Majopo 15 yaliyoundwa na Rais yavunjwa na mahakama

Na RICHARD MUNGUTI

MAJOPO 15 ambayo wanachama wake waliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta na mawaziri mbalimbali yatafutiliwa mbali kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba yanapasa kuteuliwa na Tume ya Kuajiri Watumishi wa Idara ya Mahakama (JSC).

Kufuatia uamuzi wa Jaji Maureen Onyango , majopo hayo yanapasa kuvunjwa kwa vile walioyateua hawana mamlaka kisheria.

Uamuzi huo wa Oktoba 30, 2020, ulioharamisha uteuzi wa wanachama watano wa jopo la kuamua mizozo ya wapangaji na wenye mijengo (BPRT) sasa umepingwa katika Mahakama ya rufaa na wakili Charles Kanjama akisema “ umesababisha hali ya taharuki na kizugumkuti.”

Huku akiomba mahakama hii ya pili kwa ukuu nchini ifafanue sheria inayomwezesha Rais na Mawaziri kuteua wanachama waa majopo ya kuamua mizozo katika idara za serikali, Bw Kanjama amesema suala hilo ni la dharura na halipasi kuchukuliwa kwa uzembe.

Bw Kanjama anayewakilisha wanachama wa BPRT anaomba mahakama ta rufaa isitishe kutekelezwa kwa agizo kwamba JSC iteue wanachama wa majopo kwa vile.

Wakili Kanjama ameeleza mahakama ya rufaa kuwa Waziri Jane Maina aliyeteua jopo la BPRT alikuwa anatekeleza jukumu lake kisheria sawia na Rais Kenyatta na mawaziri wengine walioteua majopo mengine 14.

Baadhi ya majopo yatakayoathiriwa ni lile linalothibiti mashirika ya serikali (State Corporations Appeals Tribunal), Jopo la masula ya ushuru, BPRT na mengine.

Bw Kanjama anaomba mahakama ua rufaa iwarejeshe kazini wanachama watano wa BPRT walioanza kazi Juni 2020.

Kufikia sasa jopo hilo la BPRT imesikiza kesi za ya 10,000.

Bw Kanjama amesea wapangaji na wenye nyumba za kibiashara na za kuishi wataendelea kuteseka hadi pale uamuzi kamili utakapotolewa kuhusu uhalali wa teuzi hizi za majopo.

Kesi ya kupinga uteuzi wa BPRT iliwasilishwa mahakanani na mawqakili Okello Odero na Ian Mwiti…

Katika mlalamishi yao mawakili hao walisema sheria ya thuluthi moja haikufuatwa na Waziri Betty Maina kwa vile alimteua mwanamke mmoja badala ya wawili na wanaume watatu.

Mahakkama ya rufaa itatoa uamuzi baada ya siku tatu.

Kalonzo, Mudavadi na Weta wapinga kubuniwa kwa jopo la kuzima ufisadi

Na VALENTINE OBARA

VINARA watatu wa Muungano wa NASA wamejitenga na msimamo wa mwenzao Raila Odinga, kuhusu vita dhidi ya ufisadi.

Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula (Ford Kenya), Jumatano walipinga pendekezo la kubuniwa kwa jopokazi maalumu la kupambana na ufisadi nchini.

Pendekezo hilo lilikuwa limetolewa mwishoni mwa wiki na Bw Odinga ambaye uhusiano wake wa kisiasa na watatu hao umeonekana kudorora tangu alipoamua kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta miezi miwili iliyopita.

Kwenye taarifa ya pamoja, watatu hao walisema asasi za kupambana na ufisadi zilizopo kwa sasa zinahitaji tu kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kupewa uhuru wa kutosha ili zifanikiwe kuangamiza janga hilo sugu.

“Huu si wakati wa kuunda taasisi nyingine kwa minajili ya kupambana na ufisadi. Kuunda taasisi inayofanana na zile zilizopo na kuchukua hatua za kisiasa kutachangia tu kuficha wahusika wakuu, kutoa nafasi zaidi ya wahusika kupeana bakshishi na kuadhibu tu wahusika wadogo,” wakasema.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa vinara hao kutoa taarifa ya pamoja kuhusu ufisadi nchini baada ya sakata mpya kufichuliwa katika shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), wiki chache zilizopita.

Tofauti na jinsi ilivyokuwa wakati Bw Odinga alipokuwa akishirikiana pamoja na watatu hao, upande wa upinzani umeonekana kukosa makali ya kushinikiza serikali ibadilishe mienendo yake inapokosea.

