Tutapendekeza wanawake watengewe 50% ya nafasi za uongozi – Waiguru

Na BERNARDINE MUTANU

GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru Jumanne alisema viongozi wa kike watapendekeza kuondolewa kwa viti ‘maalum’ wakati wa kura ya maamuzi.

Akiwahutubia zaidi ya wasimamizi 300 wa wadi, kutoka kaunti zote 47, waliokuwa wamehudhuria mkutano wa siku tatu taasisi ya mafunzo ya kifedha (KSMS), Bi Waiguru alisema viongozi wa kike watatoa pendekezo la kugawana kwa asilimia 50-50 nafasi za uongozi nchini hasa kutokana na kuwa kanuni ya thuluthi mbili imekataa kufanya kazi.

Alisema, pendekezo hilo, ambalo watatoa wakati wa kura ya maamuzi ikiwa itafanyika, halina ‘nafasi maalum’ ambazo zitatolewa kwa wanawake wanaotafuta nafasi za uongozi.

“Tutatuma pendekezo la kishujaa ikiwa kutakuwa na kura ya maamuzi. Kanuni ya thuluthi mbili haifanyi kazi na tunapendekeza kugawana nafasi za uongozi kwa asilimia 50 -50,” alisema.

Gavana huyo alisema licha ya changamoto nyingi, uwakilishi wa wanawake nchini umeimarika na wanatarajia (wanawake) kupata magavana 10 wa kike 2022.

Hii ni kutokana na marekebisho ya kikatiba na utekelezaji unaoendelea wa usawa wa kijinsia na vile vile kujitolea kwa wanasiasa kuimarisha nafasi ya wanawake nchini.

Kwa sasa, kuna mawaziri sita wa kike, mawaziri wasaidizi wawili(CAS) kati ya 16 na makatibu wakuu nane kati ya 31.

“Siku za kesho zitakuwa nzuri na nafasi ya mwanamke itatambulika. Lakini wanafaa kuwa na uwezo wa kushindania nafasi katika sekta tofauti,” alisema, na kuwashauri wasimamizi hao kutwaa nafasi zilzoundwa na ugatuzi, Katiba, Agenda 4 za Maendeleo na mpango wa kujenga madaraja (BBI).

Aliwataka wasimamizi hao kufanya kazi na wasimamizi wa kaunti kwa lengo la kuwasaidia kukabiliana na changamoto za usimamizi. Aliongeza kuwa mkutano wa sita wa ugatuzi utaendeshwa Kirinyaga mnamo Machi 2019.

Aukot awarai Wakenya kuunga mkono kampeni ya #PunguzaMzigo

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Chama cha ThirdWay Alliance Ekuru Aukot amewataka Wakenya kuungana mkono mchakato wa marekebisho ya katiba unaopigiwa debe na chama hicho, akisema unalenga kuhakikisha kuwa pesa za umma zinagatuliwa hadi ngazi ya wadi.

Alisema kampeni yake maarufu kama “Punguza Mzigo Punda Amechoka” kufikia Jumanne asubuhi ilikuwa imepata sahihi 800,000 za Wakenya.

“Tunataraji kuwa ifikiapo Machi mwaka huu tutaweza kupata sahihi 200,00 zinazosalia ili kufikisha sahihi 1 milioni zinazohitajika kwa mujibu wa Katiba kufanikisha mpango huu. Tunawataka wananchi wengi kuunga mkono mchakato huu kwa sababu unalenga kuondoa viti mbalimbali vya uwakilishi ili pesa nyingi zielekezwe katika miradi ya afya, elimu, barabara, kati ya mingine,” Bw Aukot akawaambia wanahabari Jumanne katika makao makuu ya chama chake mtaani Lavington, Nairobi.

Alisema marekebisho ya katiba yanayopigiwa debe ya vyama vya ODM, Ford Kenya, KANU, na ANC yanalenga kuwaongeza Wakenya mzigo kupitia kubuniwa kwa nyadhifa zaidi ya uongozi kama vile cheo cha Waziri Mkuu na manaibu wake.

“Wakenya hawafai kuhadai na watu kama hawa ambao, walifaidi katika eneo ya utawala wa chama cha Kanu, lakini sasa wanawahadaa kwamba wanapigania marekebisho ya katiba. Huu ni unafiki uliokithiri mipaka,” akasema Bw Aukot.

Wakati huo huo, Bw Aukot amewasuta viongozi wa Jubilee kwa kuendeleza siasa za urithi wakati huu ambapo Wakenya wanawatarajiwa kutimiza zile ahadi ambazo walitoa wakati wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

“Inasitika kuwa vinara wakuu wa Jubilee wameanza kuzozana kuhusu siasa za 2022 ilhali hawatimiza ahadi ambazo waliwapa Wakenya. Sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto, gharama ya maisha imepanda,vijana hawana ajira na wizi wa pesa za umma unaendelea katika idara zote za serikali ihali kile ambacho ngoma inayochezwa ni ile ya uchaguzi wa 2022,” akasema.

Bw Aukot akaongeza: “Ikiwa walianza kampeni za 2022, siku chache baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 ina maana ahadi zote walizowapa Wakenya hazikuwa na maana yoyote. Waliwadanga wananchi ambao walijitokeza kwa wingi kuwapigia kura.”

Alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwa mstari wa mbele kupalilia maridhiano ya kisiasa kwa kukoma kutumia maneno makali dhidi ya wanasiasa ambao wanahoji uongozi wake.

“Yeye ni kiongozi wa taifa na anapaswa kudhihirisha uvumilivu. Hafai kuwazomea viongozi wengine hadharani kwa maneno makali,” akasema Bw Aukot.

Mnamo Jumatatu, Rais Kenyatta aliwataja kama “washenzi” wanasiasa kutoka eneo la Mlima Kenya ambao wamekuwa wakidai kuwa serikali yake imetenga eneo hilo kimaendeleo.

“Wajibu wangu kama Rais ni kutahakikisha kuwa maendeleo yanasambazwa katika pembe zote nchini. Kuanza sasa nitazunguka kuanza Kisumu hadi Mombasa, Namanga hadi Lodwar kuzindua miradi ya maendeleo. Hizi siasa za kutaka maendeleo yakite katika eneo ambako kiongozi anatoka pekee sharti zikome,” akasema.

KANU yamkemea Ruto kubadili nia kuhusu katiba

Na WYCLIFF KIPSANG

VIONGOZI wa Chama cha KANU wamemkashifu Naibu Rais William Ruto kwa kupinga kura ya maamuzi ambayo itapelekea kupunguza idadi ya kaunti na madiwani.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw Nick Salat, jana alisema naibu rais anafaa awe anasaidia taifa kupunguza gharama ya kulipa mishahara ya watumishi wa umma.

“Inaonekana hajali kuhusu Kenya. Anamaanisha tuendelee kuwa na wafanyakazi wengi shambani wanaozalisha mazao machache, au tupunguze idadi hiyo? Inafaa azingatie hali ya kifedha ya nchi hii,” akasema Bw Salat.

Aliongeza: “Ninashangaa kuona naibu rais akitetea gharama kubwa ya mishahara ambayo haiwezi kustahimiliwa na mapato yetu ya jumla ya taifa. Tunahitaji kupunguza gharama ya mishahara ikiwemo kwa kupunguza idadi ya wafanyakazi.”

Viongozi wa KANU pia walimkosoa kwa kudai kwamba rekodi yake ya maendeleo inaonyesha wazi uwezo wake wa uongozi na hahitaji kushikwa mkono na vigogo wa kisiasa ndipo ashinde urais 2022.

Mwenyekiti wa chama hicho, tawi la Kaskazini mwa Rift Valley, Bw Paul Kibet, alisema miradi ambayo Bw Ruto amekuwa akizindua maeneo mbalimbali nchini haina msingi kwani ni miradi inayotekelezwa na wabunge katika maeneobunge yao.

“Kile anachofanya ni kuharibu fedha za umma kwa kazi ambazo zinaweza kushughulikiwa hata na wasimamizi wa kaunti ndogo. Ana kipi kipya anachoweza kutuonyesha ilhali watu wake wanakumbwa na umaskini? Badala ya kujitahidi kuinua hali ya maisha kwa wananchi, anawaambia waanze kilimo cha parachichi ambayo haiwezi kuwasaidia kiriziki,” akasema Bw Kibet.

Hivi majuzi, Naibu Rais alisema ataunga mkono marekebisho ya katiba ikiwa tu yatahusu kuimarisha ugatuzi.

Wakati Dkt Ruto alipokutana na madiwani wa Kaunti za Kakamega, Baringo na Elgeyo-Marakwet bomani mwake Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu, alisisitiza ataunga mkono mjadala wowote utakaohusu tu uimarishaji wa ugatuzi na kuongeza mgao wa fedha kwa serikali za kaunti wala si kubuni nafasi za kisiasa kwa manufaa ya viongozi wachache.

“Kinyume na inavyodhaniwa, sipingi marekebisho ya katiba. Kitu chochote kitakachoathiri matunda ya ugatuzi ndicho kitapingwa. Tunataka kuona marekebisho ambayo yatawezesha kaunti kustawi,” akasema Dkt Ruto.

Kulingana naye, hakuna jinsi wapinzani wake wanaomezea mate urais 2022 watamshinda kwa kusubiri kupigiwa debe na vigogo wengine wa kisiasa kama hawana miradi ya maendeleo wanayoweza kuonyesha wananchi.

“Kuna wale wanaosubiri kutangazwa kuwa wanatosha. Unatarajiaje kupigiwa debe kama huna ajenda wala mpango utakaonufaisha nchi?” akauliza Ruto.

“Niko tayari kupambana na mtu yeyote. Acha wapinzani wangu waonyeshe kile walichofanyia nchi hii,” akasema Naibu Rais ambaye pia alikuwa na viongozi wa Magharibi mwa Kenya.

Alisema mtu yeyote anayetaka kushindana naye uchaguzini yuko huru kwani haogopi ushindani.

Kaunti zipewe ufadhili wa 47% kwenye marekebisho ya Katiba – Makanisa

Na PIUS MAUNDU

BARAZA la Kitaifa la Makanisa Kenya (NCCK) sasa linashinikiza mageuzi ya Katiba ili kustawisha ukuaji wa kiuchumi kupitia ugatuzi.

“Katiba inapaswa kutathminiwa upya ili kuongeza kiwango cha fedha ambacho kinatengewa kaunti kutoka asilimia 15 hadi 47. Hilo litaongeza kasi ya maendeleo katika kaunti hizo,” akasema Askofu Timothy Ndambuki, ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza hilo. Kulingana naye, kuongezwa kwa mgao huo wa fedha pia kutapunguza kiwango cha ufisadi katika kaunti.

Askofu huyo, alitoa kauli hiyo mnamo Jumamosi kwenye hafla ya kuwahamasisha wakazi kuhusu umuhimu wa kutega maji ya mvua katika Shule ya Upili ya Malaa, Kaunti ya Makueni. Askofu huyo, ambaye pia ndiye mkuu wa kanisa na ABC katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini aliandamana na mshirikishi wa baraza hilo katika eneo la mashariki Faith Sibairo.

“Sakata za ufisadi ambazo zimekuwa zikiripotiwa katika serikali ya kitaifa zinachangiwa na hali kuwa baadhi ya idara zinazotengewa fedha huwa hazizitumii kwani huwa hazina mipango maalum ya maendeleo. Fedha hizo zinapaswa kutengewa serikali za kaunti,” akasema Bw Ndambuki.

Alisema kuwa eneo la Ukambani lilikuwa limebaki nyuma kimaendeleo, ila hali hiyo imebadilika kutokana na uwepo wa ugatuzi.

Miongoni mwa waliohutubu kwenye hafla hiyo ni Gavana Kivutha Kibwana, Naibu Gavana Adelina Mwau, mbunge wa Mbooni Erastus Kivasu na Kiongozi wa Wengi katika kaunti hiyo Kyalo Mumo.

Waliozungumza walisifia mipango ya utegaji maji inayoendelezwa na wakulima binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na serikali ya kaunti hiyo, wakisema kuwa yatabadilisha maisha ya wakazi.

Viongozi waliwahimiza wakazi kutumia kilimo cha maji kuanza miradi itakayoimarisha maisha yao.

Makamishna wapya wa IEBC wateuliwe kabla ya referenda – Opiyo Wandayi

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Ugunja Opiyo Wandayi amesisitiza kuwa sharti nafasi za makamishna wanne wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) zijazwe kwanza kabla ya tume hiyo kuruhusiwa kuendesha kura ya maamuzi kuhusu mabadiliko ya katiba.

