WARUI: Tuzo ya Nobel ya Abdulrazak ushindi kwa elimu Afrika

Na WANTO WARUI

KWA mara nyingine tena tuzo inayoenziwa sana kote ulimwenguni imerudi katika eneo letu la Afrika Mashariki mara hii katika sekta ya elimu kwa Mtanzania Abdulrazak Gurnah.

Gurnah, mwenye umri wa miaka 72 ameshinda tuzo hiyo kutokana na uandishi wake wa fasihi usiyotetereka juu ya masuala ya ukoloni na ukimbizi.

Mnamo 2007, mwandishi Doris Lessing kutoka Zimbabwe alishinda tuzo hiyo akiwa mwandishi wa pili Mwafrika baada ya Mnaijeria Wole Soyinka aliyeshinda mwaka wa 1986.

Itakumbukwa pia, hayati Profesa Wangari Maathai kutoka Kenya alishaweza pia kujishindia tuzo hiyo ya Nobel kutokana na bidii yake ya kulinda na kutetea mazingira.

Mwandishi Gurnah, licha ya kwamba ana makao yake nchini Uingereza ameiweka Afrika Mashariki katika ramani ya wasomi na waandishi mashuhuri wenye elimu na uandishi wa kina.

Katika vitabu vyake kumi vya riwaya alivyoandika, ameonyesha msisitizo na mapenzi makubwa ya uandishi huku akidhihirisha wazi matokeo hasi ya ukoloni na athari za ukimbizi kwa jamii zinazohusika.

Gurnah, ambaye ameandika vitabu kama vile Paradise ameonyesha ukakamavu mkubwa katika kukosoa sera mbaya za ukoloni ambazo athari zake zinasikika miaka mingi baadaye.

Abdulrazak ni mwandishi maarufu kutoka eneo hili, licha ya kuwa anaadika kwa lugha ya Kiingereza.

Alitoka huku Afrika kama mkimbizi katika miaka 1960 kutokana na mateso yaliyokuwamo dhidi ya watu wenye asili ya Kiarabu chini ya utawala wa aliyekuwa rais wa Zanzibar Abeid Karume.

Tangu wakati huo, hakuweza kurudi tena ila tu mwaka wa 1984, alipomtembelea baba yake huko Unguja kabla ya kifo chake.

Kuchaguliwa kwake kwa tuzo hii kunakuja ambapo ulimwengu umeingia katika mtafaruku mkubwa wa wakimbizi kutokana na vita, njaa na siasa.

Tuzo hii ya Nobel ya Abdulrazak inaliweka eneo hili mbele na ni ishara nzuri kwa waandishi wengi wazuri kutoka Afrika Mashariki.

Eneo hili linajivunia waandishi mashuhuri wa vitabu baadhi yao wakiwa marehemu Shaaban Robert, John Ruganda, Euphrase Kezilahabi na Ken Walibora.

Aidha, orodha ya waandishi walioko sasa ni ndefu sana wakiwa ni pamoja na Shafi Adam Shafi, Ngugi wa Thiong’o, Charles Lubega, Mohamed Said miongoni mwa wengine wengi.

Huu ni motisha mkubwa kwa waandishi wakongwe wa Afrika Mashariki ambao wanaendelea kuandika ama wale ambao kazi zao tayari zinasomwa pamoja na waandishi wachanga wanaoingia katika sekta hii ya uandishi wa vitabu.

Hakuna shaka kuwa elimu inayotolewa katika shule na vyuo vyetu ina uwezo mkubwa wa kukabiliana na matatizo ya bara hili na ulimwengu kwa ujumla.

MUTUA: Mwafrika amejihini na kujitweza mwenyewe

Na DOUGLAS MUTUA

MWAFRIKA akiwajibishwa na Mzungu hupiga kamsa na kudai anaonewa, ati msingi wa maonevu ni ubaguzi wa rangi pekee.

Madai rahisi kuaminika hayo na wasiokwangura mambo wakajua mmejificha nini msimoonekana mara moja.

Imekuwa desturi yetu tangu enzi za mkoloni kwa kuwa aghalabu hatutaki kukiri kwamba tuna matatizo ya kimsingi yanayotuhini ila hatuwezi kujizuia.

Na hatutaki kubadilika.

Kelele za kila nui zilihanikiza hewani kote barani hivi majuzi Uingereza iliposimama kidete kukatalia mbali ithibati zinazotokea Afrika zikionyesha watu wamepata chanjo za corona.

Msimamo huo wa Uingereza una maana kwamba hata ukiwasilisha cheti chako kinachothibitisha umepata chanjo zote mbili, mradi umechanjiwa Afrika, hakikubaliki.

Ama utazuiwa kuingia Uingereza au utaruhusiwa kisha ufungiwe katika hoteli maalum kwa siku 14.

Ukiwa humo utapimwa mara mbili ili kuhakikisha kabisa huna korona.

Ni Wakenya na Wamisri pekee ambao wataruhusiwa kujifungia kwa muda huo wanakonuia kukaa wakiwa Uingereza, lakini wao pia lazima wapimwe mara mbili.

Agizo hilo lilitolewa mapema wiki jana Uingereza ilipotangaza orodha mpya ya mataifa ambayo yataruhusiwa kuingia humo kwa masharti nafuu kuliko awali.

Ililegezea masharti hayo jumla ya mataifa 70, lakini bara zima la Afrika lilizimwa. Haingii mtu Uingereza kwa raha zake ati!

Agizo lenyewe lilionekana kukinzana na uhalisia wa mambo kwa kuwa Uingereza imetuma mamilioni ya chanjo hizo Afrika.

Swali kuu ni je, kwani ilitutumia chanjo dhaifu ambazo yenyewe haina imani nazo? Huenda zilikuwa bandia?

Maswali hayo yanawatia hofu wanaowahamasisha watu kuhusu umuhimu wa kupata chanjo wakati huu ambapo korona inaendelea kuangamiza.

Kisa na maana ni kwamba hata bila tangazo hilo, kuna watu wengi mno wasioziamini chanjo hizo, hivyo huko ni kutia msumari moto kwenye kidonda.

Wataziamini kamwe?

Hadi hapo, huo ndio ukweli finyu anaotaka kushikilia Mwafrika anayeamini anaonewa kwa misingi ya rangi yake.

Ametia pamba masikioni, maelezo ya ziada hataki.

Hata hivyo, ukweli wa mambo ni kwamba Mwafrika akichanjiwa kwenye mataifa ambayo yanaaminiwa na Uingereza hatazuiwa kuingia taifa hilo.

Tayari, hapo unaona kuwa tatizo si rangi ya anayejaribu kuingia Uingereza bali aliyemchanja.Kumbuka Mwingereza anatujua vizuri: akitupa msaada wa chanjo tunaweza kuuuza na kutia chupa zake maji kisha tukadanganya chanjo yake hiyo na kuwapa watu.

Anajua pia tuna uwezo wa kughushi vyeti vya kuthibitisha tumechanjwa kisha tukaviwasilisha kwake bila kupepesa macho tukitaka kuingia Uingereza na virusi mwilini.

Hivi tumeghushi shahada za vyuo vikuu kufikia uzamifu, karatasi duni ya chanjo itatushinda wapi?

Ni Afrika pekee ambako unasikia kesi za ajabu kama vile mzee mzima na mvi zake kusimama mahakamani na kukaa kimya akisubiri jaji aamue mzee ana digrii au la.

Ikiwa mzee hana, mbona mwenyewe asiseme mara moja hana? Angekuwa mkweli na mwadilifu, mwanzo kesi yenyewe haingekuwapo!

Walionunua digrii Uganda bila kusoma hata siku moja wakaishia kuchaguliwa magavana na kugeuka vingang’anizi katika suala zima la ‘ninayo – hunayo’ unawajua.

Pia walioghushi digrii za vyuo vikuu vya nchini Kenya wakawa magavana, pekuzi za kina zilipotishia kuwasomba wakakimbilia kwa vigogo kutakaswa na kukingwa unawajua.

Ni Afrika pekee ambako mradi ana mafedha, mtu ataghushi cheti cha kifo chake ili atoroke jela, ausadikishe umma umchague, kisha akivuruga mambo ajisingizie Ukimwi ili asifungwe!

Ni Afrika pekee ambako viongozi hutajirika kuliko mataifa wanayoongoza, na kwa kuwa hawaziamini serikali zao hizo wanachimba mashimo ughaibuni na kufukia mafedha hayo!

Ili atie akili, Mwafrika anahitaji kuwekewa vikwazo vya kumuumiza na kumtenga na ulimwengu wa wastaarabu. Huko ndiko kumzuia mtu kujihini mwenyewe. Kunafaa.

mutua_muema@yahoo.com

KAMAU: Kenya iziige nchi nyingine duniani kulinda tamaduni zake

Na WANDERI KAMAU

MOJA ya changamoto kuu zinazokikumba kizazi cha sasa nchini ni ukosefu wa ufahamu wa lugha zao asili.

Ingawa lugha hizo humpa mtu utambulisho halisi kuhusu asili yake, inashangaza kwamba kizazi hicho kinazichukulia kama njia za “kujidunisha.”

Dhana hiyo ndiyo imejenga mtindo mpya ambapo kinyume na malezi ya awali, watoto wanalelewa kwa kulazimishwa kujifunza na kukifahamu Kiingereza pekee.

Katika mazingira hayo ya “usasa”, Kiswahili pia kinachukuliwa kuwa lugha duni! Naam, kinaonekana kuwa lugha ya watu ambao hawakuelimika, wazee na “wasioufahamu usasa.”

Binafsi, huenda fasiri yangu ya “usasa” ikakinzana na uelewa wa watu wengi.

Hata hivyo, ni wazi kuwa usasa haumaanishi jamii kusahau misingi yake ya kimaisha na utamaduni wake.

Kote duniani, kila jamii inapitia mabadiliko makubwa ya mitindo yake ya kimaisha kutokana na masuala kama mpenyo wa kiteknolojia.

Kinyume na zamani, jamii nyingi zinaendesha maisha yake kutokana na mazingira yanayosukumwa na usasa katika karibu kila nyanja.

Hivyo, ni hali isiyoepukika hata kidogo.Hata hivyo, kinyume na hali ilivyo nchini, jamii nyingi duniani zinaendelea kulinda misingi yake ya kitamaduni na kimaisha.

Kinaya ni kuwa, nyingi za jamii hizo zipo katika nchi zinazoonekana kuukumbatia usasa kwa kiasi kikubwa.

Kwa mfano, katika mataifa kama Ujerumani, lugha yao asili hadi sasa ni Kijerumani. Ni makosa kwa mtoto yeyote kukua bila kuifahamu lugha hiyo.

Kulingana na mtaala wa elimu nchini humo, Kijerumani huwa miongoni mwa masomo ya msingi ambayo kando na kuwa lugha ya msingi ya mawasiliano, mwanafunzi huwa anatahiniwa katika kila kiwango cha elimu.

Mtindo uo huo ndio unaoendelezwa katika nchi kama Norway, Ubelgiji, Ufaransa, Ureno, Uhispania kati ya nyingine.

Hapa Afrika, baadhi ya mataifa yanayoonekana kuweka juhudi kulinda lugha zake asili ni Rwanda, Burundi na Tanzania.

Nchini Rwanda, ni lazima wanafunzi katika viwango vya shule ya msingi na upili wajifunze Kinyarwanda. Katika baadhi ya taasisi, lugha hiyo huwa miongoni mwa masomo ambayo hutahiniwa katika kiwango cha kitaifa.

Vivyo hivyo, imefika wakati kwa Kenya kuyaiga mataifa mengine kwenye juhudi za kuweka msingi wa kulinda mitindo yake ya kimaisha na kitamaduni.

Kujivika ‘usasa’ ni njia ya kukipotosha na kukipoteza kizazi kilichopo. Lazima tuweke msingi bora kuhakikisha tunaendeleza tamaduni zetu bila kusombwa na usasa.

akamau@ke.nationmedia.com

KINYUA BIN KING’ORI: Vita dhidi ya jinamizi la ufisadi viendeshwe bila ubaguzi

Na KINYUA BIN KINGORI

JUHUDI za kuhakikisha taifa limefanikiwa kupiga vita ufisadi lazima ziendeshwe kuambatana na Katiba, bila njama fiche na maonevu.

Itakuwa kosa ikiwa serikali itakuwa ikitumia ufisadi kufanikisha njama za kisiasa kwa nia ya kuzima baadhi ya wanasiasa kuwania nyadhifa mbalimbali katika Uchaguzi mkuu wa 2022.

Wabunge wetu wamekuwa wanafiki kiasi cha kutumiwa na viongozi wa vyama vyao kupitisha sheria zinazokinzana na katiba bila kuhamasisha raia waliowachagua umuhumu wa miswada wanayounga mkono, kupendekeza au kupitisha bila kujifahamisha ufaafu wake kwa taifa.

Kwa sasa kuna miswada miwili ya marekebisho ya sheria za madili na uongozi bora na uchaguzi inayofadhiliwa Bungeni na mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya uhasibu wa pesa za umma (PAC), Bw Opiyo Wandanyi aliye pia mbunge wa Ugunja ambayo ikiwa itapitishwa bila marekebisho na majadiliano zaidi Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itakuwa na mamlaka kuwazuia washukiwa wa ufisadi kugombea nyadhifa za kisiasa hasa katika uchaguzi ujao.

Je, itakuwa haki mtu kuzuiliwa kuwania udiwani hadi urais kwa kisingizio cha kutuhumiwa tu kuhusika katika ufisadi?

Je, kukabiliwa na kesi yoyote mahakamani yaweza kuwa sababu tosha kwa mtu kukosa kuidhinishwa na IEBC kugombea wadhifa wa kisiasa bila kwenda kortini kupinga uamuzi huo?

Tumeona tayari baadhi ya viongozi wa mrengo mmoja wakihangaishwa ,kushikwa na kushtakiwa kwa tuhuma za ufisadi.

