TAHARIRI: Makanisa mengine nao waige mfano kanisa la ACK

NA MHARIRI

MSIMU wa siasa huwa muda wa wanasiasa kufanya lolote. Ndio wakati ambao utawaona masokoni, matangani, harusini, na hata makanisani.

Kutokana na kanuni za kuzuia maambukizi ya corona, serikali ilipiga marufuku mikusanyiko ya watu kwenye viwanja na kumbi mbalimbali.

Maeneo pekee ambako bado watu wanapatikana kwa wingi, ni katika makanisa.Si ajabu kwamba ghafla wanasiasa wanaomezea mate kumrithi Rais Uhuru Kenyatta mwaka ujao, wamekuwa waumini wakuu kila Jumapili.

Jana Kinara wa chama cha ODM, Raila Odinga na mwenzake wa Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi walikuwa kanisani Butere, Kakamega.

Kanisa la Kianglikana (ACK) lilikuwa likimtawaza Askofu wa Dayosisi ya Butere, Rose Okeno.Ingawa hafla hiyo ilikuwa ya kihistoria kwa kuwa Bi Okeno ni mwanamke wa kwanza kuchukua wadhifa huo, kuhudhuria kwa wanasiasa hao kulikuwa na lengo tofauti.

Ndio maana Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit alipotangaza kwamba hawangeruhusiwa kuhutubu, waliondoka mmoja baada ya mwengine.Kwa kawaida, wanasiasa huwa wanatumia mialiko katika hafla za makanisa na ibada zinazohudhuriwa na watu wengi, kuuza sera zao, hasa wakati huu wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Vigogo hao wa kisiasa huwa wanaandamana na wabunge na madiwani, na hugeuza hafla za kidini kuwa mikutano ya kampeni za kisiasa.

Bila aibu wanasiasa wanapopokea vipaza sauti, husahau kuwa wako mahali patakatifu. Hugeuza fursa ya kuzungumza kuwa nashambulizi dhidi ya wapinzani wao.

Askofu Ole Sapit aliwaambia wazi wanasiasa kote nchini kwamba wasitarajie kupatiwa nafasi ya kuzungumza wakihudhuria ibada katika makanisa ya ACK.

Kwamba kila mmoja anakaribishwa kanisani, lakini altari ni ya viongozi wa kidini pekee.Msimamo huu wa Askofu Ole Sapit kwamba kanisa la Kianglikana (ACK) hakitawapa nafasi wanasiasa kuzungumza, ni mzuri. Unafaa kuungwa mkono na Wakenya wote.

Viongozi misikitini wamekuwa na msimamo huu tangu zamani. Hata uwe nani, unaswali kwenye mikeka kama watu wengine. Swala ikiisha, unaondoka na kuendelea na shughuli zako.Lakini wanasiasa wamekuwa wakiotea majukwaa ya makanisa kuongea.

Wangekuwa wanazungumza mambo ya kuwajenga raia kiuchumi na kimaendeleo, hakungekuwa na sababu ya kuwa na wasiwasi.

Wengi wakipewa nafasi ya kuzungumza, huonyesha wazi kuwa hawana sera. Badala ya kueleza ni vipi wanapanga kubadili maisha ya vijana, akina mama, wazee na watu wengine, huanza kushambulia wenzao na kuvuruga heshima ya madhabau. Tabia hii si katika makanisa pekee.

Wanasiasa wamekuwa wakiotea matanga. Badala ya kuwafariji waliofiwa, hugeuza matanga hayo kuwa majukwaa ya matusi na fitina. Kwa hivyo Wakenya wengine yafaa waige hatua zilizochukuliwa na ACK.

Askofu Ole Sapit awataka wanasiasa wapunguze joto la ‘kampeni za 2022’

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Kanisa la Anglikana Nchini (ACK) Jackson Ole Sapit amewataka wanasiasa kupunguza joto la kisiasa mwaka huu wa 2020 na badala yake waangazie mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazowasibu Wakenya.

Akiongea na wanahabari Jumatano baada ya kuongoza Ibada ya kukaribisha Mpaka Mpya katika Kanisa la All Saints Cathedral, Nairobi, Ole Sapit alitaja matatizo kama ukosefu wa ajira, ufisadi, ukabila, kupanda kwa gharama ya maisha kama ambayo viongozi wa kisiasa wanapaswa kushughulikia wala sio kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.

