Chama kipya Pwani kinavyotishia Ruto na Raila

Na MAUREEN ONGALA

MIPANGO ya kuzindua chama kipya Pwani kabla uchaguzi ujao ufike, imeshika kasi na kutishia kugeuza mawimbi ya kisiasa katika ukanda huo.

Chama hicho cha Pamoja African Alliance (PAA) kinahusishwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi na wandani wake ambao husema ukanda wa Pwani unastahili kuwa na chama kikubwa kinachotambulika kitaifa.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba, chama hicho ambacho kilikabidhiwa cheti cha muda cha usajili hivi majuzi kinaendelea kujenga afisi zake katika kaunti mbalimbali kinapojiandaa kusajili wanachama.

Mojawapo ya afisi hizo iko katika Kaunti ya Kilifi, ambayo inatarajiwa kuwa makao makuu yake.Chama cha PAA kitatambuliwa kwa rangi za samawati na manjano, huku nembo yake ikiwa nyumba ya kitamaduni ya Kiafrika.

Kulingana na Bw Kingi, rangi ya samawati ilichaguliwa ili kuashiria thamani ya bahari ambayo ni kitegauchumi kikubwa kinachoweza kukomboa ukanda huo ikiwa rasilimali zake zinathaminiwa na kutumiwa inavyostahili.

“Wakati umefika sasa watu waanze kuzoea rangi ya samawati.Hiyo rangi itatenda maajabu hivi karibuni. Jamii inahitaji nyumba, lakini hatuwezi kuwa tukiita watu waungane ilhali wakati huo huo tunaunga mkono vyama vingine,” akasema Bw Kingi.

Uzinduzi wa chama hicho huenda ukawalazimu Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, na Naibu Rais, Dkt William Ruto, kupanga upya mikakati yao wakitaka kupata umaarufu Pwani kabla uchaguzi ujao ufanywe.

Dkt Ruto ambaye anatarajiwa kuwania urais kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA), amefanya ziara nyingi Kilifi tangu wakati alipofanikiwa kuwavutia upande wake wabunge walioasi ODM wakiongozwa na Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa.

Kwa upande mwingine, imebainika baadhi ya wanasiasa waliobaki katika ODM wanasubiri chama kipya kizinduliwe ili wajiunge nacho.

Hivi majuzi, Bw Kingi alipokonywa wadhifa wake wa uenyekiti katika ODM kwa kushikilia msimamo wake wa kutaka kuwe na chama kipya kikuu cha Pwani, wazo ambalo limekuwa likipingwa vikali na Bw Odinga.

Gavana huyo pia alikataa miito ya baadhi ya wanasiasa waliomtaka ajiunge na Dkt Ruto ndani ya UDA, akisema njia pekee ya Pwani kujikomboa kutokana na changamoto ambazo zimedumu kwa karne nyingi ni kupitia kwa chama kilicho na mizizi ukanda huo ambacho kitatambulika kitaifa.

Aliwataka wanasiasa wa Pwani wanaofululiza kuingia UDA wajifunze kutoka kwa wenzao wa eneo la Kati ambao wameshikilia msimamo kuwa watashirikiana na viongozi wengine wakiwa ndani ya vyama vyao wenyewe.

“Mkishaapishwa kuwa wabunge na maseneta, mtapitia yale yale ambayo mliyapitia katika ODM kwa sababu chama ni cha wenyewe. Naibu Rais hakunihusisha alipokuwa anaunda UDA, lakini ananialika nijiunge na chama hicho,” alionya.

“Mimi nitakuwa mgeni nikienda huko na baada ya siku tatu sitafurahia kuwa huko ndani. Ikiwa watu wengi wanaomuunga mkono Naibu Rais wameonelea heri wafanye hivyo wakiwa katika vyama vyao, mbona eneo la Pwani liwe tofauti? Tunahitaji chama ambacho kitatetea kikamilifu masilahi ya eneo hili. Hatutaki kutishwatishwa tena,” akasema.

Hata hivyo, alisema wakati haujafika kwa Pwani kusimamisha mgombeaji urais hadi wakati viongozi watakapokuwa na umoja.

“Wapwani wangapi wamewahi kuwania urais lakini wakapata chini ya kura 200? Nakubaliana na wale wanaotaka tujitose katika siasa za kitaifa lakini tujengeni boma letu kwanza,” akasema.

Uamuzi wa kuunda chama kipya ulifanywa baada ya juhudi za kuunganisha vyama vitano vilivyo na mizizi Pwani kugonga mwamba.

Viongozi wa vyama vya Shirikisho, Kadu-Asili, Republican Congress, Communist na Umoja Summit wangali wanasubiriwa kutoa mwelekeo kwa wanachama wao.

Wapwani wakaushwa tena

Na WAANDISHI WETU

MASAIBU yanayokumba wakazi wa Pwani wanapojitafutia riziki yanazidi kuongezeka, baada ya kubainika kuwa, wavuvi wanaotegemea Bahari Hindi sasa wanasukumwa nje na meli kubwa za makampuni ya kigeni.

Katika miaka ya hivi majuzi, mifuko ya wakazi wengi wa Pwani imekauka kwa vile sekta zilizokuwa zikitegemewa sana kiuchumi zimedorora.

Sekta ya uchukuzi ambayo kwa muda mrefu ilitegemewa kutoa nafasi za ajira kwa vijana na wawekezaji ilianza kulemewa punde baada ya reli ya SGR kukamilika.

Hali hiyo ilisababishwa na sera ya serikali kuu iliyohitaji mizigo yote inayotoka Bandari ya Mombasa hadi Nairobi isafirishwe kwa njia ya reli.

Safari za SGR ziliathiri uchukuzi wa abiria kwa basi, hali iliyopunguza mapato kwa makampuni ambayo yalilemewa zaidi wakati janga la corona lilipozuka.

Hitaji kuwa magari ya uchukuzi wa umma yapunguze idadi ya abiria kama mbinu ya kuepusha maambukizi ya virusi vya corona, lilifanya baadhi ya makampuni kama vile Modern Coast na Mombasa Raha kusitisha uchukuzi wa abiria kwa muda usiojulikana.

Hatua hii iliwaacha mamia ya watu bila ajira.Sekta ya utalii iliyokuwa imeanza kufufuka baada ya kupata pigo kutoka kwa mashambulizi ya kigaidi, ilififia tena wakati wa janga la corona.

Kufikia sasa, hoteli nyingi za Pwani bado zinatatizika kurejelea hali ya kawaida kwa sababu ya hasara zilizopatikana tangu mwaka uliopita huku idadi ya watalii pia ikipungua pakubwa kutokana na changamoto za usafiri kimataifa zinazoendelea kushuhudiwa.

Walioathirika si wamiliki na waajiriwa wa hoteli kubwa kubwa pekee bali pia wafanyabiashara wadogo kwa kuwa kufikia sasa, fuo nyingi za umma zilizokuwa zikivutia watalii wa humu nchini zingali zimefungwa.

Viongozi wa kisiasa Pwani hawana msimamo mmoja kuhusu namna ya kutatua changamoto hizi kwa sababu ya tofauti zao za kisiasa.

Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho ambaye katika miaka iliyopita alikuwa mstari wa mbele kushinikiza serikali ikomeshe dhuluma dhidi ya Wapwani, alibadili mtindo wake baada ya Kiongozi wa ODM, Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta kuamua kushirikiana kupitia kwa handisheki.

Katika hotuba zake tangu wakati huo, Bw Joho husema uamuzi wake wa kukumbatia mashauriano na viongozi wa kitaifa, akiwemo rais, kuhusu changamoto za Wapwani ndizo zimewezesha miradi mikubwa ya miundomsingi kufanikishwa eneo hilo.

Hata hivyo, wakosoaji wake wanasisitiza kuwa, Wapwani bado wanateseka licha ya miradi hiyo mikubwa inayojumuisha ujenzi wa barabara, kutekelezwa na na serikali kuu.

“Nilipokuwa nikizungumzia mambo haya awali, watu walidhani nina wazimu, mimi si wazimu. Tumeingia katika siasa sio eti kwa sababu tunapenda siasa ila tunataka kukomboa watu wetu,’ Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali alisema majuzi.

Licha ya kuwa jamii nyingi Pwani zimetegemea uvuvi kama kitega uchumi tangu jadi, sasa kuna ushindani kutoka kwa meli kubwa zinazotumia mbinu ya kukokota nyavu chini ya maji kuvua samaki.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibainisha kuwa, wavuvi wengi sasa wameamua kuacha kwenda baharini na badala yake hununua samaki kutoka kwa wafanyabiashara Wachina.

Mbali na Wachina, imebainika kuwa meli nyingine kubwa zilizopata leseni kuvua samaki nchini humilikiwa na mashirika kutoka Ushelisheli, Italia, Taiwan, na Hong Kong.

Katika mwaka wa 2020 pekee, meli saba kubwa za Uchina zilisajiliwa kufanya uvuvi katika maji makuu humu nchini na leseni zao zitadumu hadi Desemba 2031.

Samaki sasa huvuliwa na meli hizo kubwa kabla wafike katika sehemu za maji ambapo wavuvi Wakenya walikuwa wakitegemea kwa shughuli zao.

Bw Ngole Mbaji ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa kikundi cha kusimamia wavuvi Mtwapa, Kaunti ya Kilifi alisema, serikali pia imechochea masaibu yao kwa sababu kuna sheria za uvuvi zinazobagua wavuvi wadogo.

“Sasa samaki wote sokoni ni wa kutoka kwa Wachina. Wanawake ambao wanauza samaki huwa lazima waamke alfajiri kwenda katika maghala ya Wachina kununua samaki, wasafishe ndipo wauze,” akasema Bw Mbaji.

Kulingana na Bw Mbaji, serikali kupitia kwa Mamlaka ya kusimamia shughuli za majini nchini (KMA) pia ina masharti mengi yanayogharimu pesa nyingi ambazo wavuvi wanaomiliki meli kubwa ndio wana uwezo wa kugharamia.

Masharti hayo ni kama vile kutafuta cheti cha ukaguzi wa boti mara kwa mara, boti ziwe na ubora unaofikia kiwango cha kimataifa, na waendeshaji boti wapokee mafunzo kutoka kwa taasisi ya Bandari Maritime Academy.

Alisema haya yote yanagharimu zaidi ya Sh100,000 ilhali wavuvi wa Pwani huwa na mapato madogo mno.

“Kile KMA imefanya ni kama kuingiza moshi katika mzinga wa nyuki. Wanatumia udhaifu wetu kutufurusha baharini ili tuwaachie nafasi hawa raia wa kigeni,” akasema Bw Mbaji.

Wale wanaoshindwa kuafikia mahitaji hayo hukamatwa na kushtakiwa.Juhudi zetu kutafuta maoni ya KMA kuhusu suala hili ziligonga mwamba kwani Katibu wa Wizara ya Uchukuzi anayesimamia masuala ya baharini, Bi Nancy Karigithu, na Mkurugenzi Mkuu wa KMA, Bw Robert Njue walikataa kujibu maswali yetu.

Haya yote yanashuhudiwa licha ya jinsi maafisa wa serikali wamekuwa wakifanya ziara nyingi Pwani wakiahidi kustawisha sekta ya uvuvi.Mojawapo ya ziara hizo ilifanywa Februari na Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, Bw Peter Munya alipozindua meli tatu kubwa za uvuvi.

Meli hizo zilizokabidhiwa kwa Serikali ya Kaunti ya Mombasa ziligharimu Sh60 milioni na zililenga kusaidia wavuvi wa eneo hilo.

Msimamizi wa kikundi cha wavuvi wa Mtwapa, Bw Ndago Gunga alisema walipokea boti lakini limeegeshwa muda wote huo na wala hawajanufaika nalo.

“Nakumbuka lililetwa katika msimu wa uvuvi. Tulifurahi sana kwa sababu tulitumai kuvua samaki wengi katika maji makuu. Lakini kabla tuanze kulitumia, tukabainisha kuna vifaa muhimu ambavyo havikuwepo ndani. Tulihitajika kuchanga takriban Sh1 milioni ili kulifanyia ukarabati na kiwango hicho ni kikubwa sana kwetu,” akaeleza.

Utumiaji wake pia ungehitaji nahodha aliyehitimu kuliko wavuvi hao, mekanika wa kulifanyia ukarabati kila mara na mafuta mengi.Hali si tofauti kwa wavuvi wa Kaunti ya Kwale.

Mmoja wa wavuvi, Bw Omar Bonga alisema maisha ya wavuvi yamekuwa magumu mno kwani wanalazimika kuchagua kati ya kuinua uwezo wao wa uvuvi au kutunza familia zao kwa pesa kidogo wanazopata.

“Inatubidi kupunguza chakula chetu kila siku kwa sababu pesa hazitoshi. Hali huwa mbaya zaidi tunapohitajika kulipia matibabu au karo za shule,” akasema.

Huku msimu mwingine wa uvuvi ukianza mwezi huu, wavuvi Wakenya wanahofia ni wavuvi wa kigeni pekee watakaoendelea kunufaika.

Nassir na Shahbal walilia ‘tosha’ ya Raila uagavana Mombasa

VALENTINE OBARA na ANTHONY KITIMO

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, alikwepa kumwidhinisha mwanasiasa yeyote kuwania ugavana Mombasa kupitia chama hicho mwaka ujao alipozuru kaunti hiyo.

Wanasiasa wawili wanaomezea mate tikiti ya chama hicho kuwania ugavana Mombasa mwaka ujao walionekana kuzidisha juhudi za kusaka ‘baraka’ za Bw Odinga.

Wawili hao ambao ni Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir na mfanyabiashara Suleiman Shahbal, walionekana kung’ang’ania sikio la Bw Odinga alipozuru kaunti hiyo Alhamisi.

Bw Nassir na Bw Shahbal hawakukutana ana kwa ana hadharani katika hafla mbili ambazo Bw Odinga alihudhuria akiandamana na Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho.

Hafla ya kwanza ambayo Bw Odinga alihudhuria ilikuwa ni uzinduzi wa kituo cha mafuta cha Hass katika mtaa wa Nyali, ambapo Bw Shahbal alikuwepo.

Baada ya kuandamana kwa karibu katika uzinduzi huo, wawili hao walienda kufanya mkutano wa faragha nyumbani kwa Bw Shahbal katika mtaa huo.

Ingawa waliyozungumzia hayakuanikwa wazi, duru ziliambia Taifa Leo kwamba, Bw Odinga alimwahidi Bw Shahbal kutakuwa na kura ya mchujo kwa njia ya haki na uwazi kuamua watakaopewa tikiti ya chama kuwania viti vyote vya kisiasa.

Baadaye, katika hafla ya kuzindua kitengo maalumu cha matibabu ya moyo katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Pwani, Bw Odinga alikumbwa na shinikizo kutoka kwa umati uliokuwa ukimrejeaja Bw Nassir kama ‘gavana mtarajiwa.’

Ingawa Bw Joho ndiye alikuwa mwandalizi wa hafla, Bw Nassir ndiye alitembea na waziri huyo mkuu wa zamani sako kwa bako walipowasili katika hafla hiyo. Bw Joho aliwafuata kwa karibu kutoka nyuma.

Katika hotuba yake, Bw Odinga alimtambua tu Bw Nassir kama mbunge mahiri ambaye amechangia mengi hasa katika wadhifa wake wa uenyekiti katika kamati ya bunge ya kuchunguza matumizi ya fedha za umma.