Vita dhidi ya ufisadi havipaswi kuingizwa siasa, upendeleo au maonevu.

Ukweli ni kwamba baadhi ya kesi hizo huenda hazina ushahidi ila kufanikisha tu ubabe wa kisiasa.

Niambie itakuwa haki kivipi ikiwa mtu kama huyo atapigwa marufuku kuwa mgombezi wa wadhifa wowote ule kwa madai ya ufisadi na baadaye kesi yake itupwe kortini kwa ukosefu wa ushahidi toshelezi.

Katiba ya 2010 Kifungu cha 50 Ibara ya 2(a) kinasema: kila mshtakiwa ana haki ya kesi yake kusikilizwa kwa njia ya haki, ikiwemo haki ya kuaminiwa kutokuwa na hatia hadi ithibitishwe kinyume.

Hivyo, hata watuhumiwa wa ufisadi watakuwa na haki kuwania nyadhifa za kisiasa hadi kesi zao ziamuliwe, na ikiwa watapatikana na hatia watalazimika kujiuzulu nyadhifa zao.

Miongoni mwa waliopatikana na hatia ni mbunge wa sirisia John Waluke, Grace Wakhungu, Hassan Wario na wengineo.

Wanafaa kuwa wa kwanza kuzimwa kuwa wagombezi.

Wabunge wakiongozwa na Bw Wandayi wakome kujifanya malaika leo wakipitisha sheria inayoenda kinyume na katiba na kesho ya Mungu mambo yakiwabadilikia utawasikia magazetini wakilalamika na kulaumu serikali kwa kuwahangaisha.

Hatufai kukubali Bunge letu kutumiwa vibaya kupitisha sheria ambazo zitatupiliwa mbali na mahakama kama mswada wa BBI kwa kukiuka katiba yetu.

Ni kweli wafisadi hawafai kupewa nafasi kushikilia nyadhifa za umma iwe kupitia njia ya kuteuliwa au kuchaguliwa, lakini hilo kufaulu ni kupitia kuunda sheria inayoafiki hitaji la katiba na njia nyingine bora ni wananchi kuwakataa mashinani.

Mswada wa Wandayi ufanyiwe marekebisho ili uzingatie sheria na kuipa meno ya kung’ata viongozi wasiotii sheria za madili na uongozi bora.

Vita vya kupambana na ufisadi vitafaulu ikiwa serikali itaacha siasa za 2022 na kuwazuia wanasiasa wengine kuwa wagombezi kutaponza juhudi hizo zaidi na hata kuzua machafuko nchini.

KAMAU: Tamaa imegeuza Afrika kuwa ‘soko la utumwa’

Na WANDERI KAMAU

UFICHUZI wa sakata ambapo watu maarufu duniani wamekuwa wakificha mabilioni ya fedha katika akaunti za siri ng’ambo umeibua kinaya kilichopo kuhusu maana halisi ya “uhuru” barani Afrika.

Miongoni mwa watu waliotajwa kwenye ufichuzi huo ni viongozi maarufu, wanaosifika kwa kuwa “mashujaa wa ukombozi” katika nchi zao.

Kando na familia ya Mzee Jomo Kenyatta, viongozi wengine waliotajwa kuwa na akaunti za siri ughaibuni ni marais Ali Bongo (Gabon), Dennis Sassou Nguesso (Congo Brazaville) kati ya wengine.

Aliyetajwa pakubwa kwenye familia ya Mzee Kenyatta ni Rais Uhuru Kenyatta, ikizingatiwa ana umaarufu mkubwa kutokana na nafasi anayoshikilia kama rais wa Kenya.

Ingawa ufichuzi haumaanishi viongozi hao walipora fedha hizo kutoka nchi zao, kinaya ni kuwa umedhihirisha watu maskini wataendelea kuteseka katika lindi lao, huku matajiri wakizidi kuogelea katika bahari ya mamilioni ya pesa.

Lengo kuu la vita vya ukombozi katika nchi nyingi za Afrika lilikuwa kuondoa hali ambapo pengo kati ya watu maskini na matajiri liliendelea kupanuka.

Haya ndiyo maovu yaliyowakasirisha vikali Waafrika kiasi cha kuanza vita vikali kujikomboa dhidi ya udhalimu wa wakoloni.

Hata hivyo, tathmini ya matukio ambayo yameendelea katika bara hili kwa nusu karne iliyopita, yanaonyesha pengine wakati haukuwa umefika kwa wakoloni kuondoka.Kwa miaka 50 iliyopita, Afrika imebaki kama kigae.

Taswira yake imedorora.

Sekta muhimu za kiuchumi zimevurugika kutokana na utawala mbaya wa mataifa hayo.

Ni wazi kuwa hali barani humu imeathirika vibaya kuliko ilivyokuwa chini ya wakoloni.Kwa mfano, licha ya Kenya kuwa chini ya utawala wa Waingereza kati ya 1895 na 1963, hakuna wakati ambapo kuliwahi kuripotiwa baa la njaa.

Wakati huo, kila jamii ilikuwa ikijitosheleza kwa chakula bila matatizo yoyote. Hii ni licha ya jamii nyingi kuishi kwa kuambatana na mtindo wa maisha ya kikale.

Nyakati hizo ilikuwa nadra kusikia kuna chimbuko au mkurupuko wa maradhi hatari kama vile saratani, malaria au virusi vya corona.

Watu walikuwa wenye afya.

Hakukuwa na hospitali nyingi sababu wanajamii walikuwa wakila vyakula asili.Maisha yalikuwa shwari licha ya uwepo wa ukatili, dhuluma na mateso ya wakoloni.

Lakini hali iligeuka baada ya Waafrika kuchukua uongozi wa nchi zao.

Matumaini yaliyokuwepo yalibadilika kuwa vilio na majonzi yasiyoisha. Matumaini ya wananchi yakawa huzuni tupu.

Je, asili ya mahangaiko hayo ni ipi?

Ingawa wakoloni walikuwa wakatili dhidi ya Waafrika, walihakikisha wamepata mahitaji yao ya msingi kama vile chakula, mavazi na malazi.

Ukatili wao haukupita mipaka ya kushusha hadhi yao ya kibinadamu – kama kupora mali na kuielekeza kwa jamaa na familia zao pekee bila kujali hali za raia wengine.

Viongozi wa Kiafrika – maarufu kama Wakoloni Weusi – walipora kila kitu ili kufaidi familia zao huku mamilioni ya raia wakiumia.Hilo ndilo limeligeuza bara hili kuwa ‘Soko la Kisasa la Utumwa’.

Hatujajikomboa hata kidogo.

akamau@ke.nationmedia.com

NGILA: Kupotea kwa huduma za Facebook kuwe funzo

Na FAUSTINE NGILA

NINA imani kuwa iwapo kufikia sasa hujawahi kuelewa teknolojia ya blokcheni, leo utaelewa kwa kuwa jana uliathirika pakubwa kutokana na kukosa huduma ulizozoea za WhatsApp, Facebook na Instagram.

Naam, hukuweza kutuma picha, video au gumzo la vikundi vya WhatsApp ulivyozoea, hukuweza kuchangia kwenye mada katika kurasa za Facebook huku picha zako ulizotengea Instagram zikisalia kwa simu bile yeyote kuziona.

Najua ulipigia marafiki kadhaa kujua iwapo pia walikuwa na tatizo hilo, kabla ya mashirika ya Habari kukuarifu kuwa huduma zote za kampuni ya Facebook zilikuwa na kasoro.

Zilisalia kuzimwa kwa zaidi ya saa sita, na kurejea usiku wa manane huku ripoti ya gazeti la Fortune ikifichua kuwa kampuni hiyo ilipoteza takribani Sh11 bilioni kutokana na hali hiyo.

Hii imenichochea kufikiria kuhusu jinsi intaneti na kampuni za huduma za mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter, Google (YouTube), Microsoft (LinkedIn) na WeChat zinavyoweza kujiokoa kutokana na hali hii iwapo zitapanua akili na kufikiria kuhusu uwezo wa blokcheni.

Kimsingi, huduma za WhatsApp, Messenger, Instagram na Oculus zilipotea kwa kuwa huduma za mtandao wa Facebook zilitoweka.

Hii inamaanisha kuwa huduma hizo zinategema seva za Facebook, hali ambayo haifai katika nyakati hizi za Mageuzi ya Nne ya Viwanda (4IR).

Iwapo mitandao ya huduma za Facebook ingekuwa chini ya mfumo wa blokcheni, basi baada ya Facebook kupotea, ungeendelea tu kupiga gumzo kwenye WhatsApp, Instagram na Messenger.

Mnamo Januari, mkurugenzi mkuu mtendaji wa mtandao pinzani wa Twitter, Bw Jack Dorsey alitangaza kuwa kampuni yake inafadhili mradi wa kuhakikisha kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii yanaendeshwa kwa blokcheni ambapo kila huduma inajitegemea na hivyo kuwapa wadukuzi ugumu wakati wananuia kuangusha huduma.

Mradi huo kwa jina BlueSky ni mfano wa jinsi wadau katika sekta ya teknolojia duniani wanavyofaa kuanza kuchukulia jambo hili kwa uzito kwa kuwa mustakabali wa matumizi ya huduma za intaneti uko kwenye mifumo isiyoweza kutatizwa.

Ikumbukwe kuwa kutokana na kupotea kwa huduma za Facebook jana usiku, biashara nyingi zilipoteza mapato, hali inayopunguza mapato ya mataifa pia.

Twitter ilipata matatizo pia.

Kukosa kutumia blokcheni kunamaanisha kuwa suluhu ambazo Facebook imejitahidi kuletea wateja wake wapatao zaidi ya bilioni tatu kama Facebook MarketPlace, WhatsApp for Business na Instagram zilisalia bila maana kwa saa sita.

Ukiangalia intaneti ya sasa, inahusu viungo vingi vilivyounganishwa pamoja, kumaamisha kiungo kimoja kikifeli basi vingine vingi vitafeli kwani vinategemeana.

Watafiti wa intaneti ya blokcheni wamekuwa mbioni kuunda mifumo ya kisasa, hasa kutokana na ukosefu wa usalama wa data ya sisi ya watumizi ambayo kampuni kubwa za teknolojia zimekuwa zikivuna kutoka kwa watumizi bila idhini na kujizolea mabilioni ya faida.

Tukio la kupotea kwa huduma za Facebook ni funzo kwa serikali zote duniani kuwa kuendelea kutegemea mifumo ya kikale ya huduma za mtandao kutatuponza siku moja.

Tumejionea mengi katika nyakati za kampeni za urais, tunakumbuka jinsi sakata ya Cambridge Analytica ilivyoanika uozo katika mauzo ya data za wateja na kubatilisha chaguo la wananchi.

Dunia isipobuni mikakati ya kulinda huduma za mitandaoni dhidi ya wadukuzi au kupotea, basi tutaendelea kutarajia huduma mbovu katika siku za usoni, na kupunguza imani iliyopo kuhusu manufaa ya teknolojia.

fmailu@ke.nationmedia.com

WASONGA: Vijana wahimizwe kujisajili kwa miradi ya kuwanufaisha

Na CHARLES WASONGA

NI jambo la kusikitisha kuwa ni wakati kama huu ambapo uchaguzi mkuu unakaribia ndipo wanasiasa wametambua umuhimu wa vijana katika taifa hili.

Wanasiasa hao, haswa wale wanaotaka kiti cha urais, wamekuwa wakitumia majukwaa mbalimbali kuwahimiza vijana kujitokeza kwa wingi kujisajili kuwa wapiga kura ili washiriki uchaguzi mkuu wa 2022.

Hii ni kwa sababu inakadiriwa kuwa kati ya wapiga kura wapya 6.3 milioni ambao Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inalenga kusajili, 5.2 milioni ni vijana ambao walitimu umri wa miaka 18 kati ya 2017 na sasa.

Idadi hii ni muhimu zaidi katika kuamua mshindi katika uchaguzi wa urais katika uchaguzi huo utakaofanyika mnamo Agosti 9, 2022.

Lakini wanasiasa hawa wamedhihirisha ubinafsi katika miito yao kwa vijana wajiandikishe kuwa wapiga kura.

Hii ni kwa sababu sijawasikia wanasiasa wanaowahimiza vijana kujitokeza kwa wingi kuwania nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi huo.

Sijawahi kuwasikia Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM Raila Odinga, Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper) na wengine wanaomezea mate kiti cha urais wakiwahimiza vijana kuwania viti katika uchaguzi huo.

Hii ina manaa kuwa wanasiasa hawa wanawachukulia vijana katika watu ambao wajibu wao ni kuwapigia kura pekee na wala sio watu wanaostahiki kushikilia nyadhifa za uongozi.

Huu ni ubinafsi mkubwa.

Vijana wanafaa kushikilia nyadhifa za uongozi ili waweze kushiriki katika mpango wa utungaji sera na maongozi ya taifa hili.

Hii ni kwa sababu wao ndio huathirika pakubwa na makali ya uongozi mbaya kizazi cha sasa cha viongozi, hali ambayo imechangia wengine wao kupotoza matumaini maishani.

Ningehimiza kwamba huku wanasiasa wanapowahimiza vijana kujitokeza kwa wingi wajiandikishe kuwa wapiga kura, pia wawahimize kujiandikisha katika mipango ya serikali inayolenga kuboresha maisha yao.

Kwa mfano, vijana wahimizwe na waelekezwe kujiandikisha katika mipango ya kuwapa nafasi za ajira kama vile; Kenya Youth Employment Opportunities (KYEOP), Ajira Digital Youth Empowerment Programmes (ADYED), Presidential Digital Talent Development Youth Programmes, miongoni mwa mingine.

Mipango kama hii, inayodhaminiwa na serikali kuu, ndio inaweza kuwasaidia vijana kujiendeleza kimaisha kando na kujiandikisha kuwa wapiga kura.

Wanasiasa wakome kuendeleza dhana kwamba umuhimu wa vitambulisho vya kitaifa kwa vijana ni katika kushirikisha shughuli za kisiasa pekee.