Akiongea na wanahabari Jumanne katika majengo ya bunge, Nairobi mbunge alisema kuwa kura ya maamuzi “ni kibarua kikubwa ambacho hakiwezi kuendeshwa na makamishna watatu walioko sasa.”

“Kwa sababu ni wazi kuwa sharti katiba ya sasa ifanyiwe marekebisho kupitia kura ya maamuzi ningependa kamati ya bunge kuhusu haki na masuala ya sheria (JLAC) kuanza mchakato wa kubadilisha sheria ya IEBC ili kutoa nafasi ya kubuniwa kwa jopo la kuteua wamakishna wapya kuchukua mahala pa wale ambao wamajiuzulu.

Kura ya maamuzi sio uchaguzi mdogo ambao unaweza kuendeshwa na Bw Wafula Chebukati na wenzake wawili,” akasema Bw Wandayi ambaye ni ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC).

Wiki jana Bw Chebukati alinukuliwa akisema kuwa kuwa tume hiyo inaweza kuendesha kura ya maaamuzi hata kabla ya nafasi za makamishna wanne waliojiondoa kujazwa.

Na siku mbili zilizopita Kamishna Boya Molu alikariri msimamo huo akinukuu kipengee cha Katiba kinachosema kuwa tume za kikatiba sharti ziwe na angalau makamishna watatu kabla ya kuruhusiiwa kuendeshwa majukumu yazo kisheria.

“Tulivyo hapa sisi ni makamishna watatu, na hivyo sisi ni kamilifu kisheria na kiutendakazi. Tunaweza kutekeleza majukumu yote kwa mujibu wa katiba, ikiwemo kura ya maamuzi, bila sheria yoyote,” akasema Bw Molu mjini Wote wakati tume hiyo ilipozindua zoezi endelevu la usajili wa wapiga kura wa wapiga kura wapya.

Makamishna ambao walijiuzulu ni; Dkt Roselyn Akombe (aliyejiondoa kabla ya marudio ya uchaguzi wa urais wa Oktoba 26, 2017) pamoja na Consolata Maina, Margaret Mwachanya na Dkt Paul Kurgar waliong’atuka Aprili 16, mwaka huu.

Wakati huo huo, Bw Wandayi na mwenyekiti wa JLAC William Cheptumo wamependekeza kuwa makamishna na wafanyakazi wote wa IEBC wachunguzwe kuhusiana na ubadhirifu wa mabilioni ya pesa za umma kuelekea uchaguzi mkuu uliopita.

Walitoa wito kwa maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana Ufisadi (EACC) na wenzao wa afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) waanze zoezi hilo kwa kumchunguza mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati kwanza.

“Maafisa wa EACC, DPP na DCI hawafai kusibiri mwaliko wa Bw Chebukati kabla ya kuanza kuchunguza IEBC, wanafaa kuanza uchagunzi wa haraka kuanza kwa mwenyekiti mwenyewe, makamishna wenzake na wafanyakazi wote wa afisi kuu. Uchunguzi huo haufai kuleng Bw Ezra Chiloba pekee ambaye alifutwa kazi wiki jana,” Bw Wandayi, kauli iliyoungwa mkono na Bw Cheptumo.

“Wafanyakazi wa IEBC ambao walikuwa afisini kabla na wakati wa uchaguzi mkuu kama vile aliyekuwa Mkuregenzi wa Uchaguzi Bi Emmaculate Kassait pia hawafaio kusazwa,” akasema Bw Cheptumo ambaye ni Mbunge wa Baringo Kaskazini katika mahojiano tofauti.

Bw Wandayi alisema kamati ya PAC wakati huu inachambua ripoti ya Mhasibu Mkuu wa Serikali Edward Ouko ambayo inafichua kuwa Sh9.5 bilioni hazijulikani zilivyotumiwa na IEBC wakati wa ununuzi wa bidhaa na uagizaji wa hudumu kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 8, na marudio ya uchaguzi wa urais wa Oktoba 26 mwaka 2017.

“Kama kamati tunaamini kuwa makamisha na wafanyakazi kadhaa wa IEBC walihusika katika sakata hii wala sio Chiloba pekee… ndiposa tunasema wote wanafaa kupigwa darubuni na watakaopatikana na hatia waadhibiwe kwa mujibu wa sheria,” akasisitiza.

Mnamo Jumatano, Bw Chebukati alisema kuwa amewaandikia maafisa wa EACC na DPP akiwaomba wamchunguze Bw Chiloba na maafisa wengine wanaodaiwa kufuja fedha za umma kuelekea uchaguzi mkuu uliopita.

“Nimeandikia EACC na DPP ili waanzesha uchunguzi kuhakikisha kuwa wale wote waliochangia uchaguzi mkuu uliopita kuwa ghali kupita kiasi wanashtakiwa,” mwenyekiti huyo alisema mji Wote kaunti ya Makueni alipozindua zoezi la usajili wa wapiga kura wapya.

Wiki iliyopita, IEBC ilimfuta kazi Bw Chiloba kwa kile kilichosemekana na hatua ya kukataa kufiki mbele ya kamati ya nidhamu ili ajitetee kuhusiana na madai matumizi mabaya ya fedha za wakati wa ununuzi wa vifaa vya uchaguzi.

REFERENDA: Wabunge kuamua kuhusu terehe ya uchaguzi

HUENDA Wakenya wakashiriki kura ya maamuzi ikiwa wabunge Jumatano wataupitisha mswada unaolenga kubadilishwa tarehe ya uchaguzi mkuu kutoka Agosti hadi Desemba.

Hii ni kwa sababu mswada huo wa marekebisho ya Katiba utaongeza muda wa kuhudumu kwa Rais Uhuru Kenyatta kwa miezi minne zaidi ikiwa uchaguzi mkuu utafanyika Desemba 2022.

Kuongeza kuwa muda wa kuhudumu kwa Rais ni mojawapo ya masuala ambayo sharti yabadilishwe kupitia kura ya maamuzi, kulingana na kipengee cha 255 cha katiba ya sasa.

Mswada huo ambao umedhaminiwa na Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa (pichani) unapendekeza tarehe ya uchaguzi ibadilishwe kutoka Jumanne ya pili mwezi Agosti kila baada ya miaka mitano baada ya uchaguzi mkuu hadi Jumatatu ya tatu mwezi Desemba miaka mitano baada ya uchaguzi.

Mnamo Alhamisi, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alisema Rais ndiye ataamua ikiwa mswada huo utawasilishwa kwa raia kwa kura ya maamuzi endapo utaungwa mkono na angalau wabunge 233 katika kura itakayopigwa bunge leo alasiri.

Hii ni baada ya mswada huo kuwasilishwa katika bunge la Seneti na kupitishwa na angalau maseneta thuluthi mbili yao, yaani maseneta 45 kati ya maseneta wote 67.

‘Ningependa kuwajulisha wabunge kwamba uamuzi kuhusu mswada huo wa marekebisho ya katiba ili kubadili tarehe ya uchaguzi mkuu utafanywa Jumatano alasiri,’ akasema Bw Muturi.

‘Iwapo wabunge 233 watapiga kura kuunga mkono mswada huo baada ya kujadiliwa kwa Hatua ya Pili (Second Reading), Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge (HBC) itauorodhesha ili ujadiliwe kwa Kamati ya Bunge lote ambayo itafanyika katika vikao vijavyo. Baadaye mswada huu utawasilishwa kwa seneti,’ akawaambia wabunge.

Bw Muturi alisema wajibu wa Bunge ni kutekeleza mamlaka yake katika uundaji wa sheria kwa kupitisha mswada wa kuifanyia Katiba marekebisho.

‘Baada ya mswada huu kupitishwa katika mabunge yote mawili na kuwasilishwa kwa rais ili autie saini, itakuwa ni wajibu wa Afisi ya Rais kuamua kama mswada huo unahusu masuala ambayo yameorodheshwa katika kipengee cha 255.

Masuala katika kipengee hicho ni yale ambayo sharti yaamuliwe kupitia kura ya maamuzi, kama vile kuongezwa kwa kipindi cha kuhudumu kwa rais na kubadilishwa kwa mfumo wa uongozi, kati ya mengine.

Mengine ni yale yanahusu; Ukuu wa Katiba, Mipaka ya Kenya, Mamlaka ya wananchi, Maadili ya kitaifa na kanuni za uongozi, Sura kuhusu Haki, Idara ya Mahakama, Bunge, Serikali ya Ugatuzi na Tume za Kikatiba.

Spika Muturi alisema hoja ya kupigia kura mswada huo ikifeli kuuungwa mkono na angalau wabunge 233, anaweza kutoa nafasi nyingine kwa bunge kuamua kuhusu suala hilo, kulingana na mamlaka aliyepewa katika sheria ya bunge nambari 62 (2).

ONYANGO: Raila achunge sana asiwe mwathiriwa wa referenda

Na LEONARD ONYANGO

MJADALA kuhusu kuibadilisha Katiba kupitia kura ya maamuzi unazidi kuchacha huku idadi kubwa ya wanasiasa wakiunga mkono.

Wito huo ambao ulitolewa kwa mara ya kwanza na kiongozi wa ODM Raila Odinga umepingwa na baadhi ya wanasiasa wakiongozwa na Naibu wa Rais William Ruto wanaodai kuwa kiongozi huyo wa upinzani analenga kutumia Katiba kujipatia wadhifa wa waziri mkuu serikalini.

Bw Odinga alikuwa katika mstari wa mbele kupigia debe rasimu ya Katiba mnamo 2010 lakini yeye pia ni miongoni mwa waathiriwa walioonja makali ya Katiba hiyo.

Kwa mfano, wakati wa kampeni za kura ya maamuzi miaka minane iliyopita Bw Odinga alieleza Wakenya kuwa polisi wangepigia saluti washukiwa kabla ya kuwakamata.

Bw Odinga alisema Katiba ya 2010 ingalifikisha mwisho udhalimu wa maafisa wa polisi.

Lakini kiongozi huyu wa upinzani ndiye ameshuhudia udhalimu mkubwa wa polisi, haswa kabla ya uchaguzi uliopita.

Bw Odinga na viongozi wengine wa muungano wa NASA pamoja na wafuasi wao walitawanywa kwa vitoa machozi na hata kupigwa viboko na polisi wakati wa maandamano ya kutaka kuondoa afisini baadhi ya maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Udhalimu wa polisi bado unaendelea kudhihirishwa dhidi ya Wakenya wanaoandamana kulalamikia haki zao. Madaktari, wauguzi, wanaharakati wa mashirika mbalimbali ya kijamii pia wamepokea vipigo kutoka kwa polisi wakati wa maandamano.

Udhalimu

Hivyo basi, Bw Odinga anapopigania mabadiliko ya Katiba ahakikishe kuwa udhalimu huo wa polisi unakomeshwa endapo kutakuwa na kura ya maamuzi.

Katiba ya 2010 ilifutilia mbali afisi kama vile za Kiongozi wa Upinzani na nyadhifa nyinginezo kama vile kuwania urais pamoja na ubunge kwa pamoja.

Katiba ya 2010 ilipoanza kutumika katika uchaguzi wa 2013, Bw Odinga aliambulia patupu na kujipata kwenye baridi ya kisiasa.

Bw Odinga alibandikwa ‘cheo’ cha kiongozi wa upinzani licha ya Katiba kutotambua afisi hiyo.

Kufikia sasa, Bw Odinga ambaye ana wafuasi zaidi ya milioni tano, yungali katika baridi ya kisiasa licha ya kukubali kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta.

Wanaounga mkono mabadiliko ya Katiba wahakikishe kuwa viongozi walio na uungwaji mkubwa nchini wanapata majukumu ya kutekeleza badala ya kutelekezwa kisiasa kama ilivyo kwa sasa.

Afisi ya kiongozi wa upinzani inafaa irejeshwe ili kumwezesha kiongozi aliyebwagwa katika urais lakini aliye na idadi kubwa ya wafuasi aweze kutekeleza majukumu ya kuchunguza serikali na kufichua sakata mbalimbali za ufisadi.

Afisi ya kiongozi wa upinzani inastahili kutengewa fedha za kutekeleza majukumu yake.

Mara hii Bw Odinga anapopigania mabadiliko ya Katiba achunge asije akajipata mateka wa mabadiliko hayo.

Referenda ni nafasi murua kwa wanawake kutetea jinsia – Karua

IRENE MUGO na OSCAR KAKAI

KIONGOZI wa chama cha Narc Kenya, Bi Martha Karua, amewataka wanawake kutetea usawa wa jinsia kwenye mageuzi ya Katiba yanayopendekezwa.

