000. Hilo lilifuatia mkataba uliotiwa saini miongoni mwa nchi hizo tatu jijini Arusha mnamo Novemba 1999, kuhusu haja ya kuufufua upya.

Kulingana na Dkt Sang’, sababu kuu ya kuvurugika kwa jumuiya hiyo kati ya 1977 na 2000 ilitokana na hatua ya viongozi waliokuwepo kukosa kuanza mazungumzo kutathmini haja ya ufufuzi wake.

“Marais Daniel Moi (Kenya), Yoweri Museveni (Uganda), Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa (Tanzania) walikosa kubuni utaratibu maalum ambao ungerejesha upya ushirikiano kati yao. Walingoja hadi mwaka 2000 kurejesha mahusiano hayo. Hilo lilikuwa kosa kubwa,” asema.

Dkt Geoffrey Musila, aliye mdadisi mahusiano ya kimataifa, anailaumu Tanzania kuwa sababu kuu ya kuvurugika kwa “awamu ya kwanza ya EAC.”

“Kutokana na mfumo wa kisiasa wa Ujamaa, ambao ulisisitiza kuhusu haja ya raslimali za nchi kumilikiwa na wananchi wenyewe, viongozi na raia wa Tanzania waliwaona wenzao walioegemea mfumo wa kibepari kama Kenya na Uganda kama ‘maadui’ na ‘wabinafsi.’ Hilo ndilo lililoifanya nchi hiyo kutilia maanani uanachama wake katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),”akasema Dkt Musila.

Msimamo wa Magufuli

Wachanganuzi wanasema kuwa hata baada ya jumuiya kufufuliwa upya, Tanzania ndio ilichangia tofauti zilizoibuka, hasa wakati wa utawala wa Rais Magufuli.

“Kutokana na msimamo wake mkali, Rais Magufuli alivuruga tena uthabiti ambao ulikuwepo baada ya jumuiya hiyo kufufuliwa tena. Utawala wake uliathiri vikali ujirani mwema ambao ulikuwepo awali kati ya Tanzania na majirani wake. Kwa namna moja, hilo liliathiri sana mafanikio ambayo yalikuwa yamefikiwa katika ukuaji wa jumuiya hiyo,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni msomi wa historia.

Hivyo, anasema kuwa mwelekeo mpya ambao Rais Suluhu ameonyesha ni “suluhisho” la “kosa” ambalo alifanya Magufuli, kwani lilivuruga sana ukuaji wa jumuiya hiyo.

“Ikiwa Rais Suluhu ataepuka makosa ambayo yalifanywa na watangulizi wake, basi kuna uwezekano mkubwa kwa jumuiya hii kuwa na mwanzo mpya. Ni mwanzo ambao utaiwezesha kutimiza baadhi ya malengo yaliyokuwepo awali,” akasema Prof Munene.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kuwa bado ni mapema kuanza “kusherehekea”mwelekeo wa jumuiya hiyo, ijapokuwa Bi Suluhu ameonyesha dalili za kuridhisha.

JAMVI: Ukimya uliogubika OKA ni ishara mbovu, Uhuru amewaacha mataani?

Na CHARLES WASONGA

MASWALI yameibuka kufuatia ukimya wa vinara wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) miezi miwili baada ya wao kuchangamsha ulingo wa kisiasa kufuatia ushindi wao katika changuzi ndogo katika maeneo bunge Matungu, Kabuchai na kiti cha useneta wa Machakos.

Hii ni licha ya kwamba vinara hao; Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na mwenyekiti wa KANU Gideon Moi kunasibisha ushindi wagombeaji wao katika chaguzi hizo na mwanzo wa safari ya kuwezesha mmoja wao kuingia Ikulu 2022.