“Nataka kutoa shukrani kwa mbunge wa hapa kwa kazi anayofanya kufichua ufisadi katika bunge. Tunataka wabunge wetu waendelee kufanya kazi yao,” akasema Bw Odinga, huku mbunge huyo akisimama kando yake. Bw Nassir alisema kila mtu yuko huru kujiunga na ODM Mombasa lakini ana matumaini makubwa kwamba wapigakura watamchagua yeye kurithi kiti cha Bw Joho.

“Tumeona baadhi ya watu waliokuwa wakikashifu ODM katika uchaguzi uliopita wakirudi kutafuta kiti cha ugavana. wajue mimi ndiye nitakuwa gavana Mombasa” alisema Nassir.

JAMVI: Mkanganyiko mkuu unaogubika siasa za urithi Pwani

Na MOHAMED AHMED

KWA muda sasa magavana watatu kutoka Pwani akiwemo wa Mombasa Hassan Joho, Salim Mvurya wa Kwale na mwenzao wa Kilifi Amason Kingi wameonekana kuweka mipango yao ya kisiasa ambayo itakuja baada ya kumaliza hatamu zao.

Magavana hao wapo kwenye hatamu zao za mwisho kwenye viti hivyo ambavyo itakuwa wamevishikilia kwa muda wa miaka kumi wakati awamu zao zitakapokamilika mwaka 2022.

Wakati viongozi hao wanapopanga kuondoka kwenye nafasi hizo, tayari kuna wale ambao wanamezea mate viti hivyo na kutaka kuwarithi. Baadhi ya wanaomezea mate ni wale ambao magavana hao pia wangependelea wachukue nafasi hizo wakati watakapokuwa wameondoka.

Miongoni mwa viongozi ambao kufikia sasa wameonyesha azma ya kurithi viti hivyo ni pamoja na naibu gavana wa Kwale Fatuma Achani ambaye pia anaungwa mkono na Bw Mvurya

Mpinzani

Kufikia sasa mbunge wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani ameonekana kuwa mpinzani wa karibu wa Bi Achani.

Licha ya Bw Mvurya kuwa chama kimoja cha Jubilee na Bw Mwashetani gavana huyo amesisitiza kwamba Bi Achani ndiye anastahili zaidi kumrithi ifikapo 2022

Katika mkutano wa hivi majuzi kwenye mazishi ya Askofu Morris Mwarandu Bw Mvurya alisema ni Bi Achani pekee atakayeweza kuendeleza mafanikio ambayo kaunti hiyo imeshuhudia tangu 2013

“Ni vile hapa ni mazishini sitaongea zaidi. Lakini Askofu aliniambia ‘muda wako unaisha ututayarishie ya mbele’. Naibu gavana ametayarishwa. Mnaona Tanzania hakujakuwa na msukosuko? Katika taasisi ni lazima watu watayarishwe,” akasema.?

Wengine wanaoaminika kumezea mate kiti hicho ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Mtuga Chirau Mwakwere, na katibu wa Wizara ya Kilimo Hamadi Boga.? Mara kwa mara Bi Achani na Bw Mwashetani wamekuwa wakitoleana cheche za maneno ambazo zinaelekezwa na mipango yao ya kurithi Bw Mvurya

Cheche hizo za maneno ya kisiasa pia zimekuwa zikushuhudiwa katika kaunti ya Mombasa ambapo baadhi ya viongozi wanalenga kumrithi Gavana Joho.

Viongozi hao ni pamoja na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo na mfanyabiashara Suleiman Shahbal ambao kufikia sasa ndio viongozi ambao wamejitosa ulingoni wazi wazi wakitaka kumrithi Bw Joho.? Hata hivyo, ukali wa siasa hizo za urithi zimeonekana kuelemea upande wa Bw Nassir na Bw Shahbal ambao ndio mahasimu wa karibu.

Huku Bw Nassir akionekana kusubiri kuidhinishwa na Bw Joho katika azma yake, Bw Shahbal ambaye pia sasa ana uhusiano wa karibu na Bw Joho amekuwa akiendeleza kampeni za mapema kupitia vikao vinavyotambulika kama “Gumzo Maskani”.

Kati ya mwezi wa Februari hadi mwezi jana, kiongozi huyo amefanya mikutano kadhaa katika maeneo bunge ya Mombasa ikiwemo Likoni, Changamwe, Mvita Kisauni na Jomvu kueleza sera zake.

Bw Nassir naye kwa upande amekuwa akitumia nafasi yake kama kiongozi kukutana na wakazi hususan wa eneo bunge lake la Mvita na kueneza azma yake ya kutaka kuwania ugavana.

Hata hivyo, Bw Nassir hajakuwa akionekana zaidi kwenye maeneo bunge mengine kufanya kampeni zake kama vile Bw Mbogo ambaye pia ameshikilia kampeni zake mashinani katika eneo bunge lake la Kisauni.

Uchanganuzi wa Jamvi umeonyesha katika miezi hiyo miwili iliyopita, Bw Nassir amezuru makanisa katika eneo la Changamwe mara tatu huku Bw Shahbal akitekeleza mikutano takriban 20 katika muda huo huo.

Kampeni hizo za mapema pia zimeibua tumbo joto katika chama cha ODM baada ya Bw Shahbal kutangaza kuwa anarudi kwenye chama hicho.

“Walinifungia mlango wakati ule wa nyumba lakini sasa si handisheki imekuja. Si tumerudi nyumbani?” Bw Shahbal alisema katika mmoja ya mikutano yake.? Tangazo hilo la Bw Shahbal lilipelekea Bw Nassir naye kumpiga vijembe mpinzani wake huyo na katika mkutano wa eneo la Jomvu akaonya wakazi dhidi ya kuchagua watu ambao ‘wanazuka saa hizi.’

“Mimi nataka kuwauliza wao walikuwa wapi wakati sisi tulikuwa tunapambana? Mimi nawaambia muwe makini na watu hao,” akasema Bw Nassir.? Licha ya wawili hao kujitokeza kumenyana kwenye kiti hicho, bado haijakuwa wazi iwapo Bw Joho atamuunga mkono yeyote kati yao.

Iwapo Bw Joho atajitokeza wazi kutaka kumuunga mkono kiongozi wa kumrithi basi naibu wake Dkt William Kingi atakuwa miongoni mwa wale wanaotarajia kuungwa mkono.

Dkt Kingi pia amewahi kutangaza kuwa atawania kiti cha ugavana, hata hivyo hakuna mikutano yoyote ya wazi ambayo ameanza kutekeleza.? Aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar pia anatarajiwa kuwepo kwenye kinyang’anyiro hicho. Hata hivyo, bado pia yeye hajaanza kujitosa kwenye kampeni za mapema.

Kwa sasa, mwezi mtukufu wa Ramadhan utasitisha kampeni hizo kama ilivyo ada ya wanasiasa wa Mombasa huku kindumbwendumbwe kikitarajiwa baada ya mwezi huu ambao umeanza jana kukamilika.

Kwengineko katika kaunti ya Kilifi mihemko ya kisiasa ya kurithi Gavana Amason Kingi yamevutia aliyekuwa mbunge Gideon Mung’aro na mbunge wa Malindi Aisha Jumwa

Bado siasa hazijapamba moto eneo hilo lakini Bi Jumwa alikuwa ameonekana kuendesha siasa za chini kwa chini.

Bw Mung’aro naye ameonekana kuwa karibu na Bw Kingi ambaye kwa muda amekuwa akiendesha siasa za chama cha Pwani. Naibu gavana Gideon Saburi pia ametajika katika siasa hizo za urithi.

Raila awaonya Wapwani dhidi ya kuunda chama

LUCY MKANYIKA na MAUREEN ONGALA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amepinga msukumo wa baadhi ya viongozi wa Pwani kuunda chama cha kisiasa cha kutetea maslahi ya eneo hilo.

Akizungumza katika Kaunti ya Taita Taveta alipoanza ziara ya kuvumisha pendekezo la kurekebisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), Bw Odinga alisema pendekezo la kuunda chama cha ukanda huo kitaleta mgawanyiko wa nchi.

Wito wa uundaji chama cha Wapwani umekuwa ukivumishwa na viongozi wengi katika ukanda wa Pwani.

Hata hivyo, katika wiki chache zilizopita, wengi wao waliachana na mipango hiyo ambayo sasa inaonekana kuendelezwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi na wandani wake pekee.

Bw Odinga alisema kuwa katiba inawapa Wakenya haki ya kuunga mkono mrengo wowote bila kueneza ukabila nchini.Viongozi wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto katika ukanda huo walitangaza wataingia katika Chama cha United Democratic Alliance badala ya kuendeleza mipango ya awali ya kuunda chama cha Wapwani.

Kwa upande mwingine, Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho alisema aliwekeza sana katika uundaji wa chama cha ODM kwa hivyo hana nia ya kukihama chama hicho kwa sasa, anapolenga kutafuta tiketi yake kuwania urais 2022.

Bw Odinga alionya kuwa, kutakuwa na hatari ya kusababisha migawanyiko endapo viongozi wa Pwani wataunda chama ambacho hakitakuwa na mtazamo wa kitaifa.

“Katika katiba, Kenya ni demokrasia ya vyama vingi na tunataka kuwa na vyama vya kitaifa. Tukianza kuwa na vyama vya majimbo, tutagawanya Kenya. Kama unataka kuunda chama, katiba haikuruhusu kuanzisha chama cha ukoo au kikabila. Huo ni ushauri ningetaka kuwapa watu wa Pwani,” akasema.

Hapo jana, balozi huyo wa miundomsingi katika Muungano wa Afrika (AU), alifanya mikutano mbalimbali Kaunti ya Taita Taveta.Alikuwa ameandamana na viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na Gavana Granton Samboja.

Katika mikutano ya hadhara, viongozi waliohutubu waliahidi wananchi kwamba mswada wa BBI ukipitishwa utaleta manufaa kwa maendeleo na uongozi bora.

Kulingana nao, mapendekezo kama vile kuongeza mgao wa fedha kwa kaunti na kutengea madiwani pesa za maendeleo ya wadi, yatasaidia kustawisha nchi katika maeneo ya mashinani.Msafara wa Bw Odinga leo umepangiwa kuelekea Kaunti ya Kilifi ambayo imegeuka kitovu cha wito wa uundaji chama cha Wapwani.

Mbunge wa Ganze, Bw Teddy Mwambire, alisema kuwa ziara ya Bw Odinga haihusu masuala ya chama bali BBI.Jumatatu wabunge wa chama ODM Kaunti ya Kilifi pamoja na wajumbe wa Kaunti hiyo walifanya kikao kirefu na Bw Kingi kujiandaa kwa ziara ya Bw Odinga.

 

Joto la siasa lapanda Pwani Ruto na Raila waking’ang’ania kura za wakazi

NA MOHAMED AHMED

JOTO la siasa limepanda Pwani huku migawanyiko ikizuka katika kambi za kiongozi wa ODM Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto.

Kambi ya Bw Odinga imeingiwa na kiwewe kufuatia tangazo la Gavana Amason Kingi kuwa atazindua chama cha Wapwani kufikia Juni mwaka huu huku mwenzake wa Mombasa Hassan Joho akihimiza umoja wa wakazi.

Mianya pia imeibuka katika kambi ya Dkt Ruto baada ya Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na Owen Baya wa Kilifi Kaskazini kuanza kuvutana kutokana na azma zao za kuwania kuwania ugavana 2022.

Hii ni baada ya Bi Jumwa kutangaza KADU Asili kuwa chama cha Wapwani, naye Bw Baya akitangaza kuwa chama cha wakazi wa mwambao kitazinduliwa mwezi Machi.

Mvutano katika kambi ya Dkt Ruto pia unashuhudiwa Taita Taveta kati ya wabunge Naomi Shaban (Taveta), Jones Mlolwa (Voi) na Lydia Haika (Mwakilishi wa Wanawake).

Joto hilo la siasa kati ya Bw Odinga na Dkt Ruto linasukumwa na ushindani wa kuzoa jumla ya kula milioni 1.7 za eneo hilo, ambapo Tangatanga wamepata matumaini kufuatia ushindi wa mgombeaji wao katika uchaguzi mdogo wa Msambweni, Feisal Bader mwezi uliopita.

Hii imechochea magavana Kingi na Joho kuanza mikakati ya kuzima mawimbi ya Tangatanga eneo la Pwani.

Wachanganuzi wanasema kuwa msukumo wa kubuni chama cha Wapwani ni mbinu ya ODM kukabili upepo wa Dkt Ruto kwa kushawishi wakazi kuunga mkono chama kinachohusishwa nao, kisha baadaye waingie katika muungano na ODM.

Bw Joho anaungwa mkono na maseneta Mohammed Faki (Mombasa) na Stewart Madzayo (Kilifi), pamoja na wabunge Ali Wario (Garsen), Abdulswamad Nassir (Mvita), Mishi Mboko (Likoni), William Kamoti (Rabai), Said Hiribae (Galole), Andrew Mwadime (Mwatate), Omar Mwinyi (Changamwe), Badi Twalib (Jomvu), Ken Chonga (Kilifi South) na Teddy Mwambire (Ganze).

Wengine ni wabunge waakilishi wa wanawake, Gertrude Mbeyu (Kilifi), Aisha Mohammed (Mombasa) na Ruweida Obbo (Lamu).Mrengo wa Tangatanga nao una aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar na wabunge Mohamed Ali (Nyali), Jumwa (Malindi), Khatib Mwashetani (Lunga Lunga), Benjamin Tayari (Kinango), Baya (Kilifi North), Paul Katana (Kaloleni), Ali Wario (Bura), Shariff Athman ( Lamu Mashariki), Feisal Bader (Msambweni) na wabunge waakilishi, Bi Haika (Taita Taveta) na Rehema Hassan (Tana River).

Mchanganuzi wa siasa za Pwani, Profesa Hassan Mwakimako anapuzilia mbali juhudi za viongozi wa mirengo hiyo miwili akisema wote wanasukumwa na maslahi yao ya kibinafsi wala sio kwa ajili ya wakazi.

Njama ya Joho, Kingi ‘kupiga chobo’ vinara wa Tangatanga

Na CHARLES LWANGA

MIBABE wa chama cha ODM eneo la Pwani sasa wamepanga njama kuwapiku wafuasi wa Naibu Rais William Ruto eneo hilo, wanaotaka kubuni chama kipya cha Wapwani.

Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, na mwenzake wa Kilifi, Bw Amason Kingi, wametangaza mipango ya kuzindua chama ambacho Wapwani watajitambulisha nacho kuanzia uchaguzi wa 2022.

Tangazo lao kwamba watazindua chama hicho mwezi Juni, lilikujia saa kadha baada ya wafuasi wa Dkt Ruto katika ukanda huo wametia moto wito wa kubuni chama cha Wapwani.

Mwishoni mwa wiki, Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, alifichua kuwa chama cha Kadu Asili ndicho wamepiga msasa ili wakitumie katika chaguzi zijazo, bila kutegemea vyama ambavyo vigogo wake si Wapwani.

Lakini Bw Joho alipinga mpango wa Bi Jumwa na wenzake akidai ni mbinu ya kutia kura za Wapwani katika kapu moja kwa manufaa ya Dkt Ruto.

Mnamo Jumamosi katika mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Kaloleni, Gunga Mwinga, Gavana Kingi – ambaye ni mwandani wa Bw Joho – alisema eneo hilo lina kura takribani milioni tatu na wakati umefika kwao kujisimamia kisiasa.

“Nataka kuhakikishia wakazi wa Pwani kuwa ifikapo Juni mwaka huu tutakuwa na chama chetu wenyewe ambacho kitaongoza kampeni za uchaguzi,” akasema.

Wakati huo huo, Bw Kingi alikashifu viongozi wa Pwani kwa kupigana wenyewe kwa wenyewe akisema hicho ndicho kizuizi kikuu cha umoja wa kanda hiyo.