Alisema anaunga wito wa kura ya maamuzi ambapo maeneobunge yatabadilishwa kuwa wadi kila moja ikiwakilishwa na mwanamume na mwanamke kama njia moja ya kuhakikisha usawa wa jinsia.

“Mageuzi ya Katiba yanafaa na yanapaswa kutumiwa kujaza pengo la jinsia,” alisema. Alikuwa akihutubia madiwani wanawake wa bunge la Kaunti ya Nyeri walipozindua mwongozo wao.

Alipendekeza mageuzi ya Katiba ambapo wanawake watakuwa wakiwa wagombeawenza ikiwa anayegombea kiti cha urais ni mwanamume.

“Kama wanawake, ni lazima tuchangie katika mageuzi ya Katiba na kuhakikisha tumefaidika na pia tuhakikishe Katiba imebadilishwa ili mgombea urais akiwa mwanamume, mgombeamwenza awe ni mwanamke na iwapo ni mwanamke mgombea mwenza anafaa kuwa mwanamume,” alisema Bi Karua.

Alipendekeza kuwa wabunge na maseneta hawafai kuzidi 188 badala ya 416 ilivyo kwa sasa.

Alisema maeneobunge 290 yanapaswa kubadilishwa kuwa wadi kila moja na yawakilishwe na mwanamume na mwanamke ili kuwe na usawa wa jinsia.

Aidha, Bi Karua alisema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inafaa kufanyiwa mageuzi kabla ya nchi kuandaa kura ya maamuzi.

“Huu ndio wakati wa kurekebisha mambo kwa kupunguza bajeti ya IEBC. Uchaguzi Kenya unagharimu pesa nyingi kuliko nchi zinazoendelea ulimwenguni,” alisema.

Kwingineko, walimu wa Pokot Magharibi wametishia kuunga mkono pendekezo la kurekebisha Katiba ili kuirejesha Tume ya Huduma kwa walimu nchini (TSC) chini ya wizara ya Elimu.

Waliapa kushiriki mgomo wa kitaifa kulemeza mitihani ya kidato cha nne na darasa la nane, ikiwa mkutano wao na mwajiri wao ambao umepangwa kufanyika Jumatano wiki hii hautazaa matunda.

Wakihutubia wanahabari mjini Kapenguria, walimu hao walitoa wito kwa TSC kuipiga msasa sera yake kuhusu uhamisho ili kuimarisha utendakazi wa walimu.

Katibu wa Knut tawi hilo, Bw Martin Sembelo, aliwaongoza walimu kuilaumu TSC kwa kupuuza mahangaiko wanayopitia.

“Ikiwa TSC haitaelewa kuwa walimu ndio walichangia tume hiyo kuwa huru kwenye Katiba ya mwaka wa 2010, tutairudisha kwenye wizara ambapo matakwa ya walimu yanaweza kusikilizwa. Sera hiyo inafaa kuangaliwa na kuchunguzwa kwa kina,” alisema.

Bw Sembelo alisema kuwa walimu wengi wameshindwa kufika katika vituo mbalimbali kutokana na suala la umri na wengi wamekuwa wagonjwa.

Mjadala kuhusu kuifanyia marekebisho Katiba umeshika kasi, na sasa walimu nao wanasema watatumia fursa hii kupendekeza TSC isiwe tume huru.

Wanaamini kuwa endapo itakuwa chini ya wizara ya Elimu, itakuwa ikibuni na kutekeleza sera chini ya uangalizi wa wizara, ambayo itakuwa ikitoa ushauri unaofaa kuhusu sera hizo.

REFERENDA: Raila amchenga Uhuru

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya kinara wa ODM, Raila Odinga kupigia debe marekebisho ya Katiba imekiuka makubaliano kati yake na Rais Uhuru Kenyatta kwenye mwafaka wao wa maelewano.

Kulingana na mwafaka huo ulioafikiwa Machi 9, miongoni mwa waliyokubaliana ni kubuni kamati ya watu 14 ambayo ingekuwa na jukumu la kukusanya maoni kutoka kwa Wakenya, ili waeleze wanayotaka yafanyike katika kujenga uwiano nchini.

Kamati hiyo ilibuniwa ikiongozwa na Wakili Paul Mwangi na Balozi Martin Kimani na ndiyo ingetoa mwelekeo wa iwapo Katiba itafanyiwa mageuzi, aina ya mageuzi wanayotaka Wakenya na lini.

Hata hivyo, hata kabla ya kamati hiyo kuanza kukusanya maoni ya wananchi, Bw Odinga alianza kupigia debe kura ya maamuzi. Hii inaonekana kama mbinu ya kuwekea kamati hiyo ajenda na kushawishi mapendekezo yake.

Kwa upande wake Rais Kenyatta amekuwa kimya kuhusu mjadala wa marekebisho ya Katiba.

Bw Mwangi, ambaye ni mwandani wa Bw Odinga na wakili wake, anasema ni mapema kuendeleza mjadala kuhusu kura ya maamuzi.

“Ninahisi kwamba Rais Kenyatta na Bw Odinga hawatasita kufanya mageuzi yanayofaa baada ya kamati kukusanya maoni,” alisema Bw Mwangi kwenye mahojiano na runinga ya Citizen.

Kulingana na Dkt Edward Kisiang’ani, mhadhiri na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, kwa kuzua mjadala wa Katiba hata kabla ya ripoti ya kamati, Bw Odinga anacheza sarakasi za siasa.

“Kwanza anaonekana kutoelewa anachotaka katika kura ya maamuzi. Tunaona mtu anayetaka kuweka vipengele katika Katiba kulinda maslahi yake ya kibinafsi na hii huenda isifurahishe Wakenya,” alisema Dkt Kisiang’ani.

Bw Odinga anaonekana kujikanganya katika msimamo wake kwani amekuwa akikiri kwamba ni kamati hiyo ya watu 14 itakayotoa ripoti ya mwisho kuhusu mageuzi ya kikatiba ambayo Wakenya watataka.

“Wakenya wakisema tupige nyundo hapa, tulainishe pale, hakuna makosa,” kiongozi huyo wa upinzani amenukuliwa akisema mara kwa mara.

Kwenye hafla zingine amekuwa akisisitiza kuwa ni sharti mageuzi ya Katiba yafanyike.

Rais Kenyatta kwa upande wake ameepuka suala hilo akisisitiza kuwa lililo muhimu kwake kwa wakati huu ni kuwahudumia Wakenya.

“Uhuru anafahamu kwamba wanasiasa wana misimamo yao na yuko makini sana kutomwaga mtama kuhusu msimamo wake kabla ya kamati kukusanya maoni kutoka kwa Wakenya,” alisema mbunge mmoja wa chama cha Jubilee.

Anasema Rais Kenyatta hataki suala hilo lionekane kama maafikiano ya watu wawili na ndio sababu waliunda kamati ya watu 14 kukusanya maoni ya Wakenya.

Msemaji wa Ikulu Kanze Dena pia alisema hawezi kueleza msimamo wa Rais kwa sababu hajazungumzia suala hilo.

Kulingana na mdadisi wa masuala ya kisiasa Mutahi Ngunyi, ikiwa Rais na na Bw Odinga wanaunga kura ya maamuzi hakuna atakayezuia ifanyike.

Hata hivyo, aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale anahisi kwamba mbio za Bw Odinga huenda zikamtumbukiza pabaya.

“Raila alikubali kutumiwa na serikali ya Jubilee. Wakati wake wa kuaibika utafika na atagundua hakuna chake,” alisema Bw Khalwale.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna naye anakiri kwamba kura ya maamuzi itategemea jopo la watu 14.

Wabunge kuamua tarehe mpya ya uchaguzi

Na DAVID MWERE

WABUNGE Jumatano wataupigia kura mswada unaopendekeza tarehe ya uchaguzi mkuu ujao ibadilishwe kutoka Jumanne ya pili ya mwezi Agosti hadi Jumatatu ya kwanza ya mwezi Disemba, hali itakayoongeza muda wao ofisini kwa miezi minne.

Mswada huo wa Marekebisho ya Katiba 2017 unadhaminiwa na Mbunge wa Kimilili, Dkt Chris Wamalwa na itahitaji theluthi mbili ya wabunge kuupitisha, hii ikiwa ni wabunge 233 kulingana na katiba.

Kwa mujibu wa mbunge huyo wa chama cha Ford Kenya, mswada wake unaugwa mkono na idadi kubwa ya wabunge wenzake.

Anasema kwamba karibu wabunge 250 wamemhakikishia kuwa wataupitisha wakati wa kuupigia kura saa nane mchana.

“Sina shaka kwamba mswada huu utapitishwa kwa sababu ninaungwaji mkono wa wenzangu wengi,” akasema Dkt Wamalwa.

Alisisitiza kwamba tarehe ya uchaguzi lazima iheshimu tamaduni na mienendo zilizizokuwepo kabla ya kurasmishwa kwa katiba mpya.

Iwapo utapitishwa, mswada huo pia unatarajiwa kuathiri uchaguzi wa maseneta, wawakilishi wadi, magavana na urais ambao pia watasalia mamlakani kwa miezi minne zaidi.

Sababu nyingine anayoitaja Dkt Wamalwa ya kutaka mabadiliko hayo yatekelezwe ni mitihani na kitaifa ya KCPE na KCPE inayoandaliwa mwezi Oktoba na Novemba, akisema kura za mwezi Agosti huathiri masomo ya watahiniwa haswa kukiandaliwa uchaguzi wa marudio jinsi ilivyokuwa mwaka jana.

Hata hivyo, kikwazo kikuu ni hitaji la sheria kwamba mabadiliko hayo yatakumbatiwa tu kupitia kuandaliwa kwa kura ya maamuzi kwa kuwa kubadilishwa kwa tarehe ya kura pia husogesha muda wa kuhudumu kwa rais.

Kikwazo kingine ni gharama ya kura ya maoni inayokadiriwa kuwa Sh12 bilioni kulingana na Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ambayo kwa sasa haiwezi kuwajibika kikamilifu baada ya makamishina wanne kujiuzulu mwaka jana na bado nafasi zao hazijajazwa.

Mswada kama huo ulikataliwa mwaka wa 2014 ulipowasilishwa na aliyekuwa Mbunge wa Ugenya, Bw David Ochieng.

Raila na Ruto wateka mageuzi ya Katiba

Na BENSON MATHEKA

WITO wa kura ya maamuzi ili kufanyia Katiba marekebisho, umegeuka safu mpya ya vita vya ubabe kati ya Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga. Hii inaibua maswali kuhusu iwapo mabadiliko yanayokusudiwa yanalenga kufaidi mwananchi wa kawaida ama wanasiasa.

Viongozi hao wawili wameonekana kuteka mjadala kuhusu marekebisho hayo, na kufanya suala hilo kuchukua mkondo wa siasa za mgawanyiko zinazolenga hasa uchaguzi mkuu wa 2022.

Imeibuka kuwa Bw Ruto na Bw Odinga wanachukua fursa hii kujipigia debe kwa kutaka wananchi wawaone kama wanaowajali kwa kusukuma wapunguziwe mzigo wa maisha unaotokana na mahitaji ya Katiba ya sasa, ambayo imebuni nyadhifa nyingi za uongozi zenye gharama kubwa.

Wakiandamana na wandani wao, Bw Odinga na Bw Ruto wamekuwa wakizunguka nchini wakitoa misimamo tofauti kuhusu kura hiyo, kila mmoja akivutia kwake.

Ingawa Bw Odinga amekuwa akidai kwamba mabadiliko ya Katiba ni miongoni mwa masuala aliyokubaliana na Rais Kenyatta, Bw Ruto amekuwa akidai kwamba kiongozi huyo wa ODM analenga kutumia kura ya maamuzi kubuni nyadhifa mpya serikalini.

Awali, Bw Ruto alikuwa amepinga kufanyika kwa kura hiyo lakini juzi alishangaza wengi alipobadilisha msimamo na kuunga mkono.

Kufikia sasa, wanasiasa hao wawili na wandani wao wamegawanyika kuhusu masuala yanayofaa kushirikishwa kwenye kura ya maamuzi ili kupigiwa kura.

Kambi ya Bw Ruto inasisitiza kuwa kuna viongozi wanaotaka kura hiyo iwe ya kubuni nyadhifa mpya ili kufaidi wanasiasa wachache katika kile wanachodai ni kuhusisha Wakenya wote serikalini.

Akiongea akiwa Meru siku moja baada ya kukubali kura ya maamuzi, Bw Ruto alisema atakubali kura ya maamuzi inayolenga kupunguzia raia mzigo wa kupanda kwa gharama ya maisha.