Vijana, haswa wale wanaoishi mashambani, watambue kuwa wanaweza kutumia stakabadhi hizo za utambulisho kwa shughuli nyingine nyingi za kuboresha maisha yao kando na kupiga kura.

WANGARI: Mikakati yahitajika kupunguza mzigo wa matibabu nchini

Na MARY WANGARI

IDADI ya watu wanaoandaa hafla za uchangishaji pesa za kugharamia matibabu imeongezeka pakubwa katika siku za hivi majuzi, huku mzigo wa gharama ya afya ukizidi kuwalemea Wakenya.

Iwe ni katika sehemu za ibada, kazini, makazi, mitandao ya kijamii na kwingineko, imekuwa kama ada kila uchao kupata matangazo ya kuomba msaada kuchangisha mamilioni ya fedha kugharamia malipo ya hospitali.

Uhalisia uliopo unajitokeza bayana hasa katika kizazi hiki cha utandawazi ambao umeufanya ulimwengu kuwa kijiji.

Si ajabu siku hizi mtu kujipata katika kundi zaidi ya moja katika mitandao ya kijamii anapotakiwa kusaidia kuchangisha mradi tu kusaidia familia, jamaa au marafiki waliolemewa baada ya wapendwa wao kulazwa hospitalini.

Kwa muda mrefu, mzigo wa kugharimia matibabu nchini umekuwa kero ambayo imewafilisisha raia wengi.

Familia nyingi zimelazimika kuuza mali yao yote na kutumia kila walicho nacho katika juhudi za kugharamia matibabu ya wapendwa wao hasa wanaougua maradhi sugu.

Hali pia imevurugika zaidi kutokana na janga la Covid-19 ambalo limesababisha madhara yasioelezeka kijamii na kiuchumi.

Katika baadhi ya visa vya kuvunja moyo, familia zimegubikwa na majonzi maradufu baada ya kupatwa na msiba, kisha usimamizi wa hospitali walimolazwa hasa katika hospitali za kibinafsi, kukatalia miili ya wapendwa wao.

Ndiposa umuhimu wa kuwepo mikakati kabambe ya kuwapunguzia Wakenya gharama ya matibabu hauwezi ukasisitizwa vya kutosha.

Japo hospitali za kibinafsi huwa ghali, Wakenya hujipata hawana hiari ili kwenda huko kutafuta huduma bora za matibabu ikilinganishwa na hospitali za umma, katika juhudi za kuokoa wapendwa wao.

Serikali imepiga hatua katika juhudi za kuboresha sekta ya afya nchini kuambatana na malengo ya Afya kwa Wote (UHC).

Mfano mzuri ni kupitia mswada mpya wa NHIF unaoagiza kila mwananchi mwenye umri kuanzia miaka 18 kujisajilisha na Hazina ya Afya Nchini.

Ingawa mswada huo una vipengele kadhaa vinavyohitaji kupigwa msasa ili kuwafaidi Wakenya kikamilifu, bila shaka ni ishara njema.

Isitoshe, wiki chache zilizopita, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitoa ilani kwa hospitali za kibinafsi zinazotoza ada ghali kupindukia na kukatalia miili ya wagonjwa wanapoaga kabla ya kukamilisha malipo.

Ili kutoa afueni kwa Wakenya, Bunge linapaswa kubuni sheria zitakazoweka ada mahsusi inayostahili kuzingatiwa na hospitali za kibinafsi kuhusu utowaji huduma mbalimbali.

Serikali pia inafaa kutumia vyema ushuru unaokusanywa kutoka kwa wananchi kuimarisha huduma za afya katika vituo vya umma.

Hii ni kupitia ukarabati wa miundomsingi, kuboresha utowaji huduma za afya, kuhakikisha kuwepo kwa dawa za kutosha na vifaa vya kisasa vya matibabu.

ODONGO: Kanu ina kibarua kurejelea umaarufu wake wa awali

Na CECIL ODONGO

CHAMA cha Kanu bado kina safari ndefu kurejelea umaarufu wake wa enzi za utawala wa chama kimoja na miaka ya 90 hata baada ya kumteua mwenyekiti wake Gideon Moi kuwania Urais mwakani.

Wajumbe 3,000 wa Kanu mnamo Alhamisi wiki jana waliandaa Kongamano katika ukumbi wa Bomas ambapo seneta wa Baringo aliidhinishwa kugombea Urais mwaka 2022.

Wengi walinasibisha kongamano hilo na lile la 2002 ambalo liliidhinisha Uhuru Kenyatta kuwania kiti cha Urais wakati Daniel Arap Moi alikuwa akistaafu baada ya miaka 24 uongozini. Rais wa Pili wa Kenya alifariki Februari 2020.

Hata hivyo, ni jambo lisilofichika kuwa chama hicho kimesalia kigae na itabidi kijikaze kisabuni iwapo kina nia ya kurejelea umaarufu huo.

Ni vyema ifahimike kwamba wakati wa utawala wa Mzee Moi, ngome ya Kanu ilikuwa eneo la Bonde la Ufa japo chama hicho pia kilikuwa kikifanya vyema hata katika baadhi ya ngome za upinzani.

Hili lilikuwa dhahiri katika matokeo ya uchaguzi wa 1992 ambao ulikuwa wa kwanza baada ya mfumo wa vyama vingi kukumbatiwa nchini.

Bonde la Ufa lilichangia nusu ya kura ambazo Mzee Moi alipata katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkubwa.Katika uchaguzi huo, Mzee Moi alijizolea kura milioni 1.9 huku karibu kura milioni moja zikitoka Bonde la Ufa.

Vivyo hivyo, kwenye kura ya kutetea wadhifa wake 1997, Bw Moi alijizolea asilimia 70 ya kura za bondeni huku mpinzani wake wa karibu Mwai Kibaki akipata asilimia 20 pekee.

Hata hivyo, jinsi ilivyo kwa sasa, Seneta Moi hana ushawishi mkubwa Bondeni akilinganishwa na Naibu Rais William Ruto anayeonekana kuwa kigogo wa siasa za jamii ya Wakalenjin.

Ushawishi

Ni kutokana na ushawishi wa Dkt Ruto ambapo eneo hilo lilimpigia Kinara wa ODM Raila Odinga kura kwa wingi mnamo 2007 kisha Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2013 na 2017.

Kwa hivyo, Bw Moi ana mlima mrefu wa kukwea kuhakikisha kuwa Kanu inasalia hai katika Bonde la Ufa kisha maeneo mengine ila kwa sasa itakuwa vigumu kutokana na ushawishi wa Dkt Ruto katika jamii ya Wakalenjin.

Aidha, kumezuka vigogo wa kieneo ambao wana ushawishi katika maeneo yao na kuifanya iwe vigumu sana kwa Kanu kupenya maeneo hayo kama zamani.

Kwa mfano, Kanu enzi hizi ina nafasi finyu sana ya kushinda kiti cha ubunge Nyanza au Pwani kwa kuwa wakazi wengi wanaegemea ODM.

Vivyo hivyo, ilikuwa vigumu kwa chama hicho kushinda viti eneo la Kati au Bondeni mnamo 2017 kutokana na ushawishi wa Jubilee.

Mwanzo wa kupungua kwa umaarufu wa Kanu ulikuwa baada ya uchaguzi 2002 ambapo aliyekuwa Waziri na mwandani wa Mzee Moi, Nicholas Biwott alikihama chama hicho baada ya kushindwa kumbandua Uhuru Kenyatta kama mwenyekiti 2005.

Kabla ya uchaguzi wa 2007, Dkt Ruto alikihama chama hicho na viongozi wengi kisha kujiunga na ODM huku Rais Uhuru Kenyatta pia akibanduka mnamo 2012 na kubuni TNA kisha kuacha chama hicho kigae tu.

Katika uchaguzi mkuu ujao, Kanu inaweza kuongezea idadi ya wabunge wake 10, maseneta wawili na gavana ila kurejelea umaarufu wake wa enzi za utawala wa chama kimoja na miaka ya 90 ni kibarua kigumu.

WASONGA: Chiloba, wenzake wasaidie IEBC kufanikisha kura 2022

Na CHARLES WASONGA

UTEUZI wa waliokuwa maafisa wanne wa ngazi za juu katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kushikilia nyadhifa kuu katika asasi zitakazohusika na uchaguzi mkuu wa 2022 ni mtihani mkubwa kwao.

Ezra Chiloba, Emmaculate Kassait, James Muhanji, na Anne Nderitu watahitaji kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi mkubwa ili kuondoa lawama zilizoelekezwa kwao kuhusiana na dosari zilizokumba chaguzi za 2013 na 2017, waliposhikilia nyadhifa za juu katika IEBC.

Bw Chiloba, ambaye alikuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Mawasiliano Nchini (CA).

Anatarajiwa kutekeleza wajibu mkubwa katika uchaguzi huo kwa sababu asasi hiyo inatwikwa jukumu la kuhakikisha kuna mawasiliano ya masafa ya 3G na 4G katika vituo vyote vya kupiga kura nchini na hivyo kuiwezesha IEBC kutuma, haswa matokeo ya uchaguzi wa urais hadi kituo cha kitaifa cha ujumuishaji bila matatizo yoyote.

Tayari mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amelalamika kuwa kuna maeneo ya humu nchini ambayo hayajafikiwa na masafa ya 3G ambayo watategemea kupeperusha matokeo ya uchaguzi.

Ikumbukwe kwamba hitilafu katika upeperushaji wa matokeo ya uchaguzi wa urais kutoka jumla ya vituo 11,500 vya upigaji kura ndio mojawapo ya sababu zilizochangia kufutiliwa mbali kwa matokeo ya uchaguzi wa urais mnamo 2017.

Hatua hiyo ilitumbukiza taifa hili katika lindi la taharuki ya kisiasa na hasara baada ya IEBC kuamuriwa irudie uchaguzi wa urais.Naye aliyekuwa Mkurugenzi wa Elimu kwa Wapigakura katika IEBC Emmaculate Kassait ambaye aliteuliwa kuwa Kamishna wa Data Novemba 2020, anasimamia data muhimu kuhusu uchaguzi mkuu kama vile idadi ya watu nchini.

Ni wajibu wa Bi Kassait kuhakikisha kuwa data zote kuhusu Wakenya ni salama na haziingiliwi wala kuvurugwa kwa njia yoyote.

Kwa upande mwingine, aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) katika IEBC James Muhati ndiye Afisa Mkuu Mtendaji wa Huduma Kenya.

Katika idara hii, Bw Muhati anasimamia miongoni mwa mengine data zilizoko katika stakabadhi za utambulisho kama vile vitambulisho vya kitaifa vitakavyotumika katika shughuli za usajili wa wapiga kura wapya unaoanza leo na upigaji kura mnamo Agosti 9, 2022.

Kwa upande wake Bi Anne Nderitu ambaye zamani alihudumu kama afisa wa mafunzo kuhusu Masuala ya Uchaguzi katika IEBC ndiye Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Afisi yake ina wajibu mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao kwa sababu ndiyo inasajili vyama vipya na kuidhinisha miungano ya kisiasa.

Miungano hiyo ambayo inaendelea kubuniwa itakuwa kiunga muhimu katika kuamua mgombeaji wa urais atakayeshinda katika uchaguzi.

Bi Nderitu pia ndiye anasimamia orodha ya wanachama wa vyama vya kisiasa na ambayo itatumika katika michujo ya vyama hivyo kuelekea uchaguzi huo mkuu.

Kwa hivyo, kwa mtazamo wangu, ufanisi wa uchaguzi mkuu ujao utategemea zaidi utendakazi wa maafisa hawa wanne ambao zamani walihudumu katika IEBC.

Japo wengine wao walielekezewa lawama kuhusiana na dosari mbalimbali zilizotokea walipokuwa wakihudumu katika tume hiyo, sasa wanayo nafasi ya kujitakasa kwa kufanya kazi mzuri katika asasi hizi muhimu wanazozisimamia wakati huu.

WARUI: Wazazi watumie fursa ya likizo kunasihi watoto wao

Na WANTO WARUI

VISA vya utovu wa nidhamu na vile vya wanafunzi kutaka kujitoa uhai vimekuwa vingi sana siku hizi.

Huku visa vya kujitoa uhai kwa watu wazima vinasababishwa na mambo mawili makuu: umaskini na mapenzi, kwa wanafunzi huenda ni matatizo tofauti kabisa.

Baadhi ya mambo yanayopelekea wanafunzi kujipata katika hali hizi mbaya ni pamoja na kujiunga na vikundi vya marafiki wabaya, kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, kutokuwa na kazi maalum nyumbani na zaidi ni kukosa ushauri nasaha kutoka kwa wazazi wao.

Wanafunzi wengi hasa walio katika shule za malazi huwa na muda mfupi sana wa likizo wa kuwa na wazazi wao.

Kuna wale wazazi ambao huwa wanaenda kazini asubuhi na mapema kisha kurudi jioni au usiku kabisa.

Hawa hawapati muda mwafaka wa kuweza kuzisoma tabia za wana wao hasa zile geni.

Wanafunzi wanapokuwa pamoja hushiriki katika mambo tofauti shuleni au popote pale walipo.

Kuna mambo mema na mengine yasiyo mema ambayo huwa wanajadiliana.

Miongoni mwa wanafunzi hao, kuna wale huathirika na mambo mabaya na hatimaye kujipata wakiyatenda.

Haya ni pamoja na kujikuta wakianza kutumia dawa za kulevya, kutazama filamu mbaya ama hata kujiingiza katika mapenzi ya kiholela.

Ni jukumu la kila mzazi kuweza kutenga muda maalum ili ajadiliane na mwanawe kuhusu mambo ambayo yanaweza kumharibia maisha yake ya baadaye.

Kwa mfano, mwanafunzi anaporudi nyuma katika matokeo yake ya masomo mwisho wa muhula, haitoshi tu mzazi kuambiwa kuwa mtihani ulikuwa mgumu.

Kuna sababu nyingi tu ambazo husababisha matokeo mabaya kwa mwanafunzi.

