Kagwe atishia kuadhibu walipishao chanjo

Na WINNIE ONYANDO

WAZIRI wa Afya, Mutahi Kagwe ametishia kuyaondoa kwenye orodha majina ya vituo vya afya vyenye mazoea ya kuwatoza wananchi chanjo ya corona.

Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi kuhusu hali ya corona nchini, Bw Kagwe alisema majina ya vituo hivyo yataondolewa mara moja kwenye orodha ya vinavyotoa huduma za afya nchini.

“Ukienda hospitalini na udaiwe pesa ya chanjo, kubali kuchanjwa ila ukatae kulipa. Serikali inatoa chanjo bure. Watu kama hao wanaozidi kuwakandamiza raia watachukuliwa hatua,” akaonya Bw Kagwe.

Alisema serikali inatumia mabilioni ya pesa kuhakikisha kuna chanjo ya kutosha kwa wananchi wote. “Chanjo ni haki ya kila mmoja. Kila kituo cha afya lazima kitoe chanjo bure bila malipo kwa kila mmoja,” akasisitiza Bw Kagwe.

Waziri huyo alisema kuwekuwa na ripoti za madaktari wanaotembea mtaani bila mavazi rasmi na kuwachanja raia.Alisema madaktari kama hao pia wanajiweka katika hatari ya kupoteza kazi yao.

“Madaktari au maafisa wa afya wanaotembea mtaani wakitoa chanjo bila mavazi rasmi au beji za hudumu watachukuliwa kama matapeli. Tumepata ripoti kuwa kuna watu wanaovalia suruali aina ya jeans wakitoa chanjo kwa raia. Watu kama hao hawafai kutoa chanjo,” akaongeza Bw Kagwe.

Kutokana na hayo, Bw Kagwe alielekeza Chama cha Madaktari na Baraza la Madaktari wa Meno kuviondoa kwenye orodha vituo vyote vya afya vinavyotoza pesa kwa chanjo za corona.

Alisema kila kituo cha afya lazima kitoe ripoti kila wiki kuhusu matumizi ya dozi zote za chanjo ya corona huku akionya kuwa kituo chochote kitakachoshindwa kufanya hivyo kitaondolewa orodhani.

Kadhalika, waziri huyo alisisitiza kuwa hakuna chanjo inayopaswa kutolewa nje ya vituo maalumu vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya.

“Kuna vituo maalum vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya ili kutoa chanjo. Vituo hivyo vina maafisa wa afya waliopata mafunzo maalum ya namna ya kutoa chanjo. Kama mwananchi, hakikisha kuwa unapata chanjo katika vituo hivyo,” akasema Bw Kagwe.

Hata hivyo, aliwahimiza wananchi wawe waangalifu na kuhakikisha kuwa wamepata chanjo. Kulingana na ripoti ya wizara ya Afya, nchi imetumia dozi zaidi ya 2.8 milioni kuwachanja raia.

Aina hatari ya corona imetua nchini – Kagwe

Na BENSON MATHEKA

Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe, amekiri kwamba visa vya maambukizi ya aina mpya hatari ya corona iliyogunduliwa Afrika Kusini na Uingereza vimethibitishwa nchini.

Hata hivyo, Bw Kagwe aliondolea Wakenya hofu kuhusu athari za aina hizo akisema inayoambukiza watu wengi nchini ni ile iliyothibitishwa Kenya mwaka jana.

“Aina ya virusi vya corona inayosambaa Kenya kwa wingi ni iliyothibitishwa nchini mwaka jana. Hata hivyo, kumekuwa na visa vya aina mpya iliyogunduliwa Afrika Kusini na Uingereza,” Bw Kagwe alisema jana.

Kenya inakumbwa na wimbi la tatu la maambukizi ya corona ambayo yamefanya serikali kuchukua hatua za kuikabili kwa kufunga kaunti tano za Nairobi, Machakos, Kiambu, Kajiado na Nakuru. Akitangaza kufungwa kwa kaunti hizo mnamo Ijumaa wiki jana, Rais Uhuru Kenyatta alisema zimechangia asilimia 70 ya maambukizi ya virusi hivyo nchini.

Idadi ya maambukizi na vifo vinavyosababishwa na virusi hivyo inaendelea kuongezeka huku nchi ikikumbwa na uhaba wa oksijeni.

Bw Kagwe alisema kuna viwanda 75 vya oksijeni nchini ingawa baadhi havifanyi kazi.