“Watu wa Matungu, Kabuchai na Machakos sasa wametupa motisha kubwa zaidi. Ushindi huu umetupa nafasi ya kuanza rasmi safari ya kwenda Ikulu. Wale wanaolalamika umoja wetu ndio nguvu yetu,” Bw Mudavadi akawaambia wanahabari baada ya ushindi wa Seneta Agnes Kavindu Muthama katika uchaguzi mdogo wa useneta wa Machakos uliofanyika Machi 18.

Awali, muungano huo ulivuna ushindi katika chaguzi ndogo za maeneo bunge ya Matungu (Kakamega) na Kabuchai (Bungoma) zilizofanyika Machi 4, kupitia Peter Oscar Nabulindo (ANC) na Majimbo Kalasinga (Ford-Kenya), mtawalia.

Ilidaiwa kuwa baraka za Rais Uhuru Kenyatta zilichangia ushindi huo, lengo likiwa kuzima nyota za kisiasa za Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga, haswa katika eneo la magharibi. Chama cha ODM, kupitia katibu mkuu Edwin Sifuna, kilidai kushindwa kwa ODM katika eneo bunge la Matungu kulichochewa na serikali.

Isitoshe, ni baada ya matokeo hayo ambapo Seneta wa Siaya James Orengo na Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo, ambao hadi wakati huo walikuwa watetezi sugu wa Bw Odinga, walidai Katibu katika Wizara ya Usalama Karanja Kibicho alikuwa akiendesha njama ya kuzima azma ya kiongozi huyo wa ODM kuingia Ikulu 2022.

Mbw Orengo na Amollo walidai kuwa “serikali inapanga kuunga mkono mmoja wa vinara ya One Kenya Alliance 2022” ilhali wao sio wadau katika handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Lakini tangu, Aprili 1, Rais Kenyatta alipoandamana na Bw Odinga kukagua miradi ya wa ujenzi wa kituo cha kisiasa cha magari ya uchukuzi cha Green Park, Nairobi na barabara kadha katika kaunti ya Kajiado, shughuli zimefifia ndani ya muungano wa One Kenyatta.

Kando na kufanya mikutano miwili katika makazi ya Bw Kalonzo na Bw Wetang’ula, siku tofauti, vinara hao wamekomesha mtindo wao wa kutoa taarifa kwa wanahabari kila mara huku wakimpiga vita Bw Odinga.

Hata hivyo, duru ziliambia Taifa Jumapili kuwa kando na hisia kuwa Rais Kenyatta “amerejelea ukuruba kati yake na Bw Odinga” kumeibuka vuta nikuvute kati ya vyama hivyo kuhusu nani kati ya vinara hao anafaa kuungwa mkono kama mgombeaji urais kwa tiketi ya OKA.

JAMVI: Mvutano ODM wazidisha ubutu kwa makali ya Raila

Na LEONARD ONYANGO

MVUTANO unaoendelea ndani ya ODM huenda ukamfanya kinara wa chama hicho Raila Odinga kukosa makali iwapo ataamua kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanaonya kuwa hatua ya chama cha ODM kumwadhibu mbunge wa Rarieda Otiende Amollo kwa kumng’oa kutoka wadhifa wa Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) na kutishia kumchukulia hatua Seneta wa Siaya James Orengo, ni pigo kwa juhudi za Bw Odinga kutaka kuingia Ikulu 2022.

Aliyekuwa Katibu wa Mipango wa ODM Wafula Buke anasema kuwa mvutano huo utakosesha ODM nguvu hivyo kumnyima Bw Odinga fursa ya kushinda urais.

“Kumekuwa na ripoti kwamba kuna baadhi ya wakuu serikalini ambao wamekuwa wakipanga njama ya kutaka kumwacha Bw Odinga akiwa mpweke kisiasa.

“Ikiwa kweli kuna mpango huo, basi mvutano huo ndani ya ODM itakuwa fursa murua kwao kuendeleza juhudi hizo. Mvutano huo hauna tija kwa ODM bali unasababisha chama kuwa dhaifu,” anasema Bw Buke.