“Ikiwa wale wanafikiri watatumia kura ya maamuzi kubuni nyadhifa mpya tunawaambia wasahau,” Bw Ruto alisema.

Bw Odinga naye amekuwa akipendekeza mfumo wa ugatuzi unaohusisha viwango vitatu kwa kubuni maeneo 16 badala ya kaunti 47 zilizopo kwa wakati huu.

Pendekezo hili tayari limepingwa na wengi wakidai mfumo wa ugatuzi wa sasa umefaidi Wakenya mashinani na haufai kubadilishwa.

Wandani wa Bw Odinga wamekuwa wakipendekeza mfumo wa serikali ya bunge ambao utakuwa na waziri mkuu na manaibu wake wawili.

Ingawa walikaribisha hatua ya Bw Ruto ya kukubali kura hiyo, wanasiasa wanaomuunga Bw Odinga wanasema Naibu Rais hafai kutoa masharti kuhusu yanayopaswa kushirikishwa na pia wanasisitiza kukubali kwake kuna unafiki ndani yake.

Malumbano ya viongozi hao na wandani wao yanaonyesha kuwa wanasiasa wanalenga kutimiza malengo yao ya kibinafsi.

Kwa upande mwingine wananchi wameonekana kutazama tu huku mashirika ya kijamii na kitaaluma yakikaa kimya.

Ni Baraza la Kitaifa la Makanisa (NCCK) ambalo limejitokeza wazi kujadili suala hili. Baraza hili linaunga pendekezo la kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu lakini linaunga kupunguzwa kwa viti vya uwakilishi. Kulingana na katibu mkuu wa NCCK Canon Peter Karanja, idadi ya mawaziri pia inafaa kupunguzwa.

Lakini muungano wa mashirika ya kijamii (CSRG) unaonya kuwa pendekezo la kupunguza idadi ya wawakilishi halifai kulenga wanawake na vijana katika juhudi za kupunguza gharama ya maisha katika serikali kuu na serikali za kaunti.

Mshirikishi wa shirika hilo Suba Churchil anasema kwamba madai kwamba wawakilishi wa wanawake wanaongeza gharama ya serikali hayana msingi.

Kulingana na Bw Churchil, Seneti haifai kufutiliwa mbali kama baadhi ya watu wanavyopendekeza.

TAHARIRI:Tutafakari kuhusu mageuzi ya Katiba

NA MHARIRI

HATUA ya Naibu Rais William Ruto kubadili msimamo wake kuhusu kura ya maamuzi, huenda sasa inaashiria umuhimu wa kila mmoja kutafakari vyema kile kinachohitajika katika marekebisho hayo.

Kwa muda mrefu sasa, ubishani kati ya wanaounga mkono marekebisho ya katiba na wale wanaopinga umefanya kuwe na hali ambapo suala hilo limechukuliwa kisiasa.

Ilifikia kiwango ambapo marekebisho ya katiba yalikuwa yanachukuliwa kama jambo linalohusu ubabe wa kisiasa kati ya Bw Ruto na Kiongozi wa Upinzani, Bw Raila Odinga.

Hali hii ilikuwa imeanza kuibua taharuki nchini kwani kama ilivyo kawaida, misimamo mikali kuhusu masuala aina hii husababisha mgawanyiko wa wananchi kwa mirengo tofauti ya kisiasa katika hali inayoweza kuathiri utulivu wa nchi.

Wakati huu kutokana na kuwa pande zote zimekubali kwamba katiba inahitaji marekebisho, hakuna haja tena ya ushindani bali ushirikiano utakaoleta manufaa kwa kila mwananchi wa taifa hili.

Viongozi wote wanahitaji kupatanishwa, kuwe na mashauriano katika mandhari tulivu, na wote waelewane kuhusu marekebisho yanayofaa. Lakini ikumbukwe hili si suala linalohusu viongozi pekee, kwani katiba ni mwongozo muhimu zaidi wa jinsi taifa linavyosimamiwa na linavyoendesha shughuli zake zote.

Kwa msingi huu, mashauriano yajumuishe wadau wote, wakiwemo viongozi wa kijamii na wananchi ndipo tupate katiba itakayokubaliwa na kila mmoja wetu. Kwa wananchi, ni vyema wote wawe macho wasipotoshwe na viongozi ambao huenda wakataka kutumia marekebisho ya katiba kujitakia makuu kibinafsi.

Marekebisho yoyote yatoe kipaumbele kwa mahitaji ya mwananchi, kwa mfano, kwa kuondoa nafasi za uongozi ambazo hazihitajiki au zile zisizotoa mchango wowote wa maana katika uongozi bora wa taifa.

La muhimu zaidi ni kwamba inapaswa tutilie maanani hali ya kiuchumi inayotukumba kwa sasa.

Mchakato mzima wa kurekebisha katiba usiwe kwa hali ambayo itasababishia mwananchi gharama zaidi kwani sasa tayari wengi wao wanalalamikia hali ngumu ya kimaisha.

Kila pendekezo liwekwe wazi, lizingatiwe na kupigwa msasa ndipo tusonge mbele kwa pamoja kama taifa moja bila migawanyiko isiyo na maana.

Lazima katiba ibadilishwe, Raila asisitiza

ELISHA OTIENO na RUTH MBULA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, ametaka wale wanaopinga marekebisho ya katiba wakae kando na kuachia wananchi nafasi ya kujiamulia kuhusu wanavyotaka kuongozwa.

Akizungumza Alhamisi akiwa Kaunti ya Migori, Bw Odinga alisema wakati umefika kwa katiba kurekebishwa na hakuna kitakachozuia hilo.

“Huwezi kuzuia utekelezaji wa jambo ambalo wakati wake umefika,” akasema mjini Awendo, alipoongoza kampeni za Bw Ochillo Ayacko anayewania useneta kupitia ODM.

Kulingana naye, katiba za nchi nyingi ulimwenguni hubadilishwa baada ya angalau miaka minane hivyo basi haistahili watu waseme bado ni mapema kwa katiba iliyopitishwa 2010 kufanyiwa marekebisho.

“Ni lazima tufanye utathmini wa kama ugatuzi umetufaa, na kutatua changamoto ibuka kupitia kwa marekebisho ya sheria. Tujiulize kama serikali kuu ina uwakilishi mkubwa kupita kiasi, na pia masuala ya kimazingira,” akasema.

Baadhi ya viongozi akiwemo Naibu Rais William Ruto, wamekuwa wakipinga marekebisho ya katiba.

Wamekuwa wakidai kuwa Bw Odinga na wenzake wanashinikiza marekebisho ya katiba ili waingie serikalini kupitia nyadhifa mpya zitakazobuniwa kama vile Waziri Mkuu na manaibu wake.

“Wale wanaopinga suala hili ni kama vilio vya chura ambavyo havitazuia ng’ombe kunywa maji,” akasema.

Alipozungumza mjini Rongo ambapo aliandamana na Gavana wa Siaya Cornel Rasanga, Naibu Gavana wa Kisumu Mathew Owili, Kiongozi wa Wachache Bungeni John Mbadi na wabunge mbalimbali, waziri huyo mkuu wa zamani alisema jopo alilounda na Rais Uhuru Kenyatta limepiga hatua katika majukumu yake.

Alisema wanachama wa jopo hilo wataanza kuzunguka nchini hivi karibuni kukusanya maoni ya wananchi kuhusu jinsi ya kutatua changamoto zinazokumba taifa.

Kuhusu uteuzi wa moja kwa moja wa Bw Ayacko ambao ulisababisha mgawanyiko miongoni mwa wanachama wa ODM katika kaunti hiyo, alisema chama kiliamua hivyo kwa sababu Bw Ayacko ndiye alipatikana kuwa bora zaidi miongoni mwa waliotaka tikiti ya ODM.

“Tulifanya kura ya maoni akaibuka mshindi na pia uzalendo wake kwa chama umedumu kwa muda mrefu,” akaambia umati.

Uteuzi wa Bw Ayacko ulimfanya Gavana wa Migori Okoth Obado kuasi chama hicho na kumuunga mkono Bw Eddy Oketch, 27, wa chama cha Federal Party of Kenya.

Bw Odinga amekita kambi katika kaunti hiyo kwa siku mbili kabla uchaguzi mdogo wa useneta ufanywe Jumatatu.

Bw Oketch ameonyesha upinzani mkali dhidi ya Bw Ayacko kufikia sasa na amekuwa akitumia helikopta kwenye kampeni zake mbali na rasilimali nyingine za bei ghali.

Mwanasiasa huyo kijana alipuuzilia mbali madai ya baadhi ya viongozi wa ODM waliodai anafadhiliwa na Bw Ruto, akasema rasilimali anazotumia sasa ni zile zile alizoruhusu viongozi hao kutumia wakati wa kampeni za urais mwaka uliopita kwa hivyo waache unafiki.

OBARA: Uboreshaji katiba wataka maarifa, si hisia

Na VALENTINE OBARA

MJADALA kuhusu mabadiliko ya katiba umezidi kushika kasi katika miezi ya hivi majuzi. Mdahalo huo ulikuwa umetulizwa tangu wakati Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga aipoweka muafaka wa maelewano na Rais Uhuru Kenyatta mapema mwaka huu.

Tetesi za Bw Odinga zilihusu kuwezesha uchaguzi huru na wa haki baada ya uchaguzi uliopita, na sasa watetezi wamezinduka kufuatia kupitishwa kwa sheria ya fedha ambayo imeongeza ushuru wa bidhaa muhimu ikiwemo mafuta.

Mbali na Bw Odinga, wanaotaka marekebisho ya katiba ni viongozi wa kidini, chama cha Thirdway Alliance na baadhi ya wabunge.

Kile kinachofaa kueleweka ni kwamba marekebisho ya katiba ni suala zito ambalo linafaa kufanywa kwa makini.

Urekebishaji katiba ni shughuli inayotumia rasilimali nyingi za nchi na haifai kuchukuliwa kama jambo la mzaha la kutatua matatizo ya muda, bali iwe suluhisho la kudumu kwa changamoto za kitaifa.

Inavyoonekana kwa sasa, viongozi wanaopendekeza marekebisho haya wanatumia hisia za wananchi kuhusu hali ya maisha ili wapate kuungwa mkono na wengi.

Imekuwa jambo la kawaida sio Kenya pekee bali pia katika mataifa mengine mengi ulimwenguni kwamba katiba hurekebishwa tu wakati ambapo nchi inakumbwa na majanga ya aina mbalimbali.

Humu nchini, tulipata fursa ya kurekebisha katiba yetu punde tulipopata ukombozi kutoka kwa utawala wa mkoloni, kisha tukairekebisha tena katika mwaka wa 2010.

Marekebisho yaliyofanywa 2010 yalifanikishwa kufuatia ghasia za baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007 ambapo watu zaidi ya 1,000 walifariki na maelfu wengine wakaachwa bila makao. Makovu ya ghasia hizo bado hutuandama hadi hii leo.

Kilichobainika katika kipindi hiki cha miaka minane ya katiba mpya iliyotuletea utawala wa ugatuzi ni kwamba tulifanya marekebisho kwa msingi wa hisia zilizotukumba wakati wa ghasia za 2007.

Tulikuwa na matarajio makubwa kwamba katiba hii ingetatua changamoto ambazo zilikuwa chanzo cha ghasia hizo za kikabila na zingine ambazo tulikuwa tumeshuhudia katika chaguzi zilizotangulia.

Ingawa ugatuzi umetatua baadhi ya changamoto zilizokuwa zikikabili wananchi mashinani, ni vigumu kuona mafanikio yoyote ambayo katiba hii imeleta kubadilisha mbinu za uongozi katika serikali kuu.

Bunge lililopaswa kuwa na mamlaka makubwa ya kutetea maslahi ya wananchi limeishia kutekwa na afisi ya rais.

Vile vile, lengo la kuleta uwakilishi sawa wa kijinsia serikalini limeishia kuletea mwananchi mzigo wa kugharamia mishahara mikubwa na marupurupu ya watumishi wa umma.

Zaidi ya hayo, mapendeleo ya kikabila katika kuajiri watumishi wa umma bado ni changamoto kubwa.

Licha ya haya, haitakuwa busara kuharakisha kubadilisha katiba wakati huu kwa kuchezea hisia za wananchi wanaotatizwa na hali ngumu ya maisha.

Tukifanya hivi tutarejea tena kwa wananchi hawa miaka michache baadaye tutakapogundua kwamba marekebisho yaliyofanywa hayakuzingatia hili na lile, bali yalikuwa tu ya kutimiza maslahi ya watu wachache wenye ushawishi mkubwa nchini.