Waziri Kagwe alisema oksijeni ni silaha muhimu katika vita dhidi ya janga la corona wagonjwa wanapolazwa hospitalini. Mnamo Ijumaa, Rais Kenyatta alisema zaidi ya Wakenya 950 walikuwa wamelazwa na katika vyumba vya wagonjwa mahututi na maelfu walikuwa wameongezewa oksijeni kuwasaidia kupumua. Aliagiza serikali za kaunti kushirikiana na Wizara ya Afya kuthibitisha kiwango cha oksijeni nchini. Rais Kenyatta aliagiza oksijeni iliyoko nchini itengwe kwa vita dhidi ya corona pekee.

Jana, Bw Kagwe alisema kiwango cha oksijeni nchini kinatishiwa na mambo kadhaa vikiwemo viwanda visivyofanya kazi.

Alisema moja ya changamoto kuu ni kuwa, mitungi 20,000 ya oksijeni iko katika nyumba za watu na taasis mbalimbali.

“Wanatakiwa kuirudisha mara moja, ni makosa kuweka mitungi hiyo huku watu wakifariki kwa kukosa oksijieni,” alisema.

Bara la Afrika lalala huku dunia ikianzisha chanjo ya corona

LEONARD ONYANGO na MASHIRIKA

NCHI za Afrika zimo hatarini kubaki nyuma katika vita dhidi ya virusi vya corona wakati mataifa mengine yakipiga hatua kubwa kuwapa raia wao chanjo ya kuzima maambukizi.

Kufikia jana, mamilioni ya watu katika mataifa ya nje ya bara la Afrika walikuwa wamepewa chanjo, huku nchi za barani zikiendelea kujikokota.Waziri wa Afya Mutahi Kagwe wiki iliyopita alitangaza kuwa chanjo ya corona itatolewa bure itakapowasili humu nchini.

Lakini Bw Kagwe hajasema ni lini chanjo hiyo itakapofika humu nchini.Kenya imeagiza chanjo hiyo kupitia muungano wa kimataifa kuhusu chanjo (Gavi).

Muungano wa Gavi unalenga kusaidia nchi maskini kupata chanjo ya corona kwa bei nafuu. Hata hivyo, chanjo inayoletwa na Gavi itatumika kuchanja asilimia 20 tu ya Wakenya.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kudhibiti Maradhi (CDC) ulionyesha kuwa asilimia 75 ya Waafrika watakubali kupewa chanjo iwapo itathibitishwa kuwa salama.

Huku mataifa ya Afrika yakiendelea kungojea chanjo, mataifa tajiri duniani yanaendelea kutoa kinga kwa mamilioni ya raia wayo.

Nchi tajiri tayari zimeagiza dozi bilioni 9 za chanjo ambazo zimetengenezewa katika mataifa ya Magharibi na kuacha Afrika katika hali ya sintofahamu. Hiyo inamaanisha kwamba kiasi kikubwa cha chanjo itakayotengenezwa mwaka ujao kitachukuliwa na nchi tajiri.

Nchini Amerika, zaidi ya watu milioni mbili kati ya watu milioni 331 tayari wamepata chanjo hiyo. Serikali ililenga kuhakikisha kuwa watu milioni 20 wanapewa chanjo hiyo kufikia Ijumaa, wiki hii.

Visa zaidi ya 19.2 milioni vya watu walioambukizwa na virusi vya corona vimethibitishwa nchini Amerika tangu Januari mwaka huu.Umoja wa Mataifa ya Ulaya (EU) umeanza harakati za kuhakikisha kuwa watu milioni 446 wanapewa chanjo hiyo katika nchi zote 27 wanachama.Mamlaka ya Matibabu ya Ulaya (EMA) imeidhinisha matumizi ya chanjo iliyotengenezwa na Pfizer-BioNTech ya Amerika.

Rais wa Tume ya EU Ursula von der Leyen jana alisema kuwa chanjo hiyo imesambazwa katika mataifa yote ya Ulaya. Watu 800,000 tayari wamepewa chanjo ya corona nchini Uingereza.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Bw Boris Johnson alisema kuwa watu milioni 15 ambao wanastahili kupata chanjo hiyo kwa dharura wametambuliwa.

Uingereza imekuwa ikitumia chanjo ya Pfizer lakini serikali imesema kuwa itazindua matumizi ya chanjo ya pili iliyotengenezwa na AstraZeneca kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza.Uingereza inalenga kutoa chanjo kwa raia wake milioni 2 ndani ya wiki mbili zijazo.