Baadhi ya mambo ya utovu wa nidhamu yanaweza kuonekana madogo tu na kupuuziliwa mbali hatimaye yawe mwiba usiong’oleka.Hii ndiyo sabau wazazi wanastahili kuwa macho sana na yale yote yanayoendelea katika maisha ya wana wao.

Wakati mwingine visa vya utovu wa nidhamu vinaweza kuibuka kutoka shuleni.

Endapo tabia mbaya zipo shuleni na hazijakabiliwa na uongozi wa shule ipasavyo, patakuwa na uwezekano mkubwa zikaenea hata kwa wale wanafunzi wazuri wasio na kinga ya ushauri kutoka kwa wazazi.

Ni muhimu sana kwa kila mzazi ambaye ana mtoto shuleni kuchukua fursa hii ya likizo aweze kumhoji mwanawe na kuchunguza kama ameingilia mienendo isiyofaa ili kama atagundua mambo yasiyofaa kwa mtoto aweze kukabiliana nayo mapema.

Matatizo mengi yanayowapata watoto siku za baadaye hutokana na wazazi kukosa kurekebisha makosa madogo madogo mapema yanapojitokeza nyumbani ama kukosa muda wa kujadiliana na watoto ili wawajue vyema.

Bila shaka usipoziba ufa utajenga ukuta.

KAMAU: Ni aibu kuwatelekeza mashujaa waliopigania uhuru

Na WANDERI KAMAU

KULINGANA na majarida mbalimbali ya historia, vita vya Maumau ni miongoni wa harakati zinazotambulika duniani kote kutokana na jinsi Wakenya walivyojitolea kuukabili utawala wa kikoloni wa Waingereza.

Wasomi wa historia wanasema kuwa kwa namna moja, kujitolea kwa Wakenya kwenye vita hivyo ndiko kulikowapa msukumo Waafrika wengine katika nchi kama Algeria, Msumbiji, Angola na Afrika kusini.

Nchini Algeria, vita vya ukombozi wa taifa hilo vilidumu kati ya mwaka 1954 hadi 1962, wakati taifa hilo lilijinyakulia uhuru wake kutoka kwa Ufaransa.

Vikosi vya Ufaransa vilijipata taabani, wakati raia wa Algeria walijitokeza kwa ujasiri kuwakabili kutokana na dhuluma ambazo walikuwa wakiwafanyia.

Nchini Msumbiji, vita vya ukombozi vilidumu kati ya 1964 hadi 1974, wakati taifa hilo lilipata uhuru wake kutoka kwa Ureno, kupitia kubuniwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Nchini Angola, harakati hizo zilidumu kati ya 1961 hadi 1974.Bila shaka, ni wazi kuwa vita vya Maumau vilibuni msingi mzuri wa harakati hizo, kwani vilidumu kati ya 1952 hadi 1958.

Licha ya vita hivyo kubuni msingi thabiti kuhusu jinsi Afrika ilipigania uhuru wake, inasikitisha kuwa hadi sasa, Kenya ni miongoni mwa nchi ambazo zimewatelekeza mashujaa hao.

Hadi sasa, wapiganaji wa Maumau wamekuwa wakilalamikia jinsi serikali nyingi zimekosa kushughulikia maslahi yao tangu miaka ya sitini.

Hii ni licha ya Uingereza kutoa mabilioni ya fedha kwa wapiganaji hao kulipwa kama ridhaa, kutokana na mateso na dhuluma ambazo walipataSerikali ya Mzee Jomo Kenyatta, marehemu Daniel Moi na Rais Mstaafu Mwai Kibaki zilifumbia macho vilio vyao vyote.

Hata hivyo, Bw Kibaki alijaribu jinsi awezavyo kushughulikia maslahi yao, ingawa juhudi hizo hazikuzaa matunda sana.

Ni wakati wa utawala wa Mzee Kibaki ambapo minara ya mashujaa kama Dedan Kimathi na mwahaharakati Tom Mboya ilijengwa, kama njia ya kukumbuka michango waliyotoa kwenye harakati za ukombozi wa nchi.

Inasikitisha kuwa wapiganiaji wengi wamekuwa wakidai kiwango kikubwa cha fedha walizopaswa kulipwa ziliporwa na maafisa na mawakili waliosimamia taratibu za kuwalipa.

Je, Kenya kwelininawajali wazalendo wake?

Imefika wakati tujifunze kutoka kwa nchi kama Afrika Kusini, kuhusu njia bora za kuwathamini mashujaa na wanaharakati waliopigania uhuru.

akamau@ke.nationmedia.com

MUTUA: Wakenya walio ng’ambo wana haki ya kupiga kura

Na DOUGLAS MUTUA

NILICHEKA kidogo kisha nikakereka kweli-kweli hivi majuzi kutokana na matamshi ya mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Bw Wafula Chebukati.

Akiongea na makundi ya kidini, Bw Chebukati aliahidi kwamba angewapa haki za kupiga kura, katika uchaguzi ujao, Wakenya wanaoishi nje ya nchi.

Wanaoishi kwenye mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Afrika Kusini walishiriki chaguzi kuu za 2013 na 2017.

Kwa walio kwingineko Afrika, Marekani, Uropa, Asia, Mashariki ya Kati na kadhalika, hiyo imesalia ndoto isiyoagulika – hadaa baada ya hadaa, na hadaa zaidi.

Serikali ikidai haina uwezo wa kifedha kuendesha shughuli hiyo kokote waliko Wakenya milioni 3.5, lakini ikipokea kwa pupa ushuru wanaolipa kwa mamilioni.

Sikwambii mfuko mnono unaotengewa tume ya uchaguzi huishia kuwa kitoweo cha watu wabadhirifu wanaoitafuna nchi kana kwamba kiyama chaja kesho.

Sasa Bw Chebukati anadhani amefanya kitu cha maana sana kutangaza huenda wanaoishi Marekani, Canada, Sudan Kusini, Uingereza, Qatar na Muungano wa Mataifa ya Kiarabu (UAE) wakamchagua rais mwaka 2022.

Nilicheka kwa kuwa nilidhani hiyo ni danganya-toto ya kawaida ambayo tumeisikia tangu mwaka wa 2010 tulipoipitisha Katiba ya sasa.

Huwa raha ukihadaiwa ukajua.

Yaliyoniudhi hadi ya kuniudhi ni matamshi ya ‘kuwapa haki ya kupiga kura Wakenya wanaoishi ughaibuni’.

Yangetolewa na kabwela wa watu ningemmpuuza tu, hazidishi hapunguzi! Lakini Bw Chebukati ndiye mkuu wa uchaguzi hasa, tena wakili anayeielewa Katiba sawasawa.

Anajikweza sana mtu wa kiwango chake anapodai atawapa haki Wakenya walionyanyasika miaka yote hii ilhali anajua ni haki yao ya kikatiba.

Hata heri angetanguliza kwa kuomba msamaha kwani amekiuka Katiba miaka mingi tu kwa kutoweka mikakati ya kuwawezesha Wakenya kupata haki hiyo.

Hii si mara ya kwanza kwa ahadi kama hiyo kutolewa, lakini kila uchaguzi unapokaribia vinavyoandamana ni visingizio.

Hata baada ya makundi kadha ya Wakenya kuishtaki serikali mahakamani wakidai haki hiyo, wasimamizi wa uchaguzi wametokea kushupaa shingo na kupuuza kilio hicho.

Kupanga mikakati ya Wakenya kupiga kura kokote waliko hakuigharimu serikali kama miradi ambayo imeishia kufyonzwa na kupe wanono wanatao kwenye nundu ya umma.

Tatizo ni ukosefu wa utashi wa kisiasa; wanasiasa hawaoni tija katika kuwawezesha Wakenya walio ughaibuni kushiriki upigaji kura.

Hakika, wanasiasa wanawaogopa watu hao kwa kuwa wanadhani wamepambazukiwa na dunia kwa kuishi nchi za watu ambako mambo hufanywa tofauti na kwa uwazi.

Kwa makadirio ya wanasiasa, watu milioni 3.5 walioonja ubora wa maisha nje ya nchi ni hatari ikilinganishwa na ‘kondoo’ wa mtaani waliozoea kupelekwa machinjioni kimyakimya kila baada ya miaka mitano.

Wanasiasa huhofia kuwa watu hao, kutokana na mtagusano wao na watu wa asili nyingine, wanaweza kuukiuka ukabila wakamchagua mwaniaji aliye na sera bora.

Na kwa kuwa wanasiasa wetu ni wakora wasiojiamini, hawana hakika sera zao zinaweza kuwashawishi Wakenya hao, hivyo ni heri waliwe njama, watulize boli huko waliko.

Ukiwaona waambie wasihofu kwa kuwa huku nje tumetengana kishenzi tu, tumeshindwa kuuacha ukabila, hata makundi ya WhatsApp tunaunda kwa misingi ya makabila yetu!

Wanasiasa pia huogopa uwezo wa kifedha wa wanaoishi ughaibuni kwani, kinyume na wanavyofanya nchini, wanasiasa hawawezi kwenda kuwagawia vihela vyao huko nje.

Kwa jumla, Wakenya tumelimatia sana kudai haki zetu za kimsingi kama hii ya kupiga kura.

Tumezembea kuwawajibisha wanasiasa wetu, wakatugawa mafungu, sasa wanacheza nasi kama mwanasesere.

Wataanza kutuheshimu tutakapoacha uzembe na upofu wa kupanga tuliojitwika, tudai haki zote za kimsingi hata zisizotufaa moja kwa moja.

mutua_muema@yahoo.com

WASONGA: Wabunge wapiganie kurejea kwa bei nafuu

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi na wabunge wameamua kuwachezea shere Wakenya kuhusiana na suala muhimu la bei ya mafuta wakijifanya kuwa watetezi wao.

Lakini ukweli ni kwamba Bw Muturi na wabunge wote 349 ndio wamewasababishia Wakenya madhila yanayowakumba wakati huu kutokana na ongezeko la bei ya mafuta kwa kiwango cha juu kupita kiasi.

Ni unafiki mkubwa kwa Bw Muturi, ambaye ametangaza azma ya kuwania urais 2022, kuamuru Kamati ya Fedha kuchunguza ikiwa kuna sababu nyinginezo zilizochangia hatua hiyo mbali na msururu wa ushuru ambao hutozwa bidhaa za mafuta.

Aidha, ameitaka kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Homa Bay kuandaa mswada wa marekebisho ya sheria za ushuru wa ziada ya thamani (VAT) kukinga bidhaa za mafuta kutokana na ushuru huo.

Bw Muturi aliamuru kamati hiyo kuwasilisha ripoti, na mswada huo bungeni baada ya siku 14 kuanzia Jumanne, Septemba 21, 2021.

Kabla ya Spika kutoa amri hiyo mjadala mkali ulishamiri bungeni huku wabunge wakielekeza ‘mishale’ ya lawama kwa serikali, Rais Uhuru Kenyatta na muafaka kati yake na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Kwa kuwa nyongeza ya kati ya Sh7.5 na Sh12 kwa bei za petroli, dizeli na mafuta taa itaendelea kutekelezwa hadi Oktoba 14, agizo la Bw Muturi kwa wabunge halitawakinga wananchi dhidi ya makali ya bei hizo mpya zilizotangazwa na Mamlaka ya Kusimamia sekta za Kawi na Mafuta (EPRA).

Kamati ya Bi Wanga itakapokuwa ikiwasilisha ripoti yake, na kielelezo cha mswada wa marekebisho ya sheria za ushuru, hapo Oktoba 7, tayari zitakuwa zimesalia siku saba kabla ya Epra kutangaza bei zitakazotumika kati ya Oktoba 14 hadi Novemba 14, 2021.

Isitoshe, hata ingawa Bw Muturi atatumia mamlaka yake kulingana na kanuni za Bunge kufupisha muda wa kushughulikiwa kwa mswada huo wa marekebisho ya sheria hiyo ya VAT, muda huo unaweza tu kupitshwa mapema mwezi Desemba.

Kwa mtazamo wangu, spika huyu na wabunge hawajawasaidia Wakenya kwa njia yoyote kwa hatua waliyochukua ya kuanzisha mchakato wa kuondoa ushuru huo ulioanza kutekelezwa baada ya wao kupitisha Mswada wa Fedha wa 2018.

Kadhalika, tayari kiongozi wa wengi Amos Kimunya na mwenzake wa upande wa wachache John Mbadi wamepinga kuondolewa kwa ushuru wa VAT wa kiwango cha asilimia nane kwa mafuta.

Bw Kimunya, ambaye ni waziri wa zamani wa Fedha, alisema kuondolewa kwa ushuru huo kutavuruga bajeti ya serikali na kuinyima mapato ya kiwango cha Sh35 bilioni kwa mwaka.

Ikizingatiwa kuwa Bw Kimunya ndiye mwakilishi wa Rais Kenyatta na serikali yake bungeni, uwezekano wa bunge kupitisha mswada utakaoandaliwa na kamati ya Bi Wanga ni finyu mno.

Pendekezo langu ni kwamba wabunge washinikize Serikali Kuu irejeshe afueni ya bei ya mafuta ili kudhibiti ongezeko la bei ya bidhaa hizo.

Hii ni kwa sababu mojawapo ya sababu zilizochangia ongezeko la bei ya mafuta kwa kiwango kikubwa mwezi huu, kulingana na Epra, ni kuondolewa kwa nafuu hiyo ya kiwango cha Sh1.4 bilioni.

Pili, wabunge waandae sera ya kuihimiza serikali kuimarisha matumizi ya kawi mbadala kama vile mvuke na jua na upepo katika mahitaji ya kila siku badala ya kutegemea mafuta ambayo bei yake inapanda kila mara katika masoko ya kimataifa.

KINYUA BIN KING’ORI: Masharti ya wandani kisiki kwa ‘handisheki’ ya UhuRuto

Na KINYUA BIN KINGORI

JUHUDI zilizoanzishwa na viongozi wa makanisa kupatanisha Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Dkt William Ruto, zinafaa kulenga maslahi ya Wakenya si binafsi ya viongozi hao wawili wenye mamlaka makuu serikalini.