“Changamoto kubwa tuliyonayo ni kwamba hata tukiitisha umoja wa Wapwani tunaendelea kupigana wenyewe kwa wenyewe kisiasa, na hata kupigia debe wagombeaji wa kutoka maeneo mengine ya Kenya,” alieleza.

Wiki mbili zilizopita, wabunge wa Tangatanga walimuidhinisha Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya, kama kinara na msemaji wao eneo la Pwani.

Lakini Jumatano iliyopita wabunge 25 na waziri msaidizi wa usalama, Bw Hussein Dado, wakiandamana na Bw Joho eneo la Garsen kupigia debe Mpango wa Maridhiano (BBI), walimuidhinisha Bw Joho kama kinara na msemaji wao atakayeunganisha Pwani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw Joho alisema wakati umefika Wapwani pia wasikizwe na maeneo mengine ya Kenya na kufanya misimamo yao wenyewe ya kisiasa.

“Wakati umefika kufanya uamuzi wetu kisiasa. Tumekuwa tukitumiwa na watu kwa manufaa yao; wakati wa kuwa wafuasi wa watu wengine umepita,” akasisitiza.

Alisema matumaini yake kwamba Kiongozi wa ODM Raila Odinga ataunga mkono mgombeaji urais kutoka Pwanii, kwani eneo hilo limemuunga mkono kwa miaka mingi.

“Kuna wale wanadai ati tunataka kiti cha naibu waziri mkuu, hayo si kweli kwa sababu tunalenga kiti cha urais,” alisema.Bw Joho alisema watajaribu mahojiano na wapinzani wao Pwani ili wawarudishe upande wao na wasonge pamoja nao kwa madhumuni ya kuunganisha eneo zima.

Matokeo ya uchaguzi mdogo Kwale yalivyowapa maadui wa Joho sauti

Na MOHAMED AHMED

SIASA za uchaguzi mdogo wa Msambweni, Kwale uliofanyika mwezi uliopita, zilikuwa zimechukuliwa kama kipimo cha umaarufu na ufuasi miongoni mwa viongozi wa Pwani.

Kati ya viongozi hao ni pamoja na Gavana Hassan Joho na baadhi ya wabunge ambao zamani walikuwa maswahiba wa Bw Joho lakini baadaye wakamtoroka.

Wabunge hao wanaongozwa na Bi Aisha Jumwa (Malindi), Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Mohammed Ali (Nyali) na Khatib Mwashetani wa Lunga Lunga.

Wabunge hao walikuwa wameshikana pia na kusukumwa na aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar ambaye ni mpinzani mkubwa wa Bw Joho.

Katika uchaguzi huo, wapinzani hao walikuwa wanamuunga mkono Feisal Bader ambaye alinyakua kiti hicho dhidi ya Bw Omar Boga ambaye alikuwa anaungwa mkono na Bw Joho.

Kuanzia kumalizika kwa uchaguzi huo, moto wa kisiasa ulianza rasmi kati ya Bw Joho na viongozi hao wenzake wa Pwani. Mzozo huo wa kisiasa baina ya pande hizo mbili pia umelenga kumuondolea Bw Joho sifa za kuwa kiongozi ama “Sultan” wa Pwani kama anavyojiita.

Sasa, wabunge hao wamezamia kwa nguvu mpya, kuendeleza ‘injili’ yao ya kutaka kuwepo kwa chama cha Pwani huku baadhi yao wakimpendekeza Gavana Salim Mvurya wa Kwale kuwa ndiye anayestahili kuwa kiongozi wa Pwani.

“Sisi hatukuogopi. Wewe kama unataka siasa za kujipiga kifua na majivuno basi tunakwambia tuko tayari. Tutapambana na wewe. Kama ulisema huu ndio mwaka utakaoongoza Pwani basi sisi tuko tayari kupambana,” akasema Bi Jumwa wiki jana kufuatia kauli ya Gavana Joho kuwa chama cha ODM kitaanza rasmi kampeni zake mwaka huu.Aidha, wabunge hao wakiongozwa na Bw Baya walisema nembo na rangi za chama wanachotaka kusajili ziko tayari.

Chama hicho kipya, wabunge hao walisema, kinalenga kuendeleza umoja wa Pwani na kujitoa kwenye utawala wa ODM ambapo Bw Joho ndiye naibu kiongozi.

Chama hicho kulingana nao pia kitaungana na vuguvugu la Hustler Nation ambalo linaongozwa na Naibu Rais William Ruto.Wabunge hao walitoa matamshi hayo yote baada ya Bw Joho kutoa taarifa ya akiikashifu mipango yao ya kuunda chama kipya cha Pwani akisema kuwa tayari kuna vyama vya kutosha Pwani.

Badala yake, Bw Joho alidai kuwa viongozi hao wanapanga mipango hiyo ili kumridhisha Dkt Ruto ambaye ndiye kiongozi wao wa mipango hiyo.Mnamo Alhamisi alipozuru Kaunti ya Tana River, Bw Joho kwa mara nyingine aliwafokea wabunge hao na kusema kuwa umoja huo wa Pwani haufai kuelemea kwa kiongozi ambaye wanamtaka wao.

“Msiambiwe tu kushikana kwa sababu ya mtu fulani. Kama ni kushikana, tushikane kwa sababu yetu wenyewe. Mimi nataka kubadilisha hayo mawazo ya kufuata watu wengine. Safari hii sisi tusikubali kuwa wafuasi, ni lazima sisi pia tufuatwe,” akasema Bw Joho.

Alisema kuwa kusimama kwa Pwani na Bw Raila Odinga ni kwa matarajio kuwa ataunga ukanda huo siku za usoni. Bw Joho alisema ukanda wa Pwani unapaswa kulenga kuwa na kiongozi atakayewakilisha eneo hilo katika mjadala wa kitaifa na si kuendelea kuwakilishwa kila mwaka.

“Sisi tutafanya mashauriano na watu wetu.  Hatuwezi kuendelea kufuata kila siku. Tunataka kuwa tunakaa kwenye meza na kuwa na sauti na si kila siku sisi tuwe ndio ‘menu’. Haiwezi kuwa kila hesabu zikipigwa sisi hatumo. Sisi pia tuna uwezo,” akasema Bw Joho.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa za Pwani, Prof Hassan Mwakimako viongozi hao wote wamekuwa na tabia ya ubinafsi na kwa muda sasa wanaangalia maslahi yao kuliko yale ya Pwani.

Katika mahojiano, Prof Mwakimako alisema kuwa umoja wa Pwani utasimama iwapo wanasiasa watakuwa na nia safi na wakazi na si kupitia vyama.

“Sioni kama wanasiasa hawa wana nia ya ukweli kuhusiana na umoja wa Pwani. Kama ni umoja si lazima pawepo chama kipya ama tuendelee kukaa kwenye vyama vinavyoongozwa na wengine. Nia ikiwa safi basi hapo ndipo watakapofaulu,” akasema.

Ukiwa umesalia mwaka mmoja hadi kufikia uchaguzi mkuu ujao, itaangaliwa ni vipi ukanda huo utakavyoenda kuhusiana na siasa za 2022 kwani kwa muda eneo hilo limekuwa likiongozwa na wanasiasa wakuu kwa sababu ya mgawanyiko na kutoshikana kwa viongozi kama ilivyo sasa.

Viongozi hao wakuu wameendelea kunufaika na kukosekana kwa umoja wa Pwani ambayo huajawa na kiongozi wa kuiendesha na kuwa na sauti moja kama jamii.

Shahbal aonekana kufaidika na siasa za kumrithi Joho

Na MOHAMED AHMED

SIASA za urithi wa kiti cha Gavana wa Mombasa Hassan Joho zimeonekana kuchukua mkondo tofauti ambao unaonekana kumfaidi mfanyabiashara Suleiman Shahbal ambaye anawinda kiti hicho mwaka 2022.?

Kufikia sasa, kiti hicho kimevutia wagombeaji kadha wakiongozwa na Bw Shahbal pamoja na mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir ambao ndio wameonekana kuwa washindani wa juu zaidi.

Wawili hao wote wanatarajia kupata kuidhinishwa na Bw Joho wakati uchaguzi huo utakuwa unakaribia mnamo 2022.? Licha ya Bw Joho kuonyesha dalili kuwa atamuunga mkono Bw Nassir, watu wake wa karibu ambao wamehusika katika mipango yake ya siasa wameonekana kuelemea upande wa Bw Shahbal, hatua ambayo inaibua masuali mengi kuliko majibu.

Miongoni mwa watu hao wa karibu wa Bw Joho ni washauri wa kisiasa wa gavana huyo akiwemo Rashid Bedzimba ambaye alikuwa mbunge wa Kisauni na aliyekuwa mshauri wa Bw Joho, Idriss Abdurahman ambaye sasa ni mshauri wa masuala ya usalama katika afisi ya gavana.

Bw Bedzimba ambaye ana ushawishi wa kutosha katika eneo bunge la Kisauni alipanga mkutano na viongozi wa kampeni zake na kuwakutanisha na Bw Shahbal.

Hatua hiyo ni baada ya kubainika kuwa Bw Abdurahman naye ndiye aliyechukua uongozi wa mipango ya kampeni ya Bw Shahbal.? Kwa upande Bw Bedzimba analenga kumkusanyia Bw Shahbal kura za Kisauni kulingana na ufuasi alionao.

Bw Bedzimba amehudumu eneo bunge hilo kwa zaidi ya miaka 15 kama diwani na mbunge.? Hata hivyo, mwaka 2017 alipoteza kiti hicho kwa mbunge wa sasa Ali Mbogo ambaye kwa sasa analenga kiti cha ugavana.

Aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar pia analenga kiti hicho.? Siku za hivi karibuni, ni Bw Shahbal na Bw Nassir ambao ndio wameonekana kuzunguka zaidi kuuza sera zao mapema kwa wananchi.

Akizungumza katika ukumbi wa Sheikh Zayed eneo la Bombolulu baada ya kukutana na wafuasi hao wa Bw Bedzimba, Bw Shahbal alisema kuwa ana matumani kuwa kushikana na Bw Bedzimba kutamuezesha kunyakua kiti hicho cha ugavana.

Alisema pamoja watapigana na changamoto za utovu wa usalama, utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana na ukosefu wa kazi.

“Nataka kumshukuru Bw Bedzimba kwa nafasi hii ya kunikutanisha na majemedari wake. Mimi nawaomba tushikane mkono ili tuhudumie watu wetu wa Kisauni na Mombasa kwa jumla tukiwa pamoja,” akasema Bw Shahbal.

Bw Bedzimba kwa upande wake alisema kuwa ameaumua kumuunga mkoni Bw Shahbal kwa sababu miongoni mwa wale wote ambao wanataka kuwania kiti hicho yeye yupo mbele.

Alimtaja Bw Shahbal kuwa kiongozi mwenye maono na mwenye azma ya kuhudumia wakazi wa Mombasa kwa hali na mali..? ? ? “Mimi madhali alikuja akaniomba anataka kukutana na nyinyi nikasema tumpe nafasi. Kwa sababu hata tukiangalia kwa wote wale ambao wanataka kiti hicho Bw Shahbal yupo mbele yao tayari,” akasema Bw Bedzimba.

Hayo yalijiri huku mbunge wa Mvita Bw Nassir akionekana kuondeleza siasa zake katika maeneo bunge ya Kisauni, Nyali na Changamwe.? ? ? Bw Nassir amekuwa akifanya mikutano na kujipigia debe ili apate nafasi hiyo baada ya kumaliza hatamu yake kama mbunge wa Mvita.

Aidha, mbunge wa Kisauni Ali Mbogo naye ameonekana kushikilia siasa za mashinani ambapo amekuwa akiendesha kampeni zake za kiti cha ugavana.

Ikiwa imesalia zaidi ya mwaka mmoja, wandani wa masuala ya siasa wanatazama iwapo wale ambao wameanza mapema siasa zao watatoboa hadi mwisho wa ushindani huo wa mwaka 2022.

Hii pia ni kwa sababu inatarajiwa kuwa kutaibuka wawaniaji wengine katika kumezea mate kiti hicho.? ? Ikisubiriwa hilo, kwa sasa viongozi waliopo wamepata wasaa wa kujipigia debe na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kupata kiti hicho ifikapo mwaka wa uchaguzi.

Corona yasimamisha ‘Reggae’ Pwani

Na MOHAMED AHMED

KIVUMBI cha kisiasa kilichoanza kushika kasi katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Msambweni kimeanza kufifia kufuatia agizo la serikali kusitisha mikutano ya kisiasa.

Rais Uhuru Kenyatta alitoa agizo hilo wiki jana na kuelekeza wanasiasa nchini kusitisha mikutano ya hadhara kwa siku 60 ili kupunguza maambukizi ya virusi vya corona.

Tayari, mgombeaji wa kiti cha ODM, Omar Boga ametangaza kuwa ameambukizwa corona na yuko karantini.Rais Kenyatta alisema kuwa, wanasiasa wataruhusiwa kufanya mikutano katika kumbi ambazo zitaruhusu watu wachache pekee.

Agizo hilo, hivyo basi limefifisha ubabe wa kisiasa uliokuwa unatazamiwa kujitokeza kati ya Naibu Rais William Ruto na mpinzani wake kinara wa ODM Raila Odinga.

Wawili hao walitarajiwa kuongoza kampeni katika eneo bunge hilo ili kuwapigia debe wawaniaji wanaowaunga mkono kwenye uchaguzi huo ambao utafanyika mnamo Disemba 15.

Bw Odinga anampigia debe Omar Boga ambaye ndiye anapeperusha bendera ya chama cha ODM huku Bw Ruto naye akiegemea upande wa Feisal Bader ambaye anawania kiti hicho kama mgombeaji huru.Tayari, washirika wa wawili hao walikuwa wameanza kampeni za kuwapigia debe wawaniaji wao.

Upande wa Bw Ruto unaongozwa na waliokuwa maseneta Johnson Muthama (Machakos), Hassan Omar (Mombasa) na Boni Khalwale wa Kakamega.Kundi hilo limekuwa likiendeleza siasa eneo hilo kwa muda wa wiki mbili mfululizo sasa.

Wanasiasa wa ODM wakiongozwa na katibu wa chama Edwin Sifuna pia walikuwa wamepigga kambi eneo hilo.Kufuatia agizo hilo, pande zote mbili zimetangaza kusitisha siasa zake za mikutano ya hadhara.

Bw Ruto amesema atafanya hilo hadi pale ataeleza wafuasi wake tofauti. “Nimeamua kusitisha mikutano mpaka baadaye. Mikutano ambayo ilikuwa nimepanga katika kaunti tofauti pia nimesitisha,” akasema Bw Ruto kwenye mtandao wake wa Twitter.ODM nao walisema kuwa watafuata agizo la serikali kama lilivyotangazwa na Rais Kenyatta.

“Leo tumechangisha pesa kwa ajili ya kampeni zetu za maeneo bunge ya Msambweni, Wundanyi/Mbale, Kisumu Kaskazini na Dabaso kwa ajili ya uchaguzi wa Disemba 15. Katibu wetu Edwin Sifuna ametangaza kuwa kampeni zetu zitafanywa chini ya kanuni mpya ambazo zimetangazwa,” ilisema taarifa ya ODM.

Kampeni hizo zimeanza kuchukua mkondo mpya huku wale wanaongoza kampeni wakionekana kufuata agizo la serikali la kufanya mikutano kwenye kumbi.