Kumekuwa na ripoti kwamba baadhi ya wakuu serikalini wamekuwa wakiunda njama ya kutaka kumaliza ushawishi wa ODM katika ngome zake; ambazo ni maeneo ya Pwani, Magharibi, na Nyanza. Huku viongozi wa ODM wakiendelea na juhudi za kutaka kuunda chama kitakachotetea masilahi yao, juhudi zinaendelea kuzima umaarufu wa chama hicho katika maeneo ya Magharibi.

Kumekuwa na juhudi za kuvumisha chama cha Amani National Congress (ANC) chake Musalia Mudavadi na Ford Kenya kinachoongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.

Bw Mudavadi na Seneta Wetang’ula wameafikiana kushirikiana katika kinyang’anyiro cha Urais.

Vyama hivyo viwili viko ndani ya muungano wa Kenya One Alliance (OKA) ambao pia unajumuisha chama cha Kanu kinachoongozwa na Seneta wa Baringo Gideon Moi.

Rais Uhuru Kenyatta anaegemea muungano wa OKA. Gavana wa Kakamega ambaye ndiye muhimili wa Bw Odinga katika maeneo ya Magharibi amejitokeza na kuunga mkono kundi la Seneta Orengo na Dkt Otiende.

Bw Orengo, Gavana Oparanya na Dkt Otiende wanapinga ugavi wa maeneobunge mapya 70 yaliyopendekezwa ndani ya Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Viongozi hao wanasema kuwa eneo la Mlima Kenya limependelewa kwa kutengewa maeneobunge 35 huku maeneo mengine yakipunjwa.

Kumng’oa dkt Otiende kutoka wadhifa wake bungeni, kulingana na Gavana Oparanya, hakukufaa na hakuna manufaa kwa ODM.

Bw Orengo amejitokeza kuwa hatatishika na yuko tayari kukabiliana na Bw Odinga ‘kupigania haki’.

Hii ni mara ya kwanza kwa Bw Odinga kutofautiana kisiasa na Bw Orengo tangu 2002.

Japo baadhi ya wadadisi wanasadiki kwamba uasi huo unasababisha na siasa za ugavana 2022 katika Kaunti ya Siaya, mdadisi wa masuala ya kisiasa Mark Bichachi anasema kuwa mvutano huo unatokana na juhudi za kutaka kumrithi Bw Odinga.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga. Picha/ Maktaba

“Mvutano tunaoshuhudia ndani ya ODM unatokana ubabe wa kutaka kurithi uongozi wa jamii ya Waluo. Bw Orengo anajiona kwamba yeye ndiye atakuwa kiongozi wa jamii baada ya Odinga.

“Orengo anatumia maeneo 70 kujidhihirisha kwamba yeye ndiye mtetezi wa jamii. Lakini juhudi hizo huenda zikagonga mwamba kwani huu si wakati mwafaka wa kupigania urithi,” anasema Bw Bichachi.

Bw Orengo tayari ameonyesha nia yake ya kutaka kuwania ugavana wa Siaya 2022. Dkt Otiende aliambia Taifa Jumapili kuwa atatetea kiti chake cha ubunge wa Rarieda.

“Sina nia ya kuwania ugavana, azma yangu ni kutetea kiti cha ubunge,” akasema Dkt Otiende.

Gavana wa Migori Okoth Obado pia ameapa kumaliza ushawishi wa Bw Odinga katika maeneo ya Nyanza.

Bw Obado wiki iliyopita alikutana na Bw Mudavadi wiki chache baada ya kutembelewa na Gavana wa Nandi Stephen Sang ambaye ni mwandani wa Naibu wa Rais William Ruto.

Profesa Medo Misama anasema kuwa iwapo Bw Odinga atakuwa na maadui wengi katika eneo la Nyanza, atakosa nguvu ya kisisa hivyo kutoa mwanya kwa muungano wa OKA na Dkt Ruto kupenya.