Wandani wao wameanza kutoa masharti ambayo lazima yazingatiwe ili mapatano hayo kufanikiwa.

Aidha, wanalaumiana kwa kutoa vijisababu visivyo na maana, na huenda wakavuruga juhudi za viongozi hao kuridhiana.

Imebakia miezi 11 kwa serikali ya Jubilee kumaliza muda wake na kupisha utawala mpya baada ya uchaguzi mkuu 2022.

Lakini nyingi ya ahadi ambazo UhuRuto walitoa hazijatekelezwa.

Hakuna maendeleo ya kujivunia ambayo tumepata kipindi hiki cha pili, na katika kipindi hiki cha lala salama hatutarajii maendeleo yoyote ikiwa viongozi hao hawatazika tofauti zao.

Hivyo, kuna haja kubwa Wakenya kuunga mkono viongozi hao wapatane ili tuone ikiwa watasuka mipango ya haraka kuokoa wananchi na madhila ya uchumi mbaya sababu ya utendakazi duni wa serikali hii ya Jubilee.

Je, serikali ambayo viongozi wakuu wanatumia muda wao mwingi kulumbana, kuchimbana na kupigana kisiasa kwa manufaa yao, watarajia ipate muda lini kujua wananchi wamelemewa na ugumu wa maisha?

Je, wanaweza kupata suluhisho litakalohakikisha Wakenya wanaohangaika kwa makali ya njaa wamepata msaada wa chakula? Kushindwa kwa Jubilee kushughulikia matatizo yanayokumba Wakenya kumechochewa na uhasama kati ya Rais na Dkt Ruto.

Ajenda kuu ziliwekwa kando, miradi mingi kupuuzwa na mafaniikio waliyotuahidi ya maziwa na asali yamebakia kitendawili.

Badala yake, wamechochea chuki serikalini hadi bungeni ambako wabunge wanatekeleza wajibu wao kutegemea mrengo wao wa kisiasa wala si kwa manufaa ya wananchi walala hoi.

Leo hii tunaumizwa kwa bei ya juu ya mafuta baada ya wabunge kupitisha mswada wa kuongeza ushuru.

Maisha yataendelea kubakia magumu katika miezi michache inayokuja kabla uchaguzi, ikiwa Uhuruto hawatajitolea kumaliza uhasama wao.

Dkt Ruto ametangaza hadharani kwamba yuko tayari kufanya mazungumzo na Rais bila masharti, naye Rais anafaa kujtokeza kukumbatia maridhiano ili juhudi za viongozi wa makanisa zifaulu.

Pia watumie nafasi hiyo kuelezea Wakenya kiini cha uhasama wao maana hatujui kilichoenda mrama baada ya uchaguzi wa 2017.

Rais na Dkt Ruto waweke kando maslahi ya binafsi na matamanio ya kisiasa ya 2022 ili kulenga msamaha na masikizano bila unafiki.

Taifa linahitaji mshikamano wao ili kumaliza baa la njaa, kuimarisha udhibiti wa corona na utoaji chanjo yake, kuunda nafasi za ajira kwa vijana, kuboresha elimu kwa kutatua changamoto zinazotishia ubora wa mtaala wa CBC, kupunguza gharama ya maisha, na kukamilisha miradi ya maendeleo kabla Agosti 2022.

Rais Kenyatta atafaulu kuacha nchi iliyo salama na yenye amani na umoja iwapo atapatana na naibu wake ili wamalize safari yao pamoja.

KAMAU: Mizozo UoN inatishia ndoto za vijana wetu

Na WANDERI KAMAU

MOJA ya ndoto zangu za utotoni ilikuwa kusomea katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Ingawa ndoto za utotoni hubadilika kadri mtu anapokuwa mkubwa, yangu haikubadilika kamwe. Ilibaki kwenye nafsi yangu.

Ulipofika wakati wa kuchagua kozi za kusoma nitakapoingia chuoni, karibu zangu zote zilikuwa katika chuo hicho.

Msukumo wa ndoto zangu ulitokana na sifa nzuri nilizosikia vijijini kuhusu taasisi hiyo, maarufu UoN.

Sifa hizo zilitokana na simulizi za wazee, walimu wangu na maelezo niliyosoma kwenye majarida kadhaa.

Watu wachache waliofaulu kujiunga na vyuo vikuu walikuwa wakialikwa katika shule za msingi kuwapa wanafunzi manufaa ya kujiunga na chuo kikuu.

Walitupa simulizi nyingi za kututia moyo, wakirejelea jinsi chuo cha Nairobi kilichangia uwepo wa watu maarufu kama Prof Ngugi wa Thiong’o, Prof Micere Githae Mugo.

Pia kuna Prof Arthur Obel (aliyeaminika kuvumbua tiba ya virusi vya HIV) na mwandishi Wahome Mutahi (maarufu kama Whispers) kati ya wengine wengi.

Binafsi, nilijipa msimbo wa ‘Whispers Junior’ – kwani nilimuenzi sana Wahome Mutahi na simulizi nilizopewa kumhusu.

Chuo Kikuu cha Nairobi kilikuwa na hadhi kubwa katika jamii kwa mchango wake katika kuendeleza nchi, hasa kupitia sekta ya elimu.

Hata hivyo, inasikitisha kuona taasisi hiyo ikiyumba.

Kwa sasa chuo kinakumbwa na mizozo si haba – hali inayozua wasiwasi kuhusu mustakabali wake.

Mzozo wa kwanza unatokana na tofauti kali ambazo zimezuka kati ya Naibu Chansela, Prof Stephen Kiama, na baadhi ya wasimamizi wakuu kufuatia pendekezo la kubadilisha utaratibu wa kiusimamizi wa UoN.

Mzozo wa pili umeibuka kati ya Prof Kiama na wanafunzi kutokana na hatua ya usimamizi wa chuo kuongeza karo maradufu na kodi ya malazi.

Kwenye malalamishi yao, wanafunzi wanadai hawakushirikishwa hata kidogo wakati maamuzi hayo yakiafikiwa.

Vivyo hivyo, malalamishi kama hayo ndiyo yametolewa na wasimamizi wa idara mbalimbali, ambao hawakuridhishwa na pendekezo la kuunganishwa kwa baadhi ya idara huku zingine zikifutiliwa mbali.

Kimsingi, ni kinaya kwa mizozo kama hii kushuhudiwa katika mojawapo ya taasisi muhimu sana ya elimu nchini.

Taasisi hiyo ndiyo ilikuwa ya kwanza kupewa hadhi ya chuo kikuu nchini, baada ya Kenya kujinyakulia uhuru kutoka kwa wakoloni.

Kabla ya hapo, Wakenya wengi walioonyesha nia ya kuendeleza walikuwa wakienda katika vyuo vikuu vya nchi jirani, kama Makerere nchini Uganda na kile cha Dar es Salaam nchini Tanzania.

Inavunja moyo kuona mizozo, malumbano na mivutano inayozidi kuchipuka kwani inatishia kuzamisha na kupaka tope taasisi hiyo kubwa zaidi ya elimu ya juu nchini.

Madhara yake yatasambaa mbali kwani yatavunja ndoto za maelfu ya vijana vijijini wanaopania kusomea katika chuo hicho kwa wakati mmoja maishani mwao.

Wito wangu ni kwa usimamizi mkuu wa chuo kusuluhisha mizozo hiyo ili kurejesha hadhi yake tena kama ilivyokuwa awali.

akamau@ke.nationmedia.com

NGILA: Teknolojia mpya ya mbegu sawa ila wapi hamasisho?

Na FAUSTINE NGILA

WIKI iliyopita nilihudhuria uzinduzi wa ripoti kuhusu hali ya kilimo barani Afrika ambapo matokeo ya utafiti kuhusu mbegu yalitolewa.

Habari njema ni kuwa matumizi ya teknolojia yamepelekea kuimarika kwa ubora wa mbegu wanazopanda wakulima wa humu nchini, hali inayochangia kwa juhudi dhidi ya ukosefu wa chakula nchini.

Ripoti hiyo iliyotangazwa na shirika la The African Seed Access Index (TASAI) ilionyesha kuwa visa vya mbegu feki kusambazwa mashambani vimepungua kutoka 36 mwaka wa 2013 hadi 12 mwaka wa 2019.

Pia, ilieleza kuwa jitihada za kampuni za mbegu nchini katika kutokomeza uuzaji wambegu feki umeimarika kutoka asilimia 39 mwaka wa 2013 hadi asilimia 70 mwaka wa 2019.

Lakini ni teknolojia gani hasa, ilitumika kupata matokeo haya?

Kimsingi, wakulima hununua mbegu katika maduka ya kuuza mbegu. Katika karatasi za kupakia mbegu hizo, kuna nambari 12 ambazo zimefichwa kwa stika.

Wakulima hukwaruza stika hizo na kufichua nambari hizo ambazo wanatuma bila malipo kupitia ujumbe mfupi wa SMS na kupokea ujumbe mara moja kuthibitisha kuwa mbegu hizo ni halali.

Kwa mara ya kwanza, nimeona sheria ambazo serikali imeweka kulinda wakulima zikifuatwa.

Katika sheria za kilimo, mbegu zote ambazo zinauzwa kwa mifuko ya chini ya kilo tano inatakiwa kuwa na stika za ithibati.Huu ndio uwezo mkubwa wa teknolojia.

Bila ubunifu huu, mbegu nyingi zinazopandwa Kenya zingetuletea mazao dhaifu tu na kuchangia baa la njaa ambalo hukumba nchi hii kila mwaka.

Hata hivyo, juhudi hizi zinahitaji kupigwa jeki kwani si wakulima wote wanatambua kuwa kuna stika katika mifuko ya mbegu wanayonunua.

Utafiti tofauti uliofanywa na Muungano wa Biashara ya Mbegu nchini (STAK) katika kaunti nane umefichua kuwa kiwango cha wakulima wanaojua kuwa kuna stika hizi ni asilimia 85 kwa wastani.

Hii inamaanisha kuwa asilimia 15 ya wakulima bado wamo katika hatari ya kupanda mbegu feki sababu kuu ikiwa ukosefu wa Habari kuhusu teknolojia hiyo.

Lakini katika utafiti mwingine, licha ya asilimia 85 kutambua stika hizo, ni asilimia 35 pekee kwa wastani ambao wanazikwaruza na kutuma nambari kupitia arafa kuthibitisha ubora wa mbegu.

Yaani, tunajua umuhimu wa teknolojia lakini hatuitumii kutufaa katika njia ambayo inastahili. Sasa basi inakusaidiaje iwapo matapeli watanunua au kuunda stika feki na kupachika kwenye mfuko wa mbegu?

Licha ya kupungua kwa visa vya mbegu feki, bado kuna hatari kuwa ya kuendelea kupata mazao duni hali ambayo katika miaka ya hivi majuzi imekuwa ikipandisha bei ya chakula nchini na kuumiza wananchi ambao tayari wamechoshwa na kupanda kwa gharama ya Maisha kila mwezi.

Ni wajibu sasa wa serikali, kupitia Wizara ya Kilimo, kueneza Habari kuhusu stika hizi katika kaunti zote. Uhamasisho kwa wakulima wadogo na wakubwa ndio utaifaa nchi hii iwapo tunataka kujitegemea katika uzalishaji wa chakula.

WANGARI: Elimu ya juu iwekeze zaidi katika ujuzi wa kiufundi na kitaaluma

Na MARY WANGARI

WATAHINIWA waliokamilisha mitihani yao ya Cheti cha Elimu ya Sekondari Nchini (KCSE) wataanza kujiunga na taasisi za elimu ya juu wiki hii.

Maelfu ya watahiniwa hao tayari wamepokea barua za mialiko kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali vya umma na vya kibinafsi, huku baadhi wakijiandaa kujiunga na taasisi za kiufundi kote nchini.

Kwa hakika, ni jambo la kufurahia na kuhuzunisha kwa pamoja hasa kwa kuzingatia mamia ya mahafali wanaozidi kutaabika kwa kukosa ajira hata baada ya kufuzu kwa shahada za digrii, uzamili na uzamifu.

Kisa cha hivi majuzi kuhusu Wakenya watatu wenye umri wa makamo kutoka Kaunti ya Homa Bay, waliolazimika kufundisha shule za chekechea licha ya kuwa na vyeti vya uzamifu, ni ithibati tosha ya uhalisia mchungu uliopo.

Viwango vya ajira vingali chini mno nchini licha ya Kenya kuwa miongoni mwa mataifa yanayokua kwa kasi zaidi kiuchumi barani Afrika.

Hali hii imewafanya mahafala wengi waliokuwa na matumaini makubwa kuhusu mustakabali wao kukata tamaa huku baadhi yao wakijitosa katika uhalifu ili kupata riziki.

Kwa kuzingatia hilo, umuhimu wa kuwepo mfumo jumuishi unaotilia maanani ujuzi wa kiufundi na kitaaluma, hauwezi ukasisitizwa vya kutosha.

Kwa miaka mingi, ukosefu wa wafanyakazi wenye ujuzi umekuwa kero kuu ambayo imegharimu pakubwa mashirika ya umma na ya kibinafsi mamilioni ya fedha huku yakilazimika kusafirisha wataalamu kutoka mataifa ya kigeni nchini.

Ili kuziba pengo hilo, serikali inapaswa kushirikiana na wadau husika kuimarisha taasisi zinazotoa mafunzo na ujuzi wa kitaaluma utakaowezesha vijana kustawi nyanjani.

Taasisi hizo zitawezesha kuwepo kwa watu walio na ujuzi unaohitajika viwandani hivyo kufanya iwe rahisi kwao kupata ajira pindi wanapokamilisha mafunzo yao.

Ili Kenya iweze kufanikisha Ruwaza ya 2030 kuhusu ajira na maendeleo kiuchumi, ni sharti ihakikishe kuwepo kwa wafanyakazi walio na ujuzi unaohitajika katika taaluma husika.