Pendekezo la kubadilisha Katiba lagawanya Jubilee

Na WANDISHI WETU

PENDEKEZO la kinara wa ODM Raila Odinga kutaka Katiba ifanyiwe mabadiliko limegawanya chama cha Jubilee.

Kile kimejitokeza ni kuwa wabunge wa uliokuwa mrengo wa TNA wanataka mabadiliko huku wa URP wakipinga.

Miongoni mwa waliojitokeza kuunga mkono ni Mbunge Maalum Maina Kamanda, Moses Kuria (Gatundu Kusini), Michael Muchira (Ol-Joro Orok, Kinuthia Gachobe (Subukia), Kimani Kuria (Molo), Bi Faith Gitau (Mwakilishi wa Kike wa Nyandarua), Patrick Mariru (Laikipia Magharibi), Patrick Munene (Chuka-Igamba-Ng’ombe) na Bw Peter Kimari (Mathioya).

Wabunge hao wanasema kubadilisha Katiba kutasaidia kupunguza mzigo wa kulipa ushuru wa juu.

Lakini Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen amepuuzilia mbali wito wa kuandaa kura ya maamuzi.

Bw Murkomen ambaye ni Kiongozi wa Wengi katika Seneti alisema wanaopigania kufanyika kwa kura ya maamuzi wanaongozwa na masilahi ya kibinafsi.

“Wanaotaka Katiba ifanyiwe mabadiliko wanataka kufanya hivyo ili waweze kujipatia nafasi ya kuingia mamlakani 2022,” akasema.

Wakati huo huo, kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula ameunga mkono pendekezo hilo la Bw Odinga huku akisema kuwa Katiba inafaa kufanyiwa marekebisho ili fedha zinazotolewa kwa serikali za kaunti ziongezwe kutoka asilimia 15 hadi asilimia 45 ya bajeti ya kitaifa.

Ripoti ya Patrick Lang’at, Florah Koech na Steve Njuguna

Wataalamu nao waunga mkono Katiba igeuzwe

Na KITAVI MUTUA

WATAALAMU wa masuala ya katiba wameunga mkono shinikizo za kuifanyia mageuzi Katiba ya sasa, wakisema kuwa kuna haja ya kutathmini baadhi ya vipengele vyake.

Shinikizo hizo zimekuwa zikiendeshwa na Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga, akisisitiza hitaji la kuangazia baadhi ya mapengo yaliyopo.

Wakili maarufu wa kikatiba Nzamba Kitonga (pichani), alisema kuwa imefikia wakati ambapo katiba hiyo inapaswa kutathminiwa upya, ili kuangazia masuala ambayo tayari yamegunduliwa kuwa “tata” kwenye Katiba iliyopitishwa 2010.

Bw Kitonga, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu, iliyoandika Katiba hiyo, alisema kuwa kuna hitaji la utathmini wake, kwani baadhi ya Wakenya wanahisi kutengwa katika utaratibu wa uongozi wa nchi.

“Kama Kamati ya Wataalamu, tulitarajia kwamba utathmini mpya wa Katiba ungefanywa baada ya miaka saba hadi kumi, ili kuangazia mapengo ambayo yangekuwa tayari yamedhihirika katika utekelezaji wake,” akasema Bw Kitonga.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bw Kitonga alisema kwamba mpangilio wa sasa wa matawi makuu ya serikali unapaswa kuangaliwa upya, ili kuimarisha ushirikishi wa kisiasa na kikabila, kupunguza kiasi cha fedha kinachotumika kuziendesha na kuimarisha utendakazi wa Idara ya Mahakama.

Alieleza kuwa Katiba hiyo ni nzuri kwa ustawi wa Kenya, ila ina mapengo kadhaa ambayo lazima yashughulikiwe.

Hasa alikosoa mfumo wa urais, ambapo anayeshinda kinyang’ayiro cha urais hubuni serikali, akisema kuwa imedhihirika kwamba haiendelezi nchi, ila unazua miganyiko ya kikabila. Alisema kuwa mfumo huo unaziacha nje jamii nyingi katika utaratibu wa uongozi wan chi.

“Rasimu ambayo tulibuni ilijumuisha mifumo ya utawala ya urais na bunge, ili kuvipa nafasi vyama vya kisiasa na kupunguza taharuki na hali ya ushindani usiofaa katika siasa zetu,” akasema.

Alieleza kuwa Katiba iliyopo kwa sasa ilifanyiwa mageuzi na wanasiasa kwa kuingiza mfumo wa urais, ambao ulikuwa umekataliwa na Wakenya kwenye shughuli za mageuzi ya katiba.

“Tulikuwa tumebuni afisi ya Kiongozi wa Upizani, ambapo pia angekuwa akishiriki katika vikao vya Bunge. Hata hivyo, kipengele hicho kiliondolewa, hali ambayo imewafanya Wakenya wengi kutengwa katika mfumo wa utawala wa nchi,” akaeleza.

Alisema kuwa chini ya rasimu hiyo, Bw Odinga na mgombea-mweza wake,Kalonzo Musyoka ambao walishindwa na Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wangekuwa na afisi zao, ili kuwawezesha kufuatilia utendakazi wa serikali ya Jubilee.

Wakili Bobby Mkangi, ambaye pia alikuwa mwanakamati wa tume ya kubadilisha katiba, alisema kuwa hawakutarajia kwamba serikali ya kitaifa na zile za kaunti zingegeuzwa kuwa majukwaa ya ufujaji wa fedha za umma.

“Ni kweli kwamba baraza la mawaziri ni ndogo ikilinganishwa na awali, ila tungali tunatumia fedha nyingi kulipa mishahara ya maafisa katika serikali zote mbili,” akasema.

MAREKEBISHO YA KATIBA: Raila achokoza Jubilee

KITAVI MUTUA na VALENTINE OBARA

MSIMAMO wa Kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwa alikubaliana na Rais Uhuru Kenyatta kutakuwa na marekebisho ya Katiba walipoweka muafaka wa maelewano hapo Machi 9, huenda ukaibua upya mgogoro katika chama cha Jubilee.

Wakati Bw Odinga alipotoa pendekezo hilo wiki chache baada ya muafaka wake na Rais Kenyatta, kulizuka mvutano ndani ya Jubilee ambapo mrengo mmoja ukiongozwa na Naibu Rais William Ruto na wandani wake akiwemo Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale ulipinga vikali.

Mjadala huo ulipokuwa ukiendelea Rais Kenyatta alikuwa kimya hadi mwishowe akajitokeza na kusema hakuna muda wala rasilimali za kuandaa kura ya maamuzi ya kufanyia marekebisho Katiba.

“Hakuna nia yoyote ya kurekebisha katiba. Hatuna wakati. Tunataka kufanya kazi muhimu, sio kukimbia hapa na pale kuuliza kama mnataka Katiba mpya au la. Hilo halitatatua matatizo yetu,” akasema rais alipozungumza mwezi Mei katika Ikulu ya Nairobi.

Msimamo huo wa rais unakinzana na ule wa Bw Odinga ambaye amesisitiza walikubaliana suala hilo litakuwa moja ya ajenda kuu za maelewano yao.

Bw Ruto hakuhusishwa kwenye muafaka huo na baadhi ya wandani wake wana wasiwasi kuhusu kile wawili hao walikubaliana kwenye maelewano yao.

Akizungumza katika Kaunti ya Kitui, Bw Odinga alisisitiza ni lazima Katiba ifanyiwe marekebisho ili kuleta mabadiliko Kenya.

“Tulikubaliana na Rais Kenyatta kwamba tukifanikiwa kurekebisha makosa yaliyo kwenye Katiba tutakuwa tumefanikiwa kuleta mabadiliko Kenya kwa hali ambayo itafanya liwe taifa bora zaidi kwa vizazi vijavyo,” akasema.

Kiongozi huyo alisema Katiba iliyopo, ambayo ilipitishwa mwaka wa 2010, imedhihirisha haiwezi kutatua changamoto nyingi zinazokumba taifa hili.

Miongoni mwa marekebisho anayotaka ni kuhusu mfumo wa uongozi ili kuwe na ngazi tatu za utawala, tofauti na jinsi ilivyo sasa ambapo kuna ngazi mbili ambazo ni Serikali Kuu na za kaunti.

Kulingana naye, muafaka ulipatikana kati yake na rais baada yao kukubaliana kuwa marekebisho ya Katiba yatakuwa kati ya masuala makuu yatakayoangaziwa.

“Tuna Katiba nzuri lakini haitusaidii. Hii ndio sababu nilishirikiana na Rais Kenyatta ili kufanya marekebisho ya kisheria,” akasema.

Mtaalamu wa kisheria ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu wa uundaji wa Katiba iliyopo, Bw Nzamba Kitonga, alisema wakati huu ni mwafaka kwa Katiba kufanyiwa marekebisho.

Kulingana naye, kamati yake ilikuwa imetarajia Katiba itahitaji marekebisho baada ya miaka saba au kumi.

Lakini wandani wa Bw Ruto wamekuwa wakishikilia kuwa marekebisho ya kikatiba ni njama fiche ya Bw Odinga kumharibia nafasi ya kushinda urais 2022.

Jopokazi lililoteuliwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga limekuwa likiendeleza shughuli zake kichinichini na kufikia sasa haifahamiki hatua zilizopigwa katika majukumu yao.

Bw Odinga alisema marekebisho ya Katiba ni miongoni mwa yanayoangaziwa na jopokazi hilo, ambalo kulingana naye litaanza kuzuru maeneo tofauti ya nchi hivi karibuni kutafuta maoni ya wananchi.

Alisema baadhi ya maswali ambayo wananchi wataulizwa ni kuhusu jinsi ugatuzi unavyoweza kuimarishwa, mbinu mwafaka za ugavi wa rasilimali za nchi na kama wanataka mfumo uliopo wa uongozi uendelee kutumiwa au ubadilishwe.

Makanisa yasisitiza katiba irekebishwe kubuni uwaziri mkuu

Na CHARLES WANYORO

BARAZA Kuu la Muungano wa Makanisa nchini (NCCK) limeibua upya wito wa kutaka kufanyia Katiba mabadiliko ili kubuni wadhifa wa waziri mkuu.

Katibu Mkuu wa NCCK Canon Peter Karanja (pichani) alisema kuna haja ya kubuni wadhifa wa waziri mkuu ambaye atakuwa na manaibu wawili pamoja na afisi ya kiongozi wa upinzani atakaye kuwa akilipwa mshahara.

Kasisi huyo alisema kiongozi wa upinzani atakuwa na baraza lake la mawaziri watakaokuwa wakikosoa serikali.

Alisema kuna haja kwa nchi kutumia amani iliyoko nchini, baada ya mwafaka wa ushirikiano baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, kushinikiza mabadiliko ya Katiba ‘ili kuhakikisha amani inadumu.

Akizungumza katika Shule ya Upili ya Moi, Mbiruri katika eneobunge la Runyenjes ambapo alikuwa mgeni rasmi wakati wa hafla ya Siku ya Elimu Askofu Karanja, alisema kubuniwa kwa afisi ya kiongozi wa upinzani pamoja na baraza lake la mawaziri, kutasaidia kuhakikisha kuwa serikali inawahudumia Wakenya kwa uadilifu.

Alisema mfumo wa sasa ambapo mshindi ananyakua kila kitu husababisha mgawanyiko nchini.

“Suala la uchaguzi nchini husababisha mgawanyiko kwa sababu wanasiasa pamoja na wafuasi wao hutumia fedha nyingi katika kampeni. Hivyo, huwa na machungu mwaniaji wao anapopoteza,” akasema.

Alisema kubuniwa kwa afisi ya waziri mkuu na kiongozi wa upinzani kutahakikisha kuwa wawaniaji wenye ushawishi wanaopoteza wanapata nafasi ya kuhudumu.

Kulingana na Askofu Karanja kubuni nyadhifa zaidi serikalini na kutambua rasmi majukumu ya upinzani kutasaidia kumaliza uhasama wa kikabila.

“Kwa sababu Wakenya wote wanataka kuwa serikalini, tunatoa pendekezo kwamba nyadhifa serikalini ziongezwe ili kabila zote ziwakilishwe,” akasema.

“Wadhifa wa Kiongozi wa Upinzani urudishwe na utwaliwe na mwaniaji wa urais anayeibuka nafasi ya pili katika uchaguzi. Tulikuwa na wadhifa huo hapo awali lakini watu wa Mlima Kenya wamekuwa wakisema: ‘kama umeshindwa, enda Bondo. Hii Bondo ambayo utapeleka mtu ambaye ana wafuasi milioni sita, watatoshea wapi?” akauliza.

