Wanafunzi waliokataa kurudi shuleni wasakwa na machifu

Na Wycliffe Nyaberi

MACHIFU na maafisa wa Nyumba Kumi katika eneo la Nyamagwa, Kaunti ya Kisii, wameanzisha msako wa kuwatafuta wanafunzi ambao bado hawajarejea shuleni.

Kwa kuwa wanafunzi walisalia nyumbani muda mrefu kufuatia mkurupuko wa ugonjwa wa visrusi vya corona, wanafunzi wengi walikoma kudurusu na kujiingiza katika kazi za kujitafutia hela za haraka.

Baadhi ya wavulana walikimbilia kuendesha bodaboda na wasichana wengine wakajitosa kwenye starehe zilizowapelekea kutungwa mimba za mapema.

Hata hivyo, licha ya utundu huo, wazazi kwa ushirikiano na machifu katika eneo la Nyamagwa wameahidi kushirikiana ili wahakikishe hakuna mwanafunzi anayekatiza masomo yake licha ya changamoto zilizowapata. Wakiongozwa na chifu wao Bw Donald Aiko, wazazi hao wameapa kuwatafuta wanafunzi ambao bado hawajaripoti shuleni na kujua sababu zinazowafanya kutoendeleza masomo yao.

Kwa kuwa serikali inajitahidi kuimarisha miundomsingi na kuweka rasilimali ili kufadhili masomo, wazazi hao wanawataka watoto wote wanufaike na mpango huo.

“Tumekuwa tukiomba serikali iweze kufungua shule na imefanya hivyo. Basi mbona tuendelee kuwaweka watoto wetu nje ilhali tumekuwa tukitamani shule zifunguliwe?”Akauliza chifu Aiko.

Kwa wanafunzi waliopachikwa mimba wakiwa nyumbani, chifu huyo amewaomba wazazi kuwatia moyo warejee shuleni hadi watakapokaribia kujifungua.

Isitoshe, onyo kali limetolewa kwa wamiliki wa bodaboda ambao huwapa watoto wavulana pikipiki ili wafanye biashara nazo. Sasa afisa huyo amesema watanasa pikipiki zinazoendeshwa na wanafunzi na wenyewe kuchukuliwa hatua.

Kazi ya uchifu yaepukwa Lamu kutokana na mauaji

KALUME KAZUNGU na MISHI GONGO

WAKAZI wa vijiji vya Kaunti ya Lamu ambavyo vimekuwa vikishuhudia mauaji ya mara kwa mara ya maafisa wa usalama wanaishi kwa hofu tele, kwani sasa hakuna wakazi wanaotaka kujaza nafasi za machifu zilizoachwa wazi.

Kwa muda mrefu, kumekuwa na visa vya mauaji ya machifu, manaibu wao, wanachama wa makundi ya nyumba kumi na polisi katika vijiji vilivyo Tchundwa, Mbwajumwali na Myabogi.

Imefichuka kuwa, wakazi wa Lamu wamesusia kuwasilisha maombi ya kazi za machifu licha ya serikali kutangaza nafasi hizo kuwa wazi kwa kipindi cha miezi saba sasa.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia alikiri kwamba serikali imepata changamoto kubwa kujaza nafasi za machifu tangu chifu na naibu wake kuuawa kinyama eneo hilo mwaka uliopita.

“Tumetangaza nafasi hizi lakini hakuna mtu anayejitokeza kufanya kazi hizo katika maeneo hayo. Mbali na machifu kuogopa kuajiriwa eneo hilo, huenda hata polisi wetu pia wakaanza kughairi kupelekwa kuhudumia maeneo husika,” akasema.

Mnamo Disemba 11, 2019, chifu wa lokesheni ya Mbwajumwali Mohamed Haji Famau, 45 na Naibu wake ambaye ni wa lokesheni ndogo ya Myabogi, Malik Athman Shee, 43 waliuawa wakati watu wawili waliovalia buibui na kufunika nyuso zao kwa ninja walipowavamia ofisini mwao mjini Mbwajumwali na kuwakatakata kwa mapanga kabla ya kutoroka.

Mnamo Juni 8 mwaka huu ambapo afisa wa polisi wa cheo cha konstebo, Bw Rodgers Odhiambo aliuawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga na watu wasiojulikana akiwa mjini Tchundwa, Lamu Mashariki.

Oktoba mwaka uliopita, Konstebo wa Polisi aliyehudumu kwenye kituo hicho hicho cha Tchundwa, Hesbon Okemwa Anunda pia aliuawa kwa kukatwakatwa kwa panga na watu wasiojulikana.