“Najua itakuwa vigumu kwa viongozi wetu kukomesha siasa haswa za uchaguzi mkuu ujao, lakini nawahimiza kwamba wananchi hawataweza kuwapigia kura ikiwa matatizo yanayowazonga wakati hayatatuliwa. Kwa hivyo, ni wajibu wao kuhakikisha kuwa vijana wanapata ajira na gharama ya maisha inashuka,” akasema.

 

Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit akiongea na wanahabari Jumatano, Januari 1, 2020, baada ya kuongoza ibada ya kufungua Mwaka katika Kanisa la All Saints Cathedral, Nairobi. Amewahimiza wanasiasa kupunguza siasa na badala yake washughulikie changamoto zinazowasibu Wakenya. Picha/ Charles Wasonga

Vilevile, Dkt Ole Sapit amewaonya wanasiasa dhidi ya kuingiza siasa katika ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) bali waitumie kujadili namna ya kutatua changamoto zinazowasibu Wakenya.

“Ripoti ya BBI haifai kutumiwa kama jukwaa la kubuni miungano ya kisiasa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022. Kama Kanisa tunahimiza kuwa ripoti hii itumiwe kuanzisha mdahalo wa kitaifa kuhusu yale yanayotutatiza kama taifa na namna ya kuyatatua. Tutumie BBI kupalilia umoja wa kitaifa,” akasema.

Ole Sapit ametoa changamoto kwa viongozi wa kisiasa kutumia muda wao mwingi mwaka huu kutekeleza ahadi walizowapa wapiga kura.

“Rais na naibu wake wawe mstari wa mbele kuongoza mipango ya kutekeleza manifesto yao na ahadi zote walizotoa kwa Wakenya mwaka 2017. Na wabunge nao watumie pesa za CDF kwa miradi yenye manufaa kwa wananchi,” akasema.

Kiongozi huyo wa ACK pia amewataka viongozi wawe kielelezo bora kwa vijana kwa kutembea katika mwangaza na kuepukana na maovu na vitendo vinginevyo vinavyokwenda kinyume na sheria.

“Viongozi wakitembea katika mwangaza watafanya maamuzi mazuri na vitendo vyao vitakuwa vya kupigiwa mfano. Sisi kama viongozi wa kidini na wenzetu wa kisiasa tunastahili kufanya mambo ambayo yatanufaisha jamii bali sio kuigawa,” akasema.

 

Raila asifu Sapit kwa kupigana na ufisadi kanisani

Na RUSHDIE OUDIA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amemiminia sifa Kiongozi wa Kanisa la Anglikana (ACK) Jackson Ole Sapit kwa kupiga marufuku michango ya fedha kutoka kwa wanasiasa.

Bw Odinga alisema hatua ya Askofu Mkuu Sapit inasaidia katika kukabiliana na ufisadi ambao umekolea nchini.

Kumekuwa na mjadala kuhusiana na mamilioni ya fedha yanayotolewa na wanasiasa makanisani huku Bw Odinga na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Hajji wakiamini kuwa michango hiyo inaendeleza wizi wa fedha za walipa ushuru.

Bw Odinga alidai kuwa wanasiasa wa kundi la Tangatanga linalounga mkono Naibu wa Rais William Ruto linatumia fedha kujitafutia umaarufu nchini.

Bw Odinga alikuwa akizungumza katika Kaunti ya Siaya wakati wa hafla ya kusherekea kustaafu kwa Askofu wa Parokia ya Maseno Magharibi Dkt Joseph Otieno Wesonga.

Alisema uchumi wa Kenya umedorora kutokana na ufisadi.

“Wanasiasa sasa wanawahonga viongozi wa kidini ili wawaalike kanisani kufanya mchango. Fedha hizo zinatokana na ufisadi na wanazitumia kununua watu wa kuwaunga mkono,” Bw Odinga.

“Hata wafanyabiashara maarufu kama vile Vimal Shah na Manu Chandaria ambao wamekuwa wakisaidia jamii hawawezi kutoa mamilioni ya fedha kila wikendi,” akasema.

Suala kuhusu harambee kanisani limekuwa likiibua mjadala mkali, lakini Dkt Ruto husisitiza ataendelea kutoa michango hiyo kwa kuwa ni shukrani yake kwa Mungu.