Njia mojawapo ya kufanikisha hayo ni kwa kuwekeza katika taasisi zinazotoa mafunzo ya kiufundi ili kuhakikisha ukuaji na ustawi kiuchumi kwa jumla.

Serikali imejitahidi kuanzisha vituo vya kiufundi kote nchini ikiwemo kuwezesha wanafunzi kupata mikopo na ufadhili wa masomo kujiendeleza kielimu.

Masomo ya vyuo vikuu ni muhimu lakini ni sharti tuende na majira kwa kufanyia mageuzi mfumo wa elimu ya juu nchini.

Kando na kuwezesha vijana kupata ajira, mfumo unauopa kipaumbele ujuzi kiufundi na kitaaluma utaimarisha mustakabali wa Kenya kwa kubuni mikakati jumuishi ya ukuaji na ustawi kiuchumi.

mwnyambura@ke.nationmedia.com

WARUI: Tukumbatie changamoto za CBC ili utekelezaji uwe rahisi

Na WANTO WARUI

MFUMO mpya wa Elimu (CBC) ambao kwa sasa umefika Gredi ya 5 bado haujapokelewa vyema na asilimia kubwa ya Wakenya.

Akisisitiza kuwa mfumo huu utaendelea kote nchini, Waziri wa Elimu Profesa George Magoha, juma lililopita alisema kuwa ni makosa kuulaumu mfumo wenyewe kwa kusema kuwa ni ghali mno ilhali vifaa vingi ambavyo vinaweza kutumiwa kufanikisha masomo vinapatikana katika mazingira yetu tena kwa urahisi.

Waziri Magoha aliwaambia wazazi wanaolalamikia gharama ya elimu ya CBC kuwa serikali inatoa vitabu vya kiada katika kila shule ya umma pamoja na kuhakikisha kuwa walimu wamepata mafunzo ya mara kwa mara ili kuwawezesha wasaidie wanafunzi.

Waziri alisema kuwa changamoto ambazo wazazi na walimu wanakumbana nazo ni zile tu za kawaida ambazo ni lazima ziwepo wakati jambo jipya linaanzishwa.

Mfumo mpya wa CBC ulianzishwa baada ya majopo kadhaa kuwasilisha mapendekezo yake kwa serikali ili kubadilisha mfumo uliopo wa 8-4-4 ambao unaegemea mitihani zaidi kuliko kutoa elimu ya kumwezesha mwanafunzi kujitegemea.

Kidesturi, mfumo wowote wa elimu unahitaji kuambatana vyema na mahitaji ya jamii. Kuna mambo mengi ambayo hubadilika kadri miaka inavyosonga na ni sharti elimu pia ibadilike ili kukidhisha mahitaji ya watu.

Mfumo wa 8-4-4 umekuwako nchini kwa muda wa miaka 36 tangu 1985. Mambo mengi yamebadilika tangu kuanzishwa kwake hasa ya kiteknolojia na jinsi ya kutenda kazi.

Aidha, watoto wanaozaliwa sasa ni wa kizazi kingine tofauti kabisa kwa hivyo kuwapa wanafunzi hawa elimu isiyoambatana na mahitaji yao ya kimaisha ni kuwakosea na kutojali maisha yao ya baadaye.

Lengo

Lengo No. 4 katika Malengo ya Kitaifa ya Elimu huwa linaelezea kuwa elimu inastahili kuandaa raia mwadilifu na mwenye misingi bora ya kidini kama ilivyoelezwa katika Katiba ya Kenya.

Hii ndiyo sababu mfumo wa CBC umeteuliwa ili uweze kuwiana na mahitaji haya.Kwa minatarafu hii, kuna haja Wakenya wote kuelewa sababu za kuanzishwa kwa mfumo huu, tuuelewe mfumo wenyewe na tuelewe mahitaji ya watoto wa taifa hili kabla ya kukashifu masomo yake.

Kwa sasa kila kitu duniani kinaelekea kutekelezwa kidijitali; njia ambayo elimu ya CBC inasisitiza itumiwe katika masomo shuleni. Japo mfumo wenyewe unaonekana kuwa ghali au mgumu, wanafunzi ambao wako shuleni na wanaofunzwa masomo ya CBC inavyostahili wanafurahia masomo haya zaidi ikilinganishwa na mfumo unaoondoka.

Tunapotatizika kutokana na mambo kadhaa yaliyomo katika CBC, hatuna budi tuelewe kuwa hata jambo lolote jepesi vipi huonekana kuwa gumu linapoanzishwa.

STEPHEN JACKSON: Mifumo thabiti ya lishe kufaa uchumi na kukabiliana na njaa

Na Dkt STEPHEN JACKSON

NI mara chache ambapo sisi hufikiria kuhusu kinachohitajika ili chakula tunachokula kifike kwenye sahani zetu.

Kutoka “shambani hadi mezani,” wengi wetu hawatambui orodha kamili ya wahusika na michakato inayohusika.

Mfumo wa chakula unajumuisha wahusika wengi katika hatua mbalimbali za usafirishaji, utengenezaji, usambazaji, uhifadhi, na uuzalishaji.

Mifumo hii ikifanyika vizuri, italeta ustawi kiuchumi. Sekta ya kilimo nchini Kenya inayouza bidhaa nje ya nchi huajiri takriban robo tatu ya wafanyakazi na huzalisha robo moja ya Jumla ya Pato la Nchi (GDP) la kila mwaka.

Hata hivyo, Janga la Tabianchi la Ulimwengu lina maana kwamba kaunti nyingi za Kenya huteseka kutokana na ukame unaotokea mara kwa mara na kuongezeka kwa viwango vya upungufu wa lishe.

Matokeo yake ni upungufu wa maji, upungufu mbaya wa mimea, utapiamlo kwa watoto, upungufu wa malisho ya mifugo unaosababisha mifugo kutoa maziwa machache, hivyo basi kupunguza hali ya lishe.

Kufikia sasa, kaunti 12 kati ya 23 zilizo katika sehemu kame zimepokea tahadhari ya kukumbwa na ukame.Ulimwenguni, dunia yetu inazalisha na kutumia kiasi kikubwa cha chakula.

Lakini watu milioni 700 bado wanaathiriwa na njaa.

Teknolojia ya uzalishaji chakula imepevuka sana, lakini bado tunapambana na kiwango kikubwa kisichoweza kudumishwa cha uzalishaji wa gesi chafu zinazotoka kwenye viwanda na magari.

Hasara baada ya mavuno, hasa, ni changamoto kubwa nchini Kenya na kwingineko. Mambo mengine yanayovuruga mfumo wa chakula yanajumuisha mashambulizi kwa mabadiliko ya tabianchi, kutolingana kunakowazuia watu kufikia chakula wanachohitaji, na tatizo la uhifadhi.

Hivyo basi, kushughulikia vizuri Mifumo ya Chakula ni jambo la lazima ili kuwe na Maendeleo Endelevu. Ndiposa Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) Antònio Guterres ameitisha “Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Mifumo ya Chakula” wa ulimwengu mzima tarehe 23 Septemba 2021.

Serikali, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na watu ulimwenguni kote, watakusanyika kujadili namna ya kushirikisha mifumo ya chakula ili kuleta suluhisho kwa changamoto za ulimwengu za njaa, janga la tabianchi, umaskini, na kutokuwepo kwa usawa.

Mkutano huo wa wakuu wa nchi utatoa nafasi, si tu kwa viongozi ulimwenguni bali pia kwa wakulima, wajasiriamali, wanaharakati, na kila mtu anayehusika katika mchakato wa chakula ili kubadili jinsi ulimwengu unazalisha, unatumia na unafikiria kuhusu chakula.

Serikali ya Kenya imejitolea kugeuza mifumo yake ya chakula.

Kujitolea huku ni wazi kutokana na ruwaza ya 2030 na “Ajenda Kuu Nne” (Yanayofanya Dhamana ya Chakula na Lishe kwa Wakenya wote kuwa kipaumbele kwa taifa).

Mkakati wa Sekta ya Kilimo ya Kenya wa Ugeuzi na Ustawi unaonyesha kujitolea kwa serikali ya Kenya kuzidisha uzalishaji, kuinua mapato katika viwanda vya huduma za kilimo na kuhakikisha uthabiti wa makazi na dhamana ya chakula, kuwafanya wakulima wawe wadau wakuu ili kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Mkutano

Tunapoelekea kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Samaki na Mashirika pamoja na UN Kenya walikuwa na msururu wa mazungumzo ya kimaeneo, ya Taifa na Kitaifa ili kuwapa Wakenya nafasi ya kuchangia moja kwa moja kwa maono na malengo yanayonuia makuu ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi.

Mazungumzo hayo yameleta pamoja wadau wengi. Kwa makusudi, sauti zinazosikika mara chache zilijumuishwa na kutoa nafasi muhimu kwa washiriki kujadiliana, kushirikiana, na kupanga matendo ya kuwa na siku za usoni zilizo bora zaidi.

UN Kenya itaendelea kuisaidia serikali kwa kipindi kifupi na kirefu kuhakikisha mifumo ya chakula imeimarishwa na kusimamiwa ifaavyo.

Tunawasaidia wakulima wenye mashamba madogo kwa kuwapa mikopo na kuendeleza uwezo wao wa kufikia masoko.

Sisi hutoa usaidizi wa kutuma fedha kwa watu walio wepesi kudhurika katika mchakato wa usambazaji – hasa wakimbizi na jamii ambazo ni wenyeji wao.

Kuhusu kukabili ukame na kupunguza janga la tabianchi, UN Kenya inasaidia katika uzalishaji wa mbegu mbalimbali zinazochukua muda mfupi kukomaa na zinazostahimili ukame.

Hii inawasaidia wakulima kukuza mimea hata wakati wa ukame.

Aidha, kwa pamoja na washirikawenza, tunasaidia serikali za kaunti kukarabati au kujenga mabwawa mapya ya maji, tukiwasaidia wakulima kuongeza idadi ya mifugo yao na kukuza miradi ya fanya kazi-pata pesa.

Dkt. Stephen Jackson ni Mratibu Mkazi katika nchi ya Kenya 

KAMAU: Mapinduzi yanatoa dalili Afrika imeshindwa kujitawala

Na WANDERI KAMAU

JE, huenda lilikuwa kosa kwa baadhi ya nchi za Afrika kupewa uhuru na wakoloni?

Pengine hilo ndilo swali linaloweza kuibuka kutokana na msururu wa mapinduzi ya kijeshi ambayo yanaendelea kushuhudiwa katika baadhi ya nchi.

Mwelekeo huo unafanana na kitoto kichanga kilichoruhusiwa kujifanyia maamuzi na mzazi wake bila kufikisha umri wa utu uzima.

Jumapili iliyopita, wanajeshi nchini Guinea walimpindua aliyekuwa rais wa taifa hilo, Alpha Conde, kwa madai ya kuendeleza ufisadi, ukiukaji wa haki za binadamu na kudorora kwa uchumi.

Ijapokuwa katiba ya taifa hilo inawaruhusu marais kuhudumu kwa mihula miwili pekee, Conde alitumia ushawishi wake kubadilisha katiba na kuwania urais kwa muhula wa tatu.

Kwenye matokeo yaliyotolewa baada ya uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 2020, Conde alitangazwa kuwa mshindi katika hali tatanishi.

Ushindi wake ulizua maandamano makubwa, raia wakimtaka kung’atuka uongozini kwa kuchukua mamlaka kinyume na taratibu za kisheria zilizopo.

Kwa sasa, taifa hilo lipo kwenye njiapanda, baada ya Muungano wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) kutishia kuliondoa kama mwanachama wake.

Kando na hayo, nchi za ukanda wa Afrika Magharibi zimetishia kuliwekea vikwazo vya kiuchumi ikiwa wanajeshi hao hawatarejesha uongozi wake kwa raia.

Bila shaka, hizi zimekuwa simulizi za kawaida barani humu.

Kinachoshtua ni kwamba, matukio haya yanatokea katika karne ya 21, wakati baadhi ya jamii zinayaona kama simulizi na hadithi za Alfu Lela Ulela, kwani hazijawahi kuyasikia au yalitokea mara ya mwisho katika miaka ya sitini, sabini au themanini.

Kwa sasa, nchi kama Somalia, Mali, Sudan Kusini, Sudan, Ethiopia kati ya nyingine zinapitia katika vipindi vigumu sana kuhusu mustakabali wazo kisiasa.

Raia hawajui kesho yao itakuwa vipi kutokana na mizozo ya kisiasa inayoendelea.

Kwa mfano, nchini Somalia, imekuwa kama kawaida kwa Rais Mohamed Farmajo kuvutana na viongozi wa vitengo vingine muhimu vya utawala wake.

Nchini Mali, hali ingali tete. Mapinduzi yamekuwa kama jambo la kawaida.

Swali linaibuka: Ni wakati mataifa haya yatawaliwe tena na wakoloni hadi yapevuke kisiasa?

Bila shaka hilo halifai, kwani baadhi ya mataifa ya Ulaya yamelauliwa kwa kuvuruga uthabiti wa kisiasa katika nchi hizo kimakusudi ili kupora raslimali zake asilia.

Ni wakati bara hili lifahamu kuwa linachekwa na maadui wake Waafrika wanapogeukiana wao kwa wao.

akamau@ke.nationmedia.com

MUTUA: Tunashangilia madikteta wakipinduliwa ila ipo hofu

Na DOUGLAS MUTUA

KIMOJA kati ya vichekesho ambavyo vimetokea kuvutia sana kwenye mitandao ya kijamii ni picha za watu wakiigiza jeshi la Guinea likimkamata Rais Alpha Conde.

Rais Conde alipinduliwa wiki jana na kukamatwa na kikosi maalum ambacho kikimlinda, mtandaoni kikaweka picha zake akiwa mahabusu hoi, si amiri jeshi mkuu.