Askofu Karanja pia aliwataka wanasiasa kukoma kuingilia shughuli za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) huku akawataka kuunga juhudi zake za tume hiyo katika kurejesha imani ya Wakenya kwake.

Waliopinga marekebisho ya katiba sasa wabadili kauli

Na WYCLIFFE KIPSANG’

WANDANI wa Naibu wa Rais William Ruto, ambao awali walipinga vikali wito wa kutaka kura ya maamuzi iandaliwe ili kufanyia mabadiliko Katiba, sasa wamebadili msimamo wao kwa kusema kuwa mabadiliko hayo ni muhimu kwa ustawi wa nchi.

Seneta wa Nandi, Samson Cherargei (pichani) na Mbunge wa Soy, Caleb Kositany Jumatano walisema mabadiliko ya Katiba yatawezesha serikali kutimiza miradi yake ya maendeleo.

“Kuna madai kwamba baadhi yetu katika chama cha Jubilee tunaogopa kura ya maamuzi. Huo si ukweli. Kura ya maamuzi ya kubadili Katiba ifanyike sasa ndipo serikali ianze mchakato wa kutekeleza ahadi zake kuu nne za maendeleo,” akasema Bw Cherargei.

Wawili hao, hata hivyo, walishutumu kiongozi wa ODM, Raila Odinga kwa kutumia mwafaka wake wa kufanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta kutaka ‘kuingia’ mamlakani kwa njia ya mkato.

“Tumekuwa tukishuku mwafaka baina ya Bw Odinga na Rais Kenyatta. Mwafaka huu sasa unatumiwa na watu wachache kujinyakulia mamlaka na kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa 2022,” akasema Seneta Cherargei.

Viongozi wengine kama vile mbunge wa Turbo, Janet Sitienei, hata hivyo, walipinga wito wa kuandaa kura ya maamuzi huku wakisema kuwa kuna matatizo mengi yanayozonga nchi na yanahitaji kushughulikiwa badala ya kufanyia mabadiliko Katiba.

Akihutubia wanahabari mjini Eldoret, Bi Sitienei alisema kuwa kuna haja ya kupatia kipaumbele janga la mafuriko yanayoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

“Fedha wanazotaka kutumia kuandaa kura za maamuzi zitumiwe kuwahudumia waathiriwa wa mafuriko na kununulia wakulima mbolea,” akasema mbunge huyo ambaye alichaguliwa kama mwaniaji huru.

Wito wa kuandaa kura za maamuzi ili kubadilisha Katiba umetishia kusambaratisha mwafaka baina ya Waziri Mkuu huyo wa zamani na Rais Kenyatta. Bw Ruto anapinga vikali pendekezo la kubadilisha Katiba ili kubuni vyeo zaidi, kikiwemo kile cha waziri mkuu.

Bw Ruto amesisitiza kuwa uamuzi wa serikali ya Jubilee kushirikiana na viongozi wa upinzani haukulenga kubuni vyeo zaidi.

Naibu wa Rais ameshikilia kuwa mwafaka baina ya Kiongozi wa Nchi na Bw Odinga unafaa kunufaisha wananchi na wala si wanasiasa wachache.

“Umoja wa kitaifa tunaopigana si wa kugawana vyeo. Hata kama tunahitaji kubadili Katiba tusibuni vyeo vipya kama vile wadhifa wa waziri mkuu,” Bw Ruto alisema alipokuwa akihutubu katika Kaunti ya Nandi mnamo Jumapili.

“Wakenya wana uwezo wa kuchagua viongozi wanaowapenda na wala si watu wachache kuketi mahali fulani wakinywa chai,” akaongezea.

Hapo Jumanne, Bw Ruto alimshambulia Bw Odinga akitaja wanaoitisha mabadiliko kama watub wazembe ambao wanatafuta kisingizio cha Katiba kila mara wanaposhindwa.

Nia ya Raila yasalia kuwa siri kuu

Na VALENTINE OBARA

PENDEKEZO la Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, kuhusu marekebisho ya Katiba limezidi kuacha viongozi na wananchi wa pande zote za kisiasa wakijikuna vichwa kuhusu anachotaka kuafikia.

Sisitizo lake kuwa hana njama ya kujipangia mikakati ya 2022 kupitia muafaka huo halijazuia wanasiasa kuhisi ana nia fiche, huku wengine wakijaribu kutegua kitendawili chake.

Hali hii imezidishwa na jinsi wawili hao hawajatangaza lolote kuu kuhusu muafaka wao kufikia sasa, isipokuwa kuchagua kikundi cha watu 14 ambao pia majukumu yao hayajafafanuliwa wazi kwa umma.

“Inahitajika kuwe na ufafanuzi ili kuondoa usiri mkubwa ulio katika shughuli hii. Kwa sasa kuna hali ya kuchanganyikiwa kwani tayari kuna asasi za umma zinazofaa kushughulikia masuala yaliyotajwa kwenye muafaka wao,” alisema Katibu Mkuu wa Chama cha Amani National Congress, Bw Barrack Muluka.

Bw Odinga amependekeza kuwe na wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wake, na kuwe na ngazi tatu za uongozi.

Mahasimu wake wanahofia kwa kupendekeza hivyo anatafuta mwanya wa kuingia serikalini kwa mlango wa nyuma na kufanya iwe vigumu kwa Naibu wa Rais William Ruto kuungwa mkono eneo la Kati mwaka wa 2022 na endapo Bw Ruto atashinda uchaguzini, asiwe rais mwenye mamlaka makubwa.

Mbunge wa Ndaragua, Bw Jeremiah Kioni, alisema ingawa Katiba inahitaji kurekebishwa, mbinu inayotumiwa ni ya kutiliwa shaka kwani inaonekana lengo ni kumvuruga Bw Ruto kisiasa.

“Jamii yetu iliahidi kumuunga mkono Bw Ruto. Huwezi kutufanya tuonekane tunamtoroka wakati huu. Tunahitaji marekebisho ya Katiba lakini mdahalo huu wote ulianzishwa kwa njia isiyofaa,” akasema Jumatatu.

Msimamo sawa na huu ulitolewa na wanasiasa wengine wa eneo la Kati ambao hawamwamini Bw Odinga.

Seneta wa Narok, Bw Ledama ole Kina ambaye ni mwanachama wa ODM, alikiri kuna hofu inayohitaji kutulizwa kabla watu wazungumzie marekebisho ya Katiba.

“Kwa kweli watu wana hofu. Hata mimi ningeogopa kama ningekuwa naibu wa rais kisha mtu aseme anataka kubadilisha katiba wakati nimekaribia kuingia mamlakani,” akasema.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Chama cha Third Way Alliance, Dkt Ekuru Aukot, alipendekeza katiba irekebishwe ili watu ambao wamewahi kuwa rais, naibu au makamu wa rais, waziri mkuu au naibu wasiruhusiwe kuwania urais.

Kulingana naye, hatua hii itafanya marekebisho yasilenge kutimiza maazimio ya wanasiasa ya kibinafsi, na itatoa nafasi kwa viongozi wapya kuongoza nchi.

JAMVI: Wito wa Atwoli watikisa msingi wa chama cha Jubilee

Na BENSON MATHEKA

WITO wa kutaka mabadiliko ya katiba ili Rais Uhuru Kenyatta aendelee kuhudumu serikalini baada ya kumaliza kipindi chake cha pili 2022, ni pigo kwa ustawi wa demokrasia nchini na linaweza kusambaratisha chama cha Jubilee.

Na ingawa baadhi ya washirika wa rais wanapinga pendekezo lililotolewa na katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini Cotu Francis Atwoli, kwamba katiba ibadilishwe kubuni wadhifa wa waziri mkuu kumwezesha Rais Kenyatta kuendelea kushiriki siasa baada ya 2022, wadadisi wanasema hatua kama hiyo itavunja chama cha Jubilee.

“Pendekezo la Atwoli sio hewa tupu. Katika siasa mambo hubadilika haraka sana. Usisahau washirika wa rais, hasa kutoka ngome yake wanahisi hawana mtu wa kumrithi na wangetaka aendelee kuwa serikalini kwa sababu wanahisi anawakilisha maslahi yao. Siasa za Kenya ni telezi sana,” asema Bw Alloys Mwangi, mdadisi wa masuala ya siasa.

Kulingana naye, mjadala kuhusu kubadilisha katiba kuhakikisha Rais Kenyatta ataendelea kuhudumu baada ya 2022 umekuwepo kwa muda, japo chini kwa chinichini.

“Nahisi kuna mikakati ambayo imekuwa ikiendelea chini kwa chini katika mrengo mmoja wa Jubilee. Hofu ya wakereketwa wa mabadiliko hayo ni azma ya Naibu Rais William Ruto ya kugombea urais 2022.

Rais mwenyewe pia aliahidi kustaafu baada ya kumaliza kipindi chake cha pili na kumuunga Bw Ruto. Hata hivyo, inaonekana kuna shinikizo mpya zilizojiri na muafaka wa Rais Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga,” alisema Bw Mwangi.

 

Uhuru awe Waziri Mkuu 2022

Akiongea kwenye sherehe za kuadhimisha siku ya wafanyakazi ulimwenguni katika bustani ya Uhuru Park Jumanne, Bw Atwoli alipendekeza katiba ifanyiwe mageuzi ili kubuni wadhifa wa waziri mkuu utakaoshikiliwa na Rais Kenyatta baada ya 2022.

Kulingana na Bw Atwoli, Rais Kenyatta atakuwa bado na nguvu atakapomaliza kipindi chake cha pili 2022 na anafaa kuendelea kushiriki siasa.

“Tubadilisheni katiba hii na kutumia rasimu ya Bomas ili kuhusisha watu wote kwa sababu sio kila mtu anaweza kuwa rais. Kufanya hivi kutamshirikisha Rais Kenyatta ambaye angali bado chipukizi. Tusipofanya hivyo, tutampeleka wapi?” alihoji Bw Atwoli.

“Nawaambia kwamba hata mtu mwingine akiongoza Kenya, ni lazima atashirikiana na watu wa Mlima Kenya na huo ndio ukweli wa mambo,” alisema Bw Atwoli.

Kulingana na rasimu ya katiba ya Bomas, Kenya ingekuwa na wadhifa wa waziri mkuu ambaye angechaguliwa na bunge na kuwa na na mamlaka makuu.

Wadadisi wanasema pendekezo hilo ni njama ya kuzima azima ya Naibu Rais William Ruto ambaye  amepinga mabadiliko yoyote ya katiba yanayolenga kubuni nyadhifa mpya serikalini. Wanasema si ajabu mabadiliko hayo yalikuwa miongoni mwa masuala ambayo Rais Kenyatta na Bw Odinga walikubaliana katika muafaka wao.

Mchanganuzi Barack Muluka anahisi suala la kuhakikisha Rais Kenyatta ataendelea kuhudumu kama waziri mkuu lilijadiliwa kwenye mikutano iliyotangulia muafaka wake na Bw Odinga.

 

Raila na Uhuru wana maoni sawa

“Odinga anaamini kwamba atakuwa rais pengine akiwa na naibu kutoka  Rift Valley na mwingine kutoka Pwani. Kenyatta anaweza kuwa waziri mkuu akiwa na manaibu wawili kutoka Magharibi na Mashariki. Hawa wawili wana maoni sawa,” Bw Muluka alisema.

Kwenye makala yaliyochapishwa kwenye gazeti moja la humu nchini kabla ya tamko la Bw Atwoli, Bw Muluka  alisema viongozi hao wawili watawaagiza wabunge na madiwani wa vyama vyao kuunga mabadiliko ya katiba wakisingizia wanalenga kuunganisha nchi.

“Kuna wale watakaopinga mabadiliko hayo na kwa hivyo kutazuka makabiliano ya kisiasa na kikatiba nchini Kenya,” alitabiri Bw Muluka.

Kulingana na kiongozi wa wengi katika seneti Bw Kipchumba Murkomen, ambaye ni mshirika wa Bw Ruto, katiba haiwezi kubadilishwa ili kubuni nyadhifa kwa sababu ya watu binafsi.

“Rais ameshughulikiwa ipasavyo katika katiba na hahitaji kutengewa wadhifa,” alisema Bw Murkomen na kuungwa mkono na mwenzake katika bunge la taifa, Aden Duale ambaye pia ni mwandani wa Bw Ruto.

“Rais Kenyatta ametangaza wazi kwamba, atafurahi kustaafu siasa baada ya kumaliza kipindi chake cha pili,” alisema Duale.