Aprili mwaka huo, Afisa wa Nyumba Kumi ambaye pia alikuwa mfanyikazi wa kujitolea wa Shirika la Kenya Red Cross, Bi Amina Bakari, 30, aliuawa kwa kukatwakatwa kwa panga na watu wasiojulikana wakati akifunga duka lake kijijini Mbwajumwali.

Mnamo Juni, 2016, chifu mkuu wa Mbwajumwali, Mohamed Shee, 50 aliuawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga na watu wasiojulikana wakati akielekea kazini majira ya saa tatu asubuhi.

Bw Macharia alisema matukio hayo yameingiza wakazi wasiwasi. Alisema kufikia sasa serikali imetoa matangazo mara tatu kwenye maeneo husika ya kuwataka wakazi kuwasilisha maombi ili waajiriwe machifu na manaibu wao lakini hakuna hata mmoja aliyejitokeza.

“Wengi wanachukulia kuwa chifu au naibu wa chifu maeneo hayo ni sawa na kujitia kitanzi. Ni jambo la kusikitisha,” akasema Bw Macharia.

Kamishna huyo hata hivyo aliwahimiza wananchi kutoogopa na badala yake kujitokeza kujaza nafasi hizo kwani serikali imefanya mikakati kabambe kuhakikisha usalama wa maafisa wa utawala eneo hilo unadhibitiwa vilivyo.

“Machifu wamekuwa wakiuawa kiholela kwenye maeneo husika. Siku za hivi karibuni wahalifu pia wamewageukia polisi na kuwaua,” akasema Bw Macharia.

Baadhi ya wakazi waliozungumza na Taifa Leo walikiri kuwa katu hawawezi kuchukua kazi hizo za machifu na manaibu wao, ikizingatiwa kuwa maafisa wa utawala eneo hilo wamekuwa wakilengwa na magenge hatari.

Machifu wapewe bunduki – Mbunge

Na Waweru Wairimu

MBUNGE wa Isiolo Kaskazini Hassan Odha anaitaka serikali kuwapa bunduki machifu wanaohudumu katika kaunti za wafugaji ili wajilinde nazo kando na kupambana na wahalifu.

Mbunge huyo alisema machifu na manaibu wao katika kaunti hizo wanahudumu katika mazingira hatari kutokana na hali kwamba silaha nyingi haramu ziko mikononi mwa wahalifu.

Akirejelea kisa cha wiki jana ambapo wahalifu kutoka Laikipia waliteketeza nyumba ya chifu wa Oldonyiro na nyumba zingine katika eneo la Narasha, Bw Odha alisema afisa huyo wa utawala angezuia uhalifu huo kama angekuwa na amejihami kwa bunduki.

 

Chifu kizimbani kwa kuiba mbwa!

JOSEPH WANGUI Na PETER MBURU

CHIFU kutoka eneo la Othaya alishtakiwa katika mahakama moja ya Nyeri Alhamisi, kwa madai kuwa aliiba mbwa wawili wa mhubiri wa Nairobi Thomas Wahome Njuguna, wa kanisa la Helicopter.

Paul Gachiri Wageni, naibu chifu wa Kiandemi alituhumiwa kuiba mbwa hao wa gharama ya Sh300,000 tarehe isiyojulikana, Desemba 2016 katika kijiji cha Kihuri.

Vilevile, alishtakiwa kuwa alipatikana na mali ya wizi Desemba 6, 2018 katika kijiji hicho.

Afisa huyo, hata hivyo, alikana mashtaka na akaachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000, kesi hiyo ikiratibiwa kusikizwa Juni 4, 2019.

Nakala ambazo upande wa mashtaka unategemea zinasema kuwa mlalamishi alinunua mbwa hao Desemba 2014 Arusha, Tanzania na wakasafirishwa kwa ndege walipokuwa na miezi mitatu.

Aliwasafirisha hadi nyumbani kwake Othaya, ambapo walikuwa wakichungwa na meneja wa shamba lake Stephen Macharia, ambaye alimfahamisha kuhusu kuibiwa kwao.

“Niliripoti kisa hicho kwa naibu chifu Paul Gichiri ili atangaze wakati wa mikutano ya baraza kwani nilishuku waliibiwa na mmoja wa majirani, kisha nikarejea Nairobi nikisubiri majibu,” mhubiri huyo akaeleza polisi.