Pesa zinazonyang’anywa wafisadi zitumike kulipa madeni – Ole Sapit

Na Mwandishi Wetu

KIONGOZI wa Kanisa la Kianglikana Nchini (ACK) Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit ameishauri serikali kutumia pesa na mali inazotwaa kutokana na vita dhidi ya ufisadi kulipia madeni ya kigeni.

Alisema kuwa kanisa hilo linaunga mkono juhudi za serikali kupigana na uovu huo na akahimiza asasi zilizotwikwa jukumu la kuchunguza kesi za ufisadi zipewe nafasi ya kuendesha shughuli hiyo bila kuingiliwa.

Ole Sapit alikuwa akiongea katika eneo la Badasa katika kaunti ndogo ya Marsabit mnamo Ijumaa alipoweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa Shule ya Upili ya Wavulana ya St Andrews.

Askofu huyo Mkuu alisema kuwa Kenya inadaiwa deni kubwa na mataifa ya kigeni na hivyo itakuwa jambo la busara ikiwa sehemu ya pesa zilizokombolewa kutoka kwa wafisadi zitatumiwa kulipa madeni hayo.

Kiongozi huyo wa ACK alionya wanasiasa dhidi ya kuingiza siasa katika vita dhidi ya jinamizi hilo akisema kuwa Tume ya EACC na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) zinahitaji mazingira faafu kuwakamata wahusika.

 

Fedha za umma zilizofujwa zirejeshwe upesi – Sapit

Na GERALD BWISA

SERIKALI imeombwa kushinikiza kurejeshwa kwa pesa zilizoibwa katika ufisadi huku juhudi zikiimarishwa kupambana na ufujaji wa pesa za umma.

Akizungumza na wanahabari Kitale Jumapili, Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana la Kenya, Jackson ole Sapit, alimwambia Rais Uhuru Kenyatta asilegeze kamba katika juhudi hizo.

Alisema inafaa mapambano dhidi ya ufisadi yaendelee hadi wakati pesa zote za umma na rasilimali zilizopotea zirudishwe na kutumiwa kwa manufaa ya wananchi.

“Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi na Idara ya Mashtaka ya Umma zimepiga hatua kubwa kwa kufikisha mahakamani wale wanaojihusisha katika ufisadi lakini haifai yaishie hapo. Kama kuna pesa zozote zilizopotea katika ufisadi inafaa zirejeshwe,” akasema.

Bw Sapit alisema kuna taasisi kama vile hospitali za umma ambazo zina uhaba wa mahitaji muhimu ilhali watu binafsi wanafuja pesa za umma.

“Tuna uhaba wa dawa hospitalini, pesa zinazofujwa zinafaa zirejeshwe ili zitumiwe kununua dawa hospitalini na pia kutumiwa kwa ujenzi wa miundomsingi kwa manufaa ya wananchi,” akasema.

Alitoa wito pia kwa bunge la taifa, hasa kamati inayochunguza sakata ya sukari kuhakikisha ripoti zinazotolewa zimezingatia ukweli uliopo.

Aliwataka wabunge wajiepushe kushawishiwa ili wafiche uweli bali waseme yote waliyobainisha kwenye uchunguzi wao.

Askofu huyo mkuu aliomba pia viongozi nchini wawe na malengo yatakayodumisha utulivu nchini hata wakati watakapoondoka mamlakani.

Alisema viongozi watakutana kufanya mashauriano kuhusu jinsi ya kuzuia changamoto zinazoweza kuweka vikwazo kwa utekelezaji wa malengo muhimu kwa taifa. Wakati huo huo, aliyekuwa Waziri wa Wanyamapori na Misitu, Dkt Noah Wekesa, aliunga mkono juhudi za rais kupambana na ufisadi.

Dkt Wekesa alisema ufisadi umeathiri maendeleo ya nchi. Alitoa wito kwa viongozi wa makanisa kuongoza Wakristo ili watekeleze majukumu yao ya kuchangia katika kupambana na ufisadi na kuhakikisha kuna mafanikio katika juhudi hizo.

“Rais ana ajenda nne anazolenga kufanikisha. Kwa mtazamo wangu akiendelea kupambana na ufisadi kwa moyo wake wote, hilo pekee litapewa umuhimu kuliko ajenda hizo nne kwa kuwa ufisadi umeelekeza nchi yetu pabaya,” akasema.