Wadadisi wanasema njama zozote za kumzuia Bw Ruto kugombea urais 2022 zinaweza kuvunja chama cha Jubilee.

“Bw Ruto atahisi kuwa amesalitiwa baada ya kumuunga Rais Kenyatta tangu 2013. Amekuwa akilenga urais 2022 na yeye na washirika wake hawatachukulia hatua yoyote ya kuzima ndoto yake kwa urahisi,” asema Bw Doris Chebet wakili na mdadisi wa siasa.

Anasema pendekezo la kumtaka Rais Kenyatta kuendelea kuhudumu ni njama za watu binafsi wanaomzunguka na ambao wanataka kuendelea kufurahia mamlaka.

 

Kuongezwa kwa muhula

“Usishangae kusikia baadhi yao wakipendekeza muda wa kipindi cha rais kuhudumu uongezwe kutoka miaka mitano hadi saba,” alisema Bi Chebet.

Bw Atwoli alisema kwa sababu Rais Kenyatta atakuwa na umri wa miaka 60 atakapomaliza kipindi chake cha pili, ngome yake ya kisiasa haitakubali astaafu.

Wanaopinga pendekezo hilo wanamhimiza Rais Kenyatta kuiga viongozi wanaoheshimiwa kote ulimwenguni kwa kukataa kukwamilia mamlakani.

Bw Mwangi anasema Bw Atwoli hakuwa wa kwanza kutoa pendekezo kama hilo.

“Nakumbuka mapema mwaka huu, David Murathe, ambaye ni afisa mkuu wa chama cha Jubilee (naibu mwenyekiti) alinukuliwa akisema kuna watu wanaotaka Uhuru astaafu akitimiza miaka 60 ilhali Raila anataka kuwa rais akiwa na miaka 75.

Hii inaonyesha huenda kuna njama pana zinazopikwa kuhakikisha Uhuru anasalia serikalini baada ya 2022” alisema Bw Mwangi na kuongeza kuwa washirika wa Bw Ruto wanaweza kuondoka Jubilee iwapo hilo litatendeka.

Kulingana na  Bi Chebet, mswada wa mbunge wa Tiaty, Kassait Kamket unaopendekeza katiba ibadilishwe Rais ahudumu kwa kipindi kimoja cha miaka saba na kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu mwenye mamlaka makuu, haufai kupuuzwa.

“Marais wengi wametumia mabadiliko ya katiba ili waendelee kuhudumu, hasa wakiwa na idadi kubwa ya wabunge. Jubilee ina wengi katika bunge na seneti na hata wanaomuunga Ruto wakikosa kuunga mabadiliko, wale wa ODM wanaweza kuyaunga kufuatia muafaka wa Uhuru na Odinga,” alisema.

Miguna apinga vikali juhudi za kubadili katiba

Na VALENTINE OBARA

MWANAHARAKATI wa upinzani, Dkt Miguna Miguna, amepinga juhudi za marekebisho ya katiba zinazoshinikizwa na Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga.

Kulingana na wakili huyo aliyefurushwa nchini na serikali, Bw Odinga amepoteza mwelekeo kwa kuanzisha mikakati mipya ya kisiasa ilhali mapambano aliyoanzisha baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita hayajazaa matunda.

“Hatutakaa kitako na kutazama Raila Odinga akidunisha na kuvuruga mapambano mengine ya kukomboa Kenya kikamilifu. Alifanya hivyo miaka ya 1997, 2002 na sasa ni 2018,” akasema kwenye msururu wa taarifa alizochapisha kwenye mitandao ya kijamii.

Aliongeza: “Hatutahadaiwa na kura nyingine ya maamuzi isiyo na maana. Tulikuwa na kura ya maamuzi mwaka wa 2005. Wakenya walifanikiwa kivipi kutokana nayo? Hakuna! Tunachotaka ni haki ya uchaguzi na kijamii wala si kura nyingine ya maamuzi isiyo na maana itakayogharimu kiasi kikubwa cha pesa.”

Bw Odinga amependekeza mfumo wa utawala wa ugatuzi urekebishwe, huku viongozi wengine wakiwemo wa kidini wakipendekeza utawala katika serikali kuu pia ubadilishwe ili kuwe na Waziri Mkuu na manaibu.

Kulingana naye, njia hii itawezesha utekelezaji wa maazimio ya kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikikumba taifa ikiwemo utendaji wa haki na uwepo wa uongozi bora unaofaidi wananchi.

Hata hivyo, marekebisho ya katiba yamepingwa vikali na Naibu Rais William Ruto, pamoja na wandani wake wa kisiasa wanaoona ni njama ya kufanya viongozi wa upinzani kuingia serikalini kupitia njia ya mkato.

Dkt Miguna alimkashifu Bw Odinga na kusema ushirikiano wake na Rais Kenyatta ni usaliti kwa mamilioni ya Wakenya waliomuunga mkono katika uchaguzi uliopita, wakiwemo wananchi waliouawa na polisi walipokuwa wakiandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais.

Alipuuzilia mbali msimamo wa kigogo huyo wa kisiasa kwamba hatua yake inanuia kupatanisha Wakenya akadai ushirikiano wa wawili hao unalenga tu kuwanufaisha kibinafsi.

“Kwa kusalimu amri wakati ambapo tulikuwa tushakizidi nguvu Chama cha Jubilee, Raila Odinga aliimarisha nguvu za viongozi wadhalimu, akadhoofisha na kugawanya wafuasi wake,” akasema.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Chama cha ODM, Bw Philip Etale, alimkosoa na kusema hatua ya Bw Odinga ilizuia vita na umwagikaji wa damu nchini.

“Wakenya wanataka amani, si kelele,” akasema Bw Etale.

Ingawa Bw Ruto amekuwa akidai marekebisho ya katiba yatatatiza juhudi za maendeleo, wachanganuzi wa kisiasa wamehusisha suala hilo na siasa za 2022 ambapo naibu wa rais anapanga kumrithi Rais Kenyatta atakayekamilisha hatamu yake ya pili ya uongozi ambayo ni ya mwisho kikatiba.

JAMVI: Wito wa kurekebisha Katiba wazua uhasama wa mbio za Ikulu 2022

Na VALENTINE OBARA

Pendekezo la kuandaliwa kwa kura ya maamuzi kutoa ili kuwe na mfumo wa utawala ambapo Waziri Mkuu anateua baraza la mawaziri limeibua msisimko mkubwa wa kisiasa kuelekea 2022.

Ingawa haijabainika wazi kiasi kamili cha marekebisho ya katiba yatakayohitaji kufanywa kufuatia muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Bw Raila Odinga, kuna kila ishara na uwezekano mkubwa wa kubuniwa nafasi mpya za mamlaka ya juu serikalini.

Nafasi hizo zinajumuisha Waziri Mkuu mwenye mamlaka na manaibu wake wawili, hatua ambayo inaweza kupunguza ushawishi wa rais.

Hili ni pendekezo ambalo linashinikizwa na viongozi wa upinzani na wa kidini, huku Naibu wa Rais, Bw William Ruto, na wandani wake akiwemo Kiongozi wa Wengi Bungeni, Bw Aden Duale, wakilipinga vikali.

Kwenye mazishi ya aliyekuwa mpiganiaji wa ukombozi kutokana na serikali dhalimu ya Kanu, Kenneth Matiba, Rais Kenyatta aligusia mdahalo huo akionya wale wanaozungumzia kampeni ya 2022. Inatarajiwa kuwa atazungumzia suala hili zaidi atakapotoa hotuba ya Hali ya Taifa mnamo Jumatano wiki hii.

Kulingana na Bw Ruto, marekebisho ya katiba hayifai kwa sababu yatarudisha nchi katika hali ya kisiasa wakati inahitajika viongozi waungane kuimarisha maendeleo ya taifa, mbali na mchakato huo kugharimu mabilioni ya pesa.

“Wale wanaotaka kuturudisha kwa siasa tafadhali tupeni nafasi tufanye maendeleo. Hatuwezi kuzungumzia siasa za ugavi wa mamlaka milele. Lazima tuanzishe mjadala wa siasa za kuwapa wananchi uwezo kimaisha,” akasema wiki iliyopita akiwa Nakuru.

Hii haikuwa mara yake ya kwanza kuelezea hisia zake kuhusu suala hili. Amekuwa akiligusia katika ziara zake nyingi katika pembe tofauti za nchi tangu Rais Kenyatta na Bw Odinga walipotangaza ushirikiano wao mwezi uliopita.

Pingamizi hizo zimefasiriwa na wengine kuashiria mkakati wake wa kujiepushia hasara atakayopata kimamlaka endapo atashinda uchaguzi wa urais 2022.

“Wanadhani wao pekee ndio wana haki kuzungumzia 2022 lakini pia sisi tuna haki ya kuweka mikakati,” akasema Mbunge wa Tiaty, Bw Kassait Kamket, ambaye aliwasilisha bungeni hoja ya kuunda wadhifa wa Waziri Mkuu na manaibu wake. Bw Kamket ni mwandani wa Seneta wa Baringo, Bw Gideon Moi, ambaye pia anaazimia kuwania urais 2022.

 

Madeni ya kisiasa

Kufikia sasa, Bw Ruto hana deni kubwa la kisiasa kwa yeyote ikilinganishwa na deni ambalo linabebwa na Bw Odinga kwa viongozi mbalimbali, akiwemo Bw Ruto mwenyewe.

Hivyo basi, naibu wa rais ana kila sababu ya kutetea mamlaka ya rais yasalie jinsi yalivyo kwenye katiba ya sasa. Kwa upande mwingine, Bw Odinga ana madeni hasa kwa vinara wenzake katika Muungano wa NASA ambao ni Kiongozi wa Chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula (Ford Kenya, na Kiongozi wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi.

Wandani wa vinara wenza wa Bw Odinga wamekuwa wakimshinikiza kigogo huyo wa siasa atimize makubaliano yao kwa kumuunga mkono mmoja wao kwenye uchaguzi ujao na asiwanie urais.

Endapo katiba itabadilishwa kuwe na nafasi mpya za uongozi wa taifa na vinara wa NASA waendelee kuwa pamoja, Bw Odinga anaweza kutimiza makubaliano hayo yaliyowekwa kati ya vinara, na wakati huo huo atimize azimio lake la miaka mingi la kuongoza Kenya.

Taswira ya kwanza ni kuwa, Bw Odinga anaweza kukubali kutowania urais na aunge mkono mmoja wa vinara wa NASA, kisha apewe wadhifa wa Waziri Mkuu.

 

Raila awe Rais

Taswira ya pili ni kuwa, Kiongozi huyo wa Chama cha ODM anaweza kukubaliana na wenzake apewe nafasi ya kutimiza azimio lake la kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, kisha mwingine kati yao apewe wadhifa wa Waziri Mkuu.

Hata hivyo, uwezo wa kuwa Waziri Mkuu utategemea jinsi katiba yenyewe itakavyoundwa kwa kuwa, katika mataifa mengi kwingineko duniani, wadhifa huo hushikiliwa na chama kilicho na wabunge wengi zaidi.

Wiki iliyopita, Bw Odinga alisema mabadiliko ambayo anashughulikia pamoja na Rais Kenyatta yanalenga kusuluhisha changamoto za wizi wa kura, ukabila, ufisadi, ugatuzi na usalama. Baadhi ya masuala haya yatahitaji kura ya maamuzi.

“Nilisalimiana na Uhuru kwa sababu alikubali masharti tuliyoweka. Tumeanza upya kubadilisha mambo Kenya hii. Tusiposuluhisha matatizo ya 2017 hakuna 2022. Ndio maana tumesema lazima turekebishe mambo mapema wakati huu. Uhuru amekubali na Raila amekubali, sasa wewe ni nani unapinga?” akasema mjini Kakamega.

Wazo hili liliungwa mkono na Bw Mudavadi ambaye alisema hivi majuzi kwamba, itakuwa njia mwafaka ya kurekebisha hali ambayo Wakenya wengi wanahisi inaenda mrama tangu 2010 ambapo katiba ya sasa ilipitishwa.

Lazima tuibadilishe Katiba hii – Raila

WYCLIFFE MUIA na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga amependekeza Katiba ifanyiwe mabadiliko ili kubuniwa ngazi tatu za utawala, kama ilivyopendekezwa katika rasimu ya Katiba ya Bomas.

Akiongea Jumatano katika Kongamano la Ugatuzi mjini Kakamega, Bw Odinga alisema hatua hiyo itafanikisha ugavi sawa wa rasilimali na kufanikisha malengo ya ugatuzi.