Lakini Novemba 3, 2018 meneja wa shamba lake aliripoti kuwa aliona mbwa hao nyumbani kwa chifu huyo, kisa ambacho kiliripotiwa kwa polisi Othaya.

Habari za polisi aidha zinasema kuwa meneja huyo pamoja na polisi walienda hadi nyumbani kwa chifu huyo na wakawaona mbwa hao.

Chifu huyo anadaiwa kuambia polisi kuwa aliwanunua mbwa hao kutoka kwa mamake mhubiri ambaye ni mlalamishi, mnamo Machi 2013 kwa Sh200 kila mmoja.

“Wiki mbili baada ya kuwanunua, mbwa dume alifariki na akasalia jike ambaye tangu wakati huo amezaa mara mbili,” ripoti ya chifu kwa polisi ikasema.

Wakazi wakatakata chifu na kuchoma mwili wake

Alex Njeru na Gerald Bwisa

WAKAZI wenye ghadhabu kutoka kata ya Kamaindi, Kaunti ya Tharaka-Nithi Jumanne walimkatakata chifu wao Japhet Mayau Mukengu vipande vipande kabla ya kumchoma, kufuatia mzozo wa muda mrefu.

Chifu huyo alisemekana kuuawa na wakazi ambao walighadhabishwa na uamuzi wa kakake, Gikware Mukengu, kuzuilia mbuzi wa mkazi kwa jina Gitonga Kibuibe, ambaye alitoweka Desemba mwaka jana, kabla ya mabaki ya maiti yake kupatikana karibu na mto.

Kamishna wa Kaunti hiyo Beverly Opwora alisema kuwa polisi walikuwa wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa hicho, ambacho kilishangaza wengi.

“Kulingana na ripoti, chifu huyo aliuawa na wakazi wenye hasira lakini maafisa wetu wanakusanya habari kuthibitisha madai,” akasema Bi Opwora.

Mbuzi hao walisemekana kuwa walikuwa wameingia katika shamba la Bw Mukengu.

Marehemu naye alisemekana kuwa mnamo Desemba 12, 2018 alikuwa ameenda kuoga mtoni lakini hakurudi, wakazi wakidai kuwa aliuawa na wanawe chifu huyo, pamoja na nduguye.

Baada ya kuripoti kisa hicho kwa Naibu Kamishna wa eneo la Igambang’ombe, wakazi wanasemekana kutumwa kwa chifu huyo kuwatatulia kesi yenyewe.

Hata kabla ya chifu kufika, mamia ya wakazi wakiwa na ghadhabu walivamia nyumbani kwa kakake, lakini akafanikiwa kutoroka, naye chifu alipofika wakamvamia kwa hasira, wakimkatakata kwa panga kisha kumteketeza.

Kwingineko, wezi walibomoa ukuta wa jengo la mawe wakitarajia kuiba mali ya thamani katika duka mjini Kitale, lakini wakaishia kupata sarafu za Sh2,000 pekee jana asubuhi.

Wachunguzi waliofika eneo la tukio asubuhi walikisia kuwa huenda wezi hao walitumia saa mbili kubomoa na kutoboa shimo kwenye ukuta, kabla ya kuingia katika duka hilo la Chase Drapers.

 

Machifu wakosa afisi, wachapa kazi chini ya miti

Na SAMUEL BAYA

BAADHI ya machifu katika kaunti ya Kilifi hawana afisi na wanaendesha shughuli zao chini ya miti.

Jambo hilo limekuwa kero kubwa kwa baadhi ya machifu hao ambao wanajaribu kila hali kuhudumia wakazi wanaofurika chini ya miti hiyo kusaka huduma.

Chifu wa lokesheni ndogo ya Chapungu, eneobunge la Ganze, Bw Nickson Mapenzi, ni mmoja wa wasiokuwa na afisi.

Kila asubuhi, Bw Mapenzi huhudumia wakazi wa Chapungu chini ya mti aina ya mkonga.

“Haya ndiyo maisha yetu tukifanya kazi za serikali. Hakuna afisi hapa na nimejaribu kwa muda mrefu lakini bila mafanikio. Tumejaribu kutuma maombi lakini bado hatujafaulu,” akasema Bw Mapenzi.

Hata hivyo licha ya kutekeleza kazi hiyo, changamoto alisemani nyingi.

“Nimefanya kazi hii huu ni mwaka wangu wa 10. Sijawahi kuona afisi na kivuli hiki ndiyo afisi ambayo ninatumia kila siku,” akasema huku akiendelea kuwahudumia wananchi.

Aidha chifu huyo alisema kuwa mara nyingi shida ambazo zinamkumba ni kuwa wakati wa mvua, hana mahali pa kuficha stakabadhi muhimu za serikali hivyo kazi hukwama.

“Ujue kivuli hiki ndio afisi ya umma na kila kunaponyesha siwezi kuja kwa sababu nitaharibu karatasi hizi,” akasema.

Wakazi wa kijij hicho cha Chapungu walitoa ardhi hiyo miaka kadhaa iliyopita ili kumwezesha chifu huyo kupata afisi lakini kwa sasa imeshindikana na hali alisema huenda ikaendelea hivyo.

“Jamii ya hapa ilitoa ekari mbili za ardhi ili kujenga afisi ya chifu mdogo lakini bado zoezi la ujenzi. Nasubiri kwa sababu tayari tumetoa mapendekezo yetu kwa mbunge na sasa tunasuburi,” akasema.

Katika lokesheni ya Bandari, hali ni hiyo hiyo. Katika kituo cha biashara cha Bandari, chifu Julius Mwalimu pia hana afisi.

“Nilikuwa na afisi ndogo ya matope lakini ikaharibiwa na mafuriko miaka minne iliyopita. Siku hiyo stakabadhi zote za serikali zililoa maji na hadi leo bado sijapata afisi,” akasema Bw Mwalimu.

Na ili kuwahudumia wananchi afisa huyo alisema kuwa wanakaa chini ya mti ama wakati wa mvua, huwa wanaomba chumba katika kijiji jirani ili kuwahudumia wananchi.

“Hali ni mbaya lakini tunasukumana tu hivyo. Wakati wa mvua tunaomba chumba hapa kijijini. Tunasubiri kumuona mbunge ili atueleze kuhusu changamoto ambazo tunapitia,” alisema.

Aidha chifu huyo alisema kuwa manaibu wa chifu katika lokesheni zake nne hawana afisi na wanahudumu chini ya miti.

Naye chifu mdogo katika lokesheni ya Mwakwala, Bw Henry Shujaa alisema kuwa tangu aajiriwe kama naibu wa chifu mwaka mmoja uliopita, bado hajaona afisi.

“Hata yule mtangulizi wangu alikuwa akiwahudumia wakazi wa Mwakwala akiwa chini ya mti.

Tumejaribu kuomba ufadhili lakini hali inaonekana bado. Tuko na shida sana kwa sababu wakati wa mvua, kazi huwa inakwama,” akasema Bw Shujaa.

Katika kata ndogo ya Nambani iliyoko katika lokesheni ya Mtsara Wa Tsatsu, chifu Margaret Baya pia hana afisi. Hii ni baada ya afisi ndogo ya matope ambayo alijengewa na wananchi kubomoka.

“Sasa kila jioni, mimi hubeba stakabadhi za serikali hadi nyumbani. Afisi yangu ni chini ya mti na ninaomba tu kama kuna mtu anaweza kujitolea kunijengea afisi. Wananchi wanajaribu lakini kwa sababu ya hali ngumu za kimaisha, hawajaweza kunijengea afisi,” akasema.

Akongea na Taifa Leo baada ya kuzuru vijiji vya Chapungu, Jila, na Bandari mbunge wa Ganze Bw Teddy Mwambire alikiri kuwa machifu wengi hawana ofisi na kusema kuwa kuanzia mwakani, juhudi za kuanza kuwajengea maofisi zitaanza.

“Hii ni shida ambayo ilianza zamani kwa sababu wengine wamefanya kazi hadi wamestaafu bila kuona afisi. Lakini kwa sasa tunataka kubadlisha mfumo na mambo yawe tofauti.

Tunapania kuhakikisha kwamba tunatenga fedha mwakani tuanze. Hatuwezi zote kuzijenga ila naamini tunaweza kuanzia mahali,” akasema Bw Mwambire.

Machifu kupokea mafunzo ya kijeshi

NICHOLAS KOMU na PETER MBURU

MACHIFU takriban 3,400 na manaibu wa makamishna wa kaunti 440 watahudhuria mafunzo ya lazima ya polisi katika kipindi cha miezi sita ijayo, ili maafisa wa polisi wanaowalinda wapewe majukumu mengine.

Wariri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’I alisema hivyo wakati wa mkutano na viongozi hao wa utawala Jumanne, akisema mafunzo hayo yataongozwa na Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS)

Dkt Matiang’I alisema kila afisa wa serikali kama chifu ama naibu wa kamishna wa kaunti ambaye hajahudhuria mafunzo ya polisi sharti atapitia mafunzo hayo, kama mbinu mojawapo ya kuboresha huduma na kupunguza mzigo kwa kuondoa maafisa wa polisi wa AP wanaowahudumia.

“Tutahakikisha kuwa manaibu kamishna wa kaunti wote na machifu ambao hawajapitia mafunzo ya kivita wanafanya hivyo katika kipindi cha miezi sita ijayo,” akasema waziri huyo.

Mafunzo hayo sasa yameonekana kama mpango unaooana na mabadiliko mapya yanayoendelezwa katika huduma ya polisi, ambayo yatawafanya maafisa wa AP ambao mbeleni walihudumu katika afisi za machifu wakiondolewa.

Vilevile, ni badiliko linalokuja wakati kumekuwepo visa vya mavamizi dhidi ya viongozi hao wa utawala wakati wawapo kazini.

Katika kipindi cha miezi minne, machifu wawili wameuawa kaunti za Nyeri na Turkana wakiwa kazini

“Tunataka kufanya kazi kwa mpangilio tunapoiendesha serikali kuu. Lengo letu ni kutoa huduma bora,” akasema Dkt Matiang’i.

Hatua hii aidha itawasaidia maafisa hao kuwa wakifanya kazi ya kuwa macho ya serikali ya kitaifa, kwani watakuwa wakiripoti kuhusu hali ya miradi inayoendeshwa, na ile iliyokwama kwa wizara ya usalama wa ndani, bila ya kujali mradi unaendeshwa na wizara gani.

“Washirikishi wa kanda huendesha shughuli za serikali katika kanda na hiyo inafaa kuwa hivyo tu tunapoteremka hadi kwa machifu,” akasema.

Aibu machifu kuwalinda wanajisi

Na BRUHAN MAKONG

MWAKILISHI wa Kike wa Kaunti ya Wajir Fatuma Gedi amewaonya machifu dhidi ya kuwalinda wanajisi wa wanafunzi.

Bi Gedi alisema machifu hao wanasitiri washukiwa kwa kuwapatanisha na familia za waathiriwa na kuwatoza faini nje ya mahakama.

Mbunge huyo aliyekuwa akizungumza katika shule ya msingi ya Griftu alisema washukiwa wa ubakaji wa wasichana ni sharti wafikishwe mahakamani.

Alisema machifu hawaruhusiwi kisheria kushughulikia kesi zinazohusiana na dhuluma za kimapenzi dhidi ya wasichana.

Badala yake aliwataka machifu kushirikiana na polisi kuwanasa wahalifu hao wanaonajisi wanafunzi wa kike.

Idadi kubwa ya wasichana hulazimika kuacha shule baada ya kupachikwa mimba katika kaunti hiyo.

Machifu wamekuwa wakikashifiwa kwa kutumia utaratibu wa kitamaduni unaofahamika kama ‘maslaha’ kusuluhisha kesi zinazohusiana na unajisi wa watoto.

“Machifu wanafaa kuhakikisha kwamba washukiwa wanashtakiwa mahakamani. Utamaduni wa ‘maslaha’ ambapo washukiwa wanatozwa faini kidogo na baadaye kuachiliwa huru, haufai,’ akasema.

Wajir ni miongoni mwa kaunti zilizo na visa vingi vya dhuluma za kimapenzi dhidi ya watoto wa kike.

Bi Gedi aliahidi kuendelea kutoa sodo kwa wanafunzi kuwazuia kutoenda shuleni wakati wa hedhi.

“Hakuna msichana ataacha kwenda shule kwa sababu ya hedhi. Afisi yangu itashirikiana na wahisani wengineo kuhakikisha kuwa kila msichana ananufaika kwa sodo,” akasema.

Wakenya wanaamini machifu kuliko mawakili – Utafiti

Na BENSON MATHEKA

Kwa ufupi:

  • Ni asilimia 7 pekee ya Wakenya 6005 walioshirikishwa wanaotafuta ushauri wa kisheria kutoka kwa mawakili
  • Ingawa watu wengi wanaamini machifu kwa mizozo ya kifamilia, wengi wao huanza kwa kutafuta ushauri kutoka kwa watu wa familia zao
  • Ni watu walio na elimu ya juu, matajiri au wanaochukuliwa kuwa matajiri wanaotafuta ushauri wa kisheria kutoka kwa mawakili
  • Asilimia 25 hawakutafuta habari au ushauri wa kisheria katika kipindi cha miaka minne iliyopita licha ya kukabiliwa na matatizo

WAKENYA wengi wanawaamini machifu zaidi kuwapa habari za masuala ya kisheria kuliko mawakili na hata mahakama, utafiti unaonyesha.

Kwa jumla, asilimia 54 ya Wakenya hutumia asasi za serikali kupata habari kuhusu masuala ya kisheria huku wengi wao, ikiwa ni asilimia 19, wakiamini machifu.

Utafiti kuhusu mahitaji ya haki na uridhishaji wa mfumo wa haki unaonyesha kuwa ni asilimia 7 pekee ya Wakenya 6005 walioshirikishwa wanaotafuta ushauri wa kisheria kutoka kwa mawakili.

Asilimia 13 hutafuta ushauri kutoka kwa maafisa wa polisi na asilimia 8 kutoka mahakamani.

Kulingana na utafiti huo uliofanywa na shirika la Hague Insistute for Innovation of Justice (Hiil) kwa ushirikiano na Taasisi ya Mafunzo ya Mahakama ya Kenya (JTI), asilimia 41 ya Wakenya huwa wanatafuta ushauri kwa watu wa familia, marafiki na taasisi zizo za kisheria.

“Kwa kesi zinazohusiana na ardhi, watu hupenda kwenda kwa machifu au mahakamani. Kwa mizozo na majirani, watu huenda kwa chifu ambaye wanaamini atawasaidia. Pia chifu hutatua mizozo ya kifamilia,” unasema utafiti huo.

Maafisa wa Mahakama wanasema utasaidia kuimarisha utoaji haki nchini Kenya.

 

Marafiki

Kwa wanaokabiliwa na matatizo ya kikazi, utafiti huo unaeleza kuwa, huwa wanaamini marafiki na wafanyakazi wenzao kwa ushauri. Ingawa watu wengi huwa wanaamini machifu kwa mizozo ya kifamilia, utafiti ulifichua wengi wao huanza kwa kutafuta ushauri kutoka kwa watu wa familia zao.

Watafiti waligundua kwamba watu wengi nchini Kenya wanaamini polisi na machifu wanaoweza kuwasaidia katika kesi za uhalifu. “Kuhusu mizozo ya kifedha, watu wengi huwa wanatafuta habari na ushauri kutoka kwa marafiki,” unaeleza utafiti huo.

Miongoni mwa watu 6005 walioshirikishwa kwenye utafiti huo, asilimia 25 hawakutafuta habari au ushauri wa kisheria katika kipindi cha miaka minne iliyopita licha ya kukabiliwa na matatizo tofauti.

Baadhi yao walisema wanafikiri hata wakitafuta ushauri, hawangesaidiwa, wengine walisema hakuna ushauri ambao ungewasaidia au hawangemudu gharama ya kutafuta ushauri wa kisheria.

“Kwa masuala ya uhalifu, asilimia 45 walisema hawaamini hatua zozote zitachukuliwa wakipiga ripoti. Hii inaonyesha wazi kutamaushwa kwa watu hao na mfumo wa haki. Kwa mizozo ya ardhi, kizingiti sio kushindwa kumudu gharama ya huduma za kisheria,” unasema utafiti huo.

 

Uhamasisho

Unapendekeza uwekezaji zaidi kuhamasisha watu kuhusu masuala ya kisheria na upatikanaji wa habari na ushauri wa kisheria kutoka kwa wataalamu.

“Kizingiti kikubwa cha kutafuta habari na ushauri wa kisheria ni dhana kuwa hakuna hatua zitakazochukuliwa licha ya kupata ushauri au ukosefu wa usalama katika kutafuta ushauri huo,” unaeleza utafiti huo.

Unafichua kwamba ni watu walio na elimu ya juu, matajiri au wanaochukuliwa kuwa matajiri wanaotafuta ushauri wa kisheria kutoka kwa mawakili huku wale walio na elimu ya chini wakiwaendea machifu.

Kesi nyingi za kifamilia, unaeleza utafiti huo, huripotiwa miongoni mwa watu wa mapato ya chini. Asilimia 60 ya watu wasio na mapato ya kutosha walisema waliathiriwa na kesi hizo.

Aidha, ni watu walio na elimu ya kiwango cha chini wanaoathiriwa na kesi za unyakuzi wa ardhi ikiwa ni asilimia 30.