Askofu aitaka NASA ikubali Uhuru Kenyatta ni Rais halali

Na SAMMY LUTTA na VALENTINE OBARA

Kwa Muhtasari:

  • Askofu Sapit asema kipindi cha kampeni kilikamilika 2017 na nchi inahitaji utulivu
  • Awataka Wakenya kusubiri hadi 2022 uchaguzi mwingine wa urais utakapoandaliwa
  • Mashauriano ya kisiasa yanafaa yawe kuhusu jinsi sheria za uchaguzi zinaweza kurekebishwa
  • Kiongozi huyo aonya Kenya itabaki nyuma kimaendeleo na kiuchumi hali ya kisiasa nchini ikizidi kushuhudiwa

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana la Kenya (ACK), Bw Jackson ole Sapit, Jumatatu alisema Muungano wa NASA unafaa kusubiri hadi mwaka wa 2022 ili ushiriki kwenye uchaguzi wa urais kwani Rais Uhuru Kenyatta yuko mamlakani kihalali.

Askofu Sapit alisema kipindi cha uchaguzi kilikamilika 2017 na nchi inahitaji utulivu ili kuleta maendeleo na huduma kwa wananchi baada ya serikali kuundwa.

“Tunahitaji kukomesha siasa na tusubiri hadi 2022 kwani wakati huyo ndio viti vya kisiasa vitakuwa wazi kikatiba na wale wanaotaka kuwa wagombeaji wataruhusiwa. Ninaomba walio serikalini na katika upande wa upinzani washauriane kuhusu jinsi ya kuleta umoja kwa Wakenya ambao kwa sasa wamegawanyika kisiasa,” akasema.

Alikuwa akizungumza na wanahabari katika kanisa la St Paul’s ACK, parokia ya Lodwar baada ya kuzindua lango jipya na maduka yaliyojengwa.

 

Uchumi utayumba

Kiongozi huyo wa kidini alisema Kenya itabaki nyuma kimaendeleo na kiuchumi kama hali ya kisiasa itazidi kushuhudiwa kwa muda mrefu huku upande wa upinzani ukitaka mmoja wao awe rais.

Alisema kanisa linaomba kila mmoja nchini akumbatie uwiano na uvumilivu wa kisiasa ili kuwe na amani huku akiongeza kuwa serikali iliyopo inafaa kuwa katika mstari wa mbele kueneza umoja wa kitaifa.

Bw Sapit alisema mashauriano ya kisiasa yanafaa yawe kuhusu jinsi sheria za uchaguzi zinaweza kurekebishwa ili kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa 2022 utafanywa kwa njia bora zaidi.

“Hatuhitaji mashauriano kuhusu jinsi Kenya inaweza kupata rais mpya hivi sasa kwa kuwa nchi tayari ina Rais Uhuru ambaye aliapishwa mamlakani baada ya ushindi wake kukubaliwa na Mahakama ya Juu,” akasema na kusisitiza kuwa nchi haiwezi kuwa na marais wawili kwa wakati mmoja.

 

Msimamo sawa na mabalozi 

Msimamo wake ni sawa na uliotolewa na mabalozi wa nchi za magharibi ambao walimtaka Bw Odinga atambue uhalali wa uongozi uliopo kabla kuwe na mashauriano kuhusu mabadiliko anayotaka.

Bw Odinga alikashifu mabalozi hao 11 na kusema hawana haki ya kuamulia wananchi wa Kenya kuhusu uongozi wanaotaka kwani walionyesha ubaguzi wao wakati wa uchaguzi wa urais mwaka uliopita.

Mshauri wa kiongozi huyo wa Chama cha ODM, Bw Salim Lone, pia alikosoa mabalozi hao na kusema msimamo wao unaweza kufanya pande zote mbili zizidi kuwa na misimamo mikali.

Kulingana naye, Bw Odinga amekuwa mvumilivu kwa muda mrefu na hata aliepuka wito wa wafuasi wake mara nyingi walipomtaka ajiapishe kuwa rais, na hatimaye akajiapisha tu kuwa ‘rais wa wananchi’ na wala si wa Jamhuri ya Kenya.