Mbali na kumpinga kiongozi huyo wa Chama cha ODM, watatu hao pia walikosoa hatua zilizochukuliwa na serikali kufikia sasa kupambana na ufisadi. Kulingana nao, serikali haijadhihirisha kujitolea kukamata wahusika wakuu wanaopora mali ya umma licha ya kutoa ahadi za kufanya hivyo mara kwa mara.

“NASA itaamini serikali imejitolea tu ikiwa wale walio na ushawishi ndani na nje ya serikali watapelekwa mahakamani kwa msingi wa ushahidi wa kutosha ili wafungwe, na wala si sarakasi tunazoshuhudia ambapo washtakiwa ni mawakala tu,” wakasema.

Idara ya Upelelezi wa Jinai (DPP) ilipeleka washukiwa 24 wa ufisadi wa NYS mahakamani Jumanne ingawa wengi wao ni watu wa vyeo vya chini isipokuwa Katibu wa Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Jinsia Lilian Mbogo-Omollo na Mkurugenzi Mkuu wa NYS Richard Ndubai.

MUAFAKA: Orodha ya Uhuru na Raila yapingwa vikali

Na WAANDISHI WETU

UAMUZI wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Bw Raila Odinga kuteua jopokazi la watu 14 kuwashauri kuhusu jinsi ya kuleta umoja wa kitaifa, umekosolewa kwa “kukosa uwakilishi unaostahili.

Viongozi mbalimbali jana walisema jopo lililotangazwa Jumapili halina wawakilishi wa vijana, dini tofauti na pande nyingine muhimu za kisiasa.
Kwa hivyo, wanaamini kuwa hilo ni kundi la kutaka kutekeleza maslahi ya wawili hao pekee, wala si ya taifa zima kama ilivyotarajiwa.

Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu wa Kenya (CIPK) tawi la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, Sheikh Abubakar Bini, alisema ingawa awali Rais Kenyatta na Bw Odinga walionyesha nia njema kwa kushirikiana, hatua ya kuacha makundi mengine nje kwenye jopokazi hilo haifai.

“Jinsi ilivyo kwa sasa, kikundi hicho hakina sura ya Kenya katika uwakilishi wa kidini kwani Wakristo pekee ndio wanaowakilishwa. Je, hii itaunganisha Wakenya au kuwagawanya?” akasaili kwenye kikao cha wanahabari mjini Eldoret.

Wazee wa jamii za Bonde la Ufa pia walipinga jopo hilo na kusema halitasiaidia taifa. Wakiongozwa na mwenyekiti wao, Bw Gilbert Kabage, walishangaa kwa nini Naibu Rais William Ruto anatengwa katika mashauriano hayo.

“Hatufurahishwi na jinsi Bw Ruto anavyotengwa katika hatua hizi. Sisi tunamfuata Bw Ruto na tumeghadhabishwa na mambo hayo,” akasema akiwa Nakuru.

Wakizungumza bungeni, Naibu Kiongozi wa Wachache katika Seneti, Bw Cleophas Malala, na Mbunge wa Butere, Bw Tindi Mwale, ambao ni wanachama wa ANC, walisema vijana walitengwa.

“Inavunja moyo kwamba viongozi hao wawili wa heshima hawakuona sababu ya kujumuisha vijana katika kikundi cha kuleta umoja. Ingawa ninaunga mkono walivyojitolea kuleta upatanisho, ninatoa wito kwao wazingatie kujumuisha vijana,” akasema Bw Malala.

Hata hivyo, chama cha ODM kinachoongozwa na Bw Odinga kilitetea hatua hiyo na kusema wale waliochaguliwa ni mchanganyiko wa wazee wa kijamii, wasomi, viongozi wa dini na wataalamu wenye misimamo thabiti.

“Kikundi hicho ni kizuri. Hakina watu wenye maazimio ya kibinafsi, kwa hivyo hakitasababisha migawanyiko na kitajitolea kuimarisha uwiano kikiungwa mkono,” akasema Mbunge huyo wa Suba Kusini.

Malalamishi pia yalienea kwenye mitandao ya kijamii, hasa kutoka kwa vijana ambao walishangaa kama kazi yao katika masuala ya uongozi huishia katika kampeni za uchaguzi na upigaji kura.

Miongoni mwa waliochaguliwa ni Seneta wa Busia, Bw Amos Wako, mwenzake wa Garissa, Bw Yusuf Haji na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Samburu, Bi Maison Leshomo.

Wengine ni Dkt Adams Oloo, Bi Agnes Kavindu, Bi Florence Omose, Prof Saeed Mwanguni, Mzee James Matundura, Meja Mstaafu John Seii, Bw Morompi ole Ronkai na Bi Rose Museu. Viongozi wa kidini waliochaguliwa ni Askofu Lawi Imathiu, Peter Njenga na Zacheus Okoth.

Jopo maalum kuundwa kufanikisha muafaka wa Uhuru na Raila

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila amesema yeye pamoja na Rais Uhuru Kenyatta watabuniwa jopo maalum litakalowashauri kuhusu jinsi ya kuunganisha nchi kwa manufaa ya Wakenya wote.

Wanachama wa jopo hilo pia watawaelekeza wawili hao kuhusu namna na kuzuia machafuko ya kisiasa ambayo yamekuwa yakishuhudiwa nchini kila baada ya uchaguzi.

Akiongea Jumamosi eneo la Bondo alikohudhuria hafla mazishi, Bw Odinga alielezea matumaini kuwa utaratibu huo utasaidia kusuluhisha shida ambazo zimekuwa zikilizonga taifa hili tangu uhuru.

“Tunataka kujadiliana ili kupata masuluhisho ambayo yatashughulikia mahitaji yetu. Hatutaki kuandaa uchaguzi mwingine ambao utatugawanya kama Wakenya,” akasema.

Bw Odinga aliwaambia waombolezaji kuwa Kenya inahitaji kuweka ambao utaisaidia kuafikia maendeleo katika nyanja zote kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vile vya siku zijazo.

Alisema ataendelea kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali nchini katika juhudi zake za kupalilia umoja na utangamano nchini.

“Ndoto yangu kuu ni kuunganisha nchi, bila masharti yoyote. Hii ndio maana baada ya kukutana na Rais Kenyatta na kukubaliana kuzika tofauti zetu za kisiasa, nimekuwa nikikutana viongozi wakuu nchini. Nitaendelea kufanya mikutano kama hiyo,” akasema.

Mnamo Ijumaa Bw Odinga alifanya mashauriano na Rais mstaafu Mwai Kibaki nyumbani kwake (Kibaki) katika mtaa wa Muthaiga. Mkutano huu unajiri wiki moja baada ya kiongozi huyo wa upinzani alienda Kabarak, Nakuru kufanya mashauriano na Rais mstaafu Mzee Daniel Moi.

Viongozi wengine ambao Bw Odinga amewahi kukutana nao afisini mwake jumba la Capital Hill, Nairobi ni Gavana Mike Sonko na aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo.

Tobiko aunda jopokazi la kulinda misitu

Na BERNARDINE MUTANU
WAZIRI wa Mazingira Keriako Tobiko ameunda jopokazi la kusimamia misitu nchini.

Miongoni mwa wanakamati wa jopo hilo ni watu walio na utaalam mkubwa katika masuala ya mazingira.

Jopo hilo linalenga matokeo ya haraka katika usimamizi wa misitu hasa ukataji wa miti na usimamizi wa rasilimali ya misitu.

Kulingana na taarifa kutoka kwa Wizara ya Mazingira, jopo hilo linalenga kubainisha kiwango cha uharibifu wa mazingira nchini.

Inaonekana waziri huyo ameunda jopo hilo baada ya malalamishi mengi kuhusiana na athari za uharibifu wa misitu nchini.

“Jopo hilo litapendekeza njia za kuhakikisha kuwa misitu imerudi kwa njia endelevu,” ilisema taarifa hiyo.

Litasimamiwa na mwenyekiti wa Shirika la Green Belt Movement, Marion Wakanyi Kamau na naibu mwenyekiti wa Taasisi ya Kitaifa ya Mazingira Bi Linda Munyao,

Wengine ni Christian Lambrechts (Mkurugenzi Mkuu wa Wakfu wa Rhino Ark), Bi Phyllis Wakiaga (Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Association of Manufacturers (KAM) na Mwenyekiti wa Shirika la Kenya Water Towers Agency Bw Isaac Kalua.

Adil Khawaja (Mkurugenzi KCB), Duncan Kimani(KEPSA), Ernest Nadome(COTU) na mawakili Faith Waigwa na Gideon Kilakoi.

Ripoti ya mwanzo ya jopo hilo inatarajiwa katika muda wa siku 14, alisema Bw Keriako Tobiko.