Alipendekeza kubuniwa kwa maeneo 14 zaidi ya utawala huku serikali 47 za kaunti zikiendelea kudumishwa kama ilivyo sasa.

“Napendekeza kubuniwa kwa maeneo 14 ya utawala ili kuhakikisha rasilmali zinasambazwa kwa usawa. Maeneo hayo yatasaidiana na serikali 47 za kaunti katika kufanikisha ugatuzi.

Ngazi hizi za utawala zitafanya kazi kwa ushirikiano na Serikali ya kitaifa,” akasema Bw Odinga akiongeza mfumo huo ulipendekezwa katika rasimu ya Bomas.

Baadaye akihutubia wakazi mjini Kakamega, Waziri huyo Mkuu wa zamani alifichua kuwa walikubaliana na Rais Uhuru Kenyatta ‘kubadilisha mambo’ na hakuna kurudi nyuma.

“Kama Raila na Uhuru wamekubaliana kufanya hivyo nani anaweza kupinga?” aliuliza Bw Odinga.

Gavana wa Mombasa Hassan Joho ambaye alikuwa ameandamana na Bw Odinga mjini Kakamega alisema ataongoza kampeni kali wakati ukifika wa kubadilisha katiba.

 

‘Katiba si mali ya mtu’

“Kuna watu wanafirikia katiba ni mali yao…ikisemekana katiba ibadilishwe nitakuwa mstari wa mbele kushawishi Wakenya kote nchini,” alisema Bw Joho mjini Kakamega baada ya kongamano la magavana.

Naibu Rais William Ruto hata hivyo amekuwa akipinga pendekezo la kubadilisha katiba, haswa kubuni nafasi zaidi serikalini.

Bw Ruto ameahidi kupinga hatua hiyo akisema serikali ya Jubilee kwa sasa imejitolea kutoa huduma kwa wananchi na haina wakati wa kujihusisha na mjadala wa kubadilisha katiba.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi alisema chama hicho kinaunga mkono mswada wa mbunge wa Tiaty, Kassait Kamket lakini akafafanua kuwa haitafaa kumpa waziri mkuu mamlaka yote ya kuendesha serikali bila kumhusisha rais.

“ODM kilikuwa chama cha kwanza kupendekeza kuwepo na mfumo wa uongozi wa nchi kupitia bunge kama ilivyo nchini Uingereza alisema mbunge huyo wa Suba Kusini.

Katika hotuba yake jana, Bw Odinga pia aliwataka magavana kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika vizuri huku akilaani ufisadi uliokithiri katika serikali za kaunti.

 

Ruto atengwa kuhusu marekebisho ya katiba

Na BERNADINE MUTANU

NAIBU RAIS William Ruto Jumamosi aliendelea kutengwa kwa upinzani wake kwa mapendekezo ya kufanyia marekebisho Katiba iliyopitishwa 2010.

Jumamosi, Muungano wa vyama vya wafanyakazi (COTU-K) ulimwambia Bw Ruto abadili msimamo wake na badala yake awe katika mstari wa mbele kuunga mkono marekebisho kwa lengo la kuhakikisha uwakilishi mpana serikalini.

COTU iliungana na Kanisa Katoliki ambalo Askofu Mkuu Kadinali Njue amesema marekebisho ya Katiba ni muhimu katika kuleta maridhiano ya kitaifa. Muungano wa Makanisa (NCCK) pia umekuwa ukihimiza marekebisho.

Kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi mnamo Ijumaa aliunga mkono marekebisho akisema kuna haja ya kuwa na mfumo wa utawala unaojumuisha wengi.

Wengine ambao wanaunga mkono marekebisho ni kinara wa ODM Raila Odinga ambaye washirika wake wa karibu wametangaza wazi msimamo wao na magavana Alfred Mutua (Machakos) na Wycliffe Oparanya (Kakamega).

Akiongea wakati wa mkutano na wasimamizi wa wafanyikazi, Katibu Mkuu Francis Atwoli alisema muungano huo unataka marekebisho ya Katiba kwa lengo la kuongeza nafasi kuu serikalini.

Alisema marekebisho hayo yanafaa kubuni nafasi ya rais na manaibu kadhaa na waziri mkuu na manaibu wake, kwa lengo la kuzima joto la kisiasa nchini.

“Walete hiyo Katiba turekebishe. Bw Ruto anastahili kujua kuwa anaweza tu kuongoza taifa hili ikiwa kuna amani. Anafaa kuwa katika mstari wa mbele kupigia debe marekebisho ya Katiba,” alisema Bw Atwoli, na kumuonya kuwa ikiwa hataunga mkono azimio hilo, huenda akajipata pabaya.

Wikendi iliyopita, Bw Ruto alipuzilia mbali mjadala kuhusu marekebisho ya Katiba akisema hatua hiyo haifai kwani inalenga kunufaisha watu wachache.

Imeonekana kinaya kwa Bw Ruto kupinga marekebisho ikizingatiwa alikuwa mpinzani mkuu wa Katiba iliyopitishwa 2010, ambapo alikuwa akisisitiza ilikuwa na dosari zilizofaa kurekebishwa kabla ya kuipitisha.

Mapema wiki hii, Bw Ezekiel Njeru aliwasilisha ombi kwa Bunge akihimiza marekebisho. Spika Justin Muturi alisema ombi hilo lilikuwa na uzito uliofaa kutiliwa maanani na akaitaka Kamati ya Sheria kulitathmini na kuwasilisha ripoti katika muda wa siku 60.

 

Kupunguza gharama

Kiongozi huyo wa COTU alisema sababu ya kuunga mkono marekebisho ya Katiba pia ni kupunguza idadi kubwa ya wabunge, ili kupunguza gharama, hasa katika ulipaji wa mishahara na marupurupu, pamoja na kubadilisha sheria za uchaguzi.

“Kenya ni yetu sisi wote, lazima tubadilike jinsi mambo yanavyozidi kubadilika,” alisema Bw Atwoli.

Wakati huo huo, COTU ilimtaka Waziri wa Leba Ukur Yattani “kutopotoshwa” na wanasiasa kuunga mkono mabadiliko ya sheria kuhusu bodi ya Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF).

“Ikiwa sheria kuhusu itabadilishwa, COTU itaenda mahakamani kutafuta haki, ikiwa mahakama itashindwa kabisa, tuko tayari kuunda hazina yetu ya pensheni,” alisema.

Chama hicho kinapinga mabadiliko yoyote katika hazina hiyo kwa kusema yanalenga kuibua usimamizi mbaya, wizi na uharibifu wa fedha za wafanyakazi.

Pia, muungano huo ulipinga marekebisho ya kifungu cha katiba kinacholinda migomo ya wafanyikazi na mikataba ya mishahara na marupurupu.

Alisema mabadiliko hayo yanahitaji marekebisho ya Katiba kupitia kwa kura ya maamuzi lakini sio kupitia Bungen kama wanavyopendekeza baadhi ya wanasiasa.

Muungano huo uliitaka serikali kutathmini uwezo wa Shirika la Bima la Afya (NHIF) kuchukua kiwango kikubwa cha fedha katika mradi wa bima kwa wanafunzi, kwa kusema huenda shirika hilo likatumiwa kuiba fedha za umma.

Wakati huo, aliitaka serikali kuwaruhusu maafisa wa polisi kuunda chama cha kuwatetea.

Mwanasheria Mkuu mpya mtarajiwa aahidi kutatua janga la ufisadi nchini

Na LUCY KILALO

Kwa ufupi:

  • Jaji Kariuki aahidi kukabiliana na ufisadi akisema kuwa atafanya vikao na afisi husika kubainisha changamoto za vita dhidi ya ufisadi
  • Sijawahi kutuhumiwa kwa ufisadi, kushindwa kutekeleza kazi ama kushawishiwa kwa njia yoyote nyingine. Nguvu yangu inatokana na tajriba yangu, amesema
  • Aahidi kufuatilia suala la kurejesha mali iliyopatikana kutokana na ufisadi na kubainisha chanzo cha  baadhi ya mawakili wanaowakilisha serikali kudai kiasi kikubwa cha pesa
  • Awahakikishia Wakenya kuwa katika utendakazi wake, atafuata Katiba na hataegema upande wowote wa kisiasa

JAJI Paul Kihara Kariuki aliyeteuliwa kwa nafasi ya Mwanasheria Mkuu Alhamisi ameahidi kudumisha Katiba na Sheria za nchi na kuishauri serikali vilivyo, bila kushawishiwa kisiasa ama kwa njia nyingine yoyote.

Jaji Kariuki ambaye amekuwa Rais wa Mahakama ya Rufaa  alikuwa mbele ya Kamati ya Uteuzi ya Bunge la Kitaifa, inayoongozwa na Spika Justin Muturi, kupigwa msasa alielezea misimamo yake kuchangiwa zaidi na malezi yake, dini katika kanisa la Kianglikana pamoja na kuthamini utekelezaji wa haki.

“Ikiwa nitaidhinishwa, ninawahakikishia kuwa nitaelekezwa na Katiba. Afisi ya Mwanasheria Mkuu inawakilisha watu wa Kenya na sio chombo cha chama chochote cha kisiasa,” alisema.

Jaji Kariuki pia aliahidi kukabiliana na ufisadi akisema kuwa atafanya vikao na afisi nyingine husika kama ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Idara ya Upelelezi (DCI) na hata Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) kuweza kubainisha changamoto ziko wapi, kuhusiana na kesi za ufisadi.

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Adan Duale alitaka kujua kwa nini katika miaka michache iliyopita, uhusiano baina ya urais, bunge na mahakama haujakuwa wa kuridhisha, huku akimtaka aeleze ikiwa mtangulizi wake alishindwa na kazi.

Akijibu, Jaji Kihara alisema haitakuwa vyema kumjadili mwenzake, ingawa alikiri kuwepo kwa mivutano hiyo, na kuahidi kubadilisha hali hiyo.

 

Daraja la mazungumzo

“Lazima tufanye kazi pamoja. Lazima tuongee, kwani hiyo ndiyo njia ya pekee ya kupatia katiba nafasi, kibinafsi na kwa pamoja. Afisi ya Mwanasheria Mkuu inaweza kuwa daraja la mazungumzo kwa pande hizo tatu.”

Wakati huo huo, Jaji Kihara alijitetea kuhusiana na kesi ambayo mahakama ya Rufaa ilidaiwa kufanya kikao usiku na kubatilisha uamuzi uliokuwa umetolewa na Mahakama Kuu wakati wa uchaguzi 2017.

Alisema wajibu wake kama rais ulikuwa wa kuunda kikao kitakachosikiza kesi pekee, hata hivyo hangetoa maelezo zaidi kwa kuwa alihojiwa na Tume ya Idara za Mahakama (JSC), na aliwasilisha majibu yake, na anachosubiri ni uamuzi wa tume hiyo.

“Sijawahi kutuhumiwa kwa ufisadi, kushindwa kutekeleza kazi ama kushawishiwa kwa njia yoyote nyingine. Nguvu yangu inatokana na tajriba yangu na kwamba haki lazima itekelezwe.’

“Sitatingishwa kufanya kile kinachoenda kinyume na Katiba na Sheria.”

Pia alitetea uamuzi wake wa kukubali uteuzi huo baada ya Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma ambaye bali na kumsifia utendaji kazi wake akiwa mahakamani, alishangaa kwa nini akubali nafasi ambayo itamnyima amani.

Jaji Kariuki alisema lengo lake ni kutumikia nchi yake, akieleza kuwa hata akiwa jaji amekabiliwa na shinikizo nyingi.

 

Uaminifu

“Kubadilisha nchi hii, lazima tupate wanawake na wanaume ambao ni waaminifu tayari kutumikia nchi yao,” alisema akiongeza kuwa hakuna haja kwa mtu “kuupata ulimwengu wote lakini kuiuza nafsi yake.”

Vile vile, aliahidi kufuatilia suala la kurejesha mali iliyopatikana kutokana na ufisadi na kubainisha chanzo cha  baadhi ya mawakili wanaowakilisha serikali kudai kiasi kikubwa cha pesa, baada ya Spika Muturi kuzua hofu kuwa huenda ni njama nyingine ya kufuja pesa kutoka kwa serikali.

Jaji Kariuki ambaye aliwasifia wazazi wake na mkewe kuweza kufikia mahali alipo, alieleza kuwa alikuzwa kuthamini Wakenya kama watu wanaoamini ukweli na haki.

Akitoa mfano wa jinsi ua linalovyochanuka na mwishowe urembo wake kubainika, ndivyo kila Mkenya anafaa ajaribu kuona uzuri kwa mwenzie ili kukuza utaifa.