Serikali yatisha kuwapiga kalamu madaktari wagonjwa wakizidi kuteseka

BENSON MATHEKA, DIANA MUTHEU, TITUS OMINDE na LEONARD ONYANGO

HUDUMA za matibabu ziliendelea kukwama katika hospitali za umma kote nchini jana, na kuacha wagonjwa wakizidi kutekesa, huku maafisa wa serikali na wahudumu wa afya wanaogoma wakilaumiana.

Maafisa wa Wizara ya Afya wanasisitiza kuwa madaktari hawafai kugoma, wakisema wametimiziwa matakwa yao. Kulingana na Waziri Mutahi Kagwe, madaktari wamelipwa mishahara yao na hawafai kuhadaa Wakenya.

Siku ya Jumatatu wakati wa mazishi ya Dkt Stephen Mogusu katika Kaunti ya Kisii, maafisa wa Chama cha Matabibu na Madaktari wa Meno (KMPDU) walisema baadhi ya madaktari hawajalipwa mishahara yao kwa miezi kadhaa.

Jana, hata hivyo, Bw Kagwe alisema ingawa mishahara ilicheleweshwa hakuna daktari anayedai malipo.

Waziri alisisitiza kuwa madaktari wanaogoma wanafaa kufutwa kazi, kauli ambayo magavana wanakubaliana nayo. “Hatuwezi kuacha wagonjwa wakiteseka,” akasema Bw Kagwe.

Miongoni mwa matakwa ya madaktari ni bima ya matibabu na maisha, vifaa vya kuwakinga dhidi ya maambukizi ya janga la Covid-19 wakiwa kazini na kupandishwa cheo.

Naibu Waziri wa Afya Dkt Mercy Mwangangi alisema matakwa saba kati ya tisa yametimizwa.“Kilichobaki na ambacho kinashughulikiwa ni marupurupu,” akaeleza.

Waziri Kagwe alifafanua kwamba kile madaktari wanataka ni kudumishwa kwa marupurupu ambayo walipewa wakati janga la Covid-19 lilipoanza.

Hata hivyo, wahudumu wa afya walilaumu serikali na magavana kwa kutojali maslahi yao. Jana, Gavana wa Kisumu Profesa Peter Nyong’o aliunga mkono kauli ya Waziri Kagwe kwamba madaktari waliolemaza huduma katika hospitali za umma watafutwa kazi.

Katika Kaunti ya Mombasa, wahudumu waliomlaumu Gavana Hassan Joho kwa kuwapuuza, huku wakisisitiza kuwa wataendelea na mgomo hadi watendewe haki.

Wakizungumza baada ya kuandamana hadi nje ya majengo ya ofisi za Bw Joho, wahudumu hao wa afya walimtaka gavana ashughulikie malalamishi yao haraka iwezekanavyo.

“Mara nyingi tumemuona gavana wetu akitilia maanani mambo ya siasa, lakini tunapokuwa na changamoto katika sekta ya afya huwa hajitokezi kwa mazungumzo,” alihoji Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi Nchini (KNUN), Bi Miriam Mbithe.

Kupitia kwa viongozi wao, wahudumu hao zaidi ya 850 walisema vitisho havitawazua kuendeleza mgomo wao kitaifa ulio katika wiki ya tatu.

“Hatuogopi kufutwa kazi. Zaidi, hatutaki kufanya kazi katika mazingira yanayohatarisha maisha yetu, na katika sekta inayopuuza malalamishi ya wafanyakazi wake,” akaeleza Katibu wa Chama cha Kutetea Haki za Matabibu (KUCO) Kaunti ya Mombasa, Bw Franklin Makanga.

Wahudumu wa afya 800 Uasin Gishu walilaumu serikali ya Gavana Jackson Mandago kwa kutowapandishwa vyeo kwa miaka zaidi ya kumi, licha yao kuhitimu.

Mwenyekiti wa KNUN tawi la Uasin Gishu, Bw Francis Chepkwony, alikanusha madai kwamba shughuli za kawaida za matibabu ziliendelea katika hospitali za kaunti hiyo

.“Wanaodanganya eti huduma za afya zinaendelea katika kaunti hii wanawakejeli wakazi maskini wanaotegemea vituo vya afya vya umma kwa matibabu,” akasema Bw Chepkwony.

Gavana Mandago ni mmoja wa magavana ambao wamewapuuza wafanyikazi wa afya kwa gharama ya shughuli ambazo haziongeza thamani kwa wakaazi wa kaunti hii,’ akaongeza.

Hofu ya maafa mgomo ukichacha

Na WAANDISHI WETU

MAAFA yanawakodolea macho wagonjwa nchini baada ya wahudumu wa afya wanaogoma kuacha hospitali na vituo vya afya vya umma vikiwa mahame.

Wagonjwa waliofika katika vituo hivyo kote nchini walisononeka kwa maumivu bila wa kuwahudumia huku walinzi wakiwaagiza kutafuta huduma katika hospitali za kibinafsi.

Madaktari walioanza mgomo jana, waliungana na wauguzi na matabibu kusema hakuna vitisho vinakavyowafanya kufuta mgomo huo kabla ya matakwa yao kutimizwa.

“Hakuna vitisho vitakavyofanya madaktari kurudi kazini. Maagizo ya mahakama hayatazuia madaktari kufariki au kuambukizwa maradhi,” alisema kaimu Katibu Mkuu wa chama cha Madaktari na wataalamu wa meno (KMPDU) Dkt Chibanzi Mwachonda alipozindua rasmi mgomo huo mjini Kisii.

Mnamo Jumamosi, waziri wa afya Mutahi Kagwe aliwalaumu wahudumu wa afya kwa kugoma licha ya mahakama kuharamisha mgomo wao na kuagiza serikali za kaunti kuwafuta kazi.

Dkt Mwachonda alitaja kauli hiyo kama vitisho na kuingiza siasa katika masuala ya afya.“Madaktari nchini Kenya hawawezi kusubiri, hawawezi kuendelea kuhudumu katika mazingira hatari,” alisema.

Katika hospitali ya rufaa ya Pwani, wagonjwa waliofika kutafuta huduma za dharura waliagizwa kwenda katika hospitali za kibinafsi, jambo ambalo ni mlima kwa Wakenya wengi wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na athari za janga la corona.

Hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi huku maambukizi ya virusi vya corona yakiendelea kuongezeka nchini.Mkurugenzi wa huduma za uuguzi katika hospitali ya rufaa ya Pwani , Elizabeth Kivuva alidai wameajiri madaktari na wauguzi kwa kandarasi kusaidia kukabiliana na mzozo huo.

“Tunashughulikia wagonjwa wa corona pekee. Wengine wote wanahamishwa,” alisema.Katika kaunti ya Tana River, wagonjwa na akina mama wajawazito waliachwa katika wodi bila wahudumu wa kuwashughulikia.

Baadhi waliweka maisha yao hatarini kwa kutafuta huduma za wakunga wa kitamaduni kwa kukosa pesa za kwenda hospitali za kibinafsi.

“Nilikuja hapa na nikapata milango yote imefungwa, hakuna daktari au muuguzi hata mmoja,” alisema Mwanaharusi Jillo. Wagonjwa wa figo waliofika kusafishwa damu walisononeka wasijue pa kuelekea.

Katika kaunti ya Kilifi, hakuna hospitali ya umma iliyokuwa ikipokea wagonjwa. Baadhi ya walioonekana kupata nafuu waliruhusiwa kuondoka wodi hata kabla ya kupona.

Mwenyekiti wa tawi hilo la KMPDU, Dkt Sammy Kiptoo alisema kwamba, madaktari hawatarudi kazini matakwa yao yasipotimizwa.Huduma za afya katika kaunti ya Taita Taveta, pia zililemazwa huku maafisa wa chama hicho wakisema hawatarudi kazini.Hali ilikuwa sawa katika kaunti ya Lamu wagonjwa wakisononeka kwa kukosa huduma.

Wagonjwa wanaotafuta huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Uasin Gishu walitaabika wakitafuta matibabu bila wa kuwahudumia.

Mwanamke mwenye umri wa makamo ambaye alikuwa akitafuta huduma kujifungua mtoto alisema alielekezwa na walinzi kutafuta huduma kwingine.Doreen Rotich ambaye anatarajia mtoto wakati wowote aliomba magavana na serikali ya kitaifa kuingilia kati.

‘Nilikuja hapa mapema saa tatu asubuhi tangu wakati huo hakuna huduma ambazo nimepokea. Wafanyikazi wa pekee ambao tunakutana nao ni walinzi. Serikali zote za kitaifa na kaunti lazima zipate suluhisho la mgomo huu,”akasema Bi Rotich.

Mwenyekiti wa chama cha wauguzi kaunti ya Uasin Gishu, Francis Chekwony alisema hakuna huduma katika hospitali za kaunti.Hali ilikuwa sawa Elgeyo Marakwet ambapo zaidi ya wauguzi 600 na wahudumu wengine wa afya wamesusia kazi.

Katibu Mkuu wa tawi la kaunti hiyo la chama cha wauguzi, Benson Biwott alitaka viongozi wa kaunti hiyo kukoma kuwatishia wauguzi wanaogoma.

Ripoti za Ruth Mbula,Benson Matheka, Lucy Mkanyika, Maureen Ongalo, Kalume Kazungu, Stephen Oduor, Winnie Atieno, Titus Ominde

Madaktari washinikiza kupewa bima ya afya

JUMA NAMLOLA na WINNIE ATIENO

MADAKTARI katika hospitali za umma Kaunti ya Mombasa, sasa wanataka serikali iwape bima ya afya huku visa vya maambukizi nchini vikifika 22,053.

Ingawa Mombasa ilikuwa na kisa kimoja pekee kati ya watu 690 walioambukizwa kote nchini jana, madaktari wanaotibu wagonjwa wa corona walisema wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa, ilhali hawana bima ya afya.

“Ni kinaya kwamba madaktari katika kaunti hii hawana bima ya afya, hata baada ya kujitolea kusaidia nchi kukabiliana na janga hili la corona,” alisema Dkt Abidan Mwachi, mwakilishi wa Pwani katika chama cha KMPDU.