Hali hiyo tayari imeondoa mihemko ya kisiasa ambayo huletwa na mikutano ya siasa inayozua hisia tofauti.Kwa sasa, itasubiriwa kuonekana ni vipi siasa hizo zitaendelea hadi siku ya kura huku ikiwa wazi kuwa wale wanaowania watapata wakati mgumu kuuza sera zao.

Wengine wanaowania kiti hicho ni pamoja na wale wa vyama huru, Bi Sharlet Mariam Akinyi, Mansury Kumaka, Charles Bilali, Shee Abdulrahman (Wiper), Ali Hassan Mwakulonda (Party of Economic Democracy), Marere Wamwachai (National Vision Party) and Khamis Mwakaonje (United Green Movement).

Gavana wa Mombasa, Hassan Joho na mwenzake wa Kwale, Salim Mvurya pia walikuwa wameahidi kuonyeshana kivumbi. Bw Joho anamuunga Bw Boga naye Mvurya anampigia debe Bw Bader.

Tayari, uhasama wa kisiasa ulikuwa umeanza kujitokeza kati ya magavana hao wawili kuhusiana na uchaguzi huo mdogo. ? Bw Mvurya alikuwa amemuonya Bw Joho na kusema kuwa hatakubali kaunti yake ya Kwale itumike kama ‘kiwanja cha vita’ akimaanisha siasa za ubabe ambazo Bw Joho ametambulika nazo.

Kwa sasa, itasalia kutazamwa namna viongozi hao watakavyomenyana kisiasa kwenye uchaguzi huo mdogo ambao wengi wamesema kampeni zake zimekosa makali kufuatia kusitishwa kwa mikutano ya hadhara.

Vuguvugu la Pwani latishia Raila

Na MOHAMED AHMED

KINARA wa ODM Raila Odinga ana kila sababu ya kuwa na wasiwasi kufuatia kuanzishwa kwa vuguvugu la mageuzi eneo la Pwani baada ya baadhi ya viongozi kutishia kuunda chama kipya.

Vuguvugu hilo la mageuzi ambalo limekuwa na ming’ong’ono ya chini kwa chini kwa muda lilipata fursa ya kutoa kucha zake baada ya baadhi ya wabunge wa Pwani kueleza kutoridhishwa kwao na baadhi ya mambo yanayoendeshwa na chama cha ODM.

Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya na mwenzake wa Malindi Aisha Jumwa sasa wameonekana kuwa viongozi wa gurudumu hilo la mageuzi ambalo linalenga uchaguzi wa 2022.

Wawili hao hivi majuzi waliongozana na wenzao jijini Nairobi kumkashifu Bw Odinga kwa kupigia upato mpango mpya wa ugavi wa mapato ambao utaumiza kaunti zote za Pwani kwa kuzipokonya fedha za maendeleo.

Wabunge hao wengine waliokuwa kwenye mkutano huo ni pamoja na Mohammed Ali (Nyali), Michael Kingi (Magarini), Sharif Ali (Lamu East), Andrew Mwadime (Mwatate), Khatib Mwashetani (Lunga Lunga), Jones Mlolwa (Voi) Paul Katana (Kaloleni) na Benjamin Tayari (Kinango).

Kwa jumla, kaunti hizo za Pwani zinatazamiwa kupoteza takriban Sh1 bilioni iwapo mswada huo utapitishwa. Hata hivyo wiki hii Bw Odinga alionekana kubadilisha msimamo huo na kupinga mswada huo wa fedha.

Hata hivyo, mpango wa kuanzishwa kwa vuguvugu hilo Jamvi la Siasa limegundua kuwa limeletwa na msururu wa matukio ambayo viongozi, wasomi na wakazi kwa jumla kuona kuwa kwa muda sasa kanda ya Pwani limekuwa likipitia shida kuntu mikononi mwa chama cha ODM ambacho kimekiunga mkono kwa muda.

Kabla ya mzozo wa masuala ya fedha, Bw Baya alikuwa ameeka wazi lalama kuhusiana na ODM kutowapa nafasi za kamati wabunge wa Pwani ambazo zilipatikana hivi majuzi baada ya wabunge wa Jubilee kuondolewa.

Lalama hizo zilifuatwa zile za baadhi ya wabunge kusemekana kufungwa mdomo na uongozi wa vyama na kutoweza kuunga mkono mswada wa mbunge wa Nyali Mohammed Ali wa kumuondoa waziri wa uchukuzi James Macharia.

Kufuatia hayo, wabunge hao wameeleza haja ya kuwepo kwa chama cha Pwani ambacho kitakuwa kinaipa sauti eneo la Pwani na kuhusika kwake katika siasa za 2022.

Sasa, wabunge hao wameanza kutoa mwito kwa baadhi ya magavana wa Pwani na kuwataka wawaunge mkono kwenye msukumo huo.Wiki hii, Bi Jumw alitoa mwito kwa Gavana wa Kilifi Amason Kingi na kumtaka ajiunge naoi li kuwekeza kwenye chama cha Pwani.

“Gavana Kingi toa shaka, toa hofu na uungane nasi. Safari ya kuunganisha Wapwani imeng’oa nanga. Sisi viongozi wa Pwani na wakazi tumejipanga na hakuna kurudi nyuma,” Bi Jumwa alisema katika mkutano wa hivi majuzi uliofanyika eneo bunge lake la Malindi.

Siku moja baadaye, Bw Baya naye akamtembelea Gavana wa Kwale Salim Mvurya ambapo waliongea kuhusiana na suala hilo la ugavi wa pes ana vugu vugu hilo la mageuzi.

Baada ya mkutano huo katika afisi za Bw Mvurya ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani (JKP), gavana huyo alisema kuwa iwapo Pwani itaungana basi kutakuwa na urahisi wa kuendesha ajenda zao katika siku za usoni.

“Tulikubaliana kuwa ni lazima tuungane sote ili tuhusishe kila mmoja katika safari hii ya mageuzi ya Pwani,” akasema Bw Baya.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa za Pwani Profesa Hassan Mwakimako viongozi hao wa Pwani wamepata fursa ya kuongea yale ambayo wameogopa kusema kwa muda sasa kwa sababu ya vizuizi vinavyowekwa na uongozi wa chama tofauti ambavyo wapo ndani yake.

Alisema kuwa ni bayana kuwa viongozi hao pamoja na wakazi wamejiona kutengwa na kutosikika kwa sababu ya kukosekana kwa umoja wao kupitia chama.

“Ni wazi kuwa hata magavana walikuwa na nia hiyo hapo awali lakini wakanyamaza. Wabunge hao wameonekana kupata nafasi ya kueleza mawazo ya wengi ya wakazi wa Pwani,” akasema Profesa Mwakimako.

Aliongeza kuwa iwapo viongozi hao watashikana kweli basi watakuwa na nafasi ya kubwa zaidi ya kusikika kisiasa katika mwaka wa 2022.Hata hivyo, azma hiyo ya baadhi ya viongozi hao bado haijaleta pamoja viongozi wote kwani kuna wale ambao wanalemea upande wa Bw Odinga.

Miongoni mw ani mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir ambaye ni rafiki wa karibu wa Gavana Hassan Joho na ambao mara nyingi huwa na usemi sawia kwenye masuala ya siasa.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa maendeleo eneo la Tudor wiki hii, Bw Nassir aliwashutumu viongozi ambao wametishia kutoka chama cha Bw Odinga na kuwataja wao kutokuwa wanachama thabiti wa chama hicho cha ODM. “Viongozi hawa hawajawahi kuwa waaminifu wa chama cha ODM.

Baadhi yao hata hawapo kwenye orodha ya wanachama wa ODM, hivyo basi sielewi ni kwa nini wanaendelea kutaja ODM,” akasema Bw Nassir.

Kwengineko, mwenyekiti wa Ngumu Tupu Hassan Chitembe ambalo ni vugu vugu linalomuunga mkono Bw Odinga alisema kuwa viongozi hao wanaotishia chama cha ODM hawana nguvu zozote za kisiasa za kumtishia kiongozi huyo.

Bw Chitembe ambaye ni mwanasiasa mkongwe wa Pwani alisema kuwa viongozi hao wameinuliwa kisiasa na Bw Odinga hivyo basi ni lazima wampee heshima yake.

“Pwani haitaki vyama vipya. Hao wanasiasa wanaopiga kelele kutaka vyama vipya ni kwa sababu wamekosa mwelekeo. Sisi watu wa Kwale tutasimama na Bw Odinga maana tunamtambua yeye kama kiongozi wetu,” akasema Bw Chitembe.

Kajembe apumzishwa kwa kanuni za corona

Na MOHAMED AHMED

ALIYEKUWA mbunge wa Changamwe, Ramadhan Seif Kajembe alizikwa jana katika maziara ya Kwa Shee eneo la Jomvu katika hafla ambayo ilitamatisha safari ya mkongwe huyo wa siasa.

Mazishi hayo yalifanywa kwa msingi wa sheria za kudhibiti uenezaji virusi vya corona, kwa usimamizi wa maafisa wa afya waliobeba mwili hadi kaburini.Kwa msingi huu, mazishi yake yaliyohudhuriwa na watu wachache yalitofautiana na maisha yake ya kisiasa ambapo alikuwa akizingirwa na watu wakati mwingi.

Bw Kajembe ni miongoni mwa viongozi wa Pwani waliohudumu kwa miaka mingi zaidi, akiwa na miaka 30 uongozini.Ndani ya miaka hiyo, Bw Kajembe aliyefariki Ijumaa akiwa na miaka 76 alihudumu kama mbunge wa eneo la Changamwe kwa miaka 15 na miaka mengine 15 akahudumu kama diwani wa eneo la Mikindani.

“Kila uchaguzi ukija mimi nilikuwa nikienda kuwaaga wenzagu ambao walikuwa miongoni mwa wabunge 21 kutoka Pwani kwa maana kati yao ni watano ama sita ndio walikuwa wanapata fursa ya kurudishwa mamlakani na mimi nilikuwa miongoni mwao,” akasema Bw Kajembe katika mahojiano ya mwaka jana katika runinga.

Bw Kajembe alianza siasa kama kijana katika chama cha Kanu mwaka 1960 kabla kuingia kwenye nafasi ya udiwani wa Mikindani aliyoishikilia kwa miaka 15.

Kuanzia mwaka wa 1997, Bw Kajembe alishinda kiti cha ubunge kupitia tiketi hiyo ya KANU na kushinda tena katika uchaguzi wa 2002 na 2007 kupitia tiketi ya chama cha NARC na cha ODM mtawalia.

“Uwezo wake wa kuelewana na watu ndio ulimuezesha kuweza kupewa nafasi kwa muda mrefu. Tulikuwa na yeye bungeni na mimi nilipoondoka yeye bado akaendelea kwenye nafasi hiyo na kuhudumia watu wake,” akasema aliyekuwa mbunge wa Likoni Rashid Shakombo.

Bw Kajembe alijisifia kuwa miongoni mwa viongozi walionzisha chama cha ODM wakiongozwa na Raila Odinga.Kwa upande wa maendeleo, alikuwa miongoni mwa viongozi ambao walipigania kugawanywa kwa eneo bunge la Changamwe na kupelekea kuzaliwa kwa eneo bunge la Jomvu.

Alijitaja pia kupigania kuzaliwa kwa kata ndogo za Kipevu na Airport ili kupeleka huduma karibu na wananchi.Aidha, upande wa elimu Bw Kajembe alijivunia kuanzisha ujenzi wa shule tatu za upili ikiwemo shule ya upili ya Kajembe, shule ya upili ya wasichana ya Jomvu na shule ya upili ya Miritini.

Bw Kajembe ambaye pia alikuwa mwanachama wa wafanyabiashara alipigania haki za wafanyabiashara na vijana kwa kuwasaidia kwa mahitaji mbalimbali.

Mwaka 2013, Bw Kajembe ambaye pia aliwahi kuhudumu kama naibu waziri wa mazingira alijaribu bahati ya kuwania kiti cha useneta lakini akashindwa na aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar.

Baadaye mwaka 2016 akateuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa mwenyekiti wa bodi ya shirika la huduma za feri (KFS) kwa muda wa miaka mitatu.

Wakati wa uongozi wake huo KFS, Bw Kajembe alisaidia kuzuia mabwenyenye kunyakua ardhi inayomilikiwa na shirika hilo na pia akapokea feri ya Mv Jambo ambayo ni miongoni mwa zile mpya ambazo zilinunuliwa kwa gharama ya Sh2 bilioni.

Kajembe alifariki katika hospitali ya Pandya ambapo alikuwa amelazwa. Kifo chake kilitokea wiki chache baada ya kufariki kwa mkewe wa kwanza Aziza ambaye miezi minne baada ya yule wa pili Zaharia.

Jana, miongoni mwa viongozi waliokuwa hapo ni pamoja na mshirikishi wa kanda ya Pwani John Elungata, naibu kamanda wa polisi wa Mombasa Joseph Chebii, mbunge wa Jomvu Badi Twalib ambaye ameoa mtoto wa marahemu pamoja na kiongozi wa wengi katika bunge la Mombasa Hamisi Mwidani ambaye pia ni jamaa yake marehemu.

Bw Elungata alisoma risala ya rambi rambi za Rais Uhuru Kenyatta ambaye alimtaja Bw Kajembe kuwa kiongozi mwenye maono na anayefaa kuigwa.

Naibu Rais William Ruto kiongozi wa ODM Raila Odinga Gavana wa Mombasa Hassan Joho na Seneta Mohammed Faki pia walitoa rambi rambi zao kwa marehemu na kumtaja kielelezo chema.

Toka ODM tuunde chama chetu, Jumwa amsihi Kingi

CHARLES LWANGA na FARHIYA HUSSEIN

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa amemtaka Gavana wa Kilifi Amason Kingi aunge wito wa wabunge wa Pwani kuuganisha wakazi kwa ajili ya kuunda chama cha siasa kitakachotumika katika uchaguzi wa 2022.

Mbunge huyo ambaye ameasi chama cha ODM anamtaka Bw Kingi aunge wito huo bila hofu, ili Pwani ijikwamue kutoka kwa udhibiti wa kinara wa ODM Raila Odinga.

“Gavana Kingi toa shaka, toa hofu na uungane nasi. Safari ya kuunganisha Wapwani imeng’oa nanga. Sisi viongozi wa Pwani na wakazi tumejipanga na hakuna kurudi nyuma,” alisema wikendi katika mkutano mjini Malindi.

Mwanzoni mwa mwaka wa 2018, Bw Kingi ambaye ndiye mwenyekiti wa chama cha ODM katika kaunti ya Kilifi, aliwakashifu wabunge wa ODM katika mrengo wa ‘Tangatanga’ akisema wao ni wasaliti kwa kuitisha umoja wa Wapwani, huku wakimpigia debe Naibu Rais William Ruto kuwa rais mwaka wa 2022 badala ya kiongozi wa Pwani.

Wabunge wengine ambao wameungana na Bi Jumwa kuuganisha Wapwani kwa nia ya kuunda chama ni Mohammed Ali (Nyali), Michael Kingi (Magarini), Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Sharif Ali (Lamu Mashariki), Andrew Mwadime (Mwatate), Khatib Mwashetani (Lunga Lunga), Jones Mlolwa (Voi), Paul Kahindi (Kaloleni) na Benjamin Taya (Kinango).

Lakini wiki jana, Katibu Mkuu wa Chama cha ODM, Bw Edwin Sifuna alipuuzilia mbali madai ya wabunge hao akisema kuwa wengi wao si wa ODM na wachache waliosalia walifukuzwa chamani au wamekuwa katika mrengo wa ‘Tangatanga.’

Bi Jumwa alisema kuwa viongozi wa Pwani ambao wameanza shughuli ya kuuganisha wakazi na kuunda chama hawana nia ya kumsimamisha mwaniaji wa urais kutoka maeneo mengine ya nchi.

“Nia yetu ni kuwa na gari letu la siasa litakalotupa nguvu bungeni katika miswada kama ile ya ugavi wa rasilimali na uongozi,” alisema.

Hata hivyo, mbunge wa Mvita, Abdulswamad Nassir amewashutumu vikali wenzake wa Pwani wanaotishia kuhama ODM. Akizungumza na Taifa Leo, alimtetea Bw Odinga na kusema wanasiasa hao si waaminifu kwa chama.

‘Watu hawa hawajawahi kuwa waaminifu kwa chama. Baadhi yao hata hawapo kwenye chama cha ODM. Kwa hivyo sielewi ni kwa nini wanaendelea kutaja ODM,’ akasema.

Kulingana na mbunge huyo, viongozi hao wanaopanga kuunda chama kipya, walikuwepo wakati wa mkutano wa ripoti ya BBI na wote wakapata nafasi ya kutoa maoni yao.

Kulingana na baadhi ya viongozi, uamuzi wa Bw Odinga kuunga mkono mswada tata wa ugawaji wa mapato uliwakasirisha viongozi wa Pwani.

Hii ndiyo sababu mojawapo iliyoshinikiza baadhi ya viongozi akiwemo mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya ambaye amekuwa kwenye mstari mbele kuunga mkono uzinduzi wa chama kipya cha siasa kuunganisha Wapwani.

ODONGO: Viongozi wa Pwani hawana nia ya kuungana kisiasa

Na CECIL ODONGO

WITO wa viongozi wa Pwani wa kuunda chama kimoja kufikia 2022 utakuwa kibarua kigumu kwa kuwa ni jambo ambalo huchipuka kila mara wanapohisi wamebaguliwa kwenye masuala ya kitaifa.

Lakini msukumo huo hutokemea eneo hilo linapomezwa na mawimbi ya kisiasa wanapounga mkono vigogo au wawaniaji wa urais kutoka maeneo mengine.

Wiki iliyopita, baadhi ya wabunge wa ODM kutoka Pwani walitishia kung’atuka chamani ifikiapo 2022, baada ya kinara wa ODM Raila Odinga na baadhi ya maseneta kuunga mfumo mpya wa Ugavi wa Mapato.

Mfumo huo ambao bado haujapitishwa na utarejeshwa bungeni kesho kujadiliwa zaidi, unalenga kupunguzia kaunti za Pwani mgao wa fedha za ugatuzi zinazopokea kutoka kwa serikali kuu.

Eneo la Pwani lilikuwa chimbuko la ugatuzi kwa kuwa aliyekuwa kigogo wa siasa za ukanda huo hayati Ronald Ngala, alipendekeza mfumo wa utawala majimbo utumike hata kabla ya Kenya kujinyakulia uhuru 1963.

Hii ndiyo sababu kuu ya viongozi wake kuja pamoja na kuungana kulinda maslahi ya raia wao kwa kupinga kupunguzwa kwa mgao kutoka serikali kuu.

Inashangaza kwamba viongozi wa Pwani hurudia suala la uundaji wa chama chao kila mara ilhali uchaguzi unapofika wanaunga mkono na kuwania viti kupitia vyama vingine.

Tabia hii ilianza zamani kwani waliokuwa vigogo wa siasa za Pwani Marehemu Sharif Nassir na Karisa Maitha walielekeza kura za Wapwani kwa uongozi wa Kanu na Narc.

Baada ya kifo cha Bw Maitha mnamo 2004, waziri wa sasa wa Utalii Najib Balala alikuwa mwenge wa Pwani katika chama cha ODM kutoka 2007-2012 kabla Gavana wa Mombasa Hassan Joho kuchukua usukani waziri huyo alipohamia Jubilee mnamo 2013.

Kwa kifupi, chama cha ODM kina umaarufu Pwani huku baadhi ya vyama vilivyoundwa kushughulikia maslahi ya Pwani na kuwaunganisha vikikosa kushabikiwa na raia.

Vyama kama Shirikisho, Kaddu-Asili, USPPK, DPK na NLP viliundwa kwa kusudi la kuwaleta Wapwani pamoja lakini vikakosa kushamiri.

Hii ndiyo maana wabunge Aisha Jumwa (Malindi) na Owen Baya wa Kilifi kati ya wengine huenda wasitimize ndoto ya Pwani kuwa na chama kimoja hata kama mfumo mpya wa ugavi wa mapato utapitishwa bungeniKinachotia doa zaidi kwenye mpango wao ni kimya cha Bw Joho na Gavana Amason Kingi wa Kilifi kuhusu suala hilo.

Hii ni kwa kuwa wawili hao ndio wanaonekana kuwa wasemaji wa Wapwani kwa sasa.Ingawa ni haki ya kidemokrasia kwa kila kiongozi kuzungumzia suala analohisi linabagua jamii yake, bado viongozi wa Pwani wana kibarua kigumu kuzima migawanyiko na kuungana chini ya chama kimoja.

Kilicho wazi ni kuwa siasa kuhusumfumo wa ugavi wa mapato utakaopunguza mgao kwa kaunti za Pwani hazitoshi kuwashawishi wakazi kutema ODM na kuungana chini ya chama kimoja.

KURUNZI YA PWANI: Shirika lawataka wanaojiuza kimwili waanze kuuza sabuni

Na MISHI GONGO

SHIRIKA la kijamii la Nkoko Iju Africa linapanga kuwafaidi makahaba 4,000 mjini Mombasa kwa kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kujipatia mkate wao wa kila siku badala ya kujiuza kimwili.

Mradi huo unalenga kunufaisha asilimia 90 ya makahaba waliyopoteza ajira kufuatia kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19.

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa katika uzinduzi wa mradi huo Jumatano, mkurugenzi mtendaji katika shirika hilo Bi Maryland Laini alisema kufungwa kwa vilabu vya burudani na mikahawa ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona kumewaathiri makahaba pakubwa.

“Makahaba hupata wateja wao katika sehemu hizi, lakini tangu kuwekwa kwa marufuku ya kutembea baada ya saa moja usiku na kufungwa kwa sehemu hizo, uchumi wa kundi hilo umepata pigo kubwa,” akasema.

Mradi uliozinduliwa unalenga kuwapa makahaba hao ujuzi wa kutengeneza sabuni na maziwa kutokana na maharagwe ya soya; bidhaa ambazo watauza ili kujipatia riziki.

Bi Laini alisema mradi huo unawalenga makahaba na wanawake walioachiwa majukumu ya kulea watoto wao.

Aliongezea kuwa kuwekwa marufuku ya kuingia na kutoka katika baadhi ya kaunti pia kunawazuia makahaba kukutana na wateja wao.

Alisema kufuatia kudorora kwa biashara hiyo makahaba wamelazimika kutoza wateja wao Sh20 kuwapa huduma kinyume na hapo awali ambapo waliwatoza Sh50 hadi 10,000 kutegemea na umri, sehemu waliyokutana na mambo mengine.

Mkurugenzi mtendaji katika shirika la Nkoko Inju Africa (kushoto) Bi Maryland Laini akiwa na baadhi ya makahaba walionufaika. Picha/ Mishi Gongo

Mbali na kuwapa ujuzi huo, pia watawaelimisha kuhusu haki zao za kikatiba.

“Tumeona makahaba wakinyanyaswa na wateja na hata maafisa wa polisi bila ya wao kuripoti matukio haya kwa kuchelea kutiwa mbaroni, katika mradi huu tutawafunza kuhusiana na haki zao,” akasema.

Alisema katika eneo la Nyali pekee kuna makahaba 2,900 huku Kisauni ikiwa na makahaba takriban 2,000.

“Kufuatia kufungwa kwa shule, idadi ya makahaba inaongezeka. Watoto wanapopata mimba za mapema huingilia ukahaba ili kujimudu wao na watoto wao,” akasema.

Mmoja wa wanachama katika shirika hilo Bi Elizabeth Mbuli aliiomba serikali kuwajumuisha makahaba katika mradi wa chakula unaolenga familia zisizojiweza.

Aidha aliwahimiza wanawake kuunda vyama ili kujiendeleza kiuchumi.

Bi Mbodze Katana ambaye ni mmoja wa waliofaidika na mradi huo alisema tangu janga la Covid-19 makahaba wengi wanashindwa kumudu mahitaji yao.

Alisema kuna baadhi ambao wanahitaji dawa za kupunguza makali ya Ukimwi lakini kufuatia hali ngumu ya maisha, wanashindwa kununua dawa hizo.

“Tunahofia kufa na makali ya njaa. Tunaomba serikali kutupa msaada wa chakula,” akasema.

Awali makahaba hao waliomba serikali kuwaorodhesha katika kundi la watu wanaotoa huduma muhimu.

KURUNZI YA PWANI: Wakazi wahimizwa wajiandae hali ya kawaida ikitarajiwa

Na MISHI GONGO

ENEO la Pwani limeanza mikakati ya kujitayarisha kurejea kwa hali ya kawaida kama alivyodokeza Rais Uhuru Kenyatta wiki iliyopita.

Akizungumza na wanahabari Jumatatu, mshirikishi wa usalama katika eneo la Pwani Bw John Elungata alisema ni wakati mwafaka wa sekta mbalimbali kuanza matayarisho ya kurejea kwa hali ya kawaida siku chache zijazo.

Bw Elungata aliwahimiza wamiliki wa hoteli kuanza kuandaa matayarisho ya kuwakaribisha watalii.

“Wamiliki wa hoteli wamekuwa na muda wa kutosha kurekebisha hoteli zao ili kuanza kupokea wageni pale nchi itakapofunguliwa,” akasema Bw Elungata.

Wiki iliyopita Rais Kenyatta alitangaza kuwa serikali italegeza marufuku ili kufufua uchumi ambao umedorora kutokana na athari hasi za Covid-19.

Rais Kenyatta alieleza kuwa nchi haiwezi kuendelea kujifungia.

Alisema ugonjwa utakuwa nasi kwa muda kabla ya kudhibitiwa vilivyo.

Bw Elungata alisema miongoni mwa matayarisho wanayoweka ni kuchimba visima 15 katika kaunti za Kilifi, Kwale na Mombasa ambazo zina idadi kubwa ya maambukizi ili kuhakikisha kuwa wakazi wanapata maji ya kutosha.

Aidha Bw Elungata alisema vijana 18,000 wataandikwa kuhakikisha kuwa wanachunga wanyamapori.

“Vijana wasipoajiriwa katika shughuli hii, wanyamapori ambao ni kivutio kikuu cha utalii watakuwa katika hatari,” akasema.

Alisema shule zitapanuliwa ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanakuwa katika mazingira mazuri watakaporudi shuleni.

Bw Elungata pia alisema serikali inapanga kujenga daraja katika kivuko cha feri, ambalo litasaidia kupunguza msongamano unaoshuhudiwa kwa sasa.

“Daraja litakuwa na uwezo wa kufunga na kufunguka ili kuwezesha meli kupita, lakini ujenzi wake utachukua muda wa miezi sita ndipo likamilike. Daraja hili litasaidia kudhibiti virusi vya corona kwani litaruhusu wakazi kuekeana nafasi,” akasema.

Hata hivyo Bw Elungata aliwatahadharisha wakazi kuwa zuio na kafyu vikishaondolewa, ni muhimu waendelee kuzingatia masharti yaliyowekwa ili kudhibiti kueneo kwa ugonjwa huo hatari.

“Mikahawa na sehemu za burudani zitafunguliwa lakini tutapaswa kuendelea kuzingatia masharti yaliyowekwa kama kuvaa barakoa ili kujikinga,” akasema.

Aidha alisema magari ya usafiri wa umma yatalazimika kutobeba abiria kupita kiasi.

“Maisha yatageuka; hayatakuwa kama awali. Tutalazimika kuendelea kuvaa barakoa na kuekeana umbali baina ya mtu na mwenzake,” akasema mshirikishi huyo.

Pia alisema barabara zilizoharibika kufuatia mafuriko yanayoendelea kushuhudiwa katika kaunti za Taita Taveta na Tana River zitakarabatiwa.

Aliongezea kuwa vijana wanaosafisha mitaa watapata Sh3,000 kwa siku kutoka kwa serikali.

“Pesa hivi tunatumai kuwa zitawasaidia katika kujiendeleza kiuchumi na pia kusafisha mazingira. Haya yote ni kuhakikisha kuwa uchumi wetu unarudi pale ulipokuwa kabla kuzuka kwa ugonjwa huu,” akasema.

Vyoo vijengwe ufuoni msimu huu wa likizo, wakazi Mombasa wasema

Na DIANA MUTHEU

WAKAZI wa Mombasa wameomba vyoo vya umma vijengwe na vingine viongezwe katika fuo za bahari hasa msimu huu wa likizo.

Wafanyabiashara katika fuo hizi walilalamika kuwa wageni wanaozuru maeneo hayo wanachafua mazingira kwa kuenda haja kubwa na ndogo kwenye vichaka na mawe yaliyo kwenye ufuo.

Fuo za umma katika kaunti ya Mombasa ni kama vile Mombasa, Nyali na Jomo Kenyatta (Pirates).

Uchunguzi wa Taifa Leo ulionyesha kuwa ufuo wa umma wa Jomo Kenyatta ndio pekee una vyoo na viko mita 100 kutoka kwa bahari.

Akizungumza na Taifa, mwanachama wa kikundi cha waokoaji katika ufuo wa Jomo Kenyatta, Hamis Abdallah alisema kuwa vyoo hivyo ni vichache na haviwezi kukidhi mahitaji ya wageni wanaotembelea ufuo huo.

Kutumia vyoo hivi, mja anapaswa kulipa Sh10. Bw Abdallah aliongeza kuwa watu wenye ulemavu hawawezi kutumia vyoo hivi.

Bilal Yusuf , mwanabiashara katika ufuo wa Nyali alisema kuwa kungekuwa na vyoo vya umma hawangepata changamoto kuokota taka nyingi vikiwemo visodo na vibinda vya watoto.

KURUNZI YA PWANI: Wabunge 4 wasema 2022 Pwani itatoa mgombea urais

Na CHARLES LWANGA na KALUME KAZUNGU

WABUNGE wanne kutoka eneo la Pwani wamesema watahakikisha eneo hilo limesimamisha mgombeaji wa urais atakayekabiliana na vinara wengine katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Wakiongozwa na mbunge wa Ganze, Bw Teddy Mwambire, ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa chama cha ODM kaunti ya Kilifi, walisema eneo hilo litaungana na kukubaliana mbombeaji atakayemenyana na wagombeaji wengine wa urais nchini.

Wabunge hao walisema hayo walipohudhuria mazishi ya jamaa ya mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya, eneo la Matsangoni.

Walisema wakati umefika ambapo eneo hilo ambalo lina watu zaidi ya milioni mbili kulingana na sensa ya 2009 kusimamisha mgombeaji wao wa urais.

“Tuko tayari kuunganisha eneo hili kabla ya kukabiliana na wagombeaji wengine kupata urais,” alisema na kuongeza, “hapo ndio tutaungana na maeneo mengine ili kuunda serikali baada ya uchaguzi.”

Baadhi ya wabunge kutoka pwani waliohudhuria mazishi hayo ni mbunge wa Kilifi Kusini, Ken Chonga na mwenzake wa Changamwe, Bw Omar Mwinyi.

Bw Chonga alisema wakati huu maeneo mengine ya Kenya yatashawishiwa ma Wapwani katika siasa za 2022 ili kuunda serikali.

Mbunge huyo pia alisema wanafanya kila wawezalo kuhakikisha eneo hilo halitagawanyika wakati wa uchaguzi mkuu sawa na inavyoshuhudiwa kila wakati kunapokuwa na uchaguzi.

“Tumekuwa tukigawanywa kwa miaka mingi na saa hizi tumeanza kampeni wa kuunganisha Wapwani kuwa kitu kimoja bila kuzingatia dini au kabila ili tuongee kwa saunti moja katika uchaguzi ujao,” alisema.

Kugawanyika

Mbunge wa Changamwe alisema wakazi wamekuwa wakigawanyika kwa msingi wa dini na kufanya eneo hilo kutengwa kimaendeleo na kusalia kuwa maskini kwa miaka mingi.

“Wanatumia utengano wetu kama unyonge ya kutufanya kusalia watumwa wa kupigia debe wagombeaji wao,” alisema.

Aliongeza: “ Tunafaa tuungane kufanya mambo makuu.”

Haya yanajiri wakati ambapo Gavana wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi, Bw Amason Kingi wametangaza kuwa watagombea kiti cha urais katika siasa za 2022.

Kwa upande wake, mbunge wa Soi Caleb Kositany ambaye pia alihudhuria mazishi hayo, alimtaka Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake William Ruto pamoja na kinara wa ODM, Raila Odinga waunganishe wananchi hata wakati wanapokabiliana na vita didhi ya ufisadi.

Kwingineko, Gavana wa Lamu, Fahim Twaha ametimiza ahadi yake ya kubandika jina la mpinzani wake wa kisiasa, Issa Timamy kwenye moja ya wodi za wanaume katika hospitali kuu ya King Fahad mjini Lamu. Bw Twaha amechukua hatua hiyo licha ya mpinzani wake kupinga wazo hilo awali.

Katika kile kilichotajwa kuwa kejeli dhidi ya mpinzani wake, ambaye pia alikuwa gavana wa eneo hilo, Bw Twaha alihakikisha ahadi hiyo imetimizwa.

Alikuwa ametangaza mpango huo wakati wa kusherehekea ushindi wake baada ya kesi ya kuupinga iliyowasilishwa na Bw Timamy, kutupiliwa mbali.

Bw Twaha alisema wazo hilo ni dhirisho kwamba hana kinyongo na mtangulizi wake.

“Nataka kuwafahamisha wale ambao tulikuwa tukishindana nao kwamba mimi sina kinyongo nao kwani hayakuwa mashindano ya kivita,” alisema.

KURUNZI YA PWANI: Bunge la Kilifi laidhinisha hoja kufuta vibarua 1,000

Na CHARLES LWANGA

WAFANYAKAZI takriban 1,000 walioajiriwa kama vibarua huenda wakapoteza ajira baada ya Bunge la Kaunti ya Kilifi kuidhinisha hoja ya kuwafuta kazi.

Wafanyakazi hao wako chini ya Bodi ya Kuajiri Wafanyakazi Kaunti (CPSB).

Hatua hiyo imeibua hofu kuu kwa wanaotegemea kazi hizo huku baadhi ya wakazi wakiingia kwa mitandao ya kijamii kuikashifu.

Hoja hiyo ambayo iliwasilishwa na diwani wa Kayafungo, Bw Alphonce Mwayaa, inasimamisha kazi watu wote wanaofanya vibarua chini ya bodi hiyo, isipokuwa wale wanaohudumu hospitalini.

Katika hoja hiyo, Bw Mwayaa analenga kuwafuta wafanyakazi wote waliondikwa na maafisa wakuu wa serikali ya kaunti kufanya kazi za mkataba bila idhini ya bodi ya CPSB.

Akizungumza na Taifa Leo kwa simu, Bw Mwayaa alisema lengo la hoja hiyo ni kuhakikisha kuwa sheria imefuatwa kikamilifu ili kuleta uwazi katika huduma serikalini na jinsi ya kupata ajira.

“Tunataka kuhakikisha kuwa mambo ya kuandikwa kazi kwa sababu mtu ni shangazi au mjomba au ana uhusiano wa kijamii au urafiki na maafisa wakuu serikalini inatupwa katika kaburi la sahau,” alisema.

Aliongeza,“Wakishafutwa, wakazi watawasilisha maombi ya kazi upya na kuajiriwa kulingana na stakabadhi zao.”

Wakati huo huo, Bw Mwayaa alisema hoja hiyo pia inanuia kupunguza gharama inayotumika kulipa mishahara kwani huenda baadhi ya fedha hutumika kulipa wafanyakazi hewa.

“Kwa mfano, katika idara ya maji pekee imekuwa na takriban wafanyakazi 478 wanaofanya vibarua na kusababisha gharama ya mishahara ya Sh17 milioni kwa kipindi cha miezi minne pekee,” alisema.

Lakini baadhi ya madiwani ambao hawakutaka kutajwa walidai kuwa hoja hiyo ilitokana na msukumo wa kisiasa baina ya madiwani ambao wanataka kuwaajiri ‘watu wao’.

“Baadhi ya madiwani wamekuwa wakitaka kuwaajiri watu wao lakini wamekuwa wakishindwa kwa sababu nafasi hizo zimemilikiwa na wafanyakazi waliowekwa na wapinzani wao katika serikali iliyopita,” alisema.

Wakati huo huo, diwani wa Sokoni, Gilbert Peru, ambaye alikosa kuhudhuria kikao hicho cha bunge, alimkashifu diwani mwenzake kwa kuwasilisha hoja hiyo akisema kuwa anawagandamiza vijana wanaopambana kupata ajira.

“Wakati sisi viongozi vijana tunalalamika kuwa fedha zinazotengewa idara ya vijana ni kidogo na zinafaa kuongezwa, wewe unajishughulisha na kuwasilisha hoja wa kuhatarisha vijana. Nia yako kwa masuala ya vijana si nzuri hata kidogo,” alisema.

Kutatua mzozo

Hata hivyo, Karani wa Kaunti hiyo, Bw Anorld Mkare, aliambia Taifa Leo kuwa watahakikisha wametatua mzozo huo kwa njia ya haki na utaratibu unaostahili ili kuhakikisha hakuna yeyote atakayedhulumiwa.

Mnamo Jumanne kaunti ya Mombasa pia ilionekana kwenda kinyume na matarajio ya Gavana Ali Hassan Joho, ilipoidhinisha hoja ya kumtimua waziri wake wa barabara na miundomsingi, Tawfiq Balala, wakidai hajamakinika na pia utendaji kazi duni
Gavana Joho aliomba utulivu miongoni mwa wakazi na kuhimiza ripoti kuhusiana na hatua hiyo iwe ya haki bila mapendeleo yoyote.

KURUNZI YA PWANI: Waganga 20 sasa waililia serikali iwatambue

Na CHARLES LWANGA

KUNDI la waganga 20 eneo la Magarini, Kaunti ya Kilifi wameitaka serikali itambue kazi yao ya kutibu wagonjwa ili waepuke kushambuliwa na umma kwa madai ya kufanya uchawi.

Kundi hilo linaloongozwa na Bi Dahabu Ngumbao lilisema linataka kutambuliwa na serikali na kupewa leseni itakayowawezesha kuendelea na ‘kazi yao nzuri’ ya kutibu wagonjwa bila haya na uwoga wowote.

“Hii ni kwa sababu kizazi cha sasa ambacho hakitambui mila na utamaduni hutusingizia kuwa tunafanya uchawi, kisha wanauwa wazee hao bila sababu yoyote,” alisema na kuongeza kuwa “jambo hili limeweka maisha yetu hatarini kwani wazee huuliwa kila uchao kwa madai ya uchawi.”

Wakizungumza na wanahabari katika eneo la kimatamaduni huko Gongoni, alisema hakuna haja yoyote ya serikali kupiga vita waganga na akasisitiza kuwa wanatelekeleza kazi yao kulingana na utamaduni.

“Tunatibu watu kutumia tiba za kiasili baada ya kurithi na kusomea tiba za kiasili msituni,” alisema na kuongeza “pia tunatibu mapepo yanayomwingia mtoto mchanga kichwani wakati wa kuzaliwa ambazo humfanya ajae maji kichwa.” Bi Ngumbao ambaye pamoja na wenzake walizungukazunguka nyungu iliyowekwa tiba za kiasili huku wakiimba, alisema amefanya kazi hiyo kwa miaka 55 baada ya kurithi uganga kutoka kwa nyanya zake.

Vilevile, alisema leseni itapatia umma imani kufanya waondolewe lawama itakayopunguza visa vya mauwaji ya wazee kwa madai ya kufanya uchawi.

“Tunataka serikali ituruhusu tubebane na vifaa na tiba zetu hadi hospitali ili tusaidie wauguzi wa kisanyansi na utaalamu wetu wa kitamaduni,” alisema.

Mguzi huyo alisema wanaujuzi wa kutibu baadhi ya magonjwa sugu wanayosumbuwa jamii kwa bei nafuu kama vile Sh1,000 pekee.

Isitoshe, Bi Ngumbao alizidi kusema kuwa wanaotafuta hudumu zao kwa sasa ni wazee ambao ni waaminifu kwa mila na utamaduni ya jamii ya Mijikenda.

Kulingana na idara ya polisi, takriban wazee 400 wasiokuwa na hatia haswa mababu na wajane wameuwawa na umma kwa kipindi cha miaka mitano zilizopita kwa madai ya uchawi katika Kaunti ya Kilifi pekee.

KURUNZI YA PWANI: Kampeni kuhusu mimba za mapema yazinduliwa

Na FADHILI FREDRICK

NAIBU Gavana wa Kwale Bi Fatuma Achani ameanzisha kampeni itayojumuisha wanawake katika juhudi za kupambana na mimba za mapema kwa wasichana wa shule.

Bi Achani alisema kampeni hiyo itahusisha wanawake katika vitengo vyote vya vijiji 77 kupitia programu ya uhamasishaji.

Mpango huo unafuatia idadi kubwa ya wasichana wadogo iliyoripotiwa kupachikwa mimba kote nchini kama ilivyoonekana wakati wa mtihani wa KCPE na mtihani unaoendelea wa KCSE ambapo wasichana kadhaa walifanya mtihani wao hospitalini na hata wengine kukosa mtihani huo.

Kaunti ya Kwale pekee ilikuwa na wanafunzi wawili wa kike waliofanya mtihani wao wa KCPE hospitalini baada ya kujifungua.

Bi Achani alisema mimba za mapema kwa vijana zimekuwa tishio kubwa kwa elimu ya wasichana nchini, akisistiza umuhimu wa kukabiliana na changamoto hiyo.

“Tunalenga kujumuika pamoja katika Kampeni ambayo itahusisha kuwawezesha wazazi na wasichana kiuchumi,” akasema.

Kampeni hiyo imepigwa jeki na baadhi ya mashirika ya kijamii ambayo pia yana malengo kuhamasisha wasichana kuepukana na mimba za mapema.

Takwimu zilizotolewa na shirika la Moving the Goalpost (MTG) zinaonyesha asilimia 40 ya wasichana wadogo kaunti hiyo wako na ujauzito.

Mkurugenzi wa MTG, Bi Dorcus Amakobe, amesema ukosefu wa habari juu ya afya ya uzazi ndio moja wapo inayosababisha mimba na ndoa za mapema na hata vijana wengi hawajui mabadiliko yao ya kimwili.

Bi Amakobe anasema katika juhudi za kuelimisha vijana juu ya mimba za mapema, shirika hilo limesajili wasichana 800 chini ya mpango wa uwezeshaji kwa njia ya michezo na kwamba lengo lao ni kuwasajili wasichana wengi zaidi.

“Tunalenga kuandikisha wasichana wengi iwezekanavyo ili waweze kufaidika na mpango huu kwa kuwa unawapa fursa ya kujifunza kuhusu afya ya uzazi wao,” akasema.

Pia aliongeza kuwa wako na mpango wa kutoa huduma kwa wasichana kwenye vituo vya afya kwa ushauri juu ya Ukimwi na magonjwa ya zinaa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Kwale Welfare and Education Association (KWEA) Bi Sabina Saiti amewahimiza wazazi kuwaongoza watoto wao vizuri kuwa na malengo katika maisha na kutoa msaada katika kufikia malengo yao.

Alieleza kuwa wazazi wanamchango mkubwa katika kuwalea watoto wao na hawapashwi kulaumu walimu kwa kushindwa kuwakuza watoto wao vyema.

“Idadi ya mimba za mapema inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko kile tunachosikia. Ukweli ni kwamba watoto wanafanya mahusiano ya ngono wakati wakiwa nyumbani kama wazazi hawawafuatilii hasa wakati wa likizo, “akasema.

Alibainisha kuwa ikiwa wazazi hawana makini na watoto wao, kuna uwezekano wa matukio mengi ya ujauzito kuripotiwa Januari kwani watoto wengi huenda wakajihusisha na ngono wakati wa likizo ndefu ya Disemba.

Bi Saiti aliwahimiza wazazi kuhakikisha watoto wao wanafanya kazi wakati wa likizo na kuwaepusha kujihusisha na watu wenye malengo ya kuwaharibia maisha yao.

Pia aliwaonya wazazi kutokuwa chanzo cha watoto kuiga tabia mbaya Kutokana na matendo yao, Kwani familia nyingi hufanya watoto wao kuwa kitega uchumi.

“Kuna wazazi wanaohusika na wanaokosa maadili na hivyo basi kusababisha watoto wao kupotaka kimaadili,” akasema akiongeza kuwa watoto wengine hata wanalazimika kufanya ukahaba ili kuhudumia mahitaji yao ya familia.

PWANI: Siasa za viuno zilivyotenganisha Jumwa na Mboko

NA MOHAMED AHMED

MGAWANYIKO mkubwa umezuka kati ya wanawake wawili maarufu kisiasa katika eneo la Pwani, Aisha Jumwa na Mishi Mboko kuhusu ni nani wa kumuunga mkono kuwa rais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Huku Bi Mboko, ambaye ni Mbunge wa Likoni akisisitiza kuwa bado ni mfuasi sugu wa ODM, Bi Jumwa (Malindi) amejitoza wazi na kutangaza kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto. Na wanasiasa hao sasa wanapapurana hadharani kwa kutumia silaha kali waliojaliwa nayo: Semi na mafumbo.

Wawili hao wana ujuzi wa kutumia kinaya na kejeli tele katika maneno yanayosisimua wafuasi wao na kuwakwaza wapinzani wao. Hii ni kati ya sababu urafiki wao ulishamiri, hususan, wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Kunawiri kwa usuhuba wao kulijitokeza zaidi katika mtindo wao wa kumuandama kwa cheche za maneno yeyote aliyejaribu kudunisha chama chao cha ODM.

Na mwathiriwa mkuu wa kejeli za wabunge hawa machachari ambao wanasifika eneo la Pwani kama “masimba jike” ni aliyekuwa seneta wa Mombasa, Hassan Omar ambaye walimwangushia makombora huku, kwa weledi mkubwa, wakikejeli umbo lake.

Lakini sasa, urafiki wa viongozi hao wawili umeonekana kusambaratishwa na maneno hayo hayo ya mafumbo ambayo wamebobea kwayo.

Kwa sasa, siasa za mafumbo ya viuno baina ya wawili hao zinaonekana kunogoa na kuzua mwanya mkubwa baina yao.

“Sisi hatuna biashara ya kuuza viuno katika cha ODM. Huku tunaauza sera na maendeleo. Kuna wale ambao wanauza viuno na tunawambia wanajua maskani ya kuuzwa viono ni wapi,” akasema Bi Mboko wiki iliyopita katika sherehe moja eneo la Changamwe.

Matamshi ya Bi Mboko yalitiliwa mkazo na rafikite wake aliyechukuwa nafasi yake ya awali ya kiti cha mwakilishi wa wanawake Bi Aisha Hussein.

Bi Hussein alisema: “Msimamo wetu si wa viuno, sisi misimamo yetu ni wa kazi. Kama wataka kuendesha kiuno, peleka biashara hiyo mbele. Sisi ndio masimba wa kike,” akasema Bi Hussein.

Matamshi ya wawili hao yalikuwa yanaelekezwa wazi kwa hasimu wao wa sasa, Bi Jumwa ambaye wakati wa ziara ya mwisho ya Naibu Rais William Ruto katika kanda ya Pwani mwezi jana, alichemsha wakazi Kwale na Mombasa aliposema anaitambua zaidi kazi ya kiuno.

KURUNZI YA PWANI: EACC yachunguza ubaguzi katika ugavi wa basari Kibarani

NA SAMUEL BAYA

Tume ya kupambana na ufisadi (EACC) eneo la Pwani imeanzisha uchunguzi kuhusu ugawaji duni wa basari katika kamati ya basari ya wadi ya Kibarani, Kaunti ya Kilifi.

Kamati hiyo imekumbwa na madai ya ubaguzi katika ugawaji wa basari na tayari hazina ya basari katika kaunti ya Kilifi ilikuwa imeisimamisha kazi kamati hiyo mwezi uliopita.

Kumekuwa na madai kutoka kwa wakazi kuwa bodi hiyo iko na upendeleo katika kugawa fedha za masomo.

Ingawa lengo la basari ni kuwasaidia wanafunzi werevu kutoka jamii maskini kuendelea na masomo, kamati hiyo imelaumiwa kwa kuwanufaisha washirika wa karibu wa wanakamati.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo afisini mwake, mwenyekiti wa hazina hiyo Bw Mulewa Katana alisema waliarifiwa na EACC kwamba tume ilikuwa ikichunguza kamati hiyo hivyo ilikuwa ni makosa kuivunja. Na Samuel Baya

“Ni kweli tulikuwa tumesimamisha bodi hiyo baada ya lalama nyingi kutoka kwa wananchi. Wakazi wengi walikuwa wakilalama kuhusu jinsi wasimamizi wa kamati hiyo wamekuwa wakijitengea fedha nyingi kwa washirika wao na jamii zao.

Baada ya sisi kama hazina kuisimamisha kamati hiyo, mmoja wao aliamua kulipeleka suala hilo kwa tume ya kukabiliana na ufisadi. Tume hiyo baadaye ilituandikia barua kutuarifu kwamba wanafanya uchunguzi,” akasema Bw Mulewa.

Alisema kupitia kwa ushauri wa EACC hazina hiyo ilibatili uamuzi wake ili kutoa fursa kwa tume hiyo kuendelea na uchunguzi wake.

Bw Mulewa alisema hayo huku katibu wa kaunti hiyo Bw Arnold Mkare akiwaonya maafisa wasimamizi wa wadi kwamba watachukuliwa hatua kali endapo itabainika wanahusika na ubadhirifu wa fedha hizo za basari.

“Fedha za basari ni za umma na wala sio pesa za mtu binafsi. Tumepata habari kwamba kuna baadhi ya wasimamizi wa wadi wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya kamati za basari za wadi kufanya ufisadi na upendeleo. Hili ni onyo kwamba hatutavumilia tena, ” akaonya Bw Mkare.

Hazina hiyo ya basari hutenga kiasi cha Sh350 millioni kila mwaka ili kugharamia masomo kwa wanafunzi ambao hawana uwezo wa kulipa karo.

Katika wadi 35 za kaunti hiyo, kila wadi hupokea kiasi cha Sh10 millioni kila mwaka kwa ajili ya kuwapa karo wanafunzi.

Tahadhari ya ufujaji na ugawaji mbaya wa fedha hizo ulianza mwezi uliopita pale mwakilishi wa wadi hiyo Bw John Mwamutsi alipomuandikia barua hazina hiyo baada ya madai kuibuka.

Katika barua hiyo ya Oktoba 26, Bw Mwamutsi aliandika akiomba kamati hiyo isimamishwe haraka na uchunguzi uanzishwe.

“Kumeibuka madai mabaya sana ya usambzaji wa fedha za kamati ya basari ya Kibarani. Tafadhali kama hazina, tunaomba muisimamishwe kamati hiyo na kuruhusu uchunguzi ufanyike,” ikasema barau hiyo ambayo Taifa Leo ilifanikiwa kupata nakala yake.

Naye Bw Mulewa katika barua yake ya Oktoba 27 alitangaza kusimamishwa kwa kamati hiyo hadi pale uchunguzi ufanyike na kupata tatizo ambalo linakumba kamati hiyo.

“Kupitia narua ambayo tulipata kutoka kwa mwakilishi wa wadi ya Kibarani ninakufahamisha kwamba kamati yako imesimamishwa kuendelea na shughuli zozote hadi uchunguzi kamili utakapofanyika.

Kwa sasa ninamruhusu mwakilsihi wa wadiu kuanzisha juhudi za kuweka kamati ya muda ili kuhakikisha kwamba kumebuniwa kamati ya muda ndani ya wiki mbili zijazo,” akasema Bw Mulewa.

Hata hivyo mnamo Oktoba 29, hazina hiyo ilipata barua kutoka kwa tume ya kupambana na ufisadi ikiitaka hazina hiyo iachane na mpango wa kusimamisha kamati hiyo.

‘Tume ya kupambana na ufisadi inachunguza utumiaji mbaya wa fedha za umma katika kamati ya basari ya Kibarani kama jambo hilo lilivyoripotiwa kwetu.

Tayari jambo hili lilikuwa limewasilishwa kwako awali kulingana na barua ambayo tuko nayo. Tuko na habari kwamba mwenyekiti wa sasa wa kamati hiyo alirekodi taarifa na afisi yetu na uchuguzi unaendelea.

Haukufaa kuivunja kamati hiyo kwa sababu uchunguzi unaendelea,” ikasema sehemu ya barua hiyo ya EACC.

Naye Bw Mulewa katika barua ya Oktoba 31, aliandikia tume hiyo ya EACC akigeuza barua ya awali ya kuivunja kamati hiyo.

“Tumeona yale ambayo mulisema katika barua yenu na yote tumeyasikia na kwa sababu hiyo hazina ya fedha za basari ya Kilifi imebatilisha uamuzi wa kuivunja kamati hiyo ya Kibarani ili kuruhusu uchunguzi uendelee,” ikasema sehemu ya barua hiyo.

Tangu ianzishwe, hazina hiyo imesaidia jumla ya wanafunzi 220,416 kuendelea na masomo yao. Idadi kubwa kati ya hawa ni wale ambao wanasomea katika shule za sekondari ambao kufikia sasa ni 157,758.

KURUNZI YA PWANI: Huenda wanaovamia ardhi si maskwota

Na SAMUEL BAYA

MASWALI yameanza kuibuka kuhusu watu wanaovamia mashamba wakidai kuwa maskwota katika eneo la Pwani.

Kuna maskwota zaidi ya 10,000 ambao aidha wamevamia mashamba na kuyauza na kisha kuondoka au wanaishi katika ardhi hizo zenye mizozo katika kaunti ya Kilifi.

Baada ya kuvamia na kuharibu makao katika eneo la Kikambala wiki iliyopita, sasa polisi wanasema kuna maeneo mengine yanayolengwa ambayo yatavamiwa karibuni.

Katika mahojiano na Taifa Leo kijiji cha Mwendo wa Panya aliposimamia harakati za kuwatimua maskwota, kamanda mkuu wa polisi Kilifi, Bw Fredrick Ochieng alisema kuwa bado wanatarajia kuzuru maeneo mengine na kuwafurusha maskwota ambao wanakalia ardhi hizo.

“Huu ni mwanzo tu, bado kuna maeneo mengi ambayo watu wamevamia na kujenga makazi. Hayo pia tutayaondoa kwa sababu ardhi hizo ziko na wamiliki halali,” akasema Bw Ochieng.

Tangazo hilo la mkuu wa usalama limeleta bayana utata mwingi ambao unakabili usimamizi wa ardhi katika kaunti hiyo na Pwani kwa jumla.

Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuongezeka kwa visa vya watu kuvamia mashamba ya kibinfasi kisha kujidai kuwa ni maskwota na kuanza kupambana na wamiliki halali mahakamani.

Kwa mfano uvamizi katika kijiji cha Mwendo wa Panya ulifanyika baada ya maskwota hao kupoteza kesi waliyokuwa wamewasilisha mahakamani wakidai kuwa ardhi hiyo ilikuwa ni ya kwao.

Baada ya mvutano huo wa miaka sita, mmiliki wa shamba hilo alishinda kesi na kupata kibali cha mahakama kuwaondoa.

Ardhi hiyo ni ya ekari 27 kulingana na hati za mahakama na kwa sasa kuna familia zaidi ya 800 ambazo zinaishi katika eneo hilo.

Hatua ya kuwafurusha ilisababisha uharibifu wa mali ya mamilioni ya fedha ihuku wakazi wakibaki nje bila makao.

Kulingana na Prof Halimu Shauri, tatizo la maskwota bandia limesababishwa na uchumi ambapo watu wengi huamua kuvamia mashamba na kujidai kuyamiliki.

Kisha baada ya kuvamia kwa muda mfupi huamua kuwauzia watu wengine na kuelekea eneo lingine lenye ardhi ya wazi na kuvamia tena.

“Wakazi wengi hutumia ardhi kama njia ya kujikimu. Wengi wao ni wavivu na huwa hawataki kujishughulisha na kazi za kufanya ili kupata riziki,” alisema Prof Shauri.

Aliongeza, “Mara nyingine wanapovamia mashamba haya, huwa wanatarajia kwamba serikali itawasaidia kwa kuwapatia hati za kumiliki ardhi hiyo.Kisha baadaye huuza na kuondoka na hili ni tatizo kubwa.”

Prof Shauri alisema kuwa wengi wa maskwota wanafahamu vyema historia ya mashamba katika eneo la Pwani na mara nyingi huamua kutumia sababu hizo kusema kuwa ardhi ni ya mababu zao na kuivamia.

“Hii shida ya umiliki wa mashamba ni tatizo kubwa sio tu katika eneo la Pwani ila katika taifa lote.Tunaona yale ambayo yanaendelea katika msitu wa Mau, eneo la Mlima Elgon. Changamoto ni nyingi sana na zinasabishwa na sera mbaya za ardhi ambazo zimeshinda kusimamia tatizo hili,” aliongeza.

Prof Shauri alisisitiza umuhimu wa sheria ambazo zitatua suala la ardhi nchini.

Mshirikishi wa Kenya National Land Alliance, Bw Naghib Shamsan alisema kuwa tume ya kusimamia ardhi nchini imeshindwa kufanya kazi yake ndiyo maana uvamizi wa ardhi unaendelea.

kutafuta makazi na hivyo basi kuvamia mashamba ambayo wanaona yako karibu na kuanza kujenga makazi.

“Uvamizi wa mashamba katika Kikambala na kaunti ya Kilifi kwa ujumla kumewatia hofu wawekezaji wengi kuwekeza katika maeneo hayo ya Kikambala.

Maskwota hawa wale ambao wako Kikambala, utawapata ni wale walikuwa Kwa Bulo, Mwembe Legeza na hata katika maeneo ya Kilifi,” akasema Bw Shamsan.

Afisa huyo alisema kuwa suluhisho ni kwa serikali kutoa fedha ili kuwanunulia mashamba maskwota halali na kisha waweke kwa mtandao wa serikali kuzima maskwota laghai.

“Mchezo wanaofanya maskwota hawa ni kwenda katika ardhi ya mwenyewe na kuingia dani, kisha baadaye waanze kutafuta usaidizi wa mahakama.

Baadaye mahakama huwapatia kibali cha kuendelea kuishi katika ardhi hiyo lakini wanapofurushwa, mamilioni ya fedha kupotea. Hili ni tatizo kubwa,” akasema Bw afisa huyo.

Bw Shamsan alisema kuwa tume ya NLC imefeli katika kutoa hamasisho kwa wakenya jinsi ya kufanya kuhusiana na masuala ya ardhi.

“Nilifanya utafiti wa wale ambao walikuwa wamevamia ardhi ya wenyewe katika eneo la Junda kaunti ya Mombasa na kugundua baadhi yao walikuwa wametoka katika kaunti za Kilifi, Kwale nna maeneo mengine ya eneo la Mikindani.

Tulipata kufahamu hiyo kwa sababu ya data ambayo tulichukua mwaka wa 2009,” akasema Bw Shamsan.

Aliongeza kwamba endapo NLC haitawajibika basi asilimia 100 ya uvamizi wa mashamba utaendelea.

Kaunti ya Kilifi imeshuhudia visa vingi vya uvamizi wa mashamba kuanzia katika eneo la Kibarani, Mavueni,na Kikambala.

Akiwahutubia viongozi wa mashinani katika hoteli ya Wild Waters jijini Mombasa Jumamosi iliyopita, Gavana wa Kilifi Bw Amason Kingi alisema kuwa tatizo la ardhi na uskwota ni baadhi ya dhuluma za kihistoria Wapwani wamepitia.

Viongozi hao walitarajiwa kuyaweka bayana wakati kamati ya mwafaka kati ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta ingefika Pwani. Kamati hiyo hata hivyo haikuweza kufika.

 

Pwani yaanza mikakati ya kujiimarisha kiuchumi

Na SAMUEL BAYA

KAUNTI zote sita za Pwani zimeanza mikakati ya kujiimarisha kiuchumi.

Kaunti hizo kupitia kwa mwavuli wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani(JKP) zitaandaa kongamano la kilimo biashara, lengo kamili likiwa ni jinsi ya kufaidika na rasilmali zilizopo Pwani.

Kongamano hilo linalojulikana kama JABEIC litafanyika katika hoteli maarufu ya Ocean Beach iliyoko mjini Malindi.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo jana, afisa mkuu wa JKP, Bw Emanuel Nzai alisema kuwa kongamano hilo litakuwa na mada ‘kubadilisha stori’ likimaanisha kubadilisha habari kuhusu kudorora kwa uchumi wa Pwani.

“Jambo muhimu katika kongamano hilo ni kuhakikisha kwamba kaunti zote sita zinakuja pamoja na kushirikiana kuboresha maendeleo. Ile habari ya kila siku kwamba tumedorora kimaendeleo inafaa kukoma,” akasema Bw Nzai.

“Kongamano hilo pia litatumika kama matayarisho ya kongamano kubwa la uchumi wa bahari ambalo litafanyika katika jiji la Nairobi mwezi ujao.

Kongamano hilo la linafanyika ili kuonyesha jinsi eneo la Pwani limejaaliwa kuwa na raslmali nyingi kama vile bahari na pia katika nyanja za kilimo na uwekezaji.

“Tuko na bahari na ardhi kubwa kwa ajili ya kilimo. Tukitumia rasilmali hizi vizuri, ikiwemo madini, tunaweza kupiga hatua kubwa sana kimaisha na maendeleo kwa ujumla,” akasema Bw Nzai.

Aidha afisa huyo alisema tani 150,000 hadi 300,000 za samaki zinaweza kupatikana eneo hilo na hivyo kusaidia pakubwa kama kitega uchumi .

“Samaki zinaweza kuletea Pwani pato la kati ya Sh21 billioni na Sh42 billioni.Endapo lengo hili linaweza kufikiwa, basi tunaweza kuendeleza eneo hili kupitia kwa faida za uchumi unaotokana na bahari,” akasema Bw Nzai.

Awali juhudi za kujaribu kujikwamua kwa Pwani zilitatizwa na sababu mbalimbali ikiwemo kukithiri kwa umaskini na uhaba wa elimu, kutengwa kwa kimaeneo na hali duni ya usalama.

“Hata hivyo baada ya kuanzishwa kwa serikali za kaunti na JKP kuzinduliwa, kumekuwa na maendeleo kadha, ingawa sio mengi ambayo tunaweza kujivunia,” akasema afisa huyo.

Aidha kongamano hilo la Pwani litatekelezwa kupitia kwa awamu ya kwanza ya ustawi wa maendeleo eneo la Pwani ambayo imeorodheshwa katika kitengo cha uimarishaji wa chakula na usalama 2018-2030.

Ripoti hiyo ilitayarishwa na JKP pamoja na shirika la chakula ulimwenguni(FAO).

“Pia kongamano hili limelenga kutekeleza ajenda nne za Rais Uhuru Kenyatta ambazo baadhi yazo zimewekwa katika ustawi wa maendeleo ya taifa ya Ruwaza ya 2030. Baadhi ya ajenda hizo ni chakula cha kutosha na kuhakikisha kwamba hakuna Mkenya atakufa njaa kwa kukosa chakula,” akasema.

Eneo la Pwani kulingana na ripoti ya kiuchumi iliyotayarishwa na JKP, ina uwezo wa kuwa eneo kubwa la biashara kati ya 2015-2045.

“Ni soko kubwa la kibiashara ambalo linaweza kugeuza uchumi wa taifa hili. Eneo ambalo wawekezaji wanaweza kuja na kuwekeza,” sehemu ya ripoti hiyo ya JKP ilieleza.

Iliongeza, “Tuko na maeneo ya kuvutia ya kitalii pamoja na mbuga za wanyama za Tsavo. Tuna maeneo ambayo yanaweza kutumika kama viwanda. Ardhi ya kufanyia haya yote inapatikana Pwani.”

Serikali ya kitaifa imeanzisha mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa miradi mikuu na muhimu kwa maisha ya wakazi wa Pwani inatekelezwa.

Majuzi naibu Rais, Bw William Ruto alizindua ujenzi wa daraja ambao utagharimu Sh2.5 billioni katika eneo la Baricho, kaunti ya Kilifi. Miradi mingine inayotekelezwa ni pamoja na upanuaji wa bandari ya Mombasa na vile vile mpango wa kujenga bandari ya wazi katika eneo la Dongo Kundu.

Ni miradi hiyo ambayo Bw Nzai alisema ni muhimu kwa serikali za kaunti kuangalia jinsi ambavyo wataitumia kunufaika.

“JKP itatoa mwongozo kamili wa jinsi kaunti zote sita za Lamu, Kilifi, Kwale, Tana river, Mombasa na Taita Taveta zitatumia fursa ya miradi hii kumairisha maisha ya wakazi wa Pwani,” akasema.

KURUNZI YA PWANI: Mahangaiko ya wakazi kuhusu kivuko cha Mtongwe

Na HAMISI NGOWA

TANGU kutokea mkasa wa kuzama kwa feri katika kivuko cha Mtongwe yapata miaka 24 sasa, huduma za uchukuzi wa Feri katika kivuko hicho zimekuwa zikiendelea lakini si za kutegemewa na wakazi jinsi ilivyokuwa kabla ya mkasa huo.

Katika siku za hivi karibuni,wakuu wa Shirika la Huduma za Feri (KFS), wamekuwa wakijaribu kutuliza joto la wakazi wa eneo hilo wanaliolilia kurejeshwa kwa huduma za feri kwa kutoa hakikisho la kurejeshwa kwa huduma hizo ambazo hutolewa kwa kipindi kifupi kabla ya kukatizwa.

Kukosekana kwa huduma za feri katika kivuko hicho, kumesambaratisha kwa kiasi kikubwa maisha ya wakazi wa eneo hilo ambao wengi wao kwa sasa wanaishi katika maisha ya uchochole.

Unapotembelea baadhi ya mitaa katika eneo hilo, taswira unayokumbana nayo ni nyumba zilizogeuka kuwa magofu na zingine kuwa mahame baada ya watu waliokuwa wamepangisha nyumba hizo kuhamia Likoni ili kuwa karibu na feri.

Watu wengi wamehamia eneo la Likoni ili kuepuka gharama ya nauli wanayotumia kila siku wanapotumia usafiri wa matatu na tuktuk wanapoelekea na kurudi kutoka kazini.

Kando na usafiri, hali ya maisha katika eneo hilo inasemekena kuwa ngumu kutokana na kusambaratika kwa biashara za baadhi ya wakazi ambazo wamekuwa wakizitegemea ili kuwakimu.

Hali hiyo imeonekana kuwa kero kubwa kwa wakazi wanaoishi katika eneo hilo ambao baadhi yao sasa wametishia kuelekea mahakamani ili kushtaki Shirika la huduma za Kenya feri ili liweze kushinikizwa kurejesha huduma hiyo.

Mzee Musa Bandari alisema Shirika hilo linafaa kuwafidia wakazi wa Mtongwe kutokana na kukosekana kwa huduma za feri licha ya kwamba wao ni walipa kodi kama wakenya wengine.

Alisema inasikitisha kuona wakazi wa eneo hilo wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma za feri hata baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuigiza feri moja iweze kuhudumu katika kivuko hicho.

“Wakati Rais Uhuru Kenyatta alipozindua upya huduma za feri ya Mtongwe, alituhakikishia kwamba huduma hiyo haitasitishwa tena, lakini sasa twashangaa kuona mara huduma inapatikana mara nyengine tunamaliza miezi kadhaa bila ya kupata,” akasema.

Alisema kuharibika kwa baadhi ya feri katika kivuko cha Likoni haifai kutumiwa kuwa sababu ya kukosekana kwa feri katika kivuko cha Mtongwe akisema wakazi wa Mtongwe wamekuwa bila ya feri hata kabla ya kuharibika kwa feri hizo.

Lakini Bw Ali Sababu mzaliwa na mkazi wa Mtongwe anatofautiana na wazo la wakazi wenzake kutaka kulishtaki Shirika la huduma za feri akisema Shirika hilo linapitia kipindi kigumu baada ya feri mbili kuharibika.

Sasabu ambaye ni mwanachama wa kamati ya watu 20 inayowakilisha wakazi wa eneo hilo katika kufuatilia kinacholemeza kurejeshwa kwa huduma za feri eneo hilo, alielezea jinsi yeye pamoja na wenzake walivyojionea uhalisia wa mambo kuhusu tatizo hilo la feri.

“Najua tunapata shida kwa feri kuwa Likoni lakini kwa wakati huu ni vyema tuvumilie hadi wakati kutakuwa na feri za kutosha kwa sababu iwapo feri moja italetwa Mtongwe kutakuwa na msongamano mkubwa katika kivuko cha Likoni,’’ akasema.

Alisema wahudumu wa Kenya Ferry hawafai kulaumiwa kwa tatizo la feri katika kivuko cha Mtongwe jinsi baadhi ya wakazi wa eneo hilo wanavyofikiria.

Alisisitiza kwamba iko haja ya usimamizi wa Shirika hilo kupewa nafasi hadi wakati ambapo kutakuwa na feri za kutosha kabla ya kupelekwa kwa feri katika kivuko cha Mtongwe.

KURUNZI YA PWANI: Tana River kujiunga na Jumuiya ya Kaunti za Pwani

Na STEPHEN ODUOR

KAUNTI ya Tana River itajiunga na Jumuiya ya Pwani ili kufaidi maendeleo kwa pamoja.

Gavana Dhadho Godhana alisema wikendi mjini Hola kwamba Tana River iko na nafasi nzuri ya kunawiri kiuchumi chini ya muungano wa Jumuiya ya Pwani.

“Baada ya kushauriana na viongozi wa Taifa na wenzangu katika kaunti, tulikubaliana kuwa ni vyema tukijiunga na Jumuiya ya Pwani,ambapo tutaweza afikia malengo yetu ya kiuchumi, ” alisema.

Gavana huyo alisema kuwa kaunti ya Tana River ina maazimio sawa ya kimaendeleo kama ya kaunti nyingine za Pwani.

Zaidi, alisema kuwa majimbo ya Pwani yalikuwa mfano mwema wa kuiga, kwani uchumi wao ulikuwa ukinawiri kwa kasi, jambo ambalo Tana River lilifaa kuiga kutoka kwao.

“Iwapo jimbo hili linataka kuafikia malengo yake kiuchumi, lazima ichukue hatua ya kuiga kutoka kwa wenzetu, na sisi tumekubaliana kuwa hakuna wengine wa kuiga ila wenzetu wa Pwani,” alisema.

Bw Godhana pia aliashiria kuwa iwapo kura ya maoni ingejumlisha kaunti ya Tana River pamoja na zile za Lamu na Kilifi, hakuwa na tatizo, kwani hata naye angegombea kiti cha kanda hiyo.

Alisema kuwa jimbo la Tana River halikuwa na lolote kuiga kutoka katika majimbo ya Kaskazini, kwani wote walikuwa na tatizo moja, na mbali na hilo, majimbo hayo yangeinyima jimbo hilo haki na usawa.

“Iwapo tutakuwa katika kata moja na Garissa na Wajir, hakuna cha kuiga kule kiuchumi, sote tu wagonjwa ila hapa tuna raslimali ambazo kwa hakika zitatumiwa vibaya, na pia hapatakuwa na usawa katika uongozi maana wao ni wengi kutuliko, ” alisema.

Gavana huyo alieleza kuwa Jimbo la Tana River lilikuwa katika hatua ya kujikwamua kutoka katika umasikini, na halitarudi nyuma kwa kujenga uhusiano hafifu.

Hapo awali, gavana Dhadho Godhana alikuwa amepinga hatua na juhudi za kuunganisha majimbo ya Pwani katika kutengeneza Jumuiya ya Pwani, akisema kuwa wazo hilo lilikuwa la kisiasa, na la kuwafaidi viongozi wachache waliokuwa karibu kustaafu.

AISHA JUMWA: Ua la waridi lenye mvuto wa aina yake

Na MOHAMED AHMED

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, amezidi kuibua mijadala kwenye ulingo wa kisiasa baada ya kugeuka kutoka mtetezi mkubwa wa Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, hadi kuanza kuunga mkono azimio la Naibu Rais William Ruto ya urais mwaka wa 2022.

Bi Jumwa amekuwa kwenye mstari wa mbele miongoni mwa wabunge wa Pwani waliochaguliwa kupitia ODM ambao sasa chama hicho kinataka kuwaadhibu kwa ‘usaliti’ kwa kumuunga mkono Bw Ruto ambaye ni hasimu mkubwa wa kisiasa wa Bw Odinga.

Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita, Bi Jumwa ndiye alikuwa mwanamke ngangari ambaye angemshambulia Bw Ruto kwa mtindo wa aina yake hadi Bw Odinga akambandika jina ‘Mekatilili wa Menza’ kuashiria ujasiri wake wa uongozi wa kisiasa.? Zaidi, wengi wanamkumbuka alivyoimba, “Salama Salama Jubilee! Salama Salama! Salama Salama Bw Ruto! Mwendako muende Salama!”

Angeimba Bi Jumwa huku akifuatisha na cheche za maneno za kumkashifu Bw Ruto. Uswahiba wake na Bw Ruto ulifanya mnamo Juni, mbunge huyo akapata jina jipya la ‘Mama Rada’ wakati wa ziara ya Bw Ruto eneo la Malindi kaunti ya Kilifi kwa jinsi alivyogeuka kumkashifu Bw Odinga.

“Sisi tumekuja upande huu wa serikali kwa ajili ya manufaa ya watu wetu hivyo basi siasa za zamani za kutingisha viuno bila manufaa yoyote sisi hatuzitaki tena. Hivi viuno vina kazi yake,” akasema Bi Jumwa na kuendeleza mashambulizi dhidi ya Bw Odinga.

Katika ziara hiyo katika maeneo Kaunti hizo za Pwani Bi Jumwa alionekana kumwita majina mabaya Bw Odinga na kushutumu uongozi wa chama hicho kwa kutaka kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa sababu ya kuungana kwao na Bw Ruto.

Lakini sasa maswali yameibuka kuhusu kama ataendeleza mtindo huu kwa muda mrefu, au hiki ni kivumbi tu ambacho kitageuza mwendo wake kulingana na jinsi upepo wa kisiasa utakavyovuma Pwani katika siku zijazo.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Bi Jumwa alisema hana uhasama na kiongozi wake wa chama.

Alisema kuwa anamheshimu kiongozi huyo na wamekuwa wakizungumza kwa njia ya simu mara kwa mara.

“Raila bado ni kiongozi wa chama changu na nataka kusema kuwa sina uhasama na yeye. Hizi ni propaganda tu lakini tuko imara kwenye chama chetu,” akasema. Hata hivyo, wafuasi wa Bw Odinga eneo hilo wanasema mienendo ya Bi Jumwa haifai kushangaza yeyote ambaye anamfahamu kisiasa.

Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko, ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Bi Jumwa alisema kiongozi huyo atarudi tu chamani.

“Akiona joto limezidi, atarudi kule kule. Na sio yeye pekee bali viongozi wale wengine pia. Lakini kuondoka kwao hata hivyo hakujapunguza lolote,” akasema Bi Mboko.

Miongoni mwa viongozi wengine kutoka Pwani ambao wametangaza kumuunga mkono Bw Ruto ni pamoja na Juma Wario (Senata, Tana River), wabunge Paul Katana (Kaloleni), Ali Mbogo (Kisauni), Mohamed Ali (Nyali) Benjamin Tayari (Kinango), Michael Kingi (Magarini), Ali Wario (Garsen), Jones Mlolwa (Voi), Ali Sheriff (Lamu Mashariki), Stanley Muthama (Lamu Magharibi) Said Hiribae (Galole), Badi Twalib (Jomvu), na Mbunge Mwakilishi wa Kilifi, Getrude Mbeyu.

Hisia kwamba huenda Bi Jumwa bado ana guu moja ndani kikamilifu katika ODM unatokana pia na jinsi anapokashifu chama hicho, yeye huepuka kumshambulia Gavana wa Mombasa Hassan Joho, jinsi wafanyavyo wenzake.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Prof Hassan Mwakimako, Bi Jumwa amekuwa mjanja katika uasi wake dhidi ya ODM kwani anafahamu fika kwamba Bw Joho ana ushawishi zaidi katika eneo la Pwani.

Itakumbukwa kuwa Bi Jumwa anaazimia kuwania ugavana ifikapo 2022.? ? “Amekuwa akiepuka kumuandama Bw Joho kwa sababu siasa za Joho zimekita mizizi katika kanda hii, ukilanganisha na Bw Odinga ambaye ni mwanasiasa wa kitaifa.

Anajua wazi kuwa kuanzisha uhasama na Bw Joho kutaharibu siasa zake za eneo hilo kwani Joho ako na ushawishi wa karibu zaidi Pwani kuliko Bw Odinga,” akasema Prof Mwakimako.

Bw Joho amekuwa miongoni mwa viongozi wenye uwezo wa kushawishi siasa za kaunti nyingi za Pwani ikiwemo Kilifi.? ? Aidha, Prof Mwakimako aliongeza kuwa umakini wa Bi Jumwa unasababishwa na uwezekano wa kugeuka kwa wimbi la kisiasa wakati wanapoelekea mwaka 2022.

“Anajua wazi kuwa sasa bado ni mapema na siasa huenda zikabadilika na kwa sababu Bw Joho anataka kuwania kiti cha urais na hivyo basi ni lazima atambue kuwa huyo ni kiongozi wake wa kanda hiyo,” akasema.