Badala ya watu kumwonea imani kiongozi huyo kwa kuwa wanajeshi hao walitisha kwa silaha nzito-nzito, walifurahia hali yake na kuiona kioja kikuu.

Nchini Guinea kwenyewe hali ilikuwa shangwe, vifijo na nderemo huku wanawake wakiahidi kuwatuza wanajeshi hao kwa huduma isiyoandikwa ikaandikika hapa.

Mbona wawatuze wanajeshi kwa kumpindua rais aliyechaguliwa?

Mbona watu wamwagike mitaani kushangilia haramu? Si kuihalalisha huko?

Imekuwa desturi kwa raia kushangilia na kuwatuza wanajeshi wanaojasiria kupindua serikali dhalimu.

Wapo wanaowapa wanajeshi vyakula, vinywaji na kadhalika.

Ushangilizi ambao hufanyika, hasa Afrika, kila serikali inapopinduliwa ni kitendawili kigumu kuteguliwa na mataifa ya magharibi.

Hayaelewi fikra na mienendo yetu.

Kwa makadirio yao, utawala wa kijeshi unatabirika kuwa dhalimu kuliko wa dikteta mwingine anayepinduliwa kwani nguvu ni kigezo kikuu katika kuwadhibiti raia.

Hata hivyo, Mwafrika amenyanyasika kwa muda mrefu hivi kwamba yeyote, hata ibilisi, anayejitoa mhanga kumwondolea mtesi wake hukaribishwa kwa mikono miwili.

Ushangilizi huo hauwi wa kumwidhinisha nduli mpya aendelee kumkalia mguu wa kausha Mwafrika bali ile raha tu ya kumuona mtesi akilipia dhambi zake.

Iwapo anayemwadhibu mtesi atageuka mtesi mpya huwa si hoja wakati huo, muhimu kwa mshangilizi ni kwamba manyanyaso aliyokumbana nayo yatasitishwa.

Kwa aliyeteswa akakinai, pumziko la hata saa chache tu humpa matumaini ya kuwa na mustakabali bora kuliko dhiki aliyozoea.

Fikra za aina hii ziliwasababisha Waganda kumshangilia Iddi Amin alipompindua mtesi wao, Dkt Milton Obote.

Hawakujua kwamba Amin angewaua kinyama halafu.

Raia wa Ghana pia walishangilia pale Dkt Kwame Nkurumah alipinduliwa na wanajeshi baada ya kugeuka dikteta.

Huyo naye akidhani hadhi ya kuwa mwanzilishi wa taifa ilimwidhinisha kuisimamia nchi kama shamba lake la mpunga; alikaa miaka kadha bila kuteua makamu wake.

Mapinduzi mengi yaliyotokea Nigeria pia yalishangiliwa na raia wakitamani kumwona mtesi wao akiona cha mtema kuni.

Walikuwa radhi kupambana na hali yao halafu.

Hayo ni matukio ya miongo kadha iliyopita, muda mfupi tu baada ya mataifa mengi ya Afrika kuwa huru, hivyo raia hawakuwa wameupevuka akili umuhimu wa utawala bora.

Mwafrika wa leo amejanjaruka akajua kitu muhimu kinachoitwa katiba, kisichoruhusu maonevu na manyanyaso yoyote yale na wanafahamu fika anayewadhulumu anakikiuka.

Waafrika wamefahamu ni haramu kwa kiongozi wa nchi kubadili katiba ili kunata mamlakani, hivyo hata akifanikiwa kuibadili kinyume na mapenzi yao anavunja sheria.

Mfano bora ni kisa cha juzi nchini Guinea ambapo Rais Conde, mzee mzima wa umri wa miaka 83, alibadili katiba mwaka 2020 baada ya kutawala kwa mihula miwili ili apate wa tatu.

Alifanikiwa kufanya hivyo na hatimaye akashinda uchaguzi ambao upinzani ulisema ulikosa uhuru na uwazi. Walioandamana kumpinga ama waliuawa au wakafungwa jela.

Je, bado unashangaa kwamba kupinduliwa kwa dikteta huyo kulizua sherehe ghafla? Maskini raia wa Guinea walimpisha mwenye nguvu wasivunjwe mbavu bure ila wakabaki na vijiba vya roho wakijua hakuna mtesi atesaye kufululiza. Yamemfika ghafla, wanaona raha si haba.

Wanatarajia wanajeshi hao wawafanyie haki kwa kuwarejeshea utawala, hatua inayoweza kufanikishwa haraka na Muungano wa Kiuchumi wa Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS).

Wanajeshi hao, ikiwa waliingia mamlakani kutokana na uzalendo na wala si uchu wa mamlaka, wanapaswa kusalimu amri ya ECOWAS badala ya kuwekewa vikwazo.

mutua_muema@yahoo.com

WASONGA: Serikali itatue changamoto zinazokumba mtaala mpya

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI inafaa kushughulikia changamoto zinazozonga utakelezaji wa Mtaala mpya wa Umilisi na Utendaji (CBC) ambao ulianza kutekelezwa nchini mnamo 2019 katika shule za msingi.

Katika kipindi cha siku kadhaa zilizopita, wadau katika sekta ya elimu wameangazia changamoto kadhaa zinazokumba utekelezaji wa mtaala huu wakihofia huenda zikavurugu ufanisi wake na mustakabali wa wanafunzi.

Miongoni mwao ni gharama ya vitabu na vifaa vinavyohitajika katika ufundishaji wa masomo yaliyoko chini ya mtaala huu.

Baadhi ya wazazi wanalalamika kuwa, wanahitajika kununua vitabu vingi kiasi kwamba, baadhi yao wanajikuta kutumia Sh10,000 kununua vitabu na vifaa kwa kila mtoto.

Pili, shule nyingi haswa zile za umma hazina mitambo inayohitajika kufanikisha utelekelezaji wa mtaala huu wa CBC, kama vile kompyuta.

Licha ya hayo, walimu huwapa wanafunzi kazi za ziada za kufanyia nyumbani na ambayo inawahitaji kutoa maelezo, picha na michoro kutoka kwa intaneti.

Hali hii imewalazimu baadhi ya wazazi wenye uwezo kifedha kuwanunulia watoto wao tarakilishi.

Wale ambao hawana uwezo kifedha wanalazimika kulipia huduma hizo katika vituo vya huduma za mtandaoni, maarufu kama cyber café.

Katika maeneo ya mashambani, huduma kama hizi hazipatikani kwa haraka, hali inayowaweka wanafunzi na wazazi katika hali ngumu.

Tatu, ni jambo la kusikitisha kuwa miaka mitatu baada ya Wizara ya Elimu kuanza kutekeleza mtaala wa CBC, kuna baadhi ya walimu ambao hawajapokea mafunzo maalumu kuhusu mbinu ya kuufundisha.

Isitoshe, wale ambao wamepokea mafunzo hayo hawajapata uelewa wa kutosha, na hivyo kuchangia kutekeleza CBC kinyume na ilivyotarajiwa.

Mnamo 2019, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) Wilson Sossion alipinga kile alichotaja kama kuharakishwa kwa utekelezaji wa CBC.

Bw Sossion, ambaye pia ni Mbunge Maalumu, alilalamika kuwa Wizara ya Elimu ilianzisha utekelezaji huo pasina kufanya mashauriano tosha na wadau, haswa walimu.

Vile vile, alitaka utekelezaji wa mtaala huo uahirishwe ili kutoa nafasi kwa walimu wote kupewa mafunzo, hususan kuhusu namna ya kuzichambua dhana mbalimbali na kuzitekeleza.

Lakini Waziri wa Elimu George Magoha alimpuuzilia mbali Bw Sossion akimwonya dhidi ya “kuingiza siasa katika mpango unaonuia kuwafaidi watoto wa taifa hili.”

Hata hivyo, sasa dosari ambazo Bw Sossion alikuwa akilalamikia zimeanza kujitokeza kufuatia malalamishi kutoka kwa wadau, haswa wazazi.

Ama kwa hakika, Serikali kupitia wizara ya Elimu ilikiuka Katiba ya sasa kwa kutohakikisha mtaala huo mpya umejadiliwa kwa kina na wadau kabla ya utekelezaji wake kuanza.

Endapo maoni na mapendekezo ya wadau yangekusanywa na kujadiliwa kabla ya mtaala huu kutekelezwa, suala kuu la gharama ya utekelezaji huo lingeshughulikiwa mapema na suluhu kupatikana.

Hali ya sasa ambapo wazazi wanahitaji kununua zaidi ya kitabu kimoja cha kiada kwa somo moja, kando na vifaa vinginevyo lingeshughulikiwa.

Lakini kimsingi, mtaala wa CBC ni mzuri ila utekelezaji wake ndio ulifanywa visivyo.

Kwa mfano, masomo yanayofundishwa yanalenga kumfinyanga mwanafunzi ili aweze kujitegemea pindi atakapomaliza masomo. Mfumo huu pia unalenga kubaini uwezo na talanta za wanafunzi mapema kwa ajili ya kuzikuza kwa manufaa yake siku za usoni.

MATHEKA: Viongozi wasitumie ukame kujikweza kisiasa raia wakiumia

Na BENSON MATHEKA

IDARA ya utabiri wa hali ya hewa imetangaza kuwa mvua inayotarajiwa nchini kuanzia Oktoba haitakuwa ya kutosha.

Hii inamaanisha kuwa kutakuwa na kiangazi kitachoathiri mamilioni ya Wakenya. Hali hii ikitokea, idadi ya Wakenya wanaokabiliwa na ukame itaongezeka hadi milioni sita.

Kwa wakati huu, takwimu za serikali na mashirika tofauti zinaonyesha kuwa, watu zaidi ya milioni mbili wanakabiliwa na ukame.

Kulingana na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa, serikali imetenga Sh2 bilioni kukabiliana na ukame unaoendelea katika kaunti 13.

Mashirika ya kutoa misaada yanakadiria kuwa ukame huu utaenea hadi kaunti 23 kufikia Novemba 2021 ikiwa mvua haitanyesha jinsi wataalamu wanavyobashiri.

Hii inaashiria hatari kubwa kwa nchi kwa jumula.

Kwanza, mamilioni ya watu maskini wanakabiliwa na hatari ya kufa njaa na kiu, watoto kuathiriwa na utapia mlo na wengi kuacha masomo.

Mifugo ambao ni tegemeo la wakazi wa kaunti zaidi ya 13 nchini huenda wakaangamia kwa kukosa malisho na maji.

Kuna hatari ya mizozo kati ya wanyama na binadamu ambayo huwa inaongezeka wakati wa kiangazi.

Tayari, kumekuwa na visa vya jamii kupigania maeneo ya maji na malisho ambapo watu wameuawa.

Ingawa ukame ni janga ambalo binadamu hana uwezo wa kulizuia, serikali imekuwa ikichelewa kuchukua hatua kwa wakati unaofaa licha ya wataalamu wa hali ya hewa kutoa onyo mapema kuhusu hatari ya kiangazi au mafuriko.

Lengo la onyo hilo, ambalo huwa linatolewa mapema huwa ni kuwezesha serikali kujipanga kuzuia hasara, jambo ambalo nadra hufanyika.

Kwa kutochukua hatua, visa vya watu kuuawa na njaa na kiu au ghasia za kijamii zinaporipotiwa, serikali huwa imefeli katika jukumu lake la kulinda raia dhidi ya majanga.

Wakati mwingine serikali huonekana kutokuwa na habari watu wakifariki kwa njaa hadi masaibu yao yanapoangaziwa na vyombo vya habari.

Hii ni aibu kwa serikali iliyo na mfumo thabiti wa utawala uliofadhiliwa na pesa za umma.

Huu ukiwa msimu wa siasa za uchaguzi mkuu, wanaohangaika kwa sababu ya kiangazi wanaweza kusahaulika viongozi wakishughulika na mipango ya uchaguzi mkuu ujao.

Kinaya ni kuwa, wanasiasa watatumia mabilioni ya pesa kwa kampeni zao badala ya kusaidia raia wanaokabiliwa na njaa.

Tumeona baadhi ya viongozi wakichanga mamilioni makanisani lakini hatujawaona wakisaidia wanaokufa kwa njaa.

Sio ajabu baadhi yao wataingiza siasa kwenye masaibu ya raia wanaoangamizwa na njaa na kiu.

KAMAU: Vyombo vya habari vyafaa viwajibike 2022 ikikaribia

Na WANDERI KAMAU

MOJA ya sababu kuu ambazo zilisababisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda mnamo 1994 ilikuwa ni mchango uliotolewa na vyombo vya habari.

Kwenye ripoti mbalimbali ambazo ziliandikwa baada ya mauaji hayo na mashirika kama Umoja wa Mataifa (UN), Amnesty International (AI), Human Rights Watch (HRW) kati ya mengine, redio zilizopeperusha matangazo yake kwa lugha asili ndizo zililaumiwa pakubwa kwa kueneza chuki.

Chuki na uhasama huo ndio ulisababisha jamii za Wahutu na Watutsi kugeukiana na kuuana bila kujali wao ni ndugu wanaoishi katika nchi moja.

Lawama zaidi zilielekezwa kwa kituo cha redio cha RTL (Free Radio and Television of the Thousand Hills) ambacho kiliaminika kutumika na maafisa wakuu wa serikali ya Rwanda kueneza chuki dhidi ya Watutsi.

Kituo hicho kiliaminika kusaidiwa na Radio Rwanda kueneza propaganda dhidi ya jamii hiyo.

Vituo hivyo vinaaminika kutumika kueneza jumbe kwa wapiganaji wa Kihutu, ambazo ziliwasaidia kujua mahali ambapo watu waliowalenga walikuwa wamejificha.

Katika hali hiyo, ni wazi kuwa vyombo vya habari huwa na athari kubwa kwa jamii, na jumbe zake hutegemewa sana na hadhira yake.

Vyombo hivyo pia viliaminika kutumika pakubwa wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia (1914-1918) na Vita vya Pili vya Dunia (1939-1945).