Alisema kukosekana kwa bima ya afya ni hatari ambayo wahudumu wa afya wanakodolea macho, hasa wakati huu ambapo tayari wahudumu 45 wameambukizwa virusi hivyo wakiwa kazini.

Dkt Mwachi alimsihi Gavana Hassan Joho na Hazina ya Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) kutatua jambo hilo, ili wahudumu wa afya waweze kupata huduma hiyo muhimu

.“Mgogoro ulioko kati ya NHIF na serikali ya Kaunti ya Mombasa unafaa kutatuliwa haraka iwezekanavyo ili wahudumu wa afya waweze kuwekwa kwenye bima hiyo ya afya,” alisema Dkt Mwachi.

Pia chama hicho cha KMPDU kilitoa wito kwa serikali za kaunti kuhakikisha wahudumu wa afya wanapewa barakoa maalum za N95 ili kujikinga dhidi ya virusi hivyo.

“Barakoa za N95 ndizo zinazofaa kutumiwa na wahudumu wa afya katika janga hili. Pia tunaonya Wakenya dhidi ya unyanyapaa miongoni mwa watu wanaouguza virusi vya corona,” alisisitiza Dkt Mwachi.

Kaunti ya Mombasa bado ni ya pili kwa maambukizi ikiwa na watu 2,067 baada ya mtu mmoja kuambukizwa jana.

Nairobi jana iliongoza kwa visa 535 na kufanya idadi ya watu wote walioambukizwa katika kaunti hiyo kuwa 13,416, ambayo ni zaidi ya nusu ya maambukizi yote nchini.

Idadi ya wagonjwa walioruhusiwa kuondoka hospitalini na karantini pia iliongezeka kwa watu 58 huku watu watano wakiaga dunia.

‘Madaktari wa Cuba watalipwa mishahara sawa na madaktari wa Kenya’

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI sasa inasema kuwa madaktari 20 kutoka Cuba waliowasili nchini Kenya Ijumaa jioni kupiga jeki vita dhidi ya Covid-19 watalipwa mishahara inayowiana na wenzao wa Kenya.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe Jumamosi, Julai 18, 2020, alisema wataalamu hao wako nchini kubadilisha ujuzi na tajriba na madaktari wa humu nchini ambao wako mstari wa mbele katika vita dhidi ya janga hilo.

“Hatutawalipa zaidi ya mishahara na malipo mengine tunayowalipa madaktari wetu. Nataka hili lieleweke vizuri. Hawa na madaktari wachache wenye ujuzi katika Nyanja mbalimbali za utabibu, na ambao wamekuja kutusaidia. Tutajifunza kutoka kwao na wao pia watajifunza kutoka kwetu,”akasema Bw Kagwe alipowahutubia wanahabari katika kaunti ya Embu.

Hata hivyo, Bw Kagwe hakutoa kiwango kamili cha mishahara na marupurupu ambacho madaktari hao watakuwa wakipokea kila mwezi kwa kipindi cha miezi sita ambacho watakuwa nchini.

Alieleza kuwa madaktari hao 20 watakuwa wakishirikiana sako kwa bako na wenzao wa humu nchini ili endapo kutatokea mlipuko mkali, wanaweza kuingilia kati.

“Vilevile, tunaendelea kuajiri madaktari wataalamu katika nyanja ya tiba ya magonjwa sugu kama kansa na kisukari. Hii ni kwa sababu kuna uhaba wa wataalamu kama hao nchini,” waziri Kagwe akaongeza.

Madaktari hao ambao wanatoka katika kikundi kinachojulikana kama Brigade of Henry Reeve; na wana ujuzi spesheli wa kukaliana na Hali ya Majanga na Milipuka ya Magojwa ya Kuambukiza.

“Tunatoa shukrani kwa serikali ya Cuba na Rais Miguel Diaz-Canel kwa kukubali ombi la Rais Uhuru Kenyatta na kutuma madaktari hao nchini Kenya,” waziri akasema.

Kenya imekuwa na ushirikiano mkubwa na Cuba katika nyanja ya utabibu ambapo imekuwa ikituma madaktari huko kwa mafunzo zaidi.

Na miaka miwili iliyopita Cuba ilituma madaktari wake 100 nchini Kenya kutoa huduma katika hospitali 94 za kaunti kote nchini.

Madaktari walia Serikali haiwajali wakitoa matibabu

VALENTINE OBARA na WINNIE ATIENO

MADAKTARI na wahudumu wa afya wamelalamika kwamba, Serikali haijatilia maanani usalama wao wanapohudumia wagonjwa walioambukizwa virusi vya corona.

Chama cha Wahudumu wa Afya nchini jana kilidai mwanachama wao mmoja tayari amethibitishwa kuambukizwa corona.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw George Gibore alisema mhudumu huyo wa kike aliambukizwa akiwa kazini na sasa kuna wasiwasi huenda alisambazia familia yake na wagonjwa wengine virusi hivyo.

Bw Gibore alisema kufikia sasa, wahudumu wa afya hawajapewa mafunzo maalumu kuhusu wanavyofaa kuhudumia wagonjwa wa virusi vya corona wala kupewa vifaa vya kutosha kujikinga kuambukizwa wakiwa kazini.

“Msimamo wetu ni kwamba, tuko tayari kujitolea lakini hatutajitoa mhanga. Hatutahudumia mgonjwa yeyote bila kujikinga. Pia, tunataka serikali itoe mafunzo kwa wahudumu wa afya kabla wiki mbili zikamilike,” akasema.

Kwa upande mwingine, madaktari walitaka serikali iwahakikishie kuwa endapo watafariki kwa virusi vya corona, familia zao zitalipwa fidia sawa na jinsi familia za wanajeshi hulipwa wakati mwanajeshi anapofariki vitani.

Chama cha Wahudumu wa Matibabu na Madaktari wa Meno (KMPDU) kilitilia shaka uwezo wa serikali kulinda madaktari na wahudumu wa afya walio katika mstari wa mbele katika vita dhidi ya virusi vya corona.

Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt Chibanzi Mwachonda alisema, kuna changamoto katika vita dhidi ya ugonjwa huo, ikiwemo uhaba wa vifaa vya madaktari kujikinga wanapokuwa kazini.

Dkt Mwachonda pia alisema mafunzo ya kutosha hayajatolewa kwa madaktari na wahudumu wa afya kuhusu jinsi ya kuhudumia wagonjwa wa corona.

“Si madaktari wote wamefunzwa kuhusu hatua wanazopaswa kuchukua katika janga hili. Inafaa sote tuwazie kwa pamoja namna tutahakikisha hatutapatikana tukisinzia endapo kutakuwa na hali ya dharura,” akasema.

Alitaka serikali iimarishe utengenezaji wa vifaa vya kujikinga katika viwanda vya humu nchini kwani kuna uhaba kimataifa.

“Katika utoaji matibabu, hasa wakati wa janga kama ilivyo sasa, unahitaji kuzingatia usalama wako kwanza. Kama mhudumu wa afya ataambukizwa, ilhali yeye ndiye anategemewa kutibu mamia ya wagonjwa, hali itakuwa mbaya,” akasema.

Hata hivyo, alisema serikali kufikia sasa imeonyesha kujitolea kupambana na virusi hivyo lakini inafaa changamoto zote ziangaliwe kwa makini.

“Tumeshuhudia wahudumu wa afya wakifa katika mataifa mengine, na kuna walioambukizwa Ulaya na Asia. Tunataka kuwe na mfumo wa fidia ili daktari akiathiriwa, familia yake ilipwe ilivyo katika jeshi,” akasema Dkt Mwachonda.

Alitaka pia serikali iajiri wauguzi, madaktari na wahudumu wa afya zaidi.

Mapema wiki hii, Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe alitangaza mpango wa serikali kuajiri wafanyakazi 1,000 wa sekta ya afya.

Lakini Dkt Mwachonda alisema, idadi hiyo bado haitoshi.

“Ni hatua nzuri na tunaisifu, lakini tunahitaji zaidi ikizingatiwa matarajio ya idadi ya maambukizi kuongezeka,” akasema.

Korti yaelezwa jinsi madaktari wa Cuba walivyotekwa nyara

Na MANASE OTSIALO

MAHAKAMA ya Mandera, Alhamisi ilisimuliwa matukio ya jinsi madaktari wawili wa Cuba mjini Mandera walivyotekwa nyara mnamo Aprili 2019.

Maelezo hayo yalijitokeza wakati wa kusikizwa kwa kesi ambapo dereva ameshtakiwa kuhusiana na utekaji nyara huo.

Jopo la mahakimu wa Nairobi wanaoendesha kesi hiyo Mandera, walizuru eneo la utekaji nyara huo ili kujifahamisha na mazingira ambamo tukio hilo lilitendeka.

Dkt Landy Rodriguez (mtaalam wa upasuaji) na Dkt Herera Correa (tabibu wa masuala ya jumla), walitekwa nyara katika uvamizi wa kutisha barabarani na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa al-Shabaab, waliomuua afisa mmoja wa polisi aliyekuwa akiwasindikiza mnamo Aprili 12, 2019.

Hapo jana, Bw Ahmed Abdi, shahidi wa upande wa mashtaka alisimulia jinsi wawili hao walivutwa kutoka gari lao rasmi na kuingizwa katika gari aina ya Toyota Probox, lililoondoka kwa kasi kuelekea Somalia.

Bw Ahmed alikuwa akitoa ushahidi dhidi ya Bw Isaack Ibrein Robow, dereva anayeshukiwa kusaidia utekaji nyara wa madaktari hao wawili wa Cuba.

Bw Abdi, mfanyabiashara eneo hilo alisema alikuwa akisafirishwa kwa Tuktuk kisa hicho kilipotokea mnamo Ijumaa asubuhi.

“Nilikuwa ndani ya Tuktuk iliyokuwa ikiendeshwa na Barrow na bila shaka tulisikia milio ya risasi tulipokuwa tukisafiri kwenye barabara kuu mjini,” alisema.

Risasi

Mwendeshaji Tuktuk alitoroka na kumwacha Abdi anayeugua kisukari ndani ya kigari hicho chenye magurudumu matatu karibu na eneo ambapo risasi zilikuwa zikifyatuliwa.

“Niliona wanaume wawili wakitua upesi kutoka kwa gari lao lililokuwa mbele yangu. Walitoka upande wa kulia wa gari hilo kabla ya kutoweka,” alisimulia.

Bw Abdi alisema aligundua kwamba mmoja wa wanaume hao wawili alikuwa dereva wa gari la serikali lililokuwa limesimama mbele ya tuktuk lakini hakuweza kumtambua mwanamume wa pili.

“Dereva wa pick-up alikuwa amevalia kanzu nyeupe na ni mtu ninayemfahamu kwa sababu nimekuwa nikimwona akiendesha gari la serikali ya kaunti. Ni yeye alikuwa wa kwanza kutoka,” alisema.

Madaktari na wauguzi wakaa ngumu wagonjwa wakifa

FARHIYA HUSSEIN, WINNIE ATIENO na ANGELINE OCHIENG

WAHUDUMU wa afya na madaktari katika kaunti tofauti wameapa kuendeleza migomo yao hadi serikali za kaunti zitakapowalipa.

Wiki iliyopita, serikali kadhaa za kaunti ziliahidi kulipa wafanyakazi wao ifikapo Ijumaa iliyopita lakini imebainika kuna wahudumu wa afya ambao hawajapokea mishahara yao ya Julai.

Katika Kaunti ya Mombasa, wahudumu wa afya na madaktari walitoa wito kwa serikali ya kaunti kuwalipa mishahara yao wakisema wanataabika na kukosa pesa za kununua mahitaji yao muhimu na hata nauli ya kufika kazini.

Wakiandamana nje ya hospitali kuu ya Pwani, zaiid ya madaktari na wahudumu wa afya 300 walisema wagonwja wanateseka bila huduma ya afya.

“Serikali ya kaunti ina uwezo wa kutulipa mshahara wetu lakini hawataki. Hatuwezi kwenda kazini bila nauli ama hata pesa za kununua vyakula. Tuna mahitaji yetu kama binadamu yeyote yule. Huu ni unyama, ingekuwa serikali kuu inawacheleweshea mishahara yenu nina hakika magavana wangelikuwa wameenda mahakamani,” alisema Dkt Chibanzi Mwachonda.

Dkt Mwachonda ambaye ni naibu katibu mkuu wa chama cha madaktari nchini, alisema huduma za afya zimelemaa katika hospitali za umma huku wagonjwa wakitaabika.

Alimshtumu Gavana Hassan Joho kwa kuwacheleweshea wafanyikazi wa umma katika kaunti ya Mombasa mishahara yao akisema ni unyama.

“Anaweza kutulipa mishahara yetu kupitia mfuko wa kaunti wakisubiri fedha kutoka serikali kuu. Mombasa serikali ya kaunti ya Kwale imewalipa wafanyikazi wake? Kwani Mombasa ni spesheli?” aliuliza.

Madaktari hao ambao walisusia kazi tangu wiki iliyopita wanaitaka serikali kuu kuingilia kati maswala yao.

Wafanyakazi hao wa kaunti walisisitiza walipwe kabla mwezi huu kuisha.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo, ulibaini kuwa wagonjwa wengi waliachwa bila huduma huku wakilazimika kwenda hospitali za kibinafsi.

Katika Kaunti ya Kisumu, wahudumu wa afya waliendeleza mgomo wao kwa wiki ya pili baada ya serikali ya kaunti kushindwa kutekeleza ahadi ya kuwalipa Ijumaa iliyopita.

Waliapa kuzidisha mgomo wao ikiwa hawatalipwa mishahara yao ya Julai ifikapo Jumatano. Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi Kitaifa (KNUN) tawi la Kisumu, Bw Maurice Opetu alisema ni sharti serikali ya kaunti hiyo itambue hakuna maendeleo ya kiuchumi yanaweza kupatikana bila huduma bora za afya ya umma.

Chama sasa chataka Kaunti ziajiri madaktari waliohitimu

Na WINNIE ATIENO

CHAMA cha madaktari nchini kinataka serikali za kaunti kuajiri madaktari zaidi ya 2,500 waliofuzu ili kukabiliana na uhaba wa wataalamu hao kitaifa.

Kulingana na Chama cha Wahudumu wa Matibabu na Madaktari wa Meno (KMPDU), madaktari hao walifuzu na kuhitimu katika sekta hiyo ilhali hawana kazi.

Wakiongea kwenye kongamano lao la mwaka huko Mombasa, madaktari walisema idadi ya madaktari kwa wagonjwa ni mmoja kwa kila 16,000.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt Ouma Oluga aidha alitaka serikali za kaunti kuwaajiri madaktari hao ili kukabiliana na uhaba wa wataalamu hao katika hospitali za umma.

“Kama hakuna madaktari basi hakuna huduma za afya. Magavana wanadanganywa wasiajiri madaktari lakini mtajuta wenyewe,” alionya.

Chama hicho pia kilisema kitafanya mazungumzo na madiwani na bodi za ajira katika serikali za kaunti kuhakikisha madaktari hao wanaajiriwa.

Dkt Olunga alisema changamoto katika sekta hiyo ilianza Mei mwaka 2017, wakati baraza la magavana lilitoa agizo dhidi ya kuajiri madaktari moja kwa moja.

“Agizo hilo lilitolewa kwa haraka bila ya mashauriano sasa kuna majuto. Agizo hilo limetuathiri na kusababisha uhaba mkubwa wa madaktari. Lazima madaktari waajiriwe,” Dkt Oluga alisema.

Aliwataka magavana kupuuzilia mbali agizo hilo ili madaktari waanze kuajiriwa.

“Serikali za kaunti zimeshindwa kuajiri madaktari ambao wamefuzu ilhali wataalam hao wako tayari kufanya kazi sehemu yoyote nchini ili kutoa huduma kwa Wakenya ambao ni walipa kodi,” alisema Dkt Oluga.

Alitaja kaunti za Kirinyanga, Nyeri, Laikipia na Siaya ambazo zimekumbwa na uhaba mkubwa wa madaktari.

“Ukiangalia kati ya mwaka wa 2013 hadi 2015 kulikuwa na madaktari wengi kuliko waliopo hivi sasa kwasababu wale walioaga dunia, walioaacha kazi na walioenda masomo ya juu nafasi zao bado zi wazi,” Dkt Oluga aliongeza.

Wakati huo huo, chama hicho kilipongeza serikali za kaunti 17 ikiwemo Kitui kwa kuwapandisha vyeo madaktari na Mombasa kwa kuwekeza kwa muundomsingi wa kisasa hususan wadi ya kina mama kujifungua.

Vile vile chama hicho kimeonya kuwa kimeanza kuagiza madaktari waondoke kaunti za Kirinyanga na Laikipia kufuatia mgogoro kati yao na magavana.

Madaktari Makueni waweka historia

Na PIUS MAUNDU

MADAKTARI wa upasuaji katika hospitali ya Makindu, Kaunti ya Makueni wamefanikiwa kubadilisha goti la mgonjwa lililokuwa likimsumbua kutokana na ugonjwa wa viungo.

Bi Rael Mbula, ambaye amekuwa akipata matatizo ya goti kwa miaka bila mafanikio, alikuwa amepoteza uwezo wa kutembea.

Hata hivyo, wiki iliyopita familia yake ilifika hospitalini humo, kutafuta matibabu ya kubadilishwa goti.

Katika oparesheni ya upasuaji iliyochukua saa mbili, madaktari watatu na wauguzi walimhudumia Bi Mbula, 69, hadi wakafanikiwa kumbadilisha goti lililokuwa likimsumbua.

“Ugonjwa wa viungo kuuma ulikuwa umemwathiri mgonjwa huyo sana, kiwango cha kuwa na matatizo ya kutembea. Tulimpasua na kuondoa goti kisha kumweka jingine la chuma. Kwa sasa anaendelea kupata nafuu na kufanya mazoezi ya kutembea,” Dkt James Muoki ambaye aliongoza oparesheni hiyo alisema jana.

Mama huyo aliwashukuru madaktari na watu wa familia yake kwa oparesheni hiyo, japo akisema bado anahisi uchungu kidogo katika mguu huo, hali ambayo madaktari walisema ni hatua ya kupona.

Alisema furaha yake kubwa itakuwa atakaporuhusiwa kwenda nyumbani na atembee vyema tena.

“Alikuwa akihisi uchungu mwingi katika magoti, hali ambayo ilimfanya kushindwa kutembea. Kwa miaka miwili iliyopita, hajaweza kufanya kazi kutokana na hali hiyo. Tuna furaha kuwa hii itakuwa historia atakaporejelea maisha yake ya kawaida,” akasema Julius Kivala, mwanawe Bi Mbula.

Bw Kivala alisema familia iligharamia vifaa vya chuma ambavyo aliwekwa kama goti pekee, nayo bima ya afya ya kaunti ikashughulikia mahitaji mengine.

Oparesheni hiyo ilikuwa ya kwanza ya aina yake katika kaunti hiyo, kulingana Afisa Mkuu katika idara ya Afya, Dkt Patrick Musyoki.

Dkt Musyoki alisema kuwa gharama kubwa ya oparesheni hiyo na jinsi inahitaji utaalamu ndiyo sababu hospitali nyingi za umma zinashindwa kuitekeleza.

Madaktari waonywa dhidi ya kuanika siri za wagonjwa mitandaoni

Na FRANCIS MUREITHI

MADAKTARI vijana wanaohitimu kutoka vyuo vikuu vya umma wameonywa dhidi ya kujadili hali za wagonjwa wao katika mitandao ya kijamii kwa sababu ni kinyume cha maadili ya taaluma yao.

Kulingana na Profesa Lukoye Atwoli wa Chuo Kikuu cha Moi, chochote ambacho madaktari hao wanachojadili au maoni wanayotoa, yanawaathiri wagonjwa na yanaweza kuhatarisha kazi yao.

Mhadhiri huyo alitoa onyo hilo Jumatatu katika bewa la Nakuru mjini la Chuo Kikuu cha Egerton wakati wa kula kiapo kwa madaktari 70 na wauguzi ambao walimaliza masomo yao.

“Ninataka muwe makini sana na mnachosambaza na kufichua katika mitandao ya kijamii kwa sababu chochote mnachosema kinachukuliwa kwa makini kwa kuwa madaktari ni watu wanaoheshimiwa katika jamii,” alisema Profesa Atwoli.

Alisema kama walinzi wa habari za siri za wagonjwa wao, madaktari wanapaswa kuhakikisha hazifichuki.

“Ni muhimu muwe waangalifu na mnachochangia katika mitandao ya kijamii na majukwaa mengine,” alisema.

Aliongeza: “Kufichua habari muhimu za wagonjwa wenu kunaweza kuwaathiri zaidi na kuwafanya wakose kupona,” alieleza Profesa Atwoli.

Alisema tabia yao katika mitandao ya kijamii na maeneo ya umma hufuatiliwa na Wakenya wengi na chochote kibaya kinaweza kusambazwa kwa wingi na kuharibu imani ambayo Wakenya wako nayo kwao kama madaktari.

“Iwe ni katika mitandao ya kijamii au maeneo ya umma, ni lazima madaktari wadumishe heshima na tabia nzuri na kuepuka kutoa habari ambazo zinaweza kutafsiriwa vibaya na kwa urahisi na umma,” alisema Profesa Atwoli.

Madaktari 2,275 wafutwa kwenye sajili ya KMPDB

Na PETER MBURU

BODI ya Kusimamia Madaktari Nchini (KMPDB) Jumatano iliwaondoa madaktari 2,275 kutoka kwa sajili yake baada yao kukosa kuchukua leseni za kuhudumu mwaka huu.

Madaktari hao, wakiwa ni pamoja na 212 wa meno na 2,063 wa aina zingine kutoka hospitali za umma na za kibinafsi sasa hawatahudumu tena, hadi warejeshwe katika sajili hiyo, ambayo kila daktari anayefanya kazi humu nchini sharti awe ameorodheshwa hapo.

Kupitia tangazo lililochapishwa katika magazeti jana, Afisa Mkuu Mtendaji wa KMPDB, Daniel Yumbya alisema, madaktari wanaotaka kurejeshwa katika sajili hiyo sasa watatuma maombi kupata vyeti vya kuhudumu mwaka huu.

Bw Yumbya alisema kuwa bodi hiyo ilikutana mnamo Machi 29 na ikaamua kuwaondoa madaktari hao kutoka kwa sajili yake, kwa kuwa walikosa kutuma maombi wapewe vyeti vya mwaka huu vya kuendelea kuhudumu.

Kulingana na sehemu ya 14 ya sheria kuhusu uhudumu wa madaktari nchini “hakuna daktari anaruhusiwa kufanya kazi katika hospitali ya kibinafsi bila leseni kutoka kwa bodi ya madaktari.”

Sheria hiyo aidha inasema kuwa muda wa leseni hiyo kufanya kazi utakuwa ukiamuliwa na Mkurugenzi wa Matibabu nchini kwa ushirikiano na bodi hiyo.

Katika orodha ya madaktari, waliong’olewa kutoka sajili hiyo, baadhi yao hawajawahi kupokea leseni kutoka kwa bodi hiyo tangu 2015, japo wengi wao walipokea mwaka uliopita.

Madaktari kutoka maeneo tofauti ya nchi, yakihusisha Nairobi, Eldoret, Kisumu, Mombasa, Nandi, Bomet na mengine mengi waliathirika.

Hatua hiyo ya bodi ya madaktari aidha imetokea baada ya kufanya ukaguzi katika vituo vya afya nchini kwa miezi kadhaa na pia kuamrishwa kufungwa kwa vituo ambavyo havikuwa vimehitimu kutoa huduma za afya.

Bw Yumbya awali mwaka huu alieleza Taifa Leo kuwa, KMPDB ilikuwa ikishirikiana na asasi zingine kama ile ya wauguzi na maafisa wa kliniki kuendesha oparesheni za kuwasaka watu wanaoendesha kliniki kinyume na sheria.

“Mwaka huu pekee, tunalenga kukagua zaidi ya vituo 1,000 vya afya kwa ushirikiano na mamlaka zingine ili kubaini vifaa vilivyopo na huduma zinazotolewa. Kila kituo ambacho hakina leseni tunafunga,” akasema Bw Yumbya.

Hatua hiyo ya KMPDB inafuatia miezi minne tu baada ya serikali kuzindua Mradi wa Huduma ya Matibabu ya Bei Nafuu kwa Wote (UHC) unaoendelea kufanyiwa majaribio katika kaunti nne; Machakos, Nyeri, Isiolo na Kisumu.

Bila leseni, daktari haruhusiwi kutoa huduma za matibabu hivyo hatua hiyo ya KMPDB huenda ikatatiza mradi huo wa UHC.Kwa sasa, Kenya ina uhaba wa madaktari na wataalamu wa kutibu meno, kila daktari anatibu wagonjwa 16,000.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza angalau madaktari watatu watibu 20,000. Kuna madaktari 7,433 waliosajiliwa nchini Kenya ambao wanatibu zaidi ya Wakenya 40 milioni.

155 waliobobea katika KCSE 2018 kusomea udaktari

Na WANDERI KAMAU

IDADI kubwa ya waliong’aa kwenye mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) 2018 watasomea udaktari, kulingana na ripoti ya mpangilio wa kuwaita kwa vyuo vikuu iliyotolewa jana na Waziri wa Elimu, Prof George Magoha.

Kulingana na ripoti hiyo, wanafunzi saba kati ya 10 bora kwenye mtihani huo walichagua kusomea kozi ya udaktari katika vyuo mbalimbali nchini.

Kijumla, wanafunzi 155 kati ya 314 ambao walipata alama ya ‘A’ katika mtihani huo walichagua kusomea kozi ya udaktari.

Mwanafunzi Otieno Teddy Odhiambo ambaye aliibuka bora katika mtihani huo atasomea udaktari katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Wengine watakaosomea kozi hiyo katika chuo hicho ni Edwin Otieno Ouko, Ian Kiplagat, Matsotso Madlean Auma na Mathenge Stephanie Kirigo. Whitney Nicanor Mabwi, aliyekuwa wa nane bora atasomea udaktari katika Chuo Kikuu cha Moi.

Kozi zingine zilizoibuka kuwa maarufu miongoni mwa wanafunzi ni somo la uchumi, uhandisi wa barabara, sayansi ya kompyuta, uhandisi wa ndege, upasuaji wa meno, sheria, sayansi ya bima na somo la utaalamu wa dawa.

Msisitizo wa serikali kwa wanafunzi kuegemea masomo ya sayansi na teknolojia pia ulionekana kukumbatiwa na wengi, kwani kati ya wanafunzi 89,486 waliohitimu kujiunga na vyuo vikuu, 57,687 walichagua kozi zinazohusiana na hayo. Idadi hiyo inawakilisha asilimia 64 ya wanafunzi wote.

Kati ya hao, 36,189 ni wavulana huku 21, 498 wakiwa wasichana.

Akitoa ripoti hiyo, Prof Magoha alisema kuwa lazima wanafunzi watilie maanani umuhimu wa kozi wanayochagua kusomea.

“Wanafunzi lazima wafanye utafiti wa kina ili kubaini umuhimu wa kile wanachoenda kusomea katika vyuo vikuu, hasa kutokana na ushindani mkubwa uliopo,” akasema.

Chuo Kikuu cha Nairobi pia kiliibukia kupendelewa na wanafunzi wengi zaidi, kwani kati ya wanafunzi 314 waliopata alama ya ‘A’ 191 watajiunga na chuo hicho.

Chuo hicho kimekuwa kikiorodheshwa kuwa bora nchini na ukanda wa Afrika Mashariki na mashirika mbalimbali ya utafiti. Chuo pia kimesifiwa kwa ubora wa kozi zake.

Prof Magoha aliitaka Tume ya Elimu ya Juu (CUE) kufanya utathmini wa kina kuhusu ubora wa kozi ambazo zinatolewa katika vyuo vikuu nchini kwani kozi tisa hazikuchaguliwa na mwanafunzi yeyote katika vyuo vikuu.

Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa kozi 98 hazitapata mwanafunzi yeyote, kwani wengi waliotuma maombi kuzisomea hawakufikisha viwango vinavyohitajika.

Baadhi ya kozi hizo ni sayansi ya mazingira, usimamizi wa hoteli, sayansi ya mawasiliano, ualimu wa chekechea, sayansi ya mchanga, utaalamu wa chakula, usimamizi wa misitu kati ya zingine

Kulingana na Prof Magoha, baadhi ya matatizo yanayoandama mfumo wa utoaji kozi ni ukosefu wa utafiti wa kutosha kuhusu manufaa yake na ushindani usiofaa miongoni mwa vyuo vikuu.

Kando na hayo, vyuo mbalimbali vinatoa kozi zinazofanana, bila kuzingatia viwango vinayolingana na mahitaji ya kisasa.

Vile vile, baadhi ya kozi ambazo hazikupokea ombi la mwanafunzi yeyote ni zile kuhusu somo la dini, ustawishaji wa jamii, utatuzi wa mizozo, usimamizi wa biashara, sayansi ya mazingira kati ya zingine.

Madaktari huiba dawa za wagonjwa Migori na kuziuza TZ – Polisi

Na VIVERE NANDIEMO

MADAKTARI na walinzi katika hospitali za Kaunti ya Migori huenda wanashirikiana kuiba vifaa na dawa na kuviuza nchi jirani ya Tanzania.

Haya yalifichuka juzi baada ya polisi mjini Migori kumkamata mlinzi akiwa na vifaa vya hospitali ya rufaa ya kaunti hiyo.

Taifa Leo iligundua kwamba maafisa katika hospitali hiyo wameunda njama ya kuiba dawa na vifaa na polisi wanashuku kwamba baadhi ya maafisa wakuu, matabibu na walinzi wanahusika.

Vifaa vinavyoibwa huuziwa kliniki za kibinafsi mjini Migori na vingine katika nchi jirani ya Tanzania. Inasemekana kuwa baadhi ya madaktari wanamiliki kliniki ambazo huwa wanatumia dawa wanazoiba kutoka hospitali za umma.

Mwaka jana, Gavana Okoth Obado, alilalamika kuwa dawa na vifaa katika hospitali za umma huuzwa nchiniTanzania.

Wagonjwa katika hospitali hizo wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa dawa huku wakitumwa kuzinunua nje ya hospitali.

“Hospitali hii ni aibu kubwa. Kila wakati mtu anaambiwa akanunue dawa kwa sababu haina dawa. Hali hii imekuwa kwa muda,” alisema mkazi wa mji wa Migori.

Mnamo Jumanne, polisi walimkamata mlinzi anayeshukiwa kuwa mmoja wa wanaotumiwa kuiba dawa na vifaa kutoka hospitali ya rufaa ya Migori.

Maafisa wa polisi waliopashwa habari na umma walipata vifaa hivyo na dawa za thamani ya Sh4 milioni.

Maafisa hao walimfuata mlinzi huyo hadi katika nyumba yake na kumkamata.

“Tulipata habari kutoka kwa umma na polisi wakamfuata mlinzi hadi nyumbani kwake katika mtaa wa Oruba mjini Migori ambapo walipata vifaa hivyo,” alisema mkuu wa polisi (OCPD) Patrick Macharia.

Miongoni mwa vifaa vilivyopatikana ni mashini ya eksirei, vifaa vya kutumiwa katika chumba cha upasuaji, kompyuta na runinga.

“Mlinzi huyo atashtakiwa baada ya uchunguzi kukamilika,” alisema Bw Macharia.

Maafisa wakuu wa hospitali ya rufaa ya Migori walikiri kwamba vifaa hivyo vilikuwa mali ya hospitali hiyo.

Madaktari bondeni waruhusiwa kujifua kimasomo, watisha kugoma

MAGDALENE WANJA NA RICHARD MAOSI

ZAIDI ya madaktari 30 kutoka kaunti tano za kusini mwa Bonde la Ufa wamepokea ruhusa ya kuendeleza masomo yao wakati wa likizo.

Hii ni baada yao kutishia kugoma huku wakiwa wamepatia serikali makataa ya siku 21 kuhusu ombi lao.Wanafamasia pamoja na madaktari wa meno kupitia chama chao cha KMPDU wakiungana na viongozi katika tume zao walithibitisha haya wakisema sio jambo la kufanyiwa mzaha.

Kwa mujibu wa katibu mkuu kutoka ukanda huu Dkt Davji Atella kaunti zote sita zilikuwa zimeshindwa kutekeleza  maagano yao na idara husika kupitia (CBA), hali iliyochochea madaktari kunyimwa fursa ya kujiendeleza kimasomo wakati wa likizo pamoja na kuongezewa cheo.

Dkt Atella alieleza kuwa kaunti tano tayari zemeafikiana kuwaruhusu madaktari kuendeleza taaluma zao pamoja na kuwapandisha cheo isipokua kaunti ya Laikipia ambayo bado haijatoa maoni yake kuhusu mpangilio huu.

“Iwapo Kaunti ya Laikipia haitatupatia majibu kwa muda wa siku 21 tutaitisha mgomo wa madaktari wanaofanya kazi katika eneo hilo hadi waafikiane na matakwa ya madaktari,’’ Dkt Atella alisema.

Hata hivyo taarifa kutoka kwenye idara ya mawasiliano katika kaunti ilieleza kwamba wamekuwa wakitumia takriban milioni 10 kila mwezi kuwagharamia madaktari wanaosoma wakati wa likizo.

Pia waliongezea kwamba kwamba madaktari 20 zaidi wameongezwa ili kujaza pengo la utendaji kazi huku wakisubiri wale walio katika likizo kurejea.

‘’Tumepokea maombi 18 kutoka kwa madaktari walio katika likizo wakiomba kuendelea kulipwa wakiwa likizoni lakini jambo hili limepuziliwa na serikali ya kaunti kutokana na uhaba wa fedha pamoja na uchache wa madaktari,’’ idara ya mawasiliano kaunti ya Laikipia ilieleza huku ikiaminika zaidi ya madaktari 12 tayari wameacha kutoa huduma kabisa wakisingizia kuendeleza masomo yao.

Dkt Atella aliongeza kwamba wataendelea kujadiliana na madaktari kutoka kaunti ya Laikipia hadi watakapofikia mwafaka. Iwapo hawatakubaliana basi madaktari wataanza mgomo rasmi.

Ni hospitali chache zilizowaruhusu madaktari kuendeleza masomo kama Nakuru (13), Kericho(9), Bomet (5) na Narok (3).

Dkt Atella alionya baadhi ya hospitali zinazopanga kuwaruhusu madaktari kupata likizo kwamba hawatalipwa.

“Ni jambo ambalo ni kinyume na sheria kwani bado tunahitaji madaktari wengi tuliowaelimisha bila kuwafuta kiholela,” aliongeza. Eneo la kusini mwa bonde hili la ufa kuna madaktari zaidi ya 600.

Jaji azima madaktari wa Cuba kuanza kuhudumu Kenya

Na MAUREEN KAKAH

HATIMA ya madaktari kutoka Cuba ambao walianza kuwasili nchini juzi kuhudumu Kenya, sasa iko mikononi mwa mahakama ambayo imeagiza wasipewe vibali vya kufanya kazi Kenya.

Hii ni baada ya Mahakama ya kutatua mizozo ya wafanyakazi kuwasimamisha kwa muda kuanza kazi hadi kesi ya kupinga hatua ya serikali ya kuwaleta nchini isikilizwe na kuamuwa Juni 19.

Jaji Onesmus Makau alitoa agizo hilo akisema kwa sababu mahakama haikuthibitishiwa kwamba madaktari hao watakuwa wameanza kazi kabla ya Juni 19, hali inafaa kubaki ilivyo hadi uamuzi utolewe tarehe hiyo.

“Kwa maoni yangu, itakuwa haki mahakama inapoandika uamuzi wake, pande zote zitulie na kuwa na subira,” alisema Jaji Makau.

Aliongeza: “Kwa sasa, madaktari kutoka Cuba ambao waliajiriwa kupitia mfumo unaopingwa hawajafika katika vituo vyao vya kazi, kwa hivyo watasubiri uamuzi wa korti.”

Dkt Samson Robert Misango, ambaye ni daktari kutoka Kenya ameshtaki Waziri wa Afya, Baraza la Magavana, Mkurugenzi wa Uhamiaji na Mwanasheria Mkuu.

Dkt Misango anapinga mkataba kati ya serikali ya kitaifa, serikali 47 za kaunti na serikali ya Cuba ya kuwaleta wataalamu 100 wa afya kuhudumu nchini kuanzia Mei 30.

Analaumu serikali akidai imedanganya ulimwengu kwamba Kenya ina uhaba wa madaktari ilhali kuna madaktari wengi waliohitimu ambao hawana kazi.

Katika kesi yake anataka mahakama kuzuia idara ya uhamiaji kuwapa madaktari hao wa kigeni vibali vya kufanya kazi Kenya.

Kesi nyingine kuhusu suala hilo iliwasilishwa na Bw Samwel Nduati, Reuel Maina na Francis Thuku ambao wanadai hawana ajira. Watatu hao wanasema serikali inafaa kuwaajiri Wakenya waliohitimu kwanza kabla ya kuwaajiri raia wa kigeni.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Matibabu Dkt Jackson Kioko anatetea hatua ya serikali akisema iliwaleta madaktari hao nchini kwa sababu kuna uhaba wa madaktari.

Dkt Kioko aliambia mahakama kwamba madaktari 100 kutoka Cuba walichaguliwa kwa uangalifu na kuhojiwa ili kuthibitisha iwapo wamehitimu.

Alisema Wizara ya Afya na bodi ya kusimamia madaktari zilishiriki kuwachagua na kuwahoji madaktari hao.

Kundi la kwanza la madaktari 50 liliwasili nchini Jumanne na wengine walitarajiwa kuwasili jana.

Kundi la kwanza la madaktari wa Cuba latua nchini

Na AGGREY OMBOKI

KUNDI la kwanza la madaktari kutoka Cuba liliwasili nchini Jumanne usiku. Ndege ya KLM iliyokuwa imewabeba madaktari hao ilitua katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) saa tatu na dakika 47.

Kuwasili kwao kunatimiza mkataba uliotiwa saini baina ya Kenya na Cuba kuruhusu madaktari 100 spesheli kutoka taifa hilo la Caribbean kuja nchini kufanya kazi kwa kandarasi.

Mpango huo umeshutumiwa vikali na madaktari wa humu nchini.

Madaktari hao wa Cuba walilazimika kusubiri kwa zaidi ya saa mbili kukamilisha taratibu za idara ya uhamiaji kwa abiria wanaowasili kwenye uwanja huo.

Baada ya ukaguzi walifululizwa hadi mabasi yaliyokuwa yakiwasubiri na kuondoka mara moja.

Walipokewa na Naibu Waziri wa Afya Rashid Aman, Mkurugenzi wa Matibabu Jackson Kioko na Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o.

Kundi la pili la madaktari linatarajiwa kuwasili nchini Alhamisi, Juni 7, 2018.

Dkt Aman alisema matabibu hao watapokea mafunzo katika Taasisi ya Mafunzo ya Serikali ili kupata ufahamu wa mfumo wa matibabu humu nchini.

Alieleza: “Madaktari hao watapokea mafunzo jinsi mfumo wetu wa matibabu hufanya kazi kabla kutumwa katika vituo mbalimbali vya afya katika kaunti kadha.

“Lengo kuu la kuwaleta madaktari hawa ni kujifunza kutokana na tajriba ya Cuba ya kukuza mfumo imara wa matibabu ambao umewezesha taifa hilo kutoa huduma za matibabu za bei nafuu kwa wananchi wote.”

Kwa upande wake, alieleza naibu waziri, Kenya itatuma madaktari wake 50 nchini Cuba ili kupokea mafunzo katika tiba ya familia.

“Kama sehemu ya mkataba wa makubaliano tuliotia saini na Cuba, tutatuma madaktari wettu 50 ili wakajifunze kuhusu mfumo wa matibabu wa Cuba ambao umewezesha kutoa huduma za matibabu kwa wananchi wake wote. Kundi hilo litajumuisha daktari mmoja kutoka kila kaunti zote 47,” akasema.

Dkt Aman aliwaomba Wakenya kuwapa fursa madaktari hao kufanya kazi licha ya shutuma nyingi zilizotolewa.

“Kumekuwa na habari hasi kuhusu mkataba lakini tunaamini madaktari hao wako na jukumu muhimu la kutekeleza katika mfumo wetu wa matibabu.”

Madaktari wa Cuba kutua nchini Mei 28 kuhudumia wagonjwa mashinani

Na CECIL ODONGO

WIZARA ya Afya Jumatatu ilitia saini makubaliano kati yake na Baraza la Magavana kuhusu ushirikiano wa kiafya na kuweka mpango mahususi kuhusu jinsi madaktari 100 wataalam kutoka nchi ya Cuba watakavyohudumu hapa nchini.

Waziri wa Afya Sicily Kariuki alisema Madaktari hao ambao watahudumu kwa kandarasi ya miaka miwili, wanatarajiwa kutua hapa nchini tarehe 28 mwezi huu na kupelekwa kaunti mbalimbali ili waanze kutoa huduma katika hospitali mbalimbali.

Bi Kariuki alisisitiza kwamba kwa kuwa sekta ya afya iligatuliwa hawakuwa na jingine ila kuwashirikisha baraza la magavana katika mpango huo na kuongeza kwamba serikali kuu imehakikisha madaktari wote 100 wanaumilisi wa lugha ya Kiingereza ili kurahisisha mawasiliano kati yao na wenzao nchini.

Kulingana na waziri huyo madaktari 50 kutoka hapa nchini pia wanatarajiwa kusafiri hadi Taifa la Cuba kwa mafunzo spesheli ya kitaaluma katika mpango maalum wa kubadilishana ujuzi kati ya Kenya na Cuba mwezi Septemba mwaka huu.

“Bodi yetu imewakagua madaktari wote 100 kutoka Cuba na tumethibitisha wanauelewaji mpana wa lugha ya Kiingereza. Pia madaktari wetu 50 watasafiri hadi India kwa mafunzo ya kipekee ya ubadilishanaji wa ujuzi wa kitaaluma baadaye Septemba,” akasema Bi Kariuki.

Madaktari hao wanatarajiwa kutoa huduma spesheli na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaosafiri kutoka mbali kupata huduma spesheli za kiafya katika hospitali ya Kenyatta na ile ya rufaa ya Moi.

Hata hivyo hatua ya madaktari hao kuajiriwa kwa kandarasi hapa nchini imezua pingamizi kubwa kutoka kwa viongozi wa Chama cha cha Madaktari nchini(KMPDU) ambao wamesisitiza kwamba serikali kwanza ingewapa ajira madaktari 1200 wa hapa kabla haijawaleta wengine kutoka Cuba.

Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt Ouma Oluga amekuwa katika mstari wa mbele kupinga hatua hiyo ya serikali akisema Kenya ina madaktari wataalam wa kutosha ila tu serikali haiwathamini na haitaki kuwapa kazi.

Majuzi Dkt Oluga alilalamika kwamba serikali imeonyesha kutowajali madaktari nchini kwa kujishughulisha na kuwaleta wa nje na kufumbia macho mgomo unaoendelea wa wahadhiri ambao madaktari wanachama wa KMPDU wanashiriki.

Madaktari watoa sindano 7 kutoka tumbo la mtoto

TITUS OMINDE na DENNIS LUBANGA

MADAKTARI katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) mjini Eldoret wamefanikiwa kutoa sindano saba kutoka tumboni mwa mtoto wa miaka mitatu.

Mtoto huyo alilazwa hospitalini humo kutoka katika kaunti ya Pokot Magharibi siku tatu zilizopita.

Upasuaji huo wa saa moja na dakika 45 uliongozwa na Prof Robert Tenge ambaye anasimamia kitengo cha upasuaji watoto hospitalini humo.

Kwa mujibu wa Prof Tenge, sindano sita zilikuwa zimekwama katika maini huku sindano nyingine ikiwa imekwama katika utumbo.

Profesa Tenge alisema historia ya afya ya Dorcas Chepchumba ilionyesha kuwa amekuwa akiishi na sindano hizo za kushona nguo tumboni mwake kwa mwaka mmoja uliopita.

Sindano hizo ziligunduliwa alipolazwa katika hospitali ya kaunti ya West Pokot mjini Kapenguria mapema wiki jana akilalamikia maumivu ya tumbo.

Uchunguzi wa x-ray hospitalini humo ulibaini mtoto huyo alikuwa na sindano tumboni mwake kabla ya kuelekezwa katika hospitali ya MTRH kwa upasuaji.

“Tulipokea mtoto huyo na kumfanyia uchunguzi ambapo tulibaini kuwa alikuwa na sindano tumboni mwake, kabla ya kuanzisha mikakati ya kutoa sindano hizo tumboni humo,” alisema Profesa Tenge.

 

Wagonjwa wanafariki tukitazama, serikali iwajibike – Madaktari

Na PETER MBURU

MADAKTARI katika Hospitali ya Rufaa ya Nakuru Level Five wamekiri kuwa wagonjwa wamekuwa wakifariki humo kutokana na subira ya muda mrefu bila kuhudumiwa.

Madaktari hao walisema kuwa wagonjwa wanaofika kwenye kifaa hicho cha afya wamekuwa wakisubiri kati ya siku mbili na tatu bila kuhudumiwa, jambo ambalo limesababisha vifo vya watu wengi.

Taarifa hizo za kushtua zimerejesha kumbukumbu za malalamishi ambayo yamekuwepo kuwa wagonjwa katika hospitali hiyo wamekuwa wakipokea huduma mbovu.

Madaktari hao walilaumu uhaba  wa wafanyakazi kwa matatizo yao, wakidai kuwa japo ni hospitali ya rufaa, imekuwa ikifanya kazi kama zahanati.

Baadhi ya sehemu walizosema zimeathirika ni wanakozalia kina mama, sehemu za kufanyia upasuaji, kunakopigiwa picha za X-rei na sehemu za wagonjwa mahututi.

Walisema hayo walipotoa ilani ya mgomo utakaoanza wiki ijayo, wakilalamikia uhaba wa madaktari katika kaunti hiyo, kukosa kupandishwa vyeo kwa muda mrefu na kunyimwa bima ya afya.

 

‘Hatuwezi kuwasaidia’

“Wagonjwa wanaaga dunia kila uchao tukitazama kwani hatuwezi kuwasaidia. Baadhi ya wagonjwa wanakaa kati ya saa 48 na 72 bila kumwona daktari,” akasema Dkt Davji Atellah.

Daktari huyo alisema kuwa japo hospitali hiyo inayowahudumia wakazi wa kaunti sabaa kwa kuwa ni ya rufaa inafaa kuwa na zaidi ya madaktari 200, kwa sasa ina 20 pekee.

Madaktari hao walizidi kusema kuwa upungufu wa madaktari umepelekea baadhi ya idara kuwa na mtaalamu mmoja pekee, ilhali idadi ya wagonjwa wanaotafuta huduma ni kubwa kupita kiasi.

Walisema japo serikali ya kaunti ilinunua vifaa vya afya na kupeleka katika kifaa hicho, vimesalia kuwa maridadi tu kwa kuwa hakuna wafanyakazi wa kuvitumia.

Hii, walisema, ni licha ya hospitali nyingine kaunti hiyo kukumbwa na matatizo sawa, wakisema ile ya Subukia Level Four ina wodi zisizotumika kutokana na ukosefu wa madaktari na wahudumu wengine.

 

Miaka 4 bila likizo

Baadhi ya madaktari walieleza Taifa Leo kuwa wamekaa zaidi ya miaka minne bila kwenda likizo wala kupata siku za kupumzika, wakisema hali hiyo iliadhiri utendakazi wao na maisha yao ya kifamilia.

“Tunajua si haki kwetu kugoma kila wakati kwani hatukwenda shuleni ili tuwe tukigoma lakini serikali inatusukumia kufanyia kazi katika mazingira magumu sana na hali hii inatuweza sasa,” akasema Dkt Carolyne Masete.

Walizidi kulalamika kuwa kaunti hiyo haijafanya zoezi la kupandisha madaktari mamlaka tangu 2015, suala walilosema limeadhiri utendakazi wao.

Hii, walisema, ni licha ya wengi wao kunyimwa bima ya afya, ambayo walisema ni haki yao.

“Kwa sababu hizi, kuanzia Mei 3, madaktari kaunti hii watagoma ili kupigania tupewe haki zetu za kufanyia kazi katika mazingira mema,” akasema Dkt Atellah.

Hata hivyo, mkuu wa hospitali ya Nakuru Level Five Joseph Mburu alipinga madai ya wagonjwa kufia katika kifaa hicho kwa kukosa kupewa huduma, akiyataja kuwa yenye makosa na ya uongo.

“Tuna vifaa vyote vya kuwahudumia wagonjwa kuanzia wanapoingia hospitalini hadi wanapofikishwa kwenye wodi, na wanapofika humo hawamalizi dakika 15 bila kuonwa na mhudumu wa afya,” akasema Dkt Mburu.

Waziri atetea ajira ya madaktari kutoka Cuba

Na CECIL ODONGO

WAZIRI wa Afya Bi Sicily Kariuki amekanusha kwamba madaktari 100 wataalam kutoka Cuba wanaotarajiwa hapa nchini watatoa ushindani na kusababisha ukosefu wa kazi kwa zaidi ya madaktari 1200 ambao hawana ajira.

Kulingana na waziri huyo, madaktari hao, watakaoajiriwa kwa mkataba wa miaka miwili watawapa ujuzi madaktari wa Kenya kuhusu uendeshaji wa sekta ya afya nchini kwao na kupendekeza uboreshaji wake hapa nchini.

“Madaktari hao kando na kutoa huduma spesheli katika hospitali zetu, watakuwa na wajibu wa kuwanoa madaktari wa nyumbani na kuwapa ujuzi wa kuimarisha sekta ya afya hapa kwetu,” akasema waziri huyo.

Alisema kwamba mfumo wa ugatuzi umesaidia kutekeleza mabadiliko na kusaidia kupanuka kwa taasisi zinazotoa huduma za afya karibu na mwananchi.

“Hospitali zetu kuu zina msongamano mkubwa wa wagonjwa kwa hivyo lengo letu kuu ni kugatua huduma hadi zile za mashinani na kuwahamasisha wananchi kuamini huduma zao,” akasisitiza.

Waziri huyo alikuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa warsha ya siku tatu ya afya katika hoteli ya Laico Regency mada kuu ikiwa ni ‘Namna ya kuhakikisha huduma sawa ya afya kwa wote.’

Naibu Gavana wa Isiolo Abdi Ibrahim ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa Kamati ya afya katika Baraza la magavana Dkt Mohamed Kuti alisema kwamba kaunti zinakabiliwa na changamoto ya uchache wa madaktari na kwamba wanalazimika kuajiri wengine kutokana na vipindi vya mafunzo vya kila mara kwa waliokuwepo.

“Kaunti zina madaktari wachache sana, kwa mfano kaunti ya Isiolo asilimia sitini ya madaktari wetu huandaliwa mafunzo na waliosalia huwa wachache wasioweza kutoa huduma bora. Wao huchelewa kazini na kupinga juhudi zetu za kuwafanya wawajibike,” akasema.

Alikariri tamko la waziri la kuhakikisha kwamba msongamano mkubwa wa wagonjwa unaoshuhudiwa katika hospitali kubwa kama Kenyatta na ile ya Moi Eldoret utapungua iwapo serikali itawekeza katika kuiinua hospitali ndogo ndogo za mashinani.

Ilibainika wazi katika warsha hiyo kwamba sekta ya afya ina mianya kupitia taasisi zake dhaifu na ukosefu wa sheria zinazofaa kuhakikisha uwajibikaji.

Khama Rogo, ambaye ni mtaalam wa kiafya anayetambulika barani Afrika na Chansela wa Chuo Kikuu cha Moi Miriam Were walisisitiza kwamba ili nchi iweze kujinadi kuwa sekta hiyo imeimarika lazima wakenya maskini wajumuishwe kwenye mpango wa Bima ya afya.

Hospitali ambako wagonjwa wanafariki ziadhibiwe – Mahakama

Na RICHARD MUNGUTI

JAJI mmoja katika Mahakama Kuu amesema kwamba hospitali ambako wagonjwa wanafariki zinapaswa kuadhibiwa kwa kutokuwa na makini.

Jaji Roselyn Aburili alimwagiza mwanasheria mkuu , Tume ya kufanyia Marekebisho Sheria na Wizara ya Afya kufanyia marekebisho sheria ya bodi ya madaktari kwa lengo la kuzuia wagonjwa kufa ovyo ovyo kwa kupuuzwa.

Jaji Aburili alisema madaktari wengi wamekuwa na tabia ya kutojali . Alisema madaktari kama hawa wanapasa kuadhibiwa vikali kwa vile wanakaidi sheria ya kuwajali wagonjwa.

“Wagonjwa wengi wamepoteza maisha yao wakiwa mahospitali wanakopaswa kusaidika,” alisema Jaji Aburili.

Jaji huyo alisema hayo alipoamua kesi iliyowasiolishwa na jamii ya wakili aliyefia hospitalini katika sababu ambazo haziueleweka.

Katika kesi hiyo iliwasilishwa na Chama cha Hospitali nchini (KHA) na hospitali ya Nairobi zilizoshtaki bodi ya madaktari KMDB baada ya bintiye Bw John Paul Odero,  Sybil Masinde Odero kufia katika hospitali.

Sybil aliaga Feburuari 11, 2011 akiwa chini ya uangalizi wa Dkt Bartilol Kigen. Sybil alifanyiwa upasuaji akijifungua kisha akafariki baada ya muda mfupi.

Jaji Aburili aliamuru waliohusika wachukuliwa hatua kali.

Utepetevu hospitalini KNH unavyomsababishia mama uchungu

Na GEOFFREY ANENE

HOSPITALI ya Kitaifa ya Kenya (KNH) inamulikwa tena kwa madai ya kumfanyia mama mmoja upasuaji vibaya wakati wa kujifungua.

Susan Nekesa anasema alitembelea hospitali hii maarufu akihisi uchungu wa uzazi Januari 25 na kujifungua watoto wawili pacha siku iliyofuata.

Hata hivyo, saa chache baada ya upasuaji huo, tumbo lake lilivimba na akaanza kusikia maumivu makali.

Uchungu aliohisi, aliambia runinga ya Citizen, ulikuwa mbaya sana kiasi cha kumfanya asiongee.

Katika ripoti yake, Nekesa anajikokota kukaa kwenye kitanda chake, huku machozi yakimtoka.

Huku akilia, anasimulia kisa hicho akisema, “Naomba Mungu nisipoteze uwezo wangu wa kukumbuka.”

“Nilipokuja kumuona, nilipata amefura tumbo,” dadake Nekesa, Evelyn Anindo anasema.

“Tumbo lake pia lilikuwa moto sana na hakuwa anaweza kuzungumza. Tuliwasiliana kupitia ishara.”

Baada ya kulalamikia maafisa wa matibabu wa KNH, Nekesa alirudishwa katika chumba cha kufanyiwa upasuaji, na ni wakati huo madaktari walikiri walikuwa wamefanya kosa.

“Iligunduliwa kwamba upasuaji ulifanywa vibaya,” anasema Robert Sitati, bwanake Nekesa.

“Sehemu ya matumbo madogo, karibu sentimita 50, ilikuwa nje ya mahali inatakiwa kuwa,” anasema.

Kurekebisha hali hiyo, madaktari waliondoa sehemu iliyoathirika na kuacha mwanya mdogo (unaoitwa stoma) kumwezesha kupitisha uchafu kupitia mfuko maalum (colostomy).

Mgonjwa huyu pamoja na familia yake walisalia na matumaini kuwa atapata afueni na kurejea nyumbani na watoto hao pacha.

Ndani ya Hospitali Kuu ya Kenyatta. Picha/Hisani

Hata hivyo, familia ilipokea habari za kuhuzunisha Jumanne kwamba mtoto mmoja ameaga dunia.

“Walisema kwamba mtoto wangu alikuwa na shimo kwenye moyo wake,” anasema Nekesa kwa huzuni.

Hata hivyo, mumewe Nekesa anasema aliambiwa na mfanyakazi mmoja wa KNH kwamba mtoto wao alisongwa na maziwa.

“Mtu aliniambia kwamba mtu aliyekuwa akimpa mtoto wangu maziwa hakuwa na ujuzi,” Sitati anasema.

Kilichofuata masaibu ya Nekesa, ambaye anaomboleza kifo cha mtoto wake, ni kipindi cha huzuni, kutelekezwa na machungu dhidi ya madaktari wa KNH, ambao hawakufanya kazi yao vyema.

“Hakuna anayemshughulikia,” anasema Anindo.

“Mfuko huo maalum ukijaa, mzigo ni wake mwenyewe kujikokota hadi kwenye chumba cha kujisaidia kuufanya uwe tupu.”

Kwa wakati huu, familia yake imeshindwa la kufanya, huku hospitali hii ikiwaomba wawe na subira kwa sababu haina washauri wa kushughulikia Nekesa.

Mapema mwezi huu wa Machi, madaktari wanaojiongeza masomo waligoma baada ya wenzao kusimamishwa kazi kwa muda kutokana na upasuaji wa kichwa uliofanyiwa mgonjwa tofauti na yule alistahili kufanyiwa.

Sitati anasema hospitali hiyo imemuonya dhidi ya kuhamisha mke wake ikisema atalipia ada yote ya hospitali mwenyewe akiondoka KNH.

Nekesa anatumai siku moja atapata kuona watoto wake tena. “Wameniweka hapa kwa muda mrefu sana…Nimekuwa nikivumilia nikitumai kwamba siku moja nitaenda kuona watoto wangu,” anasema.

KNH mashakani tena kufuatia upasuaji ovyo wa utumbo

Eneo la matibabu ya dharura katika Hospitali Kuu ya Kenyatta jijini Nairobi. Picha/ Maktaba

Na BENSON MATHEKA

HOSPITALI Kuu ya Kenyatta imejipata mashakani tena kufuatia madai kwamba mwanamke aliyekuwa akijifungua kupitia upasuaji aliathirika baada ya kupasuliwa visivyo.

Mwanamke huyo, Susan Nekesa anasema alifika katika hospitali hiyo Januari 25 na akajifungua siku iliyofuata.

Hata hivyo saa kadhaa baada ya upasuaji, tumbo lake lilivimba na akapata maumivu makali.

Akiongea na runinga ya Citizen Jumatano, mwanamke huyo alisema maumivu yalimzidi akashindwa kuongea.

Kwenye mahojiano na runinga hiyo Nekesa alionekana akitatizika kuketi kitandani huku akitokwa machozi na kusema anachoomba ni asipoteze uwezo wa kukumbuka mambo.

“Nilipokuja kumuona, nilipata tumbo lake likiwa limevimba. Tumbo lilikuwa na joto sana na hangeweza kuongea,” dadake Evelyn Anindo, alisema.

Alipolalamikia hospitali ya KNH, Nekesa alirudishwa katika chumba cha upasuaji na madaktari wakakiri kwamba walikuwa wamefanya makosa.

“lligunduliwa kuwa upasuaji haukuwa umefanywa vyema,” alisema Robert Sitati, mume wa Nekesa.

“Sehemu ya utumbo wake, yaani sentimita 50 ilikuwa nje ya unapopaswa kuwa,” alisema.

Ili kurekebisha hali, madaktari walitoa sehemu iliyoathiriwa na kuacha shimo ndogo

( inayofahamika kama stoma) ili aweze kupitishia choo kupitia mfuko. Familia yake iliomba aweze kupona  ili aruhusiwe kwenda nyumbani na watoto wake pacha.

Hata hivyo, mnamo Jumanne familia ilifahamishwa kuwa mmoja wa watoto hao alikuwa amekufa.

 “Walisema mtoto wangu alikuwa na tundu kwenye roho,” alisema Nekesa kwa uchungu.

Hata hivyo, mumewe alisema alifahamishwa na mfanyakazi wa KNH kwamba mtoto huyo alilishwa na mtu asiyekuwa na ujuzi wa kulisha watoto akasakamwa na maziwa kooni.

Huku akiendelea kuomboleza kifo cha mtoto wake, Nekesa anakabiliwa na wakati mgumu na uchungu kwa madaktari anaodai wamempuuza hata baada ya kusababishia hali hiyo.

 “Hakuna anayemshughulikia,” alisema Evelyn.

Baada ya mfuko anaotumia kupitishia choo kujaa, ni yeye anayeng’ang’ana kwenda chooni kutupa uchafu.

Familia yake imechanganyikiwa huku hospitali ikiwafahamishwa kuwa haina wataalamu wa kumhudumia  na kuwataka wawe na subira.

Sitati anasema hospitali imemuonya dhidi ya kumhamishia mkewe hospitali nyingine .

KNH yarudisha kazini madaktari iliyowasimamisha kazi

Na BERNARDINE MUTANU

HOSPITALI ya Kenyatta (KNH) Alhamisi ilibatilisha barua za kuwasimamisha kazi madaktari wawili walio katika mafunzo na waliohusika katika kisa cha upasuaji wa ubongo wa mgonjwa asiyehitaji wiki iliyopita.

Hospitali hiyo ilichukua hatua hiyo na kuwasihi madaktari wote waliogoma kurudi kazini.

“Bodi imesimamisha kabisa hatua za kinidhamu dhidi ya madaktari hao.  Tumeachia jukumu hilo bodi ya chama cha madaktari,” alisema mwenyekiti wa bodi ya KNH Bw Mark Bor wakati wa mkutano wa wanahabari Alhamisi.

Bodi ya KNH ilikutana na KMPDB pamoja na Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki kujadili suala hilo ambalo lilifanya madaktari wote walio katika mafunzo kugoma na kuathiri shughuli za afya hospitalini humo.

Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki alipohutubu baada ya kubatilisha barua ya kuwasimamisha kazi madaktari waliofanya upasuaji kimakosa. Aliwataka madaktari wote waliogoma kutokana na suala hilo kurejea kazini. Hii ni baada ya kuafikiana na KMPDU. Picha/ Bernardine Mutanu

Hii ni baada ya daktari aliyehusika katika kisa cha upasuaji wa ubongo, lakini kwa mgonjwa ambaye hakuhitaji upasuaji huo, kusimamishwa kazi na KNH.

“Tunawaomba madaktari kurudi kazini, tunawathamini na kuheshimu kazi yenu,” alisema Bw Bor na kuongeza kuwa bodi hiyo pia itafanya mkutano na Baraza la Wauguzi ili kuafikiana kuhusu wauguzi wawili waliosimamishwa kazi.

Kulingana na Waziri wa Afya Bi Kariuki, kisa hicho kinachunguzwa na shirika la nje na kulitaka kutia juhudi ili kumaliza uchunguzi huo.

“Ninatarajia bodi ya KNH itashirikiana na KMPDB kwa kutoa habari inayohitajika katika uchunguzi,” alisema Bi Kariuki.

Lakini alikataa kuzungumzia suala la Mkurugenzi Mkuu wa KNH Bi Lily Koros, ambaye alimsimamisha kazi kuhusiana na suala hilo.

Kusimamishwa kazi kwa Bi Koros kumezua mjadala mkubwa wa kisiasa, suala ambalo mwenyekiti wa KMPDB Prof George Magoha alisema hangeingilia.

“Kutoka kwa bodi, tunataka madaktari kurejea kwa sababu hatutaki kuwa na vifo vinavyoweza kuepukika,” alisema, na kutoa ombi kwa KNH kubatilisha barua dhidi ya daktari aliyehusika.

“Tumepokea faili zote zilizo na ripoti kuhusiana na suala hilo, tunataka kurejea kwa madaktari kurejea kwa nia nzuri, tunataka kufanya haki kwa sababu lazima wahusika wasikilizwe,” alisema Prof Magoha.

TAHARIRI: Wizara ya Afya ichunguze tatizo la Hospitali Kuu ya Kenyatta

Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki alipohutubia wanahabari katika Hospitali Kuu ya Kenyatta baada ya madaktari kumpasua kichwa mgonjwa kimakosa. Picha/ Maktaba

TUKIO la hivi punde ambapo madaktari katika Hospitali Kuu ya Kenyatta walimfanyia upasuaji mgonjwa ambaye hakustahili upasuaji huo, ni jambo ambalo limewashangaza wengi na kuibua hisia mseto.

Katika siku za hivi punde matukio kadhaa yamejitokeza katika hospitali hii kuu, ambayo ni pamoja na wizi wa mtoto mchanga pamoja na madai ya wanawake wanaojifungua kubakwa.

Madai haya ni yale ambayo huenda yamefaulu kujitokeza hadharani ila pana uwezekano mkubwa kuwa hospitali hii imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingine tele.

Matukio haya yanahitaji uchunguzi wa kina kuhusiana na utendakazi wa kila mtu aliyeajiriwa hapo na vigezo vyake vya kuhakikisha usalama, sio tu wa wagonjwa bali hata wao wenyewe, vinadumishwa.

Hospitali hii inahudumia idadi kubwa ya wagonjwa na itakuwa vyema kwanza kubainisha ni mambo yepi ambayo huenda yakaelekeza mgonjwa kukosa kutambulishwa vilivyo na kuishia kufanyiwa upasuaji ambao hakustahili.

Hii ni kwa sababu endapo kuna tatizo lazima lichunguzwe na sio kuanzia wakuu pekee kwa sababu kila mmoja amepewa majukumu yake anayostahili kuyatekeleza vilivyo.

Madai ya ubakaji yalipoibuka, hospitali iliongeza walinzi mbali na kuahidi kutekeleza hatua nyinginezo.

Ni muhimu kwa wizara ya Afya kuangalia kwa kina jinsi hospitali hiyo inavyoendesha kazi zake, hasa kwa kuwa imekuwa ikilalamika kuhusu idadi kubwa ya wagonjwa, baadhi ambao wanaweza kutibiwa katika hospitali za kaunti na kutumwa huko tu iwapo kuna hitaji la matibabu maalum.

Hospitali ya Kenyatta inahudumia wagonjwa kutoka Afrika Mashariki na Kati na ni muhimu utendakazi wake uwe wa hali ya juu.

Lakini kwa hilo kufanyika lazima mazingira hayo ya kufanya kazi yaimarishwe pamoja na kutiliwa maanani ili kuhakikisha kuwa watu wanawajibika na kuwa na motisha ya kutoa huduma bora.

Tukio hilo la upasuaji bila shaka limeibua maswali mengi, na wizara badala ya kuwaomba radhi Wakenya inastahili kuwaeleza jinsi inavyolenga kuhakikisha kuwa baadhi ya matukio haya hayataibuka tena.

Serikali lazima iweke mikakati kabambe ya kuimarisha hospitali hii kwa kuhakikisha kuwa inajali maslahi ya wahudumu, wafanyakazi pamoja na kuajiri kulingana na ufaafu wa watu kwa nafasi hizo.

Inastahili pia kufuatilia kwa karibu shughuli zake kwa lengo la kuiboresha na kuitengea pesa za kutosha ili baadhi ya matukio yaweze kuepukwa.

WASONGA: Madaktari waliounganisha mkono wanafaa kutuzwa

Muuguzi na Afisa Mkuu wa Hospitali ya KNH jijini Nairobi wamtazama Joseph Theuri baada ya kuunganishwa mkono.
Picha/ Maktaba

Na CHARLES WASONGA

Kwa Muhtasari:

  • Joseph Theuri alikimbizwa katika hospitali hiyo baada ya kukatwa mkono na mashine ya kusaga chakula 
  • Upasuaji uliodumu kwa saa 23 uliendeshwa na kundi la wataalamu 23
  • Wataalamu hao wanafaa kujumuishwa kwenye orodha ya Wakenya ambao watapokea tuzo za kitaifa mwaka huu
  • Wamedhihirishia ulimwengu kuwa hakuna haja kwa Wakenya kusafiri nje ya nchi kusaka huduma kama hizo

KWA mara nyingine, Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) iliandikisha historia kwa kufanikiwa kuunga vipande vya mkono wa mwathiriwa aliyepelekwa humo kwa matibabu maalum.

Mgonjwa huyo, Joseph Theuri, 17, kutoka Kiambu, alikimbizwa katika hospitali hiyo baada ya kukatwa mkono na mashine ya kusaga chakula cha mifugo.

Upasuaji ulifanyawa na kundi la madaktari wakiongozwa na Catherina Kahiga na Ferdinand Nakole.
Itakumbukwa kuwa miaka miwili iliyopita (2016) madaktari wa KNH walifaulu kuwatengenisha pacha wawili waliokuwa wameshikana kiunoni.

Upasuaji huo uliodumu kwa saa 23 uliendeshwa na kundi la wataalamu 23 wakiongozwa na Mkuu wa Idara ya Upasuaji katika Shule ya Mafunzo ya Matibabu katika Chuo Kikuu cha Nairobi Prof Nimrod Mwangombe.

Kwa hakika wataalamu hawa wanafaa kutuzwa kwa kazi nzuri na kudhihirishia ulimwengu kwamba Kenya ina madaktari waliobebea si haba katika upasuaji.

Wataalamu hao wanafaa kujumuishwa kwenye orodha ya Wakenya ambao watapokea tuzo za kitaifa mwaka huu, kwa machango wao katika kuboresha maisha ya wanajamii na Wakenya kwa jumla.

Ni aibu kuwa Profesa Mwangombe na wenzake, walifanikisha upasuaji uliwatenganisha watoto hao wa kike kwa majina, Blessing na Favour, hawakuwa miongoni mwa Wakenya 54 waliopokea tuzo hizo kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2017.

Badala yake orodha hiyo ilijaa watu ambao mchango wao kwa jamii ni wa kutiliwa shaka kama vile Bw Martin Kamotho, al maarufu “Githeri Man”.

Ufanisi ambao umeandikishwa na madaktari wa KNH, hasa katika nyanja ya upasuaji, unafaa kuisukuma serikali kuwekeza hela nyingi katika ununuzi wa vifaa vya kisasa katika taasisi hiyo na na hospitali zingine za ngazi ya kaunti.

Hii ni kwa sababu wataalamu hao wamedhihirishia ulimwengu kuwa hamna haja kwa Wakenya kusafiri nje ya Kenya kusaka huduma kama hizo kuwa wana uwezo na ujuzi wa kutoa huduma hizo humu nchini na kwa bei nafuu.

Lakini sharti vifaa maalum na mazingira faafu ya utendakazi, kando na motisha uwepo. Naamini kuwa Kenya ina uwezo wa kutibu magonjwa mengine sugu kama saratani, kisukari na maradhi ya moyo.