Wataalamu wanasema kuwa huenda mataifa ya Afrika ambayo yameshindwa kupata chanjo iliyotengenezwa katika nchi za Magharibi, yatalazimika kutumia chanjo ya China.

China ina chanjo sita ambazo zinafanyiwa majaribio ya mwisho. Rais Xi Jinping ametangaza kuwa China itatengeneza jumla ya dozi bilioni 1 mwaka ujao. Taifa la Bahrain na Milki za Uarabuni (UAE) tayari zimeagiza chanjo ya corona kutoka China.

Morocco pia inalenga kutumia chanjo ya China kuanzia mwezi ujao. Mataifa ya Uturuki, Indonesia na Brazil tayari yameanza mchakato wa kuidhinisha chanjo ya China.Majaribio ya kuthibitisha usalama wa chanjo ya China pia yanaendelea nchini Urusi, Misri na Mexico.

Kagwe anapotosha Wakenya – Madaktari

WANDERI KAMAU na WAIKWA MAINA

MADAKTARI na matabibu wameilaumu serikali ya kitaifa na zile za kaunti kwa kutumia mbinu chafu kwenye juhudi za kutafuta utatuzi kwa mgomo wao unaoendelea.

Hapo jana, viongozi wa vyama vya wahudumu hao walisema serikali imekuwa ikitumia vitisho na uongo, licha ya maafisa wa Wizara za Afya na ile ya Leba kususia vikao wanavyoandaa kujadili kuhusu malalamishi yao.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wahudumu wa Kliniki (KUCO), Bw George Gibore na mwenzake wa Chama cha Madaktari na Wahudumu wa Meno (KMPDU), Dkt Chibanzi Mwachoda, walimlaumu Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, kwa “kuwadanganya” Wakenya kwamba serikali imetoa vifaa vya kuwasaidia kujikinga kuambukizwa magojwa (PPEs).

“Bw Kagwe anawadanganya Wakenya kuwa Mamlaka ya Kusambaza Dawa (Kemsa) imetoa PPEs kwa hospitali za umma lakini huo ni uongo. Wakati vifaa kama hivyo vinapotolewa, kuna fomu maalum ambazo hujazwa ili kuonyesha ni vingapi vilivyotolewa, na muda ambao vitatumika. Hakuna hospitali yoyote ya umma inayoweza kuonyesha fomu hizo kama ushahidi wa kupokea PPEs kutoka kwa Kemsa,” akasema Bw Gibore.

Wawili hao walisema Bw Kagwe anatumia uwongo ili kuwapaka tope na kuonyesha kuwa wao ndio hawataki kushiriki kwenye mazungumzo ya kutafuta mwafaka.

“Ni vibaya kwa waziri kutumia uongo kwenye mzozo kama huu ambao unawaathiri Wakenya,” akasema Dkt Mwachoda.Mnamo Jumanne, mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG), Bw Wycliffe Oparanya aliziandikia barua serikali za kaunti akiziagiza kuwafuta kazi wahudumu wote ambao wanashiriki mgomo na kuwaajiri wengine.

Hata hivyo, wahudumu walisema jana hawatababaishwa hata kidogo na vitisho hivyo, kwani hata wale wataajiriwa watakumbana na matatizo wanayolalamikia.

Wakati huo huo, Kamati ya Bunge Kuhusu Afya, jana ilimtaka Bw Kagwe kusuluhisha utata uliopo kuhusu mgomo huo kwa kutoa vifaa vya PPEs kutoka maghala ya Kemsa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bi Sabina Chege, aliwalaumu magavana kuwa kikwazo kwenye utatuzi wa mgomo huo wakati Wakenya wanahitaji huduma za afya kwa dharura.

Bi Chege aliwatetea madaktari na matatibu, akisema baadhi ya matakwa yao yangeweza kutimizwa wakati walipotoa makataa ya kuanza mgomo huo.

Kagwe akaangwa kuwatishia wahudumu wa afya

NA WANGU KANURI

Matamshi ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe yameibua hisia tata katika mtandao wa kijamii wa Twitter huku Wakenya wengi wakionekana kukerwa na aliyosema waziri huyo hapo Desemba 18.

Matamshi hayo aliyosema wakati wa kufunguliwa kwa hospitali katika Kaunti ya Muranga eneo la Kenol, yalielekezewa wahudumu wa afya ambao walikuwa wananuia kugoma kwa sababu ya kupuuzwa kwa matakwa yao.

Hii ni baada ya korti kusitisha mgomo huo wa wahudumu wa afya huku wakuu wa wahudumu wa afya wakielezwa na korti kuwa na kikao na wakuu katika wizara ya afya ili kutafuta suluhu ya malamishi ya wahudumu wa afya.

Waziri Kagwe aliwarai wahudumu wa afya kurejea kazini kwani bado ugonjwa wa Covid-19 umetukodolea macho huku akiwaomba wawe na utu na kuwasaidia wananchi. “Ninawarai mrejee kazini ili kuzuia kupoteza kazi yako. Tafadhali usiwe katika ratibu ya wanaosaka kazi mwaka ujao,” Waziri Kagwe akasema.

Wahudumu hawa wa afya wamekuwa wakiomba serikali kusikiza kilio chao kufuatia mazingira mabaya ya kazi wakati huu wa janga la Corona. Hali kadhalika, wahudumu hawa ambao wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa vifaa muhimu vya kujizuia wanapowahudumia wagonjwa, wamekuwa wakipuuziliwa huku malalamishi yao yakitupiliwa mbali.

Isitoshe, wahudumu hawa ambao wameteta kuhusu mishahara wanayopata isiyoafikiana na iliyochelewa, wameonekana kuchoshwa na ahadi tupu kutoka wizara hiyo ya afya na serikali kwa jumla huku wakisema watagoma.

Wananchi walionekana kukerwa na matamshi ya waziri Kagwe walikuwa na haya ya kusema kupitia hashtegi ya SomeoneTellKagwe:

“Azungumzie wauguzi na wahudumu wa afya na heshima,” akasema @Kinotithenurseactivist.

“Ni haki yetu kulindwa. Vifaa vya kujilinda, malipo ya bima na posho ya kutulinda dhidi ya hatari,” akaandika @TimothyBeth.

“Wauguzi wanakufa sababu ya mkurupuko wa magonjwa yanayotamba haraka sana huku wakipewa ya posho ya kutulinda dhidi ya hatari ya shilling 3850,” akasema @Stephenkeoro.

“Ni wapi vitisho vimewahi kutatua shida?” akauliza @PurityMburugu.

“Mgomo uliositishwa ulikuwa tofauti na mgomo huo ulikuwepo kwa muda wa mwezi mmoja na nusu. Mgomo wa kitaifa wa wahudumu wa afya bado unaendelea,” ukurasa wa @kUCOofficial ukasema.

“Wezi wa KEMSA wanafurahi huku madaktari wanakufa. Kumwambia daktari ahudumie mgonjwa wa Covid-19 bila vifaa vya kumkinga ni sawa na kumuua daktari huyo. Nchi yenye afya ni nchi yenye fedha. Walinde madaktari nao watawalinda wagonjwa,” akaandika @KipropDismas4.

Shinikizo zazidi Kagwe ajiuzulu au afutwe kazi

FAITH NYAMAI na ONYANGO K’ONYANGO

MUUNGANO wa Makanisa ya Kipentekosti unamtaka Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe, ajiuzulu kuhusiana na madai ya ufujaji wa fedha za Covid-19 katika Wizara yake.

Mwenyekiti wa Muungano huo, Askofu Jonah Kariuki alisema, Waziri anastahili pia kukamatwa na kushtakiwa kuhusu fedha hizo zilizodhamiriwa kuwasaidia Wakenya dhidi ya Covid 19.

‘Waziri ni mfano mbaya kabisa kwa uongozi tunaotaka katika taifa hili ndiposa kama kanisa tunamtaka ajiuzulu na kumruhusu mtu mwingine kuongoza Wizara ya Afya,’ alisema.

Aidha, muungano huo umemtaka Rais Uhuru Kenyatta ashirikiane na Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga, kuangamiza ufisadi nchini.

‘Rais alitueleza atapiga vita ufisadi lakini yote tunayoona nchini hayakubaliki kamwe,’ alisema Askofu Kariuki.

Alisema kanisa halitaunga mkono ufisadi kukita mizizi nchini huku raia wakiteseka.

“Tumeshangaa kwamba hela zilizotengwa kudhibiti ugonjwa wa Covid-19 nchini zimeporwa katika usimamizi wa Waziri Kagwe,’ alisema.

Maaskofu hao wanamtaka Bw Kagwe kuelezea kwa kina jinsi fedha hizo zilitumika.

Kwingineko, Seneta wa Bomet Dkt Christopher Lang’at anamtaka Rais Kenyatta amfute kazi Bw Mutahi Kagwe na Katibu wa Wizara Susan Mochache.

Hii ni baada ya Mkurugenzi wa Taasisi ya Usambazaji Dawa Kenya (Kemsa) Jonah Manjari kuwahusisha wawili hao Ijumaa iliyopita, na sakata ya mabilioni ya fedha za Covid-19.

Dkt Langat alisema huu ni muda mwafaka kwa Rais Kenyataa kuonyesha kwa vitendo kwamba amejitolea kuangamiza ufisadi kama sehemu ya kujenga kumbukumbu yake.

Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu alipokamatwa wakati wa mjadala kuhusu ugavi wa raslimali, Dkt Lang’at alisema Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) unaweza tu kufanikiwa ikiwa rais atawateua watu ambao hawataruhusu ubadhirifu wa fedha za umma chini ya usimamizi wao.

Msaada wa corona haukuibwa, Kagwe sasa asema

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe sasa amebadilisha msimamo na kukana madai kwamba sehemu ya shehena ya msaada wa vifaa vya kupambana na Covid-19 vilivyopewa Kenya na Wakfu wa Jack Maa viliibwa.

Hata hivyo Bw Kagwe aliwaambia wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Afya kwamba wizara yake ilialika Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ,kuanzisha uchunguzi “baada ya uvumi kuenea kwamba baadhi ya vifaa hivyo viliibwa.”

Mnamo Juni mwaka huu, Bw Kagwe alikiri hadharani akiwa Nyeri kwamba watu aliowataja kama wezi walishirikiana na maafisa wa wizara yake kuiba sehemu kubwa ya vifaa hivyo.

“Inasikitisha kuwa maafisa fulani katika Wizara yangu wameshirikiana na kuiba sehemu ya vifaa kutoka kwa wakfu wa Jack Ma. Walifanya wizi huo katika uwanja wa JKIA hata kabla ya kuwasilishwa kwa hospitali husika. Uchunguzi umeanzishwa na naamini kwamba watapatika na kuadhibiwa,” akasema Bw Kagwe wakati huo.

Shehena ya kwanza ya vifaa hivyo iliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), mnamo Machi 24, 2020 na vilijumuisha barakoa 100,000 na seti 20,000 za vifaa vya kupima virusi vya corona.

Lakini licha ya Waziri Kagwe jana kukana madai kuhusu wizi wa baadhi ya vifaa hivyo, Waziri Msaidizi wa Uchukuzi Dkt Chris Obure alifurushwa kutoka kwa kikao cha kamati hiyo kwa kutoa maelezo kuhusu suala hilo ambayo hayakuwaridhisha wabunge.

Dkt Obure ambaye alikuwa amemwakilisha Waziri wa Uchukuzi James Macharia, alifeli kutoa maelezo kuhusu idadi ya kamili ya vifaa vilivyopokewa katika uwanja wa JKIA, na ile iliyowasilishwa kwa Wizara ya Afya na asasi husika.

Hii ni baada ya Mkurugenzi wa Kupitisha Bidhaa zinazoingizwa nchini, Bw Felix Ateng kutoa maelezo ambayo yalikinzana na yale ya Dkt Obure.

“Naamuru muondoke mkaoanishe maelezo yote tunayohitaji kisha mrejee hapa kesho (leo) saa tatu asubuhi. Inaonekana wazi kwamba hamkuwa mumejiandaa kutoa maelezo yote ambayo tulitaka,” akasema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bi Sabina Chege.

Wizara yangu ilipokea Sh3b kati ya Sh48b – Kagwe

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe Jumatatu aliwaambia wabunge kwamba Wizara yake ilipokea asilimia 15 pekee ya Sh47.9 bilioni zilizotengwa na serikali kufadhili mpango wa kupambana na Covid-19.

Bw Mutahi aliwaambia wanachama wa kamati ya bunge la kitaifa kuhusu afya kwamba Hazina ya Kitaifa ndiyo inaweza kutoa maelezo kamili kuhusu namna sehemu kubwa ya fedha hizo zilitumika.

“Wizara yangu haiwezi kujibikia Sh47.9 bilioni zilizotengwa na serikali kwa ajili ya vita dhidi ya Covid-19 kwa tulipokea sehemu ndogo zaidi ya pesa hizo,” Bw Kagwe akaambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Murangá Bi Sabina Chege.

Bw Kagwe alikuwa ameandamana na Katibu katika Wizara hiyo Bi Susan Mwachache.

Katibu huyo alisema Wizara ya Afya ilipokea Sh3 bilioni ambayo ni sehemuj ya bajeti ya ziada ya Wizara ya Afya na itatuma kwa Hospitali mbalimbali nchini kufadhili maandalizi ya kuwahudumia wagonjwa wa Covid-19.

Miongoni mwa hospitali hizo ni Hospitali Kuu ya Pwani iliyopokea Sh500 milioni, Hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH) iliyopokea Sh400 milioni, Hospitali ya Kitui (Sh300 milioni), Hospitali ya Mandera (Sh300 milioni).

Hospitali zingine zilizofaidi ni Hospitali Kuu ya Kenyatta, KNH (Sh600 milion), Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (Sh400 million) na Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (Sh500 milion.)

Bi Mwachache aliongeza kuwa Wizara ya Afya pia ilipokea Sh1.5 bilioni kutoka Hazina ya Kitaifa ambazo zilielekezwa kwa Mamlaka ya Usambazaji Dawa Nchini (KEMSA) kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kupima corona na dawa na kutumika katika shughuli hiyo, inayojulikana kwa kimombo kama ‘reagent’.

“Zaidi ya hayo, Wizara ilipokea Sh300 milioni zilizopewa KEMSA kwa ajili ya ununuzi wa barokoa kwa makundi ya watu wenye mahitaji maalum,” Bi Mwachache alisema.

Afisa huyo pia aliongeza kuwa Sh200 milioni kutoka Hazina ya Kitaifa zilitolewa kufadhili utoaji huduma katika vituo vya karantini ambako watu wanaoshukiwa kuwa na virusi vya corona walikuwa wakizuiwa.

Waziri Kagwe alisema uchunguzi unaendelea kuhusu sakata ya ununuzi wa dawa na bidhaa za kimatibabu katika halmashauri ya KEMSA pamoja na bidhaa za kimatibabu zilizotolewa kama msaada na Wakfu wa Jack Maa.

COVID-19: Visa vipya ni 606 idadi jumla nchini Kenya ikifika 18,581

Na MWANDISHI WETU

VISA vipya vya ugonjwa wa Covid-19 nchini Kenya ni 606 baada ya sampuli 4,888 kufanyiwa vipimo saa 24 zilizopita; Waziri Mutahi Kagwe ametangaza akiwa Afya House, Nairobi Jumanne, visa jumla nchini vikifika 18,581 tangu kisa cha kwanza Machi 13, 2020.

Waziri Kagwe ametahadharisha kwamba Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa maambukizi akitaja eneo ambalo limeanza kuonekana kama kitovu cha janga la corona.

“Eneo la Embakasi jijini Nairobi sasa ni ngome ya Covid-19,” amesema waziri.

Visa vya hivi punde ni 409 jinsia ya kiume huku 197 wakiwa wagonjwa wa jinsia ya kike.

Aidha wagonjwa ni Wakenya 583 nao 23 wakiwa raia wa kigeni.

Waziri amefichua kwamba mgonjwa wa umri mdogo ana umri wa miezi mitano naye yule mkubwa zaidi akiwa na umri wa miaka 85.

Habari njema, Bw Kagwe amesema kwamba watu 75 wamepona wakaruhusiwa kuenda nyumbani na hivyo kufikisha 7,908 idadi ya waliopona maradhi ya Covid-19.

Kenya imefanyia vipimo takriban sampuli 284,500.

Hata hivyo, amesikitika na kutuma salamu za pole kwa familia za watu wengine 14 waliofariki kutokana na Covid-19 na kuifanya 299 idadi jumla ya wahanga.

KAGWE: Serikali Tanzania iwashughulikie raia wake wagonjwa wa Covid-19

Na SAMMY WAWERU

WIZARA ya Afya ilisema Jumanne ni wajibu wa serikali ya nchi jirani ya Tanzania kushughulikia raia wake waliopatikana na ugonjwa wa Covid-19 maeneo ya mipakani.

Mikakati ya kuzuia msambao wa virusi vya corona maeneo ya mipakani inaendelea kuimarishwa, amri ya Rais Uhuru Kenyatta ya kufungwa kwa mipaka baina ya Kenya na Tanzania na vilevile Somalia, ikitekelezwa.

Rais alisema malori ya mizigo pekee ndiyo yataruhusiwa kuingia nchini.

Alichukua hatua hiyo kutokana na ongezeko la visa vya Covid-19 miongoni mwa madereva wanaotoka katika mataifa hayo kuingia nchini na pia wanaopitia njia za mkato.

Ni hatua inayoonekana kupokea upinzani kutoka kwa taifa la Tanzania na kuzua tumbojoto, nchi hiyo ikipiga marufuku madereva wa Kenya kuingia humo.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema Jumanne matarajio yake ni kwamba Tanzania inashughulikie raia wake wagonjwa wake wa Covid-19, akieleza kwamba ni jukumu lao kama serikali.

“Tanzania itashughulikia raia wake. Sisi kama maafisa wa afya hatuwezi; kazi yetu ni kuwataarifu,” akasema.

Bw Kagwe alisema madereva wa taifa hilo waliopatikana na virusi vya corona maeneo ya mipakani wamerejeshwa nchini humo.

“Tunawarudishia watu wao, wajue watakavyowatibu. Ni jukumu lao kuwafuata. Wasipofanya hivyo, wao ndio wataumia,” akaonya.

Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, wiki kadhaa zilizopita alinukuliwa akitilia shaka vifaa vya kukagua na kupima Covid-19.

Kisa cha kwanza cha ugonjwa huu kiliripotiwa Wuhan mwishoni mwa mwaka 2019.

Licha ya uhusiano wa Kenya na Tanzania kuonekana kudorora kufuatia visa vya Covid-19 mipakani, waziri alisema mataifa haya mawili yangali ‘ndugu’ na kwamba yataendelea kushirikiana.

Nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki zimetakiwa kushirikiana ili kusaidia kuzuia maambukizi zaidi ya corona.

Serikali yaonya wakazi wa Kiambu, Murangá, Machakos na Kajiado

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Afya Mutahi amewataka wakazi wa kaunti za Machakos, Kajiado, Kiambu na Murangá kuwa waangalifu na kuzingatia maagizo ya serikali, baada ya visa vya maambukizi ya virusi vya corona kuripotiwa katika kauunti hizo.

Akihutubu katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta alipokuwa akitoa taarifa ya kila siku kuhusu hali ya janga la corona nchini, Bw Kagwe Intermittent Fasting and Strength Training – Compatible Practice axio labs the 3 basic bodybuilding exercises sportissima. alisema wakazi wa kaunti hizo zinazopakana na Nairobi wana wanajibu wa kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo kutoka Nairobi.

“Tayari idadi fulani ya wenzenu wamepata virusi hivi na tumewatenga ili watibiwe. Katika kaunti ya Machakos, kwa mfano, tuna visa saba, Syokimau (2) na kisa kimoja katika kila moja ya maeneo yafuatayo; Athi River, Kamulu, Rubi Garden Estate, Githunguri na Viraji,” akasema.

Katika kaunti ya Kiambu, maeneo ya Githuria, Githurai 45, Ndongoru, Thindigua, Tinganga, Waithaka, na Watalaam yana kisa kimoja kila moja.

Na katika kaunti ya Kajiado, Waziri Kagwe aliripoti kuwa maeneo ya Kitengela, Matasia na Ongata Rongai yameshuhudia maambukizi.

Kuna visa vingine viwili katika kaunti ya Murangá : kutoka Gatanga na eneo la Lumumba Drive.

Waziri wa Afya alisema wagonjwa hao wote wanatibiwa katika hospitali mbalimbali akiongeza kuwa…. “tunatarajiwa kuwa hivi ndivyo vitakuwa visa vya mwisho kutoka kaunti zenu”

 

Visa vingine vinatoka mtaa wa Ruaka, kaunti ya Kiambu.

Mnamo Aprili 6, Rais Uhuru Kenyatta alitoa amri ya kusitisha safari za kutoka na kuingia jijini Nairobi na maeneo ya karibu, maarufu kimombo kama Nairobi Metropolitan area.

Alisema eneo la Nairobi Metropolitan kama sehemu za Kaunti ya Kiambu hadi daraja la mto Chania, Thika, Rironi, Ndenderu, Kiambu Mjini, sehemu za kaunti ya Machakos hadi Athi River likiwemo eneo la Kathani.

Vile vile, Nairobi Metropolitan inajumuisha maeneo ya Kajiado, yakiwemo Kitengela, Kiseriian, Ongata Rongai na Ngong mjini.

Rais Kenyatta alisema hatua hiyo inalenga kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona hadi maeneo mengine ya nchini ikizingatiwa kuwa asilimia ya visa vilivyoripotiwa kote nchini vinapatikana Nairobi.

Waliomkejeli Brenda wakamatwe – Kagwe

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe ameamuru polisii kuwakamata watu wanaeneza jumbe za kuwaharibia jina Brenda Cherotich na Brian Orinda kupitia mitandao ya kijamii baada ya kukiri kupona kutokana na Covid-19.

Akiongea nje ya Jumba la Afya House, Nairobi Alhamisi kwenye kikao na wanahabari, Kagwe alilaani vitendo hivyo akisema vinawadunisha wawili hao.

“Nimekerwa mno na baadhi ya Wakenya ambao ambao wamegeukia mitandao ya kijamii kueneza kejeli punde nilipowajulisha kuhusu vijana wetu wawili wamepona kutokana na ugonjwa huo hatari lakini wengine wamedai ni mzaha,” akasema.

“Serikali inawezaje, kwa ushirikiano na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kuamua kuwatumia Wakenya hao wawili kueneza uwongo. Nawataka maafisa wa usalama wawakamate watumiaji mitandao ya kijamii wanaoeneza jumbe kama hizo,” Bw Kagwe akaongeza huku akionekana mwenye hamaki.

Alisema serikali haitavumilia mienendo ya baadhi ya Wakenya kutaja juhudi zake katika kupambana na janga hilo kama shughuli za uhusiano mwema ama hadaa.

Baadhi ya Wakenya ametilia shaka maelezo ya Brenda kuhusu namna alivyopambukizwa na virusi hivyo hadi wakati alipojiwasilisha kwa Hospitali ya Mbagathi.

Wanasema baadhi ya maelezo aliyotoa kwenye mahojiano katika runinga ya NTV yalikinzana na yale aliyotoa katika studio za runinga ya Citizen.

Bunge laidhinisha Mutahi Kagwe na Betty Maina kuwa mawaziri

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE Jumatano waliidhinisha uteuzi wa aliyekuwa Seneti wa Nyeri Mutahi Kagwe na Betty Maina kuwa mawaziri wa Afya na Viwanda, mtawalia.

Wawili hao waliteuliwa katika baraza la mawaziri, katika mabadiliko yaliyotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Januari 14, 2020.

Bw Kagwe sasa ataapishwa rasmi ili aanze kuchapa kazi kama Waziri wa Afya baada ya Bi Sicily Kariuki kuhamishwa hadi Wizara ya Maji.

Na Bi Maina, ambaye awali alihudumu kama Katibu wa Wizara ya Ustawi wa Viwanda, Biashara na UjasiriaMali sasa ataapishwa kutwaa uongozi wa wizara hiyo.

Bw Kagwe ataingia afisini wakati ambapo Kenya iweka tahadhari kubwa baada ya mkurupuko wa Homa ya China kuripitiwa nchini China Desemba mwaka jana. Kufikia sasa, ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya corona umeangamizi takriban watu 2,200 wamefariki nchini China huku zaidi ya watu 70,000 wakiambuzwa virusi hivyo, maarufu kama, Covid -19.

Vile vile, Bw Kagwe anaingia afisini wakati ambapo Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) imeelekezewa lawama nyingi baada ya madai kuchipuza kwamba haitekelezi majukumu yake ipasavyo.

Alipokuwa akipigwa msasa na wabunge wiki jana, Bw Kagwe aliahidi kutekeleza mageuzi makubwa katika hazina hiyo, hatua ya mwanzo ikiwa na kuteua Afisa Mkuu Mtendaji mpya.

Bw Nicodemus Odongo, amekuwa akishikilia wadhifa huo kama kaimu Afisa Mkuu tangu Aprili 2018 Bw Geoffrey Mwangi alipoondolewa mamlakani baada ya kushtakiwa kwa sakata ya ufisadi ya kima cha Sh2 bilioni.

Wateule wengine ambo majina yao yaliidhinishwa na wabunge ni Julius Ouma Jwan aliyeteuliwa Katibu wa Idara ya Mafunzo ya Kiufundi, Balozi Simon Nabukwesi, Katibu wa Idara ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Utafiti na Enosh Onyango Momanyi kama katibu wa Idara ya Mipango ya Miji.