Wasomi wa historia, siasa, utawala na mahusiano ya kimataifa wamekuwa wakisema mbinu iyo hiyo ndiyo imekuwa ikitumika katika maeneo mbalimbali duniani ambayo yameshuhudia vita baada ya 1945.

Cha kushangaza ni kuwa, Kenya ni miongoni mwa maeneo hayo.

Mbinu hiyo inaelezwa kutumika kwenye vita vilivyotokea nchini baada ya uchaguzi tata wa 2007, ambapo baadhi ya vyombo vya habari vililaumiwa pakubwa kutumika na wanasiasa kueneza chuki dhidi ya jamii ambazo hazikuwaunga mkono kisiasa.

Huku uchaguzi mkuu wa 2022 ukiendelea kukaribia, kumeibuka hofu kuwa baadhi ya vyombo vya habari nchini vimeanza kuonyesha wazi mirengo ya kisiasa vinavyounga mkono.

Kama hatua ya “kulipiza kisasi”, baadhi ya wanasiasa hata wameanza kususia vipindi na mijadala ya kisiasa wanayoalikwa katika vyombo hivyo kutokana na tuhuma hizo.

Bila shaka, huu si mwelekeo wa kuridhisha hata kidogo. Si hali ya kutia moyo, ikizingatiwa tumeanza kushuhudia visa vya mauaji ambavyo vinahusishwa na uchaguzi huo.

Kwa mfano, mashambulio yanayoshuhudiwa katika Kaunti ya Laikipia kati ya wakulima na jamii za kuhamahama yametajwa kuchochewa na baadhi ya wanasiasa ili “kuwaondoa watu wanaochukuliwa kuwa wageni katika eneo hilo.”

Ingawa serikali imetangaza kafyu kati ya saa 12 jioni hadi saa 12 alfajiri, mwelekeo huo unapaswa kutufungua macho kuhusu janga linalotuandama ikiwa tahadhari za mapema hazitachukuliwa kudhibiti hali hiyo.

Taasisi muhimu kama Mamlaka ya Mawasiliano Kenya (CAK) zinapaswa kuzinduka na kudhibiti utendakazi wa vyombo vya habari.

Ripoti ya Jaji Philip Waki kuhusu ghasia za 2007/2008 ilizilaumu redio hizo kwa kueneza chuki baina ya mirengo iliyowaunga mkono Rais Mstaafu Mwai Kibaki na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Ni wakati vyombo vya habari vifahamu vinaushikilia mustakabali wa taifa hili.

akamau@ke.nationmedia.com

KINYUA BIN KING’ORI: Ruto afikirie upya kuhusu kubuni miungano, hafai kuipuuza

Na KINYUA BIN KING’ORI

MALUMBANO na mgawanyiko ambao umeanza kujitokeza katika mrengo unaomuunga mkono Naibu Rais, Dkt William Ruto katika kuwania urais 2022 hayajengi bali kubomoa na kufifisha nyota ya kinara huyo wa kambi ya Hasla.

Wabunge wanaompigia debe Dkt Ruto husasan katika eneo la Mlima Kenya wameanza kuzozana na wenzao wanaotaka kuruhusiwa kutumia vyama vyao vya kisiasa kushirikiana na naibu huyo wa rais kubuni miungano ya kisiasa tukielekea uchaguzi mkuu ujao wa 2022.

Washirika damu wa Dkt Ruto katika Mlima Kenya kwenye kikao chao majuzi walisisitiza kuwa watatumia chama cha UDA kushinikiza maslahi yao kushirikishwa katika serikali ijayo.

Mtazamo huo unakinzana pakubwa na maoni ya aliyekuwa waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri aliyefutwa kazi Kwa kuhusishwa na Naibu Rais ambaye kwa sasa amebuni chama cha TSP na kukaidi uamuzi wa kuvunjwa kwa vyama vingine ili watumie chama kimoja cha UDA.

Bw Kiunjuri ni mwanasiasa mpevu, mwenye tajriba kisiasa na mkakamavu katika usemi na maoni yake hayafai kupuuzwa.

Kubuni vyama kama vile TSP hakutaifaa jamii ya Mlima Kenya katika ulingo wa kisiasa katika kudai haki katika mgao wa rasilimali serikalini.

Kundi la Mbunge Rigathi Gachagua likome kuchukuliwa kama lenye misimamo tofauti kama maadui wao kisiasa.

Hakuna haja ya wafuasi hao wa Bw Ruto kulaumiana bure. Kutoa matamshi yenye kuchochea na kujenga uhasama katika kundi lao ilhali wote wanakubaliana kumuunga mkono Naibu Rais katika kuwania urais hakufai.

Itabidi Dkt Ruto mwenyewe kukubali mambo si shwari tena anavyohadaika atazoa kwa wingi kura za eneo la Kati 2022 liwe liwalo.

Anafaa kusuka mikakati upya na kuwa mnyenyekevu, mpole asiye na kiburi ili afaulu kuwaunganisha wafuasi wake Mlimani bila kujali vyama vyao kisiasa.

Naibu Rais ingawa kweli anao umaarufu kwa sasa kisiasa kutokana na jinsi anavyoendesha kampeni zake kujivumisha mashinani kwa mikakati kabambe, ikiwa kweli anataka kushinda urais lazima akubali kukumbatia vyama vingine vinavyomuunga mkono kushirikiana na UDA bila kulazimishwa kuvivunja.

Ili kupambana na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga ambaye ni mwanasiasa jasiri na mjanja katika siasa za miungano, Dkt Ruto hana budi kulinda uhai wa kisiasa na umaarufu wake kwa kuhakikisha ameokoa dau lake lisizame kwa kuwaunganisha hata ikimaanisha kuwabembeleza.

Bila kuficha, ili kiongozi yeyote kufaulisha ndoto ya kuingia ikulu kwa namna yoyote ile lazima awe mwenye kusuka miungano ya kisiasa na zaidi ya chama kimoja na Dkt Ruto hafai kudharau hilo.

Na miungano hiyo inafaa kabla ya uchaguzi wa 2022.

Si hatia nchini wanasiasa kubuni miungano kwa manufaa ya watu wao kisiasa, hivyo UDA ikome kiburi ikiwa kweli inataka kiongozi wake apate uungwaji mkono wa kujivunia kote nchini.

Waige Bw Raila ambaye yu mbioni kuunda miungano ya kisiasa na wanasiasa wa vyama vingine kwa azma ya kuimarisha nafasi ya kumrithi Rais Uhuru Kenyatta akistaafu.

Dkt Ruto anapaswa kufanya maamuzi mapema kuepuka kupoteza wanasiasa waliokuwa wameanza kumuunga mkono katika azma yake kugombea urais kwa kufanya mashauriano na vyama vingine.

ONYANGO: Makamishna wa IEBC wasisimamie zaidi ya uchaguzi mmoja

Na LEONARD ONYANGO

SHERIA inafaa kufanyiwa marekebisho kuhakikisha kuwa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) hawaruhusiwi kusimamia zaidi ya uchaguzi mmoja.

Hatua hiyo itahakikisha kuwa Wakenya wanakuwa na imani na tume ya IEBC katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.

Kila wakati wa uchaguzi mkuu Wakenya wamekuwa wakiishi kwa taharuki kutokana na hofu ya kutokea kwa vurugu.

Fujo hizo zinasababishwa na Wakenya kukosa imani na tume ya IEBC.

Uchaguzi huru na wa haki ndio dawa ya kumaliza fujo ambazo zimekuwa zikishuhudiwa kila mara baada ya uchaguzi.

Tayari viongozi wa ODM wakiongozwa na mwenyekiti wake wa kitaifa Bw John Mbadi, wamemtaka mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kujiuzulu ili kuachia kikosi kipya shughuli ya usimamizi wa uchaguzi mkuu ujao.

Bw Chebukati pamoja na makamishna Bw Abdi Guliye na Bw Boya Molu walisimamia uchaguzi mkuu wa 2017 na sasa watasimamia tena uchaguzi wa 2022.

Watatu hao wanatarajiwa kustaafu Januari 20, 2023.

Makamishna wapya Bi Juliana Cherera, Bw Francis Wanderi, Bi Irene Masit na Bw Justus Nyang’aya, walioapishwa wiki iliyopita, pia watasimamia uchaguzi mkuu wa 2022 na 2027 na watastaafu Septemba 2, 2027.

Hiyo inamaanisha kwamba iwapo matokeo ya urais wa uchaguzi mkuu wa 2027 yatabatilishwa na Mahakama ya Juu, wanne hao hawataandaa kwani watakuwa wameondoka.

Kwa mujibu wa Katiba, uchaguzi wa marudio wa urais baada ya matokeo kubatilishwa na Mahakama ya Juu, unafaa kuandaliwa ndani ya siku 60.

Bw Chebukati pamoja na makamishna wenzake wawili, hawafai kusimamia Uchaguzi Mkuu ujao kwani imani ya Wakenya kwao ni imedorora mno.

Kubatilishwa kwa matokeo ya urais ya uchaguzi wa Agosti 8, 2017 kulitia doa Bw Chebukati na makamishna wenzake.

Kadhalika, barua iliyoandikwa na Bw Chebukati baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha matokeo ya urais 2017 ni ishara kwamba, watatu hao hawakutekeleza majukumu yao vyema.

Bw Chebukati katika barua yake kwa aliyekuwa Afisa Mtendaji wa IEBC Ezra Chiloba, kwa mfano, alitaka kujua kwa nini vifaa vya kielektroniki vya kutambua wapigakura na kupeperusha matokeo (KIEMS) vilifeli siku ya uchaguzi.

Bw Chebukati pia alitaka kufahamishwa kwa nini simu za setelaiti zilizogharimu Sh848 milioni, hazikutumiwa siku ya uchaguzi.

Hiyo inamaanisha kuwa makamishna hao waliachia sekretariati ya IEBC kuendesha shughuli zote za uchaguzi na hawakujua kilichokuwa kikiendelea.

Bw Chebukati hajajitokeza kueleza Wakenya kuhusu hatua ambazo zimevchukuliwa na tume hiyo kuzuia makosa ya aina hiyo.

WANGARI: Uhifadhi wanyamapori ni turathi kuu kwa vizazi vijavyo

Na MARY WANGARI

SHIRIKA la Huduma kwa Wanyamapori Nchini (KWS) mapema wiki jana lilitoa ripoti kuhusu idadi ya wanyamapori nchini baada ya shughuli ya kuhesabu iliyochukua muda wa miezi mitatu tangu Mei.

Ripoti hiyo iliashiria matumaini makuu huku idadi ya wanyamapori kadhaa wakiwemo twiga, pundamilia, swara, kifaru na ndovu ikionekana kuongezeka pakubwa.

Aidha, ripoti hiyo ilifichua nyanja zinazohitaji kutiliwa maanani hasa kuhusu wanyama wanaozidi kudidimia na kukabiliwa na tishio la kutoweka kabisa kama vile simba na chui.

Wanyamapori huchangia nafasi muhimu katika uchumi wa taifa kwa kuvutia watalii kutoka humu nchini na kutoka mataifa ya kigeni, wanaoleta fedha za kigeni.

Ripoti ya takwimu kuhusu idadi ya wanyamapori nchini itapiga jeki pakubwa juhudi za uhifadhi wa wanyama hao kwa kuiwezesha serikali kubuni mikakati thabiti kuhusu raslimali hiyo.

Ni vigumu kutenganisha uhifadhi wa wanyamapori na kulinda mazingira kwa jumla hasa ikizingatiwa kwamba mazingira asilia kama vile misitu, nyika ndiyo makao kwa wanyama hawa.

Aidha, wanyamapori hutegemea chemchemi za maji na hewa safi, misitu na vichaka ili kupata lishe na kuendelea kuishi.

Mbali na kuwa kitega uchumi, wanyamapori vilevile ni urithi wetu tuliopata kutoka mababu zetu tangu jadi.

Tangu jadi, babu zetu walifahamu kutangamana na wanyamapori katika mazingira asilia licha ya kuendelea na shughuli zao za kila siku, hata kabla ya mbuga na hifadhi za wanyamapori kuanzishwa.

Kwa mantiki hii, ni bayana kwamba tuna jukumu muhimu la kuwalinda wanyamapori kwa vyovyote vile ili kupokeza vizazi vijavyo fahari hii tunayojivunia kama taifa.

Inatamausha hata hivyo kwamba, kwa muda mrefu, tishio kuu dhidi ya wanyamapori limekuwa binadamu.

Kupitia uwindaji haramu, kuwafurusha wanyamapori kwenye makao yao asilia, binadamu amesalia kero kuu linalohujumu juhudi za kuhifadhi wanyama hawa na raslimali asilia.

Kadri idadi ya binadamu inavyozidi kuongezeka, ndivyo mazingira asilia wanamoishi yanavyozidi kuharibiwa kupitia ukataji wa misitu na vichaka yanayogeuzwa makazi ya binadamu na mashamba ya kilimo.

Maendeleo kimiundomsingi vilevile hayajasitiri wanyamapori ambapo baadhi ya miradi inayoendeshwa na serikali kama vile barabara na reli, inapitia kwenye makao ya wanyama hawa hivyo kuwavuruga katika mazingira yao asilia.

Hatuwezi kupuuza umuhimu wa maendeleo kimiundomsingi katika kizazi hiki.

Hata hivyo, ni sharti mikakati kabambe ibuniwe kutilia maanani mahitaji kimaendeleo katika kizazi hiki na wakati huo vilevile, kuhakikisha uhifadhi wa wanyamapori na mazingira kwa jumla.

Isitoshe, ni muhimu kuwashirikisha wanajamii wanaoishi karibu na wanyamapori ikizingatiwa kwamba asilimia kubwa huishi katika mazingira asilia nje ya mbuga na hifadhi za wanyama.

Uhifadhi wa wanyamapori unahitaji ujumuishaji wa wadau wote husika ikiwemo serikali na wanajamii ili kulinda raslimali hii na kuipokeza kwa vizazi vijavo.

mwnyambura@ke.